Saturday, 26 July 2014

UGUMU ULIOPO KATIKA KUFASILI MAANA YA NENO

ST. FRANCIS MAUA SEMINARY
Neno ni dhana iliyojadiliwa na wanaisimu kadhaa ambao walijadili katika namna tofauti, utofauti huo umesababishwa na vigezo walivyovitumia. Kuna waliolichambua neno kwa kigezo cha kifonolojia, kisemantiki, kiotografia, kisintaksia, kileksika na vigezo vinginevyo. Insha hii itajadili maana ya neno kwa vigezo hivyo (vilivyotajwa hapo juu), kuonyesha ubora au upungufu,  kuonyesha ugumu wa kifasili dhana hiyo na mwisho kuhitimisha.
Kifonolojia, neno ni silabi au mkusanyiko wa silabi zinazotamkwa au kuandikwa (TUKI, 1990), silabi hizo huwa ni tofauti kutoka lugha moja hadi nyingine. Mfano katika Kiswahili neno “karibu” lina silabi tatu (3)
$ ka $ $ ri $ $ bu $.
Kwa kigezo hiki pia, neno huwezea kufafanuliwa kama vipande vya matamshi yaani fonimu zinazopangwa katika mpangilio maalum ili zilete maana.
Mfano neno “bata” lina fonimu nne ambazo ni /b/, /a/, /t/, /a/
Mpangilio huu ukigeuzwa maana ya neno hupokea na watumiaji wa lugha hiyo hawataelewa maana yake.Mfano neno*taba, japokuwa limeundwa na fonimu zilezile halina maana kwa sababu mpangilio huo haupo katika lugha hiyo.
Vilevile kwa mujibu wa mtandao (Taz. www.sussex.ac.....), katika lugha ya Kiingereza sifa itumikayo kuonyesha kuwa hili ni neno ni mkazo msingi ambao huwa ni mmoja tu katika neno.
Mfano:Juma is going  to school.
Tungo hii ina maneno matatu “Jumas’ “going” na “school”. Kwa kigezo hiki “is” na “to” si maneno.
Pamoja na kigezo hiki kuzingatia sana viambajengo vya lugha kama fonimu, silabi  na mkazo bado ina upungufu hasa katika kipengele cha mkazo, kila lugha ina sheria zake katika uwekaji mkazo. Kwa mfano katika Kiswahili. Mkazo msingi huwekwa katika silabi ya mwisho kasoro moja na huhama kwenda katika neno la mwisho kila maneno yanapoongezeka katika tungo.
Mfano
- Anakula.
- Anakula chakula.
-Anakula chakula kitamu.
Silabi iliyopigiwa mstari ina mkazo msingi.
Mfano huo hapo juu unaonyesha kuwa mkazo msingi huhama kwa kadiri maneno yanavyoongezeka.
Vilevile kuna lugha nyingine kama Kihehe, Kidigo, Ci-ruuri hazina mkazo bali zina toni (Massamba; 2010) hivyo kwa kigezo cha mkazo ni vigumu kubaini maneno katika lugha hizo.
Kiotografia, neno limefasiliwa kama mfululizo wa herufi zilizofungamana pamoja na kuzungukwa na nafasi tupo (Mdee, 1997). Utaratibu wa kuweka nafasi hufuata taratibu maalumu za kiotografia ambazo hutofautiana kutegeana na lugha moja na nyingine.Kwa mfano katika lugha ya kiswahili ,
         -Mama alirudi jana usiku.
Tungo hii una maneno manne yaani “mama” “alirudi” “jana” na “usiku”
Kwa ujumla ubora wa mkabala huu ni kwamba, husaidia sana uandishi wa matini za kitaaluma hasa kwa lugha zinazofuata utaratibu huu. Lakini vilevile ina upungufu kama ifuatavyo.
Dhana ya nafasi tupu ipo tu kwenye maandishi, tunapozungumza hatuachi nafasi tupu baina ya maneno, tunayatamka yote kwa mfululizo.
Vilevile utaratibu wa kuweka nafasi mwanzoni au mwishoni mwa neno haupo katika lugha zote, kuna lugha kama Kigiriki na kieskimo maneno yake katika tungo hayawekewi nafasi tupu. Kwa mfano tungo hii ya lugha ya Kieskimo “Kaipiallrullinink”yenye maana ya kuwa “wote wawili walikuwa na njaa”. Tungo iliyowekwa katika herufi za italiki ni ya kieskimo ambayo haina nafasikati ya neno moja na lingine.
Pia maneno ambatani yatahesabiwa kuwa ni neno moja au mawili?, (www.sussex.ac.....).Haya ni maneno mawili au zaidi lakini yamebeba dhana moja Kwa mfano katika Kiingereza
-    “pocket money”
-    “Bus driver”
Katika Kiswahili maneno ambatani ni kama
-    Gongo la Mboto
-    Kata mbuga.
Sambamba na hayo, upungufu mwingine wa dhana hii ni kwamba, haiangalii viambajengo vinavyojenga neno kwa mfano fonimu silabi, mkazo na toni.
Kwa upande wa semantiki, neno limefasiliwa kipashio kidogo cha lugha chenye maana (Mdee, 1997) kwa maana hiyo neno ni lazima liwe na maana inayoeleweka kwa jamii inayotumia lugha hiyo. Mfano:
Mama – Mzazi wa kike
Ndama – Mtoto wa ng’ombe
Fasili hii ina mashiko kwa sababu maneno mengi katika lugha yana maana na hueleweka kwa watumiaji wa lugha. Lakini kwa aupande wa pili si kila neno linalotumika linaweza kuwa na maana ya wazi au ya kisemantiki,kwa mfano viunganishi kama na, ya, kwa, wakati n.k, ambavyo japokuwa havina maana ya kisemantiki lakini vina uamilifu kisarufi.
Wanataaluma wa kisintaksia wanafasili neno kama kipengele kidogo kabisa cha sentensi ambacho kinaweza kuhamishwa kutoka nafasi moja hadi nyingine bila kuathiri sarufi ya lugha katika tungo/sentensi hiyo. Cruse (1986) akinukuliwa na Mdee (1997). Kwa ujumla hapa kinachotazamwa zaidi ni kategoria za maneno na mpangilio wake katika tungo.
Mfano
-    Ali     alimuua     Ahmad
        N         T             N

-    Ahmad         alimuua    Ali
           N              T              N
      Hapa N ni Nomino na T ni kitenzi.
Japo nomino zimebadilishana, lakini sarufi ya lugha hiyo haijaathirika.
Kwa ujumla utaratibu huu unasaidia sana katika kujifunza sarufi ya lugha hasa miundo ya tungo kama virai,vishazi na sentensi na pia hata kujua sehemu za tungo kama kiima na kiarifu.
Lakini kwa upande mwingine kigezo hiki kina upungufu kwa sababu sio maneno yote yanayoweza kuhamishwahamishwa bila kuvuruga sarufi ya lugha.
Kwa mfano.
-    Alia amesimama kando ya mto
-    Amesimama kando ya mto Ali.
-    Kando ya mto Ali amesimama
*    Mtoto Ali amesimama kando ya
*     Mto ya kando amesimama Ali.
Sentensi mbili za mwisho (zilizowekewa) nyota kwa sababu hazikidhi haja ya usahihi wa kisarufi (Mdee, 1997:7)
Vilevile unapohamisha maneno basi maana ya neno pia hubadilika
Mfano
(i)    Zubeda anampenda Zawadi
(ii)    Zawadi anampenda Zawadi
Japokuwa nomino katika sentensi hizo zimebadilishana nafasi, haijaathiri sarufi ya lugha lakini kimaana imebadilika kwa sababu katika sentensi (i) Zubeda ndie anatenda tendo na katika sentensi (ii) Zawadi ndio anatenda tendo.
Kileksika, neno ni dhana dhania ya kileksikoni ambayo neno hurejelewa kama Leskimu. Leskimu ni msamiati ulioorodheshwa kwenye kamusi (Katamba, 199:17), neno hili (Leskimu) huwa na maana kimsamiati (TUKI: 1990). Kwa kawaida Leskimu huwa na vibadala vyake kutegemeana na leskimu yenyewe.
Mfano:
    go    -   vibadala vyake ni go, going,went, goes.
    cheza - cheze, chezea, mchezea, chazeana, n.k.
     refu -  refu,  ndefu,  mrefu,  kirefu, n.k.   
Japokuwa dhana hii inasaidia sana katika taaluma za mofolojia,  leksikografia na taaluma nyinginezo, bado ina mapungufu au haijitoshelezi kwa  sababu katika lugha kuna maneno ambayo yakisimama pake yake hayaleti maana na si leskimu katika kamusi lakini maneno hayo yakikurubishwa na maneno ya kileksika huleta maana. Katika Lugha ya Kiswahili kwa mfano  kuna viunganishi kama na, ya, kwa n.k na vitenzi vishirikishi (husishi) kama ni, si, -kuwa na ndi- (ndiye, ndio n.k) ambavyo si leskimu lakini  hufanya kazi ya kisarufi au vina uamilifu katika lugha.
Kutokana na fasili hizo tunaona kuwa kuna ugumu katika kufasili dhana ya neno, ugumu huo unasababishwa na sababu zifuatazo.
Spencer (1991) anadai kuwa ugumu wa kufasili neno unasababishwa na utofauti wa lugha kimaumbo, kimatamshi, kimuundo na kimaana, hivyo ni vigumu kuhusisha fasili moja inayoweza kuhusisha mifumo yote ya lugha kwa usahihi kwa sababu lugha hutofautiana katika vipengele hivyo.
Naye Mdee (1997) anadai kuwa kufasili neno kuna ugumu, ugumu huo unatokana na mitazamo tofauti ya wanaisimu kuhusu kipashio hicho (neno) kiotografia, kimaumbo na, kimatamshi. Hivyo kwa kuwa kila mwanaisimu anamtazamo wake hivyo hushindwa kukubaliana maana moja ya neno.
Vilevile kwa mujibu wa mtandao (w.w,w. sussex ..) unadai kuwa ugumu wa kufasili neno unasababishwa na utofauti  wa utamaduni na mazingira na maarifa ya wanaisimu. Hii ndio sababu kila mtu  anafasili neno kutokana na lugha yake ilivyo na maarifa aliyonayo, wanafonolojia wanafasili neno kwa kuzingatia nduni za fonolojia kama silabu, fomimu, toni, mkazo, wanaleksikografia wamefasili neno kama leskimu n.k.
Kwa ujumla tunaweza kuhitimisha kwa kusema kwamba, ugumu wa kufasili neno tofauti za wanaisimu kilugha, kitaaluma, kimazingira kimtazamo na kiutamaduni.Hivyo ili kuondoa au kuziba upungufu wa kigezo kimoja, vigezo zaidi ya kimoja vitumike katika kuangalia maana za maneno katika lugha tofauti.
MAREJEO
Katamba, F. (2993)  Morphology.  Macmillan Press  LTD. London.
Mdee,D. (1997)  Nadharia za Leksikografia. TUKI, Dar-es-Salaam.
Spencer, A. (1991) Morphological Theory: An Introduction to Word Stucture in Generative Grammar. Blackwell Publishers. UK.
TUKI (1990) Kamusi sanifu ya Isimu na Lugha. TUKI.  Dar-es-Salaam
www. Sussex. ac. Uk/ linguistic. doc.  Tarehe  21/05/2011. saa 4:50  asubuhi.

Wednesday, 25 June 2014

NADHARIA YA UDENGUZI


NADHARIA YA UDENGUZI KATIKA UJITOKEZAJI WA WAHUSIKA WA TAMTHILIYA ZA KISWAHILI.

Wahusika ni kitu muhimu katika kazi yoyote ya kifasihi, kwani ndio wanaosukuma mbele kazi ya kifasihi. Wataalamu mbalimbali wamezungumzia kwa namna tofauti maana na ujitokezaji wa wahusika wa kazi ya fasihi. Hii ni taka enzi za Ugiriki ya kale hadi katika fasihi ya kiswahili.
Mulokozi (1996) anasema hadithi ya tamthilia husonga mbele kwa njia ya vitendo na mazungumzo ya wahusika. Hivyo anaonesha bila wahusika hata mazungumzo hayatakuwepo.
Brecht (1898-1956) aliibua kanuni ya ukengeushi ambayo

Friday, 25 April 2014

UTAFITI KATIKA UBUNIFUUCHUNGUZI SAMBAMBA DHIDI YA MAMBO YA KUFIKIRIKA

Uchunguzi katika uandishi wa kubuni ni jambo la lazima ili mtunzi asiandike vitu ambavyo havishawishi kukubalika. Kwa maneno mengine, kufanya uchunguzi ni kufanya utafiti. Je, utafiti ni nini? Hebu tuangalie baadhi ya wataalamu wanasemaje kuhusiana na istilahi hii ya utafiti.
Kothari (2009:1) anasema kuwa, kwa msemo wa kawaida 'utafiti' ni kutafuta maarifa ili kuelewa jambo fulani. Utafiti ni utafutaji wa taarifa kisayansi na kwa kufuata utaratibu fulani kuhusiana na mada fulani. Kwa uhakika, utafiti ni

Wednesday, 23 April 2014

SINTAKSIA


SINTAKISIA HAIWEZI KUTENGANISHWA NA VITENGO VINGINE VYA LUGHA.
Katika kujadili mada hii, kwanza tutatoa fasili ya sintaksia kwa mujibu wa wataalam mbalimbali, fasili ya lugha, tutafafanua uhusiano uliopo kati ya sintaksia na vitengo vingine vya lugha na mwisho tutatoa hitimisho juu ya mjadala wetu.
Kwa mujibu wa Massamba na wenzake (1999) Sintaksia ni utanzu wa sarufi unaojihusishana uchunguzi wa mpangilio wa maneno katika sentensi na uhusiano wa vipashio vyake. Wanaendelea kusema, utanzu huu huchunguza sheria au kanuni zinazofuatwa katika kuyapanga maneno ili yalete maana inayokubalika na kueleweka katika lugha husika.
Pia Habwe na Karanja (2004) wanasema Sintaksia ni utanzu wa isimu unaoshughulikia muundo wa sentensi na elementi nyingine zinazounda sentensi kama vile kategoria za maneno, vikundi na vishazi.
Kutokana na fasili hizi inaonekana kuwa Massamaba na wenzake wamefafanua zaidi kwa kuonesha kuwa licha ya kuzingatia kanuni na sheria za kupanga maneno lakini pia ni lazima maneno hayo yawe na uhusiano. Kwa upande mwingine Habwe na Karanja wameshindwa kuelezea suala hili, wao wanaona sintaksia inashughulika na muundo wa sentensi na vipashio vyake.
Kwa mantiki hii  tunakubaliana na fasili ilyotolewa na Massamaba na wenzake kuwa Sintaksia ni utanzu wa sarufi unaojihusisha na uchunguzi wa mpangilio wa maneno katika sentensi  na uhusiano wa vipashio vyake, kwa kuzingatia sheria na kanuni za lugha husika ili kuleta mawasiliano.
Katika fasili ya lugha, wataalam wengi wanakubaliana kuwa

Monday, 3 February 2014

VIONJO VYA FASIHI SIMULIZIKUNA FAIDA GANI YA KUIENDELEZA F. SIMULIZI IKIWA JAMII NYINGI SASA HIVI ZINAJUA KUSOMA NA KUANDIKA?
Wengi mtakubaliana nami kwamba, Maendeleo ya Sayansi na Teknolojia ulimwenguni, kamwe hayaondoi uwepo wa fasihi simulizi, bali yanaleta athari katika fasihi simulizi ama chanya ama hasi.
Pia tutambue kwamba, jamii yoyote ulimwenguni inapoendelea katika nyanja yoyote ile athari hazikwepeki. Na hii ni kanuni inayofahamika ulimwenguni kote.
Hivyo basi, hata kama jamii nyingi duniani zinajua kusoma na kuandika, bado umuhimu wa kuiendeleza fasihi simulizi katika ulimwengu wa leo upo palepale. Tena katika kipindi hiki cha maendeleo ya Sayansi na Teknolojia mimi naona umuhimu huu ni mkubwa sana kuliko hata miaka ya nyuma.
Awali ya yote katika kujadili swali hili ningependa tujadili kwa kifupi

Saturday, 1 February 2014

KISWAHILI

KILIO CHA MAMA YANGU
Mwenzenu nimefikiri, nimeshindwa kung’amua,
Kila nikitafakari, najiona naelea,
Hili lazima nikiri, niufukuze utwea,
Na leo ndiyo kikiri, jipu ninalitumbua,
Kilio cha mama yangu, ni kicheko kwa mgeni.
Staajabu ya Musa, uone ya Firauni,
Nabii wamemsusa, nyumbani hana thamani,
Anazidi kuhohosa, kajibanza pembezoni,
Mgeni ndiyo kabisa, kapandishwa kileleni,
Kilio cha mama yangu, ni kicheko kwa mgeni.
Uhuru wangu ni upi, hapa kwetu Tanzania?
Na kosa langu ni lipi, mbona mwaninyanyapaa!
Nimeshindwa fanyakipi, mpaka mwanikataa!
Hata mkinena vipi, hii ni yenu junaa,
Kilio cha mama yangu, ni kicheko kwa mgeni.

Wednesday, 29 January 2014

Sunday, 29 December 2013

HOJAJI

KANUNI ZA UUNDAJI WA HOJAJI
Makala haya yanahusu kanuni za uandaaji wa hojaji. Katika kujadili mada hii tumegawa kazi hii katika sehemu tatu muhimu, sehemu ya kwanza fasili ya hojaji kulingana na wataalam mbalimbali, sehemu ya pili ni kiini cha swali ambapo inaelezea kanuni muhimu za uundaji wa hojaji, hatimaye hitimisho.
Kwa mujibu wa Kothari C.R, (2004),  uk 100, anafasili neno hojaji kuwa ni maswali yanayoandikwa katika karatasi ili yaulizwe kwa mtafitiwa kwa lengo la kupata taarifa za tatizo la utafiti.
Nayo Kamusi ya Kiswahili sanifu (2004) TUKI uk 116, inasema kwamba hojaji ni

Sunday, 22 December 2013

KUIBUKIA KWA NADHARIA YA MOFOFONEMIKI

Katika mada hii tumeangalia fasili ya mofofonemiki kwa mujibu wa wataalam mbalimbali, kisha tukaangalia kwa ufupi historia ya nadharia ya mofofonemiki na katika kiini cha mada tumejadili sababu zilizopelekea kuibuka kwa nadharia ya mofofonemiki.
Kwa kuanza na fasili ya mofofonemiki  kwa mujibu wa mtandao wa Wikipedia wanafafanua mofofonemiki kuwa ni tawi la isimu linalojishughulisha na mwingiliano wa mishakato ya kimofolojia na kifonolojia au kifonetiki. Pia hujishughulisha na

NDUNI BAINIFU ZA KONSONANTI

Strident = Sauti zenye ukelele wa frikwensi ya juu wakati wa utamkaji. Sauti hizo ni baadhi ya vikwamizi na vizuio-kwamizi:  [+stridenti] = /f, v, s, z, ʃ,  č, j/
Sonoranti = Wakati wa utamkaji mzuio wake si mwembamba kiasi cha kubana mkondo wa hewa kwenye glota; hali hii husababisha ughuna; Irabu, viyeyusho, vitambaza, na ving’ong’o ni sanoranti.
Anteria = Sauti yoyote inayotamkwa kuanzia kwenye ufizi hadi kwenye midomo.
Korona = Wakati wa utamkaji bapa la ulimi huinuliwa na kusogeleana au kugusishwa kwenye meno ya juu, ufizi wa juu na nyuma ya ufizi au baada-ufizi. Sauti zenye sifa hii ni: /t, d, s, z, ʃ, ʒ, Ɵ, ð, tʃ, ʤ, l, r, j

Tuesday, 10 December 2013

CHIMBUKO LA RIWAYA YA KISWAHILI

CHIMBUKO LA RIWAYA YA KISWAHILI.
Katika mjadala huu, tutajikita zaidi kwa kutoa maana ya riwaya kutoka kwa wataalamu mbalimbali, maana ya riwaya ya Kiswahili, maana ya chimbuko, Kisha mjadala huu utaelekea zaidi katika kuelezea chimbuko la riwaya ya Kiswahili kutokana na wataalamu mbalimbali waliopata kueleza asili ya riwaya hiyo ya Kiswahili, na hicho ndio kitakachokuwa kiini cha mjadala wetu. Mwisho kabisa hitimisho la mjadala. 
Kwa kuanza na maana ya riwaya imejadiliwa kama ifuatavyo:

Sunday, 8 December 2013

FONOLOJIA YA KISWAHILI

FONOLOJIA YA KISWAHILI
UTANGULIZI
USULI WA TAALUMA YA FONOLOJIA
Neno fonolojia linatokana na maneno mawili ya Kigiriki phone-sauti za kusemwa na logos- taaluma/mtalaa. Masimulizi yanadai kuwa taaluma hii ilianza zamani sana kati ya mwaka
460 kabla ya Masihia huko India ya kale, ambapo mtu aliyeitwa Panini, na ambaye huaminika kuwa ni baba wa isimu aliandika kuhusu fonolojia ya Kisansikriti katika matini aliyoiita Shiva Sutras. Ni katika andiko hili ndipo alipobainisha kuwepo kwa dhana ambazo leo hii hujulikana kama fonimu, mofimu na mzizi.

Baada ya andiko hilo, habari za taaluma ya fonolojia ni kama zilipotea kabisa katika uwanja wa isimu hadi ilipofika karne ya 19 ambapo wanaisimu wengine waliibuka na kuzungumzia upya masuala ya fonolojia. Miongoni mwa wanaisimu wa mwanzo

Monday, 2 December 2013

NENO


FASILI YA NENO
Makala haya yana jadili fasili ya neno kwa mujibu wa wataalamu mbalimbali, ugumu wa fasili ya neno na kiini cha utata huo. Katika kujadili hayo makala yatagawanywa katika sehemu tatu, sehemu ya kwanza itaelezea maana ya neno kwa mujibu wa wataalamu mbalimbali, Sehemu ya pili tutaelezea kiini cha ugumu huo, na sehemu ya tatu tutatoa hitimisho.
Mdee (2010:5) hueleza kwamba dhana ya neno ina utata, kwani ni umbo lenye sura nyingi, utata huo hutokana na mitazamo tofauti ya wanaisimu, kuhusu kipashio hiki kitahajia (jinsi linavyo andikwa), kimatamshi na kimaana.
TUKI (2009) Hueleza kuwa neno ni kipashio cha usemaji ambacho hujengwa na mwandamano au mkuroro wa sauti zilizopangika kisilabi na ambazo hutambuliwa na wasemaji wa lugha inayohusika, kuwa kitu kimoja chenye maana mahususi.
TUKI (2010) Huelezea kuwa neno ni sauti au mkusanyiko wa sauti zinazotamkwa au kuandikwa pamoja na kuleta maana

Kwa mujibu wa Mdee (ameshatajwa) hueleza kuwa neno ni mfululizo wa herufi zilizo fungamana pamoja na kuzungukwa na nafasi tupu. (Mdee, amekwishatajwa)
Kwa upande wake Cruse (1986:3) kama alivyo nukuliwa na Mdee, husema kuwa neno ni kipengele kidogo kabisa cha sentensi ambacho kinaweza kuhamishwa kutoka nafasi moja kwenda nyingine bila kuathiri sarufi ya lugha katika sentensi hiyo.
Vilevile neno huweza kuelezewa kama kipashio cha lugha,kinachowakilisha taarifa kama vile , matamshi, maana, tabia za kimaumbo na za kimuundo (Spencer, 1991)
Kiini cha ugumu wa kufasili neno
Zipo njia kadha za kisarufi ambazo zinaweza kutumika katika kuelezea dhana ya neno na katika kugawa mipaka ya maneno, miongoni mwa njia hizo ni, neno kama kipashio cha maana, neno kama kipashio cha kifonetiki au kifonolojia na neno kama kipashio huru na kisicho gawanyika (Rubanza, 2010). Ni vigumu kuwa na fasili toshelevu ya neno, sababu kubwa au kiini cha....

Friday, 29 November 2013

NADHARIA YA UDENGUZINADHARIA YA UDENGUZI KATIKA UHAKIKI WA WAHUSIKA WA TAMTHILIA ZA KISWAHILI
Wahusika ni kitu muhimu katika kazi yoyote ya kifasihi, kwani ndio wanaosukuma mbele kazi ya kifasihi. Wataalamu mbalimbali wamezungumzia kwa namna tofauti maana na ujitokezaji wa wahusika wa kazi ya fasihi. Hii ni taka enzi za Ugiriki ya kale hadi katika fasihi ya kiswahili.
Mulokozi (1996) anasema hadithi ya tamthilia husonga mbele kwa njia ya vitendo na mazungumzo ya wahusika. Hivyo anaonesha bila wahusika hata mazungumzo hayatakuwepo.
Brecht (1898-1956) aliibua kanuni ya ukengeushi ambayo aliitumia kukengeuka kanuni za Kiaristotle. Moja kati ya ukengeushi wake ulikuwa ni katika kipengele cha wahusika. Ambapo kwa Aristotle mhusika mkuu katika Tanzia alikuwa ni lazima atoke tabaka la juu, lakini kwa Brecht haikuwa lazima kwa mhusika kutoka tabaka la juu. Lengo la Brecht lilikuwa kuonesha kuwa hata tabaka la chini linaweza kuleta mabadiliko katika jamii.

Kanuni/dhana hii ya Brecht inalandana na nadharia ya udenguzi/ujenguzi. Udenguzi ni nadharia ya kihakiki iliyoanzishwa na mwanafalsafa wa Kifaransa Jacques Darrida (1973), ambapo anasema ujuzi na maarifa si vitu vinavyoweza kueleweka moja kwa moja, katika matini yoyote ile ujuzi hutumika katika kuunda matini hiyo, kwa kuwa ujuzi si kitu kinachoweza kueleweka moja kwa moja

Thursday, 28 November 2013

SINTAKSIA


Katika kategoria zilizokuwa ndani ya Kiswahili ni neno la kategoria gani huchagua kategoria ipi?
Makala haya yatajadili  maana ya kategoria, yataainisha kategoria mbalimbali za maneno kwa mujibu wa wataalamu, yatajadili kategoria gani huchagua kategoria ipi katika tungo za Kiswahili, yatabainisha sababu zinazopelekea kategoria kuchaguana na kujaribu kuunda kanuni mbalimbali na hatimaye kuhitimisha.
Kategoria za maneno ni aina za maneno kadri ya uainisho wake kutegemeana na sifa za maneno husika kuwekwa katika kundi moja. Mfano Kategoria ya Nomino, Kategoria ya vitenzi, kategoria ya vivumishi.
Kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili Sanifu (2004) maneno yameainishwa katika makundi nane. Makundi hayo ni Nomino, Kitenzi, Kivumishi, Kiwakilishi, Kielezi, Kihusishi, Kihisishi na Kiunganishi. Ambapo kategoria hizi zimepangwa kulingana na sifa za maneno yanayoingia ndani yake.  

Kihore na wenzake (2003) wanaainisha kategoria saba za maneno nazo ni nomino, vitenzi, vivumishi, viwakilishi, viunganishi, vielezi na viingizi.
Kwa pamoja wataalam hawa wanakubaliana kuwepo kwa kategoria za maneno ingawa wanatofutiana katika idadi ya aina za kategoria.Tofauti hizi zinatokana na baadhi ya maneno yanaonekana kutoingia katika kategoria zilizoainishwa. Kwa mfano kategoria ya maneno kama

Wednesday, 27 November 2013

UAMILIAJI LUGHA


SARUFI MAJUMUI NA UAMILIAJI LUGHA YA PILI.
Makala haya yataangalia maana ya sarufi majumui, masuala ya msingi yanayohusu maarifa ya lugha, sifa za sarufi majumui, sarufi majumui na uamiliaji lugha ya pili na mwisho tathmini.
Kwa mujibu wa Chomsky (1976:29) kama alivyonukuliwa na Ellis (1996:430) sarufi majumui ni mfumo wa kanuni na sheria ambazo ni msingi wa lugha za binadamu (tafsiri yangu). Muasisi wa nadharia hii ni Noam Chomsky.
Msingi wa nadharia hii ni kwamba binadamu anapozaliwa anakuwa na maarifa asilia ambayo humsaidia katika ujifunzaji lugha; mambo ya ndani na nje ambao husaidia katika uamiliaji wa lugha. Maarifa haya hupatikana pale tu binadamu anapozaliwa kwani huwa na kifaa cha uamiliaji lugha ambacho kinakuwa na kanuni majumui na kanuni badilifu ambazo hukutana na tajiriba (uwezo wa jamii katika lugha) na kusababisha uamiliajli lugha kutokea.

Waamiliaji wa lugha ya kwanza huwa na maarifa asilia ambayo huwawezesha kuiamili lugha yao kwa kutumia maarifa hayo. Hivyo

UTENDI WA SON-JARA


UTENDI WA SON- JARA
Dhana ya utendi katika fasihi ya Kiswahili, iliwahi kuzua utata baada ya Ruth Finnegan (1970) kusema kwamba Afrika hakuna tendi bali kuna simulizi za kisifo. Hoja hii aliipa uzito kutokana kwamba aliangalia tendi andishi na kusahau tendi simulizi. Vilevile vipengele muhimu vya tendi simulizi hakuvipa umuhimu kama vile usimulizi na utendaji. Vigezo muhimu alivyovitaja ni :
(1)Utendi uwe na umbo la kinudhumu.
(2)Urefu.
(3)Uzungumzie maisha ya shujaa.
(4)Muunganiko wa matukio.
Kutokana na vigezo hivyo aliona kwamba kuna tendi zenye sifa hizo, isipokuwa sifa ya nudhumu na tendi hizo ni Son-Jara, Mwendo na Lianja. Madai yake yaliibua wataalamu mbalimbali kufatiti na...

UTENZI WA NYAKIIRU KIBI


USHUJAA WA NYAKIIRU KIBI NA KANYAMAISHWA KWA KUTUMIA RUWAZA NA SIFA ZA SHUJAA WA KIAFRIKA
I. UTANGULIZI
Makala haya yatashughulikia vipengele vifuatavyo:- Usuli wa mwandishi,Usuli wa utendi, kiunzi cha nadharia,  ruwaza za shujaa na sifa za shujaa wa utendi wa Kiafrika, uhusishaji wa hoja na ruwaza zilizotolewa na wataalam wa tendi za Kiafrika, uhusishaji wa hoja na sifa za shujaa zilizotolewa na wataalam wa tendi za Kiafrika na hitimisho.
2. USULI WA MWANDISHI (MTUNZI)
Mtunzi wa kitabu cha Nyakiiru Kibi ni Mugyabuso Mlinzi Mulokozi. Amezaliza tarehe  5/6/1950 huko mkoani Bukoba. Mtunzi huyu ameoa na ana watoto wanne (4). Alisoma shule ya awali ya Kashasha huko Bukoba 1958-1961. Alipata elimu ya msingi na kati mwaka 1962-1965 katika shule ya Kigarama. Elimu ya sekondari katika shule ya Kahororo huko Bukoba. Kidato cha tano na sita alisoma shule ya Mkwawa huko Iringa. Mwaka 1975, Mulokozi alitunukiwa shahada ya kwanza ya elimu katika Chuo Kikuu Cha Dar es salaam. Mwaka 1987 alitunukiwa  shahada ya uzamivu (ph.D) katika chuo hichohicho.  Mtaalam huyu, aliwahi kushika nyadhifa...

UTENZI WA KALEVALA


UTENZI WA KALEVALA

UTANGULIZI
Kalevala ni utenzi wa taifa la Finiland uliotungwa na Elias Lönnrot mnamo karne ya kumi na tisa. Utenzi huu uliandikwa kwa mara ya kwanza kwa lugha ya Kisuomi na baadaye kutafsiriwa katika lugha nyingi ikiwemo lugha ya Kiswahili. Tafsiri kwa lugha ya Kiswahili ilifanywa na Jan Knappert. Utendi huu umetafsiriwa kwa Kiswahili kutokana na ushirkiano uliopo kati ya Chama cha Fasihi cha Finland na Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Utenzi wa Kalevala unahusu ustawi wa nchi ya Kalevala na mgogoro uliokuwepo kati ya nchi hiyo na utawala wa nchi ya...

UTENDI WA HAMZIYYAH


RUWAZA YA SHUJAA KAMA INAVYOJIDHIHIRISHA KATIKA UTENDI WA HAMZIYYAH.
USULI WA UTENDI WA HAMZIYYAH
Utendi wa Hamziyya ni kasda maarufu inayohusu ulimwengu wa dini ya kiislamu, chanzo cha utendi huu ni uarabuni, utendi huu uliotungwa na Muhammad bin Said Al-Busiri. Tafsiri kwa Lugha ya Kiswahili ilifanywa na Sharrif Aidarus.
Asili ya utendi huu ni kasda inayoitwa Kasidatul’l Hamziyyah fi ‘l-mada’ihi’ n Nabawiya ambayo ilihusu maneno ya kumsifu na kumtakia heri Mtume Muhammad. Kwa Kiswahili utendi huu umekuwa kama Chuo cha Hamziyyah au Maulid ya Hamziyyah au Hamziyyah tu.

FUMO LIYONGO


UHAKIKI WA UTENZI WA FUMO LIYONGO KAMA UTENDI WA KIAFRIKA
Makala haya yamejadili utendi wa Fumo Liyongo kama utendi wa Kiafrika. Makala yamegawanywa katika sehemu tatu, sehemu ya kwanza ni utangulizi ambapo tumeanza kwa kuelezea usuli wa mwandishi na usuli wa utendi wa Fumo Liyongo. Sehemu ya pili ni ya mjadala kuhusu utendi wa Fumo Liyongo kama utendi wa Kiafrika na sehemu ya mwisho ni hitimisho.    
UTANGULIZI
Usuli wa mwandishi
Kwa mujibu wa Mulokozi (1999:6) Muhammad Abubakar Kijumwa alikuwa ni mwenyeji wa Lamu nchini Kenya. Alikuwa msanii mashuhuri ambaye mbali na kutunga mashairi na tendi, alikuwa mchongaji wa milango yenye nakshi, msanii-msanifu, msawidi na mnukuzi wa miswada ya zamani. Habari za maisha yake hazijulikani vizuri. Alianza kujitokeza katika utunzi miaka ya 1980, alipoanza kuwasaidia watafiti wa kizungu waliotaka kufahamu habari za Waswahili. Alifariki mwanzoni mwa miaka ya 1940. Mbali na Utendi wa Fumo Liyongo, Kijumwa alitunga mashairi kadha ambayo si mashuhuri, ukiwemo Utendi wa Helewa.

Tuesday, 26 November 2013

UFUNDISHAJI LUGHA

UFUPISHO WA SURA YA PILI KATIKA HAMMERLY, H (1982) SYNTHESIS IN SECOND LANGUAGE TEACHING: AN INTRODUCTION TO LINGUISTICS.
LUGHA
Wakati wa vita Waziri Mkuu alikuwa akimalizia hotuba yake bungeni kwa kusema, "Tutakilinda kisiwa chetu kwa gharama yoyote, tutapigana ufukweni, tutapigana nchi kavu, tutapigana milimani, bila kukata tamaa...."Hii ilikuwa ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Winston Churchill tarehe 4.6.1940 bungeni na kuibua ghasia na kila aliyeisikia hataisahau hotuba hii. Mfano huu unaonyesha jinsi lugha inavyojitokeza kuanzia silabi moja mpaka kufikia usemaji wenye ufasaha na kupata waandishi makini.
Lugha ni nini?
Wataalamu mbalimbali wanatofautiana kuhusu maana ya lugha. Kwa karne nyingi wanafalsafa waandishi, wanasaikolojia na wanaisimu wametoa maana mbalimbali za lugha. Tukirejea kwenye Isimu na sayansi ya lugha kuna maana mbalimbali za lugha kama ilivyo Isimu. Kutokana na maana mbalimbali zilizotolewa tunaweza kuwa na maana ya jumla kama ifuatavyo:

Sunday, 17 November 2013

HADITHI

       MAJUTO NI MJUKUU  

Hapo zamani za kale, hapa kwetu kijijini,
Kijiji kilo vutia, pande zote za dunia,
Walifurika wageni, maajabu jionea,
Masikini mwananchi, majuto ni mjukuu.

Ardhi yenye madini, mito mbuga za wanyama,
Viumbe wa maajabu, mlima wenye theluji,
Maziwa yalofurika, viumbe kila aina,
Maskini mwananchi, majuto ni mjukuu.


Friday, 15 November 2013

SANAA YA USHAIRI


USHAIRI
Shaaban Robert katika uandishi wa ushairi ameandika Tenzi na mashairi ya kimapokeo.
Tenzi: Ni aina ya mashairi ya kimapokeo wenye sifa zifuatazo:
 • Kimaudhui; Ni utungo wenye maudhui yanayosimulia kwa urefu tukio fulani maalum. Waweza kuwa wasifu wa mtu au jambo la kihistoria. Mfano; S. Robert ameandika utenzi wa vita vya Uhuru, ameeleza kuhusu historia. Pia katika Mapenzi Bora, ameeleza kuhusu sifa za mapenzi bora.
 • Utenzi ni utungo wa pili kati tungo za ushairi zenye beti nyingi. Utungo wa kwanza unaoongoza kuwa na beti nyingi kuliko zote katika ushairi ni Tendi. Lakini hapa tutaangazia tenzi zaidi.

Wednesday, 13 November 2013

SHAABAN ROBERT


DHANA YA MAPENZI KATIKA KAZI ZA SHAABAN ROBERT
Mapenzi ni hali ya kuingiwa moyoni na kuthamini mtu au kitu zaidi ya mwingine au kingine.
Pia mapenzi ni hali ya kujali jambo, kitu au mtu zaidi ya mwingine. S. Robert amejaribu kufafanua dhana ya mapenzi kama dhana pana sana, anaeleza kuwa:
 • Mapenzi ni hali ya kumpenda Mungu
 • Mapenzi ni yale ya kupendana sisi kwa sisi
 • Mapenzi ni yale yasiyo bagua umri, kabila au kazi, taifa, rangi nk.
 • Mapenzi ni yale yasiyojali tofauti baina ya watu
 • Mapenzi ni ile hali ya kupendana bila kikomo 
 • Mapenzi ni yale ya kuridhika na hali zetu. Mfano; katika kitabu chake cha Mapenzi Bora nk,

KITUSHI


KITUSHI CHA BABU NA MJUKUU
Mjukuu:      Babu hebu nisaidie Mjukuu wako! maana naona maluweluwe. Hivi Babu! kile, vile, hivi na hivyo vilianza vile, hivyo au vilevile na wale je au ndo’ walewale. Maana wengi wanasema eti sawa na sawasawa ni sawasawa!! Napata mkanganyiko. Alafu na wale je? Walianza vile au vilevile kama wale? Mbona nashindwa kuelewa naona uvulivuli tu!! kati ya kile, kilekile, vile, vilevile na hivi, hivihivi na alafu tena eti hivyo na hivyo hivyo! ni sawa lakini si sawasawa!! Hapo Babu ndipo ninaposhaa’ maana kama vile ni vilevile na hivyo ni hivyohivyo na sawa ni sawasawa, sasa kwa nini vile vina kuwa hivyo, au vinakuwa sawasawa? Na kama hivyo ni vile au ni sawa na si sawasawa mbona sisi tuko hivi na si vile? Na kama kweli ni hivi kwa nini wewe unang’ang’ania vile na si hivyo wala hivyohivyo na wala hivi. Au Babu labda kwa sababu ya kale kamsemo kako ka Jembe kwanza?” na kale wimbo kako kenye ubeti mmoja wenye vipande mshororo vitatu vyenye vina vya ukwapi, utao na mwanda!! huku kakiwa na uradidi wa neno moya!! teh!eeeee teheeee! teh!eeee teh! teh! teh! teh!...ha ha haha ha haaa…!!

TAMTHILIA


UANDISHI WA TAMTHILIA
Tamthilia ni nini?
 • Tamthilia ni utanzu ambao hutegemea mazungumzo na uigizaji ili kuwasilisha ujumbe wake. Huu ni utanzu ambao huandikwa kwa mtindo wa mazungumzo ya wahusika (Wamitila, 2007).
 • Nkwera (h.t) anaelezea kuwa tamthilia ni: Tamthilia ni mchezo wa kuigiza au utungo wa kisanaa ambao huweka wazo fulani katika matendo na mazungumzo (Nkwera, h.t)
AINA ZA TAMTHILIA
 • Kwa mujibu wa Aristotle, kuna aina mbili za tamthilia. Aina ya kwanza ni tanzia na nyingine ni ramsa.
 • Tanzia ni nini?

Tuesday, 12 November 2013

MOTIFU YA SAFARI


MOTIFU YA SAFARI NA MSAKO KAMA MWEGA MKUU WA DHAMIRA KATIKA “MARIMBA YA MAJALIWA”
“Marimba ya Majaliwa ni hadithi iloyoandikwa na Edwini Semzaba mwaka (2008) ambayo inaelezea kuhusiana na marimba ya Majaliwa iliyopotea. Mwandishi ameonyesha jinsi Majaliwa alivyokuwa anatafuta marimba yake mpaka akaipata. Majaliwa alisafiri kwa kutumia njia mbalimbali kama vile ungo, fagio, na maumbo ya samaki akizunguka Tanzania nzima akisaka marimba ya nyuzi ishirini (20). Alianza Mafia, akaenda Zanzibar, Tanga, Moshi na Arusha, Iringa, Mwanza, Kigoma, na miji mingine mingi. Na Kongoti bingwa wa Taifa wa Marimba akimchenga kila mara huku akinga’nga’nia Marimba ya Majaliwa ili amzuie kushinda na ashinde yeye na bila Marimba yenye nyuzi ishirini (20) hakuna ushindi.

Friday, 8 November 2013

SHAIRI


NI WAPI TUMEKOSEA?

Mhadhara nafungua, halaiki karibuni,
Hoja yangu naitoa, kwa makini nyambueni,
Msipandwe na hisia, mkavuruga amani,
Yangu hoja inahoji, NI WAPI TUMEKOSEA?
Tumetenda ndivyo sivyo, kwa kuwaza sivyo ndivyo,
Kwangu mimi ndivyo hivyo, yote nimeona hivyo,
Nanyi wazeni vilivyo, mnene kama ilivyo,
Yangu hoja inahoji, NI WAPI TUMEKOSEA?