TASWIRA YA KIFO CHA SHUJAA KATIKA
UTENDI: SHUJAA LIYONGO NA EMANUEL KATIKA
BIBLIA
CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM
Ngoliga Foibe
SEHEMU YAKWANZA
Utangulizi
Makala hii imekusudia kufafanua taswira ya kifo cha shujaa katika utendi kwa kurejelea kifo cha shujaa Liyongo kama alivyoelezwa katika kitabu cha Tenzi Tatu za Kale kilichohaririwa na Mulokozi mwaka (1999) na shujaa Emanuel (Yesu Kristo) kama anavyoelezwa katika Biblia takatifu.
Kabla ya kujikita katika ufafanuzi huo ni muhimu kufahamu dhana ya kifo, taswira, shujaa na utendi. Kwa kuanza na dhana ya utendi, Mulokozi (1996) anaeleza kuwa, utendi ni hadithi ya kishairi kuhusu mashujaa wa kihistoria na wa kubuni, wa jamii au taifa. Anaendelea kueleza kuwa baadhi ya tendi zina sifa za kiriwaya, ila tu badala ya kuwa katika umbo la nathari zina umbo la kishairi.
Vile vile Mulokozi (1999) anarekebisha kidogo fasili yake na kueleza kuwa utendi ni utungo mrefu wa kishairi wenye kusimulia hadithi ya ushujaa na mashujaa. Ukizichunguza fasili hizi utagundua kuwa tendi zina sifa ya kishairi, zinatokana na masimulizi (zilizo nyingi), zinahusu mashujaa ambao wanaweza kuwa wa kihistoria au wa kubuni. Pamoja na sifa hizo tendi pia huhusu masuala mengine ya kijamii kama vile kutoa mawaidha kwa jamii, hivyo si lazima utendi umhusu shujaa peke yake.
Dhana ya kifo inaweza kufasiliwa kuwa ni kitendo cha kutolewa uhai au kupatwa na mauti kama ambavyo Mohamed (2002) ameeleza kuwa kisawe cha kifo ni mauti au ufu. Vile vile Wamitila (2003) amefafanua dhana ya taswira kuwa hutumiwa kuelezea neno, kirai au maelezo ambayo yanaunda picha fulani katika akili ya msomaji. Anaendelea kueleza kuwa, taswira zinaweza kuwa za kimaelezo ... (yaani maelezo fulani yaliunda picha) au za ki-ishara (zinazounda picha ambayo inaashiria jambo fulani au imeficha ujumbe mwingine).
Kwa mujibu wa Wamitila (2003) neno shujaa, hutumika kuelezea mhusika mkuu katika kazi ya kifasihi ambaye anaweza kuwa wa kike au wa kiume. Kimsingi neno hili haliashirii wema tu.
Mulokozi (1996) kwa upande mwingine ameeleza kuwa, mashujaa wa utendi wa Kiswahili ni wa aina tatu (3) ambazo ni mashujaa wa kijadi wa Kiafrika, kwa mfano Fumo Liyongo katika Utendi wa Fumo Liyongo (Mohamed Kijumwa K 1913) na Abushiri bin Salim katika Utendi wa Vita vya Wadachi Kutamalaki Mrima (Hemed Abdallah K, 1895), mashujaa wa kidini, hasa mtume Muhamadi na masahaba wake (k.m. utendi wa Ras ‘lghuli) na mashujaa wa kubuni kwa mfano Tajiri katika Utendi wa Masahibu.
Mulokozi anaendelea kueleza kuwa, kati ya aina hizo tatu za mashujaa, riwaya ya Kiswahili imetumia mbili tu. Wahusika wa kijadi wa Kiafrika na wahusika wa kubuni. Wahusika wa kidini hawajatumiwa kikamilifu (uk. 42) Kutokana na ufafanuzi huu ni dhahiri kuwa, mashujaa wa kidini bado hawajaelezwa ipasavyo na ndio sababu makala hii imejikita katika kuelezea angalau kwa sehemu kuhusu shujaa Emanuel katika Biblia akihusishwa na shujaa wa kihistoria na wa kijadi Fumo Liyongo katika Utendi wa Fumo Liyongo.
Baada ya kufahamu utangulizi huu, sehemu inayofuata itahusu historia ya mashujaa waliokwisha tajwa hapo juu.
SEHEMU YA PILI
HISTORIA YA SHUJAA FUMO LIYONGO NA EMANUEL
1.1 Historia ya Shujaa Fumo Liyongo
Fumo Liyongo ni shujaa kama alivyoelezwa na Muhamadi Kijunwa mwaka 1913 katika Utendi wa Fumo Liyongo. Mwandishi amesimulia habari za shujaa huyu kwa njia ya maandishi katika umbo la kishairi. Japo kuna utata kuhusu tarehe aliyozaliwa Liyongo lakini tarehe inayoelekea kukubaliwa zaidi ni ile ya karne ya 13 – 14 kwa kuwa kitabu cha Terehe ya Pate (Freeman-Grenville 19962: 241 – 299) kinamtaja mtawala wa eneo la Ozi aitwaye Fumo Liyongo aliyeishi wakati wa utawala wa Fumomari (Fumo Omari), mtawala wa ki-Nabhany wa dola ya Pate. Fumomari alitawala miaka ya 740 – 795 Hijriya (Miaka ya Kiislamu), sawa na 1340 – 1393 M. Liyongo huyo alipigana na Fumomari (Mulokozi 1999).
Mwandishi huyu anaendelea kutujuza kuwa vyanzo vinaonesha kuwa Liyongo aliishi Pwani ya Kaskazini mwa Kenya kwenye maeneo ya Pate na Ozi kwenye karne ya 14 au kabla. Mama yake aliitwa Samoa mwana. Liyongo alikuwa kiongozi katika jamii yake, japo hakuna uhakika kama alikuwa mfalme. Alikuwa shujaa, manju wa ngoma na malenga, na mwindaji hodari. Kwa upande wa dini, hakuna uhakika kama alikuwa ana Mkristo au Mwislamu japo nyimbo zake zinaonesha kuwa huenda alikuwa mfuasi wa dini ya Jadi ya Waswahili. Liyongo alikuwa akiwinda na kufanya biashara sehemu za bara karibu na Pate, aliweka makazi yake Ozi, na alifia na kuzikwa Kipini, mahali paitwapo Ungwana wa Mashaha (Mulokozi na Sengo 1995:52-53). Ubeti wa 230 unaeleza kwa muhtasari maisha ya shujaa Fumo Liyongo
1.2 Historia ya Shujaa Emanuel
Emanuel ni shujaa wa kidini ambaye anaelezwa katika maandiko matakatifu yaani Biblia. Kuzaliwa kwa shujaa huyu kulitabiriwa na nabii Isaya (Isaya 9:6) sura ya 9 kifungu / mstari wa 6.
Tangu utabiri wa Isaya hadi kuzaliwa kwake inakadiriwa kuwa ni miaka 400 k.k. Utabiri wa nabii Isaya ulitimia katika kitabu cha Mathayo 2:1 ambapo inaeleza kuwa shujaa alizaliwa Bethlehemu ya Uyahudi zamani za Mfalme Herode. Kama ilivyo desturi ya mashujaa wengi wa kidini , baada tu ya kuzaliwa alikutana na vikwazo vya kutaka kuuawa na Mfalme Herode ambaye alihofia kunyang’anywa madaraka, shujaa huyu atakapokuwa mkubwa (Math 2:13). Malaika wa Bwana alimtokea Yusufu (Baba wa Emanuel) katika ndoto kumweleza kuwa amchukue mtoto Emanuel na mama yake (Mariam) kisha wakimbilie Misri. Ndivyo ilivyo hata kwa mashujaa wengine, misukosuko inapozidi kukimbilia uhamishoni. Baada ya Mfalme Herode kufa shujaa Emanuel alirudishwa na wazazi wake Galilaya katika mji wa Nazareti.
Shujaa Emanuel alibatizwa na Yohana katika mto Yordani. Baada ya kubatizwa Roho wa Mungu alishuka juu yake kisha sauti ilisikika kutoka mbinguni ikisema “Huyu ni mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye” (Math 3:13 – 17). Shujaa huyu alibatizwa akiwa mtu mzima yapata miaka 27. Baada ya kubatizwa alipelekwa na Roho Mtakatifu nyikani ili ajaribiwe na ibilisi, alifunga siku arobaini, mchana na usiku, kisha alishinda majaribu yote ya Ibilisi (Shetani) (Math. 4:1 – 11).
Baada ya shujaa Emanuel kutoka nyika ni alichagua wanafunzi (wafuasi) kumi na mbili (12) ambao alikuwa anafanya nao kazi, na ndipo alipoanza huduma ya kuihubiri habari njema ya Ufalme wa Mungu na kuponya ugonjwa na udhaifu wa kila namna kwa watu (Math 4:17 – 25) akiwa na miaka 27. Baadhi ya wanafunzi, wake ni Simoni Petro, Andrea, Yohana. n.k. Habari za shujaa huyu ilienea kutoka Galilaya, Dehapoli, Yerusalemu, Uyahudi na ng’ambo ya Yordani. Shujaa Emanuel alifanya huduma kwa muda wa miaka mitatu kisha akafa. Wakati wa huduma ya kuwakomboa watu na dhambi zao, wapo waliomkubali na kumfuata na wengine walimchukia na kumshutumu kuwa alikufuru kwa kujiita mwana wa Mungu. Wale waliomchukia ndio waliofanya njama za kumuua. Hatimaye walimtumia mmoja wa wanafunzi wake aliyeitwa Yuda kwa kumpa vipande 30 (thelathini) vya fedha ili amsaliti kisha wamkamate. Yuda aliwaambia, nitakayembusu ndiye, na hapo ndipo Wayahudi walipomkamata shujaa huyu na kumsulubisha hadi kifo chake (Marko 14:10-72 na 15:1-37).
SEHEMU YA TATU
Taswira ya Kifo cha shujaa Liyongo na Emanuel katika Biblia
1. Taswira ya Kifo cha shujaa Liyongo
Liyongo ni shujaa aliyependwa na watu kwa kuwa aliwapigania na kuwasaidia, mfano aliwasaidia Waggala kupata mbegu bora (ub 40 – 41), aliishi porini na Watwa na kushirikiana nao vizuri, ushirikiano uliomsaidia kumnusuru na njama za mfalme za kutaka kumuua.
Kutokana na uhusiano mzuri aliokuwa nao na jamii yake Mfalme anamwonea wivu na anaogopa kuwa anaweza kumpokonya madaraka (ufalme). Anafanya njama za kumuua. Njama hizo hazifanikiwi na inabidi mfalme amtumie mwanawe Liyongo ili amsaliti baba yake kwa kuahidiwa kuozwa binti mfalme, kupewa uwaziri na mali nyingi. Mtoto wa Liyongo anamuuliza babaye siri ya nguvu zake, anapoambiwa kuwa ni kuchomwa sindano ya shaba kitovuni, anakubali kumchoma baba yake hatimaye Liyongo anakufa, kisha mwanawe naye anakufa kutokana na uovu wake.
Baada ya shujaa Liyongo kufa watu walisikitika, waliomboleza na wengine walionekana kukata tamaa kwa kuwa shujaa huyu alikuwa ni mtetezi wa watu katika jamii. Beti za 224 – 226 zinaeleza vizuri jinsi watu walivyomwombolezea shujaa wao.
Taswira ya kifo cha shujaa Liyongo inaweza kujitokeza kwa namna tatu (3). Kwanza kifo cha shujaa Liyongo kwa mfalme ni mafanikio kwa kuwa ana uhakika wa kuendelea kutawala maana alikuwa na hofu kuwa Fumo Liyongo atamnyang’anya ufalme kwa vile alivyokuwa na mshikamano na watu. Pili, kifo cha Liyongo kwa mwanawe ni adhabu kwani baada ya shujaa huyu kufa mwanawe naye alikufa kutokana na maradhi yasiyopona (ubeti 223) pamoja na kuchukiwa na jamii yote kwa ujumla. (beti za 217 – 222). Tatu kifo cha Liyongo kwa jamii yake ni sawa na kupoteza kitu chenye thamani kwa vile Liyongo alikuwa na mshikamano na jamii yake. Baada ya kifo chake watu wanaomboleza na wanaonekana kukosa matumaini, haya yanayojitokeza katika (beti za 224 – 227).
Kwa upande wa fasihi, kifo cha shujaa Liyongo kimejengwa katika dhana ya usaliti unaosababishwa na tamaa ya madaraka (Ufalme) na tamaa ya mali (Mtoto wa Liyongo). Mfalme (sultani) wa Pate anafanya fitina (Ubeti 49) za kumuua Liyongo akiogopa kupokonywa ufalme (ub. 93). Mwanawe Liyongo naye alikubali kumsaliti baba yake kwa matarajio ya kuozwa mke (binti wa mfalme), kupewa mali na uwaziri pia. Dhana ya usaliti imejitokeza sana katika kazi za kifasihi na inaonekana kuwa ni silaha ya kumwangusha shujaa mfano Lwanda Magere katika kitabu cha Lwanda Magere, Samsoni na Yesu katika Biblia. Kwa upande mwingine dhana hii ina sura mbili yaani faida (anayenufaika baada ya usaliti) na hasara (anayeathirika baada ya usaliti).
Kifo cha shujaa pamoja na usaliti vinatupatia motifu ya dhambi na mapatilizi. Ingawa mtoto wa Liongo alimsaliti babaye ili apewe zawadi nono hakutimiziwa ahadi hizo. Alinyanyaswa na hatimaye alikufa kama alivyokufa baba yake. Hii inaashiria kuwa katika mapigano kati ya wema na uovu, siku zote wema hushinda. Kwa hiyo hata sultani hana maisha marefu. Historia imelishuhudia hili kwa kuwa muda si mrefu uatawala wa kisultani ulivamiwa na ukoloni, hata huo ukoloni nao leo hii haupo. Maisha ya milele ni maisha ya kutenda wena na haki
2. Taswira ya Kifo cha Shujaa Emanuel katika Biblia
Shujaa Emanuel alitabiriwa kuwa atazaliwa, atakufa na siku ya tatu atafufuka na kupaa mbinguni. Jina Emanuel lina maana ya Mungu pamoja nasi. (Math 1:22-23) maneno “Mungu pamoja nasi” yanarejesha uhusiano kati ya Mungu na mwanadamu ambao ulipotea katika bustani ya Edeni baada ya Adamu na hawa kutenda dhambi. Baada ya anguko (dhambi) la Adamu na hawa, Mungu aliwaacha wanadamu kwa kuwa yeye ni mtakatifu na hashirikiani (hashikamani) na uchafu (Mwanzo 3:1 – 24).
Kwa kuwa mwanadamu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu (Mwanzo 1:26 – 27), Mungu aliwahurumia na kuamua kuwaokoa tena kutoka katika utumwa wa dhambi na matendo ambayo shetani alikuwa akiwafanyia baada ya lile anguko la bustani ya Edeni. Kwa sababu hiyo aliamua kumtoa mwanawe wa pekee Yesu Kristo (Emanuel) afe msalabani ili awakomboe wanadamu. Hivyo, kila atakayemwamini shujaa Emanuel (Yesu Kristo) ataokolewa atoke katika utumwa huo wa dhambi na mateso yote ya Ibilisi na ndipo atakuwa ameunganishwa na Mungu yaani uhusiano wake na Mungu utarejeshwa tena yaani Mungu atakuwa pamoja naye.
Kifo cha shujaa Emanuel, japo kilitabiriwa kwa kuwa Mungu aliamua kuwarudia tena wanadamu lakini Yuda Iskariote ndiye aliyepelekea kifo hiki kutokea. Alimsaliti Emanuel kwa Wayahudi kwa tamaa ya pesa ya vipande thelathini (30). Kama ilivyokuwa kwa shujaa Liyongo, Emanuel naye alisalitiwa na mtu wa karibu. (Mwanafunzi wake) kama Waswahili wasemavyo “Kikulacho ki nguoni mwako” (Luka 22:47). Habari za kifo cha shujaa huyu zimeelewa vizuri katika vitabu hivi: Mathayo sura ya 26-27, Marko sura ya 14 – 15, Luka sura ya 22 – 23 na Yohana sura ya 13 – 19. Yuda aliyemsaliti Yesu, baada ya kupewa vipande 30 vya fedha alimbusu Yesu, na Wayahudi, Waandishi na Mafarisayo wakamkamata na kumtesa hadi alipokufa.
Taswira ya kifo cha shujaa Emanuel kinajitokeza kwa namna mbalimbali kama ifuatavyo: Kwanza Wayahudi, Waandishi na Mafarisayo waliona kama wamemkomoa kwa kuwa walidai kuwa anajikweza kwa kujifanya mwana wa Mungu. Pia watawala walifurahi maana watu wengi walimfuata na kumsikiliza.
Pili, kifo cha Emanuel kilipoteza matumaini ya watu waliokuwa wakimwamini, ndugu zake (k.v. wazazi) pamoja na wanafunzi wake. Watu walilia na kuomboleza pale msalabani kwa kuwa mtetezi wao ametoweka japokuwa waliahidiwa kuwa siku ya tatu atafufuka.
Tatu, kifo cha Emanuel kwa Mungu kilikuwa ni kutimiza kusudi lake la kuwakomboa wanadamu, kwa kuwa alifanyika sadaka ya dhambi yaani alijitoa kafara ili wanadamu wasife tena kwa dhambi. Itakumbukwa kwamba jithada za kumuua zilianza tangu akiwa mchanga, lakini hazikufua dafu... hatimaye sasa zinafua dafu akiwa mtu mzima....... hii inaashiria kitu gani?
Nne, katika muktadha wa kifasihi tunaona nguvu ya usaliti katika kumwangusha shujaa. Usaliti umeonekana ukifanya kazi au kulisababisha shujaa kuanguka. Hata katika maisha ya kawaida ya kila siku dhana hii inatenda kazi kwani tunashuhudia watu wakijiua kwa kuwa wamesalitiwa na wapenzi wao, ndugu au marafiki zao.
Kwa ujumla suala la usaliti limesawiriwa vizuri katika kazi mbili za Utendi wa Fumo Liyongo na Biblia. Waandishi wamejitahidi kuonesha dhana hii kwa kuwatumia wahusika Liyongo na Emanuel. Kwa mtazamo wangu, baada ya kuwachambua mashujaa hawa naona kuwa usaliti ni kipimo kinachotumika kupima nguvu aliyonayo shujaa, na nguvu inapobainika na watu wengine ndipo anguko la shujaa hutokea. Mara nyingi anguko la shujaa husababishwa na watu wake wa karibu. Ukaribu huu mara nyingi huwa ni ukaribu wa kimwili, kwani ndio unaonesha udhaifu mkubwa.
SEHEMU YA NNE
A. Kufanana na kutofautiana kwa shujaa Liyongo na Emanuel
1. Kufanana
Mashujaa hawa wanafanana katika mambo yafuatayo
(i) Wote wanatumia nguvu isiyokuwa ya kawaida kutenda mambo ya ajabu (miujiza).
(ii) Walikuwa na ushirikiano mzuri na jamii zao.
(iii) Walipendwa na watu kiasi cha watawala kuwachukia
(iv) Walifanyiwa njama za kuuawa
(v) Wote walisalitiwa na watu wao wa karibu
(vi) Baada ya kufa watu waliwaombolezea.
(vii) Wasaliti wa mashujaa wanaahidiwa kupewa fedha, vyeo na mali nyingine baada ya kukamilisha kazi ya usaliti mfano Mfalme anaahidi kuwapa Wasanye, Wadahalo, Waboni na Watwa reale mia iwapo watamleta kichwa cha Liyongo. Pia mwanae Liyongo anaahidiwa mali, mke na cheo cha uwaziri. Pia Yuda aliahidiwa vipande thelathini vya fedha iwapo atafanikisha kukamatwa kwa shujaa Emanuel.
(viii) Waliowasaliti mashujaa Liyongo na Emanuel walikufa baada ya kifo cha mashujaa hao
(ix) Hawakuwa waoga, wote ni majasiri.
2. Kutofautiana Kwao
Shujaa Fumo Liyongo
|
Shujaa Emanuel
|
||
(i)
|
Fumo Liyongo
alitumia nguvu ya uganga au sihiri. Hadhuriki
kwa chochote isipokuwa kwa kudungwa sindano ya shaba kitovuni. (ubeti 143 – 144)
|
(i)
|
Alitumia nguvu
za Roho Mtakatifu kutenda mambo mbalimbali k.v. kutembea juu ya maji, kuponya
watu wengine (Mathayo 3:13-17, Mathayo 4: 23 – 25).
|
(ii)
|
Alioa mke na
alikuwa na mtoto wa kiume, ana nguvu za kirijali
|
(ii)
|
Hakuoa wala
hakuzaa
|
(iii)
|
Baada ya kufa
hakufufuka
|
(iii)
|
Alifufuka na
aliwatokea watu mbalimbali ili kuwadhihirishia kwamba yuko hai (Marko
16:1-14)
|
(iv)
|
Hakupaa kwenda
mbinguni
|
(iv)
|
Alipaa kwenda
mbinguni kuketi mkono wa kiume wa Mungu.
|
(v)
|
Hakufanikiwa
kuikomboa jamii yake kwa kuwa alikufa
|
(v)
|
Japo alikufa
kazi ya kuwakomboa wanadamu ilikamilika kwa kuwa kila atakayemwamini
ataokolewa na kupatanisha na Mungu.
|
B. Hitimisho
Katika kuhitimisha uchambuzi wa makala hii imebainika kuwa kila shujaa kati ya hao wawili alikuwa na wajibu fulani katika jamii yake ambao ilibidi autimize. Katika kutimiza wajibu huo shujaa lazima akutane na vikwazo ambavyo inabidi apambane na ashinde ili alete ukombozi kwa jamii yake. Katika kupambana huko, wapo watakaomuunga mkono na wengine kumpinga.Wale wanaompinga ndio hufanya njama za kumwangusha, wakifanikiwa shujaa hushindwa na wasipofanikiwa ndipo shujaa huyo hushinda na hivyo huleta mabadiliko katika jamii yake.
C. MAREJEO
Bible Societies of Tanzania and Kenya (1997). Biblia: Maandiko Matakatifu ya Mungu. The Bible Societies of Kenya and Tanzania: Nairobi na Dodoma (Mtawalia)
Graf, H. (1980). The Panarama Bible Study Coarse No. 1: The Plan of the Ages (Toleo la 1 la Kijerumani – Kiswahili. Kanisa la Biblia Publishers: Dodoma.
Mohamed, M.A. na Saidi, A.M (2002). Kamusi ya Visawe. East African Educational Publishers Ltd: Nairobi.
Mulokozi, M.M. (1996). Fasihi ya Kiswahili. Chuo Kikuu Huria cha Tanzania: Dar es Salaam.
Mulokozi, M.M. (Mh.) (1999). Tenzi Tatu za Kale. TUKI: Dar es Salaam.
Wamitila, K.W. (2003). Kamusi ya Fasihi, Istilahi na Nadharia. Focus Publications Ltd: Nairobi.
hongera nyote mliohuisika katika uchapishaji huu
ReplyDeleteHongera! Kazi njema 🙏
ReplyDelete