“ISIMUJAMII
NA ISIMU KAMA TAALUMA MBILI, HUTOFAUTIANA LAKINI KIMSINGI HUKAMILISHANA.”
Taaluma
ya isimujamii ilianza huko Marekani katika miaka ya 50 na 60. Ilianza na
wanasosiolojia kama vile Fishman (1971) na wanaanthropolojia kama vile Del
Hymes (1972) na wengine ni wanaisimu kama vile akina Labov William (1972),
Gumperz (1972) na Bright William (1965). Wataalamu hawa walitaka kujua tofauti
za tamaduni ngeni huko Marekani ambapo kulikuwepo na wamarekani wenye asili ya
kiafrika na wamarekani wahindi (wahindi wekundu). Hivyo walitaka kuzifahamu
tamaduni hizo ngeni ili waweze kuzifanyia kazi katika elimu. Na hapo ndipo
isimujamii ilipoanza Mekacha (2000).
Katika
kufasili isimujamii Msanjila na wenzake (2011) wanasema kwamba, wataalamu
mbalimbali wa lugha wanakubaliana kimsingi kwamba isimujamii ni taaluma
inayoshughulika na uchunguzi unaolenga kufafanua uhusiano uliopo kati ya isimu
na jamii. (kwa mfano Trudgill 1983; Hudson 1985 na Mekacha 2000).
Msanjila
na wenzake wanaendelea kusema kuwa, ‘kwa kifupi isimujamii ni taaluma
inayoshughulikia matumizi ya lugha katika jamii. Yaani taaluma hii inajaribu
kuelezea uhusiano uliopo baina ya lugha na jamii.’ Kwa mtazamo huu ni wazi
kwamba kuna uhusiano mkubwa sana baina ya lugha na jamii.
Vilevile wataalamu wengine wanaoonekana
kushadidia mtazamo huu ni kama vile Besha (2007:13) anasema kuwa, isimujamii ni
utanzu unaojishughulisha na uchunguzi jinsi lugha inavyotumika katika jamii.
Pia
King’ei (2010:1) anasema isimujamii ni taaluma inayoeleza uhusiano wa karibu
uliopo kati ya matumizi ya lugha na maisha ya jamii.
Vilevile
wataalam wengi wanaonekana kuwa na muelekeo sawa katika kufasili dhana ya isimu,
kwani wengi wao wanakubaliana kwamba, Isimu ni taaluma ya ufafanuzi, uchambuzi
na uchunguzi wa lugha kwa kutumia mbinu za kisayansi. (kwa mfano Massamba
2004:19; Mgullu 1990:1 akiwarejea wanaisimu mbalimbali kama vile Richard na
wenzake 1985)
Pia
Mgullu akimrejea Hartman (1972) anasema kwamba Isimu ni eneo maalumu la mtalaa
ambalo lengo lake huwa ni kuchunguza lugha. Wanaisimu huzungumza lugha zikiwa
ni nyenzo muhimu za mawasiliano ya mwanadamu.
Kwa
mtazamo huu wa wanaisimu hawa Massamba, Richard na wenzake pamoja na
Hartman nina kubaliana nao kwa kiasi
kikubwa kutokana na kwamba katika fasili zao jambo la msingi linalosisitizwa ni
kwamba, Isimu hushughulikia uchunguzi wa lugha mbalimbali kwa kutumia misingi
ya kisayansi. Hivyo kutokana na uchunguzi wake ndipo hupelekea Isimu kuitwa sayansi
ya lugha.
Pamoja
na hayo vilevile kwa upande mwingine fasili hizi zimeweka msisitizo katika
mfumo wa mawasiliano ya wanadamu. Hivyo basi kwa mujibu wa fasili hizi
inaonesha kuwa, Isimu na mwanadamu ni vitu ambavyo hushikamana kama pande mbili
za sarafu ambazo si rahisi kuzitenganisha.
Fasili
hizi za wataalamu hawa ni sawa na kusema kwamba, isimu na isimujamii ni sawa na
pande mbili za sarufi moja ambazo (hutofautiana) zina picha mbili tofauti
zisizoweza kutenganishwa bila kupoteza thamani ya sarafu.
Hivyo
basi, tofauti hizo na mkamilishano huo huweza kuonekana katika vipengele
vifuatavyo; tukianza na tofauti;
Ukongwe:
tofauti nyingine ipo katika umri. Isimu ni taaluma kongwe sana ukilinganisha na
isimujamii. Kwa mujibu wa Mekacha
akiwanukuu Viktoria Fromkin na Robert Rodman, ambao wanasema kuwa isimu
ilianza huko bara Arabu mwaka 1600 kabla ya Kristo, wakati isimujamii ilianza miaka
ya 1950 na 1960, na kupata mashiko zaidi kwenye miaka ya 1960 na 1971 ambapo
machapisho mengi ya isimujamii yalianza kuonekana. Pia ni taaluma ambayo
ilizaliwa kutokana na taaluma nyingine za isimu na zisizo za isimu.
Uchangamani;
isimujamii ni taaluma yenye uchangamani yaani inahusisha taaluma mbili ambazo
ni isimu na jamii wakati isimu yenyewe si taaluma changamani.
Maana;
Isimu na isimujamii hutofautiana katika maana, kama tulivyoona hapo juu kwamba
isimu yenyewe ni taalauma inayozingatia ufafanuzi, uchambuzi na uchunguzi wa
lugha kwa kutumia mbinu za kisayansi, wakati isimujamii yenyewe ni taaluma
inayoshughulika na uchunguzi unaolenga kufafanua uhusiano uliopo kati ya lugha
na jamii.
Tofauti
nyingine kati ya isimu na isimujamii ni kwamba, isimu inafuata mkabala wa ki-Chomsky
wa kuchambua lugha kwa misingi ya kidhahania kuwa haina tofauti ndani yake.
Wakati isimujamii hutambua kuwa lugha ina tofauti ndani yake, yaani ni mfumo
wenye mifumo mingi ndani yake. Hivyo basi
huona kuwa ni jukumu la isimujamii kuzitafiti na kuzifafanua tofauti
hizo.
Tofauti
nyingine iko katika vipengele; vipengele vinavyoshughulikiwa na isimu ni
tofauti na vile vinavyoshughulikiwa na isimujamii. Kwa mfano, isimujamii hushughulikia
vipengele kama vile, uhusiano kati ya lugha na utamaduni (elimu), matumizi ya
lugha tofauti wakati mmoja, kama katika wingilugha, ubadilishaji msimbo na
diglosia. Matumizi ya aina tofauti za lugha na mazingira yake, kama lahaja,
rejesta na mtindo. Pia hushughulikia vipengele mbalimbali vya mawasiliano
kupitia maoni ya msemaji (tawi hilo pia huitwa isimuamali). Matumizi ya lugha
baini ya jamii za watu tofauti, kama lugha mawasiliano, pijini na kreoli, upangaji
lugha na sera za lugha. Lakini isimu yenyewe hushughulikia vipengele kama
fonolojia, fonetiki, mofolojia, sintaksia na semantiki.
Pia
Florian Coulmas (1997), anadai kuwa tofauti kati ya isimu na isimujamii,
isimujamii ni taaluma ambayo hujihusisha tu na ufafanuzi wa lugha kama
inavyoonekana ikitumika katika mazingira halisi. Hivyo basi, kwa maoni yake, si
jukumu la isimujamii kutafuta na kuchanganua data kuthibitisha au kukanusha
nadharia yoyote kama ilivyo katika isimu. Kwa sababu hiyo isimijamii ni
“taaluma bila nadharia.” Hii ni kwa mujibu wa Mekacha (2000:31) akimnukuu
Coulmas (1997).
Vile
vile tofauti nyingine kati ya isimu na isimujamii ipo katika matawi/tanzu; kwa
mujibu wa Mgullu (1990:4) isimu ni taaluma pana kuliko isimujamii, hii hujidhihirisha
katika matawi yake ambayo mojawapo ni isimujamii yenyewe, matawi mengine ni
isimufafanuzi na isimukiafrika, isimuhistoria, isimulinganishi, isimutumizi,
isimutiba, isimufalsafa.
Pamoja
na kutofautiana kwa taaluma hizi mbili yaani isimu na isimujamii bado taaluma hizi
hukamilishana na vilevile hutegemeana, yaani ili kimoja kiwepo lazima kingine
kiwepo. Mkamilishano wa taaluma hizi
huweza kuoneshwa kama ifuatavyo;-
Kwa
mujibu wa Mekacha (2000:22), isimujamii inapo bainisha uhusiano uliopo wa
kijamii kati ya vilugha vilivyomo ndani ya lugha moja hutumia isimu ambayo
ndiyo sayansi ya lugha. Hivyo ili isimujamii ifikie lengo hili hutumia njia ya
sayansi ya lugha (isimu). Kwa kufanya hivyo hudhihirisha utegemezi na
mkamilishano uliopo baina ya isimu na isimujamii. Mwanaisimujamii huanza kwa
kujiuliza; Je, kutokana na tofauti za kifonetiki, kifonolojia, kimofolojia,
kisintaksia na kisemantiki inawezekana kubainisha vilugha gani, katika lugha
moja? Hivyo basi mwanaisimujamii ili aweze kubainisha vilugha vilivyopo katika
lugha moja itambidi aihusishe isimu ambayo ndiyo taaluma ya sayansi ya lugha.
Na kwa kufanya hivyo huonesha mkamilishano.
Pia
katika kutafiti na kufafanua tofauti tofauti zilizopo ndani ya lugha (isimu)
kama taaluma inayojishughulisha na kufafanua tofauti za lugha kwa njia ya
kisayansi ni lazima ishirikiane na isimujamii kama taaluma inachunguza matumizi
ya lugha katika jamii. Kutokana na kutegemeana kwa taaluma hizi mbili
husababisha ukamilishano baina ya isimu na isimujamii.
Vilevile isimujamii hutafiti na kufafanua
nafasi ya lugha katika jamii kama lengo mojawapo, katika kufanya hivyo hutumia
isimu, kwa kuwa isimu ni sayansi ya lugha hivyo ni lazima mbinu za kiisimu
zitumike ili kufikia lengo hilo. Hivyo basi kitendo cha kutumia mbinu za
kisayansi katika lengo hili la kuitafiti na kuifafanua nafasi ya lugha katika
jamii ndiyo huonesha ukamilishano huo kati ya isimu na isimujamii.
Mkamilishano
mwingine katika ya isimu na isimujamii upo katika isimujamii ya mawandafinyu. Kwa
mujibu wa Msanjila na wenzake (2011:12) wanasema kwamba, mwanaisimu Labov
(1972) katika utafiti wake alioufanya katika jiji la New York Marekani kwa
lengo la kutaka kujua sababu za tofauti za
uzungumzaji, Labov amechunguza na kufafanua maswala ya isimujamii kwa
mtazamo wa kiisimu katika kuelezea isimujamii.
Pia
katika mkabala wa mawandamapana sababu za uteuzi wa lugha kuchukua dhima ya
kitaifa, yaani kuwa lugha ya taifa, kuwa lugha rasmi au kuwa lugha ya
kufundishia hazitokani na sababu za kiisimu pekee au kiisimujamii pekee bali
hazinabudi zitokane na sababu za pande zote mbili yaani kiisimu na kiisimujamii
(Msanjila na wenzake 2011:13). Kwa kigezo hiki ukamilishano huonekana dhahiri.
Msanjila
na wenzake (2011:9) wanasema kwamba, kwa kusikiliza mazungumzo ya watu
mbalimbali utagundua kuwa kuna vibainishi vya lugha ambavyo ni vya kisayansi
(isimu) anavyovitumia mwanaisimujamii katika kubainisha aina ya watu
wanaohusika katika mazungumzo. kama ni wajamii fulani, mfano wamakonde,
wasukuma au wanyakyusa, wasomi au si wasomi. Vibainishi hivyo vyaweza kuwa ni
vya kifonolojia, kimofolojia, kileksika na kifonetiki. Mfano wazungumzaji
wengine hutamka /ch/ingine badala ya
/k/ingine, /n/tu badala ya /m/tu au ‘thatha’ badala ya sasa. Hivyo
mwanaisimujamii habaini haya endapo tu ataihusisha taaluma ya isimu.
Pia
Besha (2007:10) anasema kuwa, “lengo la isimu si kuwafundisha watu jinsi ya
kuzungumza lugha yao, yaani kipi waseme na kipi waache. Bali lengo la isimu ni
kuweka wazi kanuni zinazotawala lugha ambazo wazungumzaji wanazitumia bila wao
wenyewe kuzijua.” Hivyo katika kuweka kanuni hizo jambo la msingi awali ya yote
ni lazima isimu ijue ni namna gani lugha inatumika katika jamii. Kutokana na
hoja hii inajidhihirisha wazi kuwa isimu itategemea matokeo ya utafiti wa isimujamii
juu ya matumizi ya lugha katika jamii ndipo iweze kuweka kanuni hizo. Hivyo
basi isimu na isimujamii ni taaluma mbili zinazokamilishana.
Isimu
na isimujamii haviwezi kutenganisha kwani taaluma zote hizi mbili hutegemeana
na hukamilisha. Hivyo basi ili isimu ikamilishe malengo yake hutumia isimujamii
kwani katika jamii ndimo lugha hutumika, hali kadhalika isimujamii haiweza
kubaini tofauti za uzungumzaji katika jamii pasipo kuihusisha isimu ambayo
ndiyo sayansi ya lugha. Kwa mtazamo huu isimu na isimujamii huweza kuonekana
kama pande mbili za sarafu moja zilizo na picha mbili tofauti katika kila
upande, ambazo kimsingi hukamilishana na kuipa thamani sarafu hiyo.
MAREJEO:
Besha,
R.M. (1994). Utangulizi wa Lugha na Isimu.
Dar es salaam. Dar es salaam University Press.
King’ei,
K. (2010). Misingi ya Isimujamii.
Taasisi ya Taaluma za Kiswahili. Chuo Kikuu cha Dar es salaam.
Mekacha,
R.D.K. (2000). Isimujamii: Nadharia na
Muktadha wa Kiswali. Osaka University of Foreign Studies.
Mgullu,
R.S. (1999). Mtalaa wa Isimu.
Longhorn. Nairobi.
Msanjila,
Y.P. na wenzake. (2011). Isimujamii:
Sekondari na vyuo. (Toleo la pili).TUKI. Dar es salaam.
Kazi nzuri!
ReplyDeleteKazi mfuti
ReplyDeleteKazi mfuti
ReplyDelete