Wednesday 3 July 2013

ISIMUJAMII NA ISIMU


“Isimujamii na Isimu kama taaluma mbili, hutofautiana lakini kimsingi hukamilishana.”
Taaluma ya isimujamii ilianza huko Marekani katika miaka ya 50 na 60. Ilianza na wanasosiolojia kama vile Fishman (1971) na wanaanthropolojia kama vile Del Hymes (1972) na wengine ni wanaisimu kama vile akina Labov William (1972), Gumperz (1972) na Bright William (1965). Wataalamu hawa walitaka kujua tofauti za tamaduni ngeni huko Marekani ambapo kulikuwepo na wamarekani wenye asili ya kiafrika na wamarekani wahindi (wahindi wekundu). Hivyo walitaka kuzifahamu tamaduni hizo ngeni ili waweze kuzifanyia kazi katika elimu. Na hapo ndipo isimujamii ilipoanza Mekacha (2000).
Katika kufasili isimujamii Msanjila na wenzake (2011) wanasema kwamba, wataalamu mbalimbali wa lugha wanakubaliana kimsingi kwamba isimujamii ni taaluma inayoshughulika na uchunguzi unaolenga kufafanua uhusiano uliopo kati ya isimu na jamii. (kwa mfano Trudgill 1983; Hudson 1985 na Mekacha 2000).

Msanjila na wenzake wanaendelea kusema kuwa, ‘kwa kifupi isimujamii ni taaluma inayoshughulikia matumizi ya lugha katika jamii. Yaani taaluma hii inajaribu kuelezea uhusiano uliopo baina ya lugha na jamii.’ Kwa mtazamo huu ni wazi kwamba kuna uhusiano mkubwa sana baina ya lugha na jamii.
 Vilevile wataalamu wengine wanaoonekana kushadidia mtazamo huu ni kama vile Besha (2007:13) anasema kuwa, isimujamii ni utanzu unaojishughulisha na uchunguzi jinsi lugha inavyotumika katika jamii.
Pia King’ei (2010:1) anasema isimujamii ni taaluma inayoeleza uhusiano wa karibu uliopo kati ya matumizi ya lugha na maisha ya jamii.
Vilevile wataalam wengi wanaonekana kuwa na muelekeo sawa katika kufasili dhana ya isimu, kwani wengi wao wanakubaliana kwamba, Isimu ni taaluma ya ufafanuzi, uchambuzi na uchunguzi wa lugha kwa kutumia mbinu za kisayansi. (kwa mfano Massamba 2004:19; Mgullu 1990:1 akiwarejea wanaisimu mbalimbali kama vile Richard na wenzake 1985)
Pia Mgullu akimrejea Hartman (1972) anasema kwamba Isimu ni eneo maalumu la mtalaa ambalo lengo lake huwa ni kuchunguza lugha. Wanaisimu huzungumza lugha zikiwa ni nyenzo muhimu za mawasiliano ya mwanadamu.
Kwa mtazamo huu wa wanaisimu hawa Massamba, Richard na wenzake pamoja na Hartman  nina kubaliana nao kwa kiasi kikubwa kutokana na kwamba katika fasili zao jambo la msingi linalosisitizwa ni kwamba, Isimu hushughulikia uchunguzi wa lugha mbalimbali kwa kutumia misingi ya kisayansi. Hivyo kutokana na uchunguzi wake ndipo hupelekea Isimu kuitwa sayansi ya lugha.
Pamoja na hayo vilevile kwa upande mwingine fasili hizi zimeweka msisitizo katika mfumo wa mawasiliano ya wanadamu. Hivyo basi kwa mujibu wa fasili hizi inaonesha kuwa, Isimu na mwanadamu ni vitu ambavyo hushikamana kama pande mbili za sarafu ambazo si rahisi kuzitenganisha.
Fasili hizi za wataalamu hawa ni sawa na kusema kwamba, isimu na isimujamii ni sawa na pande mbili za sarufi moja ambazo (hutofautiana) zina picha mbili tofauti zisizoweza kutenganishwa bila kupoteza thamani ya sarafu.
Hivyo basi, tofauti hizo na mkamilishano huo huweza kuonekana katika vipengele vifuatavyo; tukianza na tofauti;
Ukongwe: tofauti nyingine ipo katika umri. Isimu ni taaluma kongwe sana ukilinganisha na isimujamii. Kwa mujibu wa Mekacha  akiwanukuu Viktoria Fromkin na Robert Rodman, ambao wanasema kuwa isimu ilianza huko bara Arabu mwaka 1600 kabla ya Kristo, wakati isimujamii ilianza miaka ya 1950 na 1960, na kupata mashiko zaidi kwenye miaka ya 1960 na 1971 ambapo machapisho mengi ya isimujamii yalianza kuonekana. Pia ni taaluma ambayo ilizaliwa kutokana na taaluma nyingine za isimu na zisizo za isimu.
Uchangamani; isimujamii ni taaluma yenye uchangamani yaani inahusisha taaluma mbili ambazo ni isimu na jamii wakati isimu yenyewe si taaluma changamani. 
Maana; Isimu na isimujamii hutofautiana katika maana, kama tulivyoona hapo juu kwamba isimu yenyewe ni taalauma inayozingatia ufafanuzi, uchambuzi na uchunguzi wa lugha kwa kutumia mbinu za kisayansi, wakati isimujamii yenyewe ni taaluma inayoshughulika na uchunguzi unaolenga kufafanua uhusiano uliopo kati ya lugha na jamii.
Tofauti nyingine kati ya isimu na isimujamii ni kwamba, isimu inafuata mkabala wa ki-Chomsky wa kuchambua lugha kwa misingi ya kidhahania kuwa haina tofauti ndani yake. Wakati isimujamii hutambua kuwa lugha ina tofauti ndani yake, yaani ni mfumo wenye mifumo mingi ndani yake. Hivyo basi  huona kuwa ni jukumu la isimujamii kuzitafiti na kuzifafanua tofauti hizo.
Tofauti nyingine iko katika vipengele; vipengele vinavyoshughulikiwa na isimu ni tofauti na vile vinavyoshughulikiwa na isimujamii. Kwa mfano, isimujamii hushughulikia vipengele kama vile, uhusiano kati ya lugha na utamaduni (elimu), matumizi ya lugha tofauti wakati mmoja, kama katika wingilugha, ubadilishaji msimbo na diglosia. Matumizi ya aina tofauti za lugha na mazingira yake, kama lahaja, rejesta na mtindo. Pia hushughulikia vipengele mbalimbali vya mawasiliano kupitia maoni ya msemaji (tawi hilo pia huitwa isimuamali). Matumizi ya lugha baini ya jamii za watu tofauti, kama lugha mawasiliano, pijini na kreoli, upangaji lugha na sera za lugha. Lakini isimu yenyewe hushughulikia vipengele kama fonolojia, fonetiki, mofolojia, sintaksia na semantiki.
Pia Florian Coulmas (1997), anadai kuwa tofauti kati ya isimu na isimujamii, isimujamii ni taaluma ambayo hujihusisha tu na ufafanuzi wa lugha kama inavyoonekana ikitumika katika mazingira halisi. Hivyo basi, kwa maoni yake, si jukumu la isimujamii kutafuta na kuchanganua data kuthibitisha au kukanusha nadharia yoyote kama ilivyo katika isimu. Kwa sababu hiyo isimijamii ni “taaluma bila nadharia.” Hii ni kwa mujibu wa Mekacha (2000:31) akimnukuu Coulmas (1997).
Vile vile tofauti nyingine kati ya isimu na isimujamii ipo katika matawi/tanzu; kwa mujibu wa Mgullu (1990:4) isimu ni taaluma pana kuliko isimujamii, hii hujidhihirisha katika matawi yake ambayo mojawapo ni isimujamii yenyewe, matawi mengine ni isimufafanuzi na isimukiafrika, isimuhistoria, isimulinganishi, isimutumizi, isimutiba, isimufalsafa.
Pamoja na kutofautiana kwa  taaluma hizi mbili  yaani isimu na isimujamii bado taaluma hizi hukamilishana na vilevile hutegemeana, yaani ili kimoja kiwepo lazima kingine kiwepo.  Mkamilishano wa taaluma hizi huweza kuoneshwa kama ifuatavyo;-
Kwa mujibu wa Mekacha (2000:22), isimujamii inapo bainisha uhusiano uliopo wa kijamii kati ya vilugha vilivyomo ndani ya lugha moja hutumia isimu ambayo ndiyo sayansi ya lugha. Hivyo ili isimujamii ifikie lengo hili hutumia njia ya sayansi ya lugha (isimu). Kwa kufanya hivyo hudhihirisha utegemezi na mkamilishano uliopo baina ya isimu na isimujamii. Mwanaisimujamii huanza kwa kujiuliza; Je, kutokana na tofauti za kifonetiki, kifonolojia, kimofolojia, kisintaksia na kisemantiki inawezekana kubainisha vilugha gani, katika lugha moja? Hivyo basi mwanaisimujamii ili aweze kubainisha vilugha vilivyopo katika lugha moja itambidi aihusishe isimu ambayo ndiyo taaluma ya sayansi ya lugha. Na kwa kufanya hivyo huonesha mkamilishano.
Pia katika kutafiti na kufafanua tofauti tofauti zilizopo ndani ya lugha (isimu) kama taaluma inayojishughulisha na kufafanua tofauti za lugha kwa njia ya kisayansi ni lazima ishirikiane na isimujamii kama taaluma inachunguza matumizi ya lugha katika jamii. Kutokana na kutegemeana kwa taaluma hizi mbili husababisha ukamilishano baina ya isimu na isimujamii.
 Vilevile isimujamii hutafiti na kufafanua nafasi ya lugha katika jamii kama lengo mojawapo, katika kufanya hivyo hutumia isimu, kwa kuwa isimu ni sayansi ya lugha hivyo ni lazima mbinu za kiisimu zitumike ili kufikia lengo hilo. Hivyo basi kitendo cha kutumia mbinu za kisayansi katika lengo hili la kuitafiti na kuifafanua nafasi ya lugha katika jamii ndiyo huonesha ukamilishano huo kati ya isimu na isimujamii.  
Mkamilishano mwingine katika ya isimu na isimujamii upo katika isimujamii ya mawandafinyu. Kwa mujibu wa Msanjila na wenzake (2011:12) wanasema kwamba, mwanaisimu Labov (1972) katika utafiti wake alioufanya katika jiji la New York Marekani kwa lengo la kutaka kujua sababu za tofauti za  uzungumzaji, Labov amechunguza na kufafanua maswala ya isimujamii kwa mtazamo wa kiisimu katika kuelezea isimujamii.
Pia katika mkabala wa mawandamapana sababu za uteuzi wa lugha kuchukua dhima ya kitaifa, yaani kuwa lugha ya taifa, kuwa lugha rasmi au kuwa lugha ya kufundishia hazitokani na sababu za kiisimu pekee au kiisimujamii pekee bali hazinabudi zitokane na sababu za pande zote mbili yaani kiisimu na kiisimujamii (Msanjila na wenzake 2011:13). Kwa kigezo hiki ukamilishano huonekana dhahiri.
Msanjila na wenzake (2011:9) wanasema kwamba, kwa kusikiliza mazungumzo ya watu mbalimbali utagundua kuwa kuna vibainishi vya lugha ambavyo ni vya kisayansi (isimu) anavyovitumia mwanaisimujamii katika kubainisha aina ya watu wanaohusika katika mazungumzo. kama ni wajamii fulani, mfano wamakonde, wasukuma au wanyakyusa, wasomi au si wasomi. Vibainishi hivyo vyaweza kuwa ni vya kifonolojia, kimofolojia, kileksika na kifonetiki. Mfano wazungumzaji wengine hutamka /ch/ingine badala ya /k/ingine, /n/tu badala ya /m/tu au ‘thatha’ badala ya sasa. Hivyo mwanaisimujamii habaini haya endapo tu ataihusisha taaluma ya isimu.
Pia Besha (2007:10) anasema kuwa, “lengo la isimu si kuwafundisha watu jinsi ya kuzungumza lugha yao, yaani kipi waseme na kipi waache. Bali lengo la isimu ni kuweka wazi kanuni zinazotawala lugha ambazo wazungumzaji wanazitumia bila wao wenyewe kuzijua.” Hivyo katika kuweka kanuni hizo jambo la msingi awali ya yote ni lazima isimu ijue ni namna gani lugha inatumika katika jamii. Kutokana na hoja hii inajidhihirisha wazi kuwa isimu itategemea matokeo ya utafiti wa isimujamii juu ya matumizi ya lugha katika jamii ndipo iweze kuweka kanuni hizo. Hivyo basi isimu na isimujamii ni taaluma mbili zinazokamilishana. 
Isimu na isimujamii haviwezi kutenganisha kwani taaluma zote hizi mbili hutegemeana na hukamilisha. Hivyo basi ili isimu ikamilishe malengo yake hutumia isimujamii kwani katika jamii ndimo lugha hutumika, hali kadhalika isimujamii haiweza kubaini tofauti za uzungumzaji katika jamii pasipo kuihusisha isimu ambayo ndiyo sayansi ya lugha. Kwa mtazamo huu isimu na isimujamii huweza kuonekana kama pande mbili za sarafu moja zilizo na picha mbili tofauti katika kila upande, ambazo kimsingi hukamilishana na kuipa thamani sarafu hiyo.
MAREJEO:
Besha, R.M. (1994). Utangulizi wa Lugha na Isimu. Dar es salaam. Dar es salaam University Press.
King’ei, K. (2010). Misingi ya Isimujamii. Taasisi ya Taaluma za Kiswahili. Chuo Kikuu cha Dar es salaam.
Mekacha, R.D.K. (2000). Isimujamii: Nadharia na Muktadha wa Kiswali. Osaka University of Foreign Studies.        
Mgullu, R.S. (1999). Mtalaa wa Isimu. Longhorn. Nairobi.
Msanjila, Y.P. na wenzake. (2011). Isimujamii: Sekondari na vyuo. (Toleo la pili).TUKI. Dar es salaam.
                          

2 comments:

  1. Hujambo ndugu msomaji! Ningependa kujua kama malumbano ya utani na tamathali za usemi zinaweza kushirikishwa kama vipengee vya isimujamii. Ahsante.

    ReplyDelete
  2. Hujambo kaka, maoni uangu ni kwamba vioengee hivi haviathiri kaida za matumixlzi ya lugha hivyo having nafasi katika kuelezea isimujamii, ila ni mifani mahususi ya mayumizi ya lugha katika jamii.
    Asanty.

    ReplyDelete