UHUSIANO WA SEMANTIKI NA TAALUMA NYINGINE
Makala haya yatashughulikia semantiki na taaluma zingine zinazokaribiana nazo kama semiolojia, leksikolojia, leksikografia na pragmantiki kwa kuangalia ufanano na utofauti wake na mwisho hitimisho.
“ wakati fonolojia, mofolojia, na sintaksia ni taaluma zinazohusu matamshi, maumbo, na miundo, semantiki inaangalia maana ya matamshi, maumbo na miundo katika lugha. Anaendelea kusema, maana ni sehemu ya umilisi na ufahamu wa lugha, kujifunza lugha ni kukubaliiana na maana za vipengele vyote vilivyopo katika lugha”
Massamba (2004:75) anafasili dhana ya semantiki kuwa ni taaluma ya isimu inayojishughulisha na uchunguzi na uchambuzi wa maana za maneno na tungo katika lugha. Semantiki imegawanyika katika makundi manne ambayo ni leksika, mantiki, muundo na nadharia.
hata hivyo hakuna ufafanuzi wa kutosha kuhusu maana ingawa katika hali ya kawaida tunaishia kutoa sifa za kitu na siyo maana.
Pamoja na Semantiki kuangalia maana kama ilivyojadiliwa hapo juu, ni dhahiri kuwa si taaluma pekee inayochunguza maana, kuna taaluma zingine zinazojitofautisha na Semantiki katika kuchunguza maana, miongoni mwa taaluma hizo ni Pragmatiki, Semiolojia, Leksikolojia na Leksikografia.
Kwa kuanza, Pragmatiki ni taaluma inayohusika na uchunguzi wa maana zinazohusiana na muktadha wa utumizi wa lugha, tofauti na semantiki inayochunguza maana kadri matamshi au maandishi yanavyojidhihirisha yenyewe, katika Pragmatiki muktadha unajumuisha msemaji, msikilizaji, mahali, wakati na mada ya mazungumzo.
Yule (1996) anafasili pragmatiki kuwa ni uchunguzi wa maana katika muktadha wa mazungumzo au maandishi na inavyofasiliwa na msikilizaji au msomaji.
Semantiki na pragmatiki ni matawi yanayoshughulikia maana katika sentensi, semantiki inashughulikia maana za maneno na kuangalia muundo wa vipashio katika sentensi na pragmatiki inashughulikia maana inayohusisha muktadha.
Pragmatiki inashughulikia maana isiyo ya msingi bali maana inayotokana na muktadha husika kwa mfano neno mtoto katika muktadha wa kimapenzi ni msichana wakati semantiki inashughulika na maana ya msingi ambayo inatoa fasili kulingana na kitu kinavyoonekana kwa mfano neno mtoto litafasiliwa kama ni kiumbe kinachozaliwa na binadamu ambacho kina umri chini ya miaka kumi na nane.
Pragmatiki huangalia lugha kama chombo cha mawasiliano na hubadilika kutokana muktadha kwa mfano jua limezama kama mzungumzaji yupo katika muktadha wa wafugaji basi ni muda wa mifugo kuingia katika zizi wakati semantiki inaangalia lugha kama mfumo dhahania wa alama zinazofafanua kilichoandikwa kwa mfano jua limezama kwa maana ya msingi usiku umeingia.
Kuna wataalamu mbalimbali wanaofasili dhana ya leksikolojia kama kipengele kinachokaribiana na semantiki, baadhi yao ni;
Ullmann (1962) ambaye anafasili leksikolojia kama ni tawi la isimu linaloshughulikia mofolojia na maana ya maneno.
Doroszewksi (1973) kama alivyonukuliwa na Mdee (2010) amefafanua leksikolojia kuwa ni tawi la isimu linalochunguza etimolojia, maana na matumizi ya maneno.
Hivyo basi leksikolojia ni tawi la isimu linalochunguza maana, mofolojia, etimolojia na matumizi ya maneno.
Uhusiano wa semantiki na leksikolojia; taaluma zote zinashughulikia maana za maneno, leksikolojia inashughulikia maana zinazopatikana kwenye kamusi na mabadiliko ya maana za maneno kwa mfano neno mtoto maana msingi ni kiumbe anayezaliwa na binadamu na maana nyingine ni mpenzi na semantiki huangalia maana ya msingi kwa mfano neno mama ni mzazi wa kike.
Pamoja na ufanano huo lakini kuna tofauti zake, semantiki haishughulikii etimolojia ya neno, tunapozungumzia etimolojia tuaangalia asili ya neno kama ni la kiarabu ama la kiingereza wakati leksikolojia hushughulikia etimolojia ya maneno kwa mfano neno kitabu limetokana na neno la kiarabu
Semantiki huchunguza uhusiano wa kimaana kisarufi na kimuundo yaani maana katika matamshi, maumbo na sintaksia wakati leksikolojia huchunguza uhusiano wa maana katika leksimu kwa mfano neno fikia, kuwa mahali fulani baada ya safari, hivyo leksikolojia imefasili maana katika kiwango cha neno.
Katika kuangalia dhana ya semiolojia Massamba (2004) amefasili semiolojia kama taaluma ya kisayansi inayojishughulisha na uchunguzi na uchanganuzi wa mifumo ya ishara mbalimbali ikiwa inazingatia zaidi uhusiano baina ya kiwakilishi na kitajwa.
Ferdinand de Saussure kama alivyonukuliwa na Morris (1971) amefasili semiolojia ni uhusiano kati ya alama na kitu, jambo au hali ya kitu inavyowakilishwa, akaaendelea alama ni kiashiria na kitu ni kiashiriwa. Hakuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya kiashiria na kiashiriwa.
Charles (1934) alishughulikia dhana ya semiotiki kwa kuunda tanzu tatu ambazo ni sintaksia, Pragmatiki na semantiki.
Sintaksia ni taaluma ya uhusiano kati ya ishara na vitu/ vielezo jinsi vinavyotumika, pragmatiki ni taaluma ya uhusiano kati ya mfumo wa ishara na mtumiaji wake na semantiki ni taaluma ya uhusiano kati ya maana na ishara. Hivyo basi semiotiki ni taaluma inayoshughulikia maana za ishara/ taswira.
Semiotiki hushughulikia neno kama kiwakilishi (utajo) cha kile kitajwa pia hushughulikia maana ya msingi. Hivyo semiotiki inaona maana inapatikana kupitia taswira. Yaani kila taswira lazima inakuwa na maana inayowakilisha. Kwa mfano rangi nyekundu duniani inaashiria upendo hivyo maana ya upendo iliyojitokeza imetokana na taswira ya rangi hiyo.
Hivyo katika taaluma hii maana zote za maneno zimefumbatwa katika alama. Ni dhahiri kwamba ingawa semiolojia na semantiki hushughukia maana, semiolojia kwa kiasi kikubwa hujihusisha na alama za kitaswira na vielezo kwa kiasi kidogo wakati semantiki huchunguza maana katika mfumo wa ishara wa lugha inayozungumzwa na binadamu.
Semantiki inatofautiana na semiolojia kwani semantiki inashughulikia alama za lugha yaani kila lugha huwa na alama zinazoashiria kitu fulani wakati alama za semiolojia hazihusu lugha yaani huwa ni maana za mawasiliano, mfano ishara za mawingu, wanyama kama bundi ishara ya uchawi.
Vilevile katika kipengele hiki tunaona jinsi dhana ya leksikografia ilivyofafanulia, uhusiano na tofauti yake na semantiki.
Mdee (2010) anafasili leksikografia ni kazi ya kisanaa na kisayansi ya kutunga kamusi ambayo hujumuisha uorodheshaji wa msamiati wa lugha inayotungiwa kamusi pamoja na maelezo yenye kufafanua kila neno lililoorodheshwa kadri ya mahitaji ya mtumiaji wa kamusi aliyelengwa.
Semantiki na leksikografia huchambua maana na sifa za neno na uhusiano wa kimaana wa maneno yenye kuunda kikoa maana. Katika leksikografia maana za maneno zinapatikana katika fasili ya leksimu. Hivyo leksikografia huangalia maana inayopatikana kupitia fasili, pia taarifa mbalimbali zinazoingizwa katika kamusi kama za etimolojia, maana/fasili, matamshi, taarifa za matumizi humsaidia msomaji kupata maana ya leksimu.
Matawi haya yanatofautiana, kwa kiasi fulani, wakati taaluma ya leksikografia ikishughulikia maana kama sehemu tu ya vigezo vyake katika kutunga kamusi, semantiki huchunguza maana kama kiunzi kinachobeba dhana nzima ya semantiki, bila maana hakuna semantiki.
Kwa kuhitimisha semantiki inahusiana na taaluma hizo kwani taaluma zote zimejikita katika kuangalia maana ya lugha, ingawa kila taaluma inaangalia maana hiyo kwa namna tofauti tofauti. Pia taaluma zote ni taaluma za lugha, hivyo zinachangia kwa kiasi kikubwa kuonesha jinsi gani lugha inavyojiumbia maana kutokana na hali halisi iliyopo.
Marejeo
Leech, G (1981), Semantics, Harmondsworth: Penguin books limited hazel Watson & veney Ltd.
Massamba P. B. D (2004) Kamusi ya Isimu na Falsafa ya Lugha. Dar es Salaam: TUKI.
Mdee, J. S (1997), Nadharia na Historia ya Leksikografia, Dar es Salaam:TUKI.
HYPERLINK "http://en.wikipedia.org/wiki/Charles_W._Morris" \o "Charles W. Morris"
Morris, Charles W. (1971), Writings on the general theory of signs, The Hague: Mouton.
Peirce, Charles S (1934), Collected papers: Volume V. Pragmatism and pragmaticism. Cambridge, MA, USA: Harvard University Press.
Ullmann, S (1962), Semantics: An Introduction to the Science of Meaning. Oxford: OUP.
Yule, G. (1996). Pragmatics. Oxford University Press: Hong Kong.
shukran sana, nimefunguka vitu ving ktk makala hii
ReplyDeleteMakala mazuri zaidi kuhusu uhusiano wa semantiki na matawi mengine ya isimu.
ReplyDeleteMakala mazuri zaidi kuhusu uhusiano wa semantiki na matawi mengine ya isimu.
ReplyDeleteMakala nzur Ila nilikua nahitaj mawanda ya semantiki
ReplyDeleteNaomba mzungumzie pia uhusiano kati ya diskosi na taaluma zingine.
ReplyDeleteNaomba mzungumzie pia uhusiano kati ya diskosi na taaluma zingine.
ReplyDeleteNaomba mzungumzie pia uhusiano kati ya diskosi na taaluma zingine.
ReplyDeleteSwali langu,
ReplyDeleteIpi imeanza kati ya taaluma hizo?
Kati ya pragmatiki,semiotiki,leksikolojia na leksigrophia
ReplyDelete