Friday, 15 November 2013

SANAA YA USHAIRI


USHAIRI
Shaaban Robert katika uandishi wa ushairi ameandika Tenzi na mashairi ya kimapokeo.
Tenzi: Ni aina ya mashairi ya kimapokeo wenye sifa zifuatazo:
 • Kimaudhui; Ni utungo wenye maudhui yanayosimulia kwa urefu tukio fulani maalum. Waweza kuwa wasifu wa mtu au jambo la kihistoria. Mfano; S. Robert ameandika utenzi wa vita vya Uhuru, ameeleza kuhusu historia. Pia katika Mapenzi Bora, ameeleza kuhusu sifa za mapenzi bora.
 • Utenzi ni utungo wa pili kati tungo za ushairi zenye beti nyingi. Utungo wa kwanza unaoongoza kuwa na beti nyingi kuliko zote katika ushairi ni Tendi. Lakini hapa tutaangazia tenzi zaidi.
 • Utenzi hauna mizani nyingi aghalabu mizani nane, hauna mshororo bali una nusu mshororo/kipande mstari.
 • Vilevile katika utenzi kipande mstari hakigawiki. Pia katika kipande mshororo kuna vipande vinne kwa kila ubeti. Mistari mitatu ya kwanza huwa na vina vyenye urari na kipande mstari cha mwisho/cha nne huwa na kina tofauti na vipande vya mwanzo. Kina cha mwisho katika mstari wa ubeti hakibadiliki katika beti zote za utenzi.
 • Amri Abead 1954 katika kanuni za kutunga mashairi anakiita kina bahari.
 • Katika utenzi beti huanzia 50-100, lakini wengine wanadai kuwa huanzia beti 100-200
 • Tenzi zote zina sifa ya tarbia
MASHAIRI YA KIMAPOKEO
FANI KATIKA MASHAIRI
lugha; lugha ya kishairi ni lugha ya mjazo, mkato na mnato yenye mpangilio maalum na isiyo na maelezo wala ufafanuzi. Tofauti kabisa na lugha ya kinadhari. Mfano; Riwaya nk.
 • Uteuzi wa sauti, silabi, maneno katika shairi ni wa kipekee usiozingatia sarufi ya lugha.
 • Mpangilio wa maneno katika mshororo huwekwa kwa utaalam zaidi kuliko katika riwaya.
 • Uteuzi wa maneno na semi katika shairi zima kwa kawaida huwa na maana maalum na si suala la kuteuwa tu kiholela holela.
 • Matumizi ya jazanda/picha na taswira. Mfano; mtunzi anaweza kumfananisha mwanamke na ua.
 • Matumizi ya tamathali za semi huwa na maana ambazo hujenga maudhui na kuleta mvuto katika shairi na kufanya kazi ya kishairi iwe ya sanaa zaidi.
 • Matumizi ya lahaja mbalimbali yaani usemaji tofauti tofauti wa lugha moja hutambulisha mkutadha wa mtunzi na muktadha wa walengwa wa lile shairi.
 • Matumizi ya lugha za kigeni – huonesha kiwango cha elimu ya mtunzi na umahiri wake katika lugha. Pia hutambulisha aina ya kazi anayofanya na vilevile, hutambulisha kiwango cha elimu ya watu wanaoandikiwa.
 • Matumizi ya vipengele vya fasihi simulizi kama vile: misemo, nahau, methali, lakabu, nk. hutumika kwa lengo la kuonesha asili ya fasihi andishi kuwa, ni fasihi simulizi na pia huonesha mwingiliano mkubwa wa kimaudhui na kifani katika fasihi simulizi.
MUUNDO WA USHAIRI
Senkoro anasema kuwa, muundo katika kazi ya fasihi ni mpangilio na mtiririko wa kazi hiyo kwa upande wa visa na matukio. Tunachunguza jinsi msanii/mtunzi alivyofuma, alivyosuka, alivyounda na alivyounganisha tukio moja na jingine, wazo moja na jingine, sura moja na nyingine, ubeti mmoja na mwingine, mshororo mmoja na mwingine.
Katika ushairi muundo tunaangalia mpangilio wa beti, mishororo katika ubeti na mtiririko wa visa na matukio katika ubeti na shairi kwa ujumla. Muundo katika ushairi hutazamwa kwa kupimwa idadi ya vina na mizani katika mshororo, idadi ya mishororo katika ubeti na idadi ya beti katika shairi. Tofauti na riwaya au tamthilia ambapo muundo wake huwa wa moja kwa moja/msago, urejeshi/rejea na changamano.
DHANA MUHIMU KATIKA SHAIRI.
 • Mshororo – ni mstari wa ushairi katika ubeti. Kwa mujibu wa wanamapokeo mshororo si lazima uwe na maana. Lakini wanausasa/mamboleo wanadai kuwa kila mshororo katika ushairi lazima uwe na maana. Mshororo huweza kuwa na kipande; kimoja, viwili, vitatu au zaidi.
Vipande katika ushairi ni sehemu ya mshororo au mstari wa ushairi katika ubeti.
 • Vibwagizo au kituo – huu ni mshororo wa mwisho katika ubeti ambao kwa kawaida hujirudia rudia. Pia huweza kuwa na majina tofauti tofauti kulingana na kinavyotumika. Huweza kuitwa kibwagizo kiini au bahari – yaani kile kinachojirudia katika kila ubeti.
Pia kuna kibwagizo kawaida – hiki hubadilika badilika katika kila ubeti.
Kwa ujumla kibwagizo husaidia sana kushadidia dhamira kuu au wazo kuu katika shairi, na pia husaidia kujenga takriri katika shairi kama kipengele cha matumizi ya lugha katika fani.
 • Ubeti – ni fungu la mistari/mishororo iliyopangwa pamoja katika shairi na inayoleta maana kamili inayojitosheleza. Beti nyingi katika mashairi hutumia tarbia/mistari minne. Pia beti huweza kuanzia mstari mmoja na kuendelea.
Majina ya mishororo katika ubeti:
 • Mshororo wa kwanza huitwa mwanzo
 • Mshororo wa pili huitwa mlato
 • Mshororo wa tatu huitwa mleo
 • Mshororo wa nne huitwa kimalizio, kibwagizo, kituo, mkarara, kipokeo.
Shairi huweza kuundwa na kipande mstari yaani ubeti wenye kipande mstari.
 • Kipande mstari cha kwanza huitwa ukwapi
 • Kipande mstari cha pili huitwa utao
 • Kipande mstari cha tatu huitwa mwanda.
 • Mizani – Idadi ya silabi katika mshororo. Hutumika kama kipimo cha ushairi kwani huhesabiwa kwa uwiano. Mashairi ya kimapokeo yana mizani 16, katika ukwapi 8 na katika utao 8 jumla 16
 • Urari – ulingano/uwiano wa vina na mizani katika mashairi. Mashairi ya kimapokeo urari ni msingi wa utunzi. Urari katika ushairi/mashairi husaidia kuimbika kwa shairi ambayo ndio sifa mahususi ya mashairi ya kimapokeo.
 • Vina – ni silabi zenye milio inayofanana, ni silabi za kati mwishoni mwa kipande mshororo na silabi za mwisho katika mshororo.
·    Vina vya kati vinaweza kuwa vina vya ukwapi na utao katika shairi lenye vipande mstari vitatu.
·   Wakati katika shairi lenye vipande mstari viwili vina vya kati huwa ukwapi. Pia katika shairi lenye kipande mstari kimoja kina cha kati huwa hakuna.
·       Shairi lenye vipande mstari vitatu; mfano, ………., …………., …………., kina cha mwisho ni mwanda.
·     Shairi lenye vipande mstari viwili, mfano; ……..…….., …………..….., kina cha mwisho ni utao.
·   Shairi lenye kipande mstari kimoja kina cha kati ni ukwapi. mfano, …………….,
DHIMA YA VINA
 • Vina huleta mvuto katika kughana shairi.
 • Husisitiza maudhui katika shairi
 • Vina vya shairi hutumika kumalizia kipande au mshororo mzima wa shairi.
 • Husaidia kuhifadhi au kushika kichwani/kukariri kwa urahisi kutokana na kujirudia rudia.
MTINDO KATIKA USHAIRI
Ni mbinu au namna anayotumia mtunzi katika kuandika kazi yake. Mtindo pia ni mbinu au namna na vilevile ni tabia ya utungaji wa mashairi unaompambanua mtunzi mmoja na mwingine.
 • Katika mtindo tunaangalia, kwa nini mtunzi ametumia lahaja au maneno magumu. Pia tunaangalia tamathali za semi, methali, nahau nk.
 • Vilevile tunaangalia mpangilio wa mishororo katika ubeti, je ni vipande vitatu au viwili au vinne.
 • Pia tunaangali mwandishi ametumiaje takriri katika shairi, je ni takriri sauti, takriri neno nk.
 • Vilevile tunaangalia mwandishi ameunda vipi shairi lake; ameanza vipi na amemalizia vipi shairi lake. Maswali haya yakijibiwa ndipo tunaweza kujua mtindo wa mshairi.
 • Pamoja na hayo, pia kuna mbinu ya kutumia michoro/vielelezo nk. mfano katika kitabu cha Insha na Mashairi.
 • Mbinu nyingine katika mtindo ni ile ya kuanza na aya za mashairi kwa kutumia herufi kubwa katika neno la kwanza.
 • Pia kuna mbinu ya kikufu; yaani kuanza na kina cha mwisho cha ubeti uliotangulia.
 • Vilevile kuna mbinu ya pindu; yaani neno la mwisho au kipande cha mwisho huanza katika mshororo wa pili. Mbinu pindu inaunganisha mshororo.
 • S. Robert pia ametumia mbinu ya kuchanganya kazi mbili au zaidi katika diwani moja “two in one”. Mfano, Tenzi, Insha na Shairi. Katika riwaya ya “Maisha yangu na Baada ya Miaka Hamsini
 • Licha ya hayo, pia tunaangalia mbinu zinazojenga maana na matumizi ya lugha. Mfano; mashairi ya S. Robert ametumia mbinu ya kidatu, yaani kufupisha mshororo mmoja au zaidi katika kila beti. Anaweza kufupisha mshororo, kipande mshororo au neno. Mfano, katika Insha na Mashairi.
 • Vilevile S. Robert ametumia mbinu ya kufasili maneno magumu/msamiati mgumu.
MUKTADHA
 • Muktadha katika kazi ya fasihi hurejelea mahali na wakati mtunzi anapoandika/alipoandika kazi yake ya fasihi. Mazingira huweza kuwa ya kihistoria, kijiografia, kijamii nk.
 • Pia katika muktadha tunaangalia watu waliozungumziwa katika muktadha huo,
 • Vilevile mazingira ya kiutendaji – hapa tunaangalia namna gani mambo yametendeka.
 • Muktadha husaidia katika kujenga wahusika au mtunzi mwenyewe. Pia husaidia kujenga lugha.
 • Pia katika uhakiki wowote usiozingatia muktadha wa kazi husika kwa kawaida hupotosha kazi husika katika upande wa maudhui au fani.
 


  

17 comments:

 1. kweli kiswahili ni tunu na johari ya Afrika, ushairi ni bahari ya kila mtu kuongelea mumo. lakini bahari hii ina zake kanuni za kumfanya mwogaji aoge pasi na shida. lakini pia kuogelea ni kuogelea tu! waweza ogelea pasi kufuata kanuni. twende zetu tuogelee. asante sana kwa kanuni hizi za ushairi. na Kapele, H

  ReplyDelete
 2. This comment has been removed by the author.

  ReplyDelete
 3. kazi nzuri sana kiswahili ni lugha yetu hatuna budi kutoa mchango na kuwa balozi mzuri ndanii na nje ya nchi.kipindi kijacho kama itawezekana eleza migogoro iliyopo baina ya wana ushairi wa kimapokeo mfano nabhany,mnyampala,amri Abeid,shaban Robert,pia wana usasa(washairi wa kimapinduzi) mfano Mulokozi,kezilahabi,T.A.Mvungi,kahigi n.k......Akhsanteeee mkuu..

  ReplyDelete
 4. Naam, hii ni bahari ya lugha, lazima tujitahidi kuelewa fika uhuru wetu wa kufikisha ujumbe

  ReplyDelete
 5. Samahani, Kuna aina ngapi za beti kulingana na idadi ya mishororo? na ni zipi hizo?
  Natanguliza shukrani.

  ReplyDelete
 6. kazi nzuri sana naitaji kukijua kiswahili kwa undani,na pia mi ni mwanamziki mdogo so inanisaidia mimi kutunga mashairi yangu kwa ufasaha asanteni sana:

  ReplyDelete
  Replies
  1. Jumuika nasi kwenye ukumbi na utafaidikia iwapo umejitolea kukijua na kukienzi Kiswahili katika kazi yako ya usanii.

   Delete
 7. Enter your comment...mashairi mepesi no yapi katika fasihi simulizi

  ReplyDelete