Thursday, 27 June 2013

TASWIRA KATIKA WASAKATONGE



Waandishi wa kazi mbalimbali za kifasihi hutumia taswira kadha wa kadha katika kujenga na kupamba kazi zao.
Fasihi ni kazi ya sanaa itumiayo lugha ili kufikisha ujumbe kwa jamii iliyokusudiwa. Zipo aina mbili za fasihi yaani fasihi andishi na fasihi simulizi. Taswira ni maneno yanayotoa picha ya kitu, hali, wazo au dhana juu ya jambo fulani. Kwa maneno mengine ni lugha ya picha.Taswira humfanya msomaji kuibua hisia na kupata maana akilini mwake juu ya kile kinachosemwa.
Katika Diwani ya Wasakatonge mwandishi Muhammed Seif Khatib ametumia taswira mbalimbali katika kuijenga na kuifanya kazi yake ivutie huku akifikisha ujumbe aliokusudia kwa jamii husika. Mwandishi ametumia taswira zifuatazo;

Kaitka shairi la “VINYONGA” ametumia taswira ya Kinyonga kiumbe mwenye tabia ya ukigeugeu asiye na msimamo akimaanisha watu wasiokuwa na msimamo ndani ya jamii. Anasema hayo katika ubeti wa 2
“Jukwaa,
meingiliwa,
Wanasiasa vinyonga,
Maisha ya ufahari,
Vitendo vyao hatari,
Ni kinyume cha maadili,
Ni usaliti.”
Hivyo mwandishi ameonesha wazi kuwa vinyonga ni wanasiasa wasaliti, jambo ambalo ni la kweli na linahalisika ndani ya jamii, kwani viongozi wetu tunaowachagua mara nyingi hubadilika na kutotekeleza ahadi wanazozitoa kwa wananchi. Hivyo mwandishi anaona kwamba hainabudi kulikemea hili ili watu waachane na tabia ya ukinyonga.
Pia katika shairi la “MIAMBA” mwandishi ametumia taswira kama vile; Miamba akimaanisha watu wa tabaka la juu au wale wenye dhamana. Vilevile ametumia taswira ya Chui na Simba akiashiria watu wenye nguvu na wakandamizaji. Pia Mbuga akimaanisha nchi, Mamba, Boko, Nyati na Ndovu ambao ni viumbe wenye nguvu. Ametumia taswira hizo akilinganisha na Digidigi na Nyani kama watu wanyonge ambao huonewa na kunyanyaswa na tabaka la juu, jambo ambalo lipo hata ndani ya jamii yetu, kwani wenye fedha na mamlaka ndio wenye jeuri na wapotoshaji wakubwa wa haki.
Vilevile katika shairi la “ASALI LIPOTOJA” mwandishi ametumia taswira ya Asali akiashiria uhuru uliopatikana toka kwa wakoloni. Anaelezea jinsi viongozi waafrika walivyowasaliti waafrika wenzao baada ya Asali kutoja. mfano; ubeti wa 4
“Asali lipotoja,
Wengine walikuja,
Na mirefu mirija
Kwao kuwa tafrija,
Wakapata faraja,
Sisi tukatengwa.”
Anaelezea jinsi hali ilivyokuwa mbaya baada ya kupata uhuru kwani uhuru walipigania wote lakini wanaofaidi keki ya taifa ni wachache.
Taswira nyingine ni katika shairi la “NAHODHA” mwandishi ametumia taswira ya Bahari akimaanisha nchi, pia ametumia Mawimbi, Tufani, Radi akimaanisha masaibu na matatizo yanayoikumba nchi; Anataja Abiria akimaanisha wananchi/Watawaliwa. Hivyo basi ametumia taswira hizo akionesha hali halisi ilivyo katika jamii ya Watanzania.
Vilevile katika shairi la “BUNDI” mwandishi ametumia picha ya Bundi kuashiria ukandamizaji, unyonyaji wa haki na maendeleo ya wengi. Ameonesha jinsi Bundi anavyong’ang’ania hataki kubanduka. Kwa mfano ubeti wa 4
“Bundi hataki kubanduka,
Yu paani amejipachika,
Lialia kila dakika,
Mambo si salama,
Hakuna uzima,
Ila ni nakama
Sote twayoyoma
      Hakujacha.”
Mwandishi anaona kuwa bado ni usiku hapajakucha. Hili ni jambo halisi kabisa ndani ya jamii kwani watu wengi wana kiu ya haki na maendeleo ila wanabaki nyuma na kushindwa kwa sababu ya wakandamizaji wachache.
Kaitka shairi la “WEWE JIKO LA SHAMBA” zipo taswira anuai kama vile Jiko ikiwa na maana ya mwanamke. Hapa mwandishi anamzungumzia mwanamke asiyejitunza na kujiheshimu, anakemea suala la tabia mbaya, anasema katika ubeti wa 1
“Wewe ni jiko la shamba, si kuka si seredani,
Mezoea kumbakumba, kila aina ya kuni,
Kwangu huwezi kutamba, nimekutoa thamani.”
Anayasema hayo akiwalenga moja kwa moja wanawake wasiotunza miili yao wenye tabia ya kujiuza kwa wanaume. Hivyo mambo haya katika jamii yetu yapo na yamezoeleka kiasi kwamba yanaonekana kuwa ni jambo la kawaida. Mwandishi ameona hilo na kulikemea ili jamii ifunguke.
Pia katika shairi la “JIWE SI MCHI” mwandishi ametuima taswira ya Mchi akimaanisha wanaume na Vinu akimaanisha wanawake. Hapa anakemea tabia ya mahusiano ya kimapenzi ya jinsia moja katika jamii. Mfano ubeti 1
“Vinu wenzake ni michi, wala sibadilishwe,
ufundi haujifichi, utwanzi na mizinguwe,
Jiwe la manga si mchi, haitakidhi hajawe.”
Mwandishi aliliona wazi jambo hili ambalo leo linajitokeza katika jamii yetu, hivyo si budi wanajamii kubadilika kwani hayo si maadili ya Kiafrika na ni kinyume na mafundisho ya dini.
Vilevile katika shairi la “WASO DHAMBI” mwandishi ametumia taswira ya Wavilemba, Wamajoho, Tasibihi, Warozali, Misalaba na Majumba ambayo ni mavazi na ishara mbalimbali za watu kufuata imani fulani. Mfano anaashiria wakristo pale anaposema Warozali, Misalaba, Wavilemba na anaposema Tasibihi, Majoho anaashiria waislamu. Mfano ubeti wa 3
Warozali!
     Misalaba, na majumba, na hutoba,
           Nyingi toba, zenye hiba, na haiba,
                Mambo yao,
                     Unafiki.”
Hapa mwandishi anakemea baadhi ya watu wanaofanya mambo ya dini bila imani thabiti, anawaona kuwa ni wanafiki. Jambo hili lina uhalisia ndani ya jamii ya leo kwani watu hujifanya wema na wacha Mungu lakini kumbe ndio wanaosababisha matatizo, fitina, majungu, ufisadi na mengine mengi.
Hivyo basi, Taswira ni muhimu sana katika uandishi wa kazi za fasihi kwani hufanya shairi liwe na mvuto na kupambwa kwa lugha. Si hivyo tu lakini pia hufikirisha msomaji kumfanya ahusianishe tabia, mambo na vitu mbalimbali na taswira anazotumia mwandishi.

12 comments:

  1. Nimefurahishwa na kazi yenu

    ReplyDelete
  2. Hii ni mzuri kwenye kukuza uelewa wa wanafunzi

    ReplyDelete
  3. Nimeisoma kazi hii, kwa kweli mchambuzi amefanya kazi nzuri sana. Uchambuzi huu unaweza kuwa msaada mkubwa sana kwa wanafunzi wa shule za sekondari. Aidha kazi hii inaweza kuwasaidia wahakiki wachanga waofanya kazi ya kuhakiki kazi mbalimbali za fasihi. Hongera sana mchambuzi.

    ReplyDelete