Wednesday, 30 October 2013

MAJIGAMBO



SANAA YA MAJIGAMBO KATIKA NYIMBO ZA KIZAZI KIPYA

(UWASILISHAJI)


Kwa hakika sanaa ya majigambo yaijapotea Barani Afrika, isipokuwa imebadilika tu kulingana na maendeleo ya Sayansi na Teknolojia.
Katika kujadili mada hii, kwanza tutaanza kufafanua dhana ya majigambo kwa kuwatumia wataalamu mbalimbali huku tukitoa maana yetu kutokana na mawazo ya wataalamu hao, pia tutaelezea kwa ufupi kuhusu chimbuko la muziki wa kizazi kipya, kisha tutaingia katika kiini cha mada tajwa kwa kuonesha jinsi gani majigambo yalivyojitokeza katika nyimbo mbili za kizazi kipya ambapo tumetumia wimbo wa msanii Prof Jay “Ndiyo mzee” na wimbo wa Sugu “Sugu”. Kisha hitimisho

Kwa mijibu wa Simiyu (2011), majigambo ni maigizo yanayotoa mwanya kwa wahusika kujisifu kwa sababu ya matendo fulani ya kishujaa au mafanikio katika nyanja fulani za maisha.
Mulokozi (1996), vivugo (majigambo) ni ghani la kujisifia. Kwa kawaida hutungwa na kughanwa na muhusika mwenyewe. Kivugo hutungwa kwa ufundi mkubwa kwa kutumia mbinu kama sitiari, vidokezi, ishara, takriri na wakati mwengine hata vina.
Wamitila (2003), hii ni aina ya maghani (sifo) yanayohusu kujisifu au sifa. Aghalabu kuhusu kutongoa utungo wa kujisifu kuhusiana na kitendo fulani, ushujaa, urijali au matendo muhimu.
Wamitila (Kishatajwa), majigambo au vivugo haya ni maigizo ambayo yanaonesha kujitapa (kujigamba) kwingi kwa mtu ambaye labda ni shujaa au ametenda mambo ya kishujaa au yenye uzito fulani. Watu wanaopatikana katika majigambo ndiyo watambaji au wasimuliaji wa majigambo yenyewe. Ni kawaida ya majigambo kuwa na lugha nzito iliyojaa tamathali zenye taswira au picha za undani na yenye hisia na mawazo mazito. Mtambaji anaweza kujitapa kwa jambo lolote lile.
Wataalamu wote wanashabihiana katika kutoa maana ya majigambo kwani wote wanaelezea kuwa majigambo huhusika na matendo ya kishujaa.
Kwa hiyo tunakubaliana na fasili ya Wamitila (2003), ambaye ameenda mbele zaidi na kueleza kuwa kuna matumizi ya lugha ya kisanaa. Pia mtambaji anaweza kujigamba au kujitapa kwa jambo lolote lile na siyo lazima liwe jambo la kishujaa tu.
Kwa asili kivugo huwa hakiandikwi, hutungwa kichwani kabla au wakati wa utambaji. Siku hizi watu wameanza kutunga au kutungiwa kwa kuandika na baadaye kusoma kivugo hicho. Hii ni kutokana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia yanayoashiria mabadiliko ya sanaa ya majigambo. Nyimbo za kizazi kipya ni zao la mabadiliko ya sanaa ya majigambo.
Muziki wa kizazi kipya hapa Tanzania ulianzia kama muziki wa Hip Hop na kwamba inaelekea kuwa mwaka 1980 na 1990 watoto wa Kitanzania kutoka kwenye familia zenye uwezo kiuchumi ndiyo waliosaidia kuleta muziki wa Hip Hop waliporudi kutoka likizo walikuja na kanda, video na majarida ya muziki kuhusu wasanii wa Hip Hop wa Marekani, Uingereza. Kwa namna hiyo muziki ulikuwa na baadaye vijana wengi walijiunga ingawa muziki huu unaendelea lakini jina la “Bongo Fleva” lilishika kasi.
Kwa kutumia wimbo wa “Ndiyo Mzee” ulioimbwa na Prof Jay na wimbo wa “Sugu” ulioimbwa na Sugu tunaweza kuthibitisha kuwa ni kweli sanaa ya majigambo haijapotea barani Afrika.
Wimbo wa “Ndiyo mzee” ulioimbwa na msanii Prof Jay, ni wimbo unaohusu sera zilizokuwa zikitolewa za mwanasiasa fulani wakati wa kampeni za uchaguzi. Pia wimbo wa “Sugu” ulioimbwa na Sugu ni wimbo ambao msanii anajitamba kwa sifa alizonazo yeye, kwamba, hawezi kulinganishwa na msanii mwingine yoyote yule.
Sanaa ya majigambo imejitokeza katika nyimbo hizi katika sifa zifuatazo:-
Watu huigiza kwa kutumia lugha nzito ya tamathali, picha na taswira zenye hisia na mawazo mazito. Katika wimbo wa “Ndiyo mzee” msanii ametumia lugha nzito  ya tamathali, picha na taswira, katika ubeti wa kwanza mtambaji anajigamba kuwa:-
                        “Nadhani nimeletwa niokoe hiki kizazi”
“Mimi ni mwanasiasa niliyebarikiwa na Mungu”
“Mimi ni mteule kusini mwa jangwa la Sahara”
Hapa msaniii ametumia lugha hii kujitofautisha na wanasiasa wengine. Pia msanii ametumia tashibiha katika kujigamba pale asemapo:-
“Nataka kuigeuza Tanzania kama ulaya”
“Kwenye mahospitali nitamwaga dawa kama mchanga”
Msanii ametumia lugha ya picha pale asemapo:-
“Mabomba yatatoa maji na maziwa nchi nzima”
Hapa hadhira inapata picha ya nchi ya Tanzania kuwa yenye mabomba ya kutoa maji na maziwa:-
“Nitajenga kumbi nyingi sana za starehe baharini”
Hapa hadhira inapata picha jinsi kumbi zitakavyojengwa kwenye bahari, jambo hili si la msingi analojigamba nalo mwanasiasa huyu kwa kuacha masuala muhimu kama kujenga daraja la Kigamboni pale kwenye kivuko nk.
Pia katika wimbo wa “Sugu” msanii ametumia tashibiha.
“Sauti yangu kwenye mic inasambaa kama upepo”.
Ametumia pia lugha nzito, lugha ya picha na tashibiha.
“Kuna kitu kimoja watu hawajajua huwezi kuzuia mvua na Sugu ni kama mvua kama ananyesha ananyesha”
Pia ametumia sitiari.
“Mimi ni dume la mbegu”
Majigambo huwa na matumizi ya chuku. Katika wimbo wa “Ndiyo Mzee” msanii ametumia sana chuku. Kwa mfano:-
“Nataka mpaka Matonya afundishe chuo kikuu”
“Wanafunzi wafanyie practical mwezini”
“Nitafungua account kwa kila mtoto mchanga“
 “Nikiwa kuliko mfalme Suleiman msiwe na wasi”
Majigambo husaidia kuelimisha, kuadilisha na kuhifadhi mila na kuzipokeza kwa vizazi vipya. Wimbo wa “Ndiyo mzee” unaelimisha wananchi hasa kwenye ubeti wa pili pale mwimbaji Juma Nature anapomkosoa mwanasiasa kwa kueleza kuwa, yale yote aliyojigamba nayo mwanasiasa huyo ni ya uongo na wala hatoweza kuyatimiza. Kwa hiyo anaelimisha jamii isikubali uongo wake. Wimbo huu unaweza kutumika kwa vizazi vya sasa na vijavyo ili kuelimisha wananchi juu ya wagombea wa kisiasa wanaoomba kura kwa wananchi.
Pia katika wimbo wa “Sugu” msanii anasema kwamba:-
“Napata matatizo natatua bila chuki”
Hapa msanii anaelimisha jamii kwamba unapopata matatizo usiyatatue kwa kuwachukia wenzako bali utafute utatuzi wa tatizo.
Mtambaji hutumia jina halisi au jina la sifa la muhusika. Katika wimbo wa “Ndiyo mzee” msanii ameanza kwa kujitamba kwa kutumia jina lake halisi pale anaposema:-
“Ok ok naitwa Joseph Haule mwana wa Msolopa Ganzi”
Vilevile katika wimbo wa “Sugu” msanii anajitapa kwa kuanza:-
“Wananiita Mr two kwa jina jingine Sugu, sasa nakubali kuwa mimi ni dume la mbegu”
Mtambaji huahidi kutenda mambo makubwa zaidi kwa ajili ya mkubwa wake ambaye anaweza kuwa mzazi, mtawala au umma. Katika wimbo wa “Ndiyo mzee” mtambaji prof Jay anatoa ahadi kadha wa kadha kwa wananchi kama vile:-
“Nitahakikisha kila baamedi anamiliki benz”
“Wanafunzi watafanyia practical mwezini”
“Kwenye mahospital nitamwaga dawa kama mchanga”
“Nitafungua account kwa kila mtoto mchanga”
“Nitafadhili wachawi waweze kutengeneza ndege”
Pia katika wimbo wa “Sugu” mtambaji pia anajitapa kwa kusema kuwa:-
“Nataka kuwa kama 2pac”
Pia majigambo huwa na tamati, kujikabidhi rasmi kwa mkubwa. Katika wimbo wa “Ndiyo mzee” kuna tamati ambayo imetambwa na Mc Babu Ayoub ambaye anamkabidhi mgombea kwa hadhira kwa kuiuliza hadhira kama ifuatavyo:-

“Ndugu wananchi kuna mtu anaswali kutoka kwa mgombea? Nauliza nasema hivii kama mtu anaswali basi ajitokeze aweze kuuliza swali”
Kwa kuhitimisha ni kuwa kutokana na athari za lugha za kimagharibi, majigambo ya muziki wa kizazi kipya yamekumbwa na mwingiliano mkubwa wa lugha kwani si ajabu kuona mtambaji akichanganya lugha ya kiingereza na lugha ya Kiswahili. Hii ni athari ya lugha kukua na kuathiriana kutokana na kukua kwa sayansi na teknolojia. Lakini majigambo ya hapo awali yalitumia lugha za asili za jamii husika na hivyo kuudumisha utamaduni wa kiafrika.

VIAMBATIZI.
Prof Jay – Ndiyo mzee.
Kibwagizo.
Naam ndugu wananchi
Mc wenu babu ayubu
Ninawaleteeni habari japo kwa kifupi kuhusiana na huyu mgombea wetu Joseph Haule
Mpeni kura za ndiyo kwa sababu yeye ni mpenda watu, nimpenda amani na ni mtu mwenye huruma kwa wananchi wote
Kwa hivyo basi nawaomba ndugu wananchi mumpe kura ya ndiyo.
Naam basi hivyo basi ndugu wananchi tafadhali na mkaribisha mgombea wetu bwana Joseph Haule ili aje aweze kuzungumza na wananchi karibi karibu.
Ubeti wa kwanza
Ok, ok naitwa Joseph Haule mwana wa msolopo ganzi,
Nadhani nimeletwa niokoe hiki kizazi
Mimi ni mwanasiasa niliyebarikiwa na Mungu
Nimeletwa kwenu waungwana niwapunguzie machungu
Mimi ni mteule kusini mwa jangwa la Sahara
Ndiyo maana nimetunukiwa cheti cha juu cha utawala
Na ikiwa kuliko mfalme Suleiman msiwe na wasi
Na hii nitadhihirisha pindi mtakaponipa nafasi
Actually nimedhamiria kuwasaidia
Taifa lenye nguvu duniani liwe Tanzania
Jamani makofi tafadhali basi jamani……
Ni mambo madogo tu
Nadhani nitarekebisha mkinipa visiku vichache
Uchumi utapanda ile ghafla bin vuu
Nataka mpaka Matonya afundishe Chuo Kikuu
Nchi ya Tanzania inang’ara ile kishenzi
Na nitahakikisha kila baa med anamiliki benz
Si mtafurahi dada zangu jamani.. ndiyoooooo
Basi endeleeni kunisifu kwa nyimbo na mapambio
Nipeni hiyo nafasi jamani hamuoni hali ni mbaya
Nataka kuigeuza Tanzania kama Ulaya
Cha kwanza nitakachofanya nitafuta umasikini
Wanafunzi mkafanyie practical mwezini
Kwenye mahospitali nitamwaga dawa kama nchanga
Nitafungua account kwa kila mtoto mchanga
Mabomba yatatoa maji na maziwa nchi nzima
Watu wa vijijini mtasahau habari za visima
Nitafadhili wachawi waweze kutengeneza ndege
Kila mtu awe na yake makonda na wapiga debe
Kiitikio.
Si mtafurahi Watanzania jamani… ndiyooo mzeee
Si ni kweli nakubalika jamani… ndiyooo mzeeee
Basi mimi ni mkombozi wenu jama.. ndiyo mzeee
Na nitafuta shida zenu zote.. ndiyo mzeee
Hivi ni nani ni vijimbamambo … ndiyo mzeee
Na vinanikera kweli kweli mimi.. ndiyo mzeee
Basi hali itabadilika sawa.. ndiyo mzeee
Na hatamu tutaishika ok…. ndiyo mzeee
 Ubeti wa pili
Wafanyakazi wa serikalini nashangaa hamna magari
Yaani hata mikweche hahaaaa hii ni hatari
Ninampango wa kuongeza mishahara iliyo minono
Mara mia ya ile ya mwanzo ilifayofanya mfanye mgomo
Nitawapa nyumba nzuri na magari ya kifahari
Watu watashangaa mtakapopita kila mahali
Mkulima kila mmoja nitampatia trekta
Nadhani hiyo kidogo itasaidia kunyanyua sekta
Mtauza nafaka zenu bilioni kwa mabilioni
Watu midomo wazi kama wamekamatwa ugoni
Walimu zawadi zenu amm nimezificha moyoni
Nadhani mtazimia siku mkizitia machoni
We acha tu mtafurahi nyinyi
Ila hapo hapamfahi mtu mwingine niwekeni mimi
By the way polisi wote ninawasifu
Jinsi mnavyokwenda sahani moja na wahalifu
Sasa kila mmoja nitampatia helicopta
Nadhani hiyo wote hapo hamjawahi kuota
Raia wa Tanzania mtalala milango wazi
Infakti nauhakika wa kuthibiti ujambazi
Nitajenga barabara tano tano juu na chini
Nitajenga kumbi nyingi sana za starehe baharini
Ninaupendo kuliko wa mshumaa kumulikia wenzangu
Mtakaoyumba kiuchumi tutagawana vya kwangu.
Kiitikio.
Kibwagizo
Ndugu wananchi kuna mtu anasawali kutoka kwa mgombea?
Nauliza hivii kuna mtu anaswali basi ajitokeze ili aweze kuuliza swalii..
Ubeti wa tatu
Nyie ndugu zangu huyu msimpe uongozi siyo vizuri
Muongo tu mnafiki na kiburi kimsuli
Anaongopeeaaaa saaanaa sijui kazaliwa muda gani alfajiri au alasiri
Au wakati wa mvua zile za kipindi kile
Amepita pita school lakini mambo yake si mazuri
Wala tusimtetee atatuangamiza
Labda angesubiri kwanza uchaguzi umekwisha
Tumemfuma mwenyewe kwa kalmanzira anasafishwa
Klamanzira akamwambia ehee shida yako
Elezea fasta fasta kabla jini hajapanda
Mmmmhhhh chyaaaaaaa
Hajakaa vizuri mashetani si yakamuanza
Kakurupuka kwa kasi kimbunga amejichanja
Tukamsikia akisema kwa kasi sauti kubwa ya kukaripia
Iihiiii chyaaaaaaaaaa
Waungwana mnisaidie ndiyooo nitamweleza
Uongo mtupu babake ameliwa
Waungwana wamempeleka njau mpaka kaibiwa
Yupo hamna……………………….amewehuka
Hajatulia huyu mpepeeni upuuuuffff upuuuuffff
Ni sauti iliyosikika kutoka kwa mzee wa pembeni
Sijui msaidizi mganga au mpelelezi
Na kwa taarifa yako uongozi hupati ng’oo
Labda urudi kwenu uende ukavunje tunguli
Na hao waganga wako waeleze hupati kitu hapa
Hata utoe chapaaaa.
Kiitikio.
Je wananchi mmenisikia.. ndiyo mzeee
Kuwa huyu jamaa hatufai… ndiyo mzeee
Na inafaa kumchukia.. ndiyo mzeee
Hatumtaki aondoke zake.. ndiyo mzeee
Tusizubae na maneno yake.. ndiyo mzeee
Tunahakikisha hatumchagui.. ndiyo mzeee
Asitufanye siye wanafiki… ndiyo mzeee
Sugu - sugu
Kiitikio.
Wanakuita sugu x 3
Ubeti wa kwanza.
Wanaita Mr. two kwa jina jingine Sugu
Sugu mtu wa vurugu
Wengi sasa wanakubali mimi ni dume la mbegu
Yaani ni mtu ambaye nipo
Na hata nisipokuwepo sauti yangu itakuwepo
Nataka kuwa kama 2pac
Itikadi zangu nazieleza kwenye mic
Napata matatizo natatua bila chuki
Shukrani za dhati kwa mashabiki
Mwanzo nilikataa mliponiita Super star
Lakini sasa nakubali siwezi tena kukataa
Ninapopita sehemu nyingi nakutana na watu wa aina nyingi
Mara nyingi wananiuliza maswali mengi
Wengine wananiuliza eti kama navuta bangi
Nakataa kujibu maswali yasiyo ya msingi
Sababu nina mambo mengi
Kila siku kwenye ziara kama vile rais
Hata mama anajua mimi ni mtu wa mitikasi ila tu basi
Na naweza kuwakamata watu nuksi
Na sipo longolongo ninapojimix na fix
Dawa ya mabishoo ni kuwa bishoo zaidi yao
Sugu na mbalimbali zaidi yao
Napata message kwenye voda kutoka kwa madem zao
Mi ndo sugu
Hata mtoto wa demu wangu ananiita uncle sugu.
Ahaaaaa staraa.
Kiitikio.
Ubeti wa pili.
Nayajua matatizo zaidi yako
Na hata kama ni msoto nimepata zaidi yako
Usinione brothemen kwa kuwa nipo na mkoko
Shoko utazima zako
Kasheshe zangu nzito
Hautaweza peke yako
Dar es salaam bongo yangu
Wa kwapi machizi wangu
Kokote kule mliko naomba muite jina langu (suguuu)
Napata flag kila ninapopita
Hata watoto wadogo wakiniona wananiita
Naitika bila kusita
Nikiamua kukomaa mbaka promota anadata
Popote heshima ilipo hapo mimi ndipo napenda niwepo
Sauti yangu kwenye mic inasambaa kama upepo
Narudia  kusema tena muziki ni kazi yangu
Nawaombe kwa mungu mashabiki wangu
Na mamc wote ambao ni kama wadogo zangu
Kuna kitu kimoja watu wengi  hawajajua
Huwezi kuizuia mvua
Sugu ni kama mvua kama kunyesha nanyesha
Kama barozi kwenye chat napandisha
Wananiita sugu machizi wote sema sugu oyaaaa sugu
Mambo namna gani sugu na siwezi kukataa kuitwa sugu
Wakati mimi ni sugu.
Kiitikio

MAREJEO:
Mulokozi, M.M. (1996), Utangulizi wa Fasihi ya Kiswahili. Dar es Salaam. TUKI.
Wamitila. K. W. (2003). Kamusi ya Fasihi. Istilahi na nadharia. Focus Publishers Ltd. Nairobi. Kenya.
Simiyu, W. (2010). Kitovu cha Fasihi Simulizi. Serengeti Bookshop. Makoroboi. Mwanza.





4 comments: