Tafiti.



UTAFITI WA FASIHI SIMULIZI
M.M. MULOKOZI
LENGO LA MUHADHARA
Kuleleza:
1. UMUHIMU WA UTAFITI WA FASIHI SIMULIZI
2. PANDE TATU KTK UTAFITI – Mtafiti, Mtafitiwa,                 Mdhamini.
3. MBINU NA VIFAA VYA UTAFITI
4. UCHAMBUZI WA MATOKEO NA UWASILISHAJI
UMUHIMU
1. Kupata taarifa muhimu kuhusu suala linalotafitiwa
2. Kuongeza hazina ya maarifa katika uwanja unaohusika
3. Kipima-joto cha hali, fikra, mitazamo, matajario na maudhiko ya jamii ya watafitiwa
4. Kuchangia katika kujenga na kuendeleza fani za fasihi simulizi na fani nyinginezo.
MDHAMINI
1. Huainisha nyanja za kufanyia utafiti na aula za utafiti
2. Huainisha watafiti
3. Hutoa fedha na nyenzo za utafiti
4. Hupokea matokeo ya utafiti.
MTAFITI
1. Ndiye mtafuta taarifa
2. Huamua madhumuni na kuweka malengo ya utafiti
3. Huchagua eneo na watu wa kutafitiwa
4. Huchagua wasaidizi wa utafiti
5. Hujenga uhusiano na watafitiwa
6. Hupokea, kuchambua na kuchakata data za uwandani
7. Hutayarisha ripoti na mapendekezo yatokanayo na utafiti wake.
Swali: Je, mtafiti ni jasusi?
MTAFITIWA
1. Ndiye mtoa taarifa
2. Hujenga uhusiano na Mtafiti
3. Huchagua taarifa za kumpa Mtafiti
MCHAKATO WA UTAFITI
1. Utafiti wa maktabani/makavazini/mtandaoni
Utafiti wowote ule sharti uanzie hapo. SOMA kazi za watangulizi kuhusu somo/mada yako.
1.1 Nyaraka za asili (k.m. barua)
1.2 Nyaraka rasmi (k.m. Ripoti za serikali)
1.3 Nyaraka zisizokuwa asilia – k.m. vitabu
2. Pendekezo la Utafiti
2.1 Ainisha mada ya utafiti – baada ya kusoma kazi kadha za watangulizi katika uwanja huo
2.2. Fafanua tatizo la utafiti – baada ya kusoma kazi kadha za kinadharia katika uwanja huo
2.3 Eeleza madhumuni na malengo ya utafiti
2.4 Eeleza nadharia tete zitakazoongoza utafiti wako
2.5 Jadili machapisho yaliyoshughulikia suala hilo na onesha dosari na mapengo yake.
2.6 Onesha namna utafiti wako utakavyorekebisha dosari na kuziba mapengo hayo, na matarajio yako
2.7 Eleza mbinu na njia za utafiti zitakazotumika, pamoja na usampulishaji wa watafitiwa au wa data iwapo utahitajika
2.8 Eleza nadharia ya/za kiuchambuzi utakazotumia kuchambulia data zako
2.9 Onesha ratiba ya utafiti
2.10 Onesha makisio ya bajeti ya utafiti; bajeti iwiane na shughuli zitakazofanyika
2.11 Weka orodha ya marejeo
2.12 Ambatisha maswali, vidadisi, na zana nyingine za utafiti utakazozitumia
3. Ukusanyaji wa Data
3.1. Vifaa vya msingi
- Kalamu na karatasi, shajara
- kinasa sauti
- kamera ya picha tuli
- kamera ya video
- vingine (k.m. kionambali) kama vitahitajika
3.2. Njia
- Mahojiano – faida na hasara zake
- Kushuhudia – faida na hasara zake
- Kushiriki – faida na hasara zake
- Kutumia vidadisi/majedwali, n.k. – faida na hasara zake
3.3 Kurekodi taarifa
Mbali na matumizi ya vifaa kama tepurekoda, tumia pia shajara na daftari kuandika yale yaliyo muhimu. Ripoti ya tukio iwe na yafuatayo:
- tarehe
- mahali
- muda
- majina ya wahusika (mtafiti, mtafitiwa/watafitiwa)
- Umri na jinsi ya mtafitiwa
- malezo ya yaliyotendeka kwenye tukio hilo, malengo yake, na matokeo yake
- hali na hisia za wahusika
3.3 Muhimu
- Haja ya kuwa mnyenyekevu
- Usidokeze jibu kwa muulizwaji
- Usihubiri, sikiliza
- Usikemee au kuudhi muhojiwa
- Usivunje mila na kanuni za utamaduni wa wahusika
- Jitahidi ukubalike kwa jamii ya watafitiwa
- Usiridhike na taarifa au ushuhuda wa mtu mmoja; pata taarifa nyingi za watu mbalimbali kuhusu jambo lilo hilo ili uweze kuzilinganisha
- Chagua wakati unaofaa kulingana na utaratibu wa maisha wa wahusika (k.m. usiwe wakati wa kuandaa mashamba, au wakati usioendana na tukio unalotaka kulitafiti)
- Chagua msaidizi/mkalimani wa kufaa iwapo kuna haja
- Kuwa na shukrani kwa wanaokusaidia.
4. Uchambuzi wa Data
4.1 Nukuu taarifa zote
4.2 Tafsiri taarifa unazohitaji (iwapo ziko katika lugha tofauti)
4.3 Tathmini data zote kwa makini (k.m. kwa kulinganisha na nyanja au vyanzo vingine, kama vile akiolojia, historia, sayansi, n.k.
4.4 Fanya uchambuzi wako kwa kutumia mbinu na nadharia ulizozichagua. Tumia pia fasili za watafitiwa au wanajamii inayohusika kama zipo.
4.5 Andika Ripoti na mahitimisho
4.6 Tayarisha Ripoti ya Fedha
4.7 Kabidhi Ripoti zote kwa Mdhamini/Msimamizi au yeyote anayehusika.
UTAFITI: UKUSANYAJI WA DATA

MBINU ZA UTAFITI
UKUSANYAJI WA DATA
1. UKUSANYAJI WA DATA HUTAWALIWA NA MAMBO 4:
a) Uwanja wa taaluma unaohusika
b) Lengo/madhumuni ya utafiti
c) Uwezo na nyenzo alizo nazo mtafiti
d) Muda alio nao mtafiti
2. VIFAA VYA UTAFITI (WA FASIHI NA LUGHA)
2.1 Vifaa vya Utafiti
Hutegemea aina ya utafiti, lakini aghalabu baadhi ya vifaa hivi, kama si vyote, hutumika:
a)     Shajara ya uwandani
b)    Kalamu na karatasi za kuandikia kumbukumbu
c)     Tepurekoda na vifaa vyake
d)    Video/kamrekoda na vifaa vyake
e)     Kamera na vifaa vyake
f)      Kompyuta na vikorokoro (accessories) vyake
g)     Vidadisi (hojaji) na dodoso
h)    Vifaa vya kupimia/kuhesabia
i)       Darubini, vionambali, n.k.
3. NJIA KUU ZA UTAFITI
a) Utafiti wa maktabani/ wa nyaraka
b) Utafiti wa uwandani
c) Utafiti wa maabarani/studioni
4. UTAFITI WA MAKTABANI/NYARAKA
4.1 Nyaraka asilia (primary documents)
a) Nyaraka rasmi/za kiserikali
b) Nyaraka binafsi (barua, shajara, majalada, kumbukumbu, vyeti, n.k.)
4.2 Nyaraka fuatizi (secondary documents)
a) Nyaraka rasmi/za kiserikali
b) Nyaraka binafsi (vitabu, kumbukumbu, ripoti, magazeti,  n.k.)
5. UTAFITI WA UWANDANI
Mbinu za utafiti:
a) Kushuhudia (observation)
b) Kushiriki (paticipation)
c) Mahojiano (interviewing)
d) Mijadala ya vikundi lengani
e) Kutumia vidadisi na majedwali
5.1 Mbinu ya kushuhudia (observation)
Kushuhudia ni mbinu ya kuangalia tukio linapotendeka na kukusanya taarifa zake.
5.1.1 Namna za ushuhudiaji
a) Uchunguzi na upimaji (k.m. katika jiografia, muziki)
Mtafiti awe na vifaa vinavyohitajika kwa kazi hiyo (k.m. rula, mizani, vipima-sauti)
b) Ushuhudiaji fungemno (highly structured observation)
- kwa kutumia mandhari yaliyodhibitiwa
- kwa kutumia majedwali yaliyosanifiwa
c) Ushuhudiaji funge (structured observation)
- unatoa uhuru zaidi
- huchanganya majedwali na mahojiano
- mtafiti si mshiriki, lakini huangalia na kukusanya taarifa waziwazi
- taarifa za ushuhudiaji husaidiana na taarifa za mahojiano na vidadisi
d) Ushuhudiaji lengani (focused observation)
- mtafiti huangalia tukio/tendo katika mazingira yake asilia bila majedwali. Taarifa hupatikana kutokana na kuzoeana na kuwa na mawasiliano ya muda mrefu na watafitiwa.
e) Ushuhudiaji huru/ usiofunge (unstructured observation)
- hufanywa kwa siri na mtafiti bila mtafitiwa kufahamu na bila mpangilio wa wazi.
5.1.2 Ukusanyaji wa taarifa za ushuhudiaji
a) Majedwali: hujazwa na mtafiti au msaidizi wake
b) Uandishi wa taarifa
Taarifa huandikwa wakati wa ushuhudiaji usio wa kificho. Taarifa hizo inabidi ziwe na mambo yafuatayo:
- tarehe
- mahali
- wakati
- mtu/watu wanaohusika
- vifaa
- maelezo ya lengo la shughuli
- maelezo ya mandhari
- mfuatano wa matukio
- ufafanuzi wa shughuli zilizofanyika
- hisia na ukereketwa wa wahusika
c) Kupata taarifa za nyongeza
Taarifa za nyongeza zipatikane kutokana na:
- mazungumzo
- mahojiano
- nyaraka
- rekodi za kanda/video
- pichatuli
- chati, michoro na ramani
5.1.3 Tafsili ya taarifa (interpretation of data)
Tafsili ya taarifa za uwandani isitokane na hisia au mawazo ya mtafiti mwenyewe tu, bali itokane na kushirikisha watafitiwa wenye ufahamu wa mambo hayo.
5.1.4 Faida na mipaka ya utafiti wa kushuhudia
a) Faida
Humwezesha mtafiti:
- kukusanya taarifa kwa mpangilio mzuri
- kutaamali matendo na matukio ya kijamii moja kwa moja yanapotokea
- kuchunguza duru za shughuli au tabia katika mazingira yake asilia ya kijamii
- kuchunguza namna watu wanavyoishi na kufanya kazi bila kuingilia shughuli zao
- kukusanya taarifa ambazo haziwezi kupatikana kwa njia ya mahojiano au mazungumzo
- ni njia inyomwezesha mtafiti kupata taarifa nyingi kwa gharama ndogo
b) Mipaka/upungufu
- baadhi ya shughuli au matukio yanayochunguzwa hayawezi kufikiwa au kuonekana na mtafiti
- wakati mwingine, kuwapo kwa mshuhudiaji huweza kupotosha au kuathiri shughuli inayohusika
- njia hii hufaa zaidi kwa matukio ya wakati uliopo; haifai kutumika kuchunguza matukio yaliyopita/ya zamani
- njia hii haifai kwa kukusanya taarifa kuhusu mikabala, maoni, nia, maana, n.k.
- njia hii haifai kwa kuchunguza makundi makubwa ya watu
- huweza kuchukua muda sana, na haifai kwa kuchunguza mwenendo au mchakato kwa muda mrefu sana
5.1.5. Matatizo ya uhusiano kati ya mshuhudiaji na mshuhudiwaji
a) Unawezaje kushuhudia bila kushuhudiwa?
b) Utawezaje kuepuka “athari ya kuangaliwa” – inayomfanya mtafitiwa kutotenda mambo kikawaida kutokana na kuwapo kwa mtafiti?
Baadhi ya njia za utatuzi
a) Kama inawezekana, jifanye mshuhudiaji-mshiriki
b) Pata imani ya wale unaowatafiti kwanza (hili huchukua muda)
c) Chunguza bila kuonekana (utafiti wa siri) -  hili nalo lina matatizo ya kiitikeli!
d) Jaribu kuwapo bila kuvutia nadhari ya washiriki
e)  Wakati wa kutafsili data yako, zingatia athari ya kuwapo kwako wakati wa kuikusanya
5.2 Utafiti kwa kushiriki
Utafiti huu unahusu kwenda kuishi na kushiriki katika shughuli za wale unaowatafiti/ unazozitafiti
5.2.1 Manufaa ya njia hii
a) Hukuwezesha kuwafahamu vizuri watu na shughuli unazotaka kuzitafiti, na pengine kukubaliwa na hao unaowatafiti
b) Kutokana na tajiriba unayoipata kwa kuangalia na kushiriki, unapata ufahamu wa undani wa yale unayoyatafiti
5.2.2 Mipaka
a) Utafiti wa kushiriki huweza kuhitaji muda mrefu zaidi kuliko ule alio nao mtafiti
b) Si mara zote unaweza kushiriki katika shughuli unayoitafiti: Mifano
- shughuli ya siri au mwiko
- shughuli haramu/ya kuvunja sheria
- shughuli isiyokubalika kijamii
- shughuli ya hatari
- shughuli inyodai sifa za kipekee kutoka kwa mtafiti (ambazo hana)
- mtafiti-mshiriki huweza kuona ugumu kukaa kando na kuichunguza shughuli inayohusika kwa uhuru bila kuelemea upande fulani
6. MAHOJIANO
6.1 Mahojiano ni nini?
Ni majibizano ya ana kwa ana (au ya simu, kidijitali/barua pepe), kati ya watu wawili au zaidi kwa lengo la kukusanya taarifa au maoni kuhusu suala fulani la kiutafiti lililoainishwa
6.2 Mambo ya kuzingatia wakati wa mahojiano
a) Uchangamfu – usioneshe uhasama au chuki
b) Kutoelemea upande fulani
c) Jieleze kikamilifu ueleweke wewe ni nani na una nia gani
- onesha vitambulisho na vibali iwapo kuna haja
d) Kujenga muamana
- mhakikishie mhojiwa kuwa mahojiano ni siri baina yenu wawili
- anza na maswali ya jumla kabla ya kuingilia maswali mahsusi
- maswali nyeti yaulizwe baadaye kabisa mkishazoeana
- mwishoni muulize mhusika kama ana swali au ombi
e) Muktadha wa kijamii: mila, utamaduni na maadili ya mahali panapohusika
- kuhoji mtu wa jinsi, umri, cheo tofauti
- miiko (k.m. kuhesabu watu, watoto)
- kanuni za maingiliano (jinsi, tabaka, ngazi za madaraka)
- uvaaji
f) Muktadha wa tukio
- ulinge wa mahojiano (wa ndani, wazi kwa kila mtu)
- madhanio ya mhojiwa kuhusu madhumuni ya mtafiti
- madhanio yako kuhusu mhojiwa
- tabia, mwenendo na heba za wahusika
6.3 Mambo ya kuepuka
- kukusanya habari usiyoihitaji
- kutafuta taarifa ili kuhalalisha msimamo au imani yako
- ushabiki
- kudokeza majibu yanayotarajiwa
- tamaa ya kujua kila kitu mpaka kuvuka malengo yaliyokusudiwa
- kuonesha “ubosi” – kuwa rasmi mno, kutosikiliza vizuri maelezo, kukatisha maelezo bila kujali hisia za mzungumzaji, n.k.
6.4 Mambo yanayoathiri wahojiwa
a) Athari hasi
- kazi nyingi
- aibu ya kuonekana kuwa mjinga
- kutovutiwa na maudhui ya mahojiano
- kutovutiwa na mwenye kuhoji
- hofu (ya matokeo)
- ukosefu wa motisha (kifedha?)
- mahusiano binafsi na mhojiwa
b) Athari chanya
- kuvutiwa na mwenye kuhoji
- kuvutiwa na maudhui
- ufahari (kuonekana unahusiana na asasi au mtu anayefanya utafiti)
- wajibu (kuonekana kuwa raia mwajibikaji)
- upweke
- matarajio ya tunzo (fedha au zawadi)
- mahusiano binafsi na mhojiwa
6.5 Matatizo ya kiutekelezaji
a) fedha
b) usafiri
c) hali ya hewa/tabianchi (muda wa utafiti uzingatie mambo haya)
d) usampulishi (sampling): nani wahojiwe, kwa nini na lini?
- sampuli kutegemea fursa (opportunity sample) – wale ambao ni rahisi kuwahoji
- sampuli nasibu (random sample)
- sampuli nasibu tabakishi (stratified random sample) – hukuwezesha kupata aina ya watu unaowahitaji
- sampuli-kusudio (purposeful sample)
- sampuli-mgawo (quota sample)
- sampuli-tajwa (snowball sample), n.k.
6.6 Aina za mahojiano
a) Mahojiano funge (structured interviews)
- hujikita katika jedwali/ hojaji zilizotayarishwa kabla
- hufaa kama maswali mengi yasiyohitaji mjadala mkubwa yataulizwa
b) Mahojiano nusu-funge (semi-structured)
- jedwali hutumika, lakini huacha mwanya kwa maswali mengine
c) Mahojiano huru (unstructured)
Haya ni mahojiano ya kina zaidi, na huhitaji ujuzi na umakinifu katika kumwongoza mhojiwa kutoa taarifa zinazohitajika
- mahojiano huweza kuwa sanifu au huru
- njia itakayoteuliwa kutumika itategemea lengo
6.7 “Mahojiano” dhidi ya “Hojaji”
Uamuzi wa kutumia njia ya usaili au hojaji hutegemea mambo yafuatayo:
a) Aina ya suala linalotafitiwa
b) Aina ya utafiti
c) Malengo ya utafiti
d) Aina za maswali yanayoulizwa
e) Walengwa (k.m. wasiojua kusoma na kuandika, wasomi, n.k.)
6.8 Faida za mahojiano
a) Hukuruhusu kuuliza maswali ya papo kwa papo na kufahamiana na mhojiwa
b) Hukuruhusu kuuliza mhojiwa maswali ya binafsi na ya ikirari (factual)
- yeye ni nani
- anafikiria nini, ana maoni gani
- anahisi nini, n.k.
c) Hukusanya tabasuri na tafsili za wahusika kuhusu matukio yanayotafitiwa
d) Huwaruhusu wahojiwa kuelezea misukumo na sababu za mienendo yao
e) Hukuwezesha kuuliza maswali tokezi au ya nyongeza
6.9 Hasara/mipaka ya mbinu ya mahojiano
a) Taarifa inayopatikana kwa kawaida huelemea upande mmoja
b) Wahojiwa wengine hushindwa kujieleza kutokana na haya au sababu nyinginezo
c) Njia hii hutegemea uhusiano unaojengeka kati ya mtafiti na mhojiwa; muulizaji mbaya huibua muulizwa mbaya
d) Njia hii hutawaliwa na muktadha mahsusi
7. HOJAJI
8.1 Hojaji ni nini?
Orodha (kwa maandishi) ya maswali au mambo yanayohitaji kujibiwa au kuelezewa na wahojiwa kwa lengo la kukusanya taarifa. Hivyo hojaji ni zana ya kukusanya na kurekodi taarifa.
8.2 Manufaa ya Hojaji
a) Ina gharama ndogo na ni rahisi kutumia
b) Huweza kupelekwa kwa wahojiwa wengi
c) Ni rahisi kuchanganua (iwapo imebuniwa kwa makini na ustadi)
d) Huweza kuibua taarifa nyingi katika muda mfupi
e) Huhifadhi usiri (hasa kama haitaji majina)
8.3 Mapungufu/hasara ya kutumia Hojaji
a) Hutegemea uaminifu wa wahojiwa (kwa vile hakuna fursa ya mahojiano ya ana kwa ana)
b) Mwitiko wakati mwingine huwa mdogo
c) Huweza kukabiliwa na matatizo ya kiutekelezaji (k.m. huduma hafifu za posta au intaneti)
d) Haziwezi kujazwa na watu wasiojua kusoma na kuandika
e) Hakuna fursa kwa mtafiti kuweza kufafanua maswali yake kwa mhojiwa
f) Hakuna fursa kwa mhojiwa kufafanua majibu yake
8.4 Namna ya kuandaa Hojaji
a) Uwe na hakika kuhusu lengo lako: ni nini hasa unataka kukifahamu na kwa nini?
b) Maswali yawe mafupi (usiingize maswali yasiyohitajika, k.m. ya kiwasifu).
c) Hojaji isizidi kurasa 10, na ikiwezekana isichukue zaidi ya dakika 15 kujaza
d) Uliza swali sahihi kwa mhojiwa sahihi
e) Epuka maswali ya kibinafsi au yanayodhalilisha au kuudhi (k.m. yahusuyo siri za binafsi)
f) Epuka lugha ya jaziba
g) Tumia lugha sahili
h) Epuka lugha ya kitaalamu, ila kama unawahoji wataalamu wa uwanja unaohusika
i) Swali lilenge jambo moja, lisiulize mambo mengi
j) Usimweke mhojiwa katika hali ngumu akashindwa kukujibu (k.m. swali kama “je, sasa umeacha wizi?”)
k) Usichanganye matakwa ya ikirari (factual) na yale ya tathmini katika swali lilelile
l) Changanya mitindo ili usimchoshe mhojiwa
m) Mpangilio
- anza na taarifa za lazima kisha nenda kwenye taarifa zisizo za lazima
- anza na maswali yasiyoelemea upande mmoja
n) Maelekezo kuhusu namna ya kujaza Hojaji yawe bayana
o) Epuka maswali yanayodokeza jibu
p) Zingatia mahitaji ya kiuchanganuzi; k.m. iwapo utatumia kompyuta kuchanganua data, ni vizuri Hojaji ikawa na mfumo unaokubalika kikompyuta, k.m. matumizi ya misimbo
q) Mwishoni mwa Hojaji andika neno la Shukrani
r) Kumbuka kuandika vizuri anwani yako (ya posta na anwani-pepe), na hata namba ya simu, kwenye Hojaji au barua utakayoambatisha
s) Toa ahadi ya kutunza siri
t) Toa ahadi ya kumpelekea mhojiwa “Muhtasari wa Matokeo ya Utafiti” iwapo atauhitaji
u) Onesha tarehe na siku ya kutuma Hojaji na tarehe na siku ya mwisho ya kurejeshwa kwa Hojaji
v) Onesha tarehe halisi ya kurejeshwa kwa Hojaji (k.m. Jumatano, 10/2/2010)
w) Hakikisha kwamba Hojaji ni safi na inavutia
8.5 Namna ya kutunga maswali ya Hojaji
a) Ikibidi maswali-funge yajaliziwe na maswali ya kujadili
b) Wakati mwingine kauli funge (structured statements) ni bora kuliko maswali
c) Maswali yanayodai maelezo, japo magumu, huweza kuibua taarifa nyingi zaidi
d) Orodha: Huweza kutumika kwa kumtaka mhojiwa ateuwe mambo fulani kutoka katika orodha
e) Maswali ya uteuzi wa jibu (multiple choice) sahihi huweza pia kutumika
f) Kupanga kingazi (rating): k.m. kitarakimu (1-9)
g) Udarajishaji (rankings): chagua njia inayofaa
h) Skeli- Liketi (Likert Scales): zitumike kupimia mikabala, hisia, n.k. Majibu huweza kupewa thamani za kitarakimu: kwa mfano: nakubali, sijaamua, sikubali, nakataa kabisa
8.6 Usambazaji wa Hojaji
a) Kutumia posta
b) Kupeleka kwa mkono (kama sampuli ni ndogo)
c) Kutumia mawakala/wasaidizi
d) Kama mwitiko ni hafifu, waandikie wahojiwa, wapigie simu au watembelee kama wapo karibu
e) Hojaji zinazorejeshwa zirekodiwe vizuri na kuhifadhiwa
f) Hojaji ziharibiwe iwapo hazihitajiki tena
MAREJELEO
Adam, J na Kamuzora, F (2008) Research Methods for Business and Social Studies.          Morogoro: Mzumbe Book Project.
Bowern, C (2008) Linguistic Fieldwork: A Practical Guide. New York: Palgrave-     Macmillan.
Kothari, C.R (2004) Research Methodology: Methods and Techniques. New Delhi: New    Age International.
Msokile, M (1993) Misingi ya Uhakiki wa Fasihi. Nairobi: EAEP.
Mulokozi, M.M. (1983) “Utafiti wa Fasihi Simulizi” katika TUKI Makala ya Semina ya          Kimataifa ya Waandishi wa Kiswahili III: Fasihi. Dar es Salaam: TUKI.: kur. 1-25.
Ogechi, N.O, N.L  Shitemi, na K. I. Simala (wah) (2008) Nadharia katika Taaluma ya Kiswahili na Lugha za Kiafrika. Eldoret: Moi University Press.
Pons, Valdo (Mh) (1992) Introduction to Social Research. Dar es Salaam: DUP.
Sewangi, S.S. and Madumulla J.S. (eds) (2007) Makala ya Kongamano la Jubilei ya TUKI (Vol. I and II) Dar es Salaam: TUKI.
Simala, K.I. (mh) (2002) Utafiti wa Kiswahili. Eldoret: Moi University Press.
MASWALI YA MTIHANI
1. Eleza na kujadili faida na mipaka ya mbinu ya kushuhudia ya utafiti wa uwandani.
2. Eleza na kujadili faida na mipaka ya utafiti-shiriki kama njia ya kukusanya taarifa uwandani.
3. Fafanua dhana ya usampulishi na aina zake. Eleza namna unavyoweza kutumia mbinu ya usampulishi katika utafiti wa lugha AU fasihi.
4.  Fafanua dhana ya hojaji. Taja na kujadili angalao mambo kumi yanayofaa kuzingatiwa wakati wa kuandaa hojaji ya utafiti wa lugha AU fasihi.
ORODHA YA ISTILAHI ZILIZOTUMIKA
ISTILAHI
hojaji (questionnaire)   
ikirari (fact); - a ikirari: factual
itikeli (ethics)
jedwali (schedule)
kauli funge (structured statement)
kidadisi (questionnaire)
kikundi-lengani (focus group)
kupanga kingazi (rating):
kushiriki (paticipation)
kushuhudia (observation)
mahojiano (interviewing)
mahojiano funge (structured interviews)
mahojiano huru (unstructured)
mahojiano nusu-funge (semi-structured)
maswali tokezi (follow-up questions)
mhojiwa (interviewee)
mijadala ya vikundi lengani (focus-group discussions)
nyaraka asilia (primary documents)
nyaraka binafsi (barua, shajara, majalada, kumbukumbu, vyeti, n.k.) (private documents)
nyaraka fuatizi  (secondary documents)
pichatuli (photographs)
sampuli (sample)
sampuli kutegemea fursa (opportunity sample)
sampuli nasibu (random sample)
sampuli nasibu tabakishi (stratified random sample)
sampuli-kusudio (purposeful sample)
sampuli-mgawo (quota sample)
sampuli-tajwa (snowball sample)
shajara (diary)
Skeli- Liketi (Likert Scale)
tabasuri (perspective)
tabianchi (climate)
tafsili (interpretation)
tajiriba (experience)
udarajishaji (rankings)
usampulishi (sampling)
ushuhudiaji fungemno (highly structured observation)
ushuhudiaji huru/ usiofunge (unstructured observation)
ushuhudiaji huru/ usiofunge (unstructured observation)
ushuhudiaji huru/ usiofunge (unstructured observation)
ushuhudiaji lengani (focused observation)


CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM
TAASISI YA TAALUMA ZA KISWAHILI
IDARA YA LUGHA YA KISWAHILI NA ISIMU.

RIPOTI YA UTAFITI.

JINA LA MWANAFUNZI:  NDUMBARO, ERIC F.

MSIMAMIZI: MWL. E. MAHENGE.  

MHADHIRI: DKT.   G. MRIKARIA.

MADA YA UTAFITI:

DHIMA NA DHAMIRA KATIKA NYIMBO ZA KABILA LA WAMATUMBI.                                             

YALIYOMO.

Shukrani
Utangulizi

SURA YA KWANZA.

1.0    Historia ya Wamatumbi ….………..……………………………….....1
1.1    Usuli wa nyimbo…………….………………………………………...4
1.2    Tatizo la utafiti …………………………..............................................4
1.3    Lengo la utafiti ………………………………………………………..5
1.4    Malengo mahususi………………………………....……………….....6
1.5    Maswali ya utafiti………………………… ……….…….…...............6
1.6    Umuhimu wa utafiti…………….…………………………………......6

SURA YA PILI.

2.0      Mapitio ya makala na vitabu……………………..……….………….8
2.1      Pengo la utafiti……………………………………………………...10
2.2      Fasili Mbalimbali…………………………………………………...10
2.2.1   Dhima…………………………………………………...………….10
2.2.2   Dhamira……………………………….....…………..……………..11

SURA YA TATU.

3.0      Mawanda ya utafiti………………………………………................12
3.1      Mbinu za ukusanyaji data …………..……………………………..12 
3.1.1   Uhojaji ………………..……………………………........................12
3.1.2   Mbinu ya maktabani ….….…………………………...……............13
3.2      Zana za utafiti………………………………...………………….....13
3.3      Uteuzi wa sampuli…………………………..………………….......13
3.4      Jedwali la sampuli ya watafitiwa………………………………..….14
3.5      Changamoto za utafiti……………………………………………....14
3.6      Nadharia ya utafiti ………................................................................15
3.6.1   Nadharia ya Uamilifu………………………………………..……..15
3.6.2   Nadharia ya Umarx……………………………..………………......15

SURA YA NNE.

4.0      Uchambuzi wa data……………………………………..……......…17
4.1      Matokeo ya utafiti…………………………………….………….....18
4.1.1   Dhima ya kuelimisha……………………....…………………….....18
4.1.2   Dhima ya kuburudisha……………………………………………...25
4.2.     Uchambuzi wa dhamira………………………………………….…26
4.2.1   Dhamira ya maadili mema………………………........................26     
4.2.2   Dhamira ya uongozi mbaya………………………………..….……26
4.2.3   Dhamira ya kuonya……………………………………..……….….27
4.2.4   Dhamira ya umoja na mshikamano…………………………..…….27
4.2.5   Dhamira ya uaminifu………………………...........................……..27
4.2.6   Dhamira ya heshima…………………………………..................…28
4.2.7   Dhamira ya uzazi wa mpango………………………………............28

SURA YA TANO.

5.0      Hitimisho………………….…………….……………….…………29
5.1      Mapendekezo……………………………...…………………..........29
5.2      Marejeo ………………………..……………………………...........31
5.3      Viambatanisho …………………………………..….…….........…..33

Shukrani.

Ni dhahiri kwamba kazi nyingi na zilizo bora hukamilika kwa ushirikiano wa watu mbalimbali, Kama wasemavyo waswahili, ‘penye wengi hapa haribiki neno’. Hivyo basi utafiti huu umeweza kukamilika kutokana na ushirikiano wa watu mbalimbali.
Nitakuwa sina fadhila kama sitawashukuru wale wote walionisaidia katika kufanikisha utafiti huu. Ni vigumu kumtaja kila mtu kwa jina lake, kwani wapo wengi sana walionisaidia katika hatua mbalimbali za utafiti huu. Haitakuwa dhambi kama nikiwataja wachache kwa niaba ya wote. Nikianza na Dkt. G. Mrikaria aliyenifundisha mbinu za utafiti akishirikiana na Mwl. E Mahenge. Shukrani nyingi zikufikie Dkt.
Pia ninatoa shukrani za dhati kwa Mwalimu wangu Elizabeth Mahenge ambaye ndiye msimamizi wangu katika utafiti huu, na mshukuru sana kwa juhudi zake ambazo ndizo zimeniwezesha kukamilisha utafiti huu.
Vile vile kwa namna ya pekee ninatoa shukrani zangu kwa Sr. Anselimina Mtumbuka kwa mchango wake mkubwa uliofanikisha ukusanyaji wa data zilizotumika katika utafiti huu na pia amesaidia sana katika kuwapata watu wa kabila la Wamatumbi niliofanya mahojiano nao.
Mwisho napenda kuwashukuru rafiki zangu, Padre Rogerio Massawe ( M.A. Linguistics and foreign languiges) pamoja na wanafunzi wenzangu wa B.A Kiswahili kwa mchango wao wa mawazo ulionisaidia katika utafiti huu. 

UTANGULIZI.
Utafiti huu unashughulikia dhima na dhamira katika nyimbo za kabila la Wamatimbi wanaoishi katika wilaya ya Kilwa mkoa wa Lindi kusini mwa Tanzania. Utafiti huu umegawanyika katika sehemu/sura tano kama ifuatavyo;
Sura ya kwanza ni historia fupi ya kabila la wamatumbi, sura ya pili imeshughulika na mapitio ya makala na vitabu mbalimbali vilivyohusu nyimbo, sura ya tatu imejikita katika mawanda ya utafiti, nadharia zilizotumika katika uchambuzi wa nyimbo za kabila la wamatumbi, sura ya nne ni uchambuzi wa data zenyewe katika vipengele vya dhima na dhamira na sura ya tano hitimisho, mapendekezo, marejeo pamoja na viambatanisho.
SURA YA KWANZA.

1.0     Historia ya kabila la Wamatumbi.
Historia ya kabila ya Wamatumbi kwa mujibu wa Wamatumbi waliohojiwa na mtafiti. Baadhi ya watafitiwa waliohojiwa ni mwanamke/mama wa kabila la kimatumbi mwenye umri wa miaka 45 pamoja na mzee wa kimatumbi mwenye umri wa miaka 78. Wahojiwa wote wawili hawakuonesha tofauti kubwa sana katika maelezo yao. Hivyo basi, kwa mujibu wa wahojiwa hawa walieleza kwamba;
Wamatumbi ni kabila la Tanzania wanaoishi katika Wilaya ya Kilwa tarafa ya Kipatimo mkoa wa Lindi kusini mwa Tanzania. Wanaendelea kusema, eneo wanamoishi Wamatumbi ni eneo la milima, kwa kilugha neno milima ni ‘itombi’ au ‘itumbu’, hivyo basi watu waliwaita hawa wanaoishi milimani ‘amatumbi’ yaani wamilimani. Aghalabu asili ya Wamatumbi ni mchanganyiko wa makabila mbalimbali yaliyofika eneo hilo kwa sababu ya kukimbia vita. Wengi wao walikuwa wametokea ungonini (wangoni) ambao kwa asili waliitwa ‘-nzalendo’ mmoja na ‘-nzalendo’ ni wingi, yaani wenyeji. Wageni waliokuja baadaye kwa matembezi au biashara ndiyo waliwaita hawa wanaoishi milimani ‘amatumbi.’
Shughuli za uzalishaji mali; wamatumbi hujishughulisha zaidi na kilimo kama shughuli yao kubwa. Katika kilimo hulima mazao ya aina mbalimbali kama vile mpunga ambao ndio chakula chao kikuu, pamoja na mpunga wamatumbi hulima mahindi, mtama, mihogo na matunda.
Mila, desturi na tamaduni; katika makala ya Profesa Chachange Seithy “Utandawazi na Migogoro ya Utamaduni”. Chachange akimnukuu Mwalimu Julius K. Nyerere (1962) katika hotuba yake ya uzinduzi wa Jamuhuri ya Tanganyika pamoja na masuala mengine, mwalimu aliongelea kuhusu historia ya utamaduni wa Tanganyika. Naye alitamka kwamba; “…Nchi isiyokuwa na utamaduni wake ni sawa na mkusanyiko wa watu ambao hawana roho iwezeshayo kuwa Taifa”.
Wamatumbi hawa waliohojiwa walieleza kwa ufahasa kuhusu utamaduni wao wakiamini kwamba utamaduni wao ni moja ya tamaduni zilizowezesha au zilizochangia kuwepo na Taifa la Tanzania. Kwa mujibu wao walieleza utamaduni wa wamatumbi kama ifuatavyo;
Kuoa na kuolewa; kwa wamatumbi mwanaume anayetaka kuoa huenda kwa wazazi wa msichana yeye pamoja na mshenga wake kueleza nia yao. Wazazi wa kikubali kwa kutambua umuhimu wa familia kama kuongeza uzao wanakaa kifamilia, kisha watamtuma mshenga kuwataka upande wa kiume wapange siku ya kwenda ‘kupiga hodi’ kwa mwanamke. Siku hii ndipo wataambiwa rasmi kwamba wamepata binti. Siku hiyo upande wa kike wataandaa chakula maalamu kwa wageni. Upande wa mwanaume anayetaka kuoa utaleta kuku jike na mchele kama alama ya shukrani kwa kukubaliwa.
Siku ya harusi yenyewe wamatumbi huita ‘Lichengele,’ siku hii upande wa mwanamke na mwanaume huandaa mali au mahitaji kwa maharusi kwa ajili ya kuanzia maisha. Hivyo, pande zote mbili hutoa vitu mbalimbali na kuweka pamoja vikiwa vimechanganywa. Tendo hili la kuweka pamoja au kuchanganya huitwa ‘nyangabano’ yaani mchanganyiko. Baada ya sherehe za harusi upande wa kiume huondoka na mke wao.
Mahari (ndweko); kwa Wamatumbi huwa ni makubaliano ya pande zote mbili. Hutolewa mali kama chakula, mifugo/kuku au pesa na hivi huletwa siku ya lichengele/harusi.
Kuzaliwa; mtoto wa kwanza akizaliwa upande wa kiume wanatoa zawadi kwa upande wa kike, tendo hili huitwa ‘lwalo’. Pia kitovu cha mtoto mchanga ni kitu muhimu sana kwa wamatumbi kwani watoto wote wanaozaliwa vitovu vyao hufichwa au huchimbiwa ardhini na hii ni siri ya mama na shangazi wa mtoto tu. Kwa nini kuficha au kuchimbia ardhini? Wanaamini kuwa wachawi hutumia vitovu kwa kulogea au wakipata kitovu huweza kumuua mtoto.
Majina; licha ya majina ya ukoo ambayo hurithiwa na ukoo mzima, wamatumbi hasa wanaume wana desturi ya kujipa majina mengine yenye sababu au maana. Majina haya huwa ya utani yenye lengo la kufurahisha jamii au kujitapa na kujionesha yeye ni nani katika jamii. Mfano wa majina hayo ni kama ifuatavyo;
Kibaga= ‘Banga’ maana ya kupiga, kibaga yaani asiyepigika/mwenye nguvu. Ngemba= asiye na chakula/wali. Chakula kikuu ni wali hivyo kutokuwa na wali ni balaa kubwa. Wali huitwa ‘mba’. Ndaune iyunge= anayetafuna uchawi yaani hawezi kulogwa. Ndaune mase mauu= mnywaji tembo aliyekithiri. Tembo ni pombe inayogemwa kwenye mnazi ambayo hufanana na maji yaliyowekwa maziwa kwa mbali. Hii ni pombe maarufu kwa wamatumbi. ‘Mase mauu’ yaani maji meupe. Mpou= anayewapooza wagonjwa na kuwapatia nafuu. Likaino= mnajisumbua bure, Nkunda bule= mnajihangaisha bure, Raisi= mkuu wa ushirikina (gwiji). Liboi= anayetoweka kwa wepesi inapotokea vurugu/fujo, Kinoga kwiye= ni mwanaume mwenye sura mbaya au umbile lakini hakosi mchumba. ‘Kwiye’ yaani ng’ambo nyingine, kwa hiyo hapa mtamwona mbaya lakini kule kuna wanaompenda ambao hawaoni ubaya wake. Mbenjege= mjeuri/hashindwi/mkorofi.  
Masuala ya Imani; Wamatumbi wanaamini juu ya Mungu wa kweli ambaye ni Mungu wa juu/mbinguni na chini ndiye wanayemtambikia. Pia wanaamini mambo ya kishirikina kama vile uchawi.
Kifo; katika kifo wanaami kuwa mtu mwema akifa ameaga dunia, anaenda juu/mbinguni na mtu mwovu anaenda ‘kumbembetu’ yaani mahali kubaya kusiko faa kuishi/motoni.
Utawala wa kijadi; mkuu wa mahali huitwa ‘Liwali’. Huyu alikuwa na eneo kubwa alilomiliki binafsi, chini yake alikuwa ‘Jumbe’ yaani makamu wake. Koo kama za akina Bungara, Litonya zilivuma kwa sifa ya uliwali huo Mingumbi.
Elimu; katika elimu licha ya unyago na jando kama elimu msingi, pia kulikuwa na mikutano iliyoongelea mambo mbalimbali kuhusu jamii.  Mikutano hii ilijumuisha wake kwa waume.
Mahakama za kijadi; katika mashtaka mbalimbali walijumuishwa wake kwa waume. Upande ulioshinda mwanawake alisimama na kupiga kigelegele kuonesha furaha na ushindi.
Vile vile katika suala la ngoma/nyimbo wamatumbi wana nyimbo za asili za kabila lao za aina mbalimbali ambazo huimbwa katika matukio tofauti tofauti. Ngoma hizo za kabila la wamatumbi ambazo huambatana na nyimbo ni kama vile zitakavyooneshwa katika lengo la utafiti.   
1.1     Usuli wa nyimbo.
Kulingana na wataalamu na watafiti mbalimbali wa fasihi simulizi kama Sengo (1978) na  Finnegan (1977) wanaeleza kuwa, nyimbo zilianza pale tu binadamu alipoanza kupambana dhidi ya mazingira yake katika shughuli mbalimbali za uzalishaji mali.
Mazigwa (1991) anaeleza kwamba, nyimbo kama kipengele kimojawapo cha fasihi simulizi ni hazina ambayo huhifadhi na kusambaza mawazo juu ya maisha ya binadamu na maendeleo yake, kwa kufanya hivyo nyimbo huweza kutoa mafunzo mbalimbali kama vile kuonya, kukosoa na kuadilisha jamii.   
Naye Mwakasaka (1977) alifanya utafiti wa nyimbo katika kabila la Wanyakyusa. Katika utafiti wake ameona kuwa sanaa ya kutunga nyimbo inahitaji kipaji maalamu, ujuzi wa kuwasilisha mawazo kiufundi na matumizi makubwa ya picha. Pia anasema kwamba wakati mwingine nyimbo huandamana na vifaa vya kimuziki.
Finnegan (1977) kwenye utafiti alioufanya kuhusu fasihi simulizi katika Afrika amebainisha kuwa nyimbo huimbwa wakati wa kazi mbalimbali mfano; uwindaji, pia nyimbo huimbwa wakati wa sherehe mbalimbali, kama vile katika harusi.
Kavugha (1977) alichunguza mila na desturi za Wapare na kuona kuwa, katika kabila la wapare siku ya harusi ni siku ya shangwe. Ndugu jamaa na marafiki wa maharusi huja nyumbani kwa bwana harusi kwa shangwe huku wakiimba.
Ingawa tafiti mbalimbali zimefanyika, hakuna tafiti zilizohusu nyimbo za kabila la wamatumbi. Hili ndiyo lililomsukuma mtafiti kutaka kujua hazina na amali ya wamatumbi zinaendelezwaje kwa ajili ya manufaa ya wanajamii wa kimatumbi pamoja na kizazi kijacho na Taifa kwa ujumla.
1.2     Tatizo la utafiti.
Utafiti huu unahusu dhima na dhamira zinazopatikana katika nyimbo za kabila la wamatumbi. Dhamira ni kipengele muhimu sana ambacho hupatikana katika nyimbo za makabila mbalimbali. Mtafiti ameibaini mada hii baada ya kusoma tanzu na vipera vya fasihi simulizi kama vilivyoainishwa na Mulokozi, M.M. (1996)
Wapo wataalamu mbalimbali waliofanya utafiti wa nyimbo za makabila mbalimbali hapa Tanzania ambao ni kama vile: Mulokozi, M.M. amechambua nyimbo za jandoni kutoka Zanzibar (1939), mwingine ni Miyuka (1990) ambaye amechambua wimbo wa jandoni, mwingine ni Mbagule, K. (1961) naye pia amechambua wimbo wa siasa katika kabila la wasukuma.
Hivyo basi, kutokana na msaada wa tafiti hizo, mtafiti alibaini kuwa baadhi ya wataalamu wameelezea maana ya nyimbo na wamefanya utafiti katika makabila hayo lakini hawajafanya utafiti kuhusu dhima na dhamira katika nyimbo za kabila la wamatumbi. Hivyo basi kutokana na kukosekana kwa tafiti zinazohusu dhima na dhamira katika kabila la wamatumbi, mtafiti ameona kuwa hili ni tatizo na linahitaji ufumbuzi. Hivyo katika kutatua tatizo hili utafiti huu utahusu uchambuzi wa dhima na dhamira zilizopo katika nyimbo za kabila la wamatumbi.
Hakuna watu ambao hawajui tatizo hilo, kwa hiyo utafiti huu ukifanywa watu wengi watajua umuhimu wa nyimbo hizo.
Vilevile tatizo lingine ni kwamba, hizi nyimbo za kabila la wamatumbi hazijaingizwa katika maandishi, kwa hiyo zikifanyiwa utafiti zitaingizwa katika maandishi, na baadaye itakuwa ni hazina kubwa kwa kizazi kijacho na Taifa kwa ujumla. Kwa hiyo basi utafiti huu utaziba pengo hilo.  
1.3    Lengo la utafiti.
Lengo kuu la utafiti huu ni kubainisha dhima na maudhui katika nyimbo za kabila la wamatumbi. Mtafiti amechagua lengo hili kutokana na kutokuwepo kwa tafiti zilizofanywa kuhusu nyimbo za kabila la wamatumbi. Kutokana na muda mfupi wa utafiti, mtafiti alichagua kufanya nyimbo za kabila la wamatumbi ambazo ni kama vile Mbola, Tikisa/Legeza, Ndonde, Kongo, Chunje, Nyimbo za jando na unyago na Njege. Mtafiti alichagua nyimbo hizi kwa sababu ya urahisi wa kupatikana kwa data zake na kutokana na uwepo kwa wamatumbi.
1.4     Malengo mahususi.
(i)                 Kuelezea dhima zinazojitokeza katika nyimbo za kabila la Wamatumbi.
(ii)               Kuchambua dhamira zinazopatikana katika nyimbo za kabila la Wamatumbi.
(iii)             Kuchanganua mambo yanayopelekea uibukaji wa dhima na dhamira katika nyimbo za kabila la Wamatumbia.
1.5     Maswali ya utafiti.
          Utafiti huu utajibu maswali yafuatayo:
(i)                 Je, nyimbo za kabila la Wamatumbi zina dhima gani katika jamii hiyo?
(ii)               Je, nyimbo za kabila la Wamatumbi zina dhamira gani?
(iii)             Je, ni mambo gani yanayopelekea uibukaji wa dhima na dhamira katika nyimbo za kabila la wamatumbi?
1.6     Umuhimu wa utafiti.
Kuna haja ya kufanya utafiti zaidi kuhusu tanzu za fasihi simulizi Mulokozi (1996:34) anasema, “Bado tunahitiji maandishi mengi zaidi yanayotokana na utafiti wa uwandani”.
Utafiti huu utasaidia kukusanya data na kuzihifadhi katika maandishi, kwani mambo mengi ya Fasihi Simulizi bado yamehifadhiwa vichwani mwa watu kama sehemu ya kutunzia kumbukumbu. Utunzaji wa kumbukumbu wa namna hii siyo thabiti, kwani wakati wowote data hizo huweza kupotea au kusahaulika kutokana na maradhi au kifo. 
Utafiti huu una umuhimu mkubwa sana kwa Taifa kwani utasaidia kufafanua nyimbo za kabila la wamatumbi ambazo zinaelekea kupotea kutokana na majilio ya wageni pamoja na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Pia utasaidia kuzifanya nyimbo hizi zisambae na kufahamika na watu wengi tofauti na wamatumbi, ndani na nje ya nchi.
Pia utafiti huu utasaidia watu watakao soma matini hii kubadilika kimtazamo na hivyo kuamsha ari ya kudadisi zaidi mambo mbalimbali ya kijamii hususani utamaduni wa jamii mbalimbali. Pia utafiti huu utasaidia wanafunzi mbalimbali katika kutumia kama rejea za tafiti zao.
Vilevile utasaidia kuonesha/kuelewa utamaduni wa Wamatumbi kwa kupitia mbinu ya kisanii ya nyimbo za kabila hilo.


SURA YA PILI.

2.0     Mapitio ya makala na vitabu.
Ili kuweza kujua nyimbo hususani za makabila, mtafiti alisoma makala na vitabu vilivyoandikwa na wataalamu mbalimbali wa fasihi simulizi kama inavyooneshwa katika sura hii;
Balisidya (1987) anatoa fasili ya nyimbo kuwa ni tungo za kishairi zenye kutumia mahadhi, melodia, mkong’osio na muwala. Pia anaeleza kuwa nyimbo huweza kuimbwa na mtu mmoja peke yake ama na wasaidizi wake wakiitikia mkarara.
Mulokozi (1996) anafasili nyimbo kuwa ni utanzu wa Ushairi Simulizi katika Fasihi Simulizi. Anaendelea kufafanua kuwa nyimbo ni kila kinachoimbwa na ambacho kinaambatana na;
(i)                 Muziki wa sauti.
(ii)               Muziki wa ala.
(iii)             Matini au maneno yanayoimbwa.
(iv)             Hadhira inayoimbiwa.
(v)               Muktadha unaofungamana na wimbo huo, kwa mfano; sherehe, ibada na kilio.
Mulokozi anaendelea kusema kuwa, nyimbo ni sanaa yenye dhima kubwa sana katika jamii za kiafrika. Hutumika kuburudisha watu kwenye sherehe au wakati wa mapumziko, kuonya, kufunza, kuarifu, kunogesha hadithi, kuomboleza, kubembeleza mtoto ili alale, kuchapusha kazi, na kutia hamasa vitani.
Nyimbo zinadhima kubwa katika jamii kama vile dhima ya kuelimisha, kuikosoa jamii na kuirekebisha jamii inapokuwa inaelekea kuzama katika dimbwi la upotofu na wakati jamii inapoacha falsafa yake (Mazingira 1991).
Ngure (2004) wimbo ni utungo na mdundo na mahadhi na unaoweza kuimbika. 
Nao Omari na Mvungi (1981) wanaelezea kuwa nyimbo zipo katika fasihi simulizi na ni za kimapokeo, kila kizazi kinapokezana nyimbo hizo, hali hii ya kupokezana siyo kashifa bali ni sifa mojawapo ambayo binadamu peke yake anayo. Kwa kuwa nyimbo hizi hurithiwa kutoka mtu mmoja kwenda mwingine, maneno fulani hubadilishwa kwa sababu ya kutoandikwa au nyongeza ya msimuliaji kutaka masimulizi yake yapendeze.
Guma (1967) amegawa nyimbo katika makundi makuu mawili, kundi la kwanza ni la nyimbo za vitendo na kundi la pili ni la nyimbo za sherehe. Mfano; nyimbo za harusi.
Chesaina (1977) naye amezigawa nyimbo katika vipengele viwili, yaani fani na maudhui ambayo hupatikana katika aina mbalimbali za nyimbo. Kwa mfano nyimbo za jando na unyago dhamira zinazoweza kupatikana ni malezi, heshima, upendo na uwajibikaji.
Nketia (1963:95) anaeleza kwamba, nyimbo huelezea shughuli za kijamii, kisiasa, kiuchumi na kidini. Nyimbo huimbwa katika nyakati tofauti tofauti kuelezea matukio au hisia tofauti, kwa mfano; huzuni, hasira, kulalamika, kuwasiliana na miungu na kuomba uponyaji. Nyimbo za asili za makabila mengi ya Afrika huimbwa kufuatana na matukio maalum.
Mlama, P (1973:37-41) anamuunga mkono kwa kueleza kuwa, dhima ya nyimbo katika kabila la Wakaguru ni kuitukuza na kuiomba miungu na mizimi ya kiluguru ili ipokee maombi ya watu. Jinsi watu wanavyosali kwa ufundi mkubwa, ndivyo wanavyoiridhisha na kuifurahisha miungu na ndivyo hivyo waombaji wanavyokuwa katika nafasi nzuri ya kusaidiwa. Nyimbo za dini zinatumika katika kuonesha woga na heshima kwa miungu na mizimu na kuifanya miungu na mizimu kupunguza hasira zao kwa watu. Mlama anaelezea kuwa, nyimbo zina dhima kubwa ya kufundisha.   
Nkwera (hakuna mwaka) anasema kuwa, wimbo (nyimbo) ni maneno yanayotamkwa kwa sauti ya muziki, ni maneno yaliyoambatana na uimbaji. Mambo haya mawili, yaani maneno na uimbaji, yamepangwa kwa jinsi ya kugusa na kumwathiri binadamu (au kiumbe kingine pia) kwa namna fulani kupitia hisi zake na akili yake. Uimbaji wenyewe huwa pamoja na mpangilio wa sauti za ala, au bila sauti za ala. Fasili hii inaudhaifu kiasi fulani, kwani sikuzote nyimbo au wimbo huleta athari na kuamsha hisia fulani kwa binadamu na si viumbe wengine kwani binadamu pekee ndiye kiumbe mwenye akili na utashi wa kuweza kupambanua mambo.
Kamusi ya Kiswahili Sanifu (1981) inafasili nyimbo kuwa ni maneno yanayotamkwa kwa sauti ya muziki.
Mtafiti amenufaika sana kwa mapitio hayo ya makala na vitabu mbalimbali kwani amepata maarifa mbalimbali kuhusu utanzu wa nyimbo. Kwa mfano; amejua tafiti mbalimbali zilizokwisha kufanyika kuhusu nyimbo, pia ameweza kubaini pengo lililopo kutokana na mapitio hayo na hivyo kumwia rahisi mtafiti kufanya utafiti wake katika nyimbo za kabila la Wamatumbi.
2.1     Pengo la utafiti.
Kutokana na mapitio hayo ya tafiti mbalimbali mtafiti ameona kwamba tafiti nyingi zimeelezea maudhui ya nyimbo za makabila mbalimbali, lakini kati ya tafiti hizo mtafiti hakuna tafiti zozote zilizoelezea dhima na dhamira katika nyimbo za kabila la Wamatumbi. Hivyo basi, utafiti huu unakusudia kuziba pengo hilo.
2.2     Fasili mbalimbali.
Utafiti huu una lengo la kubaini dhima na dhamira zinazojitokeza katika nyimbo za kabila la wamatumbi. Hivyo basi, msamiati muhimu katika utafiti huu ni dhima na dhamira kama zilivyo fasiliwa kwa mujibu wa wataalam katika kipengele kifuatacho.
2.2.1     Dhima.     
Kulingana na Gibbe (1982) anaeleza kuwa, neno dhima lina maana ya kazi au umuhimu wa kitu katika jamii, kwa hiyo dhima ya nyimbo za kabila la wamatumbi ni sawa sawa na kazi au majukumu yafanywayo na nyimbo za kabila hilo katika jamii.
Katika uchambuzi wa data mtafiti ameona kuwa nyimbo za kabila la wamatumbi zina dhima ya kuelimi na kuburudisha jamii.
2.2.2     Dhamira.
 Kwa mujibu wa Nkwera (hakuna mwaka:30) dhamira ni wazo kuu au adili ambalo mtunzi, kwa mfano mtunzi wa hadithi anataka kuliweka liwe kiini cha hadithi nzima. Ni funzo ambalo mtunzi na mtambaji wa hadithi wamependa, katika mawazo yote yaliyomo katika hadithi yao…
Ana endelea kufafanua kuwa, dhamira ndilo dhumuni mahususi la mtunzi katika kubuni na kusimulia hadithi nzima. Mawazo yake ni kama hulizunguka wazo hilo kuu, hulifafanua na kulipa uzito wake linalostahili.
Mbonde (1999) anasema, dhamira ni mawazo makuu ya kazi ya fasihi, kazi ya fasihi huweza kuwa na dhamira moja au zaidi ya moja
Wataalamu hawa kimsingi wanakubaliana kwamba dhamira ni wazo au mawazo makuu yanayopatikana katika kazi ya fasihi. Kwa mfano, katika nyimbo au hadithi.
Uibukaji wa dhamira katika nyimbo za wamatumbi hutegemeana na matukio mbalimbali yanayo jitokeza katika jamii hiyo. Mfano wa dhamira hizo ni kama vile: dhamira ya maadili mema, uongozi mbaya, kuonya, umoja na mshikamano, kusifu, upendo, uaminifu, kazi, mlezi, kuagana na uzazi wa mpango. 
SURA YA TATU.
3.0     Mawanda ya utafiti.
Kutokana na muda kuwa mfupi pamoja na utafiti yenyewe kutakiwa kufanyika ndani ya kipindi cha masomo, hivyo basi mtafiti hakuweza kwenda Mkoa wa Lindi ambako ndiko inasadikiwa kuwa makazi halisi ya Wamatumbi. Kwa hiyo, kutokana na sababu hizo mtafiti aliamua kufanya utafiti huu katika mkoa wa Dar es Salaam wilaya ya Temeke maeneo ya Mbagala ambako idadi kubwa ya wamatumbi wanaishi maeneo hayo.
3.1     Mbinu za ukusanyaji wa Data.
Katika utafiti huu mtafiti alitumia mbinu mbalimbali ambazo zilimwezesha kukusanya data alizozihitaji katika utafiti wake. Mbinu hizo ni kama vile;
3.1.1     Hojaji (Interview).
Mtafiti alitumia mbinu hii ili kuweza kupata data mbalimbali zilizohusu nyimbo za kabila la Wamatumbi. Baadhi ya maswali mtafiti aliyouliza yalikuwa kama ifuatavyo;
(i)                 Je nyimbo za kabila la Wamatumbi zina dhima gani katika jamii ya Kimatumbi?
(ii)               Je nyimbo za kabila la Wamatumbi zina dhamira gani katika jamii hiyo?
(iii)             Je dhamira zinazopatikana katika nyimbo hizo zinauhalisia wowote na maisha ya jamii hiyo?
3.1.2     Mbinu ya kimaktaba.
Pia mtafiti alitumia mbinu ya kimaktaba katika kukusanya data kutoka katika vitabu na makala za nyimbo za makabila mbalimbali, kama vile nyimbo za harusi, sherehe na kazi.
3.2     Zana za Utafiti.
Mtafiti ametumia vifaa kama vile kalamu na karatasi katika kuandika data mbalimbali alizozipata katika utafiti wake. Mtafiti alikuwa akisikiliza kwa makini na kuandika katika karatasi nyimbo zilizokuwa zikiimbwa wakati wa majadiliano aliyokuwa akifanya.
3.3     Uteuzi wa sampuli.
Sampuli ya watafitiwa haikuchaguliwa kiholela bali ilizingatia vigezo vifuatavyo; umri na jinsia ili kupata wawakilishi wa jamii nzima ya wamatumbi. Vilevile uteuzi ulizingatia umahiri wa lugha ya kimatumbi. Ingawa sampuli ilizingatia umri, jinsia na umahiri wa lugha, lakini watu wenye umri mkubwa walipewa umuhimu mkubwa kutokana na uzoefu wao wa maisha na kuaminika kwao kuwa wanaujuzi mkubwa wa lugha husuka, pia kutokana na kuishi kwao kwa muda mrefu inasadikika kuwa wameshiriki katika matukio mbalimbali na hivyo kuweza kujua vizuri zaidi dhima na dhamira katika nyimbo hizo za kimatumbi.
Hivyo basi mtafiti alichagua sampuli hii ya watu 13 ambao ni Wamatumbi halisi wanaoishi katika mkoa wa Dar es Salaam wilaya ya Temeke maeneo ya Mbagala. Watafitiwa hawa walishiriki katika utafiti wa nyimbo za kabila la wamatumbi. Mchango wao wa sampuli hiyo ulikuwa kama ufuatao;
Katika mchanganuo huo watu wa rika na jinsi hizo waliooneshwa katika jedwali hilo hapo chini walitoa data karibu zinazolingana ingawa wanawake wameonekana kuwa mahiri zaidi katika nyimbo za kabila la wamatumbi kwa sababu wanawake ndiyo wahusika wakuu katika uimbaji wa nyimbo hizo.
 3.4     Jedwali la Sampuli ya Watafitiwa.
Umri
Ke
   Me
Jumla
20 – 30
3
1
4
31 – 40
2
-
2
41 – 50
1
2
3
51 – 60
2
-
2
61 – 70
1
-
1
71 – 80
-
1
1
Jumla
13
  
3.5     Changamoto za utafiti.
Pamoja na mafanikio makubwa aliyoyapata mtafiti katika ukusanyaji wa data, vilevile mtafiti alikumbana na changamoto mbalimbali katika utafiti wake. Baadhi ya changamoto hizi ni kama vile;
Ufinyu wa uelewa juu ya utafiti; watafitiwa wengi hawana uelewa wa kutosha juu ya dhana nzima ya utafiti, kwani wengi waliamini kuwa mtafiti atapata faida kubwa zaidi kuliko wao pindi atakapo kamilisha utafiti wake. 
Changamoto nyingine ilikuwa ni uhaba wa fedha; watafitiwa hasa vijana walidai angalau malipo kidogo kutokana na kwamba wamepoteza muda wao mwingi wakati wa mahojiano na mtafiti.
Pia ufinyu wa muda; suala la ufinyu wa muda lilikuwa ni tatizo kubwa lililomsumbua mtafiti kutokana na kwamba utafiti huu ulitakiwa ufanyike ndani ya muda wa masomo, hivyo basi mtafiti hakuweza kufikia malengo yake ikiwa ni pamoja na kwenda eneo asilia la wamatumbi, pamoja na kuchambua nyimbo zaidi ya 10.
Changamoto nyingine ilikuwa ni kwamba, watu waliohojiwa walikuwa na aibu katika kuimba nyimbo za kabila lao hususani vijana wenye umri kati ya miaka 20-30. Hii ilipelekea mtafiti kupoteza muda mwingi katika kuwashawishi ili waweze kuimba.
3.6     Nadharia ya utafiti.
Mtafiti baada ya kusoma makala na vitabu mbalimbali, alipata nadharia ya kuweza kumuongoza katika utafiti wake wa nyimbo za kabila la Wamatumbi. Nadharia alizozipata ni nadharia ya Umarx na nadharia ya Uamilifu ambazo amezitumia katika uchambuzi wa dhima na dhamira katika nyimbo za kabila la Wamatumbi.
3.6.1     Nadharia ya Uamilifu.
Kutokana na tamko la utafiti, mtafiti ametumia nadharia ya Uamilifu (Functionalism literary theory). kwa mujibu wa Wamitila (2006), waasisi wa nadharia hii ya Uamilifu ni pamoja na Bronislaw Malinowski, Radcliffe Brown na Franz Boaz. Nadharia hii inatazama zaidi dhima na dhamira ya kazi mbalimbali za jamii husika. Vilevile nadharia hii inadai kuwa kazi yoyote ya fasihi ni lazima iwe na lengo fulani au ilenge kuleta ujumbe fulani katika jamii. Hivyo waasisi wa nadharia hii walitazama kila kazi ya fasihi au kipengele cha fasihi kina maana gani katika jamii husika? Hivyo nadharia hii ilimsaidia mtafiti katika kuchunguza dhima na dhamira zilizopo katika nyimbo za kabila la wamatumbi.
3.6.2     Nadharia ya Umarx.
Sambamba na nadharia ya Uamilifu, nadharia ya Umarx imetumika katika kuangalia jinsi nyimbo zinavyoweza kuibua dhima na dhamira zinazoweza kuhalisika au kuonesha uhalisia katika jamii. Pia nadharia hii ya Umarx imesaidia kuonesha uhalisia wa dhamira na matabaka yaliyopo katika jamii hiyo kwa kupitia nyimbo mbalimbali.
Kwa mujibu wa Wamitila (2006) anasema, umarx ni falsafa ya kiyakinifu hasa kwa kuwa pana msisitizo mkubwa kwenye msingi wa hali za kiyakinifu za maisha kama mazingira ya kuishi kuliko mawazo katika maisha ya binadamu (ikimaanisha kwamba mawazo yake hayategemezi kwenye dhana dhahania kama urembo, ukweli au ndoto bali anayategemeza kwenye uhalisia unaoonekana.
Nadharia ya umarx ilianzishwa na Karl Marx mwaka 1818-1863 na Fredrich Engles (1820-1895). Katika nadharia hii Marx amejikita katika historia na miundo ya kijamii kwa kupitia hoja kuu zifuatazo.
Historia ya maisha ya binadamu inaweza kuelezeka katika misingi yakinifu ya kiuchumi ambayo itachunguza njia za uzalishaji mali pamoja na miundo ya kiuchumi na pia huathiri uzalishaji mali na usambazaji wa mali hizo. Hivi vyote kwa pamoja huunda misingi ambapo kwenye misingi hiyo huunda maadili, itikadi, dini na utamaduni.
Hoja nyingine ni kuamini kuwa historia ya binadamu inadhihirisha au kuakisi harakati zinazoendelea katika matabaka ya kiuchumi-jamii. Marx alisema “Historia ya maisha ya binadamu ni ya harakati za kitabaka”.
Harakati za kitabaka katika jamii. Nadharia ya ki-marx inaangalia matabaka katika ngazi mbalimbali kama vile ngazi ya familia, dini na elimu.
Ubepari kama njia ya uzalishaji mali na mara nyingi huharibiwa na tabaka la chini, hivyo ubepari hujitengenezea njia za kujiharibu wenyewe. Kutokana na unyonyaji na ukandamizaji unaoufanya kwa tabaka la chini.   
Njia ya kuondokana na ubepari huu jamii lazima ikemee.
Mshikamano uliopo baina ya tabaka tawaliwa. Kwa mujibu wa marx ili kuondokana na mfumo wa unyonyaji na ukandamizaji, jamii lazima iungane ili kubadilisha mfumo uliopo.
Matamanio ya kitabaka yanaiakisi jamii hiyo au itikadi ya jamii iliyopo. Kwa mujibu wa nadharia ya umarx tabaka la chini itikadi yao ni kupambana na tabaka la juu ili kuondokana na unyonyaji na ukandamizaji na tabaka la juu itikadi yao inaonekana kuwa ni halali kulikandamiza tabaka la chini.

SURA YA NNE.
4.0     Uchambuzi wa Data.
Mtafiti alichunguza na kuchambua data alizokusanya ili ziweze kutumika katika utafiti wake. Ili kupata usahihi katika data mbalimbali alizokusanya, mtafiti alilinganisha na kuzichuja data hizo.
Vilevile kutokana na data alizozikusanya mtafiti ameona kuwa, nyimbo za kabila la kimatumbi ni fupi sana. Mfano; wimbo wa ‘Mbola’. Wimbo huu una ubeti mmoja lakini hurudiwa rudiwa wakati wa kuimba na kufanya wimbo huu uonekane mrefu.
Aidha mtafiti ameona kwamba nyimbo za kimatumbi zimegawanyika katika kategoria mbili kama inavyojidhihirisha katika jedwali lifuatalo;
Kategoria A
Kategoria B
Nyimbo za kuelimisha katika ngoma ya
Nyimbo za kuburudisha katika ngoma ya
1
Mbola
1
Njege
2
Tikisa/Legeza


3
Ndonde


4
Kongo


5
Chunje


6
Jando 


7
Unyago



Hivyo basi, ili kuweza kujua dhima na dhamira za nyimbo za kabila la Wamatumbi sura hii itajikita zaidi katika kuchambua dhana hizi mbili kwa kutumia nadharia hizo mbili yaani nadharia ya uamilifu na nadharia ya umarx. 
4.1     Matokeo ya utafiti/uchambuzi.
Kutokana na mada ya utafiti na asili ya data zilizokusanywa na mtafiti, uchambuzi wa data umegawanyika katika sehemu mbili, sehemu ya kwanza inashughulikia dhima za nyimbo za kabila la wamatumbi kwa ujumla, sehemu ya pili ni dhamira zinazojitokeza katika nyimbo hizo kwa ujumla. Kwa kuanza na kipengele cha dhima, mtafiti amebaini dhima ya kuelimisha na kuburudisha katika nyimbo hizi za kabila la wamatumbi kama ifuatavyo;
4.1.1     Dhima ya kuelimisha.
Nyimbo za kabila la wamatumbi zina dhima ya kuelimisha jamii kuhusu mambo mbalimbali kwa mfano; Katika kategoria A. Na.1 ni ngoma ya Mbola, wimbo unaoimbwa hulenga kutoa mafunzo kwa jamii hususani katika ndoa, heshima ya mke kwa mumewe.
Wimbo: Mwachengo bango niboi mwanja kwipata nikakinde mbola inanoga, uyende bai wabuye. (hurudiwa rudiwa)
Tafsiri: Mume wangu nakuaga naenda kibata nikacheze mbola ni nzuri sana,               nenda tu lakini urudi.
Wimbo huu huimbwa kwa kupokezana kati wanawake na wanaume. Wanawake huimba mstari wa kwanza kisha wanaume huitikia mstari wa pili.
Katika wimbo huu heshima inasisitizwa sana katika maisha ya ndoa, katika kabila hili mke kumuaga mume ni jambo la kuonesha heshima, kama inavyojidhihirisha katika wimbo huo. mke akiomba ruhusa kwa mwenzi wake naye anamruhusu bila kisita. Wimbo huu una ujumbe mzito sana kwa wanandoa na vilevile una lengo la kufundisha wanandoa uhuhimu wa heshima katika maisha ya ndoa. Kutokana na ujumbe na malengo ya wimbo huu ni wazi kwamba wimbo huu unakubaliana moja kwa moja na nadharia ya uamilifu inayodai kwamba kazi yoyote ya fasihi ni lazima iwe na lengo fulani au ilenge kuleta ujumbe fulani katika jamii. Mafunzo yanayotolewa katika wimbo huu yanaweza kuhalisika katika jamii yoyote ile hapa Tanzania. Hivyo basi wimbo huu unaonesha ukubalifu na nadharia ya umarx inayoangalia zaidi uhalisia/uamilifu wa kazi ya fasihi na jamii.  
Katika kategoria A. Na. 2 ni ngoma ya Tikisa/Legeza wimbo unaoimbwa una dhima ya kuwafundisha wanajamii suala la uangalifu/umakini katika maisha. Ngoma hii ya legeza huchezwa kwa kutikisa mwili taratibu sana bila kutumia nguvu, na kwa kawaida huchezwa na wazee tu wakiwa katika duara.
Wimbo:   Mwachengo bango’nchele wene Kingo’mbe ee, ela yene nga bampeile Chiku ee Chiku ee (3) ela bampokonywile, mbele yee mbele yee bankanile.
Tafsiri:   Mume wangu mchele wenyewe upo Kingumbi (jina la kijiji) pesa zenyewe wamempa Chiku ee, Chiku ee (3) pesa zenyewe wame mnyang’anya.
Hadithi ya wimbo huu: Mume alimuaga mke wake kwamba anaenda Kingumbi (jina la kijiji) kuuza mchele. Alipofika huko alimpenda msichana anayeitwa Chiku akampa mchele na pesa. Chiku akamlaghai mume huyu. Mwanaume huyu akaenda kwa mama yake Chiku kwa lengo la kumshitaki Chiku, mama na mume huyu wakamwendea Chiku kumdai au aende kuishi na huyo mume au arudishe pesa na mchele. Chiku alikataa na ndipo akanyang’anywa mchele na hela.
Wamatumbi wanapoimba wimbo huu wana lengo la kuwafundisha wanajamii kwamba, kila mtu anapaswa kuwa muangalifu katika maisha, kuepuka kuvamia mtu usiyemfahamu na kuanza kukubaliana naye masuala ya uchumba.
Kwa kupitia wimbo huu wa kimatumbi, jamii nzima na Taifa kwa ujumla wanajifunza madhara ya kuparamia mwanamke au mwanaume usiyemfahamu. Madhara yaliyotajwa katika wimbo huo ni kielelezo tu cha madhara ambayo mtu anaweza kuyapata katika kipindi hiki. Mfano maradhi kama vile ukimwi na magonjwa ya zinaa. Kutokana na dhima/umuhimu au lengo la wimbo huu ni wazi kwamba wimbo huu unakubaliana moja kwa moja na nadharia ya uamilifu inayodai kwamba kazi ya fasihi ni lazima ioneshe dhima na lengo lake kwa jamii husika. Vilevile wimbo huu unakubaliana na nadharia ya umarx inayoangalia uamilifu au uhalisia wa kazi ya fasihi na jamii. Ni wazi kwamba wimbo huu unaweza kuhalisika katika jamii yoyote ya kitanzania.
Katika kategoria A. Na. 3 ni ngoma ya Nonde wimbo unaoimbwa una dhima ya kuhimiza uwajibikaji katika maisha. Katika kabila la wamatumbi mtu asiye wajibika na kushindwa hata kujinga nyumba yake mwenye au hata kakibanda tu kwa ajili ya kujisitiri hudharauka sana.
Wimbo:   Nankonko mwanja kaya, nikagonje? Salima wango’eee- (hurudiwa rudiwa)
Tafsiri:   Ndege mbayuwayu naenda nyumbani nikalale wapi? Salima wangu (mpenzi wangu) - (hurudiwa rudiwa)
Wimbo huu ni baadhi ya nyimbo ambazo huimbwa jioni baada ya kutoka shambani wanapoalikana majirani kulima kwa ushirika. Kawaida mume na mke huenda pamoja. Baada ya kula chakula na kunywa pombe wakiwa wamekaa wawili wawili, yaani mke na mume, wimbo huu huimbwa kwa lengo la kuwasema, kuwahimiza au kuwaonya wale wasio na busara ya kujenga nyumba imara na zao wenyewe, wana kuwa kama ndege huyu aitwaye mbayuwayu asiye na uhakika wa maisha.
Wimbo huu unatoa mafundisho mazuri si kwa wamatumbi tu, bali kwa Taifa zima. Kwani, suala la uwajibikaji katika maisha ni suala la kila mwanajamii, maana katika kuwajibika ndipo tunaweza kuleta mapinduzi binafsi ya kiuchumi na jamii au Taifa kwa ujumla. Hivyo kutokana na nadharia ya umarx na uamilifu uwajibikaji ni suala ambalo ni muhimu na linahalisika katika jamii yoyote ile inayotaka kuwa na maendeleo.
Pia katika kategoria A. Na. 4 ni ngoma ya Kongo wimbo unaoimbwa hapa ni wimbo wa unaofundisha wanajamii masuala ya imani za jadi. Jamii ya wamatumbi inaamini kwamba kuna aina ya viumbe ambao huashiria tokio fulani baya au zuri. Mfano katika wimbo huu;
Wimbo:    Nditi, nditi nditi likumwi kubwamba, lichola mwiko (3) Litungutu litungutu litungutu likumwi pa nchengo, lichola mwiko (3)
Tafsiri:    Ndegengoma ndegengoma ndegengoma amelia alfajiri, anaashiria balaa. Bundi bundi bundi amelia nyumbani, anaashiria balaa.
Katika jamii ya wamatumbi kawaida ndegengoma halii wakati wa asubuhi sana, hivyo huaminiwa kwamba, endapo ukimsikia analia alfajiri, basi ujue kwamba anaashiria balaa au  mkosi. Sambamba na hilo pia inasadikiwa kuwa, ndege huyu anapotua juu ya nyumba au karibu  na nyumba fulani huaminiwa kuwa analeta balaa hasa kifo.
Hii ni moja kati ya tamaduni za makabila mengi ya kiafrika. Jambo la msingi katika wimbo huu wa kabila la wamatumbi ni kutaka kuifahamisha jamii kwamba kuna baadhi ya viumbe ambao wamejaliwa uwezo wa kutabiri au kutambua mambo yajayo ambayo huenda yakawa mazuri ua mabaya.  Kulingana na nadharia ya uamilifu na umarx suala hili lipo katika jamii na linahalisika na vilevile lina umuhimu mkubwa sana katika jamii ya wamatumbi.
Vilevile katika kategoria A. Na. 5 ni ngoma ya Chunje (maonyo, hisia, mafundisho) wimbo unaoimbwa hapa ni kwa lengo la kutoa mafudisho au kuamsha hisia za wanajamii juu ya uonevu unaofanywa na watawala katika kukusanya kodi. Watawala hawa hawaangalii hali halisi ya maisha ya mtu binafsi, kwani katika jamii hali za maisha hutofautiana. Hivyo kupitia wimbo huu jamii inahimizwa kuungana na kupinga kwa pamoja uonevu huo.
Wimbo:   Aiche njungu Kwitabe linalyage apendo bendakuntila, bayogopa ukale. Ntawala, natawala kwodi upongoye, komi na mwano twabauni tuiko’mbwa  sakali.
Kibwagizo:    Ntawala, kwodi upongoye, komi na mwano twabauni tuiko’mbwa sakali.
Tafsiri:     Amekuja Tawa, jina lake mzungu, wazee wanamkimbia, wanaogopa ukali.                   Mtawala, mtawala, upunguze kodi, kumi na tano sisi mabachela hatuwezi   kulipa.
Kibwagizo:   Mtwala upunguze kodi, kumi na tano sisi mabachela hatuwezi kulipa.
Wimbo huu huchezwa na watu wote ili kuonesha mshikamano na umoja katika kupinga uonevu wa tabaka tawala juu ya tabaka tawaliwa. Katika wimbo huo tunaelezwa kwamba wapo wanaume ambao hawaja funga ndoa na wengine hawajaanza kujitegemea hivyo si rahisi kuweza kulipa kodi kubwa kiasi hicho.
Hali kama hii ipo katika jamii nyingi za kiafrika hususani Tanzania. Hivyo basi katika wimbo huu wa kimatumbi unaonesha uhalisia uliopo katika Tanzania ya leo, kwani vijana wengi hata watu wazima hawana uwezo wa kulipa kodi au kuchangia huduma mbalimbali za kijamii.
Hivyo basi kulingana na nadharia ya umarx inayodai kwamba kazi ya fasihi ni lazima ioneshe matabaka ya kiuchumi, kijamii na kisiasa. Pia nadharia hii inasisitiza kwamba ili kuleta usawa katika jamii lazima tabaka tawaliwa liungane pamoja na kupinga uonevu wowote unaofanywa na tabaka tawala. Hivyo wimbo huu umelidhihirisha hilo.
Vilevile nadharia ya uamilifu inajitokeza katika wimbo huu kwani wimbo unapoimbwa huwa na lengo mahususi ambalo ni kupinga uonevu wowote katika jamii.
Nyimbo za jando na unyago.
Mulokozi (1996:67) amezipa jina la nyiso nyimbo hizi zinazoimbwa wakati wa jando na unyago. Anasema kuwa nyimbo hizi huimbwa na makabila yenye mila ya kupeleka watoto jandoni au unyagoni. Nyimbo za kumbini kwa kawaida hukusudiwa kuwaasa wari kuhusu majukumu yao mapya ya utu uzima pindi watakapohitimu jando/unyago.
Mulokozi (1996:67) wakiwanukuu Sunkuli na Miruka (1990:16-17) anaelezea vizuri dhima ya nyiso kwamba ni:
(1)   Kuwa jumumuisha na kuwatia moyo wari.
(2)   Kudhihaki woga.
(3)   Kufurahisha na kujivunia hatua ya kutoka katika utoto kiingia katika utu uzima.
(4)   Kusisitiza dhima mpya ya kiutu-uzima inayowakabili wari.
(5)   Kuwaandaa wari kihisia kuyakabili maumivu ya kimwili (k.m. tohara) watakayopata.
(6)   Kuuaga utoto.
Ngure (2003:89) yeye ameziita nyimbo hizi za jando na unyago kuwa ni nyimbo za tohara. Anasema kwamba kutahiriwa ni jambo la fahari katika jamii zinazozingatia mila hii. Inachukuliwa kuwa mapito kutoka kwa ujana hadi uzima. Anaendelea kusema, kila jamii ina mila yake ya kuwavusha vijana (wa kike na wa kiume) kutoka kwa ujana hadi kwa utu uzima.
Hivyo basi hata katika jamii ya wamatumbi mila hii ipo na inajidhihirisha wazi kupitia nyimbo za jandoni na unyagoni. Kwa wamatumbi hiki ni kipindi maalumu na ni muhimu sana katika kuwafunza vijana mambo mahimu ya maisha na tamaduni za jamii ya wamatumbi.
Wamatumbi huwa na nyimbo zinazoambatana na mafunzo haya ya jando na unyago. Wao pia huziita nyimbo za jando na unyago. Nyimbo hizi ambazo ni fupi fupi sana huimbwa kwa kurudiwa rudiwa ili kurefusha na kuweka msisitizo katika mambo wanayoambiwa.
Kategoria A. Na. 6 ni Wimbo wa Jandoni ambao ni mahususi kwa ajili ya vijana wa kiume wanaoingia hatua ya utu uzima.
Wimbo:     Utami kubende kummagulamia bembelenye (4)
Tafsiri:     Amekaa vibaya (uchi) sogea mbali (4)
Hapa vijana waliopo jandoni wanaonywa kuwa, ukiona mwanamke amekaa uchi ondoka hapo, ni heshima. Pia chukua tahadhari kwani wanawake wenye tabia mbaya hukaa uchi mbele ya wanaume ili kuwashawishi kimapenzi. Kulingana na nadharia ya umarx tunaona kwamba suala hili si la kindoto kwani linaweza kuhalisika katika jamii yoyote. Vilevile hata katika nadharia ya uamilifu tunaona kwamba wimbo huu unalenga kutoa mafundisho kwa vijana wanaoelekea kuingia utu uzima. 
Kategoria A. Na. 7 ni Wimbo wa unyagoni. Wimbo huu ni maalum kwa ajili ya mabinti au wasichana wanaofundwa ili kuweza kukabiliana na maisha ya utu uzima.
Wimbo:    Ntote ang’ula kwako? Ang’ula kwiye kwoo, kumilai (4).
Tafsiri:     Fisi analia yuko wapi? Analia ng’ambo ile huko mianzini (4).
Katika wimbo huu lugha iliyotumika si lugha ya kawaida, ni lugha ya mafumbo. Katika wimbo huu msichana anapewa taarifa kwamba mchumba wake amekuja, hivyo wanapaswa kwenda kuongea naye mbali au sehemu ya faragha, kwa maana si vizuri wakiongea hadharani.
Wimbo huu unalenga kufundisha vijana na jamii nzima kwa ujumla, umuhimu wa kufuata maadili mema.
Hivyo basi kutona na lengo la wimbo huu kwa vijana tunaona kwamba nadharia ya uamilifu inajitokeza katika kipengele hiki.
Tukiangalia uhalisia wa wimbo huu na tukihusianisha na nadharia ya umarx inayoangalia uahalisia wa jambo katika jamii tunaona kwamba, katika maisha ya sasa kwa kiasi fulani jamii haizingatii maadili mema kama hapo awali. Hivyo wimbo huu unafaa sana katika maisha ya sasa kutokana na mafundisho yake mazuri. Hivyo basi kupitia wimbo huu wa kabila hili la wamatumbi jamii inaaswa kudumisha na kuendeleza maadili yaliyo mema.      
4.1.2     Dhima ya kuburudisha.
Kategoria B. Na. 1 ni wimbo wa kuburudisha jamii baada ya uchovu wa kazi za mchana kutwa.
Wamatumbi wana nyimbo za maburudisho ambazo huimbwa wakati wa jioni baada ya kumaliza kazi wakiwa katika mapumziko. Hivyo nyimbo hizi husaidi kuchangamsha akili na kujenga umoja miongoni mwa wanajamii. Pia nyimbo hizi huleta burudani katika sherehe mbalimbali za kijamii. 
Wimbo:    Njegea njengea akalamwike, achanga pipi na lose kanywa mache (4) Chako chako akabanango, kono ndumbo kono mwana ntapotwaje (4)
Tafsiri:      Ndege ndege ni mjanja, anajenga kiota karibu na kisima ili anywe maji (4) kiko wapi mkamwanangu (unapata faida gani). Huku mimba huku mtoto utalea vipi/utabebaje watoto.
Pamoja na kwamba wimbo huu ni miongoni mwa nyimbo za maburudisho vilevile unatoa mafundisho kwa wanajamii. Kwa mfano, katika wimbo huu kuna habari ya mkamwana ambaye tayari ana mtoto mdogo wa kulea na bado tena ana mimba! Hivyo wimbo huu unaimbwa na mama anayemwimbia mkamwanae asiyezingatia uzazi wa mpango. Mkamwana ana fananishwa na ndege asiye na busarasa.
4.2    Uchambuzi wa dhamira:
Dhamira ni kipengele cha pili kilichoshughulikiwa katika utafiti huu. dhamira zilizopatikana katika nyimbo za kabila la wamatumbi ni kama vile: dhamira ya maadili mema, uongozi mbaya, kuonya, umoja na mshikamano,  upendo, uaminifu, kazi, mlezi, kuagana na uzazi wa mpango. 
4.2.1   Dhamira ya maadili mema:
Dhamira hii hujitokeza katika nyimbo za jando na unyago zilizopo kategoria A. Na. 6 na 7. Katika nyimbo hizi za jando na unyago wazazi wanaonesha wajibu wao katika kuwaelekeza na kuwafundisha vijana maadili mema, kama inavyooneshwa katika wimbo huu wazazi wakimwambia kijana kuwa anapotaka kukutana/kuongea na mpenzi wake anapaswa kwenda mbali, na maeneo ya watu. Hivyo basi, kwa kupitia tukio hili nyimbo zinazoimbwa zinalenga kutunza na kuendeleza maadili mema katika jamii yoyote ile. Kwa mtazamo wa nadharia ya uamilifu na umarx suala la maadili mema ni suala ambalo ni muhimu katika jamii na pia ni suala ambalo linahalisika katika jamii yoyote.
4.2.2   Dhamira ya uongozi mbaya.
Dhamira hii ya uongozi bora hujitokeza katika ngoma ya chunje kategoria A. Na. 5. Wimbo unaoimbwa hapa unalengo la kukosoa uongozi mbaya ambao unaonekana kuwanyonya na kuwa kandamiza wananchi wake kwa kuwadai kodi kubwa kupita uwezo wa kipato chao. Wamatumbi wanapoimba wimbo huu huonesha umoja na mshikamano wao katika kudai haki za tabaka la chini dhidi ya tabaka tawala kama inavyodai nadharia ya umarx kuwa umoja na usawa katika jamii yoyote utaletwa na ushirikiano wa tabaka tawaliwa katika kudai haki zao.
Hivyo basi wimbo huu unakubaliana moja kwa moja na nadharia ya umarx inayohusianisha dhamira na uhalisia wake katika maisha ya jamii husika. Vilevile wimbo huu unakubaliana na nadharia ya uamilifu inayosisitiza kwamba kazi ya fasihi inapofanyika huwa na makusudi au malengo mahususi kwa jamii husika.
4.2.3   Dhamira ya kuonya:
Dhamira ya kutoa maonyo hujitokeza katika ngoma ya ndonde kategoria A. Na. 3. Katika ngoma hii wimbo unaoimbwa hapa unalengo la kuwaonya wale wote wasiopenda kujishughulisha katika shughuli mbalimbali kwa ajili ya kujipatia kipato na kuweza kujenga makazi yao wenyewe. Hivyo wanafananishwa na ndege aina ya mbayuwayu asiye na makao maalum.
Dhamira hii inaweza kuhalisika katika jamii yoyote ile kutokana na kwamba, maendeleo yoyote katika jamii hupatikana kwa njia ya uwajibikaji kama inavyodai nadharia ya umarx kuwa, maendeleo huendana na ushirikiano na uwajibikaji wa watu wote katika jamii.
Wimbo huu unatoa ujumbe kwa jamii kuwa, mafanikio katika maisha hupatikana kwa njia ya uwajibikaji. Kwa kigezo cha ujumbe uliobebwa na wimbo huu, ni wazi kwamba, wimbo huu unakubaliana na nadharia ya Uamilifu inayodai kwamba, kazi yoyote ya fasihi ni lazima iwe na lengo fulani kwa jamii husika.
4.2.4   Dhamira ya umoja na mshikamano.
Vilevile dhamira hii hujitokeza katika ngoma ya chunje kategoria A. Na. 5. Wimbo unaoimbwa katika ngoma hii unaonesha umoja na mshikamano wa tabaka la chini katika kupinga unyonyaji na ukandamizaji unaofanywa na tabaka tawala. Pia hata katika nadharia ya Umarx moja ya mawazo makuu ni kwamba, mapinduzi ya kweli katika jamii yataletwa na tabaka tawaliwa kwa njia ya umoja na mshikamano.
4.2.5   Dhamira ya uaminifu:
Dhamira hii hujitoke katika ngoma ya tikisa kategoria A. Na. 2. Wimbo unaoimbwa katika ngoma hii unalenga kuwafundisha wanajamii kuwa waaminifu katika maisha. Mfano katika maisha ya ndoa. Wanandoa wanafundishwa madhara yanayoweza kumpata mtu aliye na tamaa ya wanawake au wanaume (asiye ridhika katika ndoa yake). Wimbo huu una muonesha Chiku jinsi alivyoweza kumrubuni mme wa mtu mpaka akampa fedha na mchele. Dhamira hii ina uhalisia mkubwa sana katika maisha leo.
Nadharia ya umarx inaangalia katika mambo yakinifu na wala si ya kufikirika au ya kindoto, hivyo basi suala la uaminifu si jambo la kindoto au la kufikirika ni jambo ambalo lipo katika jamii na linaweza kuhalisika kama ilivyo dhihirika katika wimbo huu wa tikisa.
4.2.6   Dhamira ya heshima.
Katika ngoma ya mbola kategoria A. Na. 1. Wimbo unaoimbwa hapa unalengo la kuwa fundisha hususani wanandoa suala zima la heshima. Wimbo huu unamuonesha mwanamke akiomba ruhusa kwa mume wake kuwa anakwenda kucheza ngoma ya mbola. Heshima katika maisha ya ndoa ni jambo la msingi sana, kwani pasipo kuheshimiana ndoa huweza kuingia katika mgogoro mkubwa na hatimae kuvunjika. Dhamira hii pia inauamilifu kubwa sana katika maisha ya sasa.
Vilevile wimbo huu unapoimbwa huwa na lengo la kusisitiza heshima baina ya wanandoa. Kwa mantiki hiyo wimbo huu unakubaliana na nadharia ya uamilifu inayodai kuwa, kazi ya fasihi haifanyiki kiholelela bali hufanyika kwa malengo maalum.
4.2.7   Dhamira ya uzazi wa mpango:
Dhamira hii inajitokeza katika wimbo wa maburudisho kategoria A. Na. 7. Wimbo huu huimbwa na mama wakati wa mapumziko, akimwimbia mkamwana wake kuwa anapaswa kuwa na mpango katika kuzaa watoto, kwani italeta urahisi katika kulea, vinginevyo itakuwa vigumu kulea mtoto huku ukiwa na mimba nyingine. Fundisho hili tunaweza kulipata hata katika jamii ya sasa, kwani uzazi wa mpango ni moja ya kanuni za afya na maendeleo katika jamii nzima na si kwa wamatumbi tu.
Kulingana na mawazo ya Kimarx pamoja na nadharia ya Uamilifu wimbo huu umebeba ujumbe ambao unahalisika katika jamii yoyote ile na wala si ujumbe wa kufikirika. Hivyo basi, dhamira hii ipo katika maisha halisi ya wanajamii wowote.
SURA YA TANO

5.0     Hitimisho.
Utafiti huu ulihusu dhima na dhamira katika nyimbo za kabila la wamatumbi. kutokana na uchambuzi wa data, utafiti umetoa matokeo yanayoonesha kwamba nyimbo za kabila la wamatumbi zina dhamira mbalimbali kama vile: dhamira ya maadili mema, dhamira ya uongozi mbaya, dhamira kuonya, dhamira ya umoja na mshikamano, dhamira ya uaminifu, dhamira ya heshima na dhamira ya uzazi wa mpango.
Pia nyimbo hizi zimeonekana kuwa na dhima ya kuelimisha jamii ya wamatumbi kwa kutoa mafunzo mbalimbali kama vile kufunza umuhimu wa kazi, kuonya kuhusu wizi na kuhimiza upendo, vile vile nyimbo hizi zina dhima ya kuburudisha kwa lengo la kupumzisha akili baada ya kazi nzito.
5.1     Mapendekezo.
Kutokana na utafiti huu wa nyimbo za kabila la wamatumbi imeonekana kuwa nyimbo hizi zina umuhimi mkubwa sana katika jamii ya wamatumbi na hata katika jamii mbalimbali kwani dhima na dhamira zake zina halisika katika jamii nyingi hapa Tanzania, hivyo mtafiti amependekeza yafuatayo;
Ili kudumisha nyimbo za asili jamii hainabudi kuipa kipaombele sanaa hii ya nyimbo na pia kuthamini mila na desturi za makabila mbalimbali kwani ndiyo chimbuko la nyimbo nyingi zinazoimbwa katika jamii ya watanzania.
Pia serikali kupitia wizara yake ya Elimu na utamaduni iweke mkazo katika kuendeleza utamaduni wa asili wa mtanzania; mfano, nyimbo za makabila mbalimbali. Hii inaweza kupunguza kasi ya vijana kupenda nyimbo za nje kama vile R&B, Ragge na Hip hop pamoja na kuiga tamaduni ngeni na hivyo kudumaza utamaduni wa mtanzania kama inavyojidhihirisha hivi leo.
Vilevile ieleweke kwamba, si jukumu la serikali peke yake katika kuendeleza na kudumisha utamaduni wa mtanzania, bali ni jukumu la watu wote, taasisi binafsi, pamoja na wadau mbalimbali wanaothamini utamaduni wa Mwafrika. Hivyo basi, katika kuendeleza na kudumisha nyimbo za makabila mbalimbali, ingefaa sana taasisi binafsi, pamoja na wadua mbalimbali kuandaa matamasha mbalimbali yatakayo jumuisha nyimbo za makabila mbalimbali na hivyo kufanya tamaduni za makabila mbalimbali kufahamika kwa urahisi ndani na nje ya nchi.
5.2     Marejeo.
Balisidya, M.L. (1987). “Tanzu na Fani za Simulizi”. Katika Mulika Na. 9. TUKI. Chuo Kikuu                           cha Dar es Salaam.

Chesaina, C. (1977). Oral Literature of Embu and Mbeere. East African Educational Publishers. Nairobi.

Finnegan, R. (1971). Oral Literature in Africa. Oxford University Press. London.

Finnegan, R. (1977). Oral Poetry Cambrige University Press. Nairobi.

Gibbe, A.G. (1980). Shaabani Robert Mshairi. Tanzania Publishing House. Dar es Salaam.

Guma, S. (1967). The form, content and technique of traditional Literature in Southern Sotho.                  J.L Van Schaik Limited. Pretoria. 

Kavugha, F.S. (1977). Desturi na Mila za Wapare. Vuga Press. Soni. 

Mazigwa, S.A. (1991). Fasihi ya Kiswahili. Benedictine Publishing Company. Ndanda                          Peramiho.

Mbonde, J.P. (1999). Uhakiki na Uchambuzi wa Riwaya na Ushahiri. Mkuki na Nyota Publishers. Dar es Salaam. 

Mlama, P. (1973). Music in Traditional Theatre. The Kaguru as a case study. M.A Thesis. University of Dar es Salaam.

Msokile, M. (1991). Uchambuzi na Uhakiki. “Karibu Ndani”.  DUP. Dar es Salaam.

Mulokozi, M.M. (1996). Fasihi ya Kiswahili. TUKI. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Mwakasaka, C.S. (1977). “The oral Literature of Banyakyusa”. (M.A. Dissertation). University                               of Dar es Salaam. 

Nketia, J.H. (1963). Drumming in Akan Communities. Thomas Nelson & Sons Ltd. London.

Nkwera, F. (Hakuna mwaka). Tamrini za Fasihi Simulizi. Ndanda Peramiho. 

Omari, C.K. na Mvuge, M. (1980). Urithi wa Utamaduni wetu. T.P.H. Dar es Salaam. 

Sengo, T.Y.S. (1978). Kudidimizwa kwa Fasihi na Wakoloni, Taamuli ya Fasihi Nadharia, Mtazamo na Mbinu za utafiti katika Fasihi Simulizi. TUKI. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. 

TUKI. (1981). Kamusi ya Kiswahili Sanifu.TUKI. Dar es Salaam. 

Wamitila, K.W. (2006). Uhakiki wa Fasihi: Misingi na Vipengele vyake. Phoenix Publishers Ltd. Mombasa.


5.3    Viambatanisho.
Kategoria A. nyimbo za kuelimisha.
Wimbo:     Mwachengo bango niboi mwanja kwipata nikakinde mbola inanoga, uyende bai wabuye. (hurudiwa rudiwa)
Tafsiri:     Mume wangu nakuaga naenda kibata ni nikacheze mbola ni nzuri sana,                             nenda tu lakini urudi.
Wimbo:     Mwachengo bango’nchele wene Kingo’mbe ee, ela yene nga bampeile Chiku ee Chiku ee (3) ela bampokonywile, mbele yee mbele yee bankanile.
Tafsiri:      Mume wangu mchele wenyewe upo Kingumbi (jina la kijiji) pesa zenyewe wamempa Chiku ee, Chiku ee (3) pesa zenyewe wamemnyang’anya.
Wimbo:     Nankonko mwanja kaya, nikagonje? Salima wango’eee- (hurudiwa rudiwa)
Tafsiri:      Ndege mbayuwayu naenda nyumbani nikalale wapi? Salima wangu (mpenzi wangu) - (hurudiwa rudiwa)
Wimbo:     Nditi, nditi nditi likumwi kubwamba, lichola mwiko (3) Litungutu litungutu litungutu likumwi pa nchengo, lichola mwiko (3)
Tafsiri:      Ndegengoma ndegengoma ndegengoma amelia alfajiri, anaashiria balaa. Bundi bundi bundi amelia nyumbani, anaashiria balaa.
Wimbo:     Aiche njungu Kwitabe linalyage apendo bendakuntila, bayogopa ukale. Ntawala, natawala kwodi upongoye, komi na mwano twabauni tuiko’mbwa sakali.
Kibwagizo: Ntawala, kwodi upongoye, komi na mwano twabauni tuiko’mbwa sakali.
Tafsiri:     Amekuja Tawa, jina lake mzungu, wazee wanamkimbia, wanaogopa ukali. Mtawala, mtawala, upunguze kodi, kumi na tano sisi mabachela hatuwezi kulipa.
Kibwagizo: Mtwala upunguze kodi, kumi na tano sisi mabachela hatuwezi kulipa.
Wimbo:     Utami kubende kummagulamia bembelenye (4)
Tafsiri:      Amekaa vibaya (uchi) sogea mbali (4)
Wimbo:     Ntote ang’ula kwako? Ang’ula kwiye kwoo, kumilai (4).
Tafsiri:      Fisi analia yuko wapi? Analia ng’ambo ile huko mianzini (4).
Kategoria B. wimbo wa kuburudisha.
Wimbo:   Njegea njengea akalamwike, achanga pipi na lose kanywa mache (4) Chako chako akabanango, kono ndumbo kono mwana ntapotwaje (4)
Fafsiri:    Ndege ndege ni mjanja, anajenga kiota karibu na kisima ili anywe maji (4) kiko wapi mkamwanangu (unapata faida gani). Huku mimba huku mtoto utalea vipi/utabebaje watoto.


18 comments:

  1. hongera bingwa..je ....naomba kusaidiwa kuadika ripoti kuhusu jinsi lugha ilivyoadhiri jinsia



    ReplyDelete
  2. hongera bingwa..je ....naomba kusaidiwa kuadika ripoti kuhusu jinsi lugha ilivyoadhiri jinsia



    ReplyDelete
  3. Hongera bwana ERICK NDUMBARO kwa mchango mzuri katika uandishi wa kazi za kifasihi, naonba nisaidiwe jinsi ya kuchambua dhamira katika utendi wa Nyakiiru kibi

    ReplyDelete
  4. HONGERA SANA KAKA.
    Kazi yako ni nzuri,fupi na inayovutia.

    Kwanza kabisa nimependa mada uliyochagua kufanyia utafiti.
    (NYIMBO ZA ASILI)

    Umetusaidia kufahamu dhima&maudhui ya nyimbo za wazee wetu.

    Pili, binafsi umeniburudisha sana kwa maneno ya nyimbo, hasa ulipozitafsiri na kutusaidia tusiokuwa waMatumbi kuelewa.

    MWISHO; Nikutakie tafiti njema, uwe unatuonjesha kupitia kurasa kama hizi mtandaoni.
    Asante sana gwiji.

    ReplyDelete
  5. Ongera kwa kazi hii nzuri. Naomba nizaidiwe vyanzo vya mada za utafiti katika taaluma ya kiswahili

    ReplyDelete
  6. Gitonga nthigirani: Kongole kwa kazi faidishi ,,tushirikianeni kukuza taaluma ya Swahili afrika

    ReplyDelete
  7. kaka jemba sana.....kazi nzuri kwa kweli....

    ReplyDelete
  8. mwanataaluma kazi nzuri nimeipenda imetoa mwanga mpana.

    ReplyDelete
  9. Safi sana ndugu kwa kazi yako nzuri

    ReplyDelete