Wednesday, 13 November 2013

TAMTHILIA


UANDISHI WA TAMTHILIA
Tamthilia ni nini?
 • Tamthilia ni utanzu ambao hutegemea mazungumzo na uigizaji ili kuwasilisha ujumbe wake. Huu ni utanzu ambao huandikwa kwa mtindo wa mazungumzo ya wahusika (Wamitila, 2007).
 • Nkwera (h.t) anaelezea kuwa tamthilia ni: Tamthilia ni mchezo wa kuigiza au utungo wa kisanaa ambao huweka wazo fulani katika matendo na mazungumzo (Nkwera, h.t)
AINA ZA TAMTHILIA
 • Kwa mujibu wa Aristotle, kuna aina mbili za tamthilia. Aina ya kwanza ni tanzia na nyingine ni ramsa.
 • Tanzia ni nini?
Tanzia ni kinyume cha ramsa kwa maana kuwa hutumika kuonesha kuanguka na kushindwa kwa mhusika maarufu, mbabe, au shujaa atokaye katika tabaka la juu yaani mtu wa nasaba bora (Mutembei, 2005 katika mihadhara ya SW 234).
Kama ilivyo kwa ramsa, tanzia ilianzia katika miviga ya kidini, katika sherehe ya kumhusu Dionisius. Wachezaji na Waigizaji walivalia na kuonekana kama mbuzi wakiimba nyimbo zilizohusu anguko la shujaa (Mutembei, 2005 katika mihadhara ya SW 234).
ARISTOTLE TANZIA ANAONA KUWA; Tanzia ni usanii uoneshao anguko la mtu ambaye kimsingi ni mwema, shujaa au mbabe kutokana na kosa la kufisha au kutokana na uamuzi mbaya ambao matokeo yake ni mateso (Mutembei, 2005 katika mihadhara ya SW 234).
Jambo hili linapompata shujaa huyo, jamii nzima huingia katika woga na kuhangaika kwa hali ya juu, kwani kiongozi wao yumo katika mateso na ni uchuro wa kufisha jamii kama hatua madhubuti hazitachukuliwa (Mutembei, 2005 katika mihadhara ya SW 234)
MISINGI YA UTOKEAJI WA TANZIA:
Kwa mujibu wa Mutembei, (kashatajwa) katika mihadhara ya SW 234 anasema kuwa, misingi ya utokeajiwa tanzia inapaswa izingatie yafuatayo:
 • Iwe na uwezo wa kuamsha hisia za woga na huruma miongoni mwa hadhira.
 • Shujaa au mbabe apataye mkasa ni lazima awe mwema na mwenye kuvutia kwa sura/umbo zuri.
 • Watazamaji huonesha kuumia, husikitika nk. kadri mtu anavyoonekana ni mwema au mzuri wa umbo lake kama ilivyokuwa kwa mhusika wa Second Chance – Salvado Solenza.
 •  Katika Tanzia, anguko la shujaa huja kutokana na ama uamuzi wake mbaya au kosa lake mwenyewe. Aristotle: alisema kuwa, hakuna kosa la bahati mbaya. Kila mkasa wa kufisha ni matokeo ya maamuzi mabaya, au kosa fulani.
ISTILAHI KATIKA TANZIA:
HUBRISI- Dhambi yenyewe. Kitendo chenyewe akitendacho shujaa ambacho humwingiza katika hamartia.
ANAGNORISIS- Utambuzi wa ndani. Ni ile saa ambapo shujaa hupata utambuzi wa ndani katika akili ya shujaa  ambao humjulisha kuwa kakosea na tayari kesha jitumbukiza katika anguko kuu. (Mutembei, 2005 katika mihadhara ya SW 234)
PERIPATEA-Matendo muhimu ambayo humtoa shujaa katika hali iliyoonekana kuwa afadhali kumdidimiza  katika hali mbaya kabisa. (Mutembei, 2005 katika mihadhara ya SW 234) 
NEMESIS- Adhabu ambayo haina budi kuwapo kutokana na matendo ya Hubrisi (Mutembei, 2005 katika mihadhara ya SW 234).
 • Ramsa ni nini?
Ni aina ya tamthilia ambayo hadhira inapoangalia isiogope au kupata uchungu bali icheke kwa kumkejeli mhusika kutokana na matendo yasiyofurahisha katika jamii. Mhusika anatakiwa amfanye matendo au tabia ambazo ni kinyume na maadili ya jamii, ili yanapomkuta masahibu – hadhira Imcheke kwa upumbavu na uzembe wake. Mfano mzuri ni mikasa inayoonesha baadhi ya wanandoa kutokuwa waaminifu katika ndoa zao – wanapokumbwa na fumanizi na kuumbuka, hadhira itamcheka mhusika kwa kuwa ayafanyayo hayakubaliki katika maadili. Vilevile aina hii ya tamthilia huishia na mwisho wa kufurahisha.
SHUJAA WA KI-RAMSA
Kwa mujibu wa (Mutembei, 2005 katika mihadhara ya SW 234), shujaa wa kiramsa ni mtu mwenye sifa zifuatazo:
 • Sio lazima awe mtu maarufu au Mbabe/Shujaa anaweza kuwa ni kichaa au mwendawazimu fulani ambaye yuko katika jamii
 • Mtu ambaye katika jamii huwa duni, na matendo yake ni ya kiucheshi-ucheshi, ila historia humlea na kumkuza hata akatokea kuwa “fulani” – akaishi raha mustarehe.
 • Mhusika ambaye akifanikiwa kila mtu atafurahia na baada ya igizo atakuwa ameridhishwa na mwisho huo mzuri wa kuishi raha mustarehe.
UHUSIKA WA WAHUSIKA WA KI-RAMSA
 • Ramsa huwahusu watu wa kawaida ambao wana kipato cha kati na chini kama vile: washona viatu, wauza mitumba, wakata nyama, wachoma mishikaki, wanafunzi, walimu, wasukuma mikokoteni, n.k. Ramsa haihusu  watu wa juu ambao ni kama vile: wafalme, malkia, viongozi, watu wote wa nasaba BORA (Mutembei, 2005 katika mihadhara ya SW 234)
 • Ramsa huhusika na mambo ya kawaida yanayowahusu watu wa kawaida katika maisha ya kila siku (Mutembei, 2005 katika mihadhara ya SW 234). Mambo kama: Kupata rafiki mpya (au Kumrudisha wa zamani) au kupata kazi au kupanda cheo kwa mfano akina Mkwere kwenye Mizengwe kila Jumapili saa tatu usiku, kituo cha ITV.
DHAMIRA ZA KI-RAMSA
Ramsa huhusika na mambo ya kawaida yanayowahusu watu wa kawaida katika maisha ya kila siku (Mutembei, 2005 katika mihadhara ya SW 234). Mambo kama: Kupata rafiki mpya (au Kumrudisha wa zamani) au kupata kazi au kupanda cheo kwa mfano akina Mkwere kwenye Mizengwe/Ucheshi kila Jumapili saa tatu usiku, kituo cha ITV.
AINA ZA RAMSA:
UTANI/VICHEKESHO (farce)
Huonekana ni upuuzi, mambo hugeuzwa kinyume. Sura za wahusika hubadilishwa - kama vinyago. Lengo ni kuchekesha na ndimo maana yake hupatikana. Mfano tunaweza kuziweka kazi za Mzee Majuto katika aina hii japo sio sifa zote za utani zinajitokeza katika kazi zao
MAHABA/MAPENZI (romance)
Wapendanao, huwekewa vikwazo (pesa, kabila, hadhi) lakini hatimaye hushinda vikwazo hivyo. Hupendana na kuoana (Mutembei, 2005 katika mihadhara ya SW 234). Tazama kazi nyingi za filamu hapa nyumbani zinaangukia katika kundi hili; mfano ni Sandra, Johari, Sikitiko langu The Game of Love kwa kuzitaja kwa uchache.
TASHTITI/ DHIHAKA- (satire) ni zile kazi zinazolenga kuwasilisha dhihaka kwa viongozi, siasa, au dini (Mutembei, 2005 katika mihadhara ya SW 234). Kwa mfano zamani Ze Comedy ilipokuwa ikirusha vipindi vyake kupitia East Africa Television (EATV); kwa sasa wanatambulikana kama Origino Komedí ila wamepwaya katika uwasilishaji wao – sio kama zamani. Nadhani kuna udhibiti ndani yake.
 • Pia tashititi hizi huhusisha kuakisi yafanywayo na wahalifu, matapeli, wanafiki, wala rushwa, wafanya magendo, waongo n.k. Mfano ni Bongo Darisalaam kilichokuwa kinachorushwa na TBC1.
 • Mhusika mkuu (ambaye ni Kiongozi) huwa na sifa hizo hapo juu na anadhihakiwa ili aache rushwa, uhalifu, utapeli, nk.
 • Ramsa hizi ni kama – njia ya walala hoi kutoa malalamiko yao kwa viongozi wao kwa mfano angalia kazi za Futuhi inayorushwa na Kituo cha Utangazaji cha Star Tv kila Alhamisi usiku saa tatu.
VIPENGELE VYA TAMTHILIA
 • Vipengele vya kifani katika tamthilia ni pamoja na: wahusika, mtindo, muundo, mandhari, jina la kazi, na matumizi ya lugha.
VIPENGELE VYA SANAA ZA MAONESHO
Vipengele vya sanaa za maonesho kwa mujibu wa Aristotle na Semzaba ni hivi vifuatavyo: uhusika na wahusika, maudhui, msuko wa matukio, uteuzi wa lugha, kionwa, na muziki.
Vipengele hivi vya sanaa za maonesho vimejadiliwa katika kitini cha Uandishi wa Kubuni kwa Kiswahili Nadharia na Vitendo kilichoandikwa na Mahenge, E. Soma vipengele hivyo na uvitumie katika kuhakiki kazi za sanaa za maonesho.
MAUDHUI YA TAMTHILIA
 • Maudhui ya tamthilia yanagusia vipengele vya: migogoro, ujumbe, falsafa, mtazamo, msimamo, na dhamira.
 • Matumizi ya tamthilia ni pamoja na: kuelimisha jamii; (katika masuala mbalimbali kama vile: uchumi, siasa, maadili, nk.) kuburudisha jamii, kuonya na kukosoa jamii, kukuza lugha, kurithisha amali za jamii (mila na desturi za jamii husika), nk.

16 comments:

 1. habari....ingekuwa vizuri zaidi ungeeleza na sifa bainifu za tanzia ramsa ili tuweze kupata maarifa,,,ahsante

  ReplyDelete
 2. Naomba, uelezee nadharia za chimbuko la tamthiliya ya kiswahili.

  ReplyDelete
 3. Hata marejeleo yakiongezwa pamoja na usuli wa tamtiliya itakua vyema

  ReplyDelete
 4. Hata marejeleo yakiongezwa pamoja na usuli wa tamtiliya itakua vyema

  ReplyDelete
 5. Mwalimu hukusema hapa kuhusu AINA ZA TANZIA

  ReplyDelete
 6. naomba kujuzwa mambo yaliyochangia kukua na kuchipuka kwa mikondo ya tamthiliya

  ReplyDelete
 7. samahani mheshimiwa uwe unaweka na marejeleo (references)

  ReplyDelete
 8. ni fleshi kuwa munaeleza mambo haya lakini tunachodhamilia kwa wingi ni sifa bainifu za kila unachokieleza.

  ReplyDelete
 9. Naomba unieleze maoni ya Aristatle kuhusu tamthlia ya kiswahili

  ReplyDelete
 10. Samahan ndugu marejeleo ni muhim pia jitahidi uwe unaweka

  ReplyDelete
 11. Kazi nzuri sana ila naomba aina za tanzia tafadhali

  ReplyDelete
 12. Kazi nzuri sana imenielewesha

  ReplyDelete
 13. Naomba nielezwe kwa kina umuhimu wa uigizaji wa tamthilia Na drama

  ReplyDelete
 14. Mtazamo mzuri...kazi yako safi

  ReplyDelete