MOTIFU YA
SAFARI NA MSAKO KAMA MWEGA MKUU WA DHAMIRA KATIKA “MARIMBA YA MAJALIWA”
“Marimba
ya Majaliwa ni hadithi iloyoandikwa na Edwini Semzaba mwaka (2008) ambayo
inaelezea kuhusiana na marimba ya Majaliwa iliyopotea. Mwandishi ameonyesha
jinsi Majaliwa alivyokuwa anatafuta marimba yake mpaka akaipata. Majaliwa
alisafiri kwa kutumia njia mbalimbali kama vile ungo, fagio, na maumbo ya
samaki akizunguka Tanzania nzima akisaka marimba ya nyuzi ishirini (20).
Alianza Mafia, akaenda Zanzibar, Tanga, Moshi na Arusha, Iringa, Mwanza,
Kigoma, na miji mingine mingi. Na Kongoti bingwa wa Taifa wa Marimba akimchenga
kila mara huku akinga’nga’nia Marimba ya Majaliwa ili amzuie kushinda na
ashinde yeye na bila Marimba yenye nyuzi ishirini (20) hakuna ushindi.
Katika
mada hii tutaanza kuelezea maana ya fasihi, fasihi ya watoto, na maana ya
motifu, na maaana ya dhamira. Kisha katika kiini cha swali letu tutachambua
motifu mbalimbali za safari na msako
kama zilivyo jitokeza katika kitabu. Baada ya hapo kuonyesha dhamira
mbalimbali.
Wataalamu
mbalimbali wameelezea maana ya fasihi. Mulokozi (1996:3) akimnukuu Egletoni (1983:20-21),
anasema fasihi ni sanaa ya lugha yenye ubunifu bilakujali kama imeandikwa au
laa.
Mulokozi
mwaka (1996), anasema ni sanaa ya lugha inayoangalia maisha na mazingira
halisi. Anaendelea kusema kuwa ni sanaa ya lugha yenye ufundi wa hali ya juu
ili kuweza kuwasilisha mawazo aliyonayo mtu kwa njia inayoweza kuathiri kwa
kutumia sanaa hiyo kimaandishi au kimazungumzo.
TUKI
(2004), wanasema mtoto ni mtu mwenye umri mdogo, katika maana hii hajatueleza
umri huo ni wa kuanzia miaka mingapi hadi miaka mingapi lakini kutokana
na maana hii Mulokozi (2008:338), anasema fasihi ya watoto na vijana ni ile
fasihi inayorejelea matini au kazi ambazo kimsingi hadhira yake ni watoto na
vijana, na hii ni kati ya umri wa miaka 0-10 na 11-17. Hivyo fasihi ya watoto
na vijana huhusisha kazi zinazowahusu bibadamu kati ya miaka 0-17. Na kazi hizo
zaweza kuwa riwaya, Hadithi fupi, Tamthilia au Ushahiri.
Motifu-
Ni dhana/jambo au kipengele kinachojirudiarudia katika kazi ya fasihi. Ambacho
kinaweza kuwa cha kifani au kinaudhui. Mfano; Motifu ya safari.
TUKI
(2004), dhamira ni kiini cha jambo au habari iliyosimuliwa ama kuandikwa hasa
katika fasihi
Madumulla
(2009), Dhamira ni wazo kuu katika kazi ya fasihi. Kwa ujumla wote
wanazungumzia jambo au wazo kuu katika
fasihi, Hivyo tunakubaliana na fasihi zote hapo juu.
Kuanzia
mwanzo hadi mwisho wa kitabu tunaona Majaliwa alisafiri sehemu mbalimbali hadi
kufikia kiwango cha kuzunguka nchi nzima huku akimsaka Kongoti ili aweze kuirejesha
Marimba yake. Safari ya Majaliwa ilianzia Mafia mkoani Pwani. Hii ni baada ya
kuchukuliwa Marimba yake na watu ambao awali hakuwafahamu na baadaye walikimbia
kichakani (ukurasa wa 2). Kwa kuwa marimba nguvu zake ziliambatana na nguvu ya
kuzimu, usiku wa manane marehemu bibi yake mzaa mama alimjia ndotoni na
kumwambia Majaliwa kuwa, Kongoti Nachienga ndiye aliiba Marimba yake kwa
wasiwasi wa kushindwa wakifika Dodoma kwenye mashindano ya marimba ya kitaifa.
Katika upande wa kuzimu babu yake Majaliwa mzaa baba yake yupo upande wa Kongoti
(ukurasa 3)
Safari
ilianza rasmi usiku wa manane kisiwa cha Mafia katika ufukwe wa kilindoni wa
Bahari ya Hindi. (uk.5). Walisafiri huku bibi yake akiwa katika umbo la samaki
(nguva na papa) (uk.5) hadi Zanzibar (uk.7-10). Akiwa huko Majaliwa aliendelea
kumsaka Kongoti bila mafanikio (uk.11). Majaliwa anaendelea na safari kuelekea
Tanga. Wanatumia aina mbalimbali za usafiri kama Ungo, Ufagio, Chai maharage,
na basi mfano (uk.21,22 na 105). Majaliwa anakumbana na misukosuko mbalimbali
baharini hatimaye anafika Tanga, lakini juhudi zake hazimpi mafanikio (sura ya
7-11). Majaliwa baada ya kusikia kwamba Kongoti alikuwa anaelekea Kilimanjaro
alianzisha safari ya kuelekea huko ili aweze kuitwaa marimba yake sura ya
(11-17) kwa usafari wa basi (uk.46). Kutokana na misukosuko mbalimbali Majaliwa
anachelewa. Kilimanjaro alikuta mashindano yamekwisha na Kongoti sasa anaelekea
Arusha. Majaliwa naye ili kuisaka marimba yake aliamua kumsaka Kongoti lakini
pasipo na mafanikio yoyote.
Baadaye
Majaliwa alisafili kwenda Singida (sura 26-27) baadaye Kondoa kwenda Tabora (sura
ya 27-30) Pia Tabora kwenda Shinyanga. Katika safari zote hizo Majaliwa
hakufanikiwa kutwaa marimba yake lakini hakukata tamaa aliendelea na safari ya
msako ukurasa 239.
Majaliwa
anaendelea na safari kutoka Shinyanga kwenda Mwanza baada ya kufika alishuka
kwenye ndege na kupanda daladala kuelekea Mwanza (uk.131) baada ya hapo
Majaliwa alisafiri kuelekea Butihama baadaye kurudi Mwanza kwa kujionea maeneo
mbalimbali ya kihistoria (uk.138-140) Wakiwa katika usafiri wa meli Majaliwa
alivamiwa na Kongoti. Akapambana naye ili airejeshe marimba yake lakini Marimba
ile ilitumbikia ziwani (uk.141) Bibi yake alipotokea akamwelezea kisha
akayafuatilia na kumwambia kuwa hayakuwa yenyewe. Wakatembelea sehemu mbalimbali
za kihistoria za Mwanza meli ilifika Kemondo Bukoba kagera ambapo palikuwa na
mashindano pia na Kongoti angekuwa miongoni mwao alisafiri sehemu mbalimbali za
karagwe kwa basi kutokana na ulinzi mkali aliondoka kutembelea sehemu mbalimbali
za kihistoria (uk.151)
Majaliwa
aliendelea na safari ya kuelekea Kigoma (uk.155) ambapo alitembelea sehemu
mbalimbali za vivutio vya watalii baadaye mashindano yalifanyika hoteli ya Lake
Tanganyika ambapo alipata nafasi ya kufanya ufunguzi na hakupata pesa nyingi
hapo usiku walisafili kwa ungo kupitia Mbozi na milima ya mrengi baadaye Mbeya
ambapo mashindano yalifanyika Kileleni lodge ambapo alitumia njia mbalimbali na
kuipata marimba lakini haikuwa yenyewe (uk.175) safari ya usiku ilikuwa ni
kutembelea maeneo mbalimbali ya kihistoria kuamkia Iringa ambapo Kongoti angetumbuiza
kwenye maadhimisho ya shujaa Mkwawa (uk.187) Baadaye Kidatu Njombe, Rudewa hadi
Manda. Baadaye Mji wa Tunduma Mola tena Mwanjerwa alisikia Kongoti bado anapiga
marimba aliamini kuwa bado ana marimba yake (uk.197)
Safari
ya Majaliwa huko Mbeya kwenda Songea kwa basi la Scandinavia (uk.198)
Mashindano ya Ruvuma Lindi na Mtwara, pia wakiwa Ruvuma walitembelea sehemu
mbalimbali za kihistoria (uk.200-205), Baadaye Ndanda, Newala, Mtwara, Mnazi
bay, Lindi (Tengeru) (uk.205) Baadaye ukumbi wa mkorosho mpya ambapo mashindano
yalifanyika lakini majaliwa hakupata nafasi ya kumsogelea Kongoti (uk.208) kwa
usafiri wa Ufagio walienda Rufiji hadi Mafia, Mkuranga, Dar es salaam, Temeke,
Mwenge, Lugalo, Bagamoyo na sehemu mbalimbali za Dar es salaam (uk.211).
Kutoka
Dar Es Salaam alifunga safari yake hadi Morogoro (uk.212) kwa usafiri wa basi
baada ya kupita sehemu mbalimbali Majaliwa alifanikiwa kuikuta Marimba Mjini
Morogoro akiwa katika harakati za safari ya kuelekea katika shindano la kitaifa
huko Dodoma ilikuwa baada ya kubadilisha marimba katika sinia la ukaguzi hapo
tena Majaliwa alianza kujiandaa kusafiri kwa basi kwenda Dodoma kwenye
mashindano ya kitaifa pamoja na misukosuko ya kukatika kwa daraja (uk.230) Baadaye
aliingia Dodoma kwa kupitia Chamwino Dodoma Mjini baadaye Milimani ambapo
mashindano yalifanyika hoteli ya Milimani huko Dodoma na kuibuka Mshindi wa
kuwabwaga wenzake wote pamoja na adui yake Kongoti na kukamilisha ndoto zake za
kuwa bigwa wa Taifa.
Maana
ya ujasiri Kwa mujibu wa TUK (2004), hali ya kukabili jambo hofu uhodari na
ushujaa. Ujasiri ni dhamira kuu katika kitabu hiki ambayo imejitokea katika
motifu zote na misako ambayo imeandikwa katika kitabu hiki Majaliwa ameonesha kuwa
jasiri kuanzia mwanzo wa hadithi pale anapoanza kutafuta marimba yake iliyoibwa
akisaidiwa na bibi yake. Hili limeonekana katika sehemu mbalimbali mfano:-
katika ukurasa wa 72 sura ya 17 ambapo majaliwa anapambana na dereva taski
baada ya kutaka kumwibia majaliwa pesa zake wakati wakimtafuta kongoti
aliyekuwa kwenye pikipiki.
“Majaliwa akiwa
ameshika jiwe lake la rubi alimpiga nalo Yule dereva kwenye macho yake yote
mawili mara mbili”
Mfano
mwingine ni pale majaliwa alipopambana na kongoti mlenzi wakinyang’anyana
marimba majaliwa alikuwa mtoto mdogo lakini aliweza kukabiliana na kongoti
ambaye alikuwa mtu mzima. Hili limeoneshwa katika ukurasa wa 141 sura ya 34.
“Nalianza kukamatana na kuangushana na ingawa
alikuwa mtoto tu, uchungu wa kudhulumiwa marimba yake ulimjaza ari na akachuana
kishujaa”
Hivyo
basi kwa kuangalia hiyo mifano tunaona majaliwa alikuwa jasiri na mwandishi
alionesha hili kama dhamira kuu
Dhamira
nyingine ni Imani za kishirikina. Imani kwa mujibu wa Kamusi TUKI (2004), ni
mambo anayoyakubali mtu kuwa ni ya kweli na anayopaswa kuheshimu, haswa katika
dini, au itikadi. Ushikirina ni tabia ya kuamini mambo ya uchawi, mizimu, nk.
Katika kitabu hiki dhamira ya imana ya kishirikina imejijenga sana katika
motifu ya safari na msako iliyojitokeza katika kitabu hiki mfano katika kitabu
hiki mwandishi alionyesha hili pale majaliwa alipokuwa anasafiri kwa njia ya
kishirikina kama vile ungo, fagio, pia kuna wakati mwingine alikuwa anasafiri
kutoka sehemu moja kwenda nyingine kwa kufumba macho na kufumbua. Mfano mwingine
ni ule kusafiri kwa ungo imeoneshwa (uk.52), Bibi alimwambia Majaliwa apande
kwenye Ungo.
“ Bibi alimwambia
mjukuu wake sasa na wewe panda kwenye ungo”
.
Pia kusafiri kwa ufagio (uk.105) Majaliwa
alimletea bibi fagio uliokuwa umeachwa kwenye takataka. “Haya panda nyuma” Kufumba na kufumbua wakajikuta wako angani.
Dhamira
nyingi ni Rushwa. Rushwa ni fedha au kitu cha dhamani kinachotolewa na kupewa
mtu mwenye madaraka ya kitu fulani ili mpaji apatiwe upendeleo. Katika kitabu
hiki rushwa ilijitokeza pale ambapo Majaliwa alimpa fedha kwa sababu hakuwa na
kibali cha kuingia sehemu za utalii ili aweze kumwachia. Hili limeoneshwa uk.66
“Majaliwa alipoangalia
saa iliyotundikwa ukutani na kuona ni saa tano, alibadilisha uamuzi wake na
kuongeza dola moja, hapo askari hakusema kitu”.
Hilo
pia limeoneshwa katika uk.213 sura ya 54.
Tamaa ni hamu kubwa ya kupata kitu au shauku
au matarajio ya kupata kitu. Hili mwandishi pia amelibainisha kwa kuanza na
Majaliwa ambaye yeye alikuwa na tamaa ya
kupata marimba yake iliyochukuliwa na kongoti kiasi cha kuamua kujitosa na
kuanza kutafuta kwa kupitia hali
mbalimbali ingawa alikuwa ni mtoto. Tamaa pia imeoneshwa pale ambapo dereva
teksi alitamani dola za Majaliwa alipokuwa anamwendesha mpaka akapata upofu kwa
kupigwa na Majaliwa. Pia bibi alihadithia hadithi moja ambayo ilikuwa
inaonyesha jinsi ambavyo tamaa ni mbaya uk.123-126.
“Bibi akamuuliza
Majaliwa hadithi inakufundisha nini? Majaliwa anajibu Tamaa ni mbaya”.
Katika uk.72 dereva teksi aliona pesa za majaliwa na kuzitamani hivyo akampeleka
porini. Dereva anamwabia, “toa pesa zote ulizonazo haraka”
Madhara
ya kutokuwa mtiifu. Hili pia mwandishi amelionesha katika kitabu chake pale
ambapo Majaliwa alikuwa anakiuka maagizo ambayo alikuwa anapewa na bibi yake na
kupata madhara. Hili mwandishi amelionesha katika uk.50 ambapo bibi anamwambia
majaliwa.
“siku
zote utii ni bora”. ‘Si nilikukataza kula kitu chochote kupitia kinywani” Hapo
ndipo Majaliwa akakumbuka alikula mayai kwenye tumbo la nyangumi. Bibi akasema “hilo ndilo kosa ndio maana Rubi haikufanya kazi yake nami nikakupa
adhabu ya kuwa peke yako usiku wote wa jana.”
Pia
Bibi alimwadithia Majaliwa Hadithi ya madhara ya kutokuwa mtiifu katika uk.169-171
ambayo ikimuelezea mvuvi ambaye alikosa utiifu na mwishowe akakosa utajiri kwa
ajili hiyo.
Dhamira
nyingine ni ile ya umuhimu wa kujua historia mbalimbali ya maeneo katika nchi.
Hili mwandishi amelionesha wazi kwani limeoneshwa na kujengwa dhamira na motifu
ya safari kwani katika safari ambazo Majaliwa alizifanya ndipo hapo aliweza
kujua historia za sehemu mbalimbali alizosimuliwa na bibi yake. Kwa ujumla
kulikuwa na hisoria ya mapango ya Amboni Tanga, Kondoa Iringa, mji wa Tabora,
hisotria ya ngome kongwe, Kaburi la Abeid Amani Karume, Wangoni. Makaburi ya
watu waliokufa kwa ajili ya Treni, Meli iliyozama ya MV Bukoba na sehemu
nyinginezo.
Pamoja
na kuwepo na dhamira hizo hapo juu zilizoelezwa kwa mapana na marefu kulikuwepo
pia dhamira nyinginezo ambazo zilizokuwepo katika kitabu hiki. Dhamira hizo ni
pamoja na wizi, wivu, mashindano, kujikinga na ukimwi, chuki, nafasi ya
mwanamke katika jamii, Ukombozi, Elimu, Ukatili, Umoja na mshikamano na hali
ngumu ya maisha. Hivyo kwa ujumla tunaweza kusema kuwa mwandishi amefanikiwa
kwa kiasi kikubwa kujadili masuala mbalimbali yaliyoko katika jamii hasa jamii
yetu ya Kitanzania.
MAREJEO
Madumulla, S. (2009), Riwaya yaKiswahili: Mature Educational
Publishers Lited.
Mulokozi, M. M. (1996), Utangulizi wa Fasihi ya Kiswahili: Taasisi
ya Uchunguzi wa Kiswahili, Dar es Salaam.
Semzaba, E. (2008), Marimba ya Majaliwa. E&D Publishers
Limited:Dar Es Salaam.
TUKI (2OO4), Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Taasisi ya
Taaluma za Kiswahili: Dar Es Salaam.
No comments:
Post a Comment