VIGEZO ALIVYOVITUMIA
MULOKOZI KATIKA KUGAWA TANZU NA VIPERA VYA
FASIHI SIMULIZI: KATIKA MULIKA (1989) NAMBA 21
Kwa mujibu wa Mulokozi katika Mulika
namba 21(1989). Pamoja na kwamba Fasihi ni kongwe lakini kitaaluma bado ni
changa kwa sababu ilianza kuchungunzwa hivi karibuni. Hivyo imepelekea
kutokuwepo kwa nadharia, marejeo, wala istilahi zenye kutosheleza mahitaji ya
taaluma hiyo. Tatizo hili linadhihirika pale tunapoangalia kazi za wataalamu
mbalimbali kuhusu tanzu za Fasihi Simulizi. Kwa upande wa nadharia kitabu pekee
kinachozijadili tanzu za Fasihi Simulizi kwa urefu ni kitabu cha Ruth Fennegan
kinachoitwa Oral Literature in Africa
(1970). Kwa upande wa Kiswahili hakuna kitabu kinachojadili uwanja wa tanzu za
Fasihi Simulizi. Badala yake kunamiongozo michache kwa ajili ya shule za
sekondari kama vile Balisidya, N (1975) na Taasisi ya Elimu (1987)
Mulika namba 21 ni jarida la kitaaluma
linalotoa fursa kwa wataalamu, waalimu na wanafunzi katika kujadili mada
mbalimbali za kiswahili. Jarida hili lililoandikwa mwaka 1989 ndani yake kuna
makala ya Fasihi Simulizi inayohusu tanzu za Fasihi Simulizi na vipera vyake
iliyoandikwa na M.M.Mulokozi.
Hivyo basi kutokana na kukosekana kwa nadharia
zinazoongoza ugawaji wa tanzu za Fasihi Simulizi ya Kiswahili wataalamu wengi
wamekuwa wakitumia vigezo mbalimbali ambavyo ni maudhui, fani, matukio, idadi
ya waimbaji, vifaa vinavyotumika na namna ya uimbaji.
Fasihisi Simulizi imejadiliwa na
wataalamu mbalimbali miongoni mwa waalamu hao ni M.M.Mulokozi (1996) anasema
Fasihi Simulizi ni fasihi inayotungwa au kubuniwa kichwani na kuwasilishwa kwa
hadhira kwa njia ya mdomo na vitendo bila kutumia maandishi.
TUKI (2004) Fasihi Simulizi ni kazi ya
fasihi inayohifadhiwa na kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine kwa njia
ya mdomo kama vile; hadithi, ngoma na vitendawili.
Hivyo basi Fasihi Simulizi ni fasihi
inayotokana na maneno ambayo huzungumzwa, hutolewa au kuimbwa ambapo mtungaji
na mwasilishaji hutumia sanaa.
Tanzu ni istilahi inayotumiwa kuelezea
au kurejelea aina ya kazi mbalimbali za kifasihi. Inawezekana utanzu mkuu kuwa
na vitanzu vingine mbalimbali kwa mfano, tanzu kuu za kifasihi ni Riwaya,
Tamthilia, Shahiri, Novela, Insha na Hadithi (Wamitila (2003).
Vipera ni dhana inayotumiwa kuelezea
vijitanzu katika fasihi hasa fasihi simulizi. Mfano: semi methali, mafumbo,
vitendawili nakadhalika. (Wamitila 2003)
M.M.Mulokozi katika makala yake ya
tanzu za Fasihi Simulizi iliyo katika jarida la Muulika namba 21(1989)
amezigawa tanzu na vipera vya Fasihi Simulizi kwa kutumia vigezo viwili ambavyo
ni,kigezo cha kwanza ni umbile na tabia ya kazi inayohusika na kigezo cha pili
ni muktadha na namna ya uwasilishaji wake kwa hadhira.
Umbile na tabia ya kazi inayohusika:
katika kigezo hiki Mulokozi ameangalia vipengele vya ndani vinavyoiumba sanaa
hiyo na kuipa muelekeo au mwenendo. Baadhi ya vipengele hivyo vya ndani ni namna
lugha inavyotumika (kishahiri, kinathari, kimafumbo, kiwimbo na kighani),
muundo wa fani hiyo na wahusika. Kwa upande wa muktadha na namna ya
uwasilishaji amezingatia kuwa, Fasihi Simulizi ni tukio hivyo huambatana na
muingiliano wa mambo matatu ambayo ni muktadha, watu na mahali. Mwingiliano huu
ndio unaotupa muktadha na muktadha ndio unaoamua fani fulani ya Fasihi Simulizi
ichukue umbo lipi, iwasilishwe vipi kwa hadhira, kwenye wakati na mahali hapo.
Hivyo hadithi inaweza kugeuzwa wimbo, utendi unaweza kuwa hadithi na wimbo
unaweza kugeuzwa ghani au usemi kutegemea muktadha unaohusika (Mulokozi 1989).
Kwa hiyo kwa kutumia vigezo hivi,
Mulokozi amezigawa tanzu na vipera vya Fasihi Simulizi kama ifuatavyo;
Masimulizi; hii ni tanzu ya Fasihi
Simulizi yenye kusimulia habari fulani. Katika kugawa utanzu huu vigezo
vilivyotumika ni pamoja na kigezo cha lugha ambapo lugha inayotumika katika
masimulizi ni ya kinathari. Pia kigezo kingine ni kigezo cha muundo, mara
nyingi masimulizi huwa na muundo unaojitofautisha na tanzu nyingine kama vile
ushairi. Katika masimulizi muundo wake mara nyingi huwa wa moja kwa moja yaani
mtiririko wa visa na matukio. Vilevile kigezo kingine ni kigezo cha wahusika
ambapo katika kigezo hiki huhusisha wahusika wa pande mbili ambao ni mtendaji
na watendwaji. Pia kigezo kingine ni kigezo cha namna ya uwasilishaji. Katika uwasilishwaji
huwasilishwa na msimuliaji mbele ya hadhira. Kigezo kingine ni kigezo cha
mandhari ambayo huwa maaluma kama vile chini ya mti mkubwa na uwanjani. Masimulizi
pia hufanyika katika muda maalum. Mfano, baada ya kazi.
Masimulizi yamegawanyika katika tanzu
kuu mbili ambazo ni tanzu za kihadithi (za kubuni) na tanzu za kisalua
(kihisitoria). Tanzu za kihadithi zina kipera kimoja ambacho ni ngano. Ngano
(vigano/hurafa), hizi ni hadithi za kimapokeo zitumiazo wahusika kama wanyama,
miti na watu kuelezea na kuonya kuhusu maisha. Vigezo vilivyotumika katika kugawa ngano ni
kigezo cha lugha ambayo ni lugha ya kinathari, kigezo cha dhima ambacho huelezea
au kuonya kuhusu maisha na kufurahisha. Kigezo kingine kilichotumika ni kigezo
cha wahusika ambao ni wanyama, miti na watu. Kipera hiki cha ngano kinajumuisha
vijipera vifuatavyo ambavyo ni istiara, mbazi na kisa.
Istiara; hii ni hadithi ambayo maana
yake ya wazi inawakilisha maana nyingine iliyofichika. Vigezo vilivyotumika
katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha lugha ambayo ni lugha ya mafumbo.
Mbazi; hii ni hadithi fupi yenye
mafunzo itolewayo kama kielelezo wakati wa maongezi au kumkanya mtu. Kigezo
kilichotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha dhima.
Kisa; hii ni hadithi fupi ya
kufurahisha kuhusu tukio la kweli. Kigezo kilichotumika ni kigezo cha kidhima.
Utanzu mwingine wa masimulizi ni utanzu
wa kisalua. Utanzu huu umegawanyika katika vipera vifuatavyo ambavyo ni
visakale, mapisi, tarihi, kumbukumbu na visasili.
Visakale; haya ni masimulizi ya mapokeo
juu ya wahenga au mashujaa wa kabila au taifa yenye kuchanganya chuku na
historia (kama hadithi ya Liyongo). Vigezo vilivyuotumika hapa ni kigezo cha
wahusika ambao wapo katika historia yaani mashujaa fulani. Kigezo kingine ni
fani ya ubunifu.
Mapisi; haya ni maelezo ya kihistoria
bila kutia mambo ya kubuni. Hapa pia kigezo kilichotumika ni kigezo cha dhima
ambacho huelezea mambo ya kihistoria yaliyo ya kweli.
Tarihi; haya ni maelezo au jedwali la
matukio muhimu na tarehe zake. Kigezo kilichotumika hapa ni kigezo cha kidhima
ambacho ni kuelezea matukio muhimu na tarehe zake. Pia kigezo kingine ni namna
ya uwasilishaji ambapo huwasilishwa kwa kutumia jedwali na lugha yake huwa
katika maandishi.
Kumbukumbu; haya ni maelezo ya matukio
muhimu yanayomuhusu mtu binafsi au jamii ya watu. Hapa kimetumika kigezo cha
fani, ambayo ni fani za wasifu na tawasifu. Pia kigezo kingine ni kigezo cha
wahusika ambao ni watu.
Visasili; hiki ni kipera kinachofungamana
na imani za dini na mizungu ya kajamii pia hizi ni hadithi za kale zenye
kuwakilisha imani na mtazamo wa jamii inayohusika kuhusu asili ya ulimwengu na
maisha yao. Kigezo kilichotumika ni kigezo cha kidhima ambacho huelezea shabaha
ya maisha.
Utanzu mwingine wa Fasihi Simulizi ni
utanzu wa Semi. Semi ni tungo au kauli fupi fupi za kisanaa zenye kubeba maana
au mafunzo. Kigezo kilichotumika katika kugawa utanzu huu ni kigezo cha lugha
ambayo ni lugha ya mkato. Kigezo kingine ni kigezo cha kidhima ambacho ni
kufunza.
Utanzu huu umegawanyika katika vipera
vifuatavyo ambavyo ni methali, vitendawili, misimu, mafumbo na lakabu.
Methali ni semi fupi fupi zenye kueleza
kwa mukhtasari fikra au mafunzo mazito yaliyotokana na uzoefu wa kijamii.
Vigezo vilivyotumika katika kipera hiki ni kigezo cha lugha ambayo ni lugha ya
mafumbo. Vilevile kimetumika kigezo cha muundo ambapo methali huundwa na muundo
wa pande mbili ambazo hutegemeana.
Vitendawili; huu ni usemi uliofumbwa
ambao hutolewa kwa hadhira ili ufumbuliwe. Vigezo vilivyotumika ni kigezo cha
lugha. Hapa lugha inayotumika ni lugha ya kimafumbo.
Misimu; ni semi za muda na mahali
maalum ambazo huzuka na kutoweka kutegemea mazingira maalum. Hivyo vigezo
vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha muktadha yaani hutokea
wakati maalum na mazingira maalum.
Mafumbo; ni semi za maonyo au mawaidha
ambazo maana zake za ndani zimefichika. Kigezo kilichotumika ni kigezo cha
kidhima ambacho ni kuonya pamoja na kigezo cha lugha ambayo ni lugha ya
mafumbo.
Lakabu; haya ni majina ya kupanga
ambayo baadhi ya watu hupewa au hujipatia kutokana na sifa zao za kimwili,
kinasaba, kitabia au kimatendo. Kigezo kilicho tumika katika kipera hiki ni
kigezo cha lugha ambayo lugha iliyotumika ni lugha kificho yaani maana yake
hufichwa.
Utanzu mwingine wa Fasihi Simulizi ni
ushairi. Huu ni utanzu wa fasihi simulizi unaowasilishwa kwa hadhira kwa njia
ya uimbaji au ughani badala ya usemaji wa kawaida. Vigezo vilivyotumika katika
kugawa utanzu huu ni kigezo cha lugha ambayo ni lugha ya kishairi. Pia
kimetumika kigezo cha fani ambapo fani inayotumika ni wizani, lugha ya mkato,
lugha ya mafumbo na uimbaji au ughani.
Katika utanzu huu kuna vipera viwili
ambavyo ni nyimbo na maghani;
Nyimbo ni kila kinachoimbwa. Vigezo
vilivyotumika katika kipera hiki cha ushairi ni kigezo cha fani ambapo
huangalia muziki wa sauti ya muimbaji au waimbaji, muziki wa ala (kama ipo),
matini au maneno yanayoimbwa. Pia kuna kigezo cha muktadha ambacho huzingatia
hadhira inayoimbiwa na muktadha unaofungamana na wimbo huo, kwa mfano sherehe,
ibada, kilio nakadhalika. Kwa vigezo hivi utanzu wa nyimbo umegawanyika katika
vijipera vifuatavyo ambavyo ni, tumbuizo, bembea, kongozi, nyimbo za dini,
wawe, tenzi, tendi, mbolezi, kimai, nyiso, nyimbo za vita, nyimbo za uwindaji,
nyimbo za taifa, nyimbo za watoto na nyimbo za kazi.
Tumbuizo; hizi ni nyimbo za furaha
ziimbwazo kuwafurahisha watu kwenye matukio mbalimbali kama vile ngomani au
harusini. Vigezo vilivyotumika hapa ni kigezo cha kidhima ambacho hulenga
kuwafurahisha watu, pia kigezo kingine ni kigezo cha kimuktadha ambapo
huwasilishwa katika matukio yanayoendana na dhima ya kufurahisha.
Bembea; hizi ni nyimbo za kubembeleza
watoto. Kigezo kilichotumika hapa ni kigezo cha kidhima ambapo hulenga
kubembeleza watoto.
Kongozi; hizi ni nyimbo za kuaga mwaka.
Vigezo vilivyotumika hapa ni kigezo cha kidhima ambapo dhima yake ni kuaga
mwaka na kigezo cha kimuktadha ambapo muktadha wake ni muktadha maalum yaani huimbwa
mwishoni mwa mwaka.
Nyimbo za dini; hizi ni nyimbo zinazoimbwa
kwa lengo la kumsifu Mungu au miungu. Vigezo vilivyotumika ni kigezo cha
kidhima ambapo dhima yake ni kumsifu Mungu au miungu, pia kimetumika kigezo cha
kimuktadha ambapo huimbwa katika muktadha wa kidini.
Wawe; hizi ni nyimbo za kilimo. Vigezo
vilivyotumika ni kigezo cha kimuktadha ambapo huuimbwa wakati wa kulima, pia
kigezo cha kidhima kimetumika ambapo dhima yake ni kuchapusha kazi.
Tenzi; hizi ni nyimbo ndefu za
kimasimulizi au mawaidha. Kigezo kilichotumika ni kigezo cha kifani ambapo fani
yake ni masimulizi au mawaidha.
Tendi; hizi ni nyimbo ndefu za
masimulizi juu ya matendo ya mashujaa. Vigezo vilivyotumika hapa ni kigezo cha
kifani ambapo wahusika wa tendi ni watu wenye historia za matendo ya kishujaa,
pia kigezo cha lugha kimetumika ambapo lugha yake ni ya kinathari.
Mbolezi; hizi ni nyimbo za kilio au
maombolezo. Vigezo vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha
kimuktadha ambapo huwasilishwa katika muktadha wa maombolezo au
kilioni/msibani, pia kimetumika kigezo cha kidhima ambapo dhima yake ni
kuomboleza.
Kimai; hizi ni nyimbo zihusuzo shughuli
za baharini. Vigezo vilivyotumika hapa ni kigezo cha kidhima ambapo dhima yake
ni kuchapusha kazi. Vilevile katika kigezo cha kimuktadha kimai huwasilishwa katika
mazingira ya baharini.
Nyiso; hizi ni nyimbo za jandoni. Vigezo
vilivyotumika ni kigezo cha kidhima ambapo dhima yake ni kutoa mafunzo kwa
vijana kuhusu maisha ya utu uzima. Kigezo kingine ni kigezo cha kimuktadha
ambapo nyiso huwasilishwa katika mazingira maalumu, kama vile porini
nakadhalika.
Nyimbo za vita; hizi ni nyimbo
ziimbwazo na askari wakati wa vita. Vigezo vilivyotumika katika kugawa kipera
hiki ni kigezo cha kimuktadha ambapo muktadha wake huwa ni wakati wa vita, na
kigezo kingine ni kigezo cha wahusika au waimbaji ambapo waimbaji wake huwa ni
maaskari.
Nyimbo za watoto, hizi ni nyimbo
waimbazo watoto wakati wa michezo yao. Vigezo vilivyotumika ni pamoja na kigezo
cha kimuktadha ambapo huwasilishwa wakati wa michezo ya watoto. Kigezo kingine
ni kigezo cha wahusika au waimbaji ambapo waimbaji wake huwa ni watoto.
Nyimbo za uwindaji; hizi ni nyimbo
ambazo huimbwa na makundi ya wawindaji wakati wa shughuli au sherehe zao.
Vigezo vilivyotumika hapa ni kigezo cha wahusika au waimbaji ambapo huimbwa na
wawindaji na kigezo kingine ni kigezo cha kimuktadha ambapo huwasilishwa wakati
wa shughuli au sherehe za uwindaji.
Nyimbo za Taifa; hizi ni nyimbo za
kisifia Taifa au kabila. Kigezo kilichotumika hapa ni kigezo cha kidhima ambapo
dhima yake ni kusifia Taifa au kabila.
Nyimbo za kazi; hizi ni nyimbo
zinazoimbwa katika shughuli mbalimbali kama vile, kulima, kutwanga, kusuka,
uvuvi, uashi, useremala na kadhalika. Vigezo vilivyotumika hapa ni kigezo cha
muktadha wa uwasilishaji ambapo huwasilishwa kulingana na shughali maalumu. Pia
kigezo kingine ni kigezo cha kidhima ambapo dhima ya nyimbo za kazi ni
kuchapusha kazi.
Maghani; hiki ni kipera cha ushairi kinachotolewa
kwa kalima badala ya kuimbwa. Kwa mujibu wa Wamitila (2003) maghani ni istilahi
inayotumiwa kuelezea aina ya ushairi ambao hutolewa kwa kalima au maneno badala
ya kuimbwa. Vigezo vilivyotumika katika kugawa utanzu huu ni lugha ambayo ni
lugha ya kishairi. Pia ametumia kigezo cha wahusika ambapo wahusika wakuu ni
binadamu. Hivyo vigezo hivi ndivyo vilivyopelekea utanzu huu kuwekwa kwenye
utanzu wa ushairi.
Kipera hiki kina vijipera vitatu ambavyo
ni maghani ya kawaida, sifo na maghani masimulizi. Maghani ya kawaida ni kundi
ambalo tunaweza kuingiza fani mbalimbali za ushahiri simulizi kama vile ushairi
wa mapenzi, siasa, maombolezo, kazi, dini ilimradi unaghanwa katika namna ya
uwasilishwaji wake.
Sifo; hizi ni tungo za kusifu ambazo
husifu watu, wanyama na mimea. Baadhi ya sifo huwa zinakashifu au kukejeli.
Vigezo vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha wahusika, wahusika
wake wakuu ni binadamu wanyama au mimea. Kigezo kingine ni muktadha ambao
huelezea matukio yaliyopita au yaliyopo. Sifo huwa na tanzu muhimu kama vile
vivugo (majigambo), pembezi na tondozi.
Kivugo; hili ni ghani la kujisifia,
hutungwa na kughanwa na muhusika mwenyewe. Vigezo vilivyotumika katika kugawa
kijipera hiki cha sifo ni lugha, katika lugha zimetumika mbinu kama vile
sitiari, mkato, vidokezo, ishara, takriri na vina. Kigezo kingine ni kigezo cha
wahusika ambapo wahusika wake wakuu ni binadamu pia kimetumika kigezo cha
muktadha ambapo muktadha wake hufungamana na tukio maalum katika maisha ya
muhusika, mfano vitani. Vilevile katika kigezo cha uwasilishaji huweza kuwa na
masimulizi ndani yake. Muundo wake hutegemea shabaha za mtunzi na jadi ya
utunzi anayoiwakilisha hakiandikwi na kutungwa papo kwa papo.
Tondozi; hizi ni tungo za kusifu watu,
wanyama au vitu. (Pembezi pia ni aina ya tondozi ambayo imekusudiwa watu wa
aina fulani tu). Vigezo vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha
wahusika ambao ni wanyama na mimea. Mfano wa wanyama ni kama vile Simba. Kigezo
kingine ni lugha ambayo ni lugha ya kishairi.
Ghani masimulizi: hizi ni ghani ambazo
hutambwa ili kusimulia hadithi, historia au tukio fulani. Vigezo vilivyotumika
kugawa kipera hiki ni pamoja na kigezo cha lugha, lugha inayotumika katika kijipera
hiki ni lugha ya kishairi na fani iliyotumika ni kusimulia hadithi/tukio kwa
kirefu. Vile vile kuna kigezo cha namna ya uwasilishaji huambatana na ala za
muziki mfano zeze na marimba.
Ghani masimulizi ina vipera vinne
ambavyo ni rara, ngano, sifo na tendi.
Rara ni hadithi fupi nyepesi ya
kishairi yenye visa vya kusisimua, vigezo vilivyotumika katika kugawa kipera
hiki ni pamoja na lugha inayotumika, lugha inayotumika katika kipera hiki ni
lugha ya kishairi, fani iliyotumika ni fani ya kihadithi ambayo ni hadithi fupi,
nyepesi na inavisa vya kusisimua na kigezo kingine ni muktadha wa uwasilishaji
ambapo huimbwa au kughanwa ikiambatana na ala za muziki.
Ngano; hizi ni hadithi za mapokeo
zitumiazo wahusika kama wanyama, miti na watu katika kuelezea au kuonya kuhusu
maisha. Katika kipera hiki kigezo kilichotumika ni muktadha wa uwasilishaji,
kwamba huwasilishwa pamoja na ala ya muziki. Ngano huwa ghani masimulizi
inapowasilishwa pamoja na ala ya muziki.
Sifo; hizi ni tungo za kusifu, kigezo
kilichotumika ni muktadha wa uwasilishaji: sifo huwa ghani masimulizi
inapoingiza muziki katika utondozi wake, lugha iliyotumika ni lugha ya
kishairi.
Tendi; hizi ni ghani ndefu za
masimulizi juu ya matendo ya mashujaa yenye uzito kijamii au kitaifa. Vigezo
vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni fani ambayo ni huhusu matukio muhimu
ya kihisitoria au ya kijamii. Kigezo kingine ni muktadha wa uwasilishaji,
hutungwa na kuwasilishwa papo kwa papo.
Utanzu mwingine wa Fasihi Simulizi ni
utanzu wa mazungumzo. Mazungumzo ni maongozi au maelezo ya mdomo katika lugha
ya kawaida juu ya jambo lolote lile. Si kila mazungumzo ni fasihi ili
mazungumzo yaitwe fasihi lazima yawe na usanii wa aina fulani. Vigezo
vilivyotumika katika kugawa utanzu huu ni kigezo cha lugha ambapo lugha
iliyotumika ni lugha ya kifasihi. Kigezo kingine ni kigezo cha kimuundo ambapo
muundo wake huwa wa kidayalojia.
Utanzu huu wa mazungumzo una vipera
vifuatavyo ambavyo ni hotuba, malumbano ya watani, soga, mawaidha na ulumbi.
Hotuba; haya ni mazungumzo ambayo
huwasilishwa kwenye vikao rasmi vya kimila, kisiasa au kidini. Vigezo
vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha lugha ambapo lugha yake
huwa rasmi, sanifu na ya kisanaa. Kigezo kingine ni kigezo cha kimuktadha
ambapo hotuba huwasilishwa katika mazingira maalumu kwa mfano katika vikao
rasmi au mikutano.
Malumbano ya watani; haya ni mazungumzo
yanayozingatia masharti yanayotawala uhusiano wao wa kiutani. Huweza kuwa utani
wa kikabila, utani wa mababu au mabibi na wajukuu. Vigezo vilivyotumika katika
ugawaji wa kipera hiki ni kigezo cha lugha ambapo lugha huwa ni ya kimafumbo.
Kigezo kingine ni kigezo cha wahusika ambapo wahusika huwa na uhusiano wa
karibu.
Soga; haya ni mazungumzo ya kupitisha
wakati ili kusubiri kitu fulani. Vigezo vilivyotumika katika kugawa kipera hiki
ni kigezo cha kidhima ambapo dhima yake ni kupitisha wakati. Kigezo kingine ni
kigezo cha lugha ambapo lugha inayotumika siyo rasmi. Vilele kuna kigezo cha
muktadha ambapo muktadha wake huwa ni mahali popote.
Mawaidha; haya ni maneno ya maonyo au
mafunzo aghalabu huwa ya kidini na yenye muongozo. Kigezo kilichotumika katika kugawa
kipera hiki ni kigezo cha kidhima ambapo dhima yake ni kuonya au kutoa muongozo.
Ulumbi; huu ni uhodari wa kuzungumza
ambao huwa ni wa kiufasaha na madoido. Vigezo vilivyotumika katika kugawa
kipera hiki ni kigezo cha kifani ambapo lugha iliyotumika ni lugha ya kimadoido
na kifasaha.
Utanzu mwingine katika Fasihi Simulizi
ni utanzu wa maigizo. Maigizo ni michezo ambayo hutumia watendaji wa kuiga
tabia na matendo ya watu au viumbe wengine ili kuburudisha na kutoa ujumbe
fulani kwa hadhira. Vigezo vilivyotumika katika kutenga utanzu huu ni kigezo
cha namna ya uwasilishaji ambapo huwasilishwa kwa kuiga matendo ya watu au
wanyama. Kigezo cha kidhima ambapo dhima yake ni kuburudisha, kuelimisha au
kuonya. Pia kimetumika kigezo cha mandhari ambapo maigizo huambatana na matukio
maalumu kama vile kwenye maadhimisho ya sherehe fulani na katika matukio ya
kijamii.
Utanzu mwingine wa Fasihi Simulizi ni
utanzu wa ngomezi. Ngomezi ni ile hali ya kupeleka ujumbe kwa kutumia mdundo wa
ngoma. Vigezo vilivyotumika katika utanzu huu ni kigezo cha kifaa cha
uwasilishaji ambacho ni ngoma. Pia kigezo kingine ni kigezo cha kidhima ambapo
dhima yake ni kupeleka taarifa fulani kwa jamii. Mfano taarifa hiyo yaweza kuwa
ya msiba, mkutano na kadhalika.
Pamoja na ugawaji huu wa tanzu na
vipera vya Fasihi Simulizi uliofanywa na Mulokozi kwa kuzingatia vigezo vyake
alivyovitumia, bado ugawaji huu unaudhaifu mkubwa tu. Udhaifu au changamoto za
vigezo alivyovitumia Mulokozi ni kama ifuatavyo:-
Vigezo vyote hivi vinaweza kuingiliana;
mfano kigezo cha kidhima, kama vile kuonya au kuelimisha huweza kuonekana katika
tanzu zaidi ya moja au hata katika vipera mbalimbali.
Pia kigezo cha namna ya uwasilishaji
huweza kuingiliana kutoka utanzu mmoja hadi mwingine. Mfano, katika utanzu wa
masimulizi na mazungumzo.
Vilevile kigezo cha wahusika; kigezo
hiki huweza kuingiliana katika utanzu mmoja na mwingine. Mfano, unaweza kuwa na
hadithi yenye wanyama, binadamu, mizimu na kadhalika. Hivyo inakuwa si jambo
rahisi kuona tofauti zilizopo.
Kwa kuhitimisha, tunaweza kusema kwamba
ni vigumu kuainisha tanzu na vipera vya Fasihi Simulizi kutokana na kwamba,
Fasihi Simulizi hubadilika badilika kifani, kimaumbo na hata kimaudhui kwa
kutegemea muktadha na namna ya uwasilishaji wake. Kwa mfano ngano iliyopo
katika masimulizi ni tofauti na ngano iliyopo katika maghani. Hivyo basi tatizo
hili linaweza kutatuliwa kwa kutumia istilahi tofauti katika vipera au tanzu
zinazoingiliana.
MAREJEO:
Mulokozi, M. M. (1989). Tanzu za Fasihi Simulizi: Katika Mulika
21. TUKI. Dar es Salaam.
Mulokozi, M.M. (1996). Utangulizi wa Fasihi Simulizi ya Kiswahili.
TUKI. Dar es Salaam.
Wamitila, K.W. (2003). Kamusi ya Fasihi, Istilahi na Nadharia.
Focus Publications Ltd. Nairobi.
TUKI, (2004). Kamusi ya Kiswahili Sanifu. (Toleo la Pili). East Africa: Oxford
University Press na
Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI).
Nzuri
ReplyDeleteNmependa
ReplyDeleteKazi njema....
ReplyDelete