Friday, 20 September 2013

USHAIRI



DHANA  NA DHIMA  YA USHAIRI WA KISWAHILI
Kwa mujibu Mulokozi (1996) anasema, wataalamu wengi wamekubaliana kuwa asili ya ushairi wa Kiswahili ni tungo simulizi, hasa ngoma na nyimbo zinazofungamana na ngoma.
Kabla ya karne ya 10 BK ushairi wa Kiswahili ulikuwa ukitungwa na kughanwa  kwa ghibu bila kuandikwa.  Wataalamu hao waliojadili historia ya ushairi ni kama (Chiraghdin 1971: 7:10, Massir 1977:1 Ohly 1985:467).
Dhana ya ushairi imejadiliwa kwa kuangalia makundi mawili ya waandishi wa mashairi ya Kiswahili, makundi hayo ni kundi la wanamapokeo, na kundi la wanausasa.
Tukianza na kundi la wanamapokeo.  Wataalamu mbalimbali wamejadili dhana ya ushairi kama ifuatavyo:

Kwa mujibu wa Shaaban Robert anasema (1968) kuwa Ushairi ni Sanaa ya vina  inavyopambanuliwa,  kama nyimbo, mashairi na tenzi  zaidi ya kuwa sanaa ya vina, ushairi una ufasaha wa maneno machache  au muhtasari, uliza  swali wimbo, shairi na tenzi ni nini?  Wimbo ni shairi dogo na shairi ni wimbo mkubwa na utenzi ni upeo wa ushairi pia anauliza kina na ufasaha huweza kuwa nini?  Anasema  kina ni mlingano wa sauti za herufi, na kwa maneno mengine huitwa mizani ya sauti, na ufasaha ni uzuri wa lugha, mawazo, maono na fikra za ndani  zinapoelezwa kwa muhtasari wa ushairi huvuta moyo kwa namna ya ajabu.  Hivyo  katika ufafanuzi wake wa ushairi inaonesha dhahiri kuwa Shaaban Robert anagusia vipengele viwili maalumu yaani fani ya ushairi na maudhui ya ushairi.
Kwa mujibu wa Mnyampala (1970) kama alivyonukuliwa na Massamba D.P.B. katika  Makala ya Semina ya Kimataifa  ya waandishi wa Kiswahili (2003) anasema ushairi ni msingi wa maneno ya hekima tangu kale.  Ndicho kitu kilicho bora sana katika maongezi ya dunia kwa kutumia maneno ya mkato na lugha nzito yenye kunata iliyopangwa kwa urari wa mizani na vina maalumu kwa shairi.
Hapo tunaona dhahiri kuwa Mnyampala anauona ushairi ukiwa umejengwa na vitu viwili mahususi, ambavyo ni maneno ya hekima na sanaa yenyewe.  Tena Mnyampala katika dibaji hiyo hiyo anasisitiza juu ya sanaa ya ushairi kwa kusema:
(i)       Shairi liwe na “poetical Swahili”  yaani Kiswahili kinachohusu mwendo wa mashairi bora.   
(ii)        Shairi liwe na urari wa mizani kamili zinazohusika na ushairi wa kawaida waka lugha yaKiswahili kisichokuwa na kashfa au matusi  ndani yake.
(iii)   Shairi liwe  na vina vinavyopatana hususani mwishoni mwa kila ubeti kwa shairi lolote zima ingawa vina vya katikati vikosane kwa utenzi wake.
(iv)    Shairi lazima liwe na muwala
(v)       Lisizidi mno maneno ya kurudia rudia.
Kwa mujibu wa Abdilatifu Abdalla (1973) katika makala ya semina  ya kimataifa ya waandishi wa Kiswahili anasema maana ya ushari ni utungo ufaao kupewa jina  la ushairi ni utungo wowote tu bali ni utungo ambao katika kila ubeti wake kuna ulinganifu wa vina vitukufu vilivyopangwa kimoja baada  ya chenziye,  wenye vipande vilivyoona ulinganifu wa mizani zisizo pungufu wala kuzidi na vipande hivyo viwe vimetandwa na maneno ya mkato maalumu  na yenye lugha nyofu, tamu na laini, lugha ambayo ni telezi kwa ulimi wa kutamka, lugha ambayo ina uzito wa kifikra, tamu kwa mdomo wa kuisema, tambuzi kwa masikio ya kuisikia, na yenye kuathiri moyo uliokusudiwa na kama ilivyokusudiwa.
Kutokana na hayo yaliyokwishasemwa, tunaona kuwa dhana ya ushairi ya wana jadi imefinywa kwenye umbo maalumu lenye utaratibu wa vina na urari wa mizani ambayo kwa kweli ni dhana ya kimaandishi.
Kundi la pili ambalo limefafanua dhana ya ushairi   ni kundi la wanausasa.  Hawa wamejadili dhana ya ushairi kama ifuatavyo:
Kwa mujibu wa Wamitila, K.W. (2010) anasema ushairi ni sanaa inayotambulishwa na mpangilio maalumu wa sentensi au vifungu, mpangilio ambao una mdundo maalumu  au ruwaza fulani inayounda wizani, lugha ya mkato na mafumbo pamoja na mpangilio usio wa kawaida wa vifungu fulani.
Mulokozi, (1989) anasema ushairi ni sanaa ya lugha inayoonesha au kueleza jambo, wazo  au tukio kwa namna inayovuta hisia kutokana na mpangilio  maalum wa maneno yaliyoteuliwa, kauli za mkato, picha na tamathali  na inayowasilishwa kwa hadhira kwa njia ya nyimbo au maandishi.  Kwa mujibu wa ufafanuzi huo ushairi hueleza tu, bali hudhihirisha, au huonyesha kusawiri,  anaendelea kusema ushairi huwajumuisha watu wawili au zaidi.  Kihisia katika tukio linalowagusa wote,  ukawatosa katika dimbwi la uchungu, au furaha, hasira au ridhaa, na kuwatoa tena wakiwa wameburudika na kuelimika.   
Kwa sababu hii ushairi  ndiyo sanaa ya fasihi inayokaribiana  zaidi na muziki na  mara nyingi sanaa hizi mbili hufungamana.           
Mulokozi na Kahigi (1979) wanamnukuu Kezilahabi kwa kusema kuwa ushairi ni tukio, hali au wazo ambalo limeonyeshwa kwetu kutokana na upangaji mzuri wa maneno  fasaha yenye mizani kwa ufupi ili kuonyesha ukweli fulani wa maisha  jambo ambalo halikutiliwa maanani katika fafanuzi la wataalamu hawa ni dhima ya fasihi na ushairi kama vyombo vya kuburudisha na kustarehesha watu.          
Wataalamu hawa wanaendelea kusema kuwa ushairi lazima uguse hisi, lazima umsisimue yule anayeusema, kusoma au kuimba na  yule ausikilizaye.  Hivyo shairi lisilogusa hisi ni  kavu na butu hata  kama limetafsiriwa katika vina na urari wa midhani, shairi hilo litaishia kuhubiri tu.           
Kwa ujumla wanausasa wanadai kuwa ushairi  ni sanaa inayopambanuliwa kwa mpangilio maalumu wa maneno fasaha  na yenye muwala, kwa  lugha   ya mkato, picha au stiari  au ishara.  Katika usemi, maandishi, au mahadhi ya wimbi ili kueleza wazo au mawazo, kujifunza au kueleza tukio au hisi fulani.  Kuhusu maisha au mazingira ya binadamu kwa njia inayogusa moyo.      
Kutokana na mawazo hayo ya washairi mbalimbali wa kimapokeo na wana usasa wote wameonesha  mambo fulani ambayo yamefanana kwa  namna moja ua nyingine.          
Wote wanakubaliana kwamba katika ushairi fani na maudhui ni vitu vya muhimu kabisa na kwamba kila kimoja  kati ya vitu hivyo kina wajibu maalumu.           
Pia washairi wengi huamini kwamba lugha ya ushairi lazima iwe ya mkato, yaani iweze kusema mambo mengi kwa kutumia maneno  machache.           
Kwa ujumla tunaweza kusema kuwa ushairi ni  sanaa ya lugha yenye ughunaji na yosawiri, kueneza au kuonesha jambo lenye  hisi au hali fulani kwa namna  ya kuvutia hisia katika mpangilio  mahususi wenye urari wa vizani na sauti           
Baada ya kuangalia  wataalamu mbalimbali walioelezea dhana ya ushairi, zifuatazo ni dhima za ushairi wa Kiswahili.           
Ushairi husaidia kurithisha  maarifa kwa jamii, kupitia ushairi jamii inaweza kujifunza mambo mbalimbali kama vile namna ya kuepukana na magonjwa, umuhimu wa kutunza mazingira.                                                                                                           
Mfano:  shairi la Binti katika diwani ya dhifa iliyoandikwa na Kezilahabi e, Mwandishi anarithisha jamii maarifa kwa kusisitiza jamii izingatie umuhimu wa elimu: anasema
                        Soma soma kwa kujiamini.
                        Elimu ni kikata kiu,
                        Huondoa pia ukungu,
                        Pasipo njia pakawa
                        Fanya kazi utayopata,
                        Kazi ni kinga ya  heba
                        Sasa umekuwa na uwe,
                        Huu usinga na kupa
                        Na unyoya nakuchomekea nyweleni.          
Ushairi husaidia kuhamasisha jamii, ushairi hutumiwa kama njia ya kuwahamasisha wanajamii katika shughuli mbalimbali. 
Mfano: katika utendi wa Fumo Loyongo ubeti wa kumi na tatu, anahamasisha wanajamii kuwa na nguvu kama simba, anasema:
                        “Ni mwanaume Swahili
                        Kama simba unazihi
                        Usiku na asubuhi
                        Kutembea ni mamoya.
Pia katika diwani ya Wasakatonge, shairi la Wanawake wa Afrika, mwandishi anawahamasisha wanawake kujikomboa, anasema:
                        Wanawake wa Afrika
                        Wakati wenu umefika,
                        Ungeneni
                        Shikaneni
                        Mjitoe utumwani,
                        Nguvu moja!           

Ushairi husaidia kudumisha na kuendeleza utamaduni katika jamii, kupitia ushairi wanajamii wanadumisha na kuendeleza utamaduni wao na  kwa njia hii  huhakikisha kuwa unabaki hai.
Mfano katika  tohara huwa kunakuwa na nyimbo zenye mafunzo kwa vijana wanaofanyiwa jando na unyago, kama vile kuandaa wanaohusika kwa majukumu ya utu uzima. Mfano katika jamii ya Waswahili wa Unguja na Pemba.
                        “Mwanangu ambaduni liono,
                        Ndoo urume,
                        Kisu kikali, kiski kibutu
                        Mrume  mwana hujikaza mrume. 
Ushairi huburudisha  hadhira, ushairi ni nyenzo kuu ya burudani, katika jamii licha ya majukumu mengine ya nyimbo, msingi mkuu ni uwezo wake wa kuweza  kuathiri hisia za wasikilizaji au washiriki wake na kuwaburudisha. Mfano katika shairi la watoto wawili kutoka kwa mwandishi Kezilahabi Kichomi (1974 uk. 62):
            Mtoto wa tajiri akilia  hupewa mkate,
            Mtoto wa tajiri akilia hupewa picha ya kuchezea,
            Akilia mtoto wa tajiri huletewa kigari akapanda,
            Akiendelea kulia hupanda mgongo wa yaya,
            Akikataa kunyamaza ulimwengu mzima hulaumiwa. 
Ushairi husaidia kukuza lugha kwa kawaida ushairi hutungwa kwa lugha nzito yenye ishara  na jazada zinazoeleweka na wanajamii wanaohusika, na kwa njia hii  hutusaidia kukuza hisia za kujitambua kwao kama watu wa kundi fulani lenye mtazamo, imani na mwelekeo fulani.           
Hivyo kwa kuhitimisha tunaweza kusema kwamba aidha ushairi uwe wa kimapokeo au  wa kisasa unaonesha mambo muhimu yanayoilenga jamii husika.  Mfano katika mambo ya kidini, kisiana na kiutamaduni.                                                                                                             
           
MAREJEO
Abdilatifu, a (1973), Sauti ya Dhiki, Oxford London.
Kezilahabi, E (1974), Kichomi, Heinemann; London.
Massamba, D.P.B. (2003), Utunzi wa Ushairi wa Kiswahili katika makala za Semina ya Kimataifa ya Waandishi wa Kiswahili (III).  Fasihi.  Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili. Dar es Salaam. 
Mulokozi, M.M na Kahigi K.K. (1979), Kunga za Ushairi na Diwani Yetu, TPH, Dar es Salaam.
Mulokozi, M.M. (1989) Uchambuzi wa Mashairi:  Mulika Namba 21; TUKI, Dar es Salaam.
Mulokozi, M.M. (1996), Fasihi ya Kiswahili, chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Dar es Salaam.
Robert, S (1968) Kielelezo cha Insha.  Nelson London.
TUKI, (2003), Makala za Semina ya  Kimataifa ya Waandishi wa Kiswahili III : Utunzi wa Ushairi wa Kiswahili, TUKI Dar es Salaam.
Wamitila, K.W.  (2010) Kichoche cha Fasihi Simulizi na Andishi, English Press.  Nairobi.

No comments:

Post a Comment