UCHOMOZAJI WA KAMUSI ZA AWALI KATIKA BARA LA ULAYA NA MAENDELEO YALIYOFIKIWA KATIKA KARNE HII
(Eric Ndumbaro)
1.0 IKISIRI
Katika jamii yoyote ile ulimwenguni dhana ya maendeleo haiji kama mvua, bali huanza hatua kwa hatua. Hali kadhalika hatua hizo hujibainisha katika historia kwa kupitia vipindi mbalimbali jamii tangu jamii ilipoanza kujikongoja katika masuala mbalimbali mpaka hivi sana na hata kubashiri mwelekeo wa jamii katika nyakati zijazo. Hivi ndivyo hata taaluma ya leksikografia ilivyoanza na hatimaye uchomozaji wa kamusi za awali katika bara la Ulaya mpaka kufikia maendele tuliyonayo katika karne hii.
2.0 UTANGULIZI
Makala hii imekusudia kujadili uchomozaji wa kamusi za awali katika bara la Ulaya na maendeleo yaliyofikiwa katika karne hii. Awali ya yote tutaanza kufasili dhana muhimu zilizojitokeza katika mjadala huu kama vile: dhana ya uchomozaji na dhana ya kamusi, kisha tutaangalia historia ya kamusi katika bara la Ulaya halafu maendeleo yaliyofikiwa katika karne hii na mwisho tutahitimisha kwa muhtasari juu ya yale tuliyojadili.
2.1 Maana ya dhana ya Uchomojazi
Neno uchomozaji linatokana na kitenzi chomoza. Kwa mujibu wa Mdee na wenzake (2011) chomoza maana yake ni tokeza juu na kuonekana. Hivyo, katika muktadha wa kilekiskografia tunaweza kuifafanua dhana hii ya “uchomozaji wa kamusi” kama utokeaji wa kamusi au namna kamusi zilivyoonza katika bara la Ulaya.
2.2 Maana ya dhana ya Kamusi
Mdee, (2006) kama alivyomnukuu Zgusta, (1971) kamusi ni kitabu cha marejeo chenye msamiati uliokusanywa kutoka kwa wazungumzaji wa jamii fulani, na kupangwa kwa utaratibu maalum, kisha kufafanuliwa kwa namna ambayo msomaji aweze kuelewa.
Aidha TUKI, (2004) wanaeleza kuwa, kamusi ni kitabu cha maneno yaliyopangwa kwa utaratibu wa alfabeti na kutolewa maana na maelezo mengine. Fasili hizi zina udhaifu kwani kamusi ya sasa sio kitabu tu, inaweza kuwa katika mfumo wa kielektroniki kama vile CD na nakala laini yaani software.
Hivyo basi, kutokana na fasili hizo tunaweza kusema kwamba, kamusi ni orodha ya msamiati wa lugha uliopangwa kwa utaratibu maalum wa ki-alfabeti na kutolewa maana kwa maelezo ya kina na ya msingi, kisha kuhifadhiwa kwa njia ya ama kitabu au kielektroniki.
3.0 HISTORIA YA KAMUSI KATIKA BARA ULAYA
Ili tuweze kuelewa vizuri uchomozaji wa kamusi za awali katika bara la Ulaya na maendeleo yaliyofikiwa katika karne hii hatuna budi kuangali kwa ufupi historia ya kamusi katika bara la Ulaya. Katika karne ya saba na ya nane kama inavyoelezewa na Hans Sauer, mchakato huu ulianza kwa faharasa za Kiingereza zilizokuwa na maneno magumu ya lugha ya Kilatini, kwani ikumbukwe kwamba, Kilatini ndio lugha iliyotumika kutolea elimu katika bara lote la Ulaya na dunia kwa ujumla.
Faharasa hizi zilikuwa za aina tatu; aina ya kwanza ni zile faharasa zilizokusanywa bila kuzingatia mpangilio wa ki-alfabeti kwa Kilatini zilijulikana kama "glossae collectae" yaani faharasa mkusanyiko. Aina ya pili ni zile zilizopangwa ki-alfabeti ambazo zilijulikana kama faharasa za ki-alfabeti na aina ya tatu ni zile zilizokusanywa kulingana na mielekeo ya ki-semantiki ambazo nazo zilijulikana kama faharasa za ki-kategoria.
Hivyo, faharasa hizi za kwanza zilichukua maneno magumu ya Kilatini kutoka katika magazeti, vitabu na machapisho mbalimbali na kuyawekea visawe katika lugha ya Kiingereza, kisha kuyatolea maelezo kwa Kiingereza ili watu waweze kujua maarifa yaliyoandikwa katika lugha ya Kilatini. Kazi hii ilifanywa na wasomi hasa watawa. Pia bado ikumbukwe kwamba wakati huo lugha ya kimataifa ilikuwa Kilatini na ndio ilikuwa lugha pekee ya kutolea maarifa ya elimu.
Mdee (2010) anaeleza kwamba, faharasa ya kwanza ya Kiingereza iliandikwa mwaka 725. Iliandikwa katika lugha ya Kilatini-Kiingereza na nakala zake zimehifadhiwa huko Ujerumani, Ufaransa Mashariki na Chuo Kikuu cha Uingereza. Faharasa hii ya kwanza ilikuwa na vitomeo zaidi ya 2000 zilivyopangwa kwa utaratibu wa alfabeti wa herufi za mwanzo (Stain 1985)
Hivyo tunaweza kuona kwamba, utokezaji wa faharasa katika bara la Ulaya ulichochewa na kuhamasishwa kwa kiasi kikubwa na hitaji la jamii hasa watawa, kama anavyosema Hausmann (1989:1ff) kwamba, tangu milenia ya pili kabla ya Kristo, hamasa na ushawishi mkubwa wa watawa ulichochea maendeleo ya taaluma ya leksikografia. Enzi za kati huko Ulaya dini ilikuwa ndio taasisi muhimu iliyochochea maendeleo ya leksikografia. Hivyo faharasa na kamusi zilihitajika sana katika kufundishia na kuwaongoza mapadre na waumini kwa ujumla ili wafahamu vizuri lugha ya ki-Biblia.
Baadaye katika karne ya 15 faharasa zilizokusanywa kutoka vitabu mbalimbali ziliwekwa pamoja na kuhaririwa vizuri na kuchapishwa kama kamusi ya maneno magumu. Mfano wa kamusi hiyo ni Promptorium Parvulorum kamusi ya Kilatini-Kiingereza ya mwaka 1440 ambayo ilichapwa (1499) akiwa na vitomeo 10,000 ambavyo ni maneno magumu yasiyofahamika. Hanks P. (__) katika makala yake anaeleza kuwa, vitomeo vyake vilikuwa ni maneno na vishazi vilivyopangwa kialfabeti kufuata kategoria, yaani nomino peke yake na vitenzi peke yake. Kazi hii iliunganishwa na Galfridus Anglicus mtawa wa shirika la Wadominikani huko Norfolk.
Mwaka 1553 walitengeneza kamusi iliyoitwa Shorte Dictionarie for Yonge Begyners ambayo ilikusanya maneno ya kundi moja (kikoa leksimu) yaani kundi moja la maneno yanayofanana yalikaa pamoja. Kamusi hizi za zamani zilikuwa kamusi za lugha mbili yaani kamusi thaniya. Unaweza kujiuliza kwa nini zilianza kamusi thaniya?
Zilianza kamusi thaniya kutokana na sababu tatu za msingi. Sababu ya kwanza ni kuongeza umilisi na kukuza umahiri wa lugha ili kuweza kuelewa matini zilizoandikwa kwa Kilatini kama vile Biblia na fasihi kongwe. Kwa mfano The store House of Word for Children and Clerics (watumishi wa kanisa), Ortus Vocabularum (Garden of Words (1500) Kilatini-Kiingereza. Vilevile Estienne alitunga kamusi ya Kifansa-Kilatini mwaka 1539 kwa lengo la kuwasaidia Wafaransa kuandika Kilatini fasaha.
Sababu ya pili ilikuwa ni haja ya mawasiliano, ili kuweza kufanya shughuli mbalimbali kama vile: kufanya biashara na wasafiri kutoka nchi mbalimbali. Hapo zilitungwa kamusi mbalimbali, kwa mfano kamusi ya Kikroati na lugha za Kiserbia, Kialbania, Kituruki na Kiitaliano.
Sababu ya tatu ilikuwa ni kupata maarifa/elimu iliyokuwa inahodhiwa na wazungumzaji wa lugha ngeni. Miongoni mwa kamusi thaniya za Kichina zilizotungwa kwa lengo hili ni: kamusi za taaluma mbalimbali kwa mfano, kamusi za kemia (1870), tiba (1887) na vipimo vya uzito (1890) kwa kuzitaja chache.
Mpaka karne ya 17 kamusi za kutenga maneno magumu zilifikia ukomo na baada ya hapo kamusi zilianza kuwa na sura mpya, sio tena chombo cha kuhifadhi maneno magumu pekee bali zilikuwa chombo cha kuhifadhi lugha. Hivyo kamusi zilizofuata zilianza kuingiza maneno magumu na maneno ya kawaida.
4.0 MAENDELEO YALIYOFIKIWA KATIKA KARNE HII.
Maendeleo yaliyofikiwa katika karne hii Mdee (Kashatajwa) anasema kuwa, yametokana na Samwel Johnson ambaye ndiye anaaminiwa kuwa aliipa kamusi ya Kiingereza umbo na maudhui kama ilivyo sasa au katika karne hii.
Jonson katika kamusi yake, Dictionary of the English Language aliangalia kamusi za waliotangulia na kuongeza mchango wake katika taaluma ya utungaji kamusi. Malengo yake yalikuwa ni: kuhifadhi maana za maneno ya Kiingereza, kusanifisha Kiingereza kwa: kuonesha matumizi sahihi na kuelekeza matumizi sahihi ya lugha.
Maendeleo yaliyofikiwa katika karne hii yanajibainisha katika kamusi za siku hizi kupitia vipengele mbalimbali kama vile: dhamira/malengo ya kamusi, muundo au miindo ya kamusi, mitindo mbalimbali, vitomeo, lugha kienzo inayotumika, nk.
Umbo au muundo, kamusi za karne hii zinajitokeza katika umbile la kielekroniki. Hii inatokana na maendeleo na jamii hasa katika nyanja ya sayansi na teknolojia. Kwa mfano siku hizi tuna kamusi za kwenye simu za mkononi, kamusi za mkondoni pia tunaweza kuhifadhi hata katika CD na Kompyuta.
Malengo, kutokana na maendeleo yaliyofikiwa katika karne hii hatuwezi kuwa na kamusi moja inayojitosheleza. Hii ni kutokana na kwamba, malengo ya kamusi siku hizi sio kukusanya maneno magumu na kuyatolea maana bali kufafanua juu ya maneno magumu na ya kawaida. Ndio maana siku hizi zinatungwa kamusi za kila nyanja kulingana na malengo tofauti.
Pia zamani lengo kuu lilikuwa ni mawasiliano tu, hivyo walikuwa wanachukua maneno na kuyatolea maana tu bila kuyaweka katika kategoria wala kuweka taarifa zingine za msingi kama ilivyo katika kamusi za siku hizi.
Vitomeo, kamusi za karne hii zinavitomeo vingi zaidi ukilinganisha na kamusi za awali. Pamoja na wingi huo wa vitomeo pia ni ndogo hata kwa mwonekano, hivyo ni rahisi sana kuchukulika. Kwa mfano Kamusi ya Kiingereza-Kiiswahili; Toleo la pili inavitomeo 50,000 lakini Ortus Vocabularium ilikuwa na vitomeo 1500.
Lugha kienzo, kamusi nyingi za karne hii lugha kienzo inayotumika husaidia kukifanya kidahizo kieleweke kwa urahisi zaidi. Hutoa maelezo ya kidahizo kwa ufupi kwa kuonesha etimolojia ya neno hilo, kategoria ya neno, na uelekezi wa neno. Kwa mfano, kama neno lina asili ya Kiarabu kifupisho >Kar hutumika, kama neno ni nomino kifupisho “nm” hutumika na kama kitenzi ni elekezi kifupisho [ele] hutumika.
Pia huweka usanaa katika kamusi, na hivyo kumfanya mtumiaji wa kamusi asichoke kutumia kamusi hiyo, yaani lugha kienzo humvutia msomaji kwa alama mbalimbali michoro, picha na vifupisho vilivyotumika.
5.0 HITIMISHO
Hata hivyo pamoja na maendeleo yaliyofikiwa katika taaluma ya lekiskografia katika karne hii bado tunaona uhitaji mkubwa wa kamusi katika sekta mbalimbali. Hii inatokana na maendeleo ya kijamii kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni ambayo yanachochea kuibuka kwa misamiati mipya kila kukicha. Hii inamaana kwamba kamusi ni kitabu kinachoishi na kisichopitwa na wakati.
MAREJEO
Geeraerts, D. (1989), Principles of monolingual dictionaries, In Hausmann et al. (Eds.),
Hanks P. ( ___) Lexicography, Printing Technology, and the Spread of Renaissance Culture. Institute of Formal and Applied Linguistics, Charles University in Prague
Mdee, J.S (2011), Nadharia na Historia ya Leksikografia, Dar es Salaam: TUKI
Mdee, J.S. (1997), Nadharia na Historia ya leksikografia, TUKI , Dar es salaam.
Sterkenburg, P. G. J. van (___) A Practical Guide to Lexicography, John Benjamins Publishing Co. ·P.O. Box 36224 · 1020 ME Amsterdam · The Netherlands
TUKI (2004), Kamusi ya Kiswahili sanifu, Oxford university press, Nairobi.
No comments:
Post a Comment