Monday, 14 December 2015

SAIKLOPEDIA NA KAMUSI


TOFAUTI BAINA YA SAIKLOPEDIA NA KAMUSI
Kamusi na Saiklopidia ni dhana mbili zenye mkanganyiko mkubwa hasa katika suala zima la maana na matumizi. Aidha wataalam mbalimbali wametoa fasili ya dhana hizi ili kuweka bayana tofauti zilizopo baina ya Saiklopidia na Kamusi.
Kwa mujibu wa The Concise Oxford Dictionary of Current English, Saiklopidia ni kitabu kilichopangwa kialfabeti ambacho aghalabu hutoa taarifa juu ya masomo mbalimbali, au vipengele mbalimbali vya somo au mada moja. (Tafsiri yangu)
Pia Kamusi ya Kiingereza-Kiswahili (2000) inafafanua kwamba, ensaiklopidia ni kitabu au seti ya vitabu vinavyotoa taarifa kuhusu mambo mengi.
Vilevile Mdee (2010) anasema saiklopidia ni kitabu chenye mkusanyiko wa makala zinazohusu nyanja anuwai za elimu ambazo hupangwa kialfabeti na kuandikwa maelezo ya kina kwa muhtasari.
Mdee (Kashatajwa) akimnukuu Zgusta (1971) kamusi ni kitabu cha marejeo chenye msamiati uliokusanywa kutoka kwa wazungumzaji wa jamii fulani, na kupangwa kwa utaratibu maalumu, kisha kufafanuliwa kwa namna ambayo msomaji anaweza kuelewa.
Hivyo basi, tunaweza kusema saiklopidia ni kitabu chenye mkusanyiko wa taarifa mbalimbali kuhusu mada au masomo mbalimbali yaliyofafanuwa kwa kina zaidi. Kwa mfano, Encyclopedia Britannica A Dictionary of Arts, Sciences, Literature and General Information (1910)
Mbali na tofauti ya maana, pia tofauti nyingine inajitokeza katika malengo. Mdee (Kashatajwa) anasema, lengo la saiklopidia ni kutoa maelezo kuhusu vitu, watu, taasisi, fikra na dhana mbalimbali kwa madhumuni ya kuelimisha, wakati katika kamusi taarifa ni chache na za kina tu.
Vilevile kuna tofauti za kimtindo. Vitomeo katika saiklopidia huweza kuwa vya herufi moja tu, yaani ama herufi A au B au E au huweza kuwa vya herufi K-P wakati katika kamusi vitomeo huanzia herufi A mpaka Z. Mfano, Kamusi ya Kiingereza-Kiswahili Toleo la Pili.
Pia katika The New Encyclopedia Britannica (1968) hakuna taarifa za kiisimu kama ilivyo katika kamusi. Kwa mfano hakuna kategoria za maneno, mifano na hawaoneshi matumizi ya kitomeo.
Aidha kuna tofauti za kimpangilio baina ya vitomeo. Katika saiklopidia ukurasa mmoja hukaa kitomeo kimoja tu. Mfano katika The New Encyclopedia Britannica (Kimeshatajwa) kitomeo Egypt kimefafanuliwa kwa kurasa 64. Wakati katika kamusi kitomeo huwa na taarifa za msingi tu. Hivyo kwa kifupi tunaweza kusema katika saiklopidia hakuna uwekevu kama katika kamusi.
Vilevile lugha kienzo ya kamusi humwezesha msomaji kupata maana ya kileksika au kisarufi ya kitomeo, wakati katika saiklopidia ufafanuzi wa kitomeo hautoi taarifa za kileksika au kisarufi.
Hivyo basi, tunaweza kusema kuwa, kamusi na saiklopidia licha ya kwamba vyote vinatoa fasili ya dhana mbalimbali lakini ni vitabu viwili tofauti hasa katika kufafanua matumizi ya kitomeo, kimuundo, kimtindo na kimaana.
MAREJEO
______(1968). The New Encyclopedia Britannica Volume 18th
______(1995). The Concise Oxford Dictionary of Current English. Oxford University Press Inc.  New York.
______(1910) Encyclopedia Britannica; A Dictionary of Arts, Science, Literature & General Information. 17th Edition. The Encyclopedia Britannica Campany.
______(1968). The New Encyclopedia Britannica Volume 18th
Mdee, J.S (2011). Nadharia na Historia ya Leksikografia. Dar es Salaam: TUKI
TUKI (2001). Kamusi ya Kiswahili-Kiingereza. Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili.
                     Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment