Tuesday, 29 December 2015

Tasnifu



UFUNDISHAJI WA NADHARIA ZA UHAKIKI WA FASIHI YA KISWAHILI KATIKA TANZANIA
FURAHA J. MASATU
SHAHADA YA UZAMILI KATIKA FASIHI YA KISWAHILI
CHUO KIKUU CHA DODOMA
JUNI 2011
UFUNDISHAJI WA NADHARIA ZA UHAKIKI WA FASIHI YA KISWAHILI KATIKA TANZANIA
Furaha J. Masatu
Tasnifu Imekusanywa kwa Ajili ya Kutimiza Sehemu ya Matakwa ya Shahada ya Uzamili katika Fasihi ya Kiswahili ya Chuo Kikuu cha Dodoma.
Chuo Kikuu cha Dodoma
Juni 2011
Aliyesaini hapa chini anathibitisha kwamba ameisoma na anapendekeza tasnifu hii inayoitwa Ufundishaji wa Nadharia za Uhakiki wa Fasihi ya Kiswahili katika Tanzania ikubaliwe kwa minajili ya kutunukiwa Shahada ya Uzamili katika Fasihi ya Kiswahili ya Chuo Kikuu cha Dodoma.
………………………..
Dkt. Elias Manandi Songoyi
(MSIMAMIZI)
Tarehe: ……………………..
IKIRARI
NA
HAKIMILIKI
Mimi Furaha J. Masatu, ninathibitisha kwamba tasnifu hii ni kazi yangu asilia, na kwamba haijawahi kuwasilishwa na wala haitawasilishwa katika Chuo Kikuu kingine chochote kwa ajili ya kutunukiwa shahada yoyote.
Saini ………………
Hairuhusiwi kuzalisha, kunakili, wala kusambaza sehemu yoyote ya Tasnifu hii kwa namna yoyote ile bila kibali cha maandishi kutoka kwa mwandishi au Chuo Kikuu cha Dodoma.

SHUKRANI

Kathleen Daniel (1997) alipata kusema, “if there’s a key, there must be a door, and I intend to find it … (kama pana ufunguo/dhamira, ni lazima pana mlango, hivyo nimedhamiria kuutafuta …).”  Hoja hii imekuwa ni dira muhimu katika kila jambo jema ninalolikusudia maishani mwangu. Hakika MUNGU ni mkuu; nimeuona mkono wake ukitenda kazi maishani mwangu. Amenikinga na kuniongoza katika kila hatua niipitayo kila kuitwapo leo. Ninamshuru kipekee sana. Ninaamini, kama asingelikuwa Yeye, hakika nisingelifika hapa nilipo leo – kimwili, kitaaluma, na kiroho maana kwa msaada Wake, makuu yametendeka.
Ninamshukuru mlezi, mwalimu na msimamizi wangu Dkt. Elias Manandi Songoyi kwa juhudi zake zisizo kikomo katika kupitia na kutathmini kila jambo lililohusu tasnifu hii hadi ikaonekana kustahili kutunukiwa alama ya ndiyo, imepita. Ameifanya kazi hii kwa moyo wa utayari, umakini, subira, na weledi wa hali ya juu pasipo kukata tamaa wala kuchoka. Endapo andiko hili litaonekana kuwa na mapungufu, basi mapungufu hayo hayatokani na yeye, bali mimi mwenyewe. Aidha, ninawashukuru Profesa Joshua S. Madumulla, na Dkt. Rose Upor kwa kukubali kuwa msaada wangu mkubwa katika hatua za awali za uandishi wa pendekezo la utafiti wa andiko hili kabla sijapangiwa rasmi msimamizi.
Ninawashukuru Taasisi ya Elimu Tanzania, Uongozi, Walimu na Wanafunzi wa Kiswahili - Kidato cha Sita katika shule mlimofanyika utafiti huu. Shule hizi ni: Elly’s, Ikizu, na Mwembeni (shule iliyotumika kutathmini vifaa na mbinu za utafiti). Kujitolea kwao kidhati kuwa wajibu hojaji/ jaribio la utafiti katika kipindi chote cha utafiti, ndiko kulikozaa tasnifu hii.
Ninamshukuru mama yangu mzazi, Bibi. Anna J. Kidata kwa upendo wake wa dhati kwetu wanawe. Hakika, pasipo yeye, shahada hii ya uzamili nisingetunukiwa katika mwaka huu wa 2011 kwani ndiye aliyebeba gharama zote za hali na mali za masomo yangu pasipo kuchoka wala kuteteleka. Ni mwalimu, mnasihi, mjasiliamali, na mjane wa kuigwa katika uwekezaji kwenye eneo la maisha na elimu vya watoto.
Ninawashukuru pia kaka yangu Tumaini, dada zangu Sara, Asante, na Neema kwa kunipenda na kuchangia kwa namna moja ama nyingine katika masomo yangu. Aidha, ninawashukuru Mwalimu Sosthenes Luhende, Mwalimu Patrick Renatus, Felix Mallya, Paul Mwamwige, Alvin B. Lema, Paschal L. Berege, mjomba wangu Alphayo J. Kidata, dada Monalisa Jackson, na Shemeji yangu, Jane Kimaro kwa mchango wao hususani wa kiutu, kiufundi, na kisaikolojia vilivyonisaidia kuyamudu maisha katika kipindi chote cha masomo na utafiti.
Ninawashukuru Wakufunzi, na Wanafunzi wenzangu wa Shahada ya Uzamili katika Fasihi ya Kiswahili 2009/ 11, marafiki, ndugu, na jamaa kwa namna mbalimbali tulivyoshirikiana na kusaidiana bila kuchoka katika kipindi chote cha masomo. Ni dhahiri, kuenenda pamoja na wenye hekima, kunampa mtu hekima.
Ninahitimisha kwa kusema, mimi sina cha kuwalipa ila Mungu wangu ndiye mpaji; atawalipa na kuwafariji hata ukamilifu wa dahari, Amin.

TABARUKU

Ninaitabaruku tasnifu hii kwa mama yangu mzazi, Bibi Anna Kidata kwa kukubali, na kuniamini kiasi cha kuthubutu kuwekeza katika elimu yangu ya Shahada ya Uzamili.

Mama, sijaona kama wewe maishani mwangu!

IKISIRI

Andiko hili linahusu ufundishaji wa nadharia za uhakiki wa fasihi ya Kiswahili katika shule za sekondari nchini Tanzania. Lengo likiwa ni kubaini, kuchunguza, na kuelezea uhusiano uliopo kati ya ufundishaji wa nadharia za uhakiki wa fasihi ya Kiswahili na uwezo wa mwanafunzi kujitegemea kivitendo ndani na nje ya darasa pasipo kugeuza tahakiki “misahafu.”
Katika mtalaa huu, mtafiti alipitia maandiko mbalimbali ya kitaaluma, zikiwemo tafiti linganishwa tatu. Muundo wa utafiti ulikuwa ni wa muktadha halisi ukitumia njia za jaribio, hojaji, na uchunguzi kukusanya data kwa miezi mitatu mfululizo katika shule za sekondari Elly’s (shule dhibitiwa), na Ikizu (shule isiyodhibitiwa).
Jumla ya wajibu hojaji/ jaribio la utafiti 25 (wanafunzi 20, walimu wanne, na mtaalamu mmoja toka Taasisi ya Elimu Tanzania) walihusika. Uteuzi wa shule na wajibu hojaji/ jaribio la utafiti ulizingatia mwongozo wa D. Ary, na wenzake (2006). Nadharia zilizotumika katika jaribio la utafiti ni U - Marx, na Umbuji wa Kirusi. Njia kuu ya uchambuzi wa data ilikuwa ni uchambuzi fafanuzi wakati nadharia ya utafiti ilikuwa ni mafunzo linganishi.
Matokeo ya utafiti yanaonyesha kutokufundishwa ila kwa kugusiwa tu kwa nadharia za uhakiki, ilhali uhakiki ukifanyika pasipo kubainisha nadharia za uhakiki zinazoongoza uchambuzi husika. Pamoja na mada ya nadharia za uhakiki wa fasihi kutokufundishwa, wajibu hojaji/ jaribio la utafiti wengi kupitia hojaji wanaeleza kuwepo kwa uhusiano kati ya nadharia za uhakiki wa fasihi ya Kiswahili na uwezo wa mwanafunzi kujitegemea kivitendo katika majukumu kadha wa kadha anayopewa ndani na nje ya darasa.
Matokeo haya yanakinzana na yale ya jaribio ambayo yanaonyesha kutokuwapo kwa tofauti ya kimtazamo na kiutendaji kati ya mwanafunzi aliyesoma na ambaye hakusoma nadharia za uhakiki wa fasihi ya Kiswahili. Kwa msingi huu, inaelekea kwa sasa hakuna sababu za kuingiza nadharia za uhakiki katika muhtasari wa Kiswahili, sekondari. Jambo lililopingwa na walimu wajibu hojaji, na wakapendekeza kufanyika utafiti wa muda mrefu wa kimajaribio utakaoanzia kidato cha tatu.

ORODHA YA MAJEDWALI

Ukurasa
Jedwali 2: Bajeti  ………………………………………………………..……………... 143
Jedwali 3: Ratiba ya Utafiti ……………………………………………...…………........ 144

ORODHA YA MICHORO

Ukurasa
Mchoro 1: Muhtasari wa Mahusiano ya Nadharia na Nyuga ………………...……….. 96

SURA YA KWANZA

UTANGULIZI

1.0 Utangulizi

Sura hii ya kwanza, ni sura inayojipambanua kwa kutoa uga wa tatizo, tatizo la utafiti, malengo ya utafiti, maswali ya utafiti, umuhimu wa utafiti, nadharia ya utafiti, mipaka ya utafiti, na hitimisho. Sura hii ni msingi wa mjadala mzima unaohusu ufundishaji wa nadharia za uhakiki wa fasihi ya kiswahili katika shule za sekondari nchini. Sura hii ni dira ya kuongoza na kujenga mtiririko jumla wa mijadala mbalimbali inayojitokeza katika sura zinazofuata, yaani sura ya mapitio ya maandiko, sura ya mbinu na vifaa vya utafiti, sura ya uwasilishaji uchambuzi na mjadala kuhusu data, na sura ya mapendekezo na hitimisho la mijadala ya utafiti.

1. 1 Uga wa Tatizo

Kwa muda mrefu sasa, baadhi ya wadau wa fasihi ya Kiswahili wamekuwa wakionyesha wasiwasi juu ya namna mada ya nadharia za uhakiki wa fasihi inavyofundishwa. Dai lao kubwa ni kwamba, baadhi ya wanafunzi  na walimu wao hawaoni umuhimu wa kumwandaa mwanafunzi katika kufahamu kwa undani nadharia za uhakiki wa fasihi ili imjengee mwanafunzi uwezo wa kuzihakiki kazi za fasihi kwa uhuru na weledi pasipo kuiba au kutegemea tahakiki zilizokwishafanyika. Yaani, mwanafunzi asiwe mtu wa kukariri na “kucheua” tahakiki zinazohusu kazi fulani ya kifasihi, pasipo hata kuiona, kuigusa, kuimiliki, kuisoma na kuitathmini kazi husika. Athari ya awali ya kukwepa kusoma kazi husika za kifashi na kuzihakiki kifasaha ni kwamba, endapo kuna makosa katika tahakiki “iliyofanywa msahafu,” basi wanafunzi na walimu wataendeleza makosa hayo katika maelezo yao.
Mfano mzuri umo katika baadhi ya tahakiki aghalabu za Kiingereza. Mathalani, tahakiki ya M. Kadeghe (mwaka haujulikani) inamtaja Gikonyo wa A Grain of Wheat (1967) ya Ngugi wa Thiong’o, kuwa alijiua ­ jambo ambalo si la kweli. Tahakiki nyingine ni ya G. R. Bukagile, na wenzake (2008) ambayo imekosea majina ya baadhi ya wahusika waliomo katika A Man of the People (1966). Dosari hizi hata kama ni kwa bahati mbaya, bado kwa mwanafunzi ambaye hakuvisoma vitabu husika atazidi kunukuu majina na maelezo hayo huku akiamini kuwa ni sahihi, jambo ambalo ni hatari kimtazamo na kiutendaji. Kwa kutokujua namna ya kuhakiki, mfano ushairi wa Kiswahili, kwa mujibu wa F. E. M. K. Senkoro (1988: vii) baadhi ya wanafunzi na walimu wanauona uhakiki wa ushairi kuwa ni kazi ngumu na hivyo kuogopa kuhakiki kazi na, au kujibu maswali yake.
Inasadikika kuwa mwanafunzi mzuri ni yule anayebobea katika nadharia ya jambo fulani. Kwani nadharia ya uhakiki ndiyo mama wa kozi nzima ya fasihi ya Kiswahili ambapo kupitia kwazo mwanafunzi ataweza kuhakiki, kuhusianisha, kutathmini, kulinganisha na kulinganua uhalisi na ubora wa tahakiki zilizokwisha kuandikwa juu ya kazi za kifasihi, na mazingira ya uhakiki husika.
Katika kuunga mkono wazo hili, S. D. Kiango katika Misingi ya Uhakiki wa Fasihi (1993: viii) anasema, “kuna wahakiki wanaoshikilia mawazo ya kuiangalia kazi ya kisanaa kwa kuzingatia umbo la kazi hiyo bila ya kuihusisha na jambo jingine lolote.” Hii ina maana kuwa ni vema na muhimu sana kuzifahamu nadharia zingine na kuzitumia katika uhakiki. Hivyo, mwanafunzi binafsi, ataweza kuhakiki kazi mbalimbali za kifasihi atakazokutana nazo ­ iwe darasani, au kwenye mtihani, ama nje ya maeneo haya mawili. Katu hatakimbia kazi au swali linalomtaka kufanya uhakiki hata kama hana tahakiki yoyote karibu yake.
Kwa kumjenga mwanafunzi katika msingi madhubuti wa kuielewa mihimili ya uhakiki, pamoja na mambo mengine, kama vile kuwepo kwa mazingira bora ya kujifunzia, kuwepo kwa vitendea kazi vya kutosha na vyenye ubora unaotakiwa, uwezo binafsi wa mwalimu na mwanafunzi katika kulimudu somo, kuwepo kwa njia bora za ufundishaji, na kadhalika, kutamsaidia mwanafunzi kujitegemea, kujiamini, kuwa mbunifu, na kulimudu vema somo la fasihi ya Kiswahili. Hivyo kumfanya awe mweledi wa fasihi ya Kiswahili. Haya yanaungwa mkono na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi (2009: iv) wanaposema, “matokeo ya kujifunza ni bora zaidi pale ambapo mwanafunzi hamtegemei mwalimu tu, kwani ujifunzaji endelevu huhitaji stadi za kusoma kwa kujitegemea.”
Zaidi ya hapo, mwanafunzi atajijengea desturi ya kupenda kujisomea na kujielimisha katika nyuga mbalimbali nje na ndani ya fasihi ya Kiswahili. Atawajibika vema, tena kwa kujiamini, pindi anapotekeleza majukumu yake kama mwanafunzi, mwalimu, kiongozi, mtawala, mtafiti, mshauri wa kitaalamu, na mwezeshaji.
Katika kudhihirisha uzito wa hoja hii, Ben Carson, mtaalamu wa neurosurgery, katika kitabu chake kiitwacho Think Big (1992), pamoja na shuhuda zake nyingi juu ya maisha na uweza wa Mungu, mwandishi huyu hasiti kukiri kuwa utamaduni wa kujituma katika kusoma vitabu mbalimbali kunampa mtu uwezo wa kukabiliana na changamoto mbalimbali. Mathalani, Ben Carson (uk. 18, 21 – 22, 161, 23) anasema:
Reading is the way out of ignorance, and the road to achievement… I did not have to be the class dummy anymore … my mother, not an educated woman … had forced me to read two books a week … I agreed to do what Mother told me… I seemingly had jumped overnight from the bottom to the top of the class … the jokes about me stopped.
Kujifunza ni njia ya kujinasua kutoka ujinga, na ni barabara ya mafanikio… sikuhitaji kuwa mjinga tena darasani… mama yangu hakuwa msomi (lakini) alinisisitiza kusoma japo vitabu viwili kwa wiki… Niliamua kukubaliana na kile alichoniambia mama… Ninajisikia kama niliyeruka usiku mmoja kutoka kuwa wa mwisho darasani (katika mitihani) hadi kuwa kinara… dharau juu yangu ikaisha (Tafsiri ya mwandishi).
Katika kuthibitisha haya, Ben Carson (uk. 20) ananukuu kauli ya Clarence Day kuwa:
The world of books is the most remarkable creation of man; nothing else that he builds ever lasts. Monuments fall; nations perish; civilizations grow old and die out. After an era of darkness, new races build others; but in the world of books are volumes that live on still as young and fresh as the day they were written, still telling men’s hearts of the hearts of men centuries dead.
Ulimwengu wa vitabu ndiyo uumbaji bora zaidi wa binadamu; hakuna alichokijenga kikadumu (isipokuwa kusoma). Sanamu au majengo ya kifahari hubomoka; mataifa huangamia; ustaarabu hukua, huzeeka na kufa. Baada ya kipindi cha ombwe/giza, jamii mpya hujenga nyingine; lakini katika ulimwengu wa vitabu mna majuzuu yanayoishi kana kwamba ni machanga na mapya ­  kama ndiyo kwanza yanaadikwa, bado mioyo yetu inazungumza na  mioyo ya watu waliofariki karne kadhaa (Tafsiri ya mwandishi).
Mawazo haya yanaungwa mkono na William Ellery Channing, kama alivyonukuliwa na Ben Carson (uk. 13). Channing anasema:
…. In the best books, great men talk to us, give us their most precious thoughts, and pour their souls into ours. God be thanked for books… Books are true levelers… to all who will faithfully use … of the best and greatest of our race.
.... Katika maandiko bora, watu maarufu huongea nasi, hutupatia fikira bora zaidi, na kutumiminia roho zao. Mungu ashukuriwe kwa kutupatia vitabu (ufahamu/maarifa?)…. Vitabu ni msawazishi wa kweli… kwa wote watakaoyatumia kikamilifu… ni msingi wa mambo bora zaidi na yaliyo makubwa kwa jamii yetu (Tafsiri ya mwandishi).
Kwa mujibu wa Ben Carson, mtu ataweza kufanikiwa maishani endapo tu atatambua kuheshimu na kutumikia kipawa/kipaji chake; atakuwa mwaminifu na mwadilifu kivitendo; atakuwa mmaizi; atakuwa mtu mwema; mwenye kutumia maarifa kiufasaha; mwenye kujikita katika kusoma vitabu mbalimbali; mwenye ubobevu wa maarifa; huku akimtanguliza Mungu katika kila jambo na kila hatua aipigayo (uk. 149 ­ 251). Mkabala huu unaungwa mkono na R. Dubos (1968: vii, xi ­ xii, 127, 135, 238, 242) pia, H. Gardner (1982: 261). Haya yote yatawezekana iwapo msomaji ataongozwa na nadharia ya uhakiki wa kile asomacho.
 Kinyume na haya, bila shaka itakuwa ni kumuandaa mwanafunzi kukariri, na hata kuiba tahakiki, majibu, na mitihani anayopaswa kuijibu katika mitalaa mbalimbali. Madhara haya kwa siku za usoni yatasababisha kuwa na watendaji katika ngazi mbalimbali ambao ni wezi, tegemezi, wasio wabunifu, wavivu wa kufikiri, wasiowajibika wala kuwa na uchungu kwa taifa lao, na kadhalika. Nao watazaa vizazi vitakavyorithi mfumo wa kiutamaduni uliojengwa na wazee wao. Na mwishoni mwa nyakati, ni kuwa na jamii yenye migogoro, vita, umasikini wa kupindukia, matabaka ya kutisha, ujinga usio kifani, maradhi yasiyo kikomo, uchumi ulio dorora, na bila shaka washirikina wa kutupwa.
Katika uga wa ufundishaji wa fasihi ya Kiswahili, hususani kipengele cha uhakiki, yaelekea Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, na Taasisi ya Ukuzaji Mitaala hawajaona umuhimu wa kumwandaa mwanafunzi katika kukabiliana na dhana nzima ya uhakiki wa kazi za fasihi. Hili linajidhihirisha vema kupitia mihtasari mbalimbali ya Kiswahili. Kuanzia muhtasari wa kwanza wa mwaka 1975 hadi huu wa sasa, wa 2009, dhana ya uhakiki inatazamwa katika tafsiri ya mwanafunzi kufahamu vipengele vya fani na maudhui na siyo nadharia mbalimbali zinazotawala na kuongoza uhakiki kwa kutumia vipengele vya fani na maudhui. Lakini wakati huo huo, mwanafunzi anatakiwa kuhakiki kazi za kifasihi kwa weledi.
Mwanafunzi huyu bila shaka, hajui kwa nini na kwa namna gani ahakiki fani, na, au maudhui. Hata hajui mitazamo ya wananadharia wa uhakiki wa kazi za kifasihi. Swali la msingi ni, Je, atatumiaje mtazamo wa kisanaa (wenye kujumuisha Umbuji wa Kirusi, Umuundo, Uhakiki Mpya, Umuundoleo) au wa kihadhira (wenye kujumuisha U ­ Marx, U ­ Feministi, Saikolojia ­ Changanuzi, na Usasa) ama yote miwili (Mbunda Msokile, 1993: viii ­ x) kuhakiki kazi ya kifasihi? Huku ndiko kutegemea tahakiki kwa asilimia miamoja.
Na katika kuiona hatari ya kutegemea tahakiki, P. M. Musau katika Uhakiki wa Tamthiliya: Historia na Maendeleo Yake (1999: xii) anawatahadharisha watu kwa kusema, “tahakiki nyingi zilizopo... hazina upeo mpana.” Jambo linaloungwa mkono na A. I. Haji, na wenzake, (1981: 5 ­ 6), na R. M. Wafula (1999: 8). Hii inamaanisha kuwa daima maishani, tahadhari na kinga ni bora zaidi kuliko tiba.
Kwa mujibu wa baadhi ya walimu, hata hivyo, wanakiri kufundisha nadharia ya uhakiki ingawa si sehemu rasmi ya muhtasari. Kwa maelezo yao, kipengele hiki huwa kigumu mwanzoni, lakini kikieleweka vema, somo na mijadala ya uhakiki wa kazi za kifasihi huwa mizuri, yenye changamoto na mantiki, kama anavyofafanua mmoja wa walimu waliomshirikisha mtafiti wazo hili:
... hakika mwalimu hutafanya tena kazi ya kuhakiki kwa ajili ya mwanafunzi wako.... watajigawa katika makundi, watabishana weee, mwishoni watafikia mwafaka... ukisikiliza vizuri uwasilishaji na mijadala yao, utagundua ujenzi wa hoja unaofungamana na nadharia kadha wa kadha.
Hoja hii bila shaka inakubaliana na lengo la kuanzishwa kwa shahada ya uzamili wa sanaa katika fasihi ya Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dodoma (uk. 5) unaoeleza kuwa, kozi (mada) ya nadharia ya uhakiki humsaidia mwanafunzi kupata stadi ya kuelewa kwa undani nadharia anuai za fasihi za zama hizi ambapo kupitia kwazo, mtu ataweza kutambua vema mikabala ya kifasihi katika miktadha mbalimbali. Hivyo, ni muhimu kufundishwa; tena kiufasaha.
Kwa jumla, mambo yaliyojitokeza katika mjadala huu wa usuli ndiyo yaliyomsukuma mtafiti kuona ulazima wa kutathmini nafasi ya nadharia ya uhakiki katika kusoma na kuhakiki kazi za fasihi ya Kiswahili katika ngazi ya shule za sekondari nchini Tanzania.

1. 2 Tatizo la Utafiti

Pamoja na serikali, kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa kushirikiana na Taasisi ya Elimu Tanzania, kufanya jitihada kadha wa kadha katika kuboresha muhtasari na mbinu za ufundishaji wa somo la Kiswahili, fasihi ikiwemo, yaelekea bado kuna tatizo la vipaumbele. Yaani, kipi kipewe kipaumbele katika ufundishaji, na kipaumbele hicho kiweje.
Kwa mfano, kwa mujibu wa Muhtasari wa Kiswahili, toleo (jipya) lililotoka mwaka 2009, halionyeshi kama mitazamo mbalimbali inapaswa kufundishwa ama la. Mitazamo inayopaswa kujadiliwa ni ile ya fasili ya fasihi (uk. 16) na nadharia ya ushairi ­ umapokeo na usasa (uk. 37). Lakini katika suala la uhakiki wa kazi za fasihi, kinachoonyeshwa ni (i) “kufafanua / kujadili vipengele vya fani na maudhui katika vitabu teule vya ushairi, riwaya na tamthiliya” na (ii) “kutathmini ubora na udhaifu wa vipengele vya fani na maudhui katika vitabu teule vya ushairi, riwaya na tamthiliya” (uk. 35, 39, 41). Zaidi ya hayo, mwanafunzi anatakiwa kufafanua kazi za kifasihi katika mifumo mbalimbali kama vile: ujima, utumwa, ukabaila, ujamaa na ubepari (uk. 19 ­ 20).
Maswali ya kujiuliza hapa ni, mwanafunzi atawezaje kufafanua / kujadili ubora na udhaifu wa vipengele vya fani na maudhui; pia mifumo ya kijamii katika kazi za kifasihi pasipo kuwa na ujuzi wowote, tena wa kutosha kufanya hivyo? Endapo mwanafunzi huyu hasomi nadharia za uhakiki wa kazi za fasihi, ni kwa vipi anahakiki kazi hizo? Je, anatumia nadharia gani kuongoza mijadala na uhakiki wake? Je, anawezaje kufaulu mitihani yake inayohusu uhakiki? Kama sivyo, bila shaka hapa ndipo umuhimu wa mwanafunzi kufahamu mitazamo mbalimbali ya uhakiki wa kazi za fasihi unapojipambanua vema.
Kutokana na haya, mtafiti alilazimika kuchunguza namna mada ya uhakiki wa fasihi ya Kiswahili inavyofundishwa mashuleni. Aidha, mtafiti alilenga kubaini sababu zinazofanya nadharia za uhakiki wa fasihi kutokuwamo katika Muhtasari wa Kiswahili shule za sekondari. Pia, mtafiti alilenga kutathmini na kueleza uhusiano wa mada ya nadharia za uhakiki katika kumjengea mwanafunzi uwezo binafsi wa kubuni, kuhakiki, kujiamini, na kupenda kujisomea na kujifunza taaluma za nyuga mbalimbali, fasihi ya Kiswahili ikiwemo.

1. 3 Malengo ya Utafiti

1. 3. 1 Malengo ya Jumla

Utafiti huu ulikusudiwa kutathmini umuhimu wa kufundisha nadharia za uhakiki wa fasihi ya Kiswahili katika shule za sekondari ili kumwezesha mwanafunzi kuyakabili majukumu anayopewa ndani na nje ya darasa kiweledi.

1. 3. 2 Malengo Mahususi

  1. Kubainisha sababu zinazofanya nadharia za uhakiki kutokuwemo katika Muhtasari wa Kiswahili shule za sekondari.
  2. Kuchunguza namna nadharia za uhakiki wa fasihi ya Kiswahili zinavyofundishwa katika shule za sekondari.
  3. Kueleza uhusiano uliopo kati ya nadharia za uhakiki wa fasihi ya Kiswahili na uwezo wa mwanafunzi kujitegemea kivitendo katika majukumu kadha wa kadha anayopewa ndani na nje ya darasa.

1. 4 Maswali ya Utafiti

Maswali yafuatao yalikuwa dira ya utafiti na mijadala mbalimbali ya utafiti huu. Maswali hayo ni:
  1. Ni sababu zipi zilizofanya nadharia za uhakiki kutokuwemo katika Muhtasari wa Kiswahili shule za sekondari?
  2. Ni kwa namna gani nadharia za uhakiki wa fasihi ya Kiswahili zinafundishwa katika shule za sekondari hata kumwezesha mwanafunzi kuzikabili changamoto mbalimbali zikiwemo za kitaaluma, kwa kujitegemea awapo ndani na nje ya darasa?
  3. Ni uhusiano gani uliopo kati ya kujifunza nadharia za uhakiki wa fasihi ya Kiswahili na uwezo wa mwanafunzi kuzikabili changamoto mbalimbali zikiwemo za kitaaluma, kwa kujitegemea awapo ndani na nje ya darasa?

1. 5 Umuhimu wa Utafiti

Matokeo ya utafiti huu ni dira na changamoto kwa wadau mbalimbali wa elimu na fasihi ya Kiswahili, wakiwemo Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Taasisi ya Elimu Tanzania, watafiti mbalimbali katika uga wa fasihi, walimu na wanafunzi wa Kiswahili kwa kutambua namna, umuhimu na sababu za kufundisha au kutokufundisha nadharia za uhakiki wa fasihi ya Kiswahili katika shule za sekondari na taasisi za elimu ya juu. Utambuzi huu utakuwa kichocheo cha ama kusababisha mada ya nadharia za uhakiki wa fasihi ya Kiswahili kuingizwa katika Muhtasari wa Kiswahili – sekondari, na kufundishwa kiufasha, au la.

1. 6 Nadharia ya Utafiti

Nadharia iliyoongoza uchambuzi wa data ni ile ya mafunzo linganishi (M. Msokile; 1993: 15) inayozingatia ubunifu, na kufafanuliwa vema na P. M. Musau katika Uhakiki wa Tamthiliya: Historia na Maendeleo Yake (1999: xii) kwa kusema:
... ulinganishaji ni kiungo muhimu cha uhakiki, mhakiki anayefahamu kazi yake vizuri anapaswa kuwa mweledi wa maandishi mengi ya kifasihi kutoka katika tamaduni mbalimbali. Kadhalika, mhakiki anapaswa kuwa na ufahamu wa nadharia kadha wa kadha za uchambuzi wa kifasihi.”
Mtazamo huu unalenga kusawiri nafasi ya mhakiki, akiwemo mwanafunzi katika kufanya uchambuzi na ujenzi wa hoja pasipo kutegemea tahakiki au wazo fulani kuongoza uchambuzi wake. Kwa mtazamo wa watalaamu hawa bila shaka, mafunzo linganishi yanampa mawanda mapana zaidi mwanafunzi kutawala idili na uhalisi wa yale anayoyachambua. Kama hivi ndivyo, utafiti huu haukuwa budi kulithibitisha hili kwa kulichunguza kupitia jaribio kati ya wanafunzi waliofundishwa na ambao hawakufundishwa nadharia za uhakiki ili kubaini udhati wake.

1. 7 Mipaka ya Utafiti

Utafiti huu haukufanya kazi ya kuchambua kazi za kifasihi, bali kutathmini tahakiki mbalimbali kwa kuzihusianisha na matini chanzi husika. Lengo lilikuwa kudhibiti madhumuni ya utafiti, na matokeo yake.

1. 8 Hitimisho

Kwa jumla, sura ya kwanza imeaksi zaidi suala la mada ya nadharia za uhakiki wa fasihi ya Kiswahili kutokuwemo katika Muhtasari wa Kiswahili, sekondari. Hali inayosababisha baadhi ya wadau wa elimu kuhisi kuwa jambo hili ni miongoni mwa mambo yanayoathiri uwezo wa mwanafunzi kujitegemea kimtazamo na kiutendaji ndani na nje ya darasa. ni mataraji kuwa sura zinazofuata zitatoa majibu ya kina kuhusiana na sababu za kwa nini mada ya nadharia za uhakiki siyo sehemu rasmi ya muhtasari wa Kiswahili, sekondari, namna mada ya nadharia za uhakiki inafundishwa, na uhusiano uliopo kati ya kujifunza nadharia za uhakiki na uwezo wa mwanafunzi kujitegemea kimtazamo na kiutendaji ndani na nje ya darasa.

SURA YA PILI

MAPITIO YA MAANDIKO KUHUSU MADA HII

2.1 Utangulizi

Katika sura hii mtafiti alipitia na kuhusianisha mawazo na hoja mbalimbali kama zinavyojitokeza katika maandiko anuai. Mapitio haya yalikuwa na lengo la kuboresha mantiki yaliyomo na yatakayopatikana katika sura ya kwanza, sura ya tatu, sura ya nne, na sura ya tano. Mapitio ya maandiko mbalimbali yamefungamanishwa na mada ndogo zifuatazo: nadharia za uhakiki wa fasihi ya Kiswahili, ufundishaji wa fasihi na nadharia za uhakiki katika shule za sekondari nchini Tanzania (ikibeba pia tafiti linganishwa tatu), pengo la msingi katika mapitio ya maandiko, na mwishoni ni hitimisho la mijadala mbalimbali kama ilivyojitokeza katika sura nzima.

2. 2 Nadharia za Uhakiki

Kwa mujibu wa A. Mushengyezi (2003: 01) nadharia ya uhakiki ni “taaluma iliyoundwa na kuthibitishwa ambayo inajaribu kuelezea elementi maalumu zenye kubainisha taaluma ya kifasihi kama taaluma ya kujitegemea sawa na taaluma zingine.” Tafsiri hii inaelekea kukubalika na wataalamu wengine kama vile A. Harrison (1990), M. Msokile (1993, 1995), na E. M. Songoyi (2008: 04).
Na ndivyo inavyoelekea pia kwa wataalamu mbalimbali kukubaliana kuwa nadharia za kifasihi au mikabala ya kifasihi ndiyo msingi wa nadharia za uhakiki, ambazo ni taaluma tu ya kujifunza nadharia za kifasihi na mikabala yake. Kwa mujibu wa Kamusi ya Encarta (2009) nadharia za uhakiki ni taaluma, njia au sanaa ya kuchanganua / kuchambua, kufasiri, na kuhukumu maudhui, ubora, na mbinu zilizomo katika matini ya kifasihi.
Kwa mujibu wa M. Msokile (1993), Rivkin & M. Ryan (1998), K. W. Wamitila (2000), Rice & P. Waugh (2001), A. Mushengyezi (2003), T. Eagleton (1998; 2008), na wataalamu wengine wanaelekea kukubaliana kuwa mwanzoni mwa karne ya 20 ndicho kipindi kilichokuwa na msukumo mkubwa wa kubainishwa, na kuanzishwa mijadala iliyosababisha kuanzishwa kwa kozi za nadharia za uhakiki na mikabala ya kifasihi katika mafunzo ya fasihi huko Ulaya. Baadhi ya nadharia hizo ni pamoja na Umbuji wa Kirusi, Umuundo, Uhakiki Mpya, Umuundoleo, U - Marx, Ufeministi, Saikolojia ­ Changanuzi, Usasa, na Usasaleo. Nazo hujulikana zaidi kama nadharia za zama hizi ijapokuwa inaelekea baadhi yazo, zilikuwepo (zilianza) hata kabla ya karne ya ishirini.
Kwa maneno mengine, baadhi ya nadharia misingi yao ilijengwa hata kabla ya karne ya 20. Kilichofanyika katika karne hii ni kupewa uzito tu kwa maana ya kuanza kujadiliwa na kufundishwa vyuoni ­ kuanzia miaka ya 1920. Baadhi ya nadharia hizi ni Umbuji wa Kirusi, U - Marx na Ufeministi (Kamusi ya Encarta, 2009).
Jambo linalojitokeza hapa ni kuwa, baadhi ya wataalamu wanaelekea kupuuza chimbuko la jambo na badala yake kushikilia kipindi ambacho umaarufu wa jambo kitaaluma ulipopata mashiko. Kwa mtalaa huu, dhana ya nadharia ya kifasihi ya uhakiki wa zama hizi ni tete. Bila shaka unapaswa kusadifu zaidi Uhakiki Mpya, Umuundoleo, Saikolojia ­ Changanuzi, Usasa, Usasaleo, Unegritudi, Ujumi wa Kiafrika, na kadhalika (A. Mushengyezi; 2003).
Hata hivyo, lengo la utafiti huu ni kujikita katika msingi wa nadharia ya kifasihi ya uhakiki ili kutoa uwili wa kila nadharia pasipo kuzingatia hoja ya ‘ukongwe’ au ‘umaarufu.’  Kikubwa hapa ni mashiko na uzito wa nadharia yenyewe dhidi ya zingine kama sehemu ya stadi ya fasihi na uhakiki ili kutoa picha  anayoisisitiza daima T. Eagleton (2008:14) kwamba kila mtu na jamii yake wana itikadi ya kuyapima, kuyabainisha na kuyaamini mambo kwa mujibu wa imani inayoongoza vipimo vyao; kauli inayoungwa mkono na E. Kezilahabi katika Nagona (1990) kuwa ukamilifu mkamilifu ni sawa na safari isiyo na mwisho katika kuutafuta uzuri au ukweli kuhusu maisha.
Kwa mujibu wa wanaUmbuji, katika ujumla wake, mkazo umetiwa katika uteuzi, ujenzi na matumizi mazuri ya vipengele vya fani, yaani, muundo (ploti, sura, wahusika pamoja na muktadha, mandhari, mazingira) na mtindo (uteuzi na utumizi wa lugha/ maneno) ili kuleta mvuto na starehe kwa msomaji. Na kwa msomaji kuweza kupata maana, ni sharti awe na weledi wa kuchambua na kupata maana ya kawaida na ile iliyofichika. Na kwa mhakiki, ni muhimu kuepuka kutafuta wasifu wa mwandishi, kujiuliza ‘nini alichokilenga/ kusudia mwandishi,’ kutafsiri kazi kwa kuzingatia namna inavyomgusa na kumuathiri, pamoja na kuepuka ubinafsi wake katika kuhakiki kazi husika ya kifasihi. Mtazamo huu waelekea kuungwa mkono na P. M. Musau (1999: x) pale anaposema:
… kilicho muhimu zaidi ni kile kilichoandaliwa, yaani maandishi yenyewe…. Ni sharti mhakiki amhukumu mtunzi kwa misingi ya kile alichoandaa mbele ya msomaji wake. Vigezo vya kifasihi vyapaswa kuwa dira inayoongoza mhakiki, na wala siyo vigezo vingine vilivyoko nje ya matini….
Umbuji, kwa kiasi kikubwa, unapuuza uzito wa kipengele cha maudhui kama eneo la msingi la kifasihi. Lengo lao ni kuburudisha (“sanaa kwa ajili ya sanaa”) na kujaribu kuweka vigezo vya kuitofautisha fasihi na taaluma zingine (B. Eichenbaum; uk. 8 ­ 15; T. Eagleton; 2008: 1 ­ 14). Baadhi ya wanaUmbuji maarufu katika ujumla wao ni pamoja na Roman Jakobson, Viktor Shklovsky (wanaumbuji wa Kirusi), T. E. Eliot, A. I. Richards (wanauhakiki mpya), Ferdinand de Saussure (baba wa Umuundo), Roland Barthes, Levi Strauss, Tzvetan Todorov (wanaumuundo mpya), na Jacques Derrida (mwanaudenguzi).
Kwa mkazo huu, baadhi ya wataalamu, hasa wanaU - Marx, wanauona Umbuji kama wenye kutetea na kujenga matabaka katika jamii. Kwa mfano, A. I. Haji (1981: 31) anauita mtazamo wa kiumbuji kuwa ni mtazamo wa kibwanyenye, huku ule wa kimarx akiuita wa kimapinduzi. S. D. Kiango (1993: viii ­ix) anauita mtazamo huu kuwa wa kisanaa. Tena anauona kuwa hauna lengo lolote katika maisha ya leo. Kwa mujibu wa A. Harrison (1990: 297) hata hivyo, anaelekea kusisitiza kuwa uzuri wa fani/ sanaa ni sharti upimwe kwa kutazama mchango wake kwa jamii husika. Yaani, fani inaisaidiaje jamii ­ bila shaka katika kuyakabili matatizo yaliyomo katika jamii husika.
Kwa jumla, wanaoupinga Umbuji yaelekea wanasahau dhima ya uburudishaji na uhamasishaji fikra wa hali ya juu katika kupata maana. Kwa kutokuthamini mchango wa Umbuji katika uhakiki, bila shaka uchambuzi wa kutumia uhalisia - mazingaombwe kwa mfano, utakuwa mgumu sana. Kwani msomaji na mhakiki watashindwa kupasua sitiari na ishara katika kazi kama Nagona, Mzingile, Sadiki Ukipenda, na Mzimu wa Watu wa Kale kama anavyosisitiza F. E. M. K. Senkoro. Katika baadhi ya maandiko Umbuji unatajwa kwa majina ya Urasimi, na Umuundo kama inavyojitokeza katika K. Njogu na R. Chimerah (1999).
Kwa upande wa U - Marx, baadhi ya wataalamu wanaelekea kukubaliana kuwa U - Marx ndicho kipimo kizuri cha kazi ya fasihi. Baadhi ya wataalamu hao ni A. I. Haji (1981: 31; 34), Karl Marx, F. Engels, T. Eagleton, Georg Lukács, na kadhalika. U - Marx ni dhana yenye maudhui ya kijamii, kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni inayojadili uhusiano na mapambano ya kitabaka kati ya watu wa tabaka la chini dhidi ya wale wa tabaka la juu. Pia, hujishughulisha na uchambuzi wa njia kuu za uzalishaji mali na maendeleo ya kijamii katika nyanja zote za maisha ya mwanadamu.
Ni nadharia inayoshadidia mapambano yenye kumkomboa mtu wa tabaka la chini (mapinduzi ya kweli na endelevu). Inamtaka msanii na mhakiki kujadili suala la itikadi tawala, utamaduni, mihimili ya dola na ya kiuchumi kwa namna ambayo itawafungua fikra, hisia na macho ya wanaonyonywa na kunyanyaswa, ili kutambua kuwa vitu hivi ndivyo vyanzo vya ukandamizaji na unyonyaji (R. Williams; 1977).
Kwa mujibu wa A. Lunacharsky (1973: 10):
… U - Marx una jukumu kubwa, tena la msingi… kujishughulisha kwa dhati na juhudi katika namna ya kumuumba mtu mpya na mfumo mpya wa maisha… U - Marx unayachukua maisha ya kijamii kuwa ni muunganiko kamili, ambao viungo mbalimbali hutegemeana na kukamilishana….
Inavyoelekea upya wa mtu na mfumo anaoujadili A. Lunacharsky ni ujamaa au mfumo wenye kujenga mshikamano na umoja miongoni mwa wanajamii. A. I. Haji (1981: 31) anamuunga mkono A. Lunacharsky kwa kuuita U - Marx kuwa ni mtazamo wa kimaendeleo. S. D. Kiango (1993: viii ­ix) anauita mtazamo huu kuwa wa kidhamira.
Hata hivyo, pamoja na T. Eagleton (2008: 14) kuwa ni m ­ Marx, bado anadhani umaendeleo ama umapinduzi au udhamira unaotwishwa U - Marx ni utata mtupu, kwani kila mtu na jamii yake wana itikadi ya kuyapima, kuyabainisha na kuyaamini mambo. Hii ina maana kuwa, hata ubwanyenye wa A. I. Haji bado ni sehemu ya maudhui ya mapinduzi na maendeleo. Kwani aliye masikini leo kwako wewe, bila shaka ni tajiri kwa mwingine.
Kwa baadhi ya wataalamu, hakuna na si rahisi jamii yoyote ile duniani iliyoweza au itakayoweza kuufikia ujamaa mkamilifu. Hoja hii hufungamanishwa na ushahidi wenye misingi ya kihistoria, kijiografia, kiuchumi, kiitikadi, na kadhalika. Shujaa Okonkwo katika Things Fall Apart (1958) amechorwa kama mhusika aliyekulia katika ufukara wa kutupwa lakini anayakabili maisha kwa juhudi na maarifa kiasi cha kuwa tajiri, shujaa, na mtu maarufu mwenye kuheshimika na jamii yote ya Umwofia na vijiji vinavyowazunguka. Endapo wazungu wasingelibadili historia ya waafrika, bila shaka vizazi kadhaa vya mbele vingeliwahesabu warithi wa utajiri wa Okonkwo kuwa ni wafisadi na mabepari wasiokuwa wajamaa!
Kwa kuupa msisitizo U - Marx, kuna hatari ya kazi za kifasihi kuwa chapwa kifani. Kwa baadhi ya watu, hasa wanademokrasia – jamii wanapinga wazo la kumkomboa mwananchi kwa njia ya kuwepo kwa mapambano ya kitabaka, mapinduzi ya vurungu, na kuwepo kwa udikteta wa tabaka la chini la wafanyakazi dhidi ya matabaka mengine. Kwa wao, U - Marx unahubiri ujamaa pasipo kuweka mizani bayana ya kuupima kisayansi. Hata hivyo, pamoja na kupinga namna U - Marx unavyoyasawiri matatizo na usuluhishi wake, wanademokrasia – jamii hawatoi njia mbadala inayoweza kuwa muafaka kwa migogoro na matabaka kuepukwa katika jamii.
Kwa mtalaa huu, hata U - Marx bado si suluhisho sahihi la mabadiliko ya jamii endapo hautatumika vizuri. Hii ndiyo kusema, U - Marx hauna uzuri mkamilifu kiasi cha kuufanya uwe ndiyo “msahafu” wa uhakiki wa kazi za kifasihi kama unavyotazamwa na jamii nyingi za ulimwengu wa tatu, Tanzania ikiwemo.
Nadharia nyingine ni Ufeministi. Kwa mujibu wa Kamusi ya Encarta (2009) Ufeministi ni dhana jumuishi kwa mifumo ya imani na nadharia ambazo zimeweka mkazo maalumu katika kusawiri haki na nafasi ya mwanamke katika utamaduni na jamii. Kwa upande wa fasihi, Ufeministi unajengwa katika ajenda yenye kutathmini namna itikadi na mfumo wa kijamii vinavyoathiri utu wa mwanamke kupitia lugha, utamaduni, utendaji wa kila siku, mahusiano ya kijinsi na kijinsia, na kadhalika. Yaani, fasihi na uhakiki wa kifeministi unajadili namna mwanamke anavyojiona, namna jamii ya wanaume inavyomuona mwanamke, na namna mwanamke anavyomuona mwanamke mwenzake. Lengo ni kumkomboa mwanamke kwa kuzingatia tamko la Beijing, China la mwaka 1995 linalotaka jamii ya mfumo dume kutambua usawa, haki, na mchango wa mwanamke katika majukumu na wajibu ndani na nje ya familia na taifa ijapokuwa hapo awali Ufeministi ulianza kama jukwaa la ukombozi wa mwanamke kisiasa (R. D. Sell; 1991, na K. H. Peterson; 2001). K. Njogu na R. Chimerah wanaongeza kuwa, kwa namna fulani, nadharia ya mtazamo kike ni ‘jibu’ la mikabala ya awali (hususani U - Marx na Umuundo wa Kirusi) na imeshika kasi zaidi mnamo miaka ya themanini na tisini.
Ukombozi dhidi ya mwanamke kwa mujibu wa Mary Ann Weathers ni sharti uanzie katika fikra za mwanamke mmoja mmoja kisha jamii nzima. Kwani kwake yeye “kama hauko huru, utawezaje kuwakomboa wengine?” Hata hivyo, kwa mujibu wa Gloria Steinam, ukombozi pekee na wa kweli wa mwanamke ni kwa yeye kujitenga/ kutokujihusisha na dini (kutokuamini katika misahafu), tamaduni (zilizojengwa katika mfumo dume), na ndoa. Kwake yeye, maeneo haya matatu ndivyo viini vya “utumwa” wa mwanamke.
Pamoja na jitihada nyingi katika kuijenga nadharia hii, bado baadhi ya wataalamu wanaijenga katika misingi ya ubaguzi wa rangi na kiuchumi. Hii inasababisha, kwa Waafrika, kuzungumzia Ufeministi katika sura mpya; sura ya Ujumi wa Kiafrika. Pia, haibabadui namna gani mwanamke ataweza kuwa huru pasipo dini, utamaduni, na ndoa. Kwani kila jambo, tukio, na desturi hufungamana na maisha halisi ya jamii husika katika kipindi husika cha kihistoria; hivyo kuwa na uwili ­ uhasi na uchanya. Hoja ya Mary Ann Weathers kwamba ukombozi wa kifikra ndiyo msingi wa mikabala mingine ya haki na wajibu wa mwanadamu, inaelekea kuwa na mashiko zaidi ya kijamii kuliko ile ya Gloria Steinam ambayo haionyeshi namna mwanamke anavyoweza kuwa huru nje ya idili za kijamii.
Hata hivyo, suala la usawa linapaswa kutazamwa kwa maana pana zaidi, tena ya kisayansi. Kwani baadhi ya wataalamu na wanajamii wanadhani kuwa hakuna na hakutakuwepo usawa chini na juu ya jua. Matini ya sasa ni mbio za kubadilishana vijiti tu, na si vinginevyo. Yaani, kama ilivyokuwa (na bado ipo kwa baadhi ya jamii) katika kipindi cha mfumo kike, kisha mfumo dume; ndivyo itakavyokuwa mbele ya safari. Tunabadilisha udongo wa juu wa leo (mfumo dume) kwa kuuzamisha ndani/ ardhini na ule wa chini kuja juu ili tupate udongo wa juu wa kesho (mfumo kike), (F. J. Masatu; 2008).
Si kwamba wanapinga harakati hizi, bali kinachopingwa ni tafsiri za harakati hizi zinazopingana na uhalisi wa kihistoria na kiimani. Hii ina maana kwamba, kuachana na mfumo dume ni mwanzo wa ufalme wa mfumo kike. Hili ndilo gurudumu la maisha ya mwanadamu ­ yamo katika mzunguko wa nyuzi 360. Daima, wakati ukuta, Ebrahim Hussein (1970) alisema. R. Dubos. (1968: 242) katika kutetea hoja ya uhalisi na historia, anasema, “zama zilizopita si historia fu; ni nyenzo yakinifu inayoishi ambayo kwayo binadamu anajiumba na kujenga wakati ujao.”
Baadhi ya waandishi na wanaufeministi ni pamoja na George Eliot, Virginia W., Margaret Fuller, Mary Ann Weathers, Naomi Wolf, Gloria Steinam, na Penina Mhando/ Mlama.
Nadharia nyingine ni Saikolojia ­ Changanuzi ambayo imejengwa katika msingi wa Mwanasaikolojia Sigmund Freud. Nadharia hii inaitazama sanaa kama zao la mawazo ya kinjozi, tamaa ya macho, ashiki, mfadhaiko, uhamisho wa kifikra, na tabia changamano. Kwa jumla, nadharia hii inaitazama ashiki kuwa ndilo zao la kiwango cha juu kwa mwandishi pindi anapounda au kuchambua kazi za kifasihi. Hii ndiyo kusema kuwa, kitovu cha nadharia hii ni ubinafsi, silka, na dhamiri, hivyo uhakiki wa kazi za kifasihi unapaswa kuzingatia mambo haya matatu (A. Mushengyezi: 2003; C. Momanyi: 2001).
Kwa kutumia nadharia hii mathalani, baadhi ya waumini wake wanamuona Odili katika A Man of the People (1966) kuwa si mwanamapinduzi wa kweli kwani kilichomfanya ajiunge na siasa, siasa ya kuwapinga chama tawala na serikali yao ni kitendo cha Mheshimiwa Chifu Nanga kufanya mapenzi na “mpenzi” wa Odili, Elsie. Kama ilivyo kwa Odili, nadharia hii pia imeathiri mtazamo “chanya” wa baadhi ya wanaU - Marx juu ya shujaa Okonkwo katika Things Fall Apart (1958). Hali hii inatokana na ugumu uliopo katika kubainisha na kuchambua tabia ya binadamu kisayansi, kwani kwa asili binadamu si kiumbe tuli, jambo linalowafanya baadhi ya waandishi na wahakiki kutokuipa uzito pindi wanapoandaa au wanapochambua kazi za kifasihi (E. Wright: 1991; P. Rice & P. Waugh: 2001).
Unegritudi, na Ujumi wa Kiafrika kwa pamoja ni nadharia zinazoaksi siasa, utamaduni, sosholojia, uzuri wa mwanamke wa kiafrika, mfumo na mtazamo chanya dhidi ya bara la Afrika. Kwa maneno mengine, nadharia hizi ni dhana zinazoshadadia Uafrika na raslimali za bara la Afrika kwa ajili ya Waafrika (Ngugi wa Thiong’o; 1994 / 1997). Hivyo basi, ubora wa kazi ya fasihi kwa mujibu wa nadharia hizi ni sharti uzingatie na kusawiri utamaduni wa kiafrika, rangi asili ya mwafrika (weusi) hususani uzuri wa mwanamke, na mapambano endelevu dhidi ukoloni, na ukoloni mamboleo (M. Msokile; 1993). Baadhi ya waumini wa nadharia hizi ni pamoja na: Leopard Sedar Senghor, Aime Ceasar, Okot p’Bitek, Chinua Achebe, Ngugi wa Thiong’o, na Wole Sonyinka.
Pamoja na malengo haya, bado nadharia hizi zinakabiliwa na changamoto ya kuendelea kuwepo kwa mabaki ya mfumo wa kikoloni, tofauti za kiimani, tofauti za kijiografia, tofauti za kiuchumi, tofauti za lugha, tofauti za rangi na kadhalika miongoni mwa waafrika wenyewe kama ilivyobainishwa na baadhi ya waandishi wa kiafrika katika D. Duerden, & C. Pieterse (wahariri; 1988). Hali inayofanya mwonekano wa nadharia hizi kwa baadhi ya wachambuzi wa kiafrika, na wa kimagharibi kutokuzielewa vema au kushindwa kubainisha uhalisi wake miongoni mwa waafrika na kazi zao za kifasihi (C. M. Ndungo; 1991, na D. Lodge & N. Wood; 2000).
Kwa jumla, picha inayojitokeza katika mjadala wa nadharia za uhakiki na mikabala ya kifasihi inadhihirisha upana wa namna binadamu anavyoyasawiri maisha na mifumo yake. Yaani, kila mtazamo umejikita na kusisitiza tafsiri yake dhidi ya fasihi na kazi za kifasihi kutathminiwa kwa mujibu wa idili za imani husika ya wanaoiamini kuwa ndiyo ya kufaa “zaidi.” Kwa jinsi uchambuzi ulivyofanyika kwa kila nadharia, ni dhahiri kuwa kila nadharia imejengwa juu ya msingi na sababu fulani mahususi za kihistoria katika nyanja mbalimbali za maisha. Hivyo, kuzifanya nadharia hizi kuwa na mashiko mtambuka pindi zinapozingatiwa katika uwili wake kwani hakuna iliyoonekana kuwa “takatifu” zaidi ya zingine. Hali hii ndiyo iliyomsukuma mtafiti kuona umuhimu wa kuchunguza namna nadharia zinavyofundishwa, uhusiano wake na weledi wa mwanafunzi katika kuzikabili changamoto mbalimbali anazokutana nazo ndani na nje ya darasa kwa kujitegemea, lakini pia sababu zilizofanya mada hii kutokuingizwa katika Muhtasari wa Kiswahili, sekondari.

2. 3 Ufundishaji Fasihi na Nadharia za Uhakiki katika Shule za Sekondari Tanzania

Katika kipengele hiki, mtafiti ameyatalii maandiko ya wataalamu kadhaa wa uga wa fasihi ya Kiswahili kupitia maandiko yao mbalimbali. Baadhi ya wataalamu hao ni pamoja na: A. I. Haji (1981), M. Msokile (1993), P. M. Musai (1999), K. W. Wamitila (2000), G. Ruhumbika (2006), F. E. M. K. Senkoro (1988; 2007), na tafiti tatu linganishwa ambazo ni: K. Njogu & R. Chimerah (1999), M. Ntarangwi (2004), na F. J. Masatu (2009). Uteuzi wao umezingatia kigezo cha maandiko yao kuwa na mjadala wa kina kuhusiana na ufundishaji wa fasihi na nadharia za uhakiki wa fasihi ya Kiswahili.
A. I. Haji (1981: 32) anabainisha kuwa “… siku hizi somo la Kiswahili linafundishwa mafamba mafamba tu katika madarasa ya juu….” Kwake yeye, suluhisho la tatizo hili, pamoja na mambo mengine, jamii ya elimu ya lugha na fasihi vya Kiswahili wanapaswa kutambua kuwa hakuna njia nyepesi au ya mkato yenye kumwezesha mwanafunzi - mhakiki kuwa mhakiki wa kutegemewa kwani ufundi wa kuhakiki unapatikana kwa kuitambua fasili yenyewe (ya uhakiki) na nadharia zake. Hoja hii inaungwa mkono na F. E. M. K. Senkoro (1988: vii), Wajumbe wa Kongamano la Kimataifa la Kiswahili katika kipengele cha 1. 5. 3, azimio namba 22 (katika M. M. Mulokozi, na wenzake, (wahariri); 2000: 09), na Z. S. M. Mochiwa (2001).
Tofauti na Wajumbe wa Kongamano waliotoa tamko la jumla kuhusu upungufu uliopo katika ufundishaji wa Kiswahili, na A. I. Haji aliyeitalii fasihi ya Kiswahili kwa jumla madarasani, F. E. M. K. Senkoro (1988: vii) anasawiri namna ushairi wa Kiswahili unavyofundishwa mashuleni. Kwa namna ushairi unavyofundishwa katika mawanda finyu, “baadhi ya walimu na wanafunzi wanauona uhakiki wa ushairi kuwa kazi ngumu na hivyo kuogopa kuhakiki kazi na, au kujibu maswali yake,” kauli inayoungwa mkono na M. Msokile (1993: iii). Kwa mujibu wa Senkoro, na Msokile, tatizo hili linachangiwa na sababu kadhaa zikiwemo kutokuzingatia ubunifu binafsi, kutokuzielewa na kuzitumia nadharia za uhakiki mathalani nadharia za umapokeo na usasa. F. E. M. K. Senkoro (2007) anasisitiza pamoja na mambo mengine, hoja ya kuzielewa na kuzitumia nadharia mbalimbali katika kufundisha na kuhakiki fasihi na kazi zake kwani hakuna nadharia yenye ukamilifu mkamilifu inayoweza kuwa alfa na omega katika Kiswahili.
Hoja ya F. E. M. K. Senkoro inaweza kutanuliwa kwa kuzitazama nadharia za uhakiki (kama zilivyopambanuliwa katika 2. 2: nadharia za uhakiki) na mifano ifuatayo kutoka kwa baadhi ya mijadala ya wataalamu kupitia tahakiki au makala zao. H. M. Njozi (1990) ‘anawalaumu’ wahakiki kama vile F. E. M. K. Senkoro, M. S. Khatib, na Joseph Mbele, kwa kutokuzingatia muktadha wa kidini (Uislamu) katika kuhakiki Utenzi wa Mwanakupona; kama anavyosema:
… this famous poem has so far received a very negative estimation in most of scholarly reviews I have seen … explanations seem to have missed the spirit behind Mwanakupona’s instructions because of their apparent neglect of the poem’s Islamic sources (uk. 55).
… shairi hili maarufu kwa muda sasa limetolewa maoni hasi sana miongoni mwa maandiko mengi ya kitaaluma niliyoyaona… ufafanuzi (wao) unaelekea kukosa imani dhidi ya maelekezo ya Mwanakupona, kwa sababu ya kupuuza, kuliko dhahiri vyanzo vya mashairi ya Kiislamu (Tafsiri ya mwandishi).
Tatizo lililopo hapa si mtazamo walioutumia F. E. M. K. Senkoro, M. S. Khatib, na J. Mbele, katika tahakiki zao. Kwani kila mmoja alihakiki kwa idili yake sawa na alivyohakiki H. M. Njozi kwa kuzingatia muktadha wa kidini, hususani wa dini ya Kiislamu. Hili ni suala la kiujumi zaidi. Kwa maneno mengine, H. M. Njozi anawakumbusha wahakiki kutokuegemea tu katika Ufeministi mathalani, kwa kudonoadonoa baadhi ya beti na kusahau uzuri wa shairi hili pindi muktadha wa kidini unapozingatiwa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya kijamii na kiutamaduni (mfano afya, ndoa na tendo la ndoa, ustaarabu, familia na kadhalika), kiuchumi, kiimani, na kisiasa.Tatizo lipo kwa mwanafunzi asiyejishughulisha na nadharia na tahakiki anuai katika kusoma na kujenga hoja na msimamo wake binafsi. Huyu ataishia kukariri na kurejelea pasipo kujua kwa nini mwandishi amesema hivyo.
Baadhi ya watu huona matokeo ya anguko la Rosa Mistika mathalani, katika riwaya ya Rosa Mistika kuwa limesababishwa na malezi ya kudhibitiwa sana kutoka kwa baba yake. Lakini, F. E. M. K. Senkoro anadhani anguko la Rosa Mistika, chanzo chake ni yeye mwenyewe; kwa hoja kuwa, ua ni moja na daima haliwezi kustahimili mikikimikiki ya dunia. Yaani hutokea, huchanua, lakini hufa mapema; tofauti na dada yake, Flora. Flora kibaolojia ni mimea mbalimbali, hivyo mimea mingi kwa pamoja huweza kuhimili vishindo vya dunia ­ kama walivyojengwa na Kezilahabi.
Aidha, kwa mujibu wa F. E. M. K. Senkoro (2007: 1 ­ 11), watu wengi pia, hudhani kuwa kazi zote zinahakikiwa kwa kutumia nadharia moja. Hili si kweli, kwani kuna baadhi ya kazi ambazo watu huzitaja kuwa ni ngumu na zisizoeleweka kama vile Nagona, Mzingile, Sadiki Ukipenda, Mzimu wa Watu wa Kale, Kufikirika, na Kusadikika. Kwake yeye kazi hizi si ngumu na zinaeleweka vema endapo, na endapo tu, msomaji / mhakiki atakuwa na uwezo wa kupasua sitiari na ishara kwa umahiri mkubwa. Na nadharia inayofaa hapa ni ‘uhalisia ­ mazingaombwe.’ Baada ya kuitumia nadharia hii ndipo nadharia zingine zinaweza kutumika kujenga hoja kwa mujibu wa mtazamo wa msomaji / mhakiki husika. Wapo pia wataalamu wanaodhani baadhi ya kazi kama vile za Mathias Mnyampala (hasa Ngonjera za Ukuta) na Shaaban Robert (Kusadikika, Kufikirika na Wasifu wa Siti Binti Saad na kadhalika) ni chapwa (Bertoncini, 1989: 38 - 46). Lakini kwa wengine kazi hizi si chapwa kabisa.
Hii ni mifano michache katika mingi inayoonyesha kugongana kwa mawazo na mitazamo ya wataalamu. Jambo linaloashiria kuwa mpaka sasa hapajaweza kuwa na ujumi wa kifasihi unaoweza kupokelewa na kukubalika kwa watu wote pasipo kutokea migongano ya kijamii (T. Eagleton; 2008: 14). Kwa upande mwingine, inaelekea utamaduni wa kutokubainisha kwa wazi aina ya nadharia itakayoongoza uhakiki wa kazi husika ya fasihi umechangia “sintofahamu” miongoni mwa wasomaji na wahakiki mbalimbali.
Katika kubainisha suluhisho la kutokufundishwa kiufasaha mada za fasihi mashuleni M. Msokile (1993, 1995) anapendekeza utumizi wa ubunifu binafsi kwa mwalimu na mwanafunzi huku mbinu shirikishi ikizingatia njia ya mafunzo linganishi kama inavyofafanuliwa vema na P. M. Musau katika Uhakiki wa Tamthiliya: Historia na Maendeleo Yake (1999: xii):
... ulinganishaji ni kiungo muhimu cha uhakiki, mhakiki anayefahamu kazi yake vizuri anapaswa kuwa mweledi wa maandishi mengi ya kifasihi kutoka katika tamaduni mbalimbali. Kadhalika, mhakiki anapaswa kuwa na ufahamu wa nadharia kadha wa kadha za uchambuzi wa kifasihi.
Inavyoelekea, lengo hasa la mbinu hii ni kumwezesha msomaji na mhakiki kutengeneza mizani itakayopanua welewa na msimamo wake juu ya kile anachokikabili ili kuepuka “athari za kusombwa na upepo wa kimaono.” Mizani hiyo ya ulinganishaji ni sharti ijipambanue katika mambo mbalimbali ikiwemo mijadala na maandiko ya kifasihi, kama asemavyo G. Ruhumbika (2006: 225):
 … kuwepo mwongozo wa vitabu vya rejea vya kuaminika na vinavyokidhi mahitaji ya wakati uliopo…: la sivyo, mwalimu wa Kiswahili mashuleni anapotea njia na kupotosha wanafunzi wake… na mwandishi wa Kiswahili anakuwa mbabaishaji anayedhuru nchi nzima kwa maandishi yake badala ya kuboresha lugha na kuendeleza fasihi yake.
Katika kuonyesha namna ya kufundisha nadharia za uhakiki kwa kutumia mbinu ya mafunzo linganishi, K. W. Wamitila (2000: 128 ­ 129; 197) anatanabaisha yafuatayo kwa wasomaji na wahakiki:
  1.  Kuelewa kuwa nadharia yoyote ile ya kihakiki ni nyenzo tu ya kutusaidia kulifikia lengo fulani. Na kila nyenzo huwa na ubora na udhaifu wake.
  2. Kuelewa kuwa nadharia huzuka katika mazingira fulani maalumu ya fasihi ambayo yana wasifu mahususi. “…. Kwa mfano, fasihi andishi ya Kiafrika inaaksi vipengele vya fasihi simulizi ambavyo havitiliwi maanani sana katika uhakiki wa kifasihi wa Ulaya.”
  3. Kuelewa kuwa makusudi ya kusoma nadharia siyo kumdidimiza msomaji/mhakiki kwenye tope la nadharia, bali ni kumjuza yaliyomo (katika kila mtazamo na makundi yake makuu manne) kwani “… huwezi kukipinga kitu ambacho kwanza hukijui vyema… tunapaswa kuyajua yaliyopo… kama hatua ya kwanza, kisha baadaye tunaweza kuzama kwenye uchunguzi wa kutafuta njia mbadala.”
Kimsingi, nadharia za kihakiki hutofautiana kutokana na malengo ya msingi (yanayofungamana na itikadi ama yake au ya kitabaka/kijamii) ya msomaji/mhakiki. Sababu kuu ya kuwako kwa nadharia ni kumwezesha mhakiki kuyaangaza masuala mbalimbali kwa kina na kwa mpangilio maalumu ili kwa kuzijua, kauli za mhakiki za kitathmini zitakuwa na mihimili mizuri ya kinadharia.
Naye M. Msokile (1993: 15) katika kuboresha hoja ya umuhimu wa kujifunza nadharia za uhakiki kwa kutumia mbinu ya mafunzo linganishi anasema:
Mara nyingi kazi za kifasihi zinazohakikiwa zinaweza kuwa katika hali mbili: kazi ambayo haijahakikiwa kabisa, na pili, kazi ambayo imekwisha hakikiwa mara moja ama pengine hata mara nyingi. Katika hali hii, mhakiki anatakiwa afanye utafiti ili kuona nini kimeandikwa na kimeandikwa vipi? Je, yeye anapohakiki anachangia nini kipya? Pengine si suala la kuchangia kipya, bali ametumia mkabala ambao ni tofauti na ule uliotumiwa?
M. Msokile ameongeza jukumu muhimu sana kwa msomaji na mhakiki mzuri wa kazi ya fasihi; nalo ni utafiti. Utafiti huu huweza kufanyika kwa njia ya kupitia tahakiki na makala mbalimbali au kuhudhuria mijadala ya kifasihi, hususani ile yenye kuwepo uwasilishwaji wa mada mbalimbali. Huku si tu kutapanua wigo wa uelewa wa mhakiki, bali pia kutamwimarisha katika kutambua haki, mipaka, na wajibu wa mhakiki wa kazi ya kifasihi.
Maoni ya wataalamu hawa yanafungamana kwa kiasi kikubwa na matokeo ya tafiti tatu linganishwa ambazo ni K. Njogu & R. Chimerah (1999), M. Ntarangwi (2004), na F. J. Masatu (2009). Tafiti hizi zinajipambanuwa kama ifuatavyo:
 K. Njogu na R. Chimerah (1999) wamefanya utafiti juu ya Ufundishaji wa fasihi: nadharia na mbinu mashuleni. Kama A. I. Haji na watafiti wengine walivyotamka, bado lipo tatizo la msingi katika ufundishaji wa somo la fasihi miongoni mwa taasisi mbalimbali za kielimu katika Afrika Mashariki. Utafiti wa K. Njogu na R. Chimerah ulitumia mbinu ya uchambuzi – maudhui kutathmini nadharia za fasihi ya kiswahili. Utafiti wao umezihusisha nadharia hizi na kazi mbalimbali za fasihi ya Kiswahili, kama mifano ya msingi katika ujenzi wa hoja.
Lengo lao kuu lilikuwa kutafsiri na kufanya muhtasari wa nadharia mbalimbali za fasihi zilizo katika lugha ya Kiingereza kwa kuziweka katika lugha ya Kiswahili kama njia mojawapo ya kurahisisha na kukidhi haja ya ufundishwaji na usomwaji wa nadharia hizi katika mazingira ya elimu, Afrika Mashariki. Hata hivyo, wataalamu hawa wameutazama ufundishaji wa nadharia katika ngazi ya sekondari na vyuo kwa jumla zaidi, jambo ambalo limemsukuma mtafiti kuainisha ngazi mahususi ya utafiti, yaani ngazi ya sekondari. Pia, kazi hii haijatanabaisha yupi ni mhakiki wa kazi ya fasihi, na kiwango gani cha elimu ambacho nadharia hizi zinapaswa kufundishwa.
M. Ntarangwi (2004) amefanya utafiti katika uga wa nadharia za uhakiki kwa ajili ya andiko lake la Shahada ya Uzamivu. Kazi yake “haitofautiani” sana na ile ya Njogu na wenzake isipokuwa ya kwake ikiwa katika lugha ya Kiswahili. Lengo kuu la utafiti likiwa kutathmini mambo ya msingi katika fasihi, na kuainisha nadharia mbalimbali za Kiswahili kwa kuzingatia maendeleo ya mikondo hiyo ya nadharia za fasihi. Kwa jumla, bado utafiti umejengwa katika sura ya jumla mno kuwashawishi wasomaji hasa wa ngazi za chini za kielimu mathalani, kuupa kipaumbele kama rejeleo muhimu, pia haujatathmini sababu, namna, na umuhimu wa kufundishwa nadharia za uhakiki wa fasihi ya Kiswahili kwa wanafunzi wa sekondari katika kumjengea mwanafunzi stadi na weledi wa kuzikabili changamoto anuai anazokutana nazo ndani na nje ya darasa.
F. J. Masatu (2009) amefanya utafiti katika uga wa nadharia na ushairi wa Kiswahili. Lengo kuu likiwa kutathmini namna Ushairi wa Kiswahili unavyofundishwa katika Shule za Sekondari na Elimu ya Juu (Kata ya Poli, Wilaya ya Meru, Mkoa wa Arusha). Mbinu za utafiti zilizotumika ni Uchunguzi, Hojaji, na Tathmini kutoka Maandiko ya kitaaluma. Utafiti ulijikita katika kutathmini mpaka - msingi uliopo baina ya ushairi wa Kiswahili na nyimbo za Kiswahili. Matokeo yanaonyesha kuwa ni vigumu kubaini mpaka – msingi uliopo baina ya aina hizi mbili za ushairi wa Kiswahili kwa kutumia mtazamo wa Kimapinduzi, hasa panapolinganishwa na kulinganuliwa kwa mashairi ya kisasa na nyimbo. Kimsingi, utafiti haukujikita katika nadharia zingine za uhakiki wa fasihi ya Kiswahili zaidi ya umapokeo na umapinduzi. Pia, utafiti wake haukuchunguza endapo mada ya nadharia za uhakiki wa fasihi ya Kiswahili inafundishwa katika ngazi ya shule za sekondari, yaani utafiti haukujibu maswali ya: kwa nini, na kwa vipi mada hii siyo sehemu ya rasmi ya Muhtasari wa Kiswahili, sekondari.

2. 4 Pengo la Msingi katika Mapitio ya Maandiko

Kwa namna moja au nyingine, wataalamu mbalimbali katika mitazamo yao wanaelekea kukubaliana kuwa upo umuhimu wa kujifunza nadharia za uhakiki. Pia, kupitia mawazo yao, yaelekea hakuna nadharia yenye ujumi mkamilifu. Zaidi ya hayo, maandiko yaliyopitiwa katika sura hii yameutazama ufundishaji wa nadharia za uhakiki katika ngazi za elimu kijumla, ijapokuwa elimu ya juu imezingatiwa zaidi. Bila shaka huku kutokana na msingi kuwa nadharia za uhakiki ni mada au sehemu ya kozi au programu rasmi katika elimu ya juu hali ambayo sivyo kwa ngazi ya elimu ya sekondari.
Zaidi ya hayo, inaelekea wataalamu wengi wanalitazama tatizo la ufundishaji wa mada za fasihi kuwa linatokana na mbinu za ufundishaji na matini yanayotumika huku “wakisahau” muundo na maudhui ya mada zilizomo katika mihtasari ya Kiswahili hususani ngazi ya sekondari. Hili ndilo pengo hasa lililozaa utafiti huu.
Kwa taswira hii, inawezekana hata tathmini ya nadharia za uhakiki wa fasihi ya Kiswahili kwa shule za sekondari ni wa chini miongoni mwa wataalamu na watafiti wa fasihi ya Kiswahili kutokana na nadharia za uhakiki kutokuwa mada au sehemu rasmi katika Muhtasari wa Kiswahili Sekondari.
Kwa mantiki hii, mtafiti anadhani upo ulazima wa kuchunguza namna nadharia zinavyofundishwa sekondari, kubaini sababu za kutokujumuishwa nadharia za uhakiki katika Muhtasari wa Kiswahili Sekondari, na kueleza uhusiano uliopo kati ya nadharia za uhakiki wa fasihi ya Kiswahili na uwezo wa mwanafunzi kujitegemea kivitendo katika majukumu kadha wa kadha anayopewa ndani na nje ya darasa katika ngazi ya sekondari. Kwa upande wa tahakiki zilizoainishwa kama mifano, imebainika kuwa wahakiki hawabainishi nadharia zinazoongoza uhakiki wao.

2. 5 Hitimisho

Kwa muhtasari, mjadala mzima uliojitokeza katika sura ya kwanza na hii ya pili unatoa uzito mpana zaidi katika mahitaji ya msingi yanayopaswa kutazamwa kwa makini pindi nadharia za uhakiki zinaposawiriwa kivitendo ndani na nje ya darasa husika.
Hatua hii inafungua ukurasa wa utafiti kama huu kuchunguza namna nadharia zinavyofundishwa, uhusiano wake na weledi wa mwanafunzi katika kuzikabili changamoto mbalimbali anazokutana nazo ndani na nje ya darasa kwa kujitegemea, lakini pia sababu zilizofanya mada hii kutokuingizwa katika Muhtasari wa Kiswahili, sekondari. Kwani katika zama hizi za utandawazi, mwanafunzi na mwalimu katika elimu ya sekondari wanapaswa kufungua silisila za utumwa wa kutegemea tahakiki na mawazo ya watu wengine kama silaha ya hoja zao. Kwani kila mtu ni muumini wa itikadi fulani katika maisha.

SURA YA TATU

MBINU NA VIFAA VYA UTAFITI

3. 0 Utangulizi

Sura hii imejikita katika kutoa dira iliyoongoza utafiti unaohusu ufundishaji wa nadharia za uhakiki wa fasihi ya kiswahili katika shule za sekondari, Tanzania. Mbinu na vifaa husika ni pamoja na:  muundo wa utafiti, eneo la utafiti, tathmini ya vifaa na mbinu, idadi ya wajibu hojaji/ jaribio la utafiti, uteuzi wa sampuli, vifaa vya utafiti (jaribio la ufahamu, hojaji, na uchunguzi), udhibiti wa vifaa vya utafiti, na uchambuzi wa data.

3. 1 Muundo wa Utafiti

Kwa mujibu wa C. R. Kothari (1993) muundo wa utafiti ni muundo changamano unaojumuisha dhana anuai ambazo huongoza utafiti. Muundo huu unamsaidia mtafiti kupata data za kina ili kukamilisha malengo ya utafiti husika.
Muundo wa utafiti ulikuwa ni wa muktadha halisi ambapo mtafiti alitumia mbinu ya majaribio kwa kulinganisha matokeo ya majibu kutoka shule mbili teule. Mtafiti ambaye kiweledi ni mwalimu wa lugha, na fasihi aliiteua shule ya sekondari Elly’s kuwa shule dhibitiwa kwa kuwafundisha wanafunzi wajibu hojaji/ jaribio la utafiti nadharia mbili za uhakiki wa fasihi ya Kiswahili (U - Marx na Umbuji wa Kirusi – nadharia moja kwa siku moja kwa juma). Baada ya siku mbili za kujifunza nadharia, wanafunzi teule walipewa muda wa juma moja ili wajisomee kabla ya kufanya jaribio la kuhakiki kazi teule ya kifasihi. Katika shule ya pili, shule ya sekondari Ikizu, wanafunzi hawakufundishwa kabisa nadharia za uhakiki isipokuwa, walitakiwa kufanya uhakiki wa kazi teule sawa na ile iliyotolewa katika shule ya sekondari Elly’s. Lengo la jaribio hili lilikuwa kuchunguza iwapo pana tofauti ya kimtazamo na kiutendaji kati ya mwanafunzi aliyejifunza na ambaye hakujifunza nadharia za uhakiki wa fasihi ya Kiswahili.
Utafiti ulifanyika kwa miezi mitatu katika shule mbili za sekondari zenye kufundisha Kiswahili, kidato cha tano na sita. Wajibu hojaji/ jaribio la utafiti wote ni wadau wa somo la Kiswahili. Zoezi hili halikufanywa na walimu isipokuwa wao walimsaidia mtafiti katika kulitathmini na kulisimamia.
Uteuzi wa nadharia zilizofundishwa ulizingatia msingi wa kwamba U - Marx ni mojawapo ya nadharia za kimaudhui wakati Umbuji ni miongoni mwa nadharia za kimuundo jambo ambalo linajenga pande mbili za uhakiki – maudhui na fani “zinazokamilishana.” Kwa sehemu kubwa, inaelekea mawanda ya nadharia hizi ndiyo yanayoongoza chambuzi za matini mengi ya kifasihi, ijapokuwa hazipambanuliwi waziwazi.

3. 2 Eneo la Utafiti

Utafiti ulifanyika katika shule ya sekondari Elly’s na shule ya sekondari Ikizu kutoka Wilaya ya Bunda, Mkoa wa Mara. Wilaya hii kwa Kaskazini inapakana na Wilaya ya Musoma Vijiji, Kusini inapakana na Ziwa Viktoria na Mkoa wa Simiu, huku ikipakana na Wilaya ya Serengeti kwa upande wa Mashariki.
Sababu ya msingi ya kuichagua Wilaya ya Bunda ni kwamba, wakati wa utafiti huu mtafiti alikuwa anafanya kazi katika moja ya taasisi za elimu wilayani Bunda, ikiwemo Shule ya Sekondari Elly’s. Pia, mtafiti anaifahamu vema wilaya hii hususani maeneo mnamopatikana shule teule – kitamaduni, kimazingira na hali ya kiuchumi ya wakazi wake, hivyo kurahisisha na kusaidia udhibiti wa hali ya ukusanyaji data, hususani kutoka shule iliyodhibitiwa. Sababu hii inafungamana na hoja ya Wanauchambuzi fafanuzi kuwa ili kupata data za kina na sahihi kutoka eneo la utafiti, ni sharti mtafiti awe ni sehemu rasmi au mmoja wa wanajamii mnamofanyika utafiti (K. Mwiria & S. P. Wamahiu; 1995).
Kifupi, uteuzi wa shule hizi ulizingatia sababu nne za msingi: (i) mbinu kuu ya utafiti ilikuwa ni majaribio, hivyo ilimpasa mtafiti kuwa na sampuli ndogo anayoweza kuimudu na kuidhibiti ili kupata picha ya kina kuhusiana na ufundishaji wa nadharia za uhakiki wa fasihi ya Kiswahili. (ii) Kijiografia, shule hizi zinapatikana katika maeneo mawili tofauti lakini yenye kufikika kirahisi; Shule ya sekondari Elly’s iko takribani mita 3800 kutoka Bunda mjini ilhali shule ya sekondari Ikizu iko pembezoni mwa mji wa Bunda takribani kilomita ishirini na nane (28 km) kutoka stendi kuu ya mabasi ya mjini Bunda. (iii) Mtafiti aliwahi kufanya kazi kama mwalimu katika Shule ya Sekondari Elly’s, hali iliyomsaidia kujipenyeza kwa uhuru zaidi katika shughuli mbalimbali zilizoongoza utafiti, pamoja na kupata ushirikiano mkubwa kutoka wanajamii wa shule hii, na (iv) Shule zote zina idadi ya kutosha ya wanafunzi wa Kiswahili ambao waliweza kushiriki kikamilifu katika utafiti.

3. 3 Tathmini ya Vifaa/ Mbinu za Utafiti

Tathmini hii ilifanyika kupitia wanafunzi wa Kiswahili, kidato cha sita, na walimu wao. Katika Shule ya Sekondari Mwembeni iliyoko Manispaa ya Musoma Mjini, Mkoa wa Mara, kabla ya utafiti rasmi kuanza. Lengo lilikuwa kuzipima mbinu na vifaa vya utafiti kama vinakidhi ubora wa utafiti huu. Mbinu na vifaa vilivyotathminiwa ni: mbinu za ufundishaji, ufahamu na swali la utafiti, mwongozo wa uchunguzi, na hojaji kwa walimu na wanafunzi. Katika maeneo ya mbinu za ufundishaji, ufahamu na swali la utafiti, na mwongozo wa uchunguzi hapakuwa na dosari wala tatizo.
Tatizo lilijitokeza katika hojaji zote mbili (ya walimu/ mtaalamu toka Taasisi ya Elimu Tanzania, na ya wanafunzi), ambapo swali namba tatu (kwa walimu) na namba sita (kwa wanafunzi) lilibainika kuwa la jumla mno kwa wajibu hojaji kubaini kilichokusudiwa hasa. Swali lilisema (kwa walimu), “ni nadharia zipi unazopenda kuzifundisha; na kwa nini?” swali hili liliathiri hata mantiki ya swali namba sita kwa walimu lililosema, “kwa mtazamo wako, unadhani mada hii inafaa kufundishwa kuanzia kidato cha ngapi; na kwa nini?” Kwa wanafunzi swali lilikuwa “ni nadharia ipi au zipi unazofundishwa darasani pako?” Majibu yao yalikuwa “nadharia ya fasihi, nadharia ya vitabu kama vile shairi, riwaya, tamthiliya, na nadharia ya lugha,” “nadharia ya uhakiki, udhamini, uhuru wa mwandishi,” “nadharia ya uhakiki na mhakiki,” “nadharia ya fasihi simulizi na fasihi andishi,” na “nadharia za fasihi kwa jumla, na sanaa.”
Tathmini hii iliendelea hata kwa shule teule ambapo swali hili liliwekwa mwishoni kupima majibu ya wajibu hojaji/ jaribio la utafiti wa Shule ya Sekondari Mwembeni na wa shule teule za utafiti. Matokeo yake ni kutokuwepo tofauti yoyote baina ya majibu yao na yale ya Shule ya Sekondari Mwembeni - kwa wanafunzi na walimu. Kwa jumla, majibu yaliyotolewa na wajibu hojaji hayakuzingatia utangulizi uliokuwapo katika hojaji husika wala mahusiano ya maswali ya awali na yale yaliyofuata. Hata hivyo, mtafiti alilazimika kubadili maswali haya ili lengo la msingi la utafiti huu liweze kupatikana. Maswali mbadala yalikuwa ni:
1.      Je, umewahi kuzisikia dhana zifuatazo (weka tiki sehemu moja kwa kila kipengele)?
                                              Nimeisikia             Sijaisikia
a.   U - Marx                                      [    ]                     [    ]                 
b.      Umbuji                                         [    ]                     [    ]  
c.       Ufeministi                                     [    ]                     [    ]
2.      (a) Kama umewahi kuzisikia/kuisikia, Je, ulizisikia/uliisikia wapi?
(b) Ulisikia zikielezwaje/ikielezwaje?
(c) Kwa mawazo yako, unazielezaje dhana za U - Marx, Umbuji, na Ufeministi?

3. 4 Idadi ya Wajibu Hojaji na Ufahamu

Idadi husika ya wajibu hojaji/ jaribio la utafiti ni ishirini na tano, wakiwemo wanafunzi ishirini, walimu wanne, na mtaalamu mmoja kutoka Taasisi ya Elimu Tanzania. Idadi hii imetokana na mwongozo wa D. Ary, na wenzake (2006) ambao wanaainisha kuwa katika mazingira fulani ya utafiti, mtafiti hana budi kuzingatia zaidi aghalabu eneo mahususi la utafiti, na aina ya wajibu hojaji/ jaribio la utafiti. Kwa kuvizingatia vitu hivi viwili, mtafiti atawatumia wajibu hojaji/ jaribio la utafiti wote atakaokuwa amewaainisha katika utafiti wake pasipo kuzingatia mathalani uwiano wa kijinsi na kiushiriki. Zaidi ya hayo, muundo wa utafiti ni wa majaribio ambao unamlazimu mtafiti kuwa na namba ya wajibu hojaji/ jaribio la utafiti atakayoimudu vema ili uchunguzi uwe wa kina na wenye tija.

3. 5 Uteuzi wa Sampuli

Uteuzi ulizingatia msingi wa D. Ary, (kama lililotangulia) ambao wanaainisha kuwa katika mazingira fulani ya utafiti, mtafiti hana budi kuzingatia zaidi aghalabu eneo mahususi la utafiti, na aina ya wajibu hojaji/ jaribio la utafiti. Kwa kuzingatia maelekezo ya wataalamu hawa, walimu na wanafunzi wote wa Kiswahili, kidato cha sita kutoka shule ya sekondari Elly’s na shule ya sekondari Ikizu walihusika. Shule zote hizi zina kidato cha sita na mchepuo unaojumuisha somo la kiswahili, kidato ambacho ndicho wanafunzi wake wa Kiswahili walihusika katika utafiti. Kwa mujibu wa D. Ary, (kama lililotangulia) uteuzi wa shule kwa kuzingatia sampuli lengwa unamsaidia mtafiti kuteua shule kutoka katika orodha ya jumla ya mashule, na kupitia uteuzi huo wajibu hojaji/ jaribio la utafiti wote waliolengwa watajumuishwa katika sampuli. Kipengele cha uwiano wa kijinsi ulifungamana na mazingira ya upatikanaji wa sampuli watu. Sampuli lengwa ilitumika kumpata mtaalamu wa Kiswahili, mjibu hojaji kutoka Taasisi ya Elimu Tanzania.
Uteuzi wa kidato cha sita ulizingatia sababu kuu mbili ambazo ni (i) kwa mujibu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi (2009) wanafunzi wa kidato cha sita wanatakiwa wawe wamekwishajifunza mada ya uhakiki uchambuzi wa kazi za fasihi ukiwemo pindi wakiwa kidato cha tano ili waanze na kuendelea kuhakiki kazi za kifasihi hata wanapohitimu masomo ya sekondari. (ii) Kidato cha sita ni darasa linalokabiliwa na mtihani wa taifa, hivyo wanafunzi wanajitahidi kutimiza ndoto zao kwa juhudi, maarifa, na mbinu mbalimbali. Kwa upande wa walimu na mtaalamu kutoka Taasisi ya Elimu Tanzania, matarajio ya mtafiti juu yao yalikuwa, walimu hawa wa Kiswahili bila shaka walisoma nadharia hizi pindi wakiwa vyuoni; uwezo wao katika kufundisha somo la Kiswahili – fasihi, pamoja na tafiti walizofanya ama zilizo rasmi au zisizo rasmi kutatoa picha kamili ya kinachoendelea darasani. Hatua iliyosaidia kubainisha sababu na umuhimu wa kufundishwa au kutokufundishwa nadharia za uhakiki.

Jedwali 1: Mchanganuo wa Wajibu Hojaji/ Ufahamu

Namba
Taasisi / Shule
Idadi ya Wajibu Hojaji/ Jaribio la Utafiti
Hadhi
1
Shule dhibitiwa
08
Wanafunzi kidato cha sita, Kiswahili
02
Mwalimu, Kiswahili kidato cha sita
2.
Shule isiyodhibitiwa
12
Wanafunzi kidato cha sita, Kiswahili
02
Mwalimu,Kiswahili kidato cha sita
3.
Taasisi ya Elimu Tanzania
01
Mtaalamu uga wa Kiswahili
Jumla kuu

25

3. 6 Vifaa vya Utafiti

Utafiti ulitumia jaribio la utafiti, hojaji na uchunguzi kama vifaa vya kukusanyia data. Vifaa hivi ni njia ambazo zilitumika kukusanya data kwa mawanda mapana na kwa ufanisi zaidi.

3. 6. 1 Jaribio la Utafiti

Katika kufanikisha ukusanyaji data kwa njia ya jaribio la utafiti, mtafiti aliandaa somo la nadharia za uhakiki kwa shule dhibitiwa pamoja na swali moja lililotokana na kifungu cha habari (ufahamu) ili mwanafunzi aisome na kuihakiki. Kazi teule ya kifasihi (ufahamu) na swali lake vilikuwa vya aina moja kwa shule zote mbili. Lengo likiwa ni kudhibiti matokeo ya jaribio la utafiti ili kubaini kama kuna tofauti ya kimtazamo na kiutendaji kati ya mwanafunzi aliyejifunza na ambaye hakujifunza nadharia za uhakiki.

3. 6. 2 Hojaji

Hojaji ilitumika kupata maoni ya wanafunzi, mtaalamu kutoka Taasisi ya Elimu Tanzania, na walimu kuhusiana na nafasi ya nadharia za uhakiki kufundishwa au kutokufundishwa katika ngazi ya sekondari. Kwa mujibu wa R. N. Sharma (2005: 206; 215) hojaji ni:
seti ya maswali teule ya mtafiti ambayo majibu yake yanatafutwa kutoka kwa wajibu hojaji ili kupata taarifa kuhusu mambo fulani mahususi…. Ni nafuu kiuchumi, inaokoa muda, ni bora katika mitalaa maalumu, inafaa katika tafiti za wigo mpana na inafaa zaidi katika aina maalumu za mwitikio ikilinganishwa na njia zingine za ukusanyaji wa data.

3. 6. 3 Uchunguzi

Mtafiti alichunguza maswali ya mtihani wa taifa wa Kiswahili ­ karatasi ya pili kuanzia 2006 hadi 2010 ili kuona iwapo mada hii huzingatiwa katika utunzi na uchaguzi wa maswali. Muhtasari wa Kiswahili, maandiko anayotumia mwalimu na mwanafunzi wa somo la fasihi ya Kiswahili, azimio la somo, na vitabu vinavyotumika kufundishia fasihi ya Kiswahili vilizingatiwa. Namna ya ufundishaji wa nadharia ya uhakiki wa fasihi ya Kiswahili nao ulipewa kipaumbele, kuona iwapo kuna uzito wa pekee unaotolewa kwa mada hii. Haya yote yalitathminiwa kwa njia ya uchunguzi. Uchunguzi, kwa mujibu wa R. N. Sharma (2005: 145; 147) ni mbinu bora zaidi ya uchunguzi katika sayansi jamii, na­ ni shughuli ya macho yenye mpaka katika lengo mahususi linalohitaji kupanga, kuona na kuwekewa kumbukumbu.
Kila jambo linalohusiana na kuonekana kuwa muhimu katika utafiti huu, lilipewa uzito stahiki katika hatua zote za utafiti. Mathalani, mtafiti hakuwa na budi kuzingatia, kutambua na kuthamini suala la ufahamu binafsi wa mwanafunzi juu ya uhakiki na nadharia ya uhakiki. Lengo likiwa kupima namna wanavyoweza kujiamini katika kujibu hoja mbalimbali.

3. 7 Udhibiti wa Vifaa vya Utafiti

Katika kuhakikisha ubora wa matokeo ya utafiti, mtafiti alipata kibali cha kuendesha utafiti katika shule zote mbili. Mazingira ya upatikanaji na uundwaji wa darasa teule la utafiti ulizingatiwa kwa hali ya juu ili kujenga utulivu na utayari wa kutosha kwa wajibu hojaji/ jaribio la utafiti wote kufanya shughuli za utafiti kwa mshikamano, uwazi na moyo wa kujitolea. Lengo likiwa kudhibiti ubora wa data na matokeo ya data husika. Muda wa kujibu zoezi la jaribio kwa wanafunzi wajibu jaribio la utafiti ulikuwa ni saa moja, na majadiliano hayakuruhusiwa miongoni mwa wajibu hojaji/ jaribio la utafiti wakati wakiendelea na shughuli ya kujibu zoezi.
Pia, wajibu hojaji/ jaribio la utafiti hawakuruhusiwa kuwa na maandiko yoyote anayohusiana na mada ya utafiti, zikiwemo tahakiki. Kila mjibu hojaji/ jaribio la utafiti alikusanya karatasi yake punde alipomaliza kuhakiki majibu yake - ndani ya muda wa jaribio. Majibu ya jaribio yalikuwa ni siri isipokuwa kwa mjibu hojaji/ jaribio la utafiti husika, mwalimu wa somo, na mtafiti.

3. 8 Uchambuzi wa Data

Mtafiti alipitia kila kipengele na mbinu zilizotumika katika utafiti ili kutathmini iwapo hatua na vigezo mbalimbali vya ukusanyaji wa data vilizingatiwa vema.  Baada ya tathmini hiyo, mtafiti alianza kuhakiki data moja baada ya nyingine kwa utulivu kisha kuzinakili, kuzipanga na kuzitathmini kwa kuzingatia malengo ya jumla, na malengo mahususi ya utafiti. Mtafiti aliepuka kuchambua data kwa kusukumwa na utashi, imani, mtazamo na hisia binafsi ili kuepuka kughushi matokeo au kuathiri masuala ya mafao ya utafiti (D. Silverman; 2005). Hata hivyo, baadhi ya matokeo ya data hayakukubalika kuwa sehemu ya ripoti hii kwa sababu yalionekana kuwa ama siyo sehemu ya malengo ya utafiti huu, au yalikuwa na dalili ya udanganyifu, na kadhalika. Mbinu ya uchambuzi fafanuzi imetumika kwa sehemu kubwa katika uchambuzi na uwasilishaji wa matokeo ya utafiti.

3. 9 Hitimisho

Sura hii ni daraja muhimu katika utafiti na matokeo ya utafiti huu. Hivyo basi, nidhamu ya hali ya juu dhidi ya mbinu na vifaa vya utafiti haikuwa budi kuzingatiwa na mtafiti ili lengo la msingi lipate kufikiwa. Ilitazamiwa kwamba mtafiti atatumia miongozo mbalimbali iliyopambanuliwa katika sura hii, pamoja na sura za awali kusudi asitoke ndani ya wigo wa utafiti huu.

SURA YA NNE

UWASILISHAJI, UCHAMBUZI NA MJADALA KUHUSU DATA

4.1 Utangulizi

Sura ya nne ni matokeo ya utafiti uliofanyika kwenye shule mbili za sekondari katika Wilaya ya Bunda, Mkoa wa Mara. Shule hizo ni: Shule ya Sekondari Elly’s, na Shule ya Sekondari Ikizu. Sura hii inajumuisha uwasilishaji, uchambuzi na mjadala wa data zilizopatikana kwa kuzingatia malengo ya jumla, na malengo mahususi yaliyoongoza utafiti wa andiko hili.

4. 2 Hoja ya Uchambuzi

Malengo ya utafiti huu yalijikita katika (i) Kubainisha sababu zinazofanya nadharia za uhakiki kutokuwemo katika Muhtasari wa Kiswahili shule za sekondari, (ii) Kuchunguza namna nadharia za uhakiki wa fasihi ya Kiswahili zinavyofundishwa katika shule za sekondari, na (iii) Kueleza uhusiano uliopo kati ya nadharia za uhakiki wa fasihi ya Kiswahili na uwezo wa mwanafunzi kujitegemea kivitendo katika majukumu kadha wa kadha anayopewa ndani na nje ya darasa. Malengo haya ndiyo yaliyopewa uzito kwani lengo kuu la utafiti huu ni kujenga taswira kwa wanazuoni mbalimbali hasa wa Fasihi ya Kiswahili kuona umuhimu wa kujikita katika kuandaa wataalamu hususani walimu, kuwa walimu wa fasihi na siyo walimu wa walimu wa fasihi. Yaani, kozi za ualimu ziandae walimu wa walimu wa fasihi – mbinu za ufundishaji, ilhali zile za fasihi, pamoja na zile za ualimu na fasihi ziandae walimu wa fasihi – nadharia na makandokando yake. Mazingira ya mfumo uliopo vyuoni unaelekea kuegemea zaidi katika uandaaji wa walimu wa walimu wa fasihi, huku “ukisahau” hitaji la kuwepo kwa walimu wa fasihi ambao ndiyo chemchem ya wataalamu stadi na weledi wa fasihi ya Kiswahili.
Ushahidi kutoka vyuo mbalimbali vyenye kozi ya fasihi unaonyesha kuwa kozi hii huchaguliwa na kusomwa na wanafunzi wachache. Hii inatokana na ukweli kuwa kozi hii imejikita zaidi katika nadharia na utumizi wa nadharia hizo katika miktadha mbalimbali ya kifasihi na kimaisha, kitu ambacho wanafunzi hawana msingi nacho toka sekondari aghalabu kidato cha tatu, kidato ambacho shughuli za uhakiki wa kazi za fasihi huanza. Jambo linalowafanya waiogope na hatimaye kutokuichagua kabisa, au pindi wanapoichagua, baadhi yao hushindwa kuimudu vilivyo kozi hii, kama ilivyojidhihirisha katika andiko la F. E. M. K. Senkoro (1988), na F. J. Masatu (2009).
Katika kufanikisha malengo haya, jumla ya mtaalamu mmoja (01) kutoka Taasisi ya Elimu Tanzania, wanafunzi 20, na walimu wanne (04) walihusika. Wajibu hojaji/ jaribio la utafiti hawa wote waliombwa kushiriki kwa hiari; hakuna aliyelazimishwa na mtu yeyote – iwe kutoka shule husika au mtafiti. Sampli jumuishi ilitumika kuwapata wajibu hojaji/ jaribio la utafiti wanafunzi na walimu, huku sampli lengwa ikitumika kumpata mjibu hojaji kutoka Taasisi ya Elimu Tanzania.
Ukusanyaji data kwa jumla, ulifanyika ndani ya miezi mitatu kupitia hojaji kwa wajibu hojaji/ jaribio la utafiti wote 25, njia ambayo ilitumika kabla ya jaribio kwa wanafunzi, na uchunguzi wa vitendea kazi vya wanafunzi na walimu, kwa mfano mtihani wa taifa Kiswahili karatasi ya Pili, Muhtasari wa Kiswahili, mihtasari ya maandiko mbalimbali ya mwalimu na mwanafunzi wa somo la fasihi ya Kiswahili, azimio la somo, vitabu vinavyotumika, na namna somo linavyofundishwa darasani. Nadharia - dira katika utafiti huu ilikuwa ni mafunzo - linganishi. Nadharia zilizofundishwa katika darasa dhibitiwa ni U - Marx na Umbuji wa Kirusi. Masuala ya mafao ya utafiti yalizingatiwa katika hatua zote za utafiti na uandishi wa ripoti ili kutoa sura halisi ya kile kinachoendelea katika elimu na fasihi mashuleni, Tanzania.
Uwasilishaji, uchambuzi, na mijadala kuhusu data umejikita zaidi katika uchambuzi fafanuzi. Uteuzi wa mbinu hii unasaidia kujibu maswali ambayo uchambuzi numerali hauwezi kuyajibu. Hii ndiyo kusema, mbinu hii hujaribu kwenda mbali zaidi katika kujenga taswira ya chanzo hasa cha jambo linalohusisha mazingira, halisi, na yasiyo halisi – ya kufikirika, ya kuhisi, na kadhalika.
Aidha, mjadala huu umeyawasilisha matokeo kwa kuyagawa katika maeneo makuu mawili: matokeo ya hojaji na uchunguzi, na matokeo ya jaribio la utafiti. Nukuu, ujenzi na utanuzi wa tafsiri za data vimezingatiwa huku baadhi yavyo vikitumika; lakini vikiwa vimepitia kwenye chujio la masuala ya mafao ya utafiti. Kwa jumla, uwasilishaji, uchambuzi, na mjadala kuhusu data umeongozwa na malengo mahususi ya utafiti na nadharia husika ya utafiti.
Uwasilishaji umeanza na malengo mahususi ya utafiti kwa kuyafungamanisha na matokeo ya hojaji, na uchunguzi, kisha kukamilisha mijadala ya sura hii kwa kujadili kipekee matokeo ya jaribio. Lengo la kutenganishwa mijadala ya matokeo ya hojaji na uchunguzi kwa pamoja, na matokeo ya jaribio peke yake ni kupata mawanda mapana ya mitazamo ya wajibu hojaji/ jaribio la utafiti na utendaji wao katika majukumu mbalimbali ndani na nje ya darasa. Hoja hii inatokana na ukweli kuwa, (i) njia tatu zilitumika kukusanya data – hojaji, uchunguzi, na jaribio vimetoa majibu yanayokinzana lakini yenye kukamilishana kimantiki. Kwa hali hii, kuyaunganisha matokeo kunaweza kuathiri uwasilishaji wa matokeo kwa kuyaminya baadhi, pia tafsiri zake. Jambo linaloweza kusababisha mkanganyiko miongoni mwa wasomaji wa tasnifu hii. (ii) Aidha, wakati mwingine katika maisha mitazamo na kile wanachokisema watu huweza kutofautiana na matendo yao.

4. 3 Uwasilishaji, Uchambuzi, na Mjadala kuhusu Data

4. 3. 1. 0 Matokeo ya Hojaji na Uchunguzi

4. 3. 1. 1 Sababu Zinazofanya Nadharia za Uhakiki Kutokuwemo katika Muhtasari wa Kiswahili Shule za Sekondari

Tathmini ya kubainisha sababu za kwa nini nadharia za uhakiki wa fasihi hazimo katika muhtasari wa Kiswahili, shule za sekondari ilifanyika kwa njia ya hojaji kupitia wajibu hojaji walimu, na mtaalamu toka Taasisi ya Elimu Tanzania. Uteuzi wao umezingatia zaidi uzoefu wa pande hizi mbili, ambapo Taasisi ya Elimu Tanzania ndiwo wanaofanya kazi ya kusimamia, kutafiti, kutathmini, kutunga, na kuboresha mitaala na njia za ufundishaji kuanzia ngazi ya elimu ya awali hadi vyuo ya kati hususani elimu ya ualimu - ngazi ya cheti na stashahada. Kwa upande mwingine, walimu ndiwo watekelezaji wa sera mbalimbali za elimu katika vituo vyao vya kazi. Kwa msingi huu, walimu ndiwo kiini cha mrejesho wa yote yanayotakiwa kutekelezwa mashuleni na vyuoni.
Tofauti na ilivyokuwa kwa walimu, mtafiti hakuweza kuonana ana kwa ana na mtaalamu kutoka Taasisi ya Elimu Tanzania kutokana na kilichoelezwa kuwa alikuwa kwenye utafiti, na uandaaji wa bajeti. Hali hii ilimfanya mtafiti kutumia mawasiliano ya barua pepe na simu ya kiganjani ili kufanikisha upatikanaji wa maoni kutoka taasisi hii.
Matokeo kuhusiana na kipengele hiki yanaonyesha kuwepo kwa tatizo la kimawasiliano kati ya Taasisi ya Elimu Tanzania na walimu mashuleni ijapokuwa taasisi “inalipinga.” Kwa mujibu wa taasisi, wadau mbalimbali wa elimu hushirikishwa na kushiriki kikamilifu katika hatua mbalimbali za uboreshaji wa elimu. Wadau wanaotajwa kushirikishwa na kushiriki ni pamoja na: Baraza la Mitihani la Taifa - Tanzania, watunga sera, walimu hususani walioko mashuleni wakifundisha, na wakaguzi wa elimu. Aidha, taasisi hupokea, hutathmini, huthamini na kuzingatia ushauri na mapendekezo kutoka kwa wadau mbalimbali, hivyo “…endapo kuna kipengele hakimo katika muhtasari ni ama hakipaswi kuwekwa katika ngazi husika ya kitaaluma au bado kinajadiliwa ili kuona uwezekano wa kukiingiza au la.” Hii inamaanisha kuwa, hata suala la nadharia za uhakiki linafanyiwa kazi kisayansi bila shaka. Mtaalamu huyu anazidi kufafanua kwamba, kilichomo kwenye muhtasari wa sekondari kinatosheleza mahitaji ya sasa kwani tatizo lipo katika njia za kufundishia na kujifunzia, kama anavyosema:
…kwa sasa njia shirikishi ndiyo inayopigiwa chepuo zaidi, na mwalimu hafungwi na muhtasari kufundisha kitu anachohisi kina tija kwa wanafunzi…. Tena kwa kufanya hivi, mwalimu kama mtekelezaji wa sera na miongozo mbalimbali ya elimu atakuwa ameturahisishia kazi ya tathmini….. Tunachoweza kusema kwa sasa ni kwamba, tatizo si kutokufundishwa nadharia bali namna gani somo hili linafundishwa hata kufikia malengo yaliyowekwa na Wizara pia jamii ya Watanzania…. Nadhani hili ndilo tatizo hasa…. Lakini tafiti zitabainisha…, hata sasa tuko kwenye utafiti… (Hojaji kwa Walimu/ Mtaalamu Taasisi ya Elimu Tanzania).
Pamoja na maelezo haya, bado mtaalamu huyu hakuweza kuthibitisha endapo pana tafiti zilizofanyika au zinazofanyika ili kuhalalisha hoja ya kujitosheleza kwa mihtasari ya Kiswahili, sekondari. Kauli ya kutokumfungia mwalimu katika muhtasari ni njema na inahamasisha ubunifu kwa walimu. Hata hivyo, uhuru kwa mwalimu ni sharti uwe na mipaka maana anaweza kufundisha chini au juu ya kiwango cha maarifa kwa wanafunzi husika (G. Ruhumbika; 2006). Aidha, kwa jinsi mazingira ya elimu yalivyo katika shule nyingi nchini Tanzania, pana hatari ya kuwepo pengo kubwa la kimaarifa miongoni mwa walimu na wanafunzi.
Mathalani, shule nyingi zina upungufu wa vitendea kazi ilhali walimu wakikosa mafunzo ya mara kwa mara yanayoendana na mabadiliko ya nyakati, sera na mitaala. Hali hii inaweza kusababisha “sitofahamu” miongoni mwa wadau wa elimu, lugha, na fasihi walimu wa Kiswahili wakiwemo hata wenye “kudhani” kukosekana kwa nadharia za uhakiki ndiyo tatizo mojawapo la msingi la utegemezi kimtazamo na kiutendaji. Kwa jumla, hoja za mjibu hojaji kutoka Taasisi ya Elimu Tanzania zina mantiki kwani kupitia tafiti mbalimbali - za muda mfupi na mrefu kama alivyosisitiza ndipo kipengele husika kinapoweza kuingizwa au kuondolewa kwenye muhtasari.
Kwa upande mwingine, walimu wanadhani ni vema kipengele hiki kiingizwe kwenye muhtasari wa Kiswahili, kidato cha tatu kwani ndiko uhakiki unaanzia. Kwa mtazamo wao, inakuwa vigumu sana kufundisha jambo ambalo halimo kwenye muhtasari, maana “hata wanafunzi wenye nakala za mihutasari watakushangaa, na kukuliza ‘tunasoma ili nini?’” Kwa mtazamo wao, kipengele cha nadharia za uhakiki hakipewi uzito na Taasisi ya Elimu Tanzania kutokana na sababu mbalimbali, zikiwemo:
a.       Usiasa uliokithiri kwenye eneo la kitaaluma.
b.      Watunzi wa mitaala ama kutokuwa wabobevu katika masomo wanayoyafanyia kazi au walikosa msingi imara katika masomo husika pindi walipokuwa sekondari, hivyo kutokuliona pengo hili toka mwanzo.
c.       Utegemezi wa kiuchumi unaosababisha watanzania wakiwemo Taasisi ya Elimu kutokuwa na maamuzi ya mwisho hususani yanayotoka kwa wadau wa ndani, hasa walimu.
d.      Kuwepo kwa mawasiliano hafifu kati ya vyuo vya ualimu, sekondari na Taasisi ya Elimu Tanzania, pia Tume ya Vyuo Vikuu.
e.       Kuwepo kwa mfumo wa elimu usio rasmi “unaoonekana kupendwa sana na wanajamii… mfumo wa kukariri matini na kufaulu vema mitihani.”
Hizi ni baadhi ya sababu (ambazo ni za jumla mno) walizobainisha wajibu hojaji walimu huku wakitoa mifano kadha wa kadha ama kutokana na uzoefu walio nao au kutokana na maelezo kutoka kwa baadhi ya walimu waliowahi kushiriki semina, warsha au vikao vya kutathmini sera na mitaala. Mathalani, mjibu hojaji mwalimu alihoji “inakuwaje mtaala au kitabu kipitie mikononi mwa wadau mbalimbali wa elimu na, au lugha halafu kiwe na makosa chungu mbovu?” Katika kuunga mkono swali hili, mjibu hojaji mwalimu mwingine akatolea mfano wa mwalimu kutoka chuo cha ualimu aliyehudhuria mara kadhaa warsha za Taasisi ya Elimu Tanzania. Kwa mujibu wa mwalimu huyo:
…walijadili na kuzipitia moduli kwa siku mbili mfululizo huku wakipata muda mfupi wa kupumzika. Wakaainisha mapungufu lukuki lakini baada ya warsha, mmoja wa wawakilishi kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi akamwambia, ‘unajua tunachokifanya hapa ni kama kukamilisha ratiba tu kwani tayari wazee wamekwishazipitisha…, na tarehe ya kuanza kuzitumia ishapangwa!’… (Hojaji kwa Walimu/ Mtaalamu Taasisi ya Elimu Tanzania).
Pamoja na walimu kutoka vyuo cha ualimu kutokuwa sehemu ya utafiti, baada ya kukutana na taarifa hii, mtafiti hakuwa budi kuwatafuta na kuonana na walimu ambao waliwahi kuhudhuria mara kadhaa warsha za Taasisi ya Elimu Tanzania. Nao bila ajizi walikiri kukutana na kauli za namna hii kutoka ama kwa wawakilishi wa wizara au taasisi ya elimu. Hata hivyo, walibainisha kuwa uthibitisho pekee wa yale wanayoyasema utapatikana tu kupitia mtafiti kuwa sehemu ya watendaji wa wizara ama taasisi ya elimu au kushiriki makongamano, na warsha mbalimbali za taasisi hizo kwa sababu nje ya hapo “…. hakuna mtendaji hata mmoja anayeweza kuthibitisha mambo haya hadharani, hakuna! Unadhani …. Unadhani nani yuko tayari kibarua chake kiote nyasi? Hii ndiyo Tanzania ndugu yangu!” mmoja wao alihitimisha maelezo yake.
Hata hivyo, mtaalamu kutoka Taasisi ya Elimu Tanzania alikana kutokuwepo kwa matukio ya namna hii ijapokuwa alikubaliana na hoja za ufinyu wa rasilimali fedha na tatizo la mawasiliano duni kwa baadhi ya wadau. Katika haya mawili mjibu hojaji kutoka Taasisi ya Elimu Tanzania anasema:
…. Walimu hawasemi ukweli…. Fedha ni tatizo la msingi. Semina hutolewa kila inapowezekana ingawa wakati mwingine tunawaseminisha walimu na wakaguzi wachache ili wakawaelimishe wenzao lakini baadhi yao wakifika huko hawatekelezi maagizo waliyopewa. Hata hivyo, semina na mafunzo yametolewa kwa shule za msingi karibu nchi nzima. Kwa sekondari mfano kanda ya ziwa, tayari Mwanza tumetekeleza hili…. Fedha ikipatikana tutaendelea na maeneo yaliyobaki.
Kwa jumla, sababu zilizotolewa na wadau hawa zinaweza kuthibitishwa kisayansi kwa tafiti za kina zaidi. Kwa vile utafiti una kipengele cha jaribio, bila shaka kitaweza kutoa picha kamili kama nadharia za uhakiki zinapaswa kuingizwa au kutokuingizwa kwenye muhtasari wa Kiswahili, sekondari.

4. 3. 1. 2 Ufundishwaji wa Nadharia za Uhakiki wa Fasihi ya Kiswahili Katika Shule za Sekondari Nchini Tanzania

Tathmini ya namna mada hii inavyofundishwa katika shule za sekondari nchini Tanzania ilianza kwa kuwahoji (kupitia hojaji) mtaalamu kutoka Taasisi ya Elimu Tanzania, wanafunzi, na walimu wajibu hojaji/ jaribio la utafiti wapatao 25 (Taasisi ya Elimu Tanzania mmoja, Wanafunzi ishirini, na Walimu wanne) ili kujua iwapo mada hii hufundishwa mashuleni ama la. Katika kulijibu swali lihusianalo na kipengele hiki, jumla ya wajibu hojaji 24, sawa na asilimia 96 walijibu Ndiyo, ilhali mjibu hojaji mmoja sawa na asilimia nne akijibu Hapana. Hata hivyo, jibu la Ndiyo linatofautiana na majibu ambayo wajibu hojaji/ jaribio la utafiti waliyatoa walipotakiwa kubainisha endapo wamewahi kuzisikia nadharia zozote za uhakiki wa fasihi ya Kiswahili kama vile U - Marx, Umbuji, na Ufeministi. Mchanganuo wa majibu ulikuwa kama ifuatavyo:
i.                    Wajibu hojaji wataalamu wa Kiswahili, yaani walimu wanne na mtaalamu kutoka Taasisi ya Elimu Tanzania walisema wanazijua kwani wamejifunza chuoni.
ii.                  Wanafunzi watano kati ya 20, sawa na asilimia 25 ya wajibu hojaji wanafunzi wote walisema wamewahi kusikia U - Marx tu, ambao kwa maelezo yao “ni nadharia ya mwanafilosofia (mwanafalsafa) Karl Max juu ya fasihi na jamii.” Lakini, kwa mawazo yao, wakadhani pia dhana ya Umbuji na Ufeministi ni dhana za nadharia ya uhakiki, kama wasemavyo baadhi ya wajibu hojaji/ jaribio la utafiti hawa “niliusikia U - Marx darasani. Umbuji na Ufeministi sijawahi kuzisikia ila nadhani nazo ni sehemu ya nadharia za uhakiki…. Nahisi hivyo!”
iii.                Wanafunzi wajibu hojaji/ jaribio la utafiti 15 kati ya 20 walisema hawajawahi kuzisikia ijapokuwa walijaribu kuonyesha nini wanachofikiri kuhusiana na dhana hizo, kama walivyotakiwa kufanya. Yafuatayo ni baadhi ya mawazo ya wajibu hojaji/ jaribio la utafiti hawa kulingana na kile wanachodhani kuhusiana na dhana hizi:
a.       Wajibu hojaji/ jaribio la utafiti wanne, sawa na asilimia 26.66 ya wanafunzi wajibu hojaji/ jaribio la utafiti 15, walisema hawazijui na hawajawahi kuzisikia mahali popote pale. Lakini kwa mawazo yao, wanadhani ni dhana zisizo sanifu, “nadhani ni maneno ya mkopo yaliyotoholewa toka lugha zingine kwani si maneno sanifu ya Kiswahili mfano, U – Marx muundo ‘- rx’ si muundo wa maneno ya Kiswahili; hatuna mfumo huu wa maandishi katika Kiswahili. Ila nadhani yanaeleweka zaidi hasa kwa watumiaji wa lugha husika,” mmoja wao alisema.
b.      Wajibu hojaji/ jaribio la utafiti sita kati ya 15, sawa na asilimia 40 walikiri kutokuzifahamu na kwamba hawajawahi kuzisikia popote zikitajwa ila kwa fikra zao, wanahisi kuwa zinaweza kuwa ni nadharia za uhakiki, kama asemavyo mjibu hojaji/ jaribio la utafiti huyu, “nadhani hizi ni uhakiki. Nadhani ni dhana mbalimbali zinazohusu nadharia ya uhakiki. Nadhani hivyo, ila sina uhakika kama niko sahihi.”
c.       Wajibu hojaji/ jaribio la utafiti wawili kati ya 15 sawa na asilimilia 13.33 wanakiri kutokuzijua kabisa na hawawezi kufikiria ni vitu gani, kama asemavyo huyu “sijui ni nini maana sijazisikia kabisaaa.”
d.      Wajibu hojaji/ jaribio la utafiti watatu kati ya 15 sawa na asilimia 20 wanasema kuwa hawajawahi kuzisikia dhana hizi na walikuwa na yao ya kusema. Mfano, mmojawao anasema:
kitu cha muhimu ni kufanya upembuzi wa kiyakinifu ili kuweza kutambua kama nadharia ya uhakiki inahusika na dhana hizi. Kwa ujumla, Umarx, Umbuji, na Ufeministi sijawahi kuzisikia… nadharia ya uhakiki hufanya mtu/ jamii kufahamu hasa nadharia hii. Hivyo ni muhimu kujifunza kwa undani nadharia hii (Hojaji kwa Wanafunzi).
Majibu haya yanatoa picha kuu mbili tofauti. Picha ya kwanza ni ile yenye kujenga fasili kuwa inaelekea wanafunzi wajibu hojaji/ jaribio la utafiti walio wengi hawajui nadharia za uhakiki ni kitu gani hasa, ingawa wanakiri kuisoma. Swali la msingi liliwataka wataje nadharia za uhakiki wanazozisoma darasani. Kinachojitokeza hapa ni kwamba, inaelekea wanachanganya vitu viwili: nadharia ya/ za uhakiki na dhana ya uhakiki. Picha hii imejitokeza hata katika swali lililowataka watoe tafsiri ya nadharia ya uhakiki. Asilimia kubwa walitoa majibu yanayoelekea kufanana. Majibu yaliyokuwa yakijibu swali “walilolitunga wao;” Uhakiki ni nini? ambapo wengi walianza na neno “uhakiki ni…” badala ya nadharia ya uhakiki ni…? Baadhi ya majibu yaliyotolewa ni pamoja na haya yafuatayo: “…ni uchambuzi na ufafanuzi wa kazi za fasihi ili zilete ujumbe ambao unaifaa jamii,” “… ni hali ya kuhakiki kazi ya msanii,” “… ni kitendo cha kusoma kazi yoyote ya fasihi na kuhakiki lengo lililozungumziwa ili jamii ifahamu.” Majibu haya yanaonyesha umahiri fulani wenye kusadifu uwezo wao katika kuhusisha hoja na jibu la wao kusoma nadharia ya uhakiki. Jambo linaloashiria kuwa mada hii haifundishwi katika mawanda yake mapana.
Kwa Kamusi ya Encarta (2009) nadharia ya uhakiki ni njia au sanaa ya kuchanganua/ kuchambua, kufasiri, na kuhukumu maudhui, ubora, na mbinu zilizomo katika matini ya kifasihi. Tafsiri hii inashabihiana na jibu lililotolewa na mmoja wa wajibu hojaji/ jaribio la utafiti tisa kati ya 20, sawa na asilimia 45 walioweza kutoa maana zinazoelekeana na dhana nzima ya nadharia ya uhakiki, kauli hiyo ilikuwa “… ni sayansi ya uchambuzi na ufupisho wa kazi ya fasihi anayotumia mhakiki kuhakiki kazi ya fasihi.”
Hapa panajenga swali kidogo; inakuwaje asilimia 45 waielezee dhana ya nadharia ya uhakiki kiufasaha ilhali asilimia 55 wakichanganya dhana ya uhakiki, na nadharia ya uhakiki? Je, ni uwezo binafsi wa kuhusisha mambo, ama wanajifunza darasani au ni jitihada binafsi za wao kuchimba na kuibuka na mambo kutoka vitabu mbalimbali vya nadharia? Na kama wanajifunza darasani, ina maana wajibu hojaji/ jaribio la utafiti hawa tisa wana darasa lao tofauti na wenzao 11? Swali hili linapata ugumu kujibika hasa pale panapotokea hoja kutoka kwa mwalimu mjibu hojaji kuwa:
Kwa namna mada hii inavyofundishwa, na kulingana na uhalisia wa mtaala haimpi mwanafunzi ule uwezo wa kuchambua na kupembua mwenyewe kazi za wasanii bali hutegemea yale yaliyohakikiwa tu… (Hojaji kwa Walimu/ Mtaalamu Taasisi ya Elimu Tanzania).
Hali hii inaashiria kuwepo kwa tatizo la msingi katika ufahamu wa wajibu hojaji/ jaribio la utafiti wanafunzi kuhusiana na kile wanachokisema kukisoma au kufundishwa darasani. Hata hivyo, kijumla, uchunguzi wa majibu ya waliosema kuufahamu U - Marx, huku “wakizihusisha” dhana za Umbuji na Ufeministi na nadharia ya uhakiki (asilimia 25), na wale waliosema hawajawahi kuzisikia dhana zote ila wanahisi kuwepo uwezekano wa dhana hizi kuhusiana na nadharia ya uhakiki (asilimia 40), pamoja na waliosema kuwepo kwa hitaji la kufanyika utafiti wa kina ili kubaini kama dhana hizi ni sehemu ya nadharia za uhakiki (asilimia 20) kunajenga asilimia 85 ya wajibu hojaji/ jaribio la utafiti wanafunzi wanaoonyesha “kufahamu fahamu” nadharia ya uhakiki kwa kiasi fulani ingawa hawaonyeshi kujiamini, na majibu ya waliosema hawazijui kabisa inathibitisha kuwa mada hii haifundishwi mashuleni.
Picha ya pili inayojipambanua vizuri zaidi pindi majibu ya wajibu hojaji/ jaribio la utafiti yanapohusishwa na Muhtasari wa Kiswahili, kidato cha tano na sita 2009, maswali ya mtihani wa taifa wa Kiswahili ­ karatasi ya pili kuanzia 2006 hadi 2010, mihtasari ya maandiko ya mwalimu na mwanafunzi wa somo la fasihi ya Kiswahili, azimio la somo, vitabu vinavyotumika kufundishia fasihi ya Kiswahili, na namna ya ufundishaji wa nadharia ya uhakiki wa fasihi ya Kiswahili, pasipo kuwepo shaka, inaonyesha kuwa nadharia za uhakiki si sehemu ya mada au mada ndogo wanazosoma. Hii ndiyo kusema, nadharia mbalimbali kama vile U - Marx, Umbuji, Usasa, Usasa leo, Ufeministi na kadhalika, zinazopaswa kujenga mada ya uhakiki kama ilivyotajwa na wajibu hojaji/ jaribio la utafiti si sehemu rasmi ya Muhtasari wao, na hivyo, hazifundishwi ila kwa “hisani” ya mwalimu husika.
Uchunguzi unaonyesha hazifundishwi kwa uwazi bali hutajwa mfano, U - Marx, Umbuji, Usasa, na Ufeministi pindi mwalimu anapofafanua jambo linalomsababisha kufika kuzitamka, yaani ni kama “bahati tu.” Bila shaka wajibu hojaji/ jaribio la utafiti watano waliosema kuusikia na kuujua U - Marx ni matunda ya walimu wao kuzisoma chuoni, hivyo “kujikuta” wakizitaja japo kwa nadra. Na huku ndiko kusema kwamba, kutokana na uzingativu wa wajibu hojaji/ jaribio la utafiti hawa wawapo darasani wamejijengea utamaduni wa kutokukubali kupitwa na kila kinachosemwa na walimu wao hata kama ni “kwa bahati mbaya,” bila shaka.
Hoja hii inafungamana kwa kiasi fulani na kauli za wanafunzi wajibu hojaji/ jaribio la utafiti 15 (75%) kati ya 20 waliokiri kuwepo kwa upungufu makubwa katika eneo la mada za kiswahili, vitabu vya fasihi, na walimu wa fasihi wanapohusianisha na kitendo cha wao kutokuzisikia au kuzifahamu nadharia za uhakiki. Kwa mfano, kauli zifuatazo zinasawiri tatizo hili, “pana uhaba mkubwa wa vitendea kazi kama vile vitabu tofauti tofauti vya waandishi tofauti tofauti…,” “nadharia ifundishwe kwa mapana yake… pawe na wataalamu wengi sana wenye umahiri sana ili iweze kueleweka zaidi,” “kinachopasa kufanyika ni kuongeza wataalamu wa nadharia ya uhakiki… na nadharia mbalimbali za vitabu vya fasihi ziongezwe kwa wanafunzi,” “… waandaliwe vema wataalamu wa fasihi wa kutosha, wakiwa na mahitaji yote muhimu ya kufundishia kwani walimu wetu wanatumia kitabu kimoja kufundishia, na katu haongezi wala kupunguza kilichoandikwa… hii itasaidia kupanua kufikiri kwa wanafunzi,” na “… kufanya tahakiki mbalimbali na utafiti wa kina, na kuweza kukutana na wataalamu wazuri na wahakiki mbalimbali wa fasihi .”
Mawazo haya ni sehemu ya ushahidi unaothibitisha hoja ya baadhi ya wanazuoni wa fasihi ya Kiswahili inayotaka hatua za haraka kuchukuliwa “kuinusulu” taaluma ya fasihi kwani inafundishwa kimafamba mafamba (Haji; 1981). Mathalani, haiwezekani kwa mwalimu mwenye shahada na amesoma fasihi ya Kiswahili kushindwa kuzihusisha nadharia katika ufundishaji wake. Hali hii inaweza kuwa imesababishwa na ama aliandaliwa kuwa mwalimu wa walimu wa fasihi au alizisoma dhana hizi lakini kutokana na kujifungia katika Muhtasari wa Kiswahili pasipo kutanua mawanda ya weledi wake amejikuta “akizisahau na kuzitupilia mbali kabisa” nadharia hizi au ni miongoni mwa wanafunzi ambao hawakuisoma mada ya nadharia ya uhakiki kiufasaha, na hivyo naye hana weledi nayo. Hili la kujifungia katika Muhtasari wa Kiswahili linaweza kuwa na mashiko zaidi kwani walimu wote wanne wamelitaja kuwa moja ya sababu za kutokufundisha rasmi mambo mengi zaidi zikiwemo dhana mbalimbali za nadharia ya uhakiki. Baadhi ya kauli zao ni pamoja na hii:
Elimu tuipatayo vyuoni haiendani na kile tunachotakiwa kukitenda darasani. Ukihangaika na ya nje ya muhtasari, ingawa wakati mwingine hata ya ndani huyapi kipaumbele… Lakini siyo siri wakati mwingine unaweza kuwavunjia (kufundisha kiufasaha) wanafunzi madude (maarifa) mazito ili kulinda heshima yako maana hawa watoto wa karne hii ukiwafundisha tu wanachokijua wakati mwingine wanaishia kukudharau, na kwa sisi wa shule za binafsi hali huwa mbaya zaidi kwani unaweza kufukuzwa kazi….
Kwa jumla, wanafunzi wako, wazazi wao, na uongozi wa shule wanapenda ufaulu wa kiwango cha juu pasipo kujua kama mwanafunzi ana uwezo wa kutetea ufaulu wake popote awapo… hata hiyo njia shirikishi utaitekeleza kwa asilimia ndogo tu …. Ndo maana mwalimu unahangaika kuchambua mavitabu na kuwakazania watoto kupitia kwa pamoja mapast paper (mitihani iliyopita) ili kubaini maswali yepi yanayopendwa zaidi na NECTA (National Examination Council of Tanzania/ Baraza la Mitihani la Taifa, Tanzania). Huwezi amini wanafunzi wengi wanashindwa kujibu lile swali la kubaini mbinu za kisanaa…. Na usijeshangaa hata matokeo ya jaribio lako yakawa hayaonyeshi tofauti kati ya aliyesoma na ambaye hakusoma nadharia; kikubwa ni NECTA ndugu yangu… (Hojaji kwa Walimu/ Mtaalamu Taasisi ya Elimu Tanzania).
Hoja ya mwalimu kufanya uhakiki kwa niaba ya wanafunzi inafafanuliwa vema na E. M. Songoyi (1990), mwandishi wa tahakiki iitwayo Looking at Language Three. Tahakiki hii inasadikiwa kuwa miongoni mwa tahakiki maarufu, na ya kipekee zaidi katika miaka ya 1990, kwa sababu “ilikidhi” kwa hali ya juu hitaji la mwanafunzi kufaulu mtihani wa fasihi pasipo hata kusoma au kukiona kitabu teule anachopaswa kukisoma na kukihakiki. Kwa sasa, mwandishi huyu ambaye ni Mkufunzi Mwandamizi katika Chuo Kikuu cha Dodoma, Idara ya Lugha na Fasihi anakiri kutokukipenda kitabu hicho kutokana na athari yake kwa jamii.
Hata hivyo, kwa maelezo yake mwenyewe, kilichosababisha atoe tahakiki hiyo ni mazingira aliyokutana nayo kwenye ajira aliyoipata mwezi Juni (punde alipohitimu masomo yake ya shahada ya kwanza) katika shule moja ya Sekondari Jijini Dar es salaam ambapo alipangiwa kufundisha kidato cha nne, Kiingereza na Kiswahili ilhali wanafunzi hao hawajawahi kusoma masomo hayo kwa muda wa miaka miwili huku ikiwa imebaki miezi minne tu wafanye mtihani wa taifa kuhitimu kidato cha nne. Pamoja na kwamba nadharia ya matendo au pragmatiki ndiyo iliyokuwa ikipewa mashiko zaidi bado vipengele vya migogoro na ujenzi wa jamii mpya na endelevu (Umaudhui) ndivyo “vilivyokuwa” roho na uti wa mgongo wa uhakiki na tahakiki. Mambo haya mawili ndiyo hasa sababu zilizofanya usawiri finyu wa tasnia ya fasihi na uhakiki.
Tahakiki ya Looking at Language Three iliandaliwa kwa kusawiri muhtasari na mitihani ya taifa iliyopita, hivyo kujikita zaidi katika “kujibu swali lolote” litakalohusu uchambuzi wa vitabu teule vya fasihi, hususani dhamira za msingi za miaka hiyo – Suala la ujenzi wa jamii mpya kwa kuzingatia siasa ya ujamaa na kujitegema, falsafa ya maisha, umuhimu wa uongozi bora, na mgogoro au suala la ushairi hususani wa Kiswahili. Matokeo ya mfumo huu uliwafanya wanafunzi wajikite katika kulisoma na kulikariri andiko hili na hatimaye wakafaulu “vizuri” masomo husika, tena kwa kiwango cha juu.
Picha hii inajipambanua tena kwa maelezo ya M. Msokile (1991: 1) pale mwandishi wa makala aghalabu utangulizi wa Miongozo ya Lugha na Fasihi anapoeleza lengo hasa la uandaaji wa matini haya, mfano wa Looking at Language Three. Mwandishi anasema:
Mfululizo huu umebuniwa kutokana na lengo la kuwasaidia wanafunzi wa lugha na fasihi katika ngazi mbalimbali za taaluma zao, hasa wale wanaojiandaa kwa mitihani ya taifa….
Wanazuoni hawa hawapaswi kulaumiwa kwa hatua walizozichukua katika nyakati zao. Bila shaka, uamuzi wao ulizingatia mazingira ya wakati huo ili kukidhi “ombwe” la kiuandishi katika tasnia za uhakiki wa maandiko na fasihi kwa jumla. Kwa baadhi ya Wanazuoni, wakati huu unaweza kutajwa kuwa wakati muhimu ambao somo la Kiswahili lilikuwa likipita katika kipindi cha kuimalika – kitaaluma, kiuhakiki, kifalsafa, na kilugha.
Uthibitisho makini wa hoja hii ya kutokuwalaumu wanazuoni wa wakati huo inajidhihirisha tena katika M. Msokile (1991: 1) ambapo tahadhari inatolewa kwa wasomaji wa matini ya kihakiki yakiwemo makala ya Miongozo ya Lugha na Fasihi, na mengine kama vile Looking at Language Three. Tahadhari hiyo inasema:
Wakati wa kusoma miongozo hii, mambo muhimu yanayotakiwa kuzingatia ni pamoja na haya yafuatayo:
i.        Kabla ya kusoma mwongozo wowote ule, inampasa mwanafunzi asome kwanza kazi ya fasihi inayohusika.
ii.      Kilichoandikwa katika mwongozo wowote kisichukuliwe kuwa ni sawa na maandiko matakatifu kama vile Quran Tukufu au Biblia Takatifu. Msomaji una nafasi kukubali au kukataa maoni yaliyomo katika mwongozo unaohusika.
iii.    Msomaji una nafasi ya kutoa uchambuzi na uhakiki mpana zaidi kuhusu kitabu kilichohakikiwa.
iv.    Msomaji ihusishe kazi ya fasihi na mazingira ambamo watu walioandikiwa wanayaishi. Jifanye kama yanakukuta utayatatuaje?
Mwishoni mwa mwongozo wowote kuna maswali ambayo yanasaidia kupanua welewa zaidi kwa mwanafunzi na msomaji wa kawaida. Msomaji aghalabu yuko huru kuijadili kwa mapana zaidi kazi inayohusika.
Pamoja na maelekezo haya, bado mwandishi hakubainisha nadharia ya/ za uhakiki i/ zitakayotumika katika uchambuzi wake uliohusu diwani ya E. Kezilahabi, Karibu Ndani. Utamaduni wa kutokubainisha kwa wazi aina ya nadharia ya uhakiki itakayotumika kuchambua kazi ya fasihi umejitokeza katika tahakiki mbalimbali za kifasihi ikiwemo ya M. Msokile na T. S. Y. Sengo (1987), pia J. A. Masebo na N. Nyangwine (2007). Hata hivyo, laiti tahadhari hii ingeweza kuwafikia, kusomwa na kuzingatiwa na wanafunzi wote bila shaka, hali ya kutegemea tahakiki isingekuwepo au ingekuwa imepungua kwa kiasi kikubwa.
Ushahidi unaotokana na uchunguzi katika utafiti huu ulibaini kuwa, maandiko mengi ya miaka ya 1990 kurudi nyuma, yakiwemo ya E. M. Songoyi na M. Msokile ni ama hayapatikani kirahisi mashuleni au kama yanapatikana ni kwa uchache tena yakiwa katika hali isiyoridhisha kutokana na matunzo duni. Jambo linalowafanya wasomaji wengi, hususani wanafunzi kuyapuuza huku baadhi yao wakitoa kauli za kejeli kama vile “sitaki mafua na TB za kujitakia,” na “yellow notice hizo, nani asome?” Yaani, haiwezekani mtu kusoma karatasi zilizobadilika rangi kutoka weupe na kuwa manjano au kahawia. Wasemaji wa kauli hizi kwa kiasi fulani wanasahau kuwa vya kale ni dhahabu; na tena si vyote ving’avyo ni lulu.
Kimantiki, mwanafunzi au mwalimu mzuri anapaswa kuwa mbunifu, tena wa hali ya juu. Kwa mujibu wa mtaalamu toka Taasisi ya Elimu Tanzania hata kama Muhtasari hauonyeshi kama kunapasa kufundishwa nadharia za uhakiki, lakini uzoefu au utafiti (hata kama si rasmi) wa mwalimu ukaonyesha kuwapo tatizo la msingi, pasipo kuchelewa mwalimu anapaswa kuchukua hatua za haraka na stahiki kadri ya miongozo inayotolewa. Hoja inayoungwa mkono na M. Msokile (1995).
Kwa maneno mengine, hitaji la wanafunzi kufaulu vizuri mitihani na changamoto zingine wanazokutana nazo ndani na nje ya darasa, havitibiwi kwa kuwakaririsha wanafunzi. Tiba sahihi, pamoja na mambo mengine, mwanafunzi anapaswa kunolewa vema zaidi katika masomo husika. Na moja ya maeneo yanayopaswa kuwekwa sawa bin sawia ni eneo la uhakiki kama mmoja wa wajibu hojaji/ jaribio la utafiti anavyotanabaisha pindi alipoelezea uhusiano wa nadharia na uwezo wa mwanafunzi kujitegemea kivitendo na kimtazamo:
Nadharia ya uhakiki inachimbua ulimwengu mzima, matatizo, changamoto zinazojitokeza katika jamii na namna ya kuepukana na matatizo au changamoto hizo mbaya. Nadharia hujenga msingi wa kupata ujumbe uliozungumzwa… (Hojaji kwa Walimu/ Mtaalamu Taasisi ya Elimu Tanzania).
Mtazamo huu unaelekea kuungwa mkono na mjibu hojaji/ jaribio la utafiti mwingine asemaye:
Pamoja na kwamba mada hii haipo, bado naamini ikifundishwa vizuri, na tukapewa mazoezi mengi na ya kutosha ya kuhakiki kazi mbalimbali kutatusaidia kujitegemea na kuepa desturi ya kutegemea tahakiki za wahakiki wengine (Hojaji kwa Wanafunzi).
Suala hapa si kuepa desturi ya kutegemea tahakiki, bali kuepa desturi ya kuzigeuza tahakiki kuwa alfa na omega kwa kila akifanyacho mtu.  Tahakiki ni sehemu mojawapo muhimu ya marejeleo kama yalivyo marejeleo mengine ya kifasihi katika kujenga jamii ya watu weledi na wenye stadi stahiki katika kuzikabili nyanja za maisha. Kwani kupitia tahakiki, msomaji anaweza kulinganisha na kulinganua mawazo na kuyatathmini kwa namna ya pekee sana hata kufikia kujenga hoja yake. Howard Gardner (1982: 261) anaelekea kuikubali hoja hii kwa kusema:
I take issue with books that purport to teach people to think better – laterally, generatively, creatively … one can be transformed from what Johnson called “a harmless drudge” into an individual of superior thinking powers.
Ninalichukua jambo kwa kulitathmini kupitia vitabu vinavyolenga kufundisha watu kufikiri vizuri zaidi – kwa kuleta mabadiliko ya muono wa kimukitadha, kivizazi, kiubunifu…. Mtu anaweza kubadilishwa kutoka kile Johnson anachokiita “umaamuma wa stadi za kazi” hadi kuwa mtu mwenye uwezo mkubwa wa kufikiri (Tafsiri ya mwandishi).
Hata suala la wanafunzi kushindwa kujibu vizuri swali la mbinu za kisanaa au usanifu wa maandishi (Mtihani wa Kiswahili, Taifa, Karatasi ya pili: Sehemu E) halitakuwa tatizo la msingi mashuleni. Kimsingi, swali hili linajibiwa vema na Umbuji. Yaani, huwezi kujibu kiufasaha swali la usanifu wa maandishi kama hutajitajirisha kifasihi kwa kuuzamia Umbuji. Umbuji umejikita zaidi katika kipengele cha fani, kinachoundwa na zana (i. e nyenzo) mbili - Muundo na Mtindo. Na ndani ya mtindo ndimo mna kipengele cha mbinu za kisanaa. Huku ndiko kusema kuwa, utajiri uliomo katika Umbuji kwa fani ya fasihi ya Kiswahili endapo, na endapo tu utafungamanika na ule uliomo katika Umaudhui, U - Marx ukiwemo, utazidi kuchochea ubunifu, kujitegemea na weledi wa walaji wa taaluma ya fasihi ya Kiswahili na taaluma zingine.
Majibu ya hojaji na mjadala wa juu vinashikamana kwa kiasi kikubwa na matokeo ya uchunguzi yaliyopatikana katika shule hizi tatu. Uchunguzi umebaini kuwa, wanafunzi na walimu wanatumia tahakiki moja tu na kitabu kingine kimoja cha nadharia ya fasihi kwa jumla, ambacho kimegusia kwa ufinyu nadharia za uhakiki; vyote hivi vikiwa vya mwandishi mmoja. Kinachopewa uzito katika kitabu cha nadharia ni mada ya fasihi kwa jumla, ambayo ni sehemu mojawapo katika mtihani wa taifa (Sehemu A). Kwa maneno mengine, wanafunzi wanasomea zaidi mtihani wa mwisho kuliko kupanua mawanda ya maarifa yao. Ina maana kuwa shule zitaweza kufundisha na kuzingatia nadharia za uhakiki endapo, na endapo tu kutakuwa na mada, na swali la nadharia za uhakiki katika Muhtasari na mtihani wa taifa.
Aidha, uchunguzi umebaini kuwepo kwa matini yasiyojulikana hata waandishi wake ilhali yakiwa na mawanda finyu ya nadharia za uhakiki wa fasihi. Mathalani, kitini kimoja kisichokuwa na jina la mhakiki wala mwaka wa uchapishwaji kinataja ya kuwa Jina la Kitabu ni kipengele kimojawapo cha msingi katika maudhui. Kimantiki, Jina la Kitabu haliwezi kuwa kipengele cha maudhui kwa sababu, kwa ufupi, jina la kitabu ni muhtasari wa mambo yaliyomo katika kazi ya fasihi. Jina la kitabu linaweza kuumbwa au kuteuliwa kutokana na haya yafuatayo:
i.   Jina la Mhusika, aghalabu mhusika mkuu, kwa mfano Shida, Kinjekitile na Rosa Mistika.
ii.  Jina la Mandhari, Mazingira au Muktadha teule, kwa mfano Kisima cha Giningi, Kusadikika, Kufikirika, na Gambushi.
iii.   Dhamira au ujumbe, hususani dhamira kuu au ujumbe mkuu. Kazi nyingi za fasihi ya Kiswahili zimetumia kigezo hiki katika uteuzi wa majina, kwa mfano Gamba la Nyoka, Kivuli Kinaishi, Nagona, na Janga Sugu la Wazawa.
iv.    Mchanyato wa vigezo ama viwili au vyote vitatu vya awali, yaani Jina la Mhusika na Dhamira / Ujumbe Mkuu (kwa mfano, Ngoswe – Penzi Kitovu cha Uzembe, Mashetani, na Pili Pilipili), au Jina la Mandhari / Mazingira / Muktadha teule na Maudhui / Ujumbe / Mhusika (kwa mfano, Kwa Heri Iselamagazi, na Jogoo Kijijini na Ngao ya Jadi).
v.    Mbinu nyingine, aghalabu sifa za kifani na kimaudhui, kwa mfano Barua Ndefu Kama Hii na Hawala ya Fedha.
Kwa kuvichungua vigezo hivi bila shaka, taswira inayopatikana hapa ni ya kwamba uteuzi wa jina la kitabu unaweza kuwa wa kigezo / vigezo vya kifani pekee ama vya kimaudhui pekee au vya mchanganyiko. Kwa mtalaa huu, si busara kuweka uteuzi wa jina la kitabu kama kipengele cha kimaudhui. Kwa mtazamo wangu, kipengele hiki kijitegemee, yaani kisiwe chini ya fani wala maudhui ijapokuwa kama pana ulazima wa kukijadili basi kijadiliwe katika namna kinavyoikamilisha au kinavyoibeba dhana nzima ya mwandishi.
Haya ndiyo mazingira halisi yanayowakabili wanafunzi walio mashuleni. Upatikanaji wa matini yasiyo na ubora, lakini yanayopatikana kirahisi na kwa bei nafuu si tu kunaathiri taaluma ya uhakiki bali pia kunaviza uwezo wa wanafunzi kuchambua, kutafakari, kuhusianisha, na kuhoji mambo wanayokumbana nayo ndani na nje ya darasa. Kwa msingi huu, pamoja na hitaji la kuwepo walimu wa Kiswahili, bado haliepukiki hitaji la kuwapo na kufundishwa kiufasaha nadharia za uhakiki wa fasihi ya Kiswahili.
Hata kama shule zitapewa vitabu vya kutosha na kuwa na wataalamu wa nadharia za uhakiki wa hali ya juu kama walivyopendekeza baadhi ya wajibu hojaji/ jaribio la utafiti, suala la mada hii kufundishwa au kupewa kipaumbele bado litakuwa tete kwani inavyoelekea kiini cha mfumo wa upimaji wanafunzi ndicho kinachowafanya wahusika kutoa au kutokutoa uzito kwa mambo mengi (ikiwemo nadharia za uhakiki wa fasihi ya Kiswahili) ambayo hayajaainishwa katika Muhtasari.
Kwa mfano, asilimia 35 ya wanafunzi wajibu hojaji/ jaribio la utafiti wanaihusisha nadharia ya uhakiki na fasihi kwa jumla, huku asilimia 50 wakiihusisha na fani na maudhui, nayo asilimia 15 wakiihusisha na kipengele cha uhakiki na mhakiki. Bila shaka utofauti huu unatokana na uzito finyu inayopewa mada hii pindi inapofundishwa au haifundishwi kabisa, au hufundishwa kwa kudonolewa tu. Hili la udonoaji linaweza kuwa na nafasi kubwa pamoja na lile la uzito finyu.
Uzoefu alioupata mtafiti katika kipindi chote cha uchunguzi wake unaonyesha kuwa nadharia za uhakiki kama vile U - Marx na Ufeministi hutamkwa kwa nadra sana toka vinywani mwa walimu pindi wanapofafanua dhana au jambo linalohusu maudhui, hasa masuala ya nafasi ya mwanamke na ukombozi. Mfano wa kauli zenye kutaja nadharia za uhakiki ni pamoja na hii:
…. lazima mjue kuwa suala la ukombozi hasa wenye kulenga matabaka, usawa, haki, umoja na mshikamano ni mambo yaliyosisitizwa na Karl Marx…. Siku hizi jamii nayo wamekuja na hoja ya kumnyanyua mwanamke. Bila kumjadili mwanamke katika muktadha wa kumpetipeti huku ukimburuza kizushi mwanamme, nakwambia utaambulia alama kichele, shauri yenu….! Mi simo (Uchunguzi wa Mtafiti).
Katika muktadha huu, wanafunzi wadadisi wangeliweza kumuuliza mwalimu kuhusu Karl Marx na kwa nini jamii ijadili au izungumzie nafasi ya mwanamke katika jamii. Lakini pia, kwa wanafunzi wadadisi wangelikwenda kutafuta vitabu ili kuyajua haya kwa undani zaidi, jambo ambalo halikufanyika. Badala yake waliishia kucheka na kutaniana; waliona ni mzaha. Inaelekea kwa wao, hoja ya mwalimu ilikuwa kuwatahadharisha dhiki ya ujenzi mbovu wa hoja na vitu gani wanavyopaswa kuvizingatia katika kujibu maswali ya fasihi na uhakiki. Kwa mujibu wa K. Daniel (1997: 478) na J. S. Madumulla (2006) jadi ya kujituma katika uga wa taaluma unamsaidia msomaji au mtaalamu kuchuja mambo na kuyafanyia kazi kwa mawanda mapana zaidi. Huku ndiko kusema kwamba, udadisi wa mambo, mathalani kwa njia ya kujifunza kupitia usomaji, humfanya mtu kutobaki maamuma. Kauli hii inashabihiana na mafundisho ya kidini yasemayo, “mtu yeyote anapoingia kwa kumaanisha katika ulimwengu wa kumjua Mungu, hakika hatobaki kama alivyoingia.” Hoja hii inaungwa mkono na The World Book (1986: 16, 112) wanaposema:
… some of the materials will not coincide with what you are studying in a particular class. But, you can use the lists to get ideas that can be applied to other topics that you are studying. Use them as springboards for your own thinking … the more you write, the better your writing skills will become ….
…. Baadhi ya matini hayatukizi kile unachokisoma katika darasa husika. Lakini utayatumia kupata na kutanua wazo au mawazo utakayoyafanyia kazi katika mada/ miktadha mingine ya kujifunza kwako. Katu usiyapuuze matini haya hata kidogo; yatumie kama mihimili ya kujenga stadi za kufikiri kwako…. Kadri unavyoandika, ndivyo unavyojenga stadi bora ya uandishi… (Tafsiri ya mwandishi).
Hoja wanayoitoa The World Book inaihamasisha jamii kuukumbuka usemi wa wahenga usemao, “jambo usilolijua ni kama usiku wa kiza kinene.” Kupuuza kitu ni hatari sana katika hatua yoyote ile ya mapambano dhidi ya kufikia kilele cha ndoto za mafanikio. Wapo wanazuoni wanaoamini kuwa kusoma ni vita kali, tena isiyo na mwisho. Bila shaka ndiyo uliokuwa mtazamo wa baba wa taifa, hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ambaye aliuita ujinga kuwa adui mmojawapo wa maadui wakuu wa taifa la Tanzania (S. N. Nyirenda, & A. G. M. Ishumi; 2007). Kama hivi ndivyo, kauli ya kujikita katika kusomea mtihani ni kidonda kinachohitaji tiba mahususi, tena ya dharura. Narudia kusema, mwanafunzi kusoma mambo kadha wa kadha yaliyomo ndani na nje ya Muhtasari kiufasaha katu hakuwezi kumfanya ashindwe mtihani. Kinachosababisha ashindwe ni pamoja na: utegemezi wa tahakiki hasa ya aina moja, uhaba wa vitendea kazi bora, na uhaba wa wataalamu weledi katika mengi.
Uchunguzi ulishuhudia pia vipindi vya somo la Kiswahili, Karatasi ya Pili vikitawaliwa na uwasilishaji wa kazi na mijadala kama njia kuu ya ufundishaji. Kwa sehemu kubwa mfumo huu ulilichangamsha somo. Hata hivyo, baadhi ya wajibu hojaji/ jaribio la utafiti walizitegemea tahakiki kwa asilimia miamoja. Yaani, uwasilishaji wao ama kwa maandishi au maelezo ulibeba neno kwa neno kutoka tahakiki inayotegemewa katika kujifunza kwao. Katika taaluma ya Komputa, tungeweza kusema kuwa wajibu hojaji/ jaribio la utafiti hawa walifanya kazi ya kunakili au kukata andiko kisha kulibandika kwingine, jambo ambalo halikuweza kupingwa wala kukemewa na ama wanafunzi wenyewe au mwalimu wa somo.
Katika kulitafutia ufumbuzi suala hili, majibu yafuatayo yalitoka kwa baadhi ya wanafunzi wajibu hojaji/ jaribio la utafiti: “sasa kaka, we unadhani tungefanyaje? Ukiwaning’iniza leo labda we usije wasilisha milele maana siku hiyo patachimbika…,” “… mwalimu mwenyewe huwa anaona lakini hunyamaza, sasa siye tufanyeje?” na “si kwamba hatujui kuwa haturuhusiwi kunakiri ila watu ni wabishi wabishi (anasita kidogo, kisha anashusha pumzi nzito)! Hawataki sikia; mbona mwalimu husema sana tu!” Hoja ya tatu inashabihiana na kauli ya mwalimu aliyesema:
Unajua watoto wa siku hizi hawasikii. Tunapiga kelele sana kila kukicha lakini wapi. Kilichobaki ni kujikalia na kubaki mtazamaji tu, ufanye nini sasa? Anayekusikia unakwenda naye. Asiyekusikia unafunika kombe mwanaharamu anapita… wazazi wao na serikali wapo watawafundisha labda watawasikia hao. Si wajua asiyefunzwa na mamaye hufunzwa na ulimwengu? (Uchunguzi).
Kinachojitokeza katika majibu haya ni kuwapo kwa tatizo la kinidhamu na kitaaluma kwa baadhi ya wanafunzi, hivyo kuathiri ushirikiano na mawasiliano chanya miongoni mwao, pia kwa walimu wanaowafundisha. Jambo linaloashirikia kwamba baadhi ya walimu wamekata tamaa na hawajui nini cha kufanya juu ya mapungufu yanayoendelea madarasani. Kwa upande mwingine, inavyoelekea, suala la mijadala kwa baadhi ya wanafunzi ni ufahari au suala la kialama zaidi. Yaani, baadhi ya wanafunzi hawajiamini wala kujisimamia katika maamuzi na ujenzi wa hoja hivyo “kutegemea huruma” kutoka kwa wenzao ili uwasilishaji wao usionekane kuwa duni. Hawa daima si ajabu kuwakuta wakitegemea hisani kuishi, kama alivyotanabaisha huyu, “sasa kaka, we unadhani tungefanyaje? Ukiwaning’inia leo labda we usije wasilisha milele maana mkitoka nje au siku yako ikifika patachimbika….”
Kimantiki, mtu anayejiamini, tena mweledi katika ujenzi wa hoja na stadi za maisha katu hawezi kuogopa changamoto zinazomkabili ndani na nje ya darasa; atajipanga vema kuzikabili. Kwa mujibu wa baadhi ya wanasosholojia na wanasaikolojia, mtu kujiandaa ni jambo lisilopingika kwani humsaidia kujiamini, na hivyo kupunguza kama siyo kuondoa hofu au shinikizo la kiafya na kadhalika ijapokuwa, haipaswi pia kujiamini kupita kiasi.
Utamaduni wa “changu kuwa bora zaidi, tena chenye ukamilifu mkamilifu, hivyo hakipaswi kupingwa au kurekebishwa na mtu,” ni hatari katika nyuga zote za kiafya, kimaadili, kiuongozi, kitaaluma na kadhalika. Tatizo hili la wanafunzi kuogopana, bila shaka linatokana na ama uelewa duni wa wanafunzi dhidi ya haki, wajibu na misingi ya kuwepo kwao shuleni kama wanafunzi au ni tatizo la kinidhamu, vivyo hivyo kwa mwalimu. Kwani uwasilishaji wa kazi mbele ya darasa huambatana na kuuliza na kufafanua hoja kwa mantiki ya kujenga uwezo wa kujisimamia, kujenga hoja bora, kuelimishana na kupanuana kifikra.
Katika hili, mfumo wa elimu na ufundishaji havina budi kujenga mawasiliano chanya miongoni mwa wanafunzi wenyewe, na wanafunzi na walimu. Na moja ya njia za kujenga mawasiliano hayo ni kutoa semina elekezi ikifuatiwa na mazoezi mbalimbali ya kimijadala kabla somo lengwa halijaanza kufundishwa rasmi. Huku kutasaidia wanamjadala kutambua majukumu yao kama wanafunzi, wataalamu, wazazi au walezi tarajari kwa maisha yao binafsi, familia zao, jamii zao, na taifa lao kwa jumla. Kwa kuyajua haya, bila shaka hawataogopa kuhoji au kushiriki kikamilifu katika mijadala kwa sababu tu, “siku nitakayowasilisha nisije kupata wakati mgumu kutetea hoja zangu.” Katika kuliona hili F. E. M. Senkoro (1988: 3) anashauri:
... kuwepo kwa makundi… usijekuwa uhasima kati ya wahakiki na wahakiki, au wahakiki na wasanii, bali wanahitaji kufikiria maendeleo yao na ya jamii yao katika muktadha halisi wa jamii zao.
Hoja hii inaturejeleza katika kuyachungua maisha kwa kuzingatia misingi na hatima ya jamii inayotegemea faida ya kusoma na kusomesha. Kukata tamaa kwa mwalimu na mwanafunzi waliotoa kauli ya kutokujali kile kinachoendelea darasani, kwa fikra finyu na majibu mepesi ni kuwa mwalimu ameshindwa kulimudu darasa. Lakini kitathmini, hii si ishara ya mwalimu kushindwa bali ni kushindwa kwa taifa zima kuzikabili changamoto za elimu, kwani kidole kimoja hakiwezi kuvunja chawa.
Kwa mujibu wa tafiti mbalimbali zilizo na zisizo rasmi, inaelekea kuwa matokeo mbalimbali ya mitihani ya taifa   kwa baadhi ya nyakati na watu, hayaonyeshi uhusiano wa moja kwa moja kati ya uwezo wa mwanafunzi darasani (katika maendeleo yake ya kila siku shuleni – mazoezi na mitihani) dhidi ya ufaulu wake katika mtihani wa taifa. Huku ndiko kusema, mtu asishangae hata kwa hawa wanaokata au kunakili tahakiki kuona wakifaulu, tena ufaulu wa kishindo. Kwani hakuna tahadhari inayochukuliwa na Baraza la Mitihani la Taifa kudhibiti utamaduni wa kuhamisha hoja kiwizi. Kwa Baraza, wizi kwao unaelekea kuwa ni ule wa kuiba na kuandaa majibu ya mtihani uliotungwa na kuandaliwa kufanyika katika wakati uliopangwa. Hivyo, wizi wa matini bila shaka si wizi kwao. Na hii inaweza kuwa moja ya sababu zinazosababisha baadhi ya wanafunzi kuendelea kukariri na kucheua jambo/ mambo kama lilivyo/ yalivyo. Hawataki taabu; Hawataki shida. Wanachotaka ni kufikia malengo yao, hata kama njia watakazozitumia zitafanikiwa au la.
Hata hivyo, bado pana changamoto ya vitendea kazi vya kutosha na vyenye ubora. Uchunguzi ulibaini kuwepo kwa kitabu kimoja cha tahakiki, na kimoja cha nadharia; vyote vikiwa vya mwandishi mmoja. Vitabu hivi ndivyo vinavyotumika katika shule zote tatu – kwa walimu na wanafunzi. Hali hii inajenga wasiwasi katika kumwandaa mwanafunzi na mtaalamu wa fasihi ya Kiswahili kikamilifu. Kwani, endapo mwalimu ni mdau au muumini wa kitabu hicho bila shaka, atawaambukiza wanafunzi imani hiyo hata kuwafanya wafikiri kuwa mwandishi husika ndiye mpishi bora na wa mfano katika uga wa fasihi ya Kiswahili. Na huku kunaua uwezo wa kulinganisha na kulinganua mambo kwa ustadi mkubwa.
Ushahidi unaojitokeza katika majibu yaliyotolewa na wanafunzi wajibu hojaji/ jaribio la utafiti 20, unaonyesha kuwa jumla ya wajibu hojaji/ jaribio la utafiti 18, sawa na asilimia 90 waliitaja tahakiki ya J. A. Masebo na N. Nyangwine (2008) kuwa tahakiki na kitabu tegemeo kwa wao kujifunza na kurejelea hoja. Jambo ambalo si baya! Ubaya ni athari wanazoweza kuzipata kupitia hoja na maelekezo kutoka kwa waandishi hawa. Majibu mengine yalikuwa kama ifuatavyo:
i.                    Kiswahili II: kidato cha 5 na 6 kilichoandikwa na JPD Company General Ltd. (5%).
ii.                  Tahakiki ya Sarufi ya Kiswahili, TAKILUKI, SAMAKISA. (5%)
iii.                Hakuna (30%).
iv.                 Sijui (35%).
v.                   Tahakiki za TUKI, Msabila, na Nyambari (5%)
vi.                 Tahakiki hizi za kawaida kama za Kadeng’e (Kadeghe?) (5%).
vii.               Tahakiki za Riwaya, Tamthiliya, Ushairi, na nadharia ya fasihi kwa jumla (5%).
viii.             Riwaya, Tamthiliya, na Ushairi (5%)
ix.                 Tahakiki ya Kiswahili na fasihi kwa jumla (5%).
Kwa kiasi fulani, majibu haya yanaonyesha mkanganyiko wa hali ya juu kwa sababu baadhi ya “vitabu” vinavyotajwa kuwa ni tahakiki si tahakiki, huku vingine hata havihusiani na fasihi, kwa mfano “Tahakiki ya Sarufi ya Kiswahili, TAKILUKI, SAMAKISA.” Aidha, majibu mengine yanaonekana kuwa ya jumla mno kubainisha usahihi wake. Majibu hayo ni pamoja na: “Tahakiki za TUKI, Msabila, na Nyambari,” “Tahakiki hizi za kawaida kama za Kadeng’e (Kadeghe?),” “Tahakiki za Riwaya, Tamthiliya, Ushairi, na nadharia ya fasihi kwa jumla,” “Riwaya, Tamthiliya, na Ushairi,” na “Tahakiki ya Kiswahili na fasihi kwa jumla.”
Aidha, vitabu vingine vilivyotajwa mathalani Kiswahili II: kidato cha 5 na 6 kilichoandikwa na JPD Company General Ltd hakikuweza kupatikana katika kipindi chote cha utafiti ili kuthibitishwa matini yake. Jambo linaloweza kutafsirika kuwa inawezekana (kama kipo) ni mali binafsi ya msomaji katika maktaba yake binafsi au alikipata sehemu na kuisoma tu. Nayo asilimia 65 ya waliojibu “hakuna” na “sijui” inaweza kutoa taswira ya ama wanafunzi hawa hawana vitabu kabisa au wamo katika mazingira msimopatikana vitabu vya fasihi au wanatumia mihtasari ya maandiko yaliyoandaliwa na walimu wao kama mhimili wa usomaji wao. Lakini pia, kwa mujibu wa F. J. Masatu (2009: 27) wapo wanafunzi ambao hawajishughulishi na usomaji wa vitabu mbalimbali hata kama ni vichache au upatikanaji wake ni duni.
Katika kubaini sababu za upatikanaji na utumikaji wa vitabu vya ama aina moja au mwandishi/ waandishi fulani mashuleni, mtafiti alibaini kuwa hata katika Maktaba ya Mkoa na Maduka ya Vitabu namo mna upungufu mkubwa wa matini ya nadharia, hasa ya uhakiki. Na hata yale machache yanayopatikana hayapewi kipaumbele maana kwa mujibu wa baadhi ya wanafunzi wajibu hojaji/ jaribio la utafiti, “mwandishi huyu amerahisisha usomaji kwa kusumarize (kufanya muhtasari) mambo tunayotakiwa kusoma.” Mwandishi anayetajwa hapa ni Nyambari Nyangwine (na wenzake ambao wameandika kazi kadhaa kwa pamoja ijapokuwa Nyambari Nyangwine ndiye anayefahamika zaidi ya wenzake).
Hali hii inaweza kutafrisika kuwa sawa na kugeuza kazi za mwandishi/ waandishi hawa “msahafu” wa kitaaluma kwa wanafunzi wa jamii husika. Picha hii ndiyo inayojitokeza hata katika maduka mbalimbali ya vitabu yaliyopo mkoani hapa ambapo vitabu vya Kiswahili kidato cha tano na sita pamoja na vile vya elimu ya juu ni adimu na vinavyoweza kupatikana angalau kirahisi ni vya mwandishi/ waandishi waliotajwa na wajibu hojaji/ jaribio la utafiti wengi, yaani kazi za Nyambari Nyangwine, na wenzake.
Swali la kujiuliza hapa ni: Kwa nini vitabu vingine vya nadharia za Kiswahili (katika mada mbalimbali) na tahakiki mbalimbali havipatikani (angalau) kirahisi na kwa wingi kama zinavyopatikana kazi za mwandishi Nyambari Nyangwine, na wenzake? Majibu yake yanahitaji utafiti wa kina ijapokuwa, sababu zinaweza zikawa: uwezekano wa kutokusambazwa vema kwa kazi za waandishi wengine au gharama ya kuzinunua kazi hizo ni kubwa ikilinganishwa na zile za mwandishi “tegemeo” au ni uamuzi jumuishi kuwa huwezi kufaulu pasipo kujisomea kazi fulani. Lakini pia, sababu nyingine inayotajwa ni kukosekana kwa Chuo Kikuu/ Vyuo Vikuu (vikiwemo vyenye kufundisha fasihi) katika Mkoa wa Mara, na wilaya zake. Mambo haya yanaweza kuwa sababu za kutokupatikana kirahisi kwa vitabu vingi na mbalimbali katika mashule, maktaba, na maduka ya vitabu.
Pia, uchunguzi ulibaini kuwa wanafunzi “wameweka” mipaka kati ya matini ya Kiswahili na yale ya lugha zingine. Yaani, endapo somo ni Kiswahili, basi matini yanayotafutwa ni yale yaliyo katika lugha ya Kiswahili tu. Kwa mfano, katika Maktaba ya Mkoa yapo matini yaliyo katika lugha ya Kiingereza, ambayo yanaelezea fasihi, Isimu, U - Marx, Ufeministi, Ukombozi, Utandawazi na kadhalika, lakini hayaguswi na wanafunzi ila wamepewa zoezi kutoka masomo mahususi yanayoainisha mambo haya kujadiliwa. Hili nalo ni tatizo ambalo kwa kiasi kikubwa linawezakuwa linatokana na mfumo wa elimu uliopo.
Vyovyote iwavyo, hitaji la kuwa na maandiko mbalimbali ya kitahakiki na kinadharia aghalabu ya nadharia ya uhakiki, kutoka waandishi tofauti tofauti kama walivyopendekeza baadhi ya wajibu hojaji/ jaribio la utafiti ni kubwa na lisilopingika, tena lenye kuhitaji hatua za makusudu na za haraka kutatulika. Matumizi ya maandiko na waandishi mbalimbali husaidia kujenga maono tofauti tofauti miongoni mwa wasomaji na wahakiki ili kuepuka kujenga na kufikia hitimisho ambalo nalo linaweza kuwa na upungufu wake pindi mhusika ataliheshimu kuwa kamilifu (K. Njogu & R. Chimerah; 1999).
Mathalani, Godfrey Rutta Bukagile, Mhariri Mkuu wa Nyambari Nyamwine Publishers, katika Utangulizi wa Tahakiki: vitabu teule vya fasihi kidato cha 5 na 6  ya J. A. Masebo na N. Nyangwine (2008) anajaribu kuonyesha upekee wa tahakiki hii kwa kusema:
… upekee wa kitabu hiki ni kuwa kimeandaliwa kwa kuzingatia kiwango cha walengwa tofauti na tahakiki za mwanzo ambazo zilihusu uhakiki na uchambuzi kwa ujumla bila kutofautisha kiwango cha wasomaji. Kitabu hiki kimekusudiwa kiwafae wasomaji wa fasihi – yaani wanafunzi wa kidato cha (5) na (6). Katika Shule za Sekondari nchini Tanzania…. Tofauti na tahakiki za awali, kitabu hiki kinaonyesha kufaulu na kutokufaulu kwa kila mwandishi ambaye kazi yake imeshughulikiwa. Kwa kufanya hivyo, itawasaidia sana wanafunzi, walimu, waandishi, wahakiki na wasomaji wengine wa fasihi kuiangalia kazi ya fasihi kwa jicho la kiyakinifu badala ya kuisifia tu kazi hiyo….
Hoja ya upekee na uyakinifu wa tahakiki hii ni suala la kiujumi zaidi. G. R. Bukagile habainishi japo baadhi ya tahakiki alizoziita za “mwanzo.” Umwanzo huu ni upi katika tahakiki zilizopo; Je, ni mwanzo kwa maana ya vitabu teule vilivyohakikiwa au ni upi hasa? Kauli hii inaweza kuwa tija kwa baadhi ya wanafunzi na wasomaji wasiojituma katika kutafuta na kutafiti matini anuai kiasi cha kuzipuuza kazi na tahakiki zingine wakidhani kuwa si bora. Kimsingi, mwanafunzi au mwanazuoni yeyote yule, aliye mdadisi hawezi kutegemea tahakiki moja katika ujenzi wa maarifa. Pia, suala la kufaulu na kutokufaulu kwa mwandishi ni hoja ya Wanaumaudhui. Lakini kwa Wanaumbuji, hasa Wanaumbuji Mpya na Wanaumbuji wa Kirusi, mhakiki hapaswi kujiipenyeza ndani ya mwandishi na kazi yake kwa kujaribu kumsemea ufaulu wake. Maana kila mwandishi ana kusudi lake ambalo linaweza kutafsirika vinginevyo. Athari ya kujipenyeza katika kazi ya mwandishi kwa kujaribu “kuwa mdomo” wake ni kuingiza na kutumia (i) wasifu wa mwandishi, (ii) kujiuliza nini alikikusudia mwandishi, (iii) hisia, itikadi au mtazamo wako, na (iv) ubinafsi wako kuhakiki kazi husika, hivyo, kupoteza thamani na uzito wa kazi halisi (Mushengyezi; 2003).
Kwa mfano, katika uhakiki wao, J. A. Masebo na N. Nyangwine (2008: 59) wanaelezea kutokufaulu kwa Shaaban Robert, Mwandishi wa Kufikirika kuwa:
Kwa kiasi mwandishi ametumia wahusika bapa ambao hawabadiliki kutokana na mabadiliko yanayojitokeza katika jamii, kutokana na hali hii, wahusika hawa hawaaminiki, yaani hawana uhalisia (uhalisi) katika jamii ya sasa. Mfano si rahisi kumkuta mhusika kama Utubusara ujingahasara katika jamii yetu ya Tanzania ya leo.
Mjadala huu unaelekea kuinyima fasihi mawanda yake mapana ya kuiakisi jamii. Inaelekea kuwa wahakiki hawa bila shaka, wao ndiyo “wameshindwa” na siyo mwandishi. Kwa maneno mengine bila shaka “… katika jamii ya Tanzania ya leo,” kunamaanisha jamii ya leo ni ya watu wanaopaswa kuwa Ndumilakuwili. Hata kama ndivyo ilivyo, jamii ya Tanzania haiwataki. Huu nao ni “mgogoro” sawa na ule wa Njozi “kuwalaumu” wahakiki kama vile F. E. M. K. Senkoro, M. S. Khatib, na Joseph Mbele kuhusu chambuzi zao juu ya Utenzi wa Mwanakupona. Fasihi ina mafungamano ya hali ya juu na nyanja mbalimbali za maisha ya binadamu – kifikra, kijamii, kisiasa, kiutamaduni, na kiuchumi. Ili kupata dhana stahiki ya uhakiki wa kifasihi ni sharti mhakiki na msomaji wasome, wazifahamu, na kuzifanyia kazi nadharia za uhakiki (K. W. Wamitila; 2000: 128 ­ 129; 197). Mtazamo huu unaungwa mkono na Vincent Kawooya na J. K. S. Makokha katika makala yao ya postcolonial criticism and globalization through Kiswahili lens kwa kuihakiki tamthiliya ya Amezidi, ya Said Ahmed Mohamed  (TUKI; 2001: 129) wanaposema “uhakiki ndio mkono ule mwingine wa fasihi, wa kwanza pengine ukiwa ni ule wa ubunifu….”
Kwa kifupi, hata U - Marx unasisitiza usawa, haki, upendo, amani, na uhalali wa namna mali zinavyozalishwa miongoni mwa wanajamii. Huku Umbuji ukisisitiza uzingativu na kuheshimu kivitendo, utawala wa sheria. Mambo ambayo hayampi ugumu mwanafasihi mcha Mungu kama Shaaban Robert.
Katika Ulimwengu wa Roho (Kidini) hakuhitajiki kuwapo mtu vuguvugu; mtu anaaswa kuwa ama baridi au moto (Ufunuo wa Yohana 3: 15 - 20). Hili ndilo lengo la dini na fasihi pia. Hakuna jamii wala fasihi yake vinayohamasisha, kushadidia, kufurahia, na hata kuruhusu uvuguvugu (undumilakuwili/ upopo), yaani mtu huyo huyo atende maovu na wakati huo huo atende mema. Kama ndivyo hivyo, kwa nini basi kunatungwa sheria na kuanzishwa kwa Mahakama? Huwezi kusema “acha tabia hii au ile” kama mtu haitendi ama haipo katika jamii husika au imeruhusiwa. Hata kama jamii ina undumilakuwili si lazima kila mwandishi apite njia aliyopita mwenzake kuuelezea utamaduni huo. Kila msanii ni mbunifu, au anapaswa kuwa mbunifu kwa kujipambanua kipekee kuelezea jambo husika. Mtazamo huu unaelekea kuungwa mkono na R. Dubos (1968: vii) kama asemavyo:
Each human is unique, unprecedented, unrepeatable… each one of us has become what he is and behave as he does, always having in mind the course of events that transformed… into a reasonably succeful citizen.
Kila binadamu ni wa pekee, asiye na mbadala, asiyejirudia… kila mmoja wetu yuko vile alivyo na kutenda vile atendavyo, daima kunasababishwa na msingi wa matukio unaomuumba… kuwa raia anayefanikiwa kiuhakika zaidi (Tafsiri ya mwandishi).
Kwa kulijua hili, katika kuijenga dhana hii kifasihi, kwa weledi mkubwa, inaelekea kuwa Shaaban Robert hataki kuzungukazunguka katika kuiasa jamii kuacha uovu, badala yake anajenga jamii mbili tofauti kimatendo ili kupembua “ubinadamu” – tabia wanazozisema wahakiki hawa. Bila shaka, S. Robert hakusudii kumjadili mtu, bali tabia zinazotawala matendo ya mtu. Huu ni upekee na ustadi wa mwandishi huyu, gwiji katika uga wa Kiswahili. Ndiyo maana kila wakati, falsafa yake ni wema kuushinda ubaya endapo mtu atamcha Muumba wake. Bila shaka hata G. R. Bukagile analitambua hili, maana pamoja na “kukipigia chepuo” kitabu hiki, bado anarudi nyuma na kukiri hivi:
Napenda kusisitiza kuwa ni kweli na wazi kwamba kuna mabingwa wa taaluma ya uhakiki zaidi ya waandishi hawa ambao wamejishughulisha sana kuandika kuhusu nadharia ya uhakiki, lakini tunaamini kuwa kitabu hiki kinakuwa ni kichocheo kizuri cha kuendeleza na kukuza na hata kupambanua  mawazo ya mabingwa hao. Vilevile napenda kusisitiza kuwa lengo la kitabu hiki ni kuziba pengo la uchache wa maandishi yanayohusu uhakiki na uchambuzi wa Fasihi ya Kiswahili (uk. viii).
Ni ukweli usiopingika kuwa uga wa Kiswahili, hususani uhahiki bado unakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo ya maandiko ya kitaaluma (S. A. Mazigwa 1991, uk. 7; S. D. Kiago katika M. Msokile uk.iv; na M. Msokile 1993, uk. ii; S. A. Mohamed 1995 - utangulizi; R. M. Wafula, 1999, uk. vii; na K. Njogu na R. Chimerah, 1999: x). Waandishi hawa wamechangia kwa sehemu yao katika upatikanaji wa maandiko ya Kiswahili - Isimu na Fasihi; hili halipingiki. Tatizo si kuzibwa kwa pengo, kama Bukagile anavyobainisha katika utangulizi wake. Tatizo ni namna pengo hilo linavyozibwa. Uzibaji pengo unapaswa kufanyika kwa makini na kwa tahadhari kubwa ili kuepuka hasara ambayo gharama ya fidia na, au marekebisho itakuwa kubwa zaidi ya ile ya uzibaji (G. Ruhumbika; 2006: 225).
Utafiti huu umebaini pia, wanafunzi wengi ni wepesi zaidi katika kujitolea kufanya kazi za kipengele cha maudhui kuliko zile za fani. Na katika Maudhui, kipengele kinachopendeka zaidi ni Dhamira, kikifuatiwa kwa mbali na kipengele cha Ujumbe. Hali hii imesababisha baadhi ya wanafunzi kujichanganya pindi wanapojibu swali linalohusu ujumbe. Yaani, wanajadili dhamira “wakidhani” wanajadili jumbe, huku migogoro ikitajwa kama moja ya Dhamira au jumbe. Hali hii imejipambanua pia katika J. A. Masebo na N. Nyangwine (2008), tahakiki ambayo ndiyo inayotumika zaidi mashuleni, lakini haibainishi nadharia zilizotumika/ iliyotumika kuongoza uhakiki wa vitabu teule walivyovifanyia kazi.
Kwa mujibu wa WanaU - Marx, migogoro ni ishara ya kutokuwepo usawa, haki, upendo, na utu miongoni mwa wanajamii. Kukosekana kwa haya ndiko kunakosababisha dhuluma, chuki, unyonyaji, unyanyasaji, matabaka, kutokuwajibika, na kadhalika. Matokeo yake ni mapambano ya kitabaka kati ya wanyonge na matajiri kwa lengo la kutafuta suluhu ya mahusiano ya kitabaka na njia za uzalishaji mali. Kwa baadhi ya tahakiki, dhana hii hutambulishwa kama dhamira ya “Ujenzi wa jamii mpya na endelevu.” Lakini dhana hii haipambanuliwi kwa mapana yake. Jambo linalowafanya baadhi ya wanafunzi kuchukulia kuwa suluhu ya matabaka ni maandamano, na, au kumwaga damu; kujitoa mhanga.
Inasadikika kuwa, huku ndiko wanakokujua wanafasihi na wahakiki chipukizi walio wengi. Mathalani, baadhi ya wawakilishi au wanavikundi wawasilishaji walipojaribu kuhusisha mambo yanayojadiliwa katika vitabu teule, hasa yale maovu, kwa haraka sana walihitimisha na kauli ya “dawa ya haya yote ni kujitoa muhanga, kupigana kwa nguvu zetu zote, hata kufa tufe ikibidi. Ni lazima tuwe wazalendo.” Na picha wanayoijenga pindi wanapojadili dhana ya “kujitoa mhanga” ni ile ya mauaji; kumwaga damu kama ishara ya ushujaa ana ukombozi wa kweli.
Kwa baadhi ya jamii, kuua au kumwaga damu si jambo jipya, wala la kushangaza miongoni mwao! Hivyo, hoja kama hii “inaweza kuhalalisha” vitendo hivi kupitia mafundisho wanayoyapata mashuleni. Ni sawa na kuchochea kuni kwenye tanuru liwakalo moto. Kwa mantiki hii, kuna uwezekano mdogo sana wa kuwa na jamii huru na isiyomwaga damu. Kwani wadhulumaji ni zao la jamii – jamii ya wasomi na wasio wasomi. Na wamwaga damu, nao ni zao la jamii ile ile, wanafunzi wakiwemo. Kwa Wanausasa na baadhi ya WanaU - Marx, maandamano, na, au kumwaga damu; kujitoa mhanga ni hatua ya juu kabisa katika kujitetea dhidi ya dhuluma iliyokita mizizi, na ambayo siyo rahisi kuing’oa kwa njia za amani. Mtazamo huu unafanana na mtazamo wa baadhi ya wananadharia za uongozi na utawala, ambao wanaiona migogoro katika jamii kuwa moja ya misingi ya maendeleo na maboresho yenye kuleta tija katika jamii endapo jamii itafikiria zaidi uchanya kuliko uhasi.
Katika muktadha huu, uhakiki wa kazi za fasihi unapaswa kuambatana na nadharia, tena kuzipambanua kwa wazi kabisa kuepuka “sitofahamu” miongoni mwa wadau wa fasihi ya Kiswahili. Huku ndiko kunakofungua hoja ya kuwepo au kutokuwepo kwa uhusiano kati ya nadharia za uhakiki wa fasihi ya Kiswahili na uwezo wa mwanafunzi kujitegemea kivitendo katika majukumu kadha wa kadha anayopewa ndani na nje ya darasa, jambo linaloungwa mkono na Judith Ferster (1947: vii).

4. 5. 1. 3 Uhusiano Uliopo kati ya Nadharia za Uhakiki wa Fasihi ya Kiswahili na Uwezo wa Mwanafunzi Kujitegemea Kivitendo katika Majukumu Kadha wa Kadha Anayopewa Ndani na Nje ya Darasa

Lengo kuu la kipengele hiki lilikuwa kubainisha kwa kuelezea uhusiano kati ya nadharia za uhakiki wa fasihi ya Kiswahili na uwezo wa mwanafunzi kujitegemea kivitendo katika majukumu kadha wa kadha anayopewa ndani na nje ya darasa. Nadharia zilizotumika kujenga mjadala huu ni Umbuji na U - Marx wa Kirusi. Uchambuzi wa kina ulifanyika kupitia matokeo ya utafiti, mapitio ya maandiko na nadharia teule katika utafiti huu ili kurahisisha mtiririko wa mjadala mzima.
Pamoja na nadharia za uhakiki kutokupewa uzito stahiki katika ufundishwaji wa fasihi mashuleni kutokana na kutokuwa sehemu rasmi ya Muhtasari wa Kiswahili katika shule za sekondari nchini Tanzania, pia utamaduni wa walimu na wanafunzi kujifungia katika mitaala rasmi, imebainika kuwa upo uhusiano kati ya kujifunza nadharia za uhakiki wa fasihi ya Kiswahili na uwezo wa mwanafunzi kujitegemea kivitendo katika majukumu kadha wa kadha anayopewa ndani na nje ya darasa. Hoja hii inatokana na jibu la Ndiyo lililotolewa na wajibu hojaji/ jaribio la utafiti 24 sawa na asilimia 96 ya wote 25 waliojibu swali la msingi lililosema: Je, unadhani kuna uhusiano wa msingi uliopo kati ya mwanafunzi kujifunza nadharia ya uhakiki na uwezo wake katika kuzikabili changamoto mbalimbali ndani na nje ya darasa? Kauli hii itajipambanua vema katika matokeo ya jaribio la utafiti kati ya wanafunzi wa shule dhibitiwa na isiyodhibitiwa ili kuthibitisha uhalali wake.
Wajibu hojaji/ jaribio la utafiti hawa walitoa majibu mbalimbali kama sababu za kutetea hoja na mitazamo vyao. Baadhi ya sababu hizo ni pamoja na “Uhusiano upo, kwani baada ya kuwa amejifunza atakuwa na uwezo wa kuchambua kwa undani mambo mbalimbali au kukosoa kwa kiasi atakachoweza na kupata mambo ya msingi atakayoweza kuyafanya hata anapokuwa nje ya darasa,” “… mwanafunzi atakuwa na uwezo wa kufanya au kuchambua taarifa, vitabu, na hotuba mbalimbali zinazotolewa na watu katika jamii yake,” na “nadhani nadharia za uhakiki wa fasihi kama tukifundishwa vizuri tutaweza kujisimamia, kuchambua mambo kwa utulivu, na kuyaamua kwa ufanisi zaidi..Kwa ufupi, fasihi na uhakiki ndiyo maisha hasa kwani uhakiki ni chujio la kila jambo limhusulo binadamu na maisha yake kupitia fasihi.”
Kinachojitokeza katika majibu haya ni kwamba, inavyoelekea pamoja na nadharia za uhakiki kutokuwa sehemu rasmi ya Muhtasari wa Kiswahili katika Shule za Sekondari nchini Tanzania, wanafunzi wanaoufahamu juu ya mchango wa mada hii katika maisha yao ya kila siku. Ufahamu huu unaweza kupambanuliwa kupitia tafsiri wanazozijenga kutoka mada ndogo ya Uhakiki na Mhakiki.
Kwa namna kipengele hiki kinavyofundishwa na “kuimbwa” na wanafunzi katika shule hizi mbili kunawafanya wanafunzi wajibu hojaji/ jaribio la utafiti 12, sawa na asilimia 60 kukihesabu kipengele cha Uhakiki na Mhakiki kuwa sehemu mojawapo muhimu ya miongozo ya wao kufanya kazi ya uhakiki. Hali hii inajipambanua kupitia majibu yanayofanana kwa sehemu kubwa miongoni mwa wajibu hojaji/ jaribio la utafiti hawa 12. Mathalani, baadhi ya wajibu hojaji/ jaribio la utafiti pamoja na kutokukaa pamoja katika kujaza hojaji walitoa kauli hii “… nadharia ya uhakiki ina umuhimu mkubwa mno. Bila mtu kupata mwongozo huwezi kuelewa, hivyo basi ili mwanafunzi aelewe lazima apate mwongozo….”
Kauli hii kwa sehemu “inaleta mkanganyiko” kiasi fulani, kwani wajibu hojaji/ jaribio la utafiti hawa hawasomi nadharia za uhakiki ila wanaanza hoja yao kwa maneno “nadharia ya uhakiki….” Kwa mtu ambaye hakufuatilia mjadala wa namna mada hii inavyofundishwa mashuleni bila shaka atapata ukakasi katika kubaini nini wanachokimaanisha hapa. Uchunguzi uliofanyika unaonyesha kuwa kisichofundishwa mashuleni ni: nadharia za uhakiki ni nini, ni zipi, na mawanda yake ni yepi lakini kwa namna ya jumla mada hii hufundishwa kikizakiza, yaani hufichika ndani ya dhana za fani, maudhui, uhakiki na mhakiki. Huku ndiko kusema, nadharia za uhakiki huguswa kwa uchache sana ama kwa kutajwa tu au kuelezewa kwa muhtasari kusikokidhi mawanda ya nadharia za uhakiki, kwa uwazi na ufasaha wake.
Uzoefu wanaoupata wanafunzi kupitia kazi teule na zisizo teule za kifasihi wanazozisoma na kuzihakiki zingeunganishwa na nadharia za uhakiki, bila shaka kungejenga muunganiko mzuri wa nadharia na vitendo, kama alivyotanabaisha mjibu hojaji/ jaribio la utafiti mwanafunzi:
… kupitia nadharia ya uhakiki, tunaweza kufanya mazoezi kwa kujiamini, na kushirikiana…. mazoezi ni muhimu sana hasa kwa mwanafunzi. Kupitia mazoezi hayo mwanafunzi huongeza ujudi (ujuzi) na kuwa mahiri…. kujenga utamaduni wa kuweza kuelewa mambo mbalimbali katika jamii mfano, ufisadi, unyonyaji, matabaka… (Hojaji kwa Wanafunzi).
Hoja hizi zinaelekea kushabihiana na ya mjibu hojaji/ jaribio la utafiti mwingine aliyesema, “Kwa kusoma nadharia tunapata kufahamu matatizo na chanzo cha matatizo hayo na kuyafanyia uchunguzi na hatimaye kuyafanyia matatuzi.” Kinachojitokeza hapa, kwa mtu aliyesoma na kuzipa nafasi nadharia katika shughuli zake za kila siku, kutamfanya kujijengea moyo wa kutokupuuza mambo, na kwa uwezo wake atakuwa makini na kila mara kufanya uchunguzi (wa kina) ili kutafuta tiba; tiba ya kudumu kwa kizazi chake na vijavyo. Yaani, pamoja na kuelewa jambo bado mtu anapaswa kuchukua hatua za makusudi na za haraka katika kuchunguza na kulifanikisha jambo kwa ufasaha zaidi ya wengine. Hoja hii inaungwa mkono na moja ya misemo ya mama mzazi wa B. Carson (1992: 149) inayosema “unaweza kufanya chochote wanachofanya wengine – lakini unapaswa kujaribu kufanya vizuri zaidi yao.”
Faida ya utamaduni huu ni kujiepusha na utegemezi wa fikra na maamuzi kutoka kwa wengine, kama anavyobainisha mjibu hojaji/ jaribio la utafiti mwingine:
… kwa sababu ukitegemea kutumia tahakiki za watu wengine tu hutaweza kubainisha makosa kwa ufasaha zaidi. Hivyo nadharia ni muhimu kusomwa… (Hojaji kwa Wanafunzi).
Hoja hii inaungwa mkono pia na mjibu hojaji/ jaribio la utafiti mwingine anayesema:
... kwa sababu wanafunzi wengi wanatumia tahakiki ambazo zinapumbaza akili zao pengine wangekuwa na elimu hii wangetumia akili zao wenyewe kuepukana na upotoshwaji utokao kwa wahakiki wengi (Hojaji kwa Walimu/ Mtaalamu Taasisi ya Elimu Tanzania).
Hata hivyo, kauli hizi inapingwa na mjibu hojaji/ jaribio la utafiti aliyekataa kuwepo kwa umuhimu wa kujifunza nadharia za uhakiki kwa sababu:
kujifunza nadharia kutamfanya mwanafunzi kushindwa kufanya upembuzi yakinifu kwa kutumia akili yake na kupelekea mwanafunzi kuwa tegemezi katika tahakiki (Hojaji kwa Wanafunzi).
Kauli hii inapingana na jibu alilolitoa mjibu hojaji/ jaribio la utafiti huyu pindi akijibu swali lililomtaka kwa mtazamo wake aweze kutoa sababu ya/ za shule kufundisha nadharia ya uhakiki. Katika eneo la shule kufundisha nadharia za uhakiki, mjibu hojaji/ jaribio la utafiti huyu anasema:
Lengo kuu la kusoma nadharia hii ya uhakiki wa fasihi ya Kiswahili katika shule za sekondari ni kuweza kumpa mwanafunzi weledi ama uwezo wa kutambua chimbuko la fasihi kwa undani zaidi (Hojaji kwa Wanafunzi).
Kwa namna kauli hii ilivyo, bila shaka panaibuka hisia kuwa mjibu hojaji/ jaribio la utafiti huyu ama hakulielewa swali au alishindwa kuhusianisha mambo haya mawili. Endapo lengo la kufundishwa nadharia mashuleni ni kumpa mwanafunzi weledi ama uwezo wa kutambua chimbuko la fasihi kwa undani zaidi, itakuwaje mwanafunzi huyo huyo ategemee tahakiki?
Kwa mujibu wa wajibu hojaji/ jaribio la utafiti wanane sawa na asilimia 32 ya wote 25 wanabainisha kuwa mtu akijifunza na kuzingatia kile anachofundishwa ndani na nje ya darasa anaweza kujikuta akifanya tathmini na tafiti zisizokwisha kuhusu kile akionacho, akisikiacho, au akijuacho. Mfano wa hoja za namna hiyo ni pamoja na hii:
... maana atakuwa akiyachambua maisha na makandokando yake. Matokeo yake anaweza kuyaogopa hata maisha yake mwenyewe… hayatendei haki…. Hawatendei wengine haki… hafai kuigwa wala kuiga (Hojaji kwa Wanafunzi, Walimu/ Mtaalamu Taasisi ya Elimu Tanzania).
Suala linalojadiliwa hapa ni “athari” ya kuyachimba maisha kiasi cha kuzamia katika Udhanaishi na kuyalazimisha maisha yajibu yote uyaulizayo. Lengo kuu hasa la nadharia za uhakiki si kumfanya mtu afanane na Plato, Aristotle, Socrates na wanafalsafa wengine wa zama hizo, wakiwemo baadhi ya Wamonaki. Lengo hasa la nadharia za uhakiki ni kumjengea msingi msomaji kuutafuta ukamilifu mkamilifu na si kumpotosha au kumuegemeza katika dhana moja na kuiamini kuwa ndiyo ukamilifu wa matendo na maneno (K. W. Wamitila; 2000: 128 ­ 129; 197).
Katika kuboresha hoja ya kuwepo uhusiano kati ya mtu aliyejifunza na ambaye hakujifunza nadharia za uhakiki, mwalimu mjibu hojaji ana haya ya kusema:
Mtu asiyezijua nadharia za uhakiki anapungukiwa kitu muhimu katika taaluma yake. Hawezi kuijua na kuitumia historia vilivyo. Hawezi kuwa hakimu au jaji mzuri. Hawezi kuwa mwanasiasa mzuri… utendaji wake ofisini utakuwa sawa na usingizi wa mang’amung’amu tu; hana kipya, hana ubunifu; atapwaya hakika (Hojaji kwa Walimu/ Mtaalamu Taasisi ya Elimu Tanzania).
Hoja hii inaelekea kuibua na kumchochea msomaji au mhakiki wa fasihi ya Kiswahili kujikita katika kuzisoma nadharia mbalimbali aghalabu nadharia za uhakiki. Mathalani, U - Marx ni mpana sana kiutumizi kwani ni dhana inayogusa kila uga wa maisha ya mwanadamu. Si rahisi kukutana na somo au kozi ambavyo havitaji wala kuzungumzia U - Marx. Hivyo, kwa kuisoma kwake kutawafanya wanafunzi kuzihakiki kazi za kifasihi katika mahusiano ya kinyuga – kijamii, kisayansi, kiuchumi, kiutamaduni, kiimani, na kisiasa. Msingi huu ndiyo utakaowafanya kujijengea desturi ya kuzifikiria nyuga zingine katika uandaaji, ubunaji, upangaji, na uchaguzi wa vipaumbele (F. J. Schuurman; 2000: 61 – 67, na E. M. Songoyi; 2008).
U - Marx unamfanya msomaji na mtunzi wa kazi za kifasihi na zisizo za kifasihi kuyachunguza kikamilifu maisha na mfumo wake kabla ya kufanya uamuzi wenye kuzingatia utashi wa, au tija kwa jamii husika. Huku kutapunguza kwa kiasi uhuru wa msomaji au mtunzi, hivyo katika kuyaepa haya kwa kiasi fulani atalazimika kuutumia Umbuji hususani Umbuji wa Kirusi ili kujitanua na kufanya hitimisho lake.
Haya yote yanajenga msingi wa kufikiri kwa kina; kuielewa na kuitumia lugha kiufasha, tena kimuktadha, kama wanavyosema baadhi ya wajibu hojaji/ jaribio la utafiti katika hoja ifuatayo:
Nadharia hujenga msingi wa kupata ujumbe uliozungumzwa, pia kufafanua lugha (zikiwemo za picha mfano), mwandishi anapotumia ‘punda’ inakuwezesha kufahamu ‘punda’ ni mwanamke; jinsi anavyonyanyaswa…. Kwa sababu mtu unakuwa na umahiri katika lugha, hivyo umuhimu upo sana na ni mada moja nzuri sana (Hojaji kwa Wanafunzi & Hojaji kwa Walimu/ Mtaalamu Taasisi ya Elimu Tanzania).
Katika kupima hoja hii, mtafiti alihitaji kujua mwitiko wa wanafunzi wajibu hojaji/ jaribio la utafiti 20 ambapo walitakiwa kubainisha jambo lililo bora zaidi katika kuwajengea uwezo wa kuyamudu masomo yao na mambo mengine kwa wepesi na urahisi. Swali liliambatana na majibu - pendekezi ya kuchagua. Majibu - pendekezi yalikuwa:
a.       kujifunza nadharia za uhakiki na kuzitilia maanani
b.      kusoma tahakiki na kuzitilia maanani
c.       kusoma vitabu teule vya fasihi na kuvitilia maanani
d.      kuzingatia jibu la (a), (b) na (c)
e.       hakuna jibu lililo sahihi
Jumla ya wajibu hojaji/ jaribio la utafiti 20 walijibu swali hili, na matokeo ya mwitiko wao yalikuwa kama ifuatavyo (asilimia ya waliochagua jibu pendekezi katika mabano):
a.      Kujifunza nadharia za uhakiki na kuzitilia maanani (45%)
b.      Kusoma tahakiki na kuzitilia maanani (05%)
c.       Kusoma vitabu teule vya fasihi na kuvitilia maanani (35%)
d.      Kuzingatia jibu la (a), (b) na (c) (15%)
e.       Hakuna jibu lililo sahihi (0%)
Kimantiki, hakuna eneo katika maisha ya mwanadamu lililo bora zaidi ya jingine ila kutokana na rasilimali zilizopo, inailazimu jamii kuwa na vipaumbele. Hapa ndipo penye ugumu; kipi kianze, kipi kifuate. Katika muktadha huu, weledi wa hali ya juu unapaswa kujipambanua vema. Na kwa mtu aliyesoma nadharia vizuri na kuzielewa kivitendo hatapata shida sana kuteua vipaumbele au kujenga hoja bora za kupata vipaumbele. Hiki ndicho kinachojitokeza katika matokeo haya.
Kimsingi, jibu ambalo lingeweza kuwa sahihi zaidi ni jibu (d) ambalo linajumuisha majibu pendekezi ya (a), (b), na (c). Kwa sababu kutegemea nadharia pekee na kuzitilia maanani hakuwezi kukufanya kuiva kitaaluma, vivyo hivyo kwa majibu mengine. Kinachoweza kujenga weledi ni pamoja na kujifunza nadharia za uhakiki na kuzitilia maanani, kusoma tahakiki na kuzitilia maanani, na kusoma vitabu teule vya fasihi na kuvitilia maanani. Hivi vyote vinasaidia kushikamanisha matini, mijadala, na hoja kwani huwa ni mifano dhahili ya kile kinachojitokeza katika mijadala.
Hata hivyo, matokeo haya yanaweza kuwa yameathiriwa na maneno “…na kuzitilia maanani.” Kama hivi ndivyo, basi kwa namna fulani inakuwa vigumu kidogo kubaini tafsiri waliyoijenga wajibu hojaji/ jaribio la utafiti hawa kwani dhana ya kutilia maanani inaweza kutafsiriwa kama ‘kufanyia kazi’ au ‘kuzingatia.’ Kwa msingi huu, kujifunza na kuzingatia nadharia pekee kunamfungia mtu nje ya makandokando mengine ya kiweledi. Yaani, kunadhoofisha dhana nzima ya mawanda mapana ya mahusiano ya kinyanja ndani na nje ya darasa kati ya nadharia za uhakiki na ujenzi (wa uwezo) wa mwanafunzi katika kuzikabili changamoto mbalimbali anazozikabili katika miktadha anuai.
Huku ndiko kunakotoa picha sahihi ya namna wanafunzi wanavyoweza kuhusisha dhana, iwe kimlalo au kiwima, ili kuleta mantiki ya jambo. Mathalani, wajibu hojaji/ jaribio la utafiti waliochagua kusoma tahakiki na kuzitilia maanani kama chaguo lao bora zaidi, wanajaribu kuonyesha kuwa kujifunza nadharia za uhakiki kuna umuhimu ila tahakiki ni bora zaidi kama wanasemavyo, “umuhimu upo tena mkubwa sana kwani baada ya kuhakiki tahakiki mbalimbali inaweza kumsaidia mwanafunzi kujibu mitihani yake kwa ufasaha na kujipanulia wigo wa kufaulu zaidi na vizuri.” Hoja hii inatofautiana na mjibu hojaji/ jaribio la utafiti mwingine aliyechagua pia tahakiki. Kwake yeye “… nadharia ya uhakiki hutuwezesha kuyatambua mambo yanayoikumba jamii.”
Katika kuakisi mawanda ya nadharia za uhakiki, K. Njogu na R. Chimerah (1999: 04) wanafafanua:
Nadharia inatufanya tufikiri, tusaili, tuweke tashwishi, tuone ‘ukweli.’  Katika ufundishaji wa fasihi, ni muhimu sana kuzingatia nadharia, kwa sababu inatusaidia kuona uhusiano baina ya matukio na wahusika, au matumizi ya lugha na maana ya kile tunachokisoma, tunachokiona, na tunachokisikia. Nadharia inatufungulia njia. Nadharia inatoa mwanga na kuweka wazi kilichofichika.
Katika kipindi cha uchunguzi, mtafiti alibaini kuwepo kwa chambuzi zenye kuichambua riwaya ya A Man of the People. Chambuzi hizi zinazotumiwa na wanafunzi karibuni wote, zinamtambua mhusika mkuu wa A Man of the People, Odili kuwa ni mwanamapinduzi wa dhati, na anayepaswa kuigwa. Na ndivyo wanavyoelewa na kuamini wanafunzi hawa. Pamoja na sababu wanazotoa kutetea mtazamo wao, bado hawataji nadharia wanayoitumia kuhalalisha uadilifu wa Odili mbele ya jamii.
Hata hivyo, kwa baadhi ya wahakiki, hususani Wanasaikolojia, wanamuona mhusika Odili kutokuwa mkombozi wa kweli bali mtu mwenye tamaa ya kingono, na mlipiza visasi asiye kifani. Hoja yao imejengwa katika chanzo cha safari na mgororo baina ya Odili na Mheshimiwa Chifu Nanga, Waziri wa Utamaduni ambao unatokana na kitendo cha Chifu Nanga “kumsaliti” Odili kwa kufanya mapenzi na “mpenzi” wa Odili, Elsie . Yafuatayo ni baadhi ya maswali yanayoongoza mijadala yao:
                                i.      Odili alikwenda mjini kuitikia wito / mihadi aliyopewa na Mheshimiwa Chifu Nanga ili amsaidie kupata nafasi ya ufadhili wa kimasomo. Je, Odili hakujua kuwa hii ni rushwa ya kindugu?
                              ii.      Iwapo Mheshimiwa Chifu Nanga “asingemsaliti” Odili, je Odili angejiunga na kuanzisha chama cha kisiasa na harakati za “ukombozi”?
                            iii.      Je, “ukombozi” aliokuwa akiutafuta Odili ulikuwa wa kitaifa au wa binafsi?
Wanasaikolojia hawa wanajaribu kuwatahadharisha waandishi, wasomaji na wahakiki kuwa makini na kazi au hoja zao kwani kuna hatari ya majambazi, wanyang’anyi, walafi, na kadhalika kutukuzwa na kupewa hadhi ya uanamapinduzi wa kweli na endelevu wakati hawastahili. Endapo jamii itafanya hivi, basi huku kutakuwa ni sawa na kumpa fisi bucha kulinda nyama au kumpelekea ngedere kesi ili amhukumu nyani kwa kula nafaka ambazo si mali yake! Hakika maumivu yake yatakuwa makubwa kuzidi ya awali; na hii ndiyo kazi ya nadharia kubeba na kuchuja mambo kwa kina.
Kwa mujibu wa matokeo ya utafiti na nadharia zilizoongoza utafiti huu, kwa pamoja vimebaini kujengeka kwa picha ifuatayo miongoni mwa wajibu hojaji/ jaribio la utafiti, yenye kuhitimisha mjadala mzima wa kuwepo kwa uhusiano kati ya nadharia za uhakiki wa fasihi ya Kiswahili na uwezo wa mwanafunzi kujitegemea kivitendo katika majukumu kadha wa kadha anayopewa ndani na nje ya darasa.
Mchoro 1: Muhtasari wa Mahusiano ya Nadharia na Nyuga
Kutafiti
 

Picha hii inaweza kufananishwa na kazi mbalimbali za kifasihi zilizojikita katika kuonyesha uwili wa jambo au kitu fulani katika maisha ya jamii. Baadhi ya kazi hizo ni pamoja na: “Chungu Tamu,” “Asali Chungu,” “Pili Pilipili,” “Lina Ubani,” na kadhalika. Wapo pia baadhi ya Wasanii Waimbaji waliotunga nyimbo zao kuhusu uwili wa mambo kadha wa kadha ya kimaisha, kwa mfano kuhusu “fedha,” Les Wanyika wakaimba “Shilingi yaua, tena maua,” kisha Mlimani Park Orchestra wakairudia dhana hii kwa kusema, “pesa maua, tena yaua” na wengine wakaimba “pesa sabuni ya roho” na kadhalika. Ingawa wote hawa hawakutaja nadharia ipi wanayoitumia kujenga hoja yao, bado kuwepo kwa uwili kunamfanya msomaji, mtazamaji au msikilizaji kupata picha pana zaidi kuhusu maisha na makandokando yake. Hali hii inamsaidia mwanajamii kuchukua hatua na tahadhari stahiki katika kuamua aina ya mfumo na maisha anayotaka kuyaishi huku akitambua kuwa kidole kimoja hakivunji chawa.

4. 5. 2 Matokeo ya Jaribio

Zoezi hili lilitolewa kwa wanafunzi wajibu hojaji/ jaribio la utafiti kutoka shule teule – Elly’s na Ikizu. Zoezi lilikuwa la aina moja kwa shule zote mbili isipokuwa shule ya sekondari Elly’s ilifundishwa nadharia za uhakiki, U - Marx na Umbuji wa Kirusi wakati shule ya sekondari Ikizu haikufundishwa. Njia ya ufundishaji wa nadharia ilikuwa ni njia shirikishi yenye kujikita hasa katika mafunzo – linganishi ambapo mwalimu (mtafiti) aliwaongoza wanafunzi katika kujadili na kubainisha dhana na sifa vya U - Marx, na Umbuji wa Kirusi kisha kulinganisha na mitazamo yao na tahakiki wanazozitumia kuhakiki.
Kutokana na ratiba ya shule, somo lilifanyika kwa majuma mawili, mara moja kwa juma – siku ya Jumanne kuanzia saa 1: 50 hadi 3: 10 asubuhi. Hii ndiyo kusema, kila nadharia ilifundishwa kwa siku moja – masaa mawili, yenye pumziko kila baada ya nusu saa au robo tatu saa kulingana na utashi wa wanafunzi wajibu hojaji/ jaribio la utafiti. Jaribio la utafiti lilifanyika kwa muda wa saa moja, siku ya Jumanne, juma la tatu. Swali la jaribio lilikuwa moja ambalo lilitungwa na mtafiti lakini kifungu cha habari kilitoka katika Mtihani wa Taifa, Kiswahili, Karatasi ya Pili kwa watahiniwa wasiokuwa shuleni – Ijumaa, 12 Februari 2010 asubuhi (Sehemu E: Usanifu wa Maandishi). Kila mjibu mwanafunzi jaribio la utafiti alitakiwa kukisoma kifungu kwa umakini na kisha kujibu swali lililosema kwa kutumia mifano dhahili kutoka habari uliyoisoma, jadili kauli hii, “mfano wa kazi za namna hii si kazi za kifasihi.”
Idadi ya wanafunzi wajibu jaribio la utafiti ilikuwa ni wanane, jambo lililofanya ufundishaji na tathmini ya mada kuwa nyepesi zaidi lakini ya kina. Sababu ya kuwa na idadi ndogo kiasi hiki ni kutokana na ukweli kuwa ndiyo idadi kamili ya wanafunzi wa kiswahili wa kidato cha sita waliokuwepo wakati wa utafiti. Na msingi wa kuitumia idadi hii unatoka kwa D. Ary, (kama ilivyotangulia) ambao wanaainisha kuwa, katika mazingira fulani ya utafiti, mtafiti hana budi kuzingatia zaidi aghalabu eneo mahususi la utafiti, na aina ya wajibu hojaji/ jaribio la utafiti. Kwa kuvizingatia vitu hivi, mtafiti atawatumia wajibu hojaji/ jaribio la utafiti wote atakaokuwa amewaweka kwenye mipaka ya utafiti wake. Hatua hii ilimfanya mtafiti aweze kulimudu zoezi la utafiti barabara.
Kwa kuzingatia matokeo hususani ya hojaji, na lengo la utafiti namba 4. 5. 1. 3, bila shaka wasomaji wa tasnifu hii wanaweza kuhitimisha kuwa matokeo hayo hayatatofautiana na matokeo ya jaribio. Katika lengo namba 4. 5. 1. 3 linaloelezea uhusiano uliopo kati ya nadharia za uhakiki wa fasihi ya Kiswahili na uwezo wa mwanafunzi kujitegemea kivitendo katika majukumu kadha wa kadha anayopewa ndani na nje ya darasa, wajibu hojaji/ jaribio la utafiti 24 sawa na asilimia 96 ya wote 25 – wakiwemo wanafunzi wote wanane kutoka shule dhibitiwa walijibu “ndiyo” wakimaanisha kuwepo kwa uhusiano.
Tofauti na kauli hiyo, matokeo ya jaribio yameonyesha kutokuwepo kwa uhusiano wa dhahiri kati ya mwanafunzi aliyesoma nadharia za uhakiki na asiyesoma. Hakuna mjibu jaribio la utafiti hata mmoja aliyetaja au kubainisha nadharia iliyotumika kujenga hoja ya jibu lake. Hata hivyo, majibu ya wajibu jaribio la utafiti watatu hayakuonyesha kuwapo kwa weledi wala desturi ya kunakili kama kielelezo 1a, kielelezo 1b, na kielelezo 1c vinavyojibainisha. Kwa maneno mengine, wajibu jaribio la utafiti hawa yaelekea walijikita katika kunakili kifungu cha jaribio badala ya kujibu swali. Kielelezo 1a ni kazi ya mshiriki kutoka shule dhibitiwa wakati kielelezo 1b na kielelezo 1c ni vya shule isiyodhibitiwa. Vielelezo hivi vinadhihilisha kuwepo kwa tatizo zaidi ya kufundishwa au kutokufundishwa kwa nadharia za uhakiki.
Kifungu cha habari katika jaribio kimejengwa na tashihisi ambayo kandambili, mhusika mkuu anawalalamikia wote wanaomtumia kwa manufaa binafsi lakini thamani yake kwa wanaomvaa ni ya chini. Katika kujenga hoja ya kubainisha kama kifungu ni mfano wa kazi za kifasihi ama la, ukiwaondoa wajibu jaribio la utafiti watatu waliotajwa awali, wajibu jaribio la utafiti wengine wawili, ambao wote wametoka shule dhibitiwa wamekiri ya kwamba kazi hii si ya kifasihi. Ifuatazo ni sehemu ya hoja hizo:
Kielelezo 2a: Hivyo tukiangalia vipengele vilivyotumika katika kifungu cha habari hapo juu ni vipengele vichache hivyo ni dhahiri kwamba kazi hii si ya kifasihi. Kwani ametumia sana fani kuliko maudhui ndio maana tunasema kuwa kazi ya fasihi ni lazima iendane na fani na maudhui…. Ujumbe, mwandishi wa kifungu hiki hana ujumbe kwani kandambili hutumika kulingana na mazingira…. Hivyo hatuoni umuhimu wa habari kuhusu kulalamika… (Jibu toka Jaribio la Utafiti).
Kinachojitokeza katika hoja ya mjibu jaribio la utafiti huyu ni kigezo cha idadi ya vipengele vya kisanaa vilivyotumika ambavyo kwake yeye ni vichache kufanya kifungu cha habari kiwe kazi ya kifasihi. Pia kwake yeye, hakuna uwiano wa fani na maudhui hali inayosababisha akiondoe kifungu hiki katika kazi za kifasihi. Mjibu jaribio la utafiti huyu hata hivyo, habainishi namna utumizi wa fani ulivyojenga maudhui. Hali hii imesababisha atoe kauli ya kuwa “mwandishi wa kifungu hiki hana ujumbe….” Kwa kifupi, mjibu jaribio la utafiti huyu anajenga hoja ya kutokuwepo ujumbe kwa kutumia maana ya kawaida na siyo ya kisanaa, yaani maana iliyofichika ambayo Umbuji na Udenguzi huusisitiza. Kimsingi, vigezo vyake vya idadi ya vipengele vya kisanaa, uwiano wa fani na maudhui, na utumizi wa maana ya kawaida katika kufasili kifungu teule ni vya msingi na vinapaswa kuzingatiwa kwani kila mtu ana namna yake ya kuona, kutambua, na kuelezea kitu – iwe kwa “ukamilifu” ama la (T. Eagleton; 2008:14).
Kielelezo 2b: …. Ni kweli kuwa si kazi ya kifasihi kutokana na kubainisha kazi yenyewe na kuangalia vipengele vyake ambavyo ni fani na maudhui. Haijazingatia mtindo wa kazi ya kifasihi unaotakiwa kujumuisha vitu mbalimbali kama tamathari za semi, mbinu nyingine za kisanaa, semi, uteuzi wa lugha, na maumbo ya kuzingatia kiuandishi habari iliyopo juu haijazingatia vitu hivyo japokuwa imetumia lugha…. Muundo wake ni kama habari.... habari hii imefanikiwa tu kuwa na lugha ya kukipa kitu uwezo wa kibinadamu (mbinu hii ameibainisha kuwa ni tashibiha – kitu ambacho siyo sahihi, usahihi hapa ni tashihisi) kukipa kitu uwezo wa kutenda kama binadamu… (Jibu toka Jaribio la Utafiti).
Maelezo ya mjibu jaribio la utafiti huyu hayajipambanui vema kumfanya msomaji kupata kiini cha hoja zake. Mathalani ukiondoa nukuu hii, mjibu jaribio la utafiti huyu anaelekea kuainisha sifa za fasihi kwa kutumia vipengele vya fani na maudhui bila kubainisha endapo kifungu teule kimezingatia sifa za kisanaa au la. Lengo la tathmini ya jaribio siyo kubainisha lipi ni jibu sahihi ama wepi wamejibu kiufasaha, bali ni kulinganisha na kulinganua uwezo binafsi kati ya mwanafunzi aliyejifunza nadharia na ambaye hajajifunza. Huku ndiko kusema, siyo kazi ya mtafiti kuainisha majibu yepi ya wajibu hojaji/ jaribio la utafiti “ni sahihi” au “si sahihi” kulingana na mtazamo na utetezi wa hoja husika. Usahihi na usosahihi ni mambo ya kimtazamo zaidi, sawa na zilivyo nadharia mbalimbali za uhakiki.
Kwa upande mwingine, wajibu hojaji/ jaribio la utafiti 16 sawa na asilimia 80 ya wanafunzi wote 20 wamebainisha kwamba kifungu teule ni kazi ya kifasihi. Hata hivyo, wajibu hojaji/ jaribio la utafiti 14 kati ya 16 wametumia kipengele cha fani pekee kujenga mijadala yao huku wakidondoa mifano dhahiri kutoka ndani ya kifungu teule. Kwa maneno mengine, ni wajibu jaribio la utafiti wawili pekee kati ya 16 walioonyesha weledi katika kujibu swali la kifungu cha habari, kama kielelezo 3a na kielelezo 3b vinavyoonyesha. Kielelezo 3a ni kutoka shule dhibitiwa ilhali kielelezo 3b kinatoka shule isiyodhibitiwa. Wajibu jaribio la utafiti hawa pamoja na kutokuainisha nadharia walizotumia kujenga hoja zao, bado wameweza kupambanua vipengele vya fani japo kwa jumla, na kupitia kwavyo wamejenga tafsiri ya maana ya kifungu kizima. Vielelezo vifuatavyo vinadhihirisha:
Kielelezo 3a: Mwandishi wa kazi hii ametumia maneno mbalimbali ili kuibua hisia na watu wa namna hii waelewe haki zao mfano, Ninavyodharauriwa na kubezwa inasikitisha! …. Hivyo basi mtu akisoma kazi hii atakombolewa kifikra kama kazi nyingine za sanaa zifanyavyo. Umasikini pia umeonesha kuwa wavaao kandambili ni masikini … (Jibu toka Jaribio la Utafiti).
Kielelezo 3b: …. Mwandishi wa habari hii ametumia lugha ya kifasihi (ngumu)… lugha ya kifasihi zaidi ambayo kwa mtu asiyeijua hawezi kuelewa kile kilichokusudiwa na mwandishi. Mfano ametumia lugha ya picha “kandambili” akimaanisha watu wa tabaka la chini, masikini, watu wanaoonewa katika jamii… kandambili anaonekana kuwa ni mtu wa tabaka la chini… anayetumikishwa kazi ngumu, … anayegandamizwa huku mhusika kiatu anaonekana kuwa ni tabaka tawala anayethaminiwa… hivyo, kulingana na mwandishi kuwachora hivyo ni dhahiri kuwa kazi hii ni ya kifasihi iliyoandikwa kwa umahiri mkubwa sana kifasihi (Jibu toka Jaribio la Utafiti).
Kielelezo 3b kinadhihirisha uwezo binafsi wa mwanafunzi ambaye hakusoma nadharia za uhakiki lakini mjadala wa hoja zake una mashiko ya kinadharia aghalabu Umbuji wa Kirusi na U - Marx kwa kiasi chake ijapokuwa hakubainisha nadharia za uchambuzi wake. Kwa jumla, vielelezo hivi viwili kwa kiasi fulani vimeonyesha mawanda ya uchambuzi wenye kujikita katika mafunzo - linganishi.
Kwa upande mwingine, chambuzi hizi hazina tofauti kubwa na chambuzi nyingi katika tahakiki zinazopatikana ama mashuleni au vyuoni. Kwa maneno mengine, taswira inayojengeka hapa inashabihiana na kauli ya mwalimu mjibu hojaji aliyesema:
Huwezi amini wanafunzi wengi wanashindwa kujibu lile swali la kubaini mbinu za kisanaa…. Na usijeshangaa hata matokeo ya jaribio lako yakawa hayaonyeshi tofauti kati ya aliyesoma na ambaye hakusoma nadharia; kikubwa ni NECTA ndugu yangu… (Hojaji kwa Walimu/ Mtaalamu Taasisi ya Elimu Tanzania).
Kauli hii inakaribiana kwa kiasi kikubwa na kauli ya mwalimu mjibu hojaji mwingine aliyepitia majibu ya jaribio. Kwa mtazamo wake, suala la kutokuwapo kwa tofauti kati ya wanafunzi waliosoma nadharia na wasiosoma ni kutokana na mambo kadhaa ambayo ni pamoja na uzoefu wa wanafunzi katika uchambuzi wa kazi za fasihi, kama anavyosema:
Unajua kazi ya kuhakiki matini ya kifasihi huanzia kidato cha tatu, kwa mujibu wa Muhtasari wa Kiswahili Sekondari. Kwa mtazamo wangu, hapa pana miaka takribani minne inayompa mwanafunzi stadi za kuchambua kazi za kifasihi. Na kwa mfumo wetu wa kusomea mitihani zaidi kuliko welewa binafsi, naamini matokeo ya jaribio yameathiriwa kwa kiasi kikubwa na mafunzo waliyoyapata na wanayoendelea kuyapata kwa walimu pia maandiko wanayoyatumia; nadhani hili linaweza kuwa na mashiko hapa (Hojaji kwa Walimu/ Mtaalamu Taasisi ya Elimu Tanzania).
Mantiki ya mjibu hojaji huyu bila shaka inajaribu kutoa angalizo na fursa kwa tafiti zinazohusiano na mada ambazo hazimo katika mihtasari kujikita zaidi katika tafiti za muda mrefu, tena kuanzia kwenye kiini cha jambo husika. Mathalani, kwa mujibu wa Muhtasri wa Kiswahili, kidato cha kwanza hadi cha nne, uchambuzi wa kazi za kifasihi unapaswa kuanzia kidato cha tatu. Kwa msingi huu, utafiti kama huu ungeweza kutoa majibu zaidi endapo, na endapo tu ungefanyika kwa wanafunzi punde wanapoingia kidato cha tatu na kuendelea nao mpaka kidato cha sita. Yaelekea huu ndiyo uliokuwa mtazamo wa mwalimu huyu.

4. 6 Hitimisho

Kutokana na matokeo yaliyopatikana katika utafiti huu, imebainika kwamba, nadharia ya uhakiki si sehemu rasmi ya Muhtasari wa Kiswahili Sekondari, hivyo kutokufundishwa, ingawa kwa nadra dhana zake hutajwa au kuelezwa kwa kifupi pindi mwalimu anapoboresha ufafanuzi wa hoja au matini fulani.  Na kwamba, anayezifahamu dhana za nadharia za uhakiki wa fasihi ya Kiswahili ni yule ama aliyezisoma au kuzizingatia wakati zinapotajwa au kuelezwa darasani. Hoja hii inathibitisha kauli iliyotolewa na mwalimu mmoja aliyenukuliwa katika sura ya kwanza akisema:
...watajigawa katika makundi, watabishana weee, mwishoni watafikia mwafaka... ukisikiliza vizuri uwasilishaji na mijadala yao, utagundua ujenzi wa hoja unaofungamana na nadharia kadha wa kadha.
Uchunguzi umebaini kuwa wanafunzi wengi hawatambui kuwa wao nao ni sehemu, tena sehemu kamili ya wahakiki wa kazi za kifasihi na zisizokuwa za kifasihi. Pia, katika tahakiki mbalimbali zilizochunguzwa, haipo hata moja inayojipambanua rasmi kwa kutaja aina ya nadharia ya uhakiki inayoongoza uchambuzi wa kazi husika. Kinachojitokeza ni kwa msomaji anayezijua nadharia hizi kutumia taaluma yake kuzibaini kama “alivyolalama” Njozi. Hali hii inadhoofisha uandaaji na ustawi wa wataalamu chipukizi wa fani ya uhakiki na tahakiki zenyewe kama walivyobainisha baadhi ya wajibu hojaji/ jaribio la utafiti.
Aidha, mbinu ya mafunzo – linganishi inatumika kwa mawanda finyu kutokana na kutokuwapo vitendea kazi vya kutosha kama vile tahakiki mbalimbali, maandiko mbalimbali ya nadharia za uhakiki, pamoja na walimu kukosa semina elekezi ama kabisa au za mara kwa mara. Hata pale Taasisi ya Elimu Tanzania inapotoa semina au warsha kwa walimu na wakaguzi wa shule wachache bado linakuwepo tatizo la ufuatiliaji au uchukuaji wa hatua za kinidhamu kwa wote wasiotekeleza maagizo ya taasisi.
Zaidi, wajibu hojaji/ jaribio la utafiti wengi wanakiri na kubaini kuwepo kwa uhusiano wa msingi kati ya nadharia za uhakiki wa fasihi ya Kiswahili na uwezo wa mwanafunzi kujitegemea kivitendo katika majukumu kadha wa kadha anayopewa ndani na nje ya darasa. Kwani kwa njia ya kujifunza nadharia mbalimbali za uhakiki, mwanafunzi na msomaji mwingine watakuwa na utambuzi kuwa hakuna jambo lenye ukamilifu mkamilifu. Hivyo, kuondoa dhana ya kudharau au kupendelea kitu au jambo fulani pekee. Matokeo yake ni kuheshimu na kutathmini mambo kwa kina, kujituma, kuwajibika, kujali na kuzingatia, kujitegemea kifikra na kiutendaji, kushirikiana na kushirikisha wengine, kujenga usikivu na utulivu, kujielimisha na kuelimisha zaidi, na mengine mengi. Hatua hii ikifikiwa vema hujenga weledi, utaifa, busara, heshima, ukombozi wa kweli na endelevu dhidi ya maadui wa ustawi na maendeleo ya jamii katika ujumla wake.
Pia, bado lipo tatizo kwa baadhi ya wanajamii ndani na nje ya shule mfano, viongozi, wazazi, wanafunzi na walimu kuendeleza jadi ya njia - mkato katika kufanikisha mambo mathalani, kuutafuta ufaulu kwa namna mbalimbali ikiwemo kutegemea tahakiki kwa asilimia miamoja, huku baadhi ya walimu wakifanya kazi ya kuhakiki vitabu kwa lengo la wanafunzi kukariri na kufaulu mitihani. Matokeo yake ni wanafunzi kujifungia katika desturi ya utegemezi bila hata kukijua kitabu au kuliona jalada la kitabu husika. Desturi hii haikomi; huendelea hata katika masomo mengine na katika hatua zingine za usoni za kitaaluma na kiutendaji. Uchunguzi umebaini kuwa tatizo hili linachangiwa kwa sehemu kubwa na mfumo wa elimu, na soko la ajira.
Pamoja na haya yote hata hivyo, jaribio limethibitisha kuwa hakuna tofauti ya kimtazamo na kiutendaji kati ya mwanafunzi aliyesoma na ambaye hakusoma nadharia za uhakiki wa fasihi ya Kiswahili. Kwa msingi huu, inaelekea kwa sasa hakuna sababu za kuingiza nadharia za uhakiki katika muhtasari wa Kiswahili, sekondari.

SURA YA TANO

MAPENDEKEZO, NA HITIMISHO LA MIJADALA YA UTAFITI

5. 1 Utangulizi

Msingi mkuu wa sura hii uko katika kujumuisha yale yote yaliyojitokeza katika sura nne za mwanzo, yaani sura ya kwanza, sura ya pili, sura ya tatu, na sura ya nne. Sura hii inajenga mapendekezo na hitimisho kuu la mijadala ya utafiti huu kwa kuzingatia vigezo anuai vilivyoongoza utafiti na uandishi wa tasnifu hii kama vile: tatizo la utafiti,  malengo ya jumla, na malengo mahususi yaliyoongoza utafiti wa andiko hili, umuhimu wa utafiti, mapitio ya maandiko, masuala ya mafao ya utafiti, matokeo ya utafiti - uwasilishaji, uchambuzi na mjadala mzima wa data zilizopatikana kwa lengo la kustawisha ufundishwaji wa fasihi ya Kiswahili katika shule za sekondari nchini na nje ya Tanzania, pamoja na kujenga jukwaa / daraja kwa tafiti zingine kufanyika.

5. 2 Hitimisho la Mijadala ya Utafiti

5. 2. 1 Sababu Zinazofanya Nadharia za Uhakiki Kutokuwemo katika Muhtasari wa Kiswahili Shule za Sekondari.

Pamoja na walimu wajibu hojaji kusisitiza mada ya nadharia za uhakiki wa fasihi kuingizwa katika muhtasari wa Kiswahili, hususani kuanzia kidato cha tatu huku “wakionyesha” kutokuridhishwa na utendaji wa Taasisi ya Elimu Tanzania kama chanzo cha mada hii kutokuingizwa, utafiti umebaini kutokuwepo tofauti ya kimtazamo na kiutendaji kati ya mwanafunzi aliyesoma na ambaye hajasoma nadharia za uhakiki wa fasihi ya Kiswahili, kwa sasa. Matokeo haya yanafanana na hoja ya mjibu hojaji kutoka Taasisi ya Elimu Tanzania anayedhani tatizo siyo kutokuingizwa kwa nadharia za uhakiki katika muhtasari wa Kiswahili, sekondari bali ni namna somo la Kiswahili linavyofundishwa mashuleni. Kipengele hiki kinaashiria kuwepo kwa tatizo ambalo linahitaji utafiti wa kina zaidi kwani Taasisi ya Elimu Tanzania inaelekea kutumia matokeo ya tafiti na majadiliano mbalimbali kuamua mada zipi ziingizwe au zisiingizwe kwenye mihtasari wakati walimu wanadhani kuna “wingu la sitofahamu” katika utendaji wa taasisi hii. Aidha, utafiti umebaini kuwepo udhaifu katika kufuatilia na kuchukua hatua za kinidhamu kwa walimu na wakaguzi wachache wanaohudhuria semina na warsha lakini hawatekelezi maagizo yanayotolewa na Taasisi ya Elimu Tanzania. Hali hii ni utumiaji wa rasilimali ambao hauleta tija kwa taifa na fasihi ya Kiswahili, hivyo hatua stahiki, na za haraka zichukuliwe.

5. 2. 2 Ufundishwaji wa Nadharia za Uhakiki wa Fasihi ya Kiswahili katika Shule za Sekondari nchini Tanzania

Utafiti umebaini kuwa mada ya nadharia za uhakiki wa fasihi ya Kiswahili haifundishwi kiufasaha. Badala yake kipengele hiki kimekuwa kama kiraka kwenye vazi la somo la fasihi katika shule za sekondari. Yaani, dhana hizi huguswa tu pindi hitaji la uboreshaji jambo linapojitokeza. Hii inatokana na mambo makuu mawili: (i) Kipengele hiki kutokuwa sehemu rasmi ya Muhtasari wa Kiswahili katika shule za sekondari, na (ii) Desturi iliyojengeka miongoni mwa wadau wa elimu, wakiwemo walimu, wanafunzi, na watahini “kutokuruhusu” jambo ambalo si sehemu rasmi ya Muhtasari kufundishwa au kuwa sehemu ya hoja katika mijadala au majibu ya mitihani rasmi hata kama hitaji hilo lipo na ni kubwa miongoni mwa wadau wa elimu, wanafunzi wakiwemo.
Utafiti umebaini pia kuwepo kwa upungufu mkubwa wa vitendea kazi na wataalamu wa fasihi. Vitabu hususani vya nadharia, na tahakiki mbalimbali mashuleni ni tatizo kubwa. Hivyo, wanafunzi wengi kutegemea aina moja ya tahakiki na mwandishi, jambo linaloua dhana ya ulinganifu na ulinganuzi wa hoja na mantiki miongoni mwa wasomaji na wahakiki, wakiwemo wahakiki chipukizi. Hali hii imesababisha baadhi ya wasomaji wakiwemo walimu na wanafunzi kutegemea na kukifanya kile walichonacho kuwa “msahafu mtakatifu” wa shughuli na hoja zao hivyo kuathiri ufundishwaji wa fasihi, nadharia za uhakiki zikiwemo. Kwa mujibu wa wajibu hojaji/ jaribio la utafiti walio wengi, hali hii inadhoofisha utumizi fasaha wa mbinu shirikishi, hususani mbinu ya mafunzo – linganishi.

5. 2. 3 Uhusiano Uliopo Kati ya Nadharia za Uhakiki wa Fasihi ya Kiswahili na Uwezo wa Mwanafunzi Kujitegemea Kivitendo katika Majukumu Anayopewa Ndani na Nje ya Darasa

Pamoja na nadharia za uhakiki wa fasihi ya Kiswahili kutokufundishwa kiufasaha katika shule za sekondari, bado wajibu hojaji/ jaribio la utafiti wameeleza kuwepo kwa uhusiano baina ya nadharia za uhakiki wa fasihi ya Kiswahili na uwezo wa mwanafunzi kujitegemea kivitendo katika majukumu kadha wa kadha anayopewa ndani na nje ya darasa.
Uhusiano huo umo katika mzunguko wa maisha ya kila siku kwenye nyuga na nyakati husika. Kupitia hojaji, utafiti umebaini kwamba, kwa kujifunza nadharia mbalimbali za uhakiki wa fasihi ya Kiswahili, mwanafunzi na msomaji mwingine watakuwa na utambuzi mpana zaidi wa kuyaakisi maisha halisi na idili zinazotawala maisha hayo kwa kuzingatia msingi wa hoja kuwa, hakuna jambo au tukio lenye ukamilifu mkamilifu. Jambo hili linaungwa mkono kwa kupembuliwa vizuri na mwanazuoni E. Kezilahabi katika Nagona (1990), na E. M. Songoyi katika Wimbo wa Binadamu Dunia na Bandari Salama (1990). Hivyo, kuondoa dhana ya kudharau au kupendelea kitu au jambo fulani pekee. Matokeo yake ni kuheshimu na kutathmini mambo kwa kina, kujituma, kuwajibika, kujali na kuzingatia, kujitegemea kifikra na kiutendaji, kujituma, kushirikiana na kushirikisha wengine, kujenga usikivu na utulivu, kujielimisha na kuelimisha zaidi, na mengine mengi. Huku ndiko kunakojenga weledi, utaifa, busara, heshima, ukombozi wa kweli na endelevu dhidi ya maadui wa ustawi na maendeleo ya jamii katika ujumla wake.
Uhusiano huu unafanya hitaji la kuingizwa kwenye Muhtasari wa Kiswahili, shule za sekondari, na tena kufundishwa kiweledi na kiustadi kwa kipengele cha nadharia za uhakiki wa fasihi ya Kiswahili kuwa kubwa na la msingi. Kwani fasihi ni zao na kioo cha jamii, lakini nadharia za uhakiki ni chujio na kioo cha fasihi hiyo ya jamii. Nadharia mbalimbali ni jicho lililoko angani ili kuimulika dunia na mfumo wa maisha ya watu wake kama ilivyo kwa jua na uso wa dunia. Katika kufafanua hoja hii kwa kuzingatia matokeo ya utafiti kwa jumla, inaweza kusemwa kwamba, nadharia za uhakiki ni jua, na fasihi ni dunia, hivyo nadharia zinaimulika fasihi ambayo ni maisha ya jamii.
Matokeo haya hata hivyo, yanapingana na matokeo ya jaribio la utafiti. Kwa mujibu wa matokeo ya jaribio, hakuna uhusiano, yaani tofauti ya kimtazamo na kiutendaji kati ya mwanafunzi aliyesoma na ambaye hakusoma nadharia za uhakiki wa fasihi ya Kiswahili.

5. 3 Mapendekezo

Ujenzi na upatikanaji wa jamii bora ni matokeo ya mambo mbalimbali mtambuka yanayotathminiwa na kutekelezwa kisayansi. Vivyo hivyo kwa uga wa elimu na fasihi. Utafiti huu umechungua eneo moja kati ya mengi yanayojenga weledi na umaizi kwa mwanafunzi, na msomaji wa fasihi ya Kiswahili. Huku ndiko kusema, matokeo ya utafiti huu hayatakuwa yenye tija endapo yatatazamwa kwa jicho la juu juu. Utekelezwaji wake unapaswa kuhusisha makandokando yote yanayofungamana na fasihi na elimu vya waswahili, kiutendaji na kisera. Katu matokeo haya yasitekelezwe kiyatima bali kifamilia kwa kuhusisha nyanja zote zinazotakikana katika tasnia ya fasihi, na elimu ndani na nje ya darasa.
Hivyo basi, inatarajiwa kuwa matokeo ya utafiti huu yatakuwa ni chachu na changamoto kwa wadau mbalimbali wa fasihi na elimu kutambua sababu, namna, na uhusiano wa kufundishwa au kutokufundishwa nadharia za uhakiki wa fasihi ya Kiswahili katika shule za sekondari na taasisi za elimu ya juu. Katika hatua hii wadau mbalimbali wanapaswa kuungana kuijenga jamii mpya na endelevu, jamii yenye kuamua na kutenda mambo kwa kuyasawiri kiweledi kupitia mbinu mbalimbali, nadharia za uhakiki zikiwemo. Baadhi ya wadau hao ni pamoja na: Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Taasisi ya Elimu Tanzania, Watafiti mbalimbali katika uga wa fasihi, Walimu na Wanafunzi wa Kiswahili.
Matokeo yanathibitisha kuwa kwa sasa hakuna tofauti ya kimtazamo na kiutendaji kati ya mwanafunzi aliyesoma na ambaye hakusoma nadharia za uhakiki jambo linaloungwa mkono na Taasisi ya Elimu Tanzania. Hata hivyo, walimu wajibu hojaji wanadhani kuna tofauti ya msingi hasa, na kwamba tofauti hiyo itajipambanua vema pindi utafiti wa muda mrefu utakapofanyika ukianzia darasa teule la kidato cha tatu na kuendelea na wanafunzi hao mpaka kidato cha sita au zaidi. Hoja hii inashikamana vilivyo na matokeo ya hojaji na uchunguzi. Kwa hali hii, panahitajika kufanyika utafiti wa muda mrefu utakaoanza na wanafunzi teule ambao watakuwa sehemu ya utafiti tokea kidato cha tatu hadi kidato cha sita, au zaidi ya hapo.
Utafiti umebaini pia kutokuwepo kwa mawasiliano mazuri kati ya waandaa sera, mitaala, na mihtasari mathalani Taasisi ya Elimu Tanzania na watekelezaji wa sera mashuleni hususani walimu. Hali hii imesababisha “kunyoosheana vidole” kati ya pande hizi husika pindi walipokuwa wanabainisha sababu za kutokuingizwa kwa mada ya nadharia za uhakiki katika muhtasari wa Kiswahili, sekondari. Jambo hili linapaswa kurekebishwa haraka na kwa ufanisi mkubwa ili kuboresha na kufikia malengo ya elimu, lugha, na fasihi, Tanzania.
Aidha, utafiti umebaini kuwa upungufu wa vitendea kazi, na vyenye ubora, upungufu wa wataalamu wa fasihi hususani wa nadharia za uhakiki, ukosefu wa semina, na mafunzo ya mara kwa mara kwa walimu watekeleza sera mashuleni ni moja ya sababu zinazofanya somo la Kiswahili kutokufundishwa kiufasaha ikiwemo mada ya nadharia za uhakiki. Pamoja na kwamba mada hii haimo katika muhtasari, bado Taasisi ya Elimu Tanzania inawashauri walimu kuwa wabunifu na kwa kufundisha kwao, inakuwa rahisi kwa taasisi hiyo kupata mrejesho wa kipi kiondolewe, kiboreshwe au kiingizwe kwenye muhtasari.

5. 4 Mchango wa Kazi Hii kwa Tafiti Zijazo

Katika mtalaa huu, wadau mbalimbali wakiwemo watafiti wanapaswa kuuhesabu utafiti huu kuwa daraja na rejeleo muhimu katika tafiti zao zitakazohusiana na nadharia za uhakiki wa kazi za fasihi, na ufundishwaji wake. Baadhi ya maeneo yanayohitaji tafiti zaidi ni pamoja na haya yafuatayo:
i.        Utafiti huu ulijikita katika njia kuu tatu za ukusanyaji data – uchunguzi, hojaji, na jaribio. Kwa namna fulani njia hizi zimetoa matokeo tofauti hususani katika vipengele vya sababu na uhusiano uliopo kati ya nadharia za uhakiki wa fasihi ya Kiswahili na uwezo wa mwanafunzi kujitegemea kivitendo katika majukumu kadha wa kadha anayopewa ndani na nje ya darasa. Hivyo, utafiti wa kina zaidi na wa muda mrefu unahitajika katika kusawazisha tofauti hii.
ii.      Kijiografia, utafiti huu ulijikita katika shule mbili za sekondari zenye kidato cha tano na sita, Wilayani Bunda, Mkoa wa Mara. Bila shaka, kunaweza kukawa na matokeo tofauti au yenye mawanda mapana zaidi kutoka tafiti zitakazofanywa katika maeneo mingine. Hivyo, kuna umuhimu wa kutathmini matokeo ya utafiti huu katika maeneo mengine.
iii.    Baadhi ya wajibu hojaji hususani walimu wanadhani uteuzi wa wanafunzi wa Kiswahili, kidato cha sita kuwa wajibu hojaji/ jaribio la utafiti haukuwa sahihi kwani “…uzoefu wa watoto wengi tulio nao, una chembechembe zilizojaa dhana ya ‘ufaulu mzuri’ na kwa namna ‘yoyote iwayo’… umechangia kwa kiasi kikubwa kuleta tofauti ya kimatokeo kati ya hojaji na jaribio.” Kwa muktadha huu, ama ni kweli au si kweli tafiti zinapaswa kufanyika kwa kuwatumia wajibu hojaji/ jaribio la utafiti wengine “… hususani kidato cha tatu maana hawa ndiyo wanaotakiwa kuanza shughuli za uhakiki kwa mujibu wa muhtasari wa kidato cha kwanza hadi cha nne….”
iv.    Muda wa utafiti huu ulikuwa ni miezi mitatu. Pamoja na yote yaliyojili katika utafiti huu, bado watafiti wanaweza kufanya utafiti wao kwa kipindi kirefu zaidi ili kutathmini kiwango cha athari zinazoweza kusabababishwa kwa kufundishwa au kutokufundishwa kwa nadharia za uhakiki wa fasihi katika shule za sekondari kama walivyobainisha baadhi ya wajibu hojaji/ jaribio la utafiti.
  1. Utafiti huu uliziteua nadharia za U - Marx na Umbuji wa Kirusi kuwa nadharia teule za jaribio la utafiti ilhali mafunzo – linganishi kuwa nadharia teule ya utafiti katika kubainisha na kuelezea sababu, namna, na uhusiano wa ufundishaji wa nadharia za uhakiki wa fasihi ya Kiswahili katika shule za sekondari, Tanzania. Watafiti wengine wanaweza ama (i) kujipambanua kwa kutathmini ufundishwaji wa nadharia moja ama kadhaa, au (ii) wakafanya utafiti wa mada hii (Ufundishaji wa Nadharia za Uhakiki wa Fasihi ya Kiswahili katika Tanzania) kama ilivyo lakini kwa kuongozwa na nadharia teule tofauti na zilizotumika kuongoza kazi hii.

5. 5 Hitimisho la Jumla

Ukombozi wa kweli na endelevu katika jamii ni msingi wa ustawi na maendeleo ya wanajamii wenyewe. Hatua hii hailetwi kwa njozi bali kwa vitendo stahiki kwa kutumia rasilimali zinazopatikana katika jamii husika. Miongoni mwa raslimali hizo ni pamoja na kuwepo kwa utafiti kama huu unaohusiana na ufundishaji wa nadharia za uhakiki wa fasihi ya Kiswahili katika ngazi ya sekondari kwa faida ya waswahili na fasihi yao.
Kwa sasa hapajaweza kubainika tofauti ya kimtazamo na kiutendaji kati ya mwanafunzi aliyejifunza na ambaye hajajifunza nadharia za uhakiki wa fasihi ya Kiswahili ijapokuwa baadhi ya wajibu hojaji/ jaribio la utafiti hususani walimu wanaelekea kupinga matokeo haya, hasa ya jaribio la utafiti. Pamoja na sababu za kutaka mada ya nadharia kuingizwa ama kutokuingizwa katika muhtasari wa Kiswahili, sekondari hata hivyo, lipo tatizo la msingi katika ufundishaji na uhakiki wa kazi za kifasihi ngazi ya sekondari. Aidha, utafiti umebainisha kuwa ni busara kubainishwa na kuainishwa kwanza nadharia ya uhakiki itakayotumika kuongoza mjadala au uhakiki wa kazi za kifasihi ili kuisaidia jamii kutoa hukumu “ya haki” kwa mawazo / wazo au tahakiki husika.
Kwa kuyazingatia haya, bila shaka ufundishaji wa nadharia za uhakiki wa fasihi ya Kiswahili kwa ngazi ya sekondari utaboreka kwani kwa mujibu wa Taasisi ya Elimu Tanzania “mwalimu hafungwi na muhtasari kufundisha kitu anachohisi kina tija kwa wanafunzi…. Lakini tafiti zitabainisha….” Na “…endapo kuna kipengele hakimo katika muhtasari ni ama hakipaswi kuwekwa katika ngazi husika ya kitaaluma au bado kinajadiliwa ili kuona uwezekano wa kukiingiza au la.”

MAREJEO

Abdullah, M. S. (). Mzimu wa Watu wa Kale.
Achebe, C. (1958). Things fall Apart. ———
Achebe, C. (1966). A Man of the People. ———
Ary, D., et al. (2006). Introduction to Research in Education. New York: Harcout Brace College.
Bertoncini, E. Z. (1989). Outline of Swahili literature: prose fiction and drama. Leiden/New York/ København/Köln: E. J. Brill.
Bukagile, G. R., et al. (2008). Advanced level: literature form 5 & 6. Dar es salaam: Nyambari Nyangwine Publishers.
Carson, B. (1992). Think big. Michigan: Zondervan.
Daniel, K. (1997). Elements of literature: introduction course (6th Edit.). Austin: Holt, Rinehart and Winston.
Dubos, R. (1968). So Human and Animal: how we are shaped by surroundings and events. NY / Canada: Charles Scribrery Sons.
Duerden, D & Pieterse, C. (wahariri). (1988). African writers talking. UK: Heinmann International Publishing, Oxford.
Eagleton, T. (2008). Literary theory: An Introduction. (Anniversary Edit.). Uk: Blackwell Publishers Ltd.
Eagleton, T. (1998). Criticism and ideology. London: Verso.
Eichenbaum, B. (1998). Introduction to the formal method. Katika J. Rivkin, & M. Ryan (wahariri), Literary theory: An Anthology. Uk: Blackwell Publishers Ltd.
Encarta Dictionaries & Encyclopaedia 2009.
Ferster, J. (1947). Arguing through literature: a thematic anthology and guide to academic writing. New York: McGraw – Hill.
Gardner, H. (1982). Art, mind, and Brain: a cognitive approach to creativity. New York: Basic Books, Inc. publishers.
Haji, A. I. (1981). Misingi ya uhakiki. katika A. I. Haji et al., (wahariri), Misingi ya nadharia ya uhakiki. Zanzibar: TAKILUKI.
Harrison, A. (1990). Mastering philosophy. London: The MaCmillan Press Ltd.
Hussein, E. N. (1970). Wakati Ukuta na Aliyekiona. Dar es salaam / Kampala / Nairobi: East African Publishing House.
Kadeghe, M. (—). The real English text book. —
Kawooya, V & Makokha, J. K. S. (2006). Post colonial criticism and globalisation. Katika S. S. Sewangi & J. S. Madumulla (wahariri.), Makala ya kongamano la kimataifa. University of Dar es salaam: TUKI.
Kezilahabi, E. (1988 / 1971). Rosa Mistika.  Dar es salaam University Press.
Kezilahabi, E. (1990). Nagona na Mzingile.  Dar es salaam University Press.
Kezilahabi, E. (1995).  Siasa, teknolojia na ukuaji wa fasihi ya Kiswahili. Katika Kioo cha lugha: jarida la Kiswahili la isimu na fasihi, 1, 55-56. University of Dar es salaam: TUKI.
Kiango, S. D. (1993). Utangulizi: nadharia mbalimbali katika uhakiki. Katika M. M. Msokile, Misingi ya uhakiki wa fasihi. Nairobi: East African Educational Publishers Ltd.
Kothari, C. R. (1993). Research methodology: methods and techniques. New Delhi: Wiley Eastern Ltd.
Lodge, D., & Wood, N. (wahariri). (2000). Modern Criticism and Theory: A Reader 2nd Edition. UK: Pearson Education Ltd.
Lunacharsky, A. (1973). On literature and art (2nd Edition). Moscow: Progress publishers.
Madumulla, J. S. (2006). Hali ya usomaji wa riwaya katika Tanzania. Katika S. S. Sewangi & J. S. Madumulla (wahariri.), Makala ya kongamano la kimataifa la jubilei ya TUKI­2005. University of Dar es salaam: TUKI.
Mailu, D. G. (1985, August 18). The former South African president P. W. Botha speech 1985. The Sunday Times. A South African Newspaper.
Masatu, F. J. (2008). Kikulacho ki nguoni mwako. Makumira University College.
Masatu, F. J. (2009). Teaching and learning Kiswahili poetry in secondary and higher learning institutions in Tanzania. Makumira University College; tasnifu ya shahada ya kwanza.
Masebo, J. A & N. Nyangwine. (2007). Nadharia ya Fasihi: kidato cha 5 & 6. Dar es salaam: Nyambari Nyangwine Publishers.
Masebo, J. A & N. Nyangwine. (2008). Tahakiki: vitabu teule vya fasihi kidato cha 5 & 6, uhakiki na maswali. Dar es salaam: Nyambari Nyangwine Publishers.
Mazigwa, S. A. (1991). Fasihi ya Kiswahili. Peramiho: Benedictine Publication Ndanda.
Mnyampala, M. (1990). Ngonjera za Ukuta I & II. Arusha: Eastern Africa Publication.
Mochiwa, Z. S. M. (2001). Elimu au maigizo? uhakiki wa sera ya lugha katika elimu Tanzania. Katika K. K. Kahigi (mhariri), Kioo cha lugha: jarida la Kiswahili la isimu na fasihi (Vol. 2, 1996/97). Chuo Kikuu cha Dar es salaam: Idara ya Kiswahili.
Mohamed, S. A. (1995). Kunga za nathari ya Kiswahili: riwaya, tamthiliya, na hadithi fupi. Nairobi: East African Educational Publishers.
Momanyi, C. (2001). Nadharia ya uchanganuzi wa nafsia katika mtazamo wa kike na uhakiki wa kifasihi. Katika K. K. Kahigi (mhariri), Kioo cha lugha: jarida la Kiswahili la isimu na fasihi (Vol. 2, 1996/97). Chuo Kikuu cha Dar es salaam: Idara ya Kiswahili.
Musau, P. M. (1999). Utangulizi. Katika R. M. Wafula, Uhakiki wa Tamthiliya: Historia na Maendeleo Yake. Nairobi: Jomo Kenyatta Foundation.
Msokile, M. (1991). Miongozo ya Lugha na Fasihi, 2; Uchambuzi na Uhakiki: karibu ndani. Dar es salaam University Press.
Msokile, M. (1993). Misingi ya uhakiki wa fasihi. Nairobi: East African Educational Publishers Ltd.
Msokile, M., & Sengo, T. S. Y. (1987). Uhakiki wa vitabu vya fasihi sekondari na vyuo-1. Nyanza Publications Agency.
Mulokozi, M. M. et al., (mhariri.). (2001). Ripoti ya kongamano la kimataifa la Kiswahili 2000. University of Dar es Salaam: TUKI.
Mushengyezi, A. (2003). Twentieth century literary theory. Makerere University: Department of Distance Education, Institute of Adult and Continuing Education.
Mwiria, K & Wamahiu, S. P. (wahariri). (1995). Issues in Educational Research in Africa. Nairobi: East African Educational Publishers Ltd.
Ndungo, C. M. (1991). Nadharia za uhakiki wa fasihi. Nairobi: University of Nairobi.
NECTA.  Advance Kiswahili results 2008 – 2010.
NECTA. Kiswahili 2 past papers 2006 – 2010.
Ngugi wa Thiong’o. (1967). A Grain of Wheat.
Ngugi wa Thiong’o. (1994/1997). Decolonizing the mind: the politics of language in African literature. London: James Currey & Heinemann.
Njogu, K., & Chimerah, R. (1999). Ufundishaji wa fasihi: nadharia na mbinu. Nairobi: Jomo Kenyatta Foundation.
Njozi, H. M. (1990). Utendi wa Mwanakupona and reception aesthetics. Katika E. Wesana-Chomi & H. J. M. Mwansoko (wahariri), Kiswahili (Vol. 57). University of Dar es salaam: TUKI.
Ntarangwi, M. (2004). Uhakiki wa kazi za fasihi (Tasnifu ya Shahada ya Uzamivu).−−−
Nyirenda, S. D., & Ishumi, A. G. M. (2007). Philosophy of Education: an introduction to concepts, principles and practice. Dar es salaam University Press Ltd.
P’Bitek, O. (2006). Song of Lawino and Song of Ocol. Nairobi: East African Educational
Peterson, K. H. (2001). First things first: problem of a feminist approach to African literature. Katika B. Ashcroft et al., (wahariri), the Post colonial studies reader. London & New York: Routledge.
Rice, P., & Waugh, P. (wahariri). (2001). Modern literary theory. New York: Hodder Arnold.
Rivkin, J., & Ryan, M. (1998). Strangers to ourselves: psychoanalysis. katika J. Rivkin, & M. Ryan (wahariri), Literary theory: An Anthology. Uk: Blackwell Publishers Ltd.
Robert, S. (). Wasifu wa Siti Binti Saad
Robert, S. (1991). Kusadikika. Dar es salaam: Mkuki na Nyota.
Robert, S. (2003). Kufikirika. Dar es salaam: Mkuki na Nyota.
Ruhumbika, G. (2006). Mwandishi wa Kiswahili na lugha yake katika Tanzania huru. Katika S. S. Sewangi & J. S. Madumulla (wahariri), Makala ya kongamano la kimataifa la jubilei ya TUKI­2005. University of Dar es salaam: TUKI.
Sell, R. D. (1988). The Politics of theory: ideological positions in the post modernist debate. Katika  D. Lodge (mhariri), Modern criticism and theory: A reader. London: Longman.
Sell, R. D. (1991). Literary pragmatics. Katika R. E. Asher (mhariri), Encyclopaedia of language and linguistics. London: Pergamon Press.
Senkoro, F. E. M. K. (1988). Ushairi: nadharia na tahakiki. Dar es salaam: DUP.
Senkoro, F. E. M. K. (1995). E. Kezilahabi: Shaaban Robert wa pili. Kioo cha lugha, 1 (1), 61­68. University of Dar es salaam: TUKI.
Senkoro, F. E. M. K. (2006). Fasihi ya Kiswahili ya majaribio: makutano ya fasihi simulizi na fasihi andishi. Katika F. E. M. K. F. E. M. K. Senkoro & K. K. Kahigi (wahariri), Kioo cha lugha, 4, 22­38. University of Dar es salaam: TUKI.
Senkoro, F. E. M. K. (2007). Uhalisiamazingaombwe katika fasihi ya Kiswahili: istilahi mpya, mtindo mkongwe. Katika F. E. M. K. F. E. M. K. Senkoro & K. K. Kahigi (wahariri), Kioo cha lugha, 5, 1­11. University of Dar es salaam: TUKI.
Sharma, R.N. (2005). Methodology of Educational Research. Delhi: Surjeet Publications.
Silverman, D. (2005). Interpreting qualitative data: methods for analysing talk, text and interaction 2nd Edition. London: SAGE publishers.
Songoyi, E. M. (1990). Looking at language three. DUP
Songoyi, E. M. (2008). Reflections on literature and literary criticism. The University of Dodoma: Department of Foreign Languages and Literature.
Songoyi, E. M. (1990). Wimbo wa binadamu dunia na bandari salama. Peramiho: Benedictine Publication Ndanda.
The Great Books Foundation. (1990). Introduction to Great Books (2nd series).———
The Ministry of National Education. (1982). Secondary school syllabuses: languages – English form V-VI, Kiswahili kidato cha VI (Vol. 6). Dar es salaam University Press.
The University of Dodoma. (2008). Dissertations Theses and other Publications Preparation Guidelines. Directorate of Graduate Studies.
The University of Dodoma. (2009). Almanac for full time graduate programmes 2009 / 2010 academic year. Directorate of Graduate Studies.
The University of Dodoma. (2009). Higher degrees prospectus 2009/10. The University of Dodoma: The office of the Deputy Vice Chancellor, Academic, Research and Consultancy.
The World Book. (1986). Learning Library: reports and term papers (Vol. 5). New York: World Book, Inc.
United Bible Societies. (1952). Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo BIBLIA.—
Wafula, R. M. (1999). Uhakiki wa tamthiliya: historia na maendeleo Yake. Nairobi: Jomo Kenyatta Foundation.
Wamitila, K. W. (2000). Uhakiki wa fasihi: misingi na vipengele vyake. Nairobi: Phoenix Publishers Ltd.
Williams, R. (1977). Marxism and literature. Oxford University Press.
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi. (2009). Muhtasari wa Kiswahili kwa elimu ya sekondari kidato cha V-VI. Dar es salaam: Taasisi ya Elimu Tanzania.
Wizara ya Elimu na Utamaduni. (1997). Muhtasari wa Kiswahili kwa elimu ya sekondari kidato cha I-IV, kidato cha V-VI. Dar es salaam: Taasisi ya Elimu Tanzania.
Wizara ya Elimu ya Taifa. (1975). Muhtasari wa sekondari: Kiswahili kidato cha sita.—
Wright, E. (1991). Modern psychoanalytic criticism. Katika A. Jefferson & D. Robery (wahariri), Modern literary theory. London: B. T. Batsford

VIAMBATISHO MBALIMBALI

Kiambatisho cha Kwanza: HOJAJI KWA WALIMU WA KISWAHILI/MTAALAMU TAASISI YA ELIMU TANZANIA

Shule:…………………..
Mimi ni mwanafunzi wa Shahada ya Uzamili ya Sanaa katika Fasihi ya Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dodoma. Nipo katika utafiti unaohusu Ufundishaji wa Nadharia za Uhakiki wa Fasihi ya Kiswahili katika Shule za Sekondari Nchini Tanzania. Lengo kuu ni kutathmini namna mada hii inavyofundishwa hata kumjengea mwanafunzi ujuzi na weledi wa kuzikabili changamoto mbalimbali anazokumbana nazo ndani na nje ya darasa. Katika utafiti huu kila jibu ni sahihi na muhimu sana, kwani kinachotakiwa ni mtazamo wako kulingana na kipengele husika. Tafadhali eleza au weka tiki [√] katika kiboma unachodhani ni sahihi kwa mujibu wa mtazamo wako.  Mawazo yako ni MUHIMU SANA, na yatakuwa ni SIRI.
A: HABARI BINAFSI
Jinsi: [  ] Ke      [   ] Me
Kiwango cha Elimu: [  ] Diploma     [  ] Shahada ya Kwanza     [  ]  Shahada ya Uzamili
Masomo uliyosomea: …........................  Masomo unayofundisha: …….……………...
Umri kazini: ………… Uzoefu katika kufundisha somo/masomo hayo: .….…………
B: MASWALI YA UTAFITI
1.      Kwa mujibu wa Muhtasari wa Kiswahili shule za sekondari, nadharia za uhakiki wa fasihi ya Kiswahili kama vile Umarx na Umbuji siyo mada rasmi zinazopaswa kufundishwa mashuleni. Kwa mtazamo wako, ni sababu zipi zinazofanya mada hii kutokuwemo katika Muhtasari wa Kiswahili shule za sekondari? ……………………
…………………………………………………………………………………………
2.      Pamoja na mada hii kutokuwemo katika Muhtasari wa Kiswahili shule za sekondari Je, unazifundisha nadharia za uhakiki wa fasihi kwa wanafunzi wako?
[  ] Ndiyo [  ] Hapana
Iwapo jibu ni Ndiyo, kwa nini unazifundisha? ………………………………………….………………………………………………………………………………
Iwapo jibu ni Hapana, kwa nini hauzifundishi mada hii? ……………………………...
……………………………………………………………………………………
3.      Ni njia zipi / ipi unayoitumia kufundisha mada ya nadharia za uhakiki, na kwa nini iwe njia hiyo/ hizo? …………………………………………………………………...
…………........................................................................................................................
4.      Kwa mtazamo wako, unadhani mada ya nadharia za uhakiki inafaa kufundishwa kuanzia kidato cha ngapi? …………………………………………………………….

Kwa nini kidato hicho? ……………………………………………………………...
…………………………………………………………………………………………
5.      Kwa mtazamo wako, unadhani kuna uhusiano kati ya mwanafunzi kujifunza nadharia za uhakiki na uwezo wake katika kuzikabili changamoto mbalimbali ndani na nje ya darasa?
[  ] Ndiyo           [  ] Hapana          [  ] Kiasi
Kwa nini Ndiyo/Hapana? ………..…………………………………………………...
…………………………………………………………………………………..…
6.      Nini tathmini yako juu ya mada ya nadharia za uhakiki kutokuwemo katika Muhtasari wa Kiswahili sekondari? …………………………………………………..

ASANTE SANA KWA USHIRIKIANO
Furaha J. Masatu
0755 - 510 589 / 0715 – 510 588 / 0688 – 50 50 10

Kiambatisho cha Pili: HOJAJI KWA WANAFUNZI WA KISWAHILI KIDATO CHA SITA

Shule:…………………..
Mimi ni mwanafunzi wa Shahada ya Uzamili ya Sanaa katika Fasihi ya Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dodoma. Nipo katika utafiti unaohusu Ufundishaji wa Nadharia ya Uhakiki wa Fasihi ya Kiswahili katika Shule za Sekondari Nchini Tanzania. Lengo kuu ni kutathmini namna mada hii inavyofundishwa hata kumjengea mwanafunzi ujuzi na weledi wa kuzikabili changamoto mbalimbali anazokumbana nazo ndani na nje ya darasa. Katika utafiti huu kila jibu ni sahihi na muhimu sana, kwani kinachotakiwa ni mtazamo wako kulingana na kipengele husika. Tafadhali eleza au weka tiki [√] katika kiboma unachodhani ni sahihi kwa mujibu wa mtazamo wako.  Mawazo yako ni MUHIMU SANA, na yatakuwa ni SIRI.
MASWALI
3.      Mada ya nadharia za uhakiki wa fasihi ya Kiswahili siyo mada rasmi katika Muhtasari wa Kiswahili, sekondari ijapokuwa inasadikiwa kufundishwa mashuleni. Je, mnaisoma mada hii shuleni kwako? ………………………………………………
Kama mnajifunza, tafadhari fafanua namna inavyofundishwa.
………………………………………………………………………………………………………………………………………………………………………………………………………………………………………………………………………………
4.      Je, umewahi kuzisikia dhana zifuatazo?
                                                                    Nimeisikia             Sijaisikia
i.                    Umarx                                            [    ]                   [    ]                 
ii.                  Umbuji                                           [    ]                   [    ]  
iii.                Ufeministi                                       [    ]                   [    ]
5.      (a) Kama umewahi kuzisikia / kuisikia, Je, ulizisikia / uliisikia wapi?
……………………………………………………………………………………
(b) Ulisikia zikielezwaje / ikielezwaje?
…………………………………………………………………………………… ……………………………………………………………………………………
(c) Kwa mawazo yako, unazielezaje dhana za Umarx, Umbuji, na Ufeministi?
.................................................................................................................................. ……………………………………………………………………………………..
6.      Nadharia za uhakiki wa fasihi ya Kiswahili siyo mada rasmi katika Muhtasari wa Kiswahili, sekondari, kwa mtazamo wako, unadhani kuna uhusiano kati ya mwanafunzi kujifunza nadharia za uhakiki na uwezo wake katika kuzikabili changamoto mbalimbali ndani na nje ya darasa?
[  ] Ndiyo           [  ] Hapana          [  ] Kiasi

Kwa nini Ndiyo / Hapana? ………..…………………………………………………
…………………………………………………………………………………………………………………………………………………………………………
7.      Nini tathmini yako juu ya mada ya nadharia za uhakiki kutokuwemo katika Muhtasari wa Kiswahili sekondari? …………………………………………………..
…………………………………………………………………………………………..………..………………………………………………………………………………








ASANTE SANA KWA USHIRIKIANO
Furaha J. Masatu
0755 - 510 589 / 0715 – 510 588 / 0688 – 50 50 10

Kiambatisho cha Tatu: Fomu ya Uchunguzi

Shule: ………………………
FOMU YA KUMUONGOZA MTAFITI KATIKA UCHUNGUZI
Swali la kuongoza uchunguzi wa mtafiti
Je, nadharia ya uhakiki wa Fasihi ya Kiswahili inajumuishwa katika kujifunza Fasihi ya Kiswahili katika Shule za Sekondari nchini Tanzania?
(weka tiki √ sehemu inayohusika)
  Ndiyo         Kiasi      Hapana
i.                    Kazi (mazoezi) anazopewa mwanafunzi
ii.                  Notisi za mwalimu na mwanafunzi
iii.                Azimio la somo
iv.                Andalio la somo
v.                  Muhtasari wa kiswahili
vi.                Karatasi ya 2 ya Mtihani wa Taifa, 2006 - 2010
vii.              Vitabu/marejeleo teule
viii.            Vitabu/Marejeleo mengine yanayotumika kujifunzia fasihi ya Kiswahili
a.       Yanayotumiwa na walimu pekee
b.      Yanayotumiwa na wanafunzi pekee
c.       Yanayotumiwa na makundi yote mawili kwa ushirikiano
Iwapo inajumuishwa ni kwa kiasi gani?
…………………………………………………………………………………………………………………………………………………………………………………………

Kiambatisho cha Nne: Ufahamu na Swali la Utafiti

Chanzo cha Kifungu cha Habari: Mtihani wa Taifa, Kiswahili, Karatasi ya Pili kwa Watahiniwa Wasiokuwa Shuleni – Ijumaa, 12 Februari 2010 Asubuhi (Sehemu E: Usanifu wa Maandishi).
Mtunzi wa Swali: Furaha J. Masatu

Kiambatanisho cha Tano: Vielelezo vya Majibu Yatokanayo na Jaribio la Utafiti

HABARI NYINGINEZO

Jedwali 2: Bajeti
S/NO
Mahitaji
Idadi/kiasi
Kiasi cha Fedha
1.       
Printa (Canon ­  three in one)
1
400, 000/-
2.       
Rimu
7
42, 000/-
3.       
Note book
1
3, 000/-
4.       
Wino wa printa
tyubu 3
450, 000/-
5.       
Kalamu za wino
10
3, 000/-
6.       
Penseli
2
200/-
7.       
Rewritable CD
5
15, 000/-
8.       
Usafiri
        i.            Kwenda ­ kurudi katika utafiti
      ii.            Kuonana na Mshauri wangu Mara ­ Dodoma ­ Mara


awamu 10


awamu 10

450, 000/-


1, 000, 000/-
9.       
Fedha ya kujikimu
Siku 90 ×15, 000/-
1, 350, 000/-
10.   
Proof ­ reading fee
200 pages × 10, 000/-
 2, 000, 000/-
11.   
Ada ya usimamizi
Msimamizi 1
300, 000/-
12.   
Uzalishaji wa tasnifu ya kukusanywa
Nakala 8
500, 000/-
Jumla Kuu


6, 513, 200/-


Jedwali 3: Ratiba ya Utafiti*
S/NO
Tarehe
Shughuli
1.       
Machi 01, 2010 ­ Machi 19, 2010
Uandishi na uwasilishaji wa mada na Iksili
2.       
Machi 20, 2010 ­ Mei 14, 2010
Uandishi wa pendekezo
3.       
Mei 15, 2010 ­ Mei 31, 2010
Tathmini ya awali ya mbinu na vifaa vya utafiti
4.       
Juni 16, 2010 ­ Juni 26, 2010
Uwasilishaji wa pendekezo
5.       
Septemba 2010-Novemba 2010
Tathmini ya jumla ya mbinu na vifaa vya utafiti.
Ukusanyaji wa data.
6.       
Desemba 2010
Uchambuzi wa data
7.       
Januari  2011
Uandishi wa awali wa rasimu ya tasnifu
8.       
Februari 2011 ­ Machi 2011
Uhariri, kusoma prufu, na uandishi wa rasimu ya tasnifu kwa ajili ya kukusanya
9.       
Aprili 2011 ­ Juni 2011
Kukusanya tasnifu na utetezi wa tasnifu
10.   
Julai 2011
Masahihisho, uzalishaji, na ukusanyaji rasmi wa tasnifu baada ya marekebisho (kama yapo)
*Ratiba hii imezingatia baadhi ya maelekezo kutoka shajara ya mwaka ya Chuo Kikuu cha Dodoma, 2009/2010, na UDOM. (2008). Dissertations Theses and other Publications Preparation Guidelines.

1 comment:

  1. Kazi njema sana. Ikawe mwanga katika jamii yetu hususani kwenye taaluma ya fasihi.
    Furaha J. Masatu, kalamu yako ie iendelee kuwa silaha muhimu ya fikra na taaluma.

    ReplyDelete