Tuesday 14 May 2013

KIDAHIZO




KIDAHIZO NI MSINGI WA KAMUSI
CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM
Ndumbaro Eric F.

IKISIRI
Jamii nyingi duniani, hasa jamii za wasomi zinaamini kuwa, kamusi ndio nyenzo kuu katika kujua maarifa mbalimbali yaliyofumbata katika nyanja mbalimbali kama vile: uchumi, siasa, utamaduni, elimu, nk. Pia hata wale wanaoamini katika BIBLIA takatifu na KORAN tukufu kamusi kwao ni rejeleo muhimu sana. Hii ni kutokana na kwamba, maana za maneno yaliyomo katika vitabu hivyo pia zimetolewa katika kamusi. Hivyo maneno yote tutumiayo katika shughuli zetu za kila siku hupatikana katika kamusi kama kidahizo.
Katika makala hii tujadili kwa kina ili tuweze kujua nini maana ya kidahizo, na inamaana gani kusema kidahizo ndio msingi wa kamusi? Au nini maana ya kidahizo kuwa msingi wa kamusi? Je bila kidahizo hakuna kamusi? Je kamusi inaundwa na kidahizo tu? Hivyo basi, ili kauli hii iweze kueleweka vizuri, itafafanuliwa kwa kuzingatia maumbo mbalimbali ya maneno yanayoweza kukaa katika nafasi ya kidahizo.
Makala hii imegawanyika katika sehemu kuu tatu: sehemu ya kwanza itajadili kwa ufupi usuli wa kamusi, sehemu ya pili, tutaangalia fasili za dhana za msingi zilizojitokeza, sehemu ya tatu ufafanuzi wa kauli kwa kuzingatia maumbo mbalimbali ya kidahizo na sehemu ya nne ni hitimisho.

Usuli wa kamusi
Kwa kifupi, utungaji wa kamusi ulianzia katika jamii zilizojua kusoma na kuandika, kama vile; jamii za Iraq, wasumeli na waakadi. Jamii ya kisumeli iliyoishi Mesopotamia ya kusini miaka ya 4000 – 2000 K.K iliendelea sana kisayansi hasa kuandika, hisabati, na kuhifadhi nyaraka mbalimbali. Nyaraka hizo walizihifadhi kwa kuandika katika matofali mabichi.
Jamii hizi zilihitaji kamusi ili kuweza kufahamu maana za maneno yasiyofahamika ambayo watumiaji wa lugha walikumbana nayo katika vitabu na magazeti. Hali hii ilisababishwa na kukua kwa lugha katika maana ya kuongezaka kwa msamiati na kupanuka kwa matumizi ya lugha. Hivyo basi, ilihitajika kamusi ili kuweza kupata ufafanuzi wa dhana mbalimbali zilizoibuka kutokana na maendeleo ya jamii. Orodha za maneno magumu zilizojulikana kama faharasa zilikusanywa pamoja na kufanya kitabu cha maneno na maana zake yaani  kamusi.
Hivyo basi, huu ni uthibitisho tosha unaotudhihirishia kwamba, tangu mwanzo wa utungaji wa kamusi ulitegemea faharasa yaani orodha ya maneno yaliyokusanywa na kutolewa maana zake. Leo hii orodha hiyo ya maneno yaliyopo katika kamusi inajulikana kama vidahizo.
Fasili ya dhana za msingi:
Kabla ya kuingia katika kiini cha mada yetu, inafaa tujue maana ya dhana za msingi zilizojitokeza ili tuwe katika nafasi nzuri ya kuweza kuelewa lengo la mjadala huu. Dhana muhimu zinazojitokeza katika mada yetu ni kama vile: kamusi, kidahizo na neno msingi. Wataalam mbalimbali wamejadili dhana hizi kama ifuatavyo:
TUKI (2004) wanaeleza kuwa, kamusi ni kitabu cha maneno yaliyopangwa kwa utaratibu wa alfabeti na kutolewa maana na maelezo mengine.
Mdee na wenzake (2011) wanafafanua kuwa, kamusi ni kitabu chenye maneno au vidahizo vilivyopangwa kialfabeti na kutolewa maana na maelezo ya matamshi, taarifa za kisarufi nk.
Zgusta (1971) akinukuliwa na Mdee (1997) anaeleza kuwa; kamusi ni kitabu cha marejeo chenye msamiati uliokusanywa kutoka kwa wazungumzaji wa jamii fulani na kupangwa katika utaratibu maalumu, kisha kufafanuliwa kwa namna ambayo wasomaji wanaweza kuelewa.
Fasili hizi zilizotolewa na wataalam hawa zinaonekana kuwa na udhaifu kidogo, kwani kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia kamusi hazihifadhiwi kwenye vitabu tu, bali hata katika mfumo wa kielektroniki. Hii ina maana kwamba, tuna kamusi zilizo katika nakala laini na nakala ngumu ambazo zinaweza kuhifadhiwa katika santuri, simu, tarakilishi, nk.
Hivyo tunaweza kueleza kuwa, kamusi ni orodha ya maneno yaliyo katika nakala ngumu au laini yaliyopangwa kialfabeti na kutolewa maana pamoja na maelezo mengine na kuhifadhiwa katika kitabu, santuri, simu, tarakilishi au katika mfumo wa kielekroniki. 
Baada ya kujua maana ya kamusi, sasa tuangalie maana ya neno kidahizo kama moja ya dhana muhimu katika mada yetu. Kidahizo kimefasiliwa na wataalam mbalimbali kama ifuatavyo:
Mdee na wenzake (kashatajwa) wanafasili kidahizo kuwa ni neno ambalo huingizwa katika kamusi na kufasiliwa na aghalabu huwa katika chapa iliyokoza.
TUKI (2001) wanasema, kidahizo ni neno linaloingizwa katika kamusi ili lifafanuliwe kwa kupatiwa maelezo yanayohusu taarifa za kisarufi, maana, matumizi, etimolojia, semi mbalimbali za lugha n.k. Kwa maneno mengine kidahizo ni msamiati unaoingizwa katika kamusi na kufasiliwa, mara nyingi huandikwa kwa maandishi yaliyokolezwa wino mfano; dubwana. Na kila kidahizo huwa katika aya yake.
Kwa kifupi tunaweza kusema kwamba, kidahizo ni neno lililoingizwa katika kamusi kama neno kuu lenye kukolezwa wino ambalo huorodheshwa kwa mpangilio maalum ndani ya kamusi na hutolewa ufafanuzi wa maana pamoja na taarifa nyingine zinazohusu neno hilo.
Pamoja na fasili tulizoziona BAKIZA (2010), wanaongeza sifa muhimu za kidahizo ambazo kwazo tunaweza kuona umuhimu wa kidahizo kama ndiyo msingi wa kamusi nyingi. Sifa hizo zimetajwa kama ifuatavyo: kidahizo hukaa mwanzoni mwa kifungu au vifungu vya maneno, hubeba dhamana ya kuwa neno kuu linalofasiliwa, huweza kuwa katika aina zote za maneno kama vile: kitenzi, nomino, kivumishi, nk.
Hivyo, kulingana na fasili ya kamusi, kidahizo pamoja na sifa za kidahizo, tunaweza kusema kwamba, utungaji wa kamusi yoyote ile unategemea sana uwepo wa vidahizo kwani, kidahizo ndiyo kitako/msingi ambapo taarifa nyingine hujengwa juu yake. Au tunaweza kusema kuwa, kidahizo ndiyo kitu cha mwanzo kabisa ambacho ni  muhimu kuwepo kabla ya vitu vingine kama vile lugha kienzo nk.
Hivyo basi, kwa kuthibitisha umuhimu wa kidahizo katika kamusi tuangalie jinsi maumbo mbalimbali yanavyotokea katika nafasi ya kidahizo na kukifanya kiwe ndio msingi wa kamusi.
Maumbo ya maneno katika nafasi ya kidahizo:
Katika sehemu hii tutazidi kufafanua maana ya kauli hii kwa kuzingatia maumbo mbalimbali yanayoweza kukaa nafasi ya kidahizo na kukifanya kidahizo kuwa msingi wa kamusi. Katika utungaji wa kamusi ni kweli kabisa kuwa, kuna maumbo tofautitofauti yanayoweza kujitokeza na kukaa katika nafasi ya kidahizo. Maumbo hayo ni kama vile:
Maumbo changamani: haya ni maneno yaliyoambishwa viambishi mbalimbali kama vile, viambishi vya wingi na umoja, viambishi vya hali nk. ili kupata kitu kipya na tofauti. Kwa mfano Mdee na wenzake (wameshatajwa) wameonesha maumbo hayo kama vile; Utepetevu [u-] umbo hili lina kiambishi awali “u-” kinachoashiria hali fulani. Pia Mtu, Mtoto maumbo haya yaani “Mtu” na “Mtoto” yameambishwa kiambishi awali cha umoja ambacho ni “m-”.
Pia kuna maumbo ambatani. Kama ilivyo katika maumbo changamani nafasi ya kidahizo pia huweza kukaliwa na maumbo ambatani yaani, maneno yaliyoungana pamoja ili kuunda neno moja lenye maana moja. Kwa mfano, rediokaseti, pepopunda, ndegechai, kichwamaji, uraiapacha, mwanamapinduzi, mwanasoka, mwanakijiji, nk.
Vilevile nafasi ya kidahizo huweza kukaliwa na maumbo radidi, yaani maneno yanayojirudiarudia au yenye viambishi vinavyojirudiarudia. Uradidi huo ndio unaoleta maana tofauti katika neno hilo. Kwa mfano TUKI (2001), wameonesha maumbo radidi kama vile; kumbikumbi, kumbakumba, guruguru, tapatapa, chapachapa, gumegume, nyondenyonde, njongwanjongwa, nk.
Pia maumbo huru/sahili huweza kujitokeza katika nafasi ya kidahizo. Maumbo haya ni yale maneno yasiyoambikwa viambishi vyovyote, yaani yameundwa na mofimu moja tu. Mfano wa maumbo hayo ni kama vile: jiwe, baba, mama, kalamu, kiti, saa, joto, amza, baridi, fimbo, mbugi, ngao, ngurumo, nk.
Vilevile nafasi ya kidahizo huweza kukaliwa na maumbo ya kiakronimi. Haya ni maumbo ya neno yaliyoundwa kutokana na herufi za mwanzo za maneno. Kwa mfano, TUKI (2006) kuna maneno kama vile; TANU (abbr) Tanganyika African National Union.  UNESCO (abbr) Shirika la Elimu Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (United Nations Educational Scientific, and Cultural Organization). TNT (abbr) Baruti kali. Pia TUKI (2004) wameonesha akronimia kama vile, VVU, UKIMWI, nk.
Vilevile Thompson (1995), ameonesha maumbo ya akronimi kama vile; St. (abbr) Street, Saint. UN (abbr) United Nations, WHO (abbr) Shirika la Afya Duniani (World Food Organization), OAU (abbr) Organization of African Union, NATO (abbr) North Atlantic Treaty Organization, nk.
Maumbo yaliyofupishwa/katishwa. Haya ni maumbo ya maneno yaliyofupishwa kutoka katika neno moja au zaidi. Kwa mfano, TUKI (wameshatajwa) wameonesha umbo kama vile: Chajio nm chakula cha jioni, bimkubwa, bikizee. Mdee na wenzake (wameshatajwa) Chamchana nm chakula cha mchana. Pia TUKI (2006) kuna maneno kama vile; Plane = Aero plane, Exam = Examination, Memo n  ̴ randum, nk.
Vilevile nafasi ya kidahizo huweza kukaliwa na maumbo pekee.  Haya ni majina maalum ya watu au mahali. Kwa mfano Mdee na wenzake (wameshatajwa) wameonesha maumbo ya pekee kama vile; Afrika, Ulaya, nk. Pia Mckean (2005) ameonesha maumbo kama vile; Gates, Henry, Newtonian/Newton, Clinton, Hitler, Austria-Hungary, Tanga, Tanzania, nk.
Naye Sewangi (2007), katika makala yake ameonesha kuwa hata homonimia zinatambulika kama kidahizo katika kamusi[1]. Hivyo kidahizo huweza kukaliwa na maumbo ya homonimia yaani neno ambalo hufanana kiumbo na neno au maneno mengine lakini lina maana tofauti na maneno hayo. Kwa mfano Mdee na wenzake (wameshatajwa) wameonesha homonimia kama vile; mbuzi1 nm kifaa cha kukunia nazi, mbuzi2 nm mnyama afugwaye na binadamu anayefanana na swala. Pia hariri1 nm aina ya nyuzi, hariri2 kt fanya masahihisho katika maandishi.
Sewangi (ameshatajwa) anataja tena umbo la sinonimia kama umbo jingine linaloweza kukaa nafasi ya kidahizo au kuingizwa kama kidahizo katika kamusi[2]. Maumbo ya sinonimia ni maneno yenye maana iliyo sawa na neno jingine. Kwa mfano TUKI (2001) wameonesha baadhi ya sinonimia kama maumbo tofauti, mfano neno munyu na neno chumvi,
Nafasi ya kidahizo pia huweza kukaliwa na maumbo dhahania. Haya ni maumbo ambayo mara nyingi huanza na “u”, huwa katika ngeli ya [u-]. Maumbo haya aghalabu huwa ni dhahania kwani ni ya kufikirika tu, hayawezi kuonekana au kushikika. Kwa mfano, maneno kama uzuri, ubaya, uchungu, ubinafsi, uadilifu, uchoyo, uchumi, uamuzi, nk.
Vilevile maumbo nyambuka nayo huweza kukaa nafasi ya kidahizo. Maumbo haya ni yale ambayo huweza kunyumbuliwa/kurefushwa kwa kuongezewa viambishi awali au viambishi tamati. Mfano wa maumbo hayo ni pamoja na; nyanyapa.a, nunu.a, nyanyu.a, chez.a, chinj.a, mpangishaji, mpepetaji, msemaji, nk.
Maumbo mzizi pia huweza kujitokeza katika nafasi ya kidahizo. Haya ni maumbo ya maneno ambayo yametolewa viambishi vyote vya awali na tamati na kubaki pekepeke. Mfano wa maumbo mzizi ni; -epesi, -eupe, -etu, -erevu, -ote, -ovu, -oga, nk.
Pia maumbo virai nayo huweza kukaa nafasi ya kidahizo, kwa mfano; mlango wa fahamu, mlango wa bahari, mpanda farasi, Umoja wa Mataifa, mwendesha mashtaka, nk.
Maumbo funge. BAKIZA (wameshatajwa), wameonesha jinsi nahau na misemo mbalimbali inavyoweza kujitokeza katika nafasi ya kidahizo. Mfano wa maumbo ya nahau yaliyopo nafasi ya kidahizo ni; Kula upepo, piga chuku, piga danadana, ng’oa nanga, nk. Pia mfano wa maumbo ya misemo; Ahadi ni deni, chanda na pete, chungulia kaburi, domo kaya, nk.
Maumbo ya methali pia yameoneshwa kama kidahizo katika kamusi, kwa mfano BAKIZA (wameshatajwa) wameonesha maumbo ya methali kama vile; Aonjaye asali huchonga mzinga, baada ya chanzo kitendo, asiye jua maana haambiwi maana.
Vilevile tuna kamusi za methali mbalimbali ambazo zimetolewa maana na matumizi yake. Kwa hiyo tunaweza kusema kuwa, nafasi ya kidahizo pia huweza kukaliwa na methali. Kwa mfano, King’ei na Ndalu (2008) wameonesha methali mbalimbali katika nafasi ya kidahizo zikiwa katika mpangilio maalum yaani kiabjadi. Mfano; Akili ni mali, Akiba haiozi, Bahari haishi zinge, Cheka uchafu usicheke kilema, nk.
Hivyo basi, maumbo yote tuliyoyaona katika nafasi ya kidahizo yanatudhihirishia kwamba, kidahizo ni muhimu sana katika kamusi. Pia ndio msingi wa kamusi, na huweza kujitokeza katika maumbo mbalimbali. Vilevile hata watumiaji kamusi hurejelea kidahizo ili kuweza kupata taarifa mbalimbali kuhusu kidahizo husika, kama vile; maana, matumizi, asili, matamshi, nk.
MAREJEO:
BAKIZA (2010). Kamusi ya kiswahili Fasaha. Oxford University Press, East African Ltd.Nairobi.

King’ei na A. Ndalu (2008). Kamusi ya Methali (Toleo Jipya). East African Education Publishers. Nairobi.
McKean, E. (2005). The New Oxford American Dictionary. (2nd. Edt). Oxford University Press. 
Mdee, J.S. (1997). Nadharia na Historia ya Leksikografia.Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili: Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Mdee, J. S. na wenzake. (2011). Kamusi ya Karne ya 21. Longhorn Publishers (K) Ltd. Nairobi, Kenya 
Sewangi, S.S. (2007) Uundaji wa Istilahi za Kiswahili Kileksikografia na Athari zake”, katika Nordic Journal of African Studies 16(3): 333–344. University of Dar-es-Salaam, Tanzania.

Thompson, D. (1995). The Concise Oxford Dictionary of Current English. (9thEdt) Clarendon Press. Oxford.
TUKI (2001). Kamusi ya Kiswahili-Kiingereza. Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Tanzania.
TUKI (2004). Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Oxford University Press.

TUKI (2006). English-Swahili Dictionary (3rd Edt). Institute of Kiswahili Research.                                           University of Dar es Salaam. Tanzania.

[1] homonimi huingizwa kama kidahizo kimoja na maana zake kutofautishwa”
[2] sinonimi huingizwa kama vidahizo tofautitofauti

No comments:

Post a Comment