Tuesday, 7 May 2013

MATATIZO NA SHUJAASHUJAA WA TENDI NA MATATIZO YA KIJAMII
CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM
Ndumbaro, Eric. F
Ikisiri
Kila kukicha matatizo yanazidi kuongezeka katika jamii tunamoishi, kiasi cha kumfanya mwanadamu kuishi kwa mashaka kila iitwapo leo. Matatizo hayana mwenyewe, si masikini si tajiri, si shujaa wala dhaifu. Watu wote huandamwa na matatizo japo katika viwango tofauti tofauti. Hali hii imewafanya hata baadhi ya wanamuzi kama Lucky Dube kuhitimisha kwamba, tunaishi katika ulimwengu uliochanganyikiwa. [1]
Makala hii inakusudia kujadili dhana ya Shujaa wa Tendi kwa ujumla na matatizo mbalimbali ya kijamii katika maisha ya shujaa. Lengo likiwa ni kuchunguza kama shujaa anaweza kukabiliwa na matatizo ya kijamii kama vile: njaa, magonjwa, vita, ukame, kukosa watoto, woga, upweke nk. Je,anayakabilije matatizo hayo, au yeye hajawahi kukabiliwa na tatizo lolote? Je, shujaa hashindwi, na kama anashindwa anashindwa kama wanavyoshindwa watu wengine? Ushujaa wake upo kwenye nini/kipi kinamfanya aitwe shujaa?
Makala hii imegawanyika katika sehemu nne. sehemu ya kwanza itajadili usuli wa shujaa na tendi, sehemu ya pili utangulizi; mashujaa wa kihistoria katika Afrika, sehemu ya tatu itachambua shujaa na matatizo ya kijamii katika tendi za kiafrika na sehemu ya nne mapendekezo na hitimisho. 
Usuli
Kabla ya kuanza kujadili mada husika inafaa kujipa wasaa kwa kupitia kazi mbalimbali za wataalamu waliotangulia ili kuona wamejadili nini kuhusiana na dhana ya tendi pamoja na shujaa wa tendi, hususani tendi za kiafrika.
Tendi zimefasiliwa na wataalamu mbalimbali katika mitazamo tofauti tofauti. Baadhi ya wataalamu wamekuwa na mtazamo hasi juu ya uwepo wa tendi kati bara la Afrika hasa wataalamu wa kimagharibi. Mfano mzuri unaothibitisha mtazamo hasi ni ule utafiti wa Finnegan katika tendi za kiafrika.
Finnegan (1970), kama alivyorejelewa na Mulokozi (2009) alidai kwamba, utanzu huu hauonekani sana katika Afrika. Alisema hivyo kutokana na vigezo vyake binafsi alivyovitumia katika utafiti wake juu ya uwepo wa tendi katika jamii za kiafrika. Kutokana na hitimisho lake kuwa Afrika ya kusini mwa Sahara hakuna tendi, umesababisha mdahalo mrefu kuhusu utanzu huu. Wataalamu kama Okpewho (1979), Johnson (1986), Mulokozi (1987) na wengi wamethibisha katika tafiti zao kuwa, tendi ni fani iliyoenea katika bara la Afrika.
Wamitila (2003) anafafanua kuwa, utenzi ni shairi refu la kisimulizi linalozungumzia kwa mapana na mtindo wa hali ya juu matendo ya mashujaa au shujaa mmoja.
Udhaifu unaojitokeza kwa mtaalamu huyu, ni kwamba amefasili tendi katika mawanda finyu sana kwani, tendi hazizungumzii masuaa la kishujaa tu bali utendi unaweza kuzungumzia hata masuala mengine ya kijamii kama vile malezi, vita, mawaidha nk.
Ngure (2004) anaeleza kwamba, huu ni utanzu wa ushairi unaosimulia hadithi ndefu, yenye maudhui mazito, mtindo na lugha ya hali ya juu, na ambao mhusika mkuu wake ni shujaa ambaye matendo na majaliwa yake huathiri jamii. Mfano ‘Utenzi wa Fumo Liyongo’, wa ‘Mohammed Kijumwa.’
Udhaifu wa wafasili hii ni kwamba, mtaalamu huyu hajabainisha hayo maudhui mazito ni yapi, je ni ya kishujaa, kiuchumi, kijamii au kisiasa? Pia hayo matendo ya shujaa yana athiri vipi jamii, je ni athari hasi au chanya?
Mulokozi (ameshatajwa) anaeleza kwamba, utendi ni mashuhuri zaidi katika kundi la ghani-simulizi. Utendi ni ushairi wa matendo. Ni utungo mrefu wenye kusimulia matukio ya kishujaa yenye uzito wa kijamii au kitaifa. Matukio haya huweza kuwa ya kihistoria, lakini tendi nyingi huchanganya historia na visakale au visasili.
Fasili hii kwa kiasi kikubwa inaonekana kuwa na mvuto kutokana na kwamba, imeangalia mambo katika mawanda mapana zaidi ukilinganisha na fasili zilizotangulia. Kwa mantiki hiyo nakubaliana na fasili hii.
Kutokana na maelezo ya wataalamu hawa, imebainika kwamba, katika Afrika tendi zimekuwepo tangu zamani isipokuwa katika umbo la kisimulizi. Umbo ambalo wanazuoni wa kimagharibi wameshindwa kulitambua. Katika kuonesha msisitizo Mulokozi anasema kwamba, tunao ushahidi wa kutosha kuhusu uwepo wa tendi[2].
Baada ya kuangalia kwa ufupi usuli wa tendi kwa mujibu wa wataalamu mbalimbali, ufuatao ni usuli wa shujaa wa tendi za kiafrika kama ulivyodadavuliwa na baadhi ya wataalamu wa kimagharibi na kiafrika.
Wataalamu wengi wametoa mitazamo inayosigana katika kumbainisha shujaa wa tendi za kiafrika. Baadhi ya wataalamu watatazamwa kupitia makala ya Deme (2007). Wataalamu hao waliopo katika makala hiyo ni pamoja na Seydou (1983), Okpewho (1979), Idowu (1973) na Ayivor (1997). Pia tutatazama mawazo ya Finnegan kuhusu shujaa kwa kupitia Mulokozi (1999) pamoja na Bowra (1964).
Tukianza na Seydou (1983), katika makala yake alichunguza tendi za kiafrika hususani Afrika Magharibi pamoja na Afrika ya Kati akang’amua kwamba, katika Afrika kuna tendi simulizi ambazo hutofautiana sana na tendi andishi kwani zenyewe hutumia ala za muziki nk.
Vilevile aliona kuwa, kazi nyingi za waandishi wa tendi za kiafrika wameziegemeza katika historia pamoja na visasili. Pia anatambua uwepo wa shujaa wa tendi za kiafrika na anaona kuwa, matendo ya shujaa na uwezo alionao ni kielelezo cha sifa binafsi na nguvu zake za kichawi humsaidia na huzitumia katika matukio maalum.
Okpewho (1979), kama ailivyorejelewa na Deme (2007), anasema kwamba uchawi/sihiri humfanya shujaa asishindwe dhidi ya maadui wake. Anatumia utendi wa Sundiata katika kuthibitisha hilo kwamba, shujaa Sundiata alimshinda Soumaoro kutokana na ama nguvu za kichawi ama kwa ushirikiano baina ya nguvu zake na nguvu za kisihiri.
Vilevile Idowu (1973), kama alivyorejelewa na Deme (kashatajwa), anaona kwamba mashujaa wa kiafrika hutumia nguvu za kichawi pamoja na za majini katika kukabiliana na matatizo mbalimbali katika jamii zao. Anasema, Sundiata amefaulu kushida nguvu za kichawi za Kita Mansa kutokana na msaada wa jini, vinginevyo asingeweza kushinda nguvu za kichawi za Kita Mansa.
Bowra (1964), yeye anaonekana kutomtambua shujaa wa kiafrika wala uwepo wa tendi za kiafrika. Hii ni kutokana na mtazamo wake kwamba, sihiri ni maudhi na si ushujaa. Anaendelea kufafanua kuwa, tendi simulizi ziwekazo msisitizo mkubwa katika nguvu za kisihiri haziwezi kufasiliwa kama tendi za kishujaa, kwa sababu badala ya kutumia sifa halisi pamoja na vipaji alivyonavyo binadamu zinatumia uwezo usiokuwa wa kibinadamu.
Pia anadai kuwa, katika tendi za kiafrika mashujaa hawatumii nguvu zao za asili na vipaji vyao walivyojaliwa katika kutatua matizo au kutekeleza majukumu mabalimbali ya kijamii, badala yake wanategemea sana nguvu za kichawi/sihiri kiasi kwamba wanapoteza uhuru wa kufanya mambo kwa matakwa yao kwa sababu wamekuwa watiifu kwa nguvu za kichawi ambazo si nguvu za shujaa wa tendi.
Katika kusisitiza hilo anaona kuwa, tendi za kishajaa zinapaswa kuwa na mtazamo wa kimagharibi kwa kuwa zinamchora binadamu halisi pamoja na sifa zake asilia kama vile nguvu, ujasiri, ustahimilivu na uwezo wa kuamuru.
Mtalaamu huyu anaonekana kubeza mashujaa wa tendi za kiafrika kwa kusema kwamba, katika tendi za kiafrika shujaa wa kweli ni yule mwenye uwezo wa kutumia nguvu zisizo za kibinadamu tu katika kufanya matendo yasiyo ya kawaida.
Mtaalamu Finnegan (1970), kama anavyooneshwa na Deme (kashatajwa) anaonekana kuwa na mawazo/fikra mgando kuhusiana na tendi za kiafrika pamoja na shujaa wake[3]. Finnegan katika utafiti wake kuhusu tendi za kiafrika anaathiriwa sana na mawazo ya kimagharibi kuhusu shujaa wa tendi anavyopaswa kuwa. Anataka shujaa wa Ulaya afanane na shujaa wa Afrika kitu ambacho hakiwezekani kutokana na tofauti za kijiografia, kiutamaduni, kihistoria na hata kiteknolojia. Hivyo mtazamo wa Finnegan kuhusu kutokuwepo kwa shujaa wa tendi za kiafrika hauna mashiko hata kidogo, kwani huu ni mtazamo finyu na wenye mawazo mgando.
Tofauti na wataalamu tuliowaona Ayivor (1997), kama alivyorejelewa na Deme (kashatajwa) yeye anakiri kamba, nguvu za sihiri kwa shujaa ndizo zinazozipa upekee wa kishujaa tendi za kiafrika[4]. Hivyo huyu anakiri kwamba, Afrika ina mashujaa wa tendi ambao ni tofauti na mashujaa wa tendi za Ulaya.
Mulokozi (1999), anasema kuwa, kutokutambulika kwa tendi za kiafrika kulikosisitizwa na Finnegan, Knappert na wenzake kuliwatia hamasa watafiti wengi wa kiafrika katika kuchunguza tendi za makabila yao kwa lengo la kupinga madai ya wanazuoni wa kimagharibi. Matokeo ya utafiti wao kuhusu shujaa wa tendi za kiafrika, walisema;
            …tulibaini kuwa shujaa wa tendi za kiafrika kwa kawaida huwa na sifa zifuatazo:
-          Nguvu: Hapa zinazungumziwa nguvu za kimwili (yaani ubabe na mabavu); nguvu za kiume na kidume, yaani urijali; nguvu za kiakili; nguvu za kivita.
-          Uganga au nguvu za sihiri
-          Mshikamano na kundi au jumuiya fulani inayomuunga mkono.”
Mulokozi katika kuthibitisha hayo, anachambua fani na maudhui katika utendi wa Fumo Liongo na kufafanua vizuri maisha ya shujaa Liongo kama shujaa wa tendi za kiafrika tangu ujana wake mpaka mauti yake.
Vilevile amebainisha sifa kemkem zilizosheheni katika utendi wa Fumo Liongo kama vile: masimulizi ya kinadhari kuhusu matukio muhimu ya kihistoria na kijamii, sifa ya kinudhumu nk. Pia ametaja sifa za shujaa wa tendi za kiafrika kuwa ni pamoja na: nguvu za kiume na kimwili, urijali, sihiri, nk.
Hivyo basi, hiyo ndio baadhi tu ya michango iliyojitokeza katika kazi za wataalamu hao. Je tumejifunza nini kupitia kazi zao?
Kwanza kabisa, nadhani itakuwa si uungwana kama hatutatambua mchango mkubwa uliotolewa na wataalamu hawa japo una madhaifu ya hapa na pale. Lakini pia, pamoja na kutambua mchango wa wataalamu hawa tuliowapitia katika makala hii, bado kuna baadhi ya mambo hayajafanyiwa kazi na nadhani yanahitaji kujadiliwa na kufanyiwa utafiti wa kina zaidi.
Jambo ambalo nadhani ni muhimu kulijadili japo kwa ufupi ni suala zima la “Shujaa wa Tendi na Matatizo ya Kijamii” kama mada ya makala hii inavyojitambulisha. Labda utajiuliza kwa nini kujadili jambo hili? Je, ni kwa sababu halijazungumziwa na wataalamu tuliowaona au? Lahasha! hatufanyi kwa sababu hizo tu, bali tunajadili jambo hili kutokana na umuhimu wake katika tendi za kiafrika, kwani katika mtazamo wa kijamii/kiafrika pamoja na kwamba shujaa ana sifa zake nyingi, lakini atatambulika tu kutokana na udhihirishaji wa sifa hizo katika kukabiliana na kutatua matatizo mbalimbali ya kijamii kama vile: njaa, vita, maradhi, umasikini, kukosa watoto, upweke woga, vitisho nk.
Utangulizi
Kabla ya kuingia katika wazo kuu la makala hii, inafaa tutalii kwa ufupi mashujaa wa kihistoria katika Afrika kama sehemu ya utangulizi. Hii itasaidia kutupa picha halisi ya ushajaa wa mashujaa hata kabla ya kuanza kupitia kazi mbalimbali za tendi za kiafrika.
Historia ya Afrika inatuonesha kwamba, Afrika imekuwa na mashujaa mbalimbali tangu zama za kale na hata kipindi cha mkoloni. Baadhi ya mashujaa wa kihistoria wanaofahamika sana ni pamoja na Dedan Kimathi Waciuri (Kenya),Chaka Zulu, Steve Biko, Nelson Mandela (mzee Madiba) wa Afrika Kusini, Mkwavinyika (Mkwawa) wa Tanzania, Kwame Nkrumah (Ghana), Patrice Lumumba, nk.
Mashujaa hawa, ushujaa wao wamebainika kutokana na matendo waliyoyafanya kwa jamii zao hususani katika kutatua matatizo mbalimbali. Kwa mfano, Shujaa Mkwawa alikuwa mstari wa mbele kupinga utawala wa wakoloni hasa Wajerumani kiasi kwamba baada ya kuzidiwa nguvu alidiriki hata kujinyonga ilihali tu asitiwe mikononi mwa Wakoloni. Hali kadhalika Chaka Zulu aliongoza mapambano makali katika kuitetea jamii yake dhidi ya mahasidi wake. Pia mzee Madiba anatambulika kama shujaa kutokana na harakati zake za kupinga kwa hali na mali utawala wa Makaburu. Hali hii ilimsababishia hata kufungwa jela na baadaye alifanikiwa na kuwa raisi wa kwanza wa Afrika Kusini.
Hivyo basi, ni dhahiri kwamba, ushajaa wa shujaa hujibainisha kutokana na namna anavyoisaidia jamii yake hasa nyakati za matatizo. Nyakati hizo ndipo mashujaa wengi hutumia akili zao, vipaji vyao na hata ikibidi kujitoa muhanga. Pia wengine hutumia hata nguvu za kichawi na sihiri katika kuhakikisha kwamba, jamii yake inabaki salama nyakati zote.
Shujaa wa tendi na Matatizo ya Kijamii
Kama kichwa cha mada kinavyojieleza, waandishi wengi wa kiafrika hususani katika tendi huwajenga mashujaa wao katika hali ya kuwafungamanisha na matatizo ya kijamii yanayoikabili jamii husika. Hufanya hivyo kwa malengo mbalimbali, kwanza kwa lengo la kuonesha kuwa shujaa ni zao la jamii, na kama ni zao la jamii hanabudi kukumbana na matatizo kama wanajamii wengine, pili kwa lengo la kuwaonesha wanajamii ushajaa wa shujaa katika kukabiliana na matatizo, kwamba hutofautiana na watu wa kawaida, tatu kwa lengo la kuwaondolea wanajamii hofu na kuwahakikishia usalama wao pindi wapatwapo na matatizo, kuwa, wanaye mwokozi atakayewaokoa katika matatizo yao.
Katika kuyathibitisha haya tutajikita zaidi katika kuchambua Utendi wa Mwindo, pia tutaangalia japo kwa ufupi Utendi wa Fumo Liyongo na Utendi wa Kirikou uliopo katika umbo la filamu kama nyenzo ya kuhifadhia utendi huo.
Utendi wa Mwindo unatoka katika jamii ya Nyanga, moja kati ya jamii zinazozungumza kibantu ziishizo katika misitu minene ya “Congo”. Utendi huu unapotambwa huandamana na nyimbo na uchezaji unaosindikizwa na wapiga ngoma nk. Katika historia ya Wanyanga haielezwi kama Mwindo ni mtu aliyekuwepo hapo zamani au ni kiumbe wa kihadithi tu. Hata hivyo, kuenea kwa hadithi yake na umashuhuri wake katika mapokezi ya matendo ya utamaduni wa Wanyanga huashiria kuwa, huenda mtu huyu ni mfano wa mashujaa waliowahi kutokea katika jamii hiyo.
Mwandishi wa utendi huu anaanza kwa kuonesha mahangaiko ya mfalme aliyejulikana kwa jina la She-Mwindo. Mfalme anatoa amri kwa wake zake wote saba pamoja na wanajamii kwamba, mtoto wa kike lazima alipiwe mahari wakati wa kuolewa na mtoto wa kiume lazima alipe mahari wakati wa kuoa. Hivyo anawaamuru wake zake wote saba wamzalie watoto wa kike tu, na yeyote atakayezaa mtoto wa kiume, mtoto huyo lazima auwawe[5]. Suala hili linakuwa ni tatizo kubwa kwa wanajamii, kwani suala la kuzaa mtoto wa kike au wa kiume halitokani na uamuzi wa mwanamke. Je jamii itafanya nini ili kuondokana na tatizo hili? Je hakuna mtu katika jamii awezaye kutatua tatizo hilo?
Wake wote saba wa mfalme wanapata mimba na mmoja tu kati yao anajifungua mtoto wa kiume, tena kwa njia isiyo ya kawaida. Akiwa bado tumboni anamwambia mama yake; nipo tayari lakini sitazaliwa kama watoto wengine, nitatoka kupitia kitovuni. “I am ready. But I will not come out like other babies. I will come out through my mother’s navel.”Anatoka na kuanza kukimbia kuzunguka chumba huku akiwa anacheza na kuimba, mkononi ameshikilia ngoma pamoja na fimbo iliyotengenezwa na manyoya ya mkia wa nyati.

Mimi ni Mwindo,                                                    I am Mwindo,
Nimezaliwa natembea,                                             The one born walking,
Nimezaliwa naongea,                                            The one born talking,
Baba yangu ni She-Mwindo, hanitaki mimi,      My father She-Mwindo does not want me.
Baba yangu mfalme, anataka kuniua mimi,       My father the chief wants to kill me.
Lakini atafanya nini dhidi yangu mimi?            But what can he do against me?”

Kuzaliwa kwa Mwindo kunaashiria kwamba, mtoto huyu atakuwa mtu wa pekee katika jamii, kwani hakuna mtu aliyewahi kuzaliwa kwa namna ile. Mwindo anatambua tatizo lililoko mbele yake hata kabla hajazaliwa, kwamba hakubaliki katika jamii ile na anapaswa kuuawa. Mfalme She-Mwindo anashangaa baada ya kumuona mtoto wa kiume[6]. Anatumia kila mbinu za kutaka kumuua, kwanza anamrushia mkuki lakini Mwindo anauzuia na kuuvunja vipande viwili. Mfalme anashangaa na kupiga kelele; mtoto huyu ni wa namna gani? “Aieeeeeee!What kind of child is this?” Mwindo anajibu kwa kuimba wimbo;
Mimi ni Mwindo,                                               I am Mwindo,
Nimezaliwa natembea,                                         The one born walking,
Nimezaliwa naongea,                                              The one born talking,
O baba yangu, hunitaki mimi,                                  O my father, you do not want me.
O baba yangu, unajaribu ukuniua mimi                   O my father, you try to kill me.
Lakini utafanya nini dhidi yangu mimi?                   But what can you do against me?                                                                  
Baada ya kushindwa kumuua mfalme anawaagiza washauri wake wamzike akiwa hai, lakini cha kushangaza kesho yake asubuhi wanamuona akiwa hai huku akiendelea kuimba wimbo wake. Mfalme anakasirika na kuamuru awekwe kwenye pipa kisha atupwe mtoni, lakini baada ya kumtupa mtoni pipa halikufuata mkondo wa mto, badala yake lilirudi lilipotoka kisha mwindo akatoka na kuliacha lili pipa ufukweni.
Mwindo aliamua kwenda kuishi kwa shangazi yake kijiji cha ng’ambo ya mto. Alipokuwa mtu mzima alirudi kupigana na baba yake, aliongozana na kundi la watu kuelekea kijiji cha baba yake, wakiwa njiani walipatwa na tatizo la njaa. Hili lilikuwa tatizo la pili kwa Mwindo baada ya lile la kutaka kuuliwa. Mwindo alianza kuimba na kucheza huku akizungusha ngoma yake;
Ndizi za baba, njoo kwangu.                              Bananas of my father, come to me.
Maharage ya baba, njoo kwangu.                      Beans of my father, come to me.
Maboga ya baba, njoo kwangu.                         Pumpkins of my father, come to me.
Kuku za baba, njoo kwangu.                             Chickens of my father, come to me.
Mbuzi za baba, njoo kwangu.                            Goats of my father, come to me.
Sufuria za baba, njoo kwangu.                           Pots of my father, come to me.
Kuni za baba, njoo kwangu.                              Firewood of my father, come to me.
Vyombo vya baba njoo kwangu.                        Dishes of my father, come to me.”
Kutoka mlimani She-Mwindo aliona vitu vyake vikipaa juu ya mlima na kutokomea; ndizi, maharage, maboga, kuku, mbuzi, sufuria, kuni, na vyombo. She-Mwindo akalia “Aieeeeeeee!”Nini hiki? Vitu vyote vikateremkia mahali alipokuwa Mwindo na watu wake, wakala na kusaza. Wote wakapata nguvu na kuendelea na safari. Walipokaribia kuingia kijiji cha baba yake, kundi la Mwindo lilitangulia kwenda kuanza kupigana kabla ya Mwindo kufika. Mwindo alipofika alikuta watu wake wote wameuawa. Akaanza kuimba wimbo;
O radi, angaza hapa.                             “O Lightning[7] look here.
O radi, uwe hakimu.                               O Lightning, be the judge.
Je baba yangu yu sahihi?                        Is my father right?
Je Mwindo yu sahihi?                             Is Mwindo right?
O radi tuma mshale wako.                      O Lightning, send your bolt.
Onesha nani yu sahihi,                            Show who’s right,
Onesha nani si sahihi                              show who’s wrong.”
Ghafla radi ikatuma mshale wake na kuwachoma wanaume wote wa Tubondo. Wanaume wote wakafa kasoro mfalme She-Mwindo na shangazi yake Mwindo.Shangazi yake alipoona hivyo alisikitika sana, akamwambia Mwindo, “umekuja kupigana na baba yako, tazama sasa mjomba wako na watu wetu wote pamoja na watu wa baba yako wamekufa.” Mwindo alisikitika sana alipoona watu wote wamekufa.
Hapa ndipo tunapopaswa kujiuliza maswali kama haya; Je shujaa anashindwa? Ushujaa wa shujaa upo wapi kama watu wote wamekufa? Atakuwa shujaa wa nani? Kwa nini aliruhusu askari wake wote wauliwe? Je hakuweza kuzuia vifo vya askari wake?
Baada ya Mwindo kuona watu wote wamekufa, alizungusha “conga[8] yake na kuanza kumgusa mmoja baada ya mmoja huku akisema; “First you sleep, now you wake.”na kila aliyeguswa na “conga” ya mwindo alifufuka. Mwisho watu wake wote wakafufuka na kuanza kushangilia huku wakisema;“What a great man is Mwindo! What can anyone do against you?”
Hivyo basi, tunaona kwamba matatizo ya kijamii huweza kumpata mtu yeyote yule katika jamii, haijalishi ni shujaa au si shujaa. Kama tulivyoona shujaa Mwindo alikabiliwa na matatizo makubwa manne, ambayo ni; kukataliwa na baba yake,  njaa, vita na kufiwa na watu wake. Katika kukabiliana na matatizo hayo, Mwindo anaonesha utofauti wake na watu wengine katika jamii. Tunaona njia alizozitumia si za kawaida katika jamii. Hii ni ishara tosha kwamba, Mwindo alikuwa na nguvu za kipekee zipitazo wanajamii wote, yaani nguvu za kisihiri.
Vilevile katika utendi wa Fumo Liongo, suala la shujaa na matatizo ya kijamii linajitokeza. Mulokozi (1999), anaeleza kwamba, utendi wa Fumo Liongo ulioandikwa na bwana Muhamadi bin Abubakar bin Omari al-Bakry, aliyejulikana zaidi kwa jina la Muhamadi Kijwana mwaka 1913.
Katika utendi huu, shujaa Liongo anatokea kupendwa na wanajamii kutokana na nguvu zake. Sifa zake zinazidi kusambaa katika jamii nzima, kiasi kwamba wanajamii wanashindwa kujizuia mpaka wanamsihi mfalme awaombe ili wapate mbegu ya uzazi wake. Suala hili linajitokeza kama tatizo linalowakabili wanajamii na linapaswa kutatuliwa na shujaa mwenyewe.
Liongo analiona tatizo hili la kupata mtoto linavyowasumbua wanajamii, hivyo anaamua kutatua tatizo hili kwa kukubali kumuoa mmoja kati wanajamii na kuzaa naye mtoto wa kiume. Tatizo jingine linalojitokeza ni hofu ya madaraka. Liongo anajikuta katika mgogoro mzito baina yake na mfalme wa Wagalla.
Chanzo cha mgogoro huu ni wivu, kwani baada ya mfalme kuona kuwa, Liongo anazidi kupata umaarufu mkubwa katika ufalme wake, anaingiwa na hofu kwamba, huenda akanyang’anywa ufalme wake. Hivyo mfalme akapanga njama za kumuua Liongo. Shujaa Liongo anaingiwa na hofu juu ya usalama wa maisha yake, hivyo anaamua kukimbilia msituni. Licha ya kujaribu kutetea uhai wake, lakini alishindwa kabisa kujinasua katika hili, mwisho Liongo anapoteza maisha yake kwa kuuliwa na mtoto wa kumzaa mwenyewe.
Pamoja na kuwa, shujaa Liongo ameuawa kama watu wengine wanavyouawa katika jamii lakini tunaona kuwa, kifo chake hakikuwa kifo cha kawaida kama ionekanavyo kwa watu wengine. Tunaambiwa kuwa, Liongo alikufa huku amepiga magoti kisimani na mkononi ameshikilia upinde wenye mshale akielekeza mjini. Watu wote hawakujua kama kweli amekufa, mpaka alipooza na kudodoka chini.
Pia suala la shujaa na matatizo ya kijamii linajitokeza vizuri zaidi kupitia filamu ya Kirikou. Filamu hii ina kila sababu ya kuitwa utendi, kwani tunaona kwamba imesheheni mambo mbalimbali yaliyopo katika tendi kwa mfano: sihiri, nudhumu, motifu ya safari, shujaa, urijali, matukio na matendo ya kishujaa, uunganifu, nk. Hapa ingefaa kueleza kidogo kabla ya kufanya uchambuzi.
Kadiri maendeleo ya sayansi na teknolojia yanavyoongezeka ndivyo na tanzu mbalimbali za kifasihi zinavyojitokeza katika maumbo mbalimbali kuendana na maendeleo hayo. Hivyo tunaona kwamba, mabadiliko hayo hayawezi kuathiri kaida za utanzu husika. Vilevile hata vialamishi (stylistic markers) vya utanzu husika hubaki kuwa vilevile.  Jambo jingine la msingi ni kwamba, tendi zote iwe za Ulaya au Afrika ninaamini kwamba, zilianza kama masimulizi na baadaye ndipo zikawekwa katika maandishi kama chombo cha kutunzia kazi hizo.
Hivyo basi, filamu ya Kirikou ninaamini kuwa ni utendi uliojitokeza katika umbo la kifilamu kama chombo cha kuhifadhia.
Kirikou ni utendi ulioandikwa na Michael Ocelotmwaka 1998. Utendi huu unatokana na simulizi za kijadi za watu wa Afrika Magharibi, zijulikanazo kama hadithi za kingano. Lengo la  mtunzi ni kuleta mabadiliko ya kifikra miongoni mwa wanajamii hasa wale wanaoendelea kukumbatia tamaduni za kijadi zilizopitwa na wakati kama vile, mila na imani potofu.
Wanakijiji wote waliamini kwamba, matatizo yote yanayokikabili kijiji chao yanatokana na uchawi wa mwanamama Karaba. Hivyo tunaona kwamba Kirikou hata kabla hajazaliwa alishaona mahangaiko ya wanakijiji ndio maana akiwa tumboni alimwambia mama yake, “mama nilite duniani.”Lakini mama yake alimwambia, “mtoto aongeaye tumbuni mwa mama yake aweza kujileta mwenyewe.” Hii inaashiria kwamba, Kirikou alikuja mwenyewe kwa lengo la kuwasaidia wanakijiji, kwani hakukuwa na mwanaume yeyote aliyeweza kutatua matatizo ya wanakijiji hao. Tatizo kubwa linalomkabili Kirikou pamoja na wanakijiji wengine ni tatizo la uhaba wa maji. Kirikou anang’amua chanzo cha tatizo na anafanikiwa kutatua tatizo hilo.
Tatizo jingine ambalo Kirukou anang’amua ni uonevu ulikithiri katika kijiji chao. Mchawi Karaba kwa kutumia nguvu zake za kichawi anajaribu kuwateka watoto, lakini Kirikou anafaulu kuwaokoa. Pia baada ya Kirikou kugundua sababu zinazomfanya mchawi Karaba kuwa katili, alitafuta mbinu ya kuweza kutatua tatizo hilo. Mwisho kabisa Kirikou anafaulu kutatua matatizo yote yanayoikabili jamii yake.
Pamoja na kwamba, Kirikou ameonesha ushujaa wake kwa kuweza kutatua matatizo mbalimbali yaliyoikabili jamii yake, ni dhahiri shahiri kwamba, njia alizozitumia katika ufumbuzi wa matatizo hayo, zinaonekana kuwa si njia za kawaida kwa mwanadamu. Hali hii inaonesha kuwa, Kirikou aliongozwa na nguvu za kisihiri, kwani; aliongea angali bado tumboni mwa mama yake, alifaulu kulitoboa dubwana lililokuwa linazuia maji, aliweza kupambana na vikwazo mbalimbali katika kutafuta ukweli juu ya mchawi Karaba na hatimaye kufanikiwa kuondoa tatizo lililokuwa linamsumbua mchawi Karaba kwa kumuondolea msumari wenye sumu mgogoni mwake ambao ulikuwa unampa nguvu za kichawi.
Kutokana na mambo mbalimbali ambayo Kirikou ameyafanya katika jamii yake ni wazi kuwa Kirikou anastahili kuitwa shujaa wa jamii hiyo.
HITIMISHO:
Hivyo basi, tumeona kwamba shujaa hupatwa na matatizo ya kijamii kama wanavyopatwa watu wengine katika jamii. Isipokuwa njia atumiazo shujaa katika utatuzi/ufumbuzi wa matatizo hayo ni tofauti na watumiazo watu wengine. Utofauti huu ndio unaomfanya atambulike kama shujaa. Kitu cha pekee ambacho humfanya shujaa aonekana ni mtu wa pekee katika ufumbuzi wa matatizo ya kijamii ni sihiri, yaani nguvu alizonazo shujaa zisizoweza kuelezeka katika mtazamo wa kisayansi.
MAPENDEKEZO:
Katika mtazamo wa kiafrika, tendi nyingi humchora shujaa kama Mungu anayekuja kutatua matatizo yaliyoshindikana katika jamii. Tena kwa kutumia nguvu zisizoelezeka katika hali ya kibinadamu, jambo ambalo haliwezi kuhalisika na kuaminika hata kwa Waafrika wenyewe na katika mtazamo wa kidunia kwa ujumla.
Hivyo basi, ingefaa sana tendi za kiafrika pamoja na kusisitiza sihiri, urijali nk. zijaribu kumchora shujaa kama mtu anayetumia akili, hekima, busara na utashi na si kutegemea sihiri kila wakati. Mfano mzuri tumeona katika utangulizi jinsi mashujaa wa kihistoria walivyo kuwa. Kwa mfano Chaka Zulu alitumia akili akaweza kutengeneza silaha mpya, mzee Madiba alitumia akili na uwezo wa kibinadamu katika kutatua matatizo ya watu wake. Pia hata Mkwavinyika alidhihirisha uwezo wake wa kibinadamu katika mapambano na wakoloni.
MAREJEO:
Biebuyck,P. D & Mateene K. C(1969) “The Mwindo Epic.”Berkeley and Los Angeles: University of California Press.
Deme, M. K. (2009) “Heroism and the Supernatural in the African Epic: Toward a Critical     Analysis.” Western Michigan University.
Mulokozi, M.M (Mh.) (1999) Tenzi Tatu za Kale. Dar es Salaam: TUKI
Mulokozi, M.M (2009) Utangulizi wa Fasihi ya Kiswahili. Dar es Salaam. KAUTTU.
Ngure, A (2003)Fasihi Simulizi kwa Shule za Sekondari. Nairobi. Phoenix Publisher.
Ocelot, M. Thiltgets, P.(Producer). (1998) “Kirikou”. West Afrika.  
Wamitila, K.W. (2003) Kamusi ya Fasihi na Nadharia. Focus Publication Ltd. Nairobi.     

[1]we are living in this crazy world
[2]Katika Afrika Mashariki, tunao ushahidi kuwa tendi ziko au zilikuweko katika jamii zifuatazo:Wachagga (Mlire); Wahehe (Mukwavinyika); Wanyambo na Wahaya (Kachwenyanja,Mugasha, nk.)...

[3]Finnegan is very skeptical about the existence of African epic and dismisses them with the claim that “all in all epic poetry does not seem to be a typical Africa form (p. 110).

[4]The belief in the supernatural is what gives the African epic its unique heroic proportion.
[5]So, all my children must be daughters. If any is a son, I will kill him.”

[6]What is this? Did I not say ‘no sons’? Did I not say I would kill him?

[7] Lightning. To the Nyanga, Lightning is a god who may be entreated to intervene in human affairs by sending down his bolts. He is the only Nyanga god who lives in the sky. How his bolts can reach underground to the land of the gods is a mystery.
[8]Conga. This is a flyswatter with a scepter-like handle of wood. The swatter attached at the top can be leaves, an antelope tail, or, as in this story, the tail of a Cape buffalo. A conga is included in the regalia of a chief, and so signifies here the destiny of Mwindo.

No comments:

Post a Comment