Saturday, 2 February 2013

MISINGI YA TAFSIRI NA UKALIMANIMISINGI YA TAFSIRI NA UKALIMANI
Tafsiri ni nini?
Tafsiri kama Taaluma (somo)
Tafsiri kama zao, (kile kinachopatikana baada ya kutafsiriwa/outcome.
Newmark (1982) Tafsiri ni jaribio la kuwasilisha ujumbe uleule ulioandikwa katika lugha moja kwa lugha nyingine.
Jaribio kwa sababu si mara zote unaweza kufanya hivyo kwani unaweza kushindwa au kufaulu.
*  Udhaifu wa Newmark katika fasili yake ni kwamba hakuzingatia umbo la kazi yenyewe au mtindo wa kazi yenyewe. Mfano; kadi ya mwaliko, barua nk.
Mwansoko na wenzake (2006) Tafsiri ni zoezi la uhawilishaji (Transferring) wa mawazo katika maandishi kutoka lugha moja hadi lugha nyingine.
*   Ukiangalia wataalamu hawa wawili utaona kwamba wanafanana; kwani wanaona kuwa tafsiri hufanywa katika maandishi.
Nida na Taber (1969) wanaona kuwa tafsiri hujumuisha upya ujembe wa lugha chanzi kwa kutumia visawe asilia vya lugha lengwa vinavyokaribiana zaidi na lugha chanzi, kwanza kimaana na pili kimtindo. Kwa mfano; “Damu nzito kuliko maji” – "Blood is thinker than water”. Ndugu yako ni muhimu zaidi kuliko mtu mwingine. “Ukistaajabu ya Musa utaona ya Firauni” – “Wonders never end”
*   Nida na Tiber wanaona kuwa katika tafsiri kitu muhimu ni kuzingatia maana na mtindo.
MFASIRI NI NANI?
Ni mtu yeyote anayejishughulisha na kazi za kutafsiri.
Ni mtu mwenye taaluma au ujuzi wa kutafsiri na ambaye anajishughulisha na kazi hizo (weledi-Professionalism)
MATINI NI NINI?
Ni wazo au mfululizo wa mawazo ambao unajitosheleza kimaana. Matini inaweza kuwa neno moja, kirai, kishazi, sentensi, aya, kifungu cha habari nk.
AINA ZA MATINI (Text)
Kuna aina mbili za matini ambazo ni Matini Chanzi/Chasili na Matini Lengwa/matini tafsiri.
·       Matini Chanzi/chasili (MC) “Source Text” ni matini ambayo iko katika lugha yake ya awali au lugha yake iliyoandikiwa kabla ya mchakato wa kutafsiri.
·      Matini Lengwa/tafsiri (ML) “Target Text” ni matini iliyotafsiriwa kutoka lugha yake iliyoandikiwa.
Lugha Chanzi/Chasili (LC) ni lugha iliyotumika kuandikia matini chanzi (Source language)
Lugha Lengwa (LL) (Target language) ni lugha iliyotumika kutafsiria  matini chanzi au lugha unayoitumia kufanyia tafsiri.
KISAWE/USAWE (EQUIVALENT/EQUIVALENCY)
Katika muktadha wa tafsiri kisawe ni neno, kirai, kishazi, sentensi au hata maneno katika lugha lengwa ambayo maana na matumizi yake yanalingana au kukaribiana na yale ya neno, kirai, kishazi, sentensi au msemo mwingine katika lugha chanzi
DHIMA / UMUHIMU WA TAFSIRI
·         Ni njia ya mawasiliano/daraja kati ya watu au jamii mbili zinazotumia lugha tofauti. Mfano; maelezo mbalimbali ya jinsi ya kutumia bidhaa mbalimbali kama vile redio, simu, kurunzi, dawa, jokofu nk.
·       Ni nyenzo ya kuelezea utamaduni kutoka jamii moja kwenda jamii nyingine. Mfano; kupitia dini – tafsiri ya Biblia au Kuruani “Koran”, Pia hata katika burudani – tafsiri ya vitabu mbalimbali ambavyo vina vipengele vingi sana vya utamaduni kama vile nyimbo nk.
·         Ni mbinu ya kujifunzia au kufundishia lugha kimsamiati na kisarufi.
·         Ni kazi ya ajira kama kazi nyingine, hivyo huweza kumpatia mtu kipato.
·         Humliwaza mfasiri; hii ni baada ya kumaliza kufasiri.
SIFA ZA MFASIRI BORA.
·     Awe mahiri wa lugha mbili zinazohusika; kuwa mahiri katika lugha maana yake nini? Ni kujua vizuri nyanja mbalimbali za Isimu ya lugha husika kama vile; Fonolojia-Matamshi, Mofolojia-Maumbo, Sintaksia-Muundo na Semantiki-Maana.
·         Ajue vizuri utamaduni wa watu mbalimbali.
·         Ajue angalau lugha mbili
·         Awe na maarifa ya TEHAMA (ICT)
·    Awafahamu watu, jamii na utamaduni wao – mitazamo kuhusu watu, mitazamo – kuhusu wanyama.
·      Apende kujisomea na kujiendeleza kulingana na mabadiliko ya jamii. Mfano; kusoma vitabu, majarida, magazeti mbalimbali kusikiliza redio na kuangalia TV nk.
·      Awe mwandishi bora.
MAADILI YA MFASIRI BORA (ETHICS)
·   Awe mwaminifu kwa matini na kwa mwenye matini; yaani asipotoshe habari au kusema uongo.
·       Awe mchapakazi (Kujituma/Bidii katika kazi)
·        Awe nadhifu – Unadhifu-mwonekano wa moyo, asiwe tapeli/laghai
·      Aelewe/kuelewa taratibu za kazi na kuzifuata. Mfano; bei ya kutafsiri kwa ukurasa au kwa maneno.
· Ushirikiano/kushirikiana na watu mbalimbali wa fani mbalimbali, makundi mbalimbali ikiwa pamoja na wafasiri wenzake.
NADHARIA YA TAFSIRI
Maana; ni maelezo muhimu kuhusu vipengele mbalimbali vya kifasiri ambavyo vinapaswa kufuatwa au kuzingatiwa na kila mfasiri pindi anapokabiliwa na kazi ya kufasiri.
Nadharia ya tafsiri ndio nguzo au mhimili muhimu wa shughuli zote za tafsiri. Vipengele vingine vitakavyojadiliwa katika nadharia ya tafsiri ni pamoja na taaluma zinazohusiana na tafsiri na dhima ya nadharia ya tafsiri.
Sababu za kuanzishwa kwa nadharia za tafsiri. Newmark (1982), Mwansoko na wenzake (2006) wanasema kuna mambo matatu yaliyosababisha kuanzishwa kwa nadharia ya tafsiri ambayo ni:-
i)          Wingi wa makosa katika tafsiri zilizochapishwa awali; ilionekana kwamba, kulikuwa na makosa mbalimbali kama vile makosa ya kimuundo, kimaumbo, kimsamiati nk. Pia ilikuwa ni nadra/muhali kupata tafsiri zisizokuwa na makosa.
ii)           Kuwepo kwa idadi kubwa (na inayoongezeka) ya asasi zinazojishughulisha na kazi za tafsiri. Hali hii ilisababisha kubuniwa kwa nadharia ya tafsiri ili kuwepo kwa misingi inayokubalika. Mfano; nchini Tanzania peke yake kuna asasi nyingi zinazojishughulisha na tafsiri kama vile: BAKITA, TATAKI, SHIHATA, WAFASIRI na vyombo mbalimbali vya habari kwa mfano: TV, Magazeti nk.
iii)       Mfumuko wa istilahi katika taaluma mbalimbali hasa Sayansi na Teknolojia. Hivyo nadharia ya tafsiri ilianzishwa kwa lengo la kuleta ulinganifu wa istilahi hizo kati ya lugha moja na nyingine ili kuwe na ufanisi zaidi.
TAALUMA NYINGINE ZINAZOHUSIANA NA TAFSIRI
Tafsiri inauhusiano mkubwa na taaluma nyingine au vipengele vingine kama ifuatavyo:
Inauhusiano na isimulinganishi; Isimulinganishi hijishughulisha na kulinganisha vipengele mbalimbali vya kiisimu vya lugha mbili au zaidi, pamoja na kuchunguza mbinu za ulinganishi huu. Uhusianao wake na tafsiri;- humsaidia mfasiri kuelewa mifumo ya lugha mbalimbali na jinsi luhga hizo zinavyotumia vipengele vyake vya kiisimu kutolea taarifa mbalimbali.
Inahusiana na isimujamii;- Isimujamii inahusika na kuchunguza uhusiano kati ya lugha fulani na jamii ambayo inatumia lugha hiyo. Rejesta mbalimbali za kijamii pamoja na maingiliano baina ya lugha. Ujuzi wa isimujamii unamsaidia mfasiri kufahamu athari zinazotokana na mahusiano baina ya lugha na jamii husika na kuzingatia mambo mbalimbali katika kutafsiri.
Inauhusiano na semantiki/pragmatiki;- Semantiki ni taaluma inayochunguza maana ya maneno katika upweke na katika makundi/taaluma inayochunguza maana ya maana. Kwa kuwa kinachotafsiriwa ni mawazo au maana ya matini (siyo neno pwekepweke) basi ujuzi huu wa semantiki utamwezesha mfasiri kujua au kung’amua kuwa maana ya matini hiyo haitokani na maana ya neno mojamoja badala yake inatokana na maana ya kimatumizi kwa ujumla katika mktadha mahususi.
Inauhusiano na elimumitindo (stylistics);- Hii inahusu uainishaji wa mitindo mbalimbali ya lugha na miktadha ya matumizi yake.
Elimumitindo
Mitindo                         Mazingira ya kutumia
Uhusiano wake na tafsiri;- Taaluma hii ya elimumitindo itamwezesha mfasiri kubaini mtindo wa matini chanzi ambao haunabudi kuhamishiwa katika matini lengwa.
Inauhusiano na mantiki (logic);- Mantiki inahusu ukweli na uhakika au usahihi wa mambo kama inavyosemwa, kuandikwa au kuaminika kwa watu. Mantiki humsaidia mfasiri kubaini kauli zisizo dhahiri na zinazokanganya katika matini chanzi ili azirekebishe kwanza kabla ya kuanza kutafsiri. Kwa mfano; The current president of United Republic of Tanzania is Mzee Ally Hassan Mwinyi. Je ni kweli?
NADHARIA YA TAFSIRI
Nadharia ya tafsiri hushughulikia mambo makubwa manne ambayo ndiyo dhima ya nadharia ya tafsiri.

1.  Kubaini na kufasili (define) tatizo la kifasiri yaani kazi au mlolongo wa shughuli za tafsiri zinazopaswa kufanywa katika utatuzi wa tatizo la tafsiri lililobainishwa.
2.  Kuonesha vipengele vyote vinavyopaswa kuzingatiwa katika utatuzi wa tatizo la tafsiri lililobainishwa.
3.  Kuorodhesha taratibu au njia zote zinazowezekana kufanikisha tafsiri inayohusika.
4.    Kupendekeza taratibu zinazofaa zaidi katika kutekeleza zoezi la kufasiri pamoja na mbinu za kutafsiri zilizomuafaka zaidi kwa matini inayohusika.
NADHARIA MAHUSUSI ZA TAFSIRI.
1.  Nadharia ya Usawe wa Kimuundo; nadharia hii inatetewa na mtaalam Catford (1969), Tunapofanya kazi ya kutafsiri tunatakiwa kuzingatia ulinganifu wa kimuundo kati ya matini chanzi na matini lengwa, maana yake ni kwamba muundo wa matini chanzi ujitokeze katika matini lengwa. katika nadharia hii muundo ni muhimu. Pia nadharia hii hutumika zaidi katika kutafsiri maandiko ya kidini hasa Biblia.
2.   Nadharia ya Usawe wa Kidhima; wa tetezi wa nadharia hii ni pamoja na Nida (1964) na Nida na Taber (1969) wanaona kuwa usawe wa kidhima ni muhimu zaidi kuliko usawe wa kimuundo. Wafasiri wanapaswa kuhakikisha kwamba dhima ya matini chanzi pamoja na athari zake zinajitokeza katika matini lengwa. Yaani kama matini chanzi inawalenga watoto inapaswa iandikwe kiasi kwamba watoto wataweza kuelewa. Pia kwa kuzingatia nadharia hii unapaswa kutumia lugha rahisi na inayoeleweka na watu wote. Vilevile tafsiri yako iwe nzuri kiasi kwamba mtu atakaposoma asiweze kujua kwamba hii kazi imetafsiriwa.
3.     Nadharia ya Usawe wa Aina-matini; matini yoyote ile ifasiriwe kwa kuzingatia aina yake. Hii inamaana kwamba kazi itakayotokea itafanana na matini chanzi. Kma matini chanzi ni ya kisheria itakapotafsiriwa matini lengwa nayo itaonekana kuwa ya kisheria. Katika nadharia hii kinachozingatiwa ni fani (muundo) na maudhui (dhima/lengo) ya matini yenyewe inayotafsiriwa. Watetezi wa nadharia hii ni Reiss (1971),  Buhler (1965) na Newmark (1982/88)
4. Nadharia Changamani (Cross Fertilization theory). Hii ni nadharia tete iliyoasisiwa na P.S.Malangwa (2010) Ndharia hii inadai kwamba huwezi kufanya tafsiri kwa kutumia nadharia moja tu, kwa sababu hakuna nadharia inayojitosheleza yenyewe.
UAINISHAJI WA MTINI
Maana: Kuainisha matini ni kuzigawa au kuziweka matini katika makundi mbalimbali kwa kuzingatia kufanana kwake.
Sababu: Tunaainisha matini kwa sababu kila matini inahitaji mbinu maalum ya kuitafsiri.
Mikabala/vigezo vya uainishaji: Wataalam wengi wanatumia vigezo vitatu ambavyo ni Kigezo cha Mada (Topic/Field), Kigezo cha Matumizi ya Istilahi, Kigezo cha Dhima kuu za Lugha
1.  Kigezo cha Mada: katika kigezo hiki tunaangalia maudhui ya jumla ya matini. Tunajiuliza matini hii inahusu uwanja gani hasa katika maisha? Kwa kutumia kigezo hiki cha mada tunapata aina tatu za matini.
i) Matini za Kifasihi (Literary Text); hizi ni matini ambazo zinahusu fani mbalimbali za fasihi kama vile riwaya, tamthilia, ushairi nk.
ii)  Matini za Kiasasi (Institutional Texts); matini hizi ni mtini za kimamlaka kama vile matini za kisiasa na kiserikali (hotuba, risala, mikataba, vyeti nk).
iii) Matini za Kisayansi (Scientific Texts); matini hizi hujumuisha masuala yote ya Sayansi na Teknolojia. Kwa mfano; Fizikia, Kemia, Biolojia nk.
2.   Kigezo cha matumizi ya Istilahi: katika kigezo hiki kinachozingatiwa hapa ni kwamba, matini huainishwa kwa kuangalia wingi au idadi za istilahi-msamiati wa uwanja maalum/husika mf: sharia nk. Kwa kutumia kigezo hiki tunapata aina tatu za matini:
a)   Matini za kiufundi (Technical Text), matini hizi huwa na idadi kubwa ya istilahi.
b)     Matini za kinusu ufundi (Semi-Techinical Text), matini hizi huwa na idadi ndogo au chache za istilahi.
c)      Matini za zisizo za kiufundi (Non Techinical Text), matini hizi ni zile ambazo hazina kabisa istilahi bali hutumia maneno ya kawaida kabisa.
3.  Kigezo cha Dhima Kuu za Lugha (Major Language Functions). Buhler (1965) alipendekeza dhima kuu 3 za lugha.
i) Dhima elezi (Expressive Function), katika dhima hii lugha hutumika kuelezea hisia za mwandishi/mzungumzaji. Anasema, mzungumzaji au mwandishi hueleza hisia zake bila kumjali msikilizaji au msomaji.
ii)  Dhima Arifu (Informative Function), dhima hii  ya lugha hujitokeza pale ambapo matini au lugha inatumika katika kutoa taarifa kuhusu jambo fulani. Dhima hii huegemea kwenye ukweli wa mambo.
iii) Dhima amili (Persuasive Function) katika dhima hii lugha hutumika kuchochea hisia za msikilizaji au msomaji. Kiini cha dhima hii ni hadhira.
Kwa hiyo, kwa kuzingatia dhima hizi tatu “3” tunapata aina kuu tatu za matini kama ifuatavyo:
1.  Matini Elezi (Expressive Texts); matini hizi huegemea upande wa mwandishi. Mwandishi hutumia matini hizi kuelezea hisia zake. Mfano, kazi mbalimbali za kifasihi, hotuba, matini mbalimbali za kimamlaka, matini za kisheria, matini mbalimbali za kitaaluma, maandishi binafsi nk.
2. Matini Arifu (informative Texts); matini hizi ni zile ambazo zinatoa taarifa au maarifa kuhusu jambo fulani. Sifa yake ni kuwa zinakuwa na umbo sanifu au umbo maalum mfano; umbo la jarida, kitabu, ripoti, tasnifu, vitabu vya taaluma mbalimbali nk.
3.   Matini Amili (Persuasive Texts); matini hizi huegemea upande wa hadhira. Katika matini Amili mwandishi hujitahidi kadiri awezavyo kuchochea hisia za wasomaji na kuwafanya watende kama ambavyo mwandishi anataka watende. Hivyo huegemea upande wa msomaji. Mfano wa matini hizo ni kama vile mialiko mbalimbali, matangazo, maelekezo mbalimbali nk.
UCHAMBUZI WA MATINI ZA TAFSIRI
Awali ya yote mchambuzi wa matini za tafsiri/mfasiri anapaswa kusoma matini kwa kina na kuyaelewa kabla ya kuanza zoezi zima la uchambuzi wa matini.  
Maana: Uchambuzi wa matini unatuwezesha kubaini sifa na vipengele vinavyojenga matini husika kimuundo, kidhima na kiitikadi.
Hatua/vipengele vya uchambuzi wa matini:
Uchambuzi wa matini unahatua tatu “3” ambazo ni kama ifuatavyo:
1.   Kusoma matini yote na kuielewa vizuri. Hii humsaidia mfasiri kuweza kuandaa marejeleo muafaka, kuandaa vitabu au machapisho mbalimbali yatayomsaidia katika zoezi zima la kufasiri matini. Kwa mfano;
-      Kuandaa kamusi mbalimbali kama vile kamusi ya lugha chanzi, kamusi ya lugha lengwa, kamusi ya visawe, kamusi ya fani maalum.
-     Inamsaidia mfasiri kuandaa orodha ya istilahi.
-      Inamsaidia mfasiri kuweza kugawana sehemu au vipengele vya matini kwa wafasiri wengine.
2.   Kuchambua matini yenyewe. Uchambuzi wa matini hulenga kupata nduni bainifu za matini husika (Distinctive Features). Kipengele hiki cha pili kina hatua ndogo ndogo tano ambazo ni kama ifuatavyo:
a) Kubaini lengo la mwandishi wa matini chanzi. Mfano; malengo ya mwandishi huweza kuwa kukweza, kusifu, kukashfu au kuarifu jambo.
Kwa kawaida waandishi wa matini chanzi wanakuwa na mitazamo mitatu;
i) Mtazamo hasi kwa mtendwa (biased) mfano, katika gazeti; “Chelsea yaichabanga Arsenal tatu nunge”
ii)Mtazamo chanya kwa mtendwa (biased) mfano katika gazeti; “Chelsea yafuta uteja kwa Arsenal”
iii) Mtazamo wa kati (neutral) mfano katika gazeti; “Chelsea yaifunga Arsenal au Arsenal yafungwa na Chelsea”
b)  Kubaini lengo la mfasiri. Mfasiri anapaswa kujiuliza kwa nini nafasiri kazi hii? Je lengo langu na mimi ni tofauti na la mwandishi?
-      Aepuke upendeleo kwa hadhira chanzi na hadhira lengwa badala yake ajikite katika ukweli. Hivyo inafaa awe katika mtazamo wa kati (neutral)
-   Kama kuna haja ya kuegemea upande mmoja basi aegemee kwa hadhira lengwa.
c)  Kubaini hadhira na umbo la matini. Kwa mfano; kama matini chanzi ni kitabu basi matini lengwa nayo iwe kitabu.
d)  Kubaini mtindo wa matini. Hapa mfasiri ahakikishe kwamba mtindo wa matini chanzi unajitokeza katika matini lengwa. Mfano; kama kuna monolojia au dayalojia basi na matini lengwa inapaswa kuwa hivyo.
e) Kubaini ubora na mamlaka ya matini chanzi. Hapa mfasiri hanabudi kuzingatia ujuzi wa mwandishi katika kutumia zana za kiisimu/vipengele mbalimbali vya lugha.
Mamlaka hutokana na hadhi au ubobevu wa mwandishi huyo katika taaluma au fani aliyoandikia. Mfano, kazi ya fasihi ya S. Robert ni bora kuliko iliyoandikwa na mimi kwa sababu yeye ni mbobevu/galacha katika taaluma hiyo.
3.   Kusoma matini kwa mara ya mwisho. Katika hatua hii ya tatu mfasiri asome tena matini chanzi ili kutoa taashira (highlight) kuhusu maneno au mambo muhimu.
Mambo muhimu ni: Majina mahususi ya watu, mahali, sehemu au miaka, maeneo ambayo hayatafsiriki kirahisi ili aweze kuyashughulikia upya hapo baadaye.
MCHAKATO WA KUTAFSIRI/KUFASIRI
Hatua muhimu katika kutafsiri
Tunapofanya tafsiri kuna hatua muhimu kuu sita kwa mujibu wa Mwansoko na wenzake (2006). Hatua hizo ni kama ifuatavyo:
1.      Hatua ya maandalizi. Hatua hii inahusisha mambo matatu ambayo ni:
a)  Kupitia tena sehemu muhimu za matini chanzi, kwa mfano; istilahi, majina ya wahusika, majina ya kijiografia, maeneo au kauli zisizofasirika kirahisi.
b)  Kupata marejeleo ili kutafuta visawe vya kisemantiki
c)   Kutafuta na kuandika visawe hivyo.
2.  Hatua ya pili baada ya maandalizi ni uhawilishaji (transferring/transference). Katika hatua hii mfasiri uhawilisha ile taarifa kutoka kwenye matini chanzi kwenda kwenye matini lengwa, hapa mfasiri anatakiwa kuzingatia sarufi ya lugha lengwa na lugha chanzi. mfano; “My new car is broken”-langu jipya gari ni vunjika. Tafsiri ya Kiswahili sanifu inapaswa kuwa “Gari langu jipya limeharibika”
Uhawilishaji maana yake ni kuhamisha maana, ujumbe nk. kutoka lugha chanzi kwenda lugha lengwa kwa kuzingatia sarufi ya lugha lengwa, lengo la matini au mwandishi, umbo la matini, mtindo nk.
Mbinu ya tafsiri ambayo inatumika katika hatua hii ya uhawilishaji ni tafsiri ya neno kwa neno.
3.  Hatua ya tatu ni kusawidi rasimu ya kwanza (drafting). Uhawilishaji wa visawe kutoka lugha chanzi kwenda lugha lengwa unapokamilika kinachopatikana ni rasimu ya kwanza ya tafsiri.
Rasimu ya kwanza ya tafsiri inakuwa na dosari nyingi na kwa hiyo haifai kupelekwa kwa mteja au hadhira. Badala yake rasimu ya kwanza lazima ipitiwe tena upya na kurekebishwa au kudurusiwa/durusu (review) rasimu (draft).
4.   Hatua ya nne ni kudurusu rasimu ya kwanza ili kuunda rasimu ya pili. Mfasiri hupata fursa ya kwanza ya kuitathimini na kuifanyia marekebisho tafsiri yake mwenyewe. Kazi ya kudurusu haipaswi kufanywa haraka. Wataalam wengine kama vile Larson (1984) anasema rasimu ya kwanza ni lazima iachwe kwa muda wa wiki moja.
Udurusu unahusisha shughuli zifuatazo:
· Kusahihisha makosa ya kisarufi, miundo isiyoeleweka vizuri.
· kunyoosha sehemu zenye tafsiri ya mzunguko na zenye matumizi potofu ya visawe. Mfano; “He rarely visits me these days – Siku hizi ni aghalabu-nadra sana yeye kunitembelea.”
·Kurekebisha sehemu zenye muunganiko tenge/mbaya ambazo zinazuia mtiririko mzuri wa matini.
·Kuhakiki usahihi na kukubalika kwa maana zinazowasilishwa katika matini lengwa. Hapa tunaangalia kama kuna mambo yameongezwa, yamepunguzwa au yamepotoshwa/kubadilishwa.
·Kuhakiki kukubalika kwa lugha uliyotumia katika tafsiri yako kwa kuzingatia umbo na mada ya matini chanzi.
·Kuona iwapo mada au ujumbe mkuu wa matini chanzi unajitokeza waziwazi katika matini lengwa.
5.   Hatua ya tano ni kusomwa rasimu ya pili na mtu mwingine. Msomaji wa rasimu ya pili anaweza kuwa mfasiri au shabiki wa tafsiri, mhakiki au mhariri wa tafsiri anaweza kuwa mteja wa tafsiri husika au mtu mwingine yeyote unayemwamini.
Namna ya kumpa mtu akusomee rasimu:
· Kumpa bila kumjulisha kwamba ni tafsiri
· Unampa matini chanzi na matini lengwa ili alinganishe.
Inapendekezwa kwamba mtu huyo asome kwa sauti ili uweze kubaini mapungufu.
6.      Hatua ya sita ni kusawidi rasimu ya mwisho. Katika hatua hii mfasiri atafanyiakazi maoni na mapendekezo ya msomaji ambaye alimpa kazi yake. Matokeo ya kufanyiakazi maoni ya mteja hutupelekea kupata rasimu ya mwisho ambayo ndiyo humfikia mteja, hadhira, wachapaji nk.
MBINU ZA UUNDAJI WA ISTILAHI
I.    Misingi ya kimataifa ya uundaji wa istilahi
i)       Istilahi ziwe fupi iwezekanavyo ili zieleweke vizuri au kirahisi.
ii)     Istilahi zifuate sarufi ya lugha lengwa.
iii)   Tuepuke istilahi za vifupisho/Akronimu
iv)   Tusiunde istilahi kwa kupanua maana ya istilahi iliyopo.
v)     Istilahi zisiwe na sinonimia au homonimia.
-          Kusiwe na maneno kadhaa ambayo yote yanarejelea kitu kimoja.
-          Au zenye maana inayokaribiana-homonimia
vi)  Istilahi ziweze kuambatanishwa kuwe na uwezekano wa kupata istilahi mbalimbali ndani ya kikoa kimoja, mfano; rekodi-rekodiwa nk.

I.    Misingi ya uundaji wa istilahi za Kiswahili
Katika lugha ya Kiswahili kuna misingi kadhaa ya uundaji wa istilahi za Kiswahili kama ifuatavyo.
i)            Istilahi ziakisi sifa bainifu za dhana zinazolengwa. Mfano; Istilahi kama vile kionambali – hapa unapata picha ya kile kinachowasilishwa.
ii)          Istilahi ambatani zizingatie mambo yafuatayo:
-          Idadi ya maneno yanayounganishwa yasizidi mawili. Mfano; Mwanajeshi.
-          Kama istilahi hizi ni maneno mawili usitumie kistari (-)
-          Zisizidi silabi nane.
iii)     Istilahi ziweze kunyambulika ili kuunda istilahi zaidi za vikoa. (semantiki field) mf; soma, somea, someana, someaneni, someshanani nk.
iv)    Istilahi ziwetoshelevu/zijitosheleze (precise) na zisiwe ndefu mno. Pia zijitosheleze kimaana.
v)           Ziwe fupi na zinazoeleweka kirahisi. Mfano; Istilahi “Autumn” – majira ya majani kupukutika karibu na kipupwe. Hii si Istilahi bali ni ufafanuzi wa istilahi “Autumn.”
vi)      Istilahi mahuluti (blending – mix & combine), finyazo (acronyms) zafaa ziepukwe kwa sababu etimolojia yake niauvulivuli/haiku dhahiri au haieleweki vizuri.
vii)         Upanuzi wa maana uepukwe kwa sababu huwachanya watumiaji.
viii)   Kila dhana iwakilishwe na istilahi moja tu/yaani kusiwe na maneno mbalimbali yanayorejelea istilahi ileile.
AINA/MBINU/NJIA YA TAFSIRI/KUFASIRI
Waandishi wengi wanakubaliana kwamba kuna njia nne zitumikazo katika tafsiri:
1.      Tafsiri ya neno kwa neno (word to word translation)
2.      Tafsiri sisisi (literal translation)
3.      Tafsiri ya kisemantiki (semantic translation)
4.      Tafsiri ya kimawasiliano
I.     TAFSIRI YA NENO KWA NENO/NENO BAADA YA NENO.
       Tunapotafsiri matini kwa mbinu ya neno kwa neno, hapo tunafanya tafsiri ya matini chanzi kwa kuzingatia maana za msingi za maneno katika lugha chanzi na kutafuta maneno hayo katika lugha lengwa.
-      Tunapotafsiri matini kwa mbinu ya neno kwa neno matini lengwa hufuata sarufi ya lugha chanzi. (MC – Sarufi LC)
-     Tunapotafsiri kwa kutumia mbinu ya neno kwa neno tafsiri yetu huandikwa chini ya neno husika katika kila mstari. Mfano;
Wa/toto/wa/dogo/wa/na/imba/kwa/ furaha
Plural/child/ plural/small/they/tens pre.cont'/sing/by,for/happiness

I/like/banana/s/more/than/orange/s
Mimi/penda,kama/ndizi/wingi/zaidi/kuliko/chungwa/wingi

II.     TAFSIRI SISISI
Katika tafsiri sisisi maneno hutafsiriwa pwekepweke kwa kuzingatia maana zake za msingi katika lugha chanzi. Tafsiri sisisi huzingatia sarufi ya lugha lengwa. Mfano;
-          Walimsaidia katika mahitaji yake ya msingi
-          They helped him/her in his/her needs of basic
-          Walimpa msukumo mkubwa katika biashara yake.
-          They gave him/her a big push in his/her business
-          One day my dreams will come true
-          Siku moja ndoto zangu zitakuja kweli
Faida ya mbinu hii: - Husaidia kufasiri dhana au matini zisizotafsirika kirahisi. Mfano; majina/maandishi ya kanga, misemo, nahau nk.
Dosari za mbinu hii: - Si mbinu nzuri kutafsiri matini ndefu ingawa ni mbinu bora ikilinganishwa na mbinu ya neno kwa neno.
III.     TAFSIRI YA KISEMANTIKI/WAZI
-          Huegemea zaidi upande wa mwandishi au upande wa matini chanzi
-          Hulenga kufasiri kila kipengele katika matini chanzi.
-          Huzingatia sarufi ya lugha lengwa
-      Huzingatia zaidi maana ya matini chanzi kiasi kwamba huwa na mwelekeo wa kuwa fafanuzi kwa sababu inataka kufasiri kila kipengele kilicho kwenye matini chanzi. Kwa mfano;
o   Tanzania Electric Supply Company Limited
o   Kampuni tanzu ya usambazaji umeme Tanzania
o   Alikwenda mpaka nyumbani kwake
o   She/he went up to her/his home
o   Wonders never end
o   Maajabu kamwe hayaishi
Faida ya mbinu hii: -
-          Husaidia sana kufasiri matini elezi
-          Husaidia kuitajirisha lugha lengwa kwa misemo au semi mbalimbali. Kwa mfano;
Natambua uwepo wako (I acknowledge your presence)
Haijalishi (It doesn’t matter)
Mwisho wa siku (At end of the day)
Mwisho lakini si kwa umuhimu (Last but not least)
Hasara ya mbinu hii:
-    Hukosa vionjo na kumfikirisha sana msomaji
-    Mbinu hii huwa ni ya mzunguko na ya kifafanuzi mno. Mfano; Tafsiri ya neno Autumn
IV.      FAFSIRI YA MAWASILIANO/KIMAWASILIANO AU TAFSIRI HURU
-          Mbinu hii huegemea zaidi upande wa hadhira lengwa
-          Huzingatia utamaduni, itikadi, mazingira na historia ya jamii lengwa.
-       Hulenga msomaji wa matini lengwa apate athari ileile kama waipatayo wasomaji wa matini chanzi.
-     hii ndiyo mbinu ya tafsiri inayotumika kutafsiria matini nyingi zaidi kuliko mbinu zilizotangulia na kwa sababu hii ndiyo mbinu bora zaidi ya nyingine mbinu hii hufaa zaidi kufasiria matini Arifu na Amili.
-     Katika mbinu hii mfasiri hutafuta visawe katika lugha lengwa kama vile misemo na methali ambazo maana zake na muktadha wake wa matumizi hufanana na methali au misemo ya lugha chanzi au matini chanzi. Kwa mfano;
a)    Walimpa msukumo mkubwa katika biashara yake
They gave him a big support in his business
They helped him a lot in his great deal/in his business
b)    Tanzania Electric Supply Company Limited
Shirika la Umeme Tanzania
c)     Wonder never end
Ukistaajabu ya Musa utaona ya Firauni
TAFSIRI NA UKALIMANI
Ukalimani ni nini? Ukalimani ni uhawalishaji wa taarifa au ujumbe kutoka kwa msemaji wa lugha chanzi kwenda katika lugha lengwa kawa njia ya mdomo au mazingumzo.
Katika ukalimani matini chanzi huwa katika mazungumzo na matini lengwa pia huwa katika mazungumzo.
Katika ukalimani mkalimani hana muda wa kutosha wa kujiandaa kwa sababu anatakiwa kukalimani kile anachosikia wakati ambapo mzungumzaji anaendelea kuzungumza mambo mengine.
Aina za ukalimani
Kuna aina mbalimbali za ukalimani kutegemeana na vigezo unavyotumia kuainisha au kupata hizo aina;
1. Kigezo cha kwanza ni kigezo cha Muktadha; Katika kigezo hiki vipengele vinavyojitokeza ndani ya muktadha ili kupata aina tunazingatia mahali, lengo, aina ya hadhi, sifa za walengwa nk.

Ukalimani wa Kijamii/community interpretation: Huu ni ukalimani ambao hufanywa katika masuala mbalimbali ya kijamii kama vile afya, ujenzi wa shule huduma za kijamii kama vile maji, umeme, masuala ya mihadhara ya kidini nk.
Ukalimani wa Mikutano au Makongamano/Conference; Huu ni ukalimani unaofanyika katika makongamano au mikutano mbalimbali. Mara nyingi aina hii ya ukalimani inafanyika katika mikutano ya kimataifa.
Ukalimani wa Mahakama/Mahakamani; Aina hii hufanywa na wanasheria katika mahakama za ngazi mbalimbali. Pia huitwa ukalimani wa kisheria.
Ukalimani wa Kitabibu; Huu ni ukalimani ambao unafanyika mahali ambapo matibabu yanapatikana, kwa kiasi kikubwa aina hii ya ukalimani inafanyika katika hospitali kubwa kubwa.
Ukalimani wa Habari/katika vyombo vya habari; Huu ni ukalimani unaofanywa katika vyombo mbalimbali vya habari, hususani redio na televisheni ili kuiwezesha hadhira lengwa iweze nayo kuelewa matangazo yanayotolewa kwa lugha chanzi.
Ukalimani Sindikizi/Escort interpretation; Katika aina hii ya ukalimani mkalimani hufuatana na mtu au kikundi cha watu katika safari au katika usaili au mahojiano.
2. Kigezo cha pili ni kigezo cha Muundo au Mfumo wa Lugha/Language mode/modality; Katika kigezo hiki lugha inayotumika katika ukalimani inaweza ikawa lugha ya kusema/kizungumza na lugha ya alama.

Kupitia lugha ya alama tunapata aina moja ya ukalimani yaani ukalimani wa viziwi
Kwa kupitia lugha ya mazungumzo au kusema tunapata aina mbili za ukalimani ambazo ni;
Ukalimani Mfululizo/Andamizi/Simultaneous interpretation; Katika ukalimani mfululizo, kama jina lenyewe linavyodokeza mkalimani huzungumza takribani sambamba na mzungumzaji wa lugha chanzi. Katika aina hii ya ukalimani mkalimani lazima afanyekazi kwa haraka sana ili kuendana na kasi ya mzungumzaji kuepuka kupitwa na mambo muhimu.
Katika ukalimani mfululizo makalimani huketi katika chumba maalum cha ukalimani (booth) ambacho hakipitishi sauti (sound proof) na kisha huzungumza kwa kutumia kipaza sauti huku akimwona na kumsikia mzungumzaji wa lugha chanzi kupitia visikizio (ear phones)
Ukalimani Fuatishi/Mtawalia (Consecutive interpretation); Katika ukalimani fuatishi makalimani huzungumza/hukalimani baada ya mzungumzaji wa lugha chanzi kumaliza ujumbe wake au hata kama hajamaliza ujumbe wake baada ya mzungumzaji wa lugha chanzi kutulia kwa sekunde kadhaa ili kumpa makalimani fursa ya kukalimani kile kilichosemwa. Katika aina hii mkalimani na mzungumzaji wa lugha chanzi mara nyingi wanakuwa pamoja wakiwa wamesimama kwenye jukwaa au wakiwa wameketi mezani.
SIFA ZA MKALIMANI BORA.
·    Awe na ujuzi wa hali ya juu wa lugha anazoshughulika nazo pamoja na utamaduni wake.
·   Ajue lugha zaidi ya mbili za kimataifa kwani kadiri unavyojua lugha zaidi ndivyo unavyokuwa mkalimani bora zaidi.
·  Awe na ujuzi au maarifa ya kutosha juu ya mada, taaluma au uwanja unaozungumziwa. Inamaana kwamba kama wewe ni mfasiri wa masuala ya kiuchumi basi hupaswi kufasili masuala ya kisheria. Mfano; ukalimani wa mahakamani hufanywa na wanasheria.
·    Awe na ujuzi wa taaluma ya ukalimani; yaani awe amepata mafunzo ya ukalimani. Katika hayo mafunzo atajifunza mbinu za ukalimani aina, changamoto na namna ya kuzikabili.
·    Mfasiri anatakiwa awe mchapakazi, mdadisi na apende kujiendeleza au kupata habari kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii mfano; magazeti, majarida, televisheni, facebook, twitter au kuzungumza na watu/kuchangamana na watu.
·         Awe na kipaji, yaani:
Uwezo wa kukumbuka
Kuteua msamiati sahihi kwa haraka
Kipaji katika kuunda istilahi haraka haraka na kuitumia.
Kipaji cha ulumbi/awe na ulumbi yaani kipaji cha kuongea na kuvuta watu (eloquency)
·         Awe na uzoefu.
UMUHIMU WA UKALIMANI
1.  Ukalimani ni daraja linalosaidia kuunganisha watu au jamii inayozungumza lugha tofauti.
2.      Ukalimani ni nyenzo ya kueneza utamaduni. mfano; dini
3.  Ukalimani husaidia katika masuala ya kidiplomasia na uhusiano wa kimataifa. Mfano; usuluhishi wa migogoro.
4.      Ukalimani hutumiwa na makampuni ya simu kuwasiliana na wateja wao
5. Ukalimani husaidia kufanikisha vikao, mikutano na makongamano ya kitaifa na kimataifa. Mfano; mikutano ya UN, AU nk.
6.   Ukalimani hutumika kama mbinu ya kijifunzia lugha ya pili au lugha ya kigeni hasa katika hatua za awali.
7.    Ukalimani unamsaidia mkalimani mwenyewe kujifunza lugha.
STADI MUHIMU KATIKA UKALIMANI
i)  Lugha na mawasiliano;- kumudu stadi za lugha na mawasiliano
ii)  Kuwa na stadi ya kusikiliza
iii)  Stadi ya kudondoa (kuandika muhtasari) – kuchukua mambo muhimu tu kati ya mengi anayoongea.
iv)  Stadi ya kumbukumbu/kukumbuka (memory rehesion skill)
v)            Sanaa ya kuzungumza hadharani. mfano; jinsi ya kuandaa hotuba, jinsi ya kuanza kwa kishindo, jinsi ya kumaliza kwa kishindo, kutoa mifano dhahiri, kuepuka kujisifia, Toa visa vya kweli/mara nyingi inashauriwa kutoa visa vyako/vinavyokuhusu wewe, kuepuka vitabia vinavyokera mfano; kuchokonoa puani, kujikuna kuna nk.
vi)   Hakikisha umevaa vizuri nk.
TAFSIRI NA UKALIMANI: KUFANANA NA KUTOFAUTIANA.
Tofauti kati ya tafsiri na ukalimani: vipengele/vigezo vya kutofautisha dhana hizi mbili;
a)     Dhana (maana/fasili)
b)     Lugha (mtindo, stadi maalum nk)
c)      Utendaji (mf; vifaa/zana)
d)     Kigezo cha mada/maandalizi/uhawilishaji
e)     Mfumo wa lugha (kuzungumza au kuandika)
f)       Uwasilishaji (mara moja tu au kuna nafasi ya kudurusu)
g)     Hadhira (papo kwa papo au mbali)
h)     Maslahi/malipo (utaratibu wa kutoza pamoja na tozo lenyewe/bei mf; kwa ukurasa au maandishi/saa.
i)       Ukongwe/umri/historia (kipi kilianza)
j)  Stadi muhimu za lugha zinazohitajika. mfano; kusoma, kuandika, kusikiliza na kuzungumza.

KUFANANA KWA TAFSIRI NA UKALIMANI
a)     Vigezo
b)     Njia (kibebeo)
c)      Lengo/dhima
d)     Vijenzi (vipengele vya modeli/muundo wa mawasiliano, mfano; sender – channel – receiver – feedback.
e)      Faida
TATHMINI KATIKA TAFSIRI (TRASLATION CRITICISM)
Katika tafsiri tunafanya tathmini ili kujua ubora na upungufu wa tafsiri husika. Kutathmini tafsiri ni zoezi la kupima kiwango cha ubora wa tafsiri husika kwa kutumia mbinu zinazokubalika.
Tunapotathmini tafsiri tunaweza kupata makundi yafuatayo ya tafsiri hizo tunazotathmini;
·         Tafsiri bora (good translation)
·         Tafsiri tenge/mbaya (mistranslation)
·         Tafsiri finyu (under translation)
·         Tafsiri pana (over translation)
TAFSIRI BORA; hii ni ile tafsiri ambayo kifani na kimaudhui inaendana na matini chanzi.
TAFSIRI TENGE; hii ni ile tafsiri ambayo haiendani na matini chanzi.
TAFSIRI FINYU; hii ni ile tafsiri ambayo imeacha vitu vingi katika kutafsiri.
TAFSIRI PANA; hii ni ile tafsiri ambayo imeongezwa mambo mengi ambayo hayapo katika matini chanzi au imefasiriwa kijumla jumla.
AINA ZA MATINI LENGWA ZINAZOFAA KUTATHMINIWA
Kuna aina mbili za matini lengwa ambazo zinafaa kutathminiwa kama ifuatavyo:
a)    Matini lengwa zilizo katika mchakato wa kufasiriwa, hii ni ile matini ambayo bado haijafikishwa kwa walengwa. Mfasiri anaweza kutathmini upya matini kabla ya kuifikisha kwa mlengwa.
b)    Matini zilizo mikononi mwa mtumiaji/mteja/hadhira. Fursa ya kuboresha kazi hiyo haipo ila hufanyiwa tathmini ili kutoa maoni ambayo yatamwezesha mfasiri kuboresha kazi nyingine zinazofuata au toleo linalofuata.
MBINU ZA KUTATHMINI TAFSIRI
1.      Ulinganishaji wa matini; hii ndiyo mbinu kongwe zaidi na ndiyo inayotumiwa na wahakiki wengi zaidi (MC na ML). Katika mbinu hii kinachofanyika ni kwamba matini lengwa hulinganishwa na matini chanzi ili kubaini vipengele vya kimuundo na kimtindo vilivyoongezwa, vilivyopunguzwa au vilivyopotoshwa ili kuvifanyia marekebisho.
2. Kupima uasili; tafsiri bora haipaswi kusomeka kama tafsiri. Hii ina maana kwamba mtu anaposoma tafsiri yako asijue kama ni kazi iliyotafsiriwa badala yake inatakiwa isomeke kama vile imeandikwa katika lugha lengwa hiyohiyo.
Hali ambapo tafsiri husomeka kama vile imeandikwa katika lugha lengwa hiyohiyo ndio ambayo huitwa uasili.
Hapa mfasiri mwenyewe au mtu mwingi anaisoma kazi hiyo. Inashauriwa apewe mtu mwingine tena bila kuambiwa kwamba kazi hiyo ni tafsiri.
3. Kupima uelewekaji; Katika mbinu hii kinachoangaliwa ni kueleweka kwa maudhui yanayotolewa katika tafsiri hiyo. Mtu anayepima uelewekaji atajiuliza yeye mwenyewe, je maudhui katika kazi hii yataeleweka kwa wasomaji au kazi hii inazungumzia nini? Hivyo inashauriwa kwamba mfasiri ampe mtu mwingine ili kuepuka kujipendelea. Tahadhari: Mtu anayepelekewa kazi hiyo inashauriwa awe mfasiri.
4.      Kupima usomekaji; Katika mbinu hii ya kupima usomekaji mfasiri au mhakiki atapima tafsiri husika ili kuona iwapo inasikika vizuri masikioni mwa msikilizaji na kama inamtiririko unaokubalika katika lugha lengwa. Hapa kunakuwa na watu wawili mmoja anasikiliza na mwingine anasoma kwa sauti.
5.  Kupima ulinganifu; Katika hii mhakiki anaangalia umakini wa mfasiri katika kutumia kwa namna inayofaa vipengele muhimu vya matini kama vile msamiati, istilahi, maudhui au maneno muhimu yanayobeba maudhui. Maana yake ni kwamba kama neno limejirudia rudia katika tafsiri usibadilishe, mfano: Aim – nia, lengo, madhumuni, kusudi, azma, shabaha, kusudi nk. Hivyo kama neno “Aim” umelifasiri kama lengo basi popote litakapojitokeza kwa mara nyingine katika matini basi libaki hivyohivyo bila kubadili badili.
6.    Tafsiri rejeshi (Back Translation); Ni mchakato wa kutafsiri matini ambayo tayari imetafsiriwa katika lugha fulani yaani lugha lengwa na kuirejesha tena katika lugha chanzi kwa lengo la kuitathmini tafsiri hiyo.

MAREJEO:
Cartford, J. C. (1965). A Linguistic Theory of Translation. London: OUP.
Larson, L. M. (1984). Meaning-based Translation. London: University Press of America.
Mwansoko, H. J. M. na wenzake (2006). Kitangulizi cha Tafsiri: Nadharia na Mbinu.                                                                      Dar es Salaam: TUKI.
Newmark, P. (1982). Approaches to Translation. Oxford: Pergamon Press.
Newmark, P. (1988). A Textbook of Translation. London: Prentice Hall.
Nida, E. A. (1964). Towards a Science of Translation. Leiden: E. J. Brill.
Nida, E. A. and C. R. Taber, (1969). The Theory and Practice of Translation. London.                                                      Prentice Hall.


19 comments:

 1. Ahsante sana Ndumbaro. Hakika wewe si mchoyo wa maarifa. Yamenisaidia sana makala haya kuhuisha maarifa niliyojipatia kwa Mwansoko katika kozi ya Nadharia ya Tafsiri.

  ReplyDelete
 2. nashukuru kwa maarifa haya.naomba unieleze umuhimu wa tafsiri katika mawasiliano.asante

  ReplyDelete
 3. Kazi njema,ahsante

  ReplyDelete
 4. Natambua uwepo wenu wapendwa asante

  ReplyDelete
 5. Taaluma hii ni muhimu sana kwani inachangia ktka kupunguza tatizo la ukosefu wa mawasiliano

  ReplyDelete
 6. Taaluma hii ni muhimu sana kwani inachangia ktka kupunguza tatizo la ukosefu wa mawasiliano

  ReplyDelete
 7. Natambua uwepo wenu wapendwa asante

  ReplyDelete
 8. Kielelezo bora.Pokea kongole zangu

  ReplyDelete
 9. Shukrani kubwa umenifaa sana kwenye kosi yangu ya uwalimu.

  ReplyDelete
 10. Maarifa muhimu sana kitika taaluma yangu.

  ReplyDelete
 11. Vigezo vya tafsiri in vipi naomba kuelezwa

  ReplyDelete
 12. Vigezo vya tafsiri in vipi naomba kuelezwa

  ReplyDelete