SANAA ZA MAONESHO KABLA YA UKOLONI
AFRIKA MASHARIKI NA MBINU ZILIZOTUMIKA KUFIFISHA AU KUUA SANAA ZA MAONYESHO
HAPA NCHINI
Dhana ya sanaa imejadiliwa na wataalamu
mbalimbali, baadhi ya wataalamu hao ni hawa wafuatao
Muhande P, and Balisidya (1976:1).
Sanaa ni uzuri unajitokeza katika umbo lililosanifiwa, umbo ambalo mtu
hulitumia kueleza hisia zinazomgusa kwa kutoa kielelezo au vielelezo vyenye
dhana maalum. Wataalmu hawa wameainisha aina tatu za sanaa ambazo ni sanaa za
uonyesho, sanaa za ghibu na sanaa za vitendo
Kwa mujibu wa Mhando na Balisidya
(1976) wamekusanya mawazo ya wanazuaoni mbalimbali katika kufasili dhana ya
sanaa za maonyesho. Mawazo makuu yaliyotolewa ni kama haya yafuatayo.
Kuna baadhi ya wataalam wanaodai kuwa
sanaa za maonyesho ni michezo ya kuigiza au ni michezo ioneshwayo kwenye jukwaa
lenye pazia na mataa mengi ya rangi au ni michezo ya Shakespeare kama vile “mabepari
wa venisi”
Wengine wanadai kuwa sanaa za maonyesho
ni vichekesho au ni maigizo yanayochekesha.
Pia sanaa za maonyesho huweza
kufasiriwa kuwa ni maigizo.
Hivyo basi, Mhando na Balisidya
(1976:2) wanasema kuwa, sanaa za maonyesho ni kitendo chochote chenye sifa nne
ambazo ni (i) michezo (ii) mchezaji
(iii) uwanja wa kuchezea na (iv)
watazamaji, mfano wa karibu kudhihirisha nadharia hii ni tamthiliya (mchezo wa
kuigiza) mfano: “wakati ukuta”.
Sanaa za maonyesho za asili yaani za
jamii ambayo utamaduni wake ulikuwa haujaingiliwa na wakoloni (kigeni)
kugawanywa katika makundi matano mbazo ni (i) sherehe (ii) ngoma (iii)
masimulizi ya hadithi (iv) kusalia miungu (v) majigambo.
Kwa hiyo basi sanaa za maonyesho za Kiafrika
ni dhana zilizo kwenye umbo linalotendeka na siyo mchezo. Ili dhana hii
itendeke inahitajika mtu wa kutenda (mtendaji), mtendaji huyu anahitaji uwanja
wa kutendea hiyo dhana na wakati akitenda hiyo dhana wanakuwepo watazamaji.
Hivyo sanaa za maonyesho za Kiafrika ni kitendo chochote chenye sifa nne ambazo
ni dhana inayotendeka, mtendaji, uwanja wa kutendea na watazamaji.
Ifuatayo ni hali ya sanaa za maonyesho
kabla ya ukoloni hapa Afrika mashariki ni kwamba ilikuwa haijaingiliwa na
utamaduni wa kigeni. Zifuatazo ni sanaa za maonyesho zilizokuwepo Afrika
Mashariki.
SHEREHE
Sanaa za maonyesho katika kundi hili
zinahusu kuingizwa kwa mwanajamii kwenye kundi la watu wa aina fualni kutoka
kundi la watu wa aina nyingine kwa mfano jando na unyago. Mtu kutoka kundi la
watoto kuingia kundi la watu wazima, au kutawazwa kwa chifu, kutoka kundi la
raia na kuingia kundi la askari shujaa nk. Hivyo, kutoka kundi moja na kuingia
kundi jingine ni hatua iliyopewa umuhimu mkubwa katika jamii ya asili.
NGOMA
Neno ngoma lina maana tatu yaani;
“Ngoma” ni chombo cha muziki. “Ngoma” pia ni uchezeshaji wa viungo vya mwili
wenye mtindo na miondoko maalum pengine
ukiambatana na muziki “Ngoma “ pia ni sherehe iwe ni jando, harusi, unyago nk.
Hapa neno ngoma lina maana ya sherehe yoyote kwa ujumla na siyo lazima kwenye
sherehe hiyo pawepo na ngoma uchezeshaji wa viungo au ngoma chombo cha muziki
ingawaje mara nyingi katika hatua fulani ya sherehe hii kimojawapo huwepo.
Ngoma tunayoongelea katika sehemu hii
ni ile yenye maana ya pili – uchezashaji wa viungo vya mwili wenye mtindo na
miondoko maalum pengine ukiambatana na muziki.
Pia hapa tunaongelea ngoma ambazo
haziamabatani na sherehe maalum mifano michache ni kama mpendo, msunyumbo
(wagogo) silanga (wapogoro), Gombasugu (wazaramo), kitoto (wangoni) mtuya, ditonga
(wakaguru) nk.
MASIMULIZI YA HADITHI
Tunazo hadithi za asili kwa maelfu
kwani katika jamii ya asili masimulizi ya hadithi yalikuwa ni mojawapo ya mambo
ya kila siku. Baada ya kazi nyingi za mchana wanajamii wakubwa kwa wadogo wake
kwa waume, walikusanyika majumbani kwao na kujipumzisha kwa kusimuliana
hadithi. Hadithi zote ziwe nikuhusu wanyama, ndege, bianadamu, mazimwi nk. Zina
maana fulani ndani yake inayohusu maisha katika jamii, ubaya autendao mhusika
katika hadithi kama vile ya “Mama wa kambo” na adhabu aipatayo huwa ni fundisho
kwa wale wanaoisikiliza, hadithi kuepukana na ubaya huo katika kuishi na
wenzao.
Mafunzo yatokanayo na hadithi
yangaliweza kutolewa kwa maneno matupu lakini umuhimu wa mafunzo hayo
ulisababisha yawekwe kwenye umbo la kisanaa ili yapate uzuri unaovutia wale
wanaohusika. Sanaa hii pia ikiwa ya vitendo ili mafunzo yadhihilike zaidi
mafano wa hadithi hizo ni “Mama wa Kambo”, “Mfalme aliyetaka Watoto wa Kike” “Kalukanga
Mtoto wa Nyoka nk.
Masimulizi ya hadithi mara nyingi
huendeshwa ndani ya nyumba kuzunguka moto ambapo wasikilizaji hukaakumzunguka
msimulizi wakati mwingine, hadi siku za mbalamwezi, masimulizi ya hadithi
huweza kuwa nje ya nyumba. Vyovyote ilivyo
hapo wakaapo wasikizaji na masimulizi ndiyo uwanja wa kutendea
KUSALIA MIUNGU
Katika jamii ya asili watu walielekeza
kwa miungu mbalimbali matatizo, ambayo wao kwa nguvu zao za kibinadamu
yaliwashinda. Walipopata tatizo la ukame au waliposhambuliwa na magonjwa ya
hatari, walipokabiliwa na manyama wala watu, walipokosa watoto nk. waliikabili
miungu yao na kuisalia iwasaidie. Ufuatao ni mfano wa kusalia miungu unaotumika
na wakagulu wakati wa kuomba mvua. Kusalia miungu huitwa Chijumba – Mulungu
watu waki shaelekezwa na mganga kuwa ukame uliopo utamalizwa na Chijumba –
Mulungu.
Katika mfano huu watendaji na uwanja wa
kutendea ni dhahiri labda tutatatanishwa na watazamaji ambapo katika kusalia
miungu watazamaji ni miungu wanaosalia kwa vile ndiyo inayotazama yale
yanayotendeka
MAJIGAMBO
Majigambo ni masimulizi ya kujigamba
kwa mtu kuhusu mambo ya kishujaa aliyopata kuyatenda maishani mwake. Majigambo
haya husimuliwa katika lugha ya kishairi na masimulizi yake huambatana na
vitendo vya mjigambaji mwenyewe. Kwa mfano, ikiwa anajigamba kuhusu vita fulani
alivyopigana basi atatenda vitendo kuonesha vile alivyokwenda vitani, alivyokabiliana
na adui, alivyomuua adui au adui alivyokimbia. Majigambo yanapatikana zaidi
katika jamii za kanda ya ziwa magharibi hasa Wahaya na pia jamii za kusini mwa
Tanzania kama Wahehe. Majigambo yalikuwa na madhumini ya kudumisha utu wa Wanaume
katika jamii.
Sura ya sanaa za maonesho ilibadilika
kutokana na kuja kwa wakoloni kutoka nchi za nje hasa Waingereza katika
kuitawala Tanzania kuanzia baada ya vita vya kwanza vya dunia hadi Tanzania
ilipopata uhuru mnamo mwaka 1961. Waingereza walisababisha mabadiliko
mbalimbali katika sura nzima ya sanaa za maonyesho zifuatazo; ni mbinu
zilizotumika kuua au kujifisha sanaa za maonyesho hapa nchini.
Waingereza walileta sanaa za maonyesho
zenye asili ya utamaduni wa kwao hasa Drama. Drama ilingizwa hasa mashuleni
ambapo waalimu wengi walikuwa Waingereza. Madhumuni ya kuingiza drama hayakuwa
na uzito mkubwa. Waingereza hawa walikuwa wanatafuta kitu cha kupitisha muda
wakati ambapo walikuwa hawana la kufanya.
Hivyo kutokana na kuingiza drama sanaa
za maonyesho za Afrika zilikosa ushiriki, kwani wengi walihamasika kushiriki katika
drama kwani walivutiwa zaidi katika uonyeshaji wenyewe mavazi ya washiriki,
matumizi ya mataa za rangi nk.
Pia waingereza kuona drama ni bora zaidi
kuliko sanaa za maonyesho za Kiafrika tamthilia zilizoongozwa ni zile zilizoandikwa
na Waingereza zaidi zikiwa za yule mwanasanaa mashuhuri William Shakespeare. Baadhi
ya kazi zilizovuma sana ni kama vile: Hamlet,
Othello, Ceaser, Macbeth, Rumeo and Juliet na The Temped. Kwa upande wa Watanzania walioshiriki katika tamthilia
walikuwa kama washiriki au watazamaji tu kwani, tamthilia hizi hazikuwa na
maana yenye uzito wowote kwao kwani zilielezea utamaduni wa kigeni tu kitu.
Hivyo sanaa zetu za maonesho hazikupata nafasi.
Mbinu nyingine walizotumia ni
kutambulisha dini ya Kikristo. Kwa kutumia dini hii walifanya kila njia
kukomesha mambo ambayo hasa yalikuwa sanaa za maonyesho za Kitanzania asilia
kwa mfano; jando na unyago, kusalia miungu pamoja na ngoma. Mambo yote haya waliyaita
ya kuwa ni ya kishenzi. Hivyo wakrito wote hawakupaswa kushiriki katika mambo
hayo na pia walipaswa kuchukua jukumu la kukomesha mambo haya. Vilevile wale
walioshiriki walionekana wanatenda dhambi. Hivyo basi kwa mbinu hii walifaulu kufifiza
au kuua sanaa za maonyesho za Kiafrika.
Dhana ya kufananisha sanaa za maonesho
na uchekeshaji, lilishika mizizi
barabara kwani hadi leo sanaa za maonesho zinaambatana na uchekeshaji,
kama shughuli haichekeshi sio sanaa za maonyesho. Kwa hiyo kuna ugumu wa
kumfanya mtazamaji mwenye mawazo haya kuelewa kuwa ngoma au unyago ni sanaa za
maonesho.
Wazo hili la uchekeshaji pia limesababisha
kudharauliwa kwa sanaa za maonesho. Watu wengi hawa kuona kuwa ni jambo la
maana kwenda kutazama maonesho ambayo umuhimu wake ni kuchekesha. Basi ikawa
sanaa za maonyesho ni shughuli ya watoto wadogo au labda watu wasiokuwa na kazi
au wanaotafuta kuchekeshwa. Mawazo haya yameendea mpaka leo na ndiyo yaliyosababisha,
kutokutiliwa mkazo kwa maendeleo ya sanaa za maonesho. Na hata vitabu vya
tamthilia vilivyochapishwa mwanzo kwa lugha ya Kiswahili, Afrika mashariki
vilikuwa na athari za vichekesho vitabu kama vile “Afadhali mchawi” “Mgeni
karibu” “Nakupenda lakini”, “Nimelogwa nisiwe na Mpenzi” vilionekana
havina umuhimu sana kwa jamii ya Afrika mashariki zaidi ya kuburudisha tu. Vitabu
kama hivi vilisaidia kudumisha wazo la kudhani tamthilia ni vichekesho tu.
Hivyo basi lilifisha au kuua sanaa za maonyeshao za kiafrika.
Uhusikaji wa Waafrika katika shughuli
mbalimbali za kiuchumi. Watu walitumia muda mwingi katika kuzalisha kwani,
walichukuliwa wengi kwenda kufanya kazi
katika sekta mbalimbali za kiuchumi zilizoanzishwa na wageni, mfano; Waafrika
wengi walichukuliwa kama manamba katika mashamba ya mkonge, hivyo basi
kushindwa kushiriki kikamilifu katika suala la kuendeleza sanaa za maonyesho
kitu ambacho kilisababisha sanaa za maonyesho kufifia kwa kiwango kikubwa kwani
walikua wakilazimishwa kufanya kazi hizo
za kiuchumi.
Hivyo basi, katika kipindi cha ukoloni, sanaa za maonesho
zilififia na kufa kutokana na mbinu zao za kukuza ukoloni. Aidha, katika kipindi
hiki cha usasa, sanaa za maonesho zinazidi kufifia na kutoweka kutokana na
mwingiliano wa jamii mbalimbali zenye tamaduni tofauti, mwendelezo wa shughuli
za kikoloni kama elimu na dini pamoja na maendeleo ya sayansi na tekenolojia
vinazidi kufifisha na kuua sanaa za maonesho za Kitanzania.
MAREJEO
Balisidya, M. L. (1987), “Tanzu na Fani za Fasihi Simulizi” katika Mulika nambari 19. Dar es Salaam:
TUKI
Mhando, P na N. Balisidya (1976), Fasihi na sanaa za maonyesho; Tanzania Publishing HouseDar es
salaam.
Wamitila, K. W. (2004), Kichocheo
cha Fasihi Simulizi na Andishi. Focus Publication: Nairobi Kenya.
No comments:
Post a Comment