Dini

      


          UTANGULIZI.
Kanisa katoliki lina utaratibu wa kutoa mafundisho ya ndoa kwa wachumba kabla ya ndoa kama sehemu muhimu sana ya matayarisho kabla ya adhimisho la ndoa takatifu ya kikristu. Mafundisho hayo ni muhimu sana ili kuwawezesha wanandoa kufahamu wajibu na haki zao katika maisha ya ndoa kufuatana na mafundisho ya imani na maadili ya kanisa kuhusu ndoa; pia kuwawezesha kujua wajibu na haki zao kufuatana na sheria za ndoa za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa ufasaha zaidi, mafundisho ya ndoa yanalenga kuwawezesha wanandoa kufahamu wajibu na haki zao kikristu na kijamii.
Mafundisho ya ndoa yatolewayo kanisani kabla ya ndoa ni muhimu sana hasa kwa kuwa yanamwezesha mtu wa ndoa kufahamu maana ya ndoa ya kikristu na tofauti iliyoko kati ya ndoa hiyo ya kikristo (kikatoliki) na ndoa za namna nyingine (ndoa ya kiserekali na ndoa ya jadi/kimila).
Mafundisho yote ya ndoa katika kanisa, iwe ni kuhusu sheria au imani na maadili yake, yana kigezo chake katika Biblia Takatifu. Kwa mfano: (soma sehemu hizo kutoka misale ya waumini au Biblia takatifu) -katika kitabu cha Mwanzo 2:18-24 tutaona kuwa Mungu ndiye aliyeratibu ndoa, na kwamba ndoa ni kati ya mwanaume na mwanamke -katika kitabu cha Tobia 8:4-8 tutaona kuwa ndoa ni kwa maisha yote (kufikia uzee maana yake ndoa ni ya kudumu) -Katika kitabu cha Waefeso 5: 2(a), 25-32 Ndoa ni muungano wa mapendo, unaofanana na ule wa Yesu kwa kanisa -katika waraka wa Petro 1Petro 3:1-9 tutaona kuwa ndoa ni muungano unaokolezwa na maisha ya fadhila -Katika Injili ya Matayo 19: 3-6 tutaona kuwa Yesu ameiinua ndoa na kuipa hadhi ya sakramenti, na hivyo kwamba katika ndoa ya wabatizwa wawili hakuna talaka kamwe.
MAANA YA NDOA. Ni muungano wa hiari kati ya mwanaume na mwanamke wenye lengo la kuishi pamoja kama mume na mke kwa maisha yao yote. MALENGO YA NDOA
(1) Kukaa pamoja (kuishi pamoja) Mwa. 2:18 Bwana Mungu akasema. “Si vema mtu huyo akae peke yake, nitamfanyia msaidizi wa kukaa naye”……
(2) Kuzaa watoto na kuwalea. Mwa. 1:27 Mungu akawabarikia akawaambia “Zaeni mkaongezeke mkaijaze dunia na kuitiisha”. Lakini kuzaa tu haitoshi, wala kuzaa si kazi bali kazi ni hasa kulea. Wazazi wanapaswa kumlea mtoto wakimtunza kwa mapendo tangu tumboni maana mtoto tumboni mwa mama mwenye mimba ni binadamu. Lk.1 : 40-42 “Ikawa Elizabeth aliposikia kule kuamkia kwake Mariamu, kitoto kichanga ndani ya tumbo lake kikaruka kwa furaha…” Mtoto alelewe na kutunzwa kama Mama Maria na Yosepf walivyomtunza mtoto Yesu na kumlea katika misingi ya imani na maadili na hivyo kukua na kuongezeka katika kimo sambamba na hekima ya Mungu Lk…..
(3) Kuwaokoa katika tama za mwili 1Kor.7:1-2 “….lakini kwa sababu ya zinaa kila mwanaume awe na mke wake mwenyewe na kila mwanamke awe na mume wake mwenyewe”
NDOA NI WITO Ndoa si shauri la kibinadamu tu, bali ni shauri la kimungu pia; ni wito. Ndoa ni wito kwa maana ya kuwa ni Mungu anayewaita watu ili wamtumikie katika maisha hayo. Watu wa ndoa wanaitwa na Mungu ili wamtumikie katika maisha ya familia. Sio kila mmoja aliyeitwa kwa maisha hayo, na si kila mmoja aliyejaliwa kuishi katika wito huo. Wengine wameitwa kuwa watawa na wengine mapadre.
NDOA NI AGANO Ndoa sio mkataba bali ni agano. Ni agano kama agano la Mungu na watu wake Israel. “Mimi nitakuwa Mungu wao na wao watakuwa watu wangu, hata wakikosa kuwa waaaminifu, mimi nitabaki mwaminifu daima ” Ndoa ni agano ambalo hata kama mmoja anakosa uaminifu basi mwingine aliye kweli mkristu anapaswa kubaki mwaminifu daima.
NDOA YA KIKRISTU KWA WABATIZWA WAWILI NI SAKRAMENTI. Yesu aliiinua ndoa na kuipa hadhi ya sakramenti pale alipotamka kuwa “….wamekuwa si wawili tena bali mwili mmoja, alichounganisha Mungu mwanadamu kamwe asitenganishe” Mt. 19 : 6. Ni sakramenti kwa maana ya kuwa ni muungano ambao kwa ishara za nje zionekanazo, neema ya Mungu isiyoonekana inamiminwa kwa wanandoa na kuwawezesha kuishi maisha mapya. Katika ndoa ya namna hii tunaona mfano wa Muungano wa Kristu na kanisa katika umoja na uimara. Yaani ndoa kwa asili yake ni ya mwanaume mmoja na mwanamke mmoja. Kujitoa kikamilifu katika ndoa kwaweza kuwepo tu kati ya mwanaume mmoja na mwanamke mmoja. Kujitoa huku kikamilifu hakuwezi kuwepo kama kuna waume wengi au wake weng. Zaidi ya hayo ndoa ya kikristu iliyo sakramenti inaakisi muungano usiovunjika wa kristu na kanisa. Ndoa iliyohalali na kamili (iliyoratibishwa na kukamilishwa au kutimizwa) haiwezi kamwe kuvunjwa na nguvu zozote za kibinadamu isipokuwa kifo. Maana yake katika ndoa iliyo sakramenti, hakuna talaka kamwe. (mt. (19 :3-6), 1Kor 7 : 10).Wanandoa hata wakipeana talaka bado ndoa yao ipo pale pale. “Kila mtu atakayemwacha mke wake na kuoa mwingine azini juu yake, na mke akimwacha mumewe na kuolewa na mtu mwingine azini” Mk. 10 : 11. Kimsingi kama kuna sababu nzito zenye kuhalalisha utengano wa wanandoa basi utengano huo utakubalika kwa masharti kwamba hakuna atakayeruhusiwa kuoa au kuolewa hadi mmoja wao atakapofariki kwa kuwa utengano hauvunji ndoa (1 Kor. 7:10-11). Baadhi ya sababu zinazowezakupelekea wanandoa kutenganishwa kisheria ni. Ugoni, ukatili/unyama dhidi ya mwenzio wa ndoa, kichaa, magonjwa, ulawiti, kuzembea wajibu kwa makusudi (yaani kumnyima mwenzio wa ndoa mahitaji yake ya lazima au kukataa kutunza watoto, uasi wa ndoa au utoro wa muda mrefu –miaka 5 na zaidi, nk.).
Talaka inayoweza kuruhusiwa katika kanisa katoliki ni ile inayozingatia kile kinachoitwa UPENDELEO WA PAULO kwa ndoa zile tu ambazo sio sakramenti; yaani kwa wanandoa ambao mmmoja wao sio mbatizwa, naye asiyebatizwa ndiye chanzo cha kutaka kuachana. (1Kor7: 15). Inaitwa upendeleo wa Mt. Paulo maana sio ruhusu ya moja kwa moja kutoka kwa Mungu. Paulo anasema, mimi binafsi nawaambia sio Bwana! 1Kor 7:12
Kwa mwanaume mwenye wake wengi na ambaye anataka kufunga au kuishi katika ndoa ya kikristu ni sharti achague mke mmoja kati ya hao na kuwaacha wengine baada ya kuwapa haki za kisheria zinazotokana na kule kuishi pamoja na sio kuwafukuza au kuwatelekeza.
NDOA HALALI NA KAMILI KATIKA KANISA. Nini kinachofanya ndoa iwe halali na kamili na pasipo kasoro yoyote?
Ndoa inaweza kuwa halali na kamili kabisa kisheria lakini bado ikawa na kasoro fulani kutokana na mapungufu yasiyoonekana hadi malalamiko yatakapotolewa na mmojawapo wa wanandoa. Kama ndoa sio halali basi ni batili; Na kama ndoa ina kasoro (ingawa ni halali)basi ni batilifu.
Ili ndoa iweze kuwa halali na kamili na pasipo kasoro, mambo mawili makubwa yanatakiwa:
(1) Ridhaa. Kuwe na makubaliano kamili kati ya wanandoa; yaani uhiari unaotoka moyoni na ulio bayana, yaani ukubali uliodhihirishwa katika ibada mbele ya mashahidi wawili na mfungishaji au msajili (Public manifestation of the consent). Bila Ridhaa, ndoa haiwezi kamwe kuwa halali.
Ridhaa kwa kawaida huanza siku nyingi kabla ya ndoa wakati wachumba hao wanapoanza kuweka mapatano na kudhihirishiana wenyewe kwa wenyewe nia ya kutaka kuoana. Kipindi hiki cha kufanya mapatano ya ndoa kabla ya ndoa yenyewe kinaitwa kipindi cha uchumba. Ridhaa inajionyesha wazi katika kutembeleana na kuzungumza pamoja kuhusu kuoana baadaye, kupeleka taarifa na kutambulishana kwa wazazi, ndugu na jamaa, kuvikana pete za uchumba, kutolea mahari (kwa makabila yanayofanya hivyo), kupeana zawadi mbalimbali, kutambulishana kanisani, uwepo wa kila mmoja kwa nafsi yake wakati wa kuandikisha ndoa, kuhudhuria mafundisho ya ndoa nk.
Lakini kama tulivyosema hapo juu, Ridhaa hatimaye, katika ndoa za wakristu ni lazima idhihirishwe katika ibada takatifu mbele ya mashahidi wawili na mfungishaji au msajili. (Hapa wachumba wafanye mazoezi ya kujifunza liturjia ya ndoa, yaani Jinsi ya kujibu yale maneno yanayoonyesha ridhaa )
(2) Kusiwepo kizuizi chochote au kikwazo kinacholeta ubatili au ubatilifu wa ndoa.
Vizuizi ni mazingira au hali inayomkataza mtu kufunga ndoa. Vizuizi vinaweza kufanya ndoa iwe batili maana ni makatatazo ya kisheria yaliyo wazi na yanayoonekana wazi mbele ya wanajamii, na hivyo yaweza kulalamikiwa na mtu yeyote yule anayeona pingamizi. Vizuizi vya namna hii vyaweza kulalamikiwa wakati wowote hata baada ya ndoa kufungwa; na ikithibitika kwamba vilikuwepo basi inachukuliwa kuwa ndoa hiyo si ndoa kabisa kisheria kwa kuwa itachukuliwa kuwa haikuwepo (c.1073). Vipo vizuizi vingine vinavyofanya ndoa iwe batilifu (illicit). Hivi ni vile vinavyotokana na kasoro au mapungufu fulani kati ya wana ndoa. Vyenyewe havifanyi ndoa kuwa batili maana ndoa ni ya kweli (valid) lakini vinaweza kuwa na athari katika uimara wa ndoa kutokana na kasoro ya kutofuata sheria (impedimentum prohibens).
Ndoa batili ni ile ambayo imefungwa ikiwa na vizuizi au vikwazo vinavyoleta kasoro kubwa na kuifanya isiwe halali. Ndoa batili ni ndoa ambayo tangu mwanzo haikuwa ndoa kwani tangu ilipokuwa inafungwa haikuwa halali. Kwa hiyo ndoa batili ni ndoa ambayo sio halali. Kwa hiyo tunaweza kusema kwa usahihi kisheria kwamba ndoa iliyofungwa isivyo halali sio ndoa, kwani hapakuwepo ndoa tangu mwanzo. Vikwazo vinavyoweza kufanya ndoa kuwa batili na hivyo kuifanya isiwe halali ni wanandoa kutokuwa na uwezo wa kuoa kisheria kutokana na umri mdogo usiokubalika (mvulana akiwa chini ya 18 na msichana akiwa chini ya 15), maharimu au ndoa kati ya jamaa, ndoa inayoendelea, kulazimisha/kutokuwepo ridhaa au kibali cha mume au mke kwa hiari, ndoa inayoendelea, kutofuata taratibu zingine muhimu mfano kufunga ndoa iliyowekewa pingamizi, kufunga bila kuandikisha nk. Ndoa batili inaweza kuvunjwa na wale waliooana bila kufika mahakamani kutokana na ule ukweli kwamba ndoa hiyo haikuwepo tangu mwanzo. Ndoa batili si ndoa kisheria.
Kasoro zinazofanya ndoa iwe batilifu ni kwa mfano uhanithi, kutokuwepo kwa kibali cha mzazi kwa msichana wa umri 15-17, mfungishaji kutokuwa na mamlaka na wale wanaooana wote hawakujua hivyo, maradhi/magonjwa//wazimu au kifaa, mimba ya mwingine iliyokuwepo wakati ndoa inafungwa, ikiwa ndoa haikutimizwa, ikiwa ndoa haikutangazwa nk. Ndoa batilifu ni ndoa kamili na halali ila ina kasoro. Ndoa batilifu ni ndoa ambayo kila mahakama itaikubali kuwa ni ndoa kamili na halali kabisa na itendelea kuonekana kuwa ni ndoa halali na kamili hadi itakapolalamikiwa na mmoja wa wanandoa (ispokuwa shauri umri kwa ndoa iliyohitaji kibali cha mzazi). Ubatilifu kwa kasoro zingine unaweza kulalamikiwa tu na mmoja wa wanandoa, na ikiwa kuna ulazima wa kuvunja ndoa basi ni mahakama pekee yenye mamlaka ya kuvunja ndoa ya namna hiyo. Mke na mume katika ndoa batilifu wana haki na wajibu ule ule wa ndoa ya kawaida, mpaka ndoa hiyo itakaopuvunjwa na mahakama kutokana na malalalamiko ya mmoja wao. ni mahakama tu inaweza kuvunjwa ndoa ya namna hiyo. Sheria za nchi zinasema kuwa watoto waliozaliwa katika ndoa batili sio halali, lakini watoto wanaozaliwa katika ndoa batilifu ni halali.
Vizuizi vinavyoweza kufanya ndoa iwe batili au batilifu ni kama vifuatavyo: --Umri mdogo --Maharimu (undugu, ujamaa) --Uhanithi. Maana yake kutokuwa na uwezo wa kufanya tendo la ndoa (kasoro iliyokuwepo kabla ya kufunga ndoa na sio tatizo lililotokea baada ya ndoa kutimizwa)
-- Kutotimiza ndoa: Ndoa hutimizwa katika tendo takatifu lililo kielelezo cha Muungano wa upendo ambapo kila mmoja anajitoa nafsi yake kwa ajili ya mwenzake, akiishiriki kikamilifu na kitakatifu furaha ya tendo hilo ambalo, kama Mungu akinuia na akipenda basi kwa njia yake yeye mwenyewe aendeleze kazi yake ya kuumba watu (c. 1061). Tendo hili ni lile linalofanyika mara ya kwanza baada ya ndoa kufungwa. kutotimiza ndoa kunafanya ndoa iwe batilifu. Ila ndoa inabaki kuwa halali kabisa, na itachululiwa hivyo hadi malalamiko yatakapotolewa maana wenye kujua mapungufu ya ndoa hiyo ni wanandoa wenyewe. Ubatilifu wa ndoa kwa shauri hili waweza tu kulalamikiwa na mmoja wa wanandoa na si mtu mwingine yeyote.
Note: Wapo watu wa ndoa wanaoshindwa kutimiza ndoa kutokana tu na kiburi au jeuri (bila sababu za msingi), wengine kwa sababu ya ujinga wa kutojua matokeo ya ndoa, wengine labda kwa sababu ya uhanithi nk.
--Ndoa ya awali inayoendelea. Hairuhusiwi kufunga ndoa nyingine wakati mwenzi wako bado yu hai kwa ndoa ya kikristo ambayo ni sacrament kwa wabatizwa wawili. -- utekaji wa mwanamke --kutokuwepo wakati wa ndoa --tofauti ya dini. Hairuhusiwi mkatoliki kuoana na mtu wa dini nyingine au dhehebu jingine pasipo ruhusa ya askofu wa jimbo kwa kujaza fomu maalum ya maombi. --daraja takatifu. Wenye daraja takatifu hawawezi kufunga ndoa halali --Nadhiri za kitawa Watawa hawawezi kufunga ndoa halali --uhusiano wa ndoa/ujamaa wa ndoa. Ni marufuku kuoa jamaa wa karibu wa mwenzio wa ndoa mf. Mume kuoa tena jamaa wa karibu wa mke. --kutokuwa na akili timamu-wendawazimu au utindio wa ubongo. Hii inaleta ubatili wa ndoa kwa kuwa inaathiri uwezo wa kufanya maamuzi sahihi na kuonyesha ridhaa. --Ujinga. Asiyetambua kuwa ndoa ni ushirika wa kudumu kati ya mwanaume na mwanamke ambao huelekezwa kwenye kuzaa watoto kwa njia ya kufanya tendo la ndoa ni mjinga, na huyu akifunga ndoa basi anaingia katika ndoa bila ndoa. --Kufunga ndoa na mchumba ambaye hakuwa amenuiwa. Kufunga ndoa kwa makosa ma mchumba ambaye hakuwa amenuiwa huifanya ndoa kuwa batili tangu mwanzo. --Ulaghai-udanganyifu. Mtu ambaye anafunga ndoa kutokana na ulaghai au udanganyifu ili mchumba mwenzake apate kutoa ukubali wa ndoa na baadaye kasoro anayoificha inaweza kuvuruga vibaya mno ushirika wa ndoa, anaingia ndoa bila ndoa.. Mfano binti ambaye amewahi kufanyiwa upasuaji wa tumbo na kuondolewa tumbo la uzazi, apatapo mchumba na kufunga naye ndoa bila ya kumfahamisha jambo hili, basi anaingia ndoa bila ndoa. -- Mtizamo wa kimakosa kuhusu ndoa. Mfano kudhania na kuchukulia kuwa ndoa ya kikristu ni sawa tu na ndoa ya kiserekali au ya kijadi na kukumbatia muungano wa ndoa ambao ni sawa na ndoa hizo nyingine na kukataa tangu mwanzo hadhi yake ya sakramenti basi anaingia ndoa bila ndoa. -- Kutoa ukubali wa ndoa kwa kujisingizia au nusu nusu. Wakati ndoa inaposhuhudiwa, kama mmoja au wote wanakataa kwa makusudi ndoa yenyewe au hata mojawapo ya mambo muhimu ya ndoa mfano kuzaa watoto na kuwalea au kukataa umoja na uimara wa ndoa watakuwa wanaingia ndoa batili moja kwa moja. -- Ndoa ya masharti. Ndoa inayofungwa chini ya masharti yanayohusu mambo yajayo ni batili. Mfano kusema, “ninafunga ndoa nawe lakini nitaishi nawe tu kwa masharti kuwa utanizalia watoto” hiyo ni ndoa batili. -- Kulazimishwa-ndoa ya shuruti, na ndoa ya hofu. Anayefunga ndoa kutokana na shuruti ya wazazi na hasa kuolewa na kijana asiye chaguo lake na asiyempenda ila akakubali tu kwa hofu ya kufukuzwa nyumbani kwa sababu ya wazazi kupokea mahari au kwa sababa ya binti huyo kupata mimba basi huyo anaingia ndoa pasipo ndoa.
--Ndoa ya muda. Ndoa sio mkataba wa muda Fulani mfupi bali ni kwa maisha. Anayefunga ndoa kwa lengo la kuishi kwa muda tu na kuachana tena baada ya muda mfupi basi anaingia ndoa bila ndoa --Jinai. Kushirikiana kumwua mchumba wa mmoja wao ili kufunga ndoa na mchumba aliyebaki kunabatilisha hiyo ndoa --uhusiano mbaya hadharani/uhawara -- Uasili /uhusiano wa kisheria (Adoption) --mfungishaji ndoa kutokuwa na mamlaka --mashahidi kuwa chini ya miaka 18 --Kuwa katika eda(waislamu) --Kuwepo kwa pingamizi --magonjwa mf. maradhi ya zinaa ya zinaa, kifafa nk) --Wazimu au kichaa (kilichokuwa kimefichika kikajitokeza baadaye) --mimba ya mwingine
Note. Ili kubaini vizuizi vya aina yoyote kati ya wachumba na hivyo kuzuia au kuepuka ubatili au ubatilifu wa ndoa ni muhimu kuzingatia sheria inayodai ndoa kutangazwa na kwamba isifungwe kabla ya siku 21 tangu ilipoandikishwa. Inashauriwa pia kwamba ni vizuri wachumba kabla ya ndoa wakapeana muda wa kutosha kwa kufanya uchunguzi (kuchunguza kama kuna undugu, kupima magonjwa, kufahamiana kitabia nk) ili kuepuka jambo lolote lenye kufanya ndoa kuwa batili au batilifu.
DHANA YA NDOA KATIKA NDOA ZISIZOFUNGWA. Katika sheria ya Tanzania, kuna ndoa katika hali mbili; yaani Ndoa zilizofungwa na ndoa zisizofungwa. --Ndoa zilizofungwa, ili ziwe halali na kamili ni lazima pawepo mambo makubwa mawili. Ridhaa, na kutokuwepo kwa vizuizi vilivyotajwa katika mada hapo juu. --Katika sheria ya Tanzania ipo pia dhana ya ndoa kwa watu wanaoishi pamoja kama mume na mke hata ikiwa hawakufunga ndoa. Mwanaume na mwanamke wakiishi pamoja huweza kuchukuliwa kuwa mke na mume mbele ya sheria japokuwa hawakuwahi kufunga ndoa. Dhana hii imeelezwa katika kifungu cha 160 cha sheria ya ndoa. Ili dhana hii iwepo ni lazima yafuatayo yathibitishwe:
(1) Lazima ithibitike kwamba mwanamke na mwanaume wameishi pamoja kwa muda wa  miaka 2 au zaidi kwa mfululizo.
(2) Lazima pia ithibitike kuwa umma unaowazunguka wanawachukulia na kuwapa heshima ya mke na mume.
(3) lazima ithibitishwe kuwa watu hao walikuwa na uwezo wa kuwa mke na mume wakati walipoanza kuishi pamoja na kwamba walikuwa na umri uliokubaliwa kisheria.
(4) Ni lazima pia ithibitishwe kuwa kati ya hao wawili au wote hakuna aliye na ndoa inayoendelea.
Note: Dhana hii imewekwa ili kulinda haki za binadamu dhidi ya watu wanaowachukua wengine na kuishi nao kama mume au mke kisha kuwafukuza baadaye pasipo kujali athari wanazopata wale wanaofukuzwa kiuonevu bila msaada.
Hata hivyo, watu wengi wameishi maisha yanayodhaniwa kuwa ni maisha ya mume na mke kumbe hata dhana ya ndoa haikuwepo na hivyo wakapata hasara na athari kubwa maishani baada ya kulazimika kuachana bila kuwa na haki ya kugawana chochote. Kwa hiyo ili kutokuwa na mashaka yoyote juu ya muungano wenu aheri kufunga ndoa.
NDOA NI MAISHA YA FADHILA.
Ndoa kisheria ni katika utekelezaji na uwepo wa zile sifa mbili kuu tulizoona hapo juu, lakini ndoa sio tu hayo bali ndoa kikristu ni matendo ya kila siku yanayodhihirishwa na zile fadhila za kikristu katika nyumba ya ndoa. Ili kuweza kweli kuishi kulingana na makusudi ya ndoa na kufikia malengo yake. Bila fadhila hizo, hakutakuwa na ndoa ya kweli kivitendo maana kutimizwa na kufikiwa kwa malengo ya ndoa kunategemea sana jinsi tutakavyokoleza muungano wetu kwa matendo ya fadhila.
(1) Kupendana kwa dhati katika maisha ya kila siku. Ndi fadhila kuu inayowaunganisha watu wa ndoa. Maisha ya ndoa ni maisha ya uhusiano wa mapendo kati ya mume na mke na sio uhusiano wa ubwana na utumwa. Tena kupendana si kati ya bwana na Bibi tu peke yao, bali kuwapenda pia wazazi na ndugu wa pande zote mbili.
Upendo upo wa aina mbalimbali-wa kimaumbile, wa vitu, wa kirafiki, wa Kimungu. Upendo wa ndoa unapaswa kuwa upendo wa Kimungu-AGAPE LOVE. Ili upendo uweze kuwepo lazima udhihirishwe na kuthibitika kwa njia ya fadhila zingine za hali na matendo. Mfano hizi zifuatazo.
(2) Kufarijiana. Kupeana moyo na kutuliozana katika shida na mahangaiko. Kujuliana hali hasa katika ugonjwa na dhili
(3) Kuheshimiana na kuthaminiana. Kumwona mwenzako kama wewe mwenyewe. Hivyo kutoruhusu chochote chenye kumdhalilisha mwingine au chenye kuvunja heshima yeke. Kulinda utu na hadhi ya mwenzio. Kutomwona mwenzako kama mtumishi (house boy au house girls). Kutoonyesha dharau, kutomnyanyasa. Tusifanye nyumba ya ndoa kuwa mahali pa amri kama jeshini au gerezani. Tusigeuze nyumba ya ndoa kuwa Jehanum, mahali pa mateso, uwanja wa mapigano na shule ya matusi. Tukumbuke kuwa familia ya kikristu ni mahali pa malezi ya msingi kwa watoto. Ni rahisi watoto kuiga tabia zetu. Hivyo tukumbuke kwamba amani na uelewano kati ya wazazi ni msingi imara kwa malezi na ujengaji wa tabia njema kwa watoto.
(4) Kushirikiana na kujadiliana. Kupanga pamoja mambo yote yanayohusu maisha na maendeleo yenu, kuamua kwa pamoja.
(5) Kuarifiana na kuafikiana. Kufanya yote kwa makubaliano, kupeana taarifa na kujulishana.
(6) Kuhudumiana na kusaidiana. Hii ni pamoja na kuhurumiana na kutunzana. Yaani kutokuwa na ubinafsi wowote. Kutojipendelea, bali kumjali kwanza mwenzako na kujali mahitaji yake. Kila mmoja aone fahari kumhudumia mwenzake. Kupokezana majukumu mazito. Kumsaidia na kumhurumia mwenzako hasa wakati akiwa katika mahangaiko.
(7) Kusikilizana na kuelekezana. Kuwa msikivu, mngwana na tayari kumsikiliza mwingine katika shida zake. Kuelekezana jinsi unmavyotaka mawenzako awe au atende. Kuelimishana na kufundishana katika mambo mbalimbali.
(8) Kushauriana. Kupeana mawazo, kukubali ukweli, kupenda mabadiliko. Kutojiona mkubwa au wa mana zaidi.
(9) Kuaminiana na kuonyeshana uaminifu. Kwanza kujiamini wewe mwenyewe. Halafu kujiaminisha kwa mwenzako; mfanye akuamini. Daima epuka tabia na mienendo yenye kuleta mashaka. Lakini pia kuepuka wivu wa kijinga usio wa lazima. Peaneni nafasi na uhuru wa kujumuika na watu wengine kwa nia njema; na kwa busara tuepuke watu wenye nia mbaya.
(10) Kuungamiana na kusameheana. Kuwa tayari kukubali na kukii kosa, kutafuta amani na maelewanao daima, na kupatana siku zote. Msikubali dunia nzima itambue kwamba kwenu kuna ugomvi. Kuondoa kinyongo na hasira zisizojenga. Kuacha kunung’unika na kulalamika juu ya mambo yasiyo na msingi.
(11) Kukosoana kusahihishana. Kurekebishana kwa busara na kwa lugha nzuri isiyoua moyo. Tuepuke lugha za karaha. Tuchunge lugha za maudhi!
(12) Kunyenyekeana. Kuonyesha utii na upole. Kuepuka kiburi, jeuri, majigambo, matusi, ubabe. Tukumbuke kuwa, kujinyenyekesha si kujidhalilisha au kujishusha bali ni kufanana na kristu aliyejinyenyekeza kwa ajili yetu hata kufa msalabani ili atupatanishe na kuleta amani kati yetu na Mungu.
(13) Kuvumiliana na kupokeana. Kumkubali mwenzako nba kumpenda kama alivyo. “Ukilipenda ua la rose (waridi) basi ukubali hata miiba yake”. Huyo ndiye Mungu aliyekupatia pamoja na mapungufu yake. Ndiye (ubavu wako) unayefanana naye.
(14) Kufurahishana na kufurahiana. Kuburudika pamoja, kusifiana,kupongezana, kutaniana (kwa nia nzuri), kupeana zawadi, kuadhimisha sikukuu na kumbukumbu mbalimbali za kifamilia pamoja (birthday, siku ya kumbukumbu ya ndoa, sherehe ya kidini nk). Pia kuzungumza pamoja mara kwa mara na kula pamoja mara nyingi. Kula pamoja ni alama na ishara ya upendo na uelewano. (Eating together at the same table is a visible sign of love and fellowship. Jesus sat at table and ate with the sinners as a clear sign, that though he hated their sins, he loved them. He used that particular moment to correct them and bring them to the way of the gospel).
(15) Kushukuru. Kushukuru ni tabia njema, ni nidhamu, ni tendo la busara. Watu wa ndoa wanapaswa kuonyeshana shukrani kwa kila jema wanalotendeana kama alama ya kuthamini kazi, juhudi, na upendo wa mwenzake kwake. Kusema « Asante » au « Nashukuru » ni neno dogo lakini lenye kumpa mtu nguvu na ari ya kuendelea kufanya makubwa zaidi, kwa uzuri zaidi na kwa moyo zaidi. Watu wa ndoa wanapaswa kuonyesha shukrani hasa kwa Mungu mara kwa mara kwa yote anayowajalia katika maisha hata kama ni madogo. Ukipata shukuru, ukikosa usikufuru!
(16) Kusali pamoja na kuombeana. Bila kujiunganisha na Mungu daima katika sala, itakuwa vigumu hata kuishi zile fadhila nyingine zote. Watu wa ndoa wanahitaji kusali siku zote ili wajaliwe neema ya kuwaimarisha na kuwadumisha katika maisha ya kifamnilia. Bila kuomba neema ya Mungu, shetani atakuwa anawahangaisha na kuwavuruga kila mara. Hivyo watu wa ndoa wanahitaji sana kuendeleza maisha ya sala na sakramenti. Kusali pamoja kila siku ili Mungu awajalie neema katika nyumba yenu, aibariki na kuidumisha katika amani na furaha. Tukumbuke kuwa, familia ni kanisa la nyumbani, ni mahali pa sala, ni mahali pa kukutana na Mungu ; ni mahali ambapo watoto hujifunza imani hai kwa maisha yote. Ukichunguza utaona kuwa matatizo makubwa ya ndoa ni katika zile nyumba ambazo hawasali.
HAKI NA WAJIBU WA WATU WA NDOA.
Kila mwanandoa ana haki na wajibu ambazo zinapaswa kuheshimiwa na kutekelezwa. Moja ya sababu zinazofanya nyumba ya ndoa iwe ya mateso kwa mmojawapo au wote wawili au hata kusababisha kuvurugika na kuvunjika kwa ndoa ni kule kukiuka haki za mwingine na/au kutotekeleza wajibu za kila siku zinazowapasa kisheria na kimaaadili au hata kule kukiuka ustaarabu wa kawaida wa mwanadamu katika maisha ya kila siku
Haki za wanandoa ni pamoja na.
(1) Haki ya kulala na mme/mke. 1Kor 7 :3 Mume na ampe mke haki yake (kutumia ndoa) na hivyo hivyo mke na ampe mume haki yake. ‘Mke hana amri juu ya mwili wake bali mumewe, hivyo hivyo mume hana amri juu ya mwili wake bali mkewe. Msinyimane isipokuwa mmepatana kwa muda ili mpate faragha kwa kusali mkajiane tena…’ (2) Haki ya kukataa kubakwa au kulazimishwa tendo la ndoa wakati usiofaa au kwa njia isiyofaa Note : --haifai kutumia ndoa (a) katika ulevi (b) katika ugonjwa © Wakati mke ana mimba-siku za mwisho kabla ya kuzaa (d) siku za kwanza mara baada ya mtoto kuzaliwa
--mamboyasiyofaa kabisa katika ndoa(a) Kuharibu na kumwaga mbegu bure kwa kuchezeana (b) kutumia dawa za kuzuia mimba au mpira ©kulawiti)
(3) Haki ya kumiliki mali. Kila mmoja ana haki ya kuwa na umiliki wa mali hasa ile aliyozalisha peke yake kabla ya kuoana. Lakini wote wana haki ya kumiliki kwa pamoja ile mali waliyoipata kwa pamoja au iliyoendelezwa kwa pamoja baada ya kuoana (mf. Ardhi, mifugo,nyumba, vyombo nk.). Kila mmoja ana haki ya kujiandikia mali ambayo ana uhakika kwamba ni ya kwake na asiyodhulumu. Lakini ni muhimu kuangalia zaidi mafaa ya familia kwa ujumla.
(4) kila mmoja ana haki ya kupendwa, kulindwa na kutunzwa na mwenzake. Haki ya kutonyanyaswa, haki ya kuheshimiwa na kuthaminiwa katika utu. Hakuna haki ya mume au mke kumpiga mwenziwe. (5) Haki ya kudai fidia kwa mtu yeyote aliyezini na mmoja wa wanandoa, au aliyemtorosha mmoja wa wanandoa. (6) Haki ya kutoa lalamiko la kutengana ikiwa kuna na sababu zenye uzito wa kutosha na kwa kawaida iwe angalau miaka miwili imepita tangu ndoa ifungwe. Lakini maombi/malalamiko lazima yapite halmashauri ya usuluhisi ya Kata ya dini ya mhusika kama ni ndoa iliyofungwa kidini. (ispokuwa kwa lalamiko la kutorokwa na mume au mke na haijulikani alipo)
Lakini tunajua hakuna haki bila wajibu.
Wajibu wa wanandoa ni pamoja na : (a) Kutunzana. Chakula, mavazi, malazi, matibabu – kumhudumia mwenzako (b) kufanya kazi na kushirikiana kazi. Sio kuzurura mchana kutwa. © uaminifu na kuheshimu nyumba ya ndoa (d) Kujiheshimu na kuheshimu nyumba ya ndoa. (e)Kuepuka tabia zote zenye kuleta karaha kwenye nyumba, mfano ulevi. Ulevi humfanya mtu aonekane pumbavu, asiyeheshimika. Ulevi unakushusha hadhi, unakuondolea heshima ambayo ungestahili. Ulevi unakufanya uionekane huna busara, si mungwana. Ulevi huleta umaskini nyumbani; na ni sumu ya umoja wa kifamilia. Ulevi husababisha kukosa usingizi, huleta ukorofi, kukufanya kuwa mchafu, unakuaibisha mbele ya watu, hudhuru afya, husababisha kupoteza kumbukumbu, humfanya mtu mjinga na zezeta baadaye, hutesa wanafamilia wanaokerwa na tabia hiyo, hukufanya uchukiwe na wanafamia na kukufanya ukose heshima mbele ya wanajamii, hukufanya uone majinamisi/hallucinations,, huleta kiu ya mambo mengine (hukusukuma kufanya mapenzi hata na machangudoa bila aibu na bila kujijali). (f)Kutunza watoto. Kuwahakikishia chakula, mavazi, malazi, matibabu, elimu (g) kulea watoto katika misingi ya dini na maadili mema. Kushirikiana katika malezi ya mtoto (h)Kuwapa watoto wote urithi bila ubaguzi)nk.
KUNA MAMBO AMBAYO SIO WAJIBU ZA KISHERIA WALA KIMAADILI BALI NI WAJIBU ZILLIZO KATIKA USTAARABU WA KAWAIDA, LAKINI NI WAJIBU ZENYE NAFASI NA UMUHIMU MKUBWA KATIKA KULINDA, KUTUNZA KUDUMISHA NA KUKOLEZA MVUTO WA UPENDO KATIKA NDOA (a) Usafi wa mwili, nguo, nyumba, mazingira nk. (B) kupika vizuri, kula vizuri © kuitana majina mazuri (e)kuvalishana nguo, kufuliana, kusafishiana viatu, kupigiana Pasi nk.
(f) Kupanga na kuamua kwa pamoja juu wa idadi ya watoto mnaotaka kuzaa mkizingatia uwezo wa kuwatunza. Kumbuka ni dhambi kuzaa watoto ma kuwaacha wateseke pasipo kujali mahitaji yao ya lazima (g) Kutumia ndoa kwa kiasi. Ndoa isipotumiwa ka kiasi inakuza mno tamaa za mwili, inaweza hata kuzuia kupata mimba na wakati mwingine inaharibu afya ya wanandoa. Nk Note: Tendo la ndoa linahitaji matayarisho, majadilianona makubaliano,linahitajiheshima nalinahitaji kuwa na kiasi.
h) Kuwa na Mpango wa uzazi. Mpango wa uzazi kwa njia ya asili ndio unaopendedezwa na kukubaliwa na Kanisa. Mpango huu kwa njia ya asili ukifuatwa vizuri ni wamafanikio. Lakini unhitaji yafuatayo: 1. Uelewa: Mwanamke ajifahamu Aelewe maana ya mabadiliko yanayotokea katika mwili wake. Azielewe hali na ishara au dalili zinazomwashiria uwezekano wa kupata mimba au kutopata mimba. Mwanaume nay eaeleweshwe juu ya hali hizo-ashirikishwe na kiungwana akubali. 2. Ustaarabu katika tendo la ndoa. Litayarishwe mapema, lisifanyike katika ulevi, lisifanyike kwa kushtukiza na wala lisifanyike kwa kulazimisha. Bali lifanyike kwa heshima na ustaarabu kwa wote wawili yaani mwanaume na mwanamke kwa kuzingatia hali halisi katika mwili wa mwanamke. Matayarisho hayo ni pamoja na kula chakula kizuri, kuoga vizuri, kuvaa vizuri na kutayarisha chumba vizuri. 2. Kiasi katika tendo la ndoa Wanandoa wawe na uwezo wa kujitawala wakijua kuwa kuna siku zisizofaa kwa tendo hilo hata kama mmoja au wote wana hamu kubwa. Hata kama mmoja alikuwa safarini na sasa amerudi nyumbani na angependa kurudi alikotoka kesho yake, kama siku hii ambayo wangependa ‘kujuana’ siyo nzuri kwa sababu yoyote basi waonyeshe uwezo wa kujitawala na kuheshimu tendo hilo. Kushindwa kujitawala kunapelekea matumizi ya mipira au dawa za kuzuia mimba, jambo ambalo ni kinyume na mpango wa Mungu : ni dhambi na ni kukiuka heshima ya tendo hilo. Matokea yake ni kuendekeza uasherati katika ndoa ikiwa hawakuzoea na hawakujifunza kujitawala. Ikiwa mwanaume atatumia ‘nyenzo’ kama hizo katika ndoa kwa sababu ya kushindwa kujitawala ataendelea kuzitumia pia nje ya ndoa pale mke atakapokuwa na mimba siku za mwisho kabla ya kuzaa au siku za mwanzo za uzazi ambapo hawapaswi kufanya tendo hilo. Pia mwnandoa ataendelea kuzitumia ‘nyenzo’ hizo nje ndoa pale ambapo mwenzake ameshindwa kufanya naye tendo hilo labda kwa sababu ya ugonjwa (malaria, kupooza, au ajali ya kuleta uhanisi). Kumbe kuwa na kiasi na kujitawala katika ndoa ni dawa muhimu katika kutufanya tujiheshimu siku za mbele tunapolazimika kutofanya tendo hilo. Kujitawala katika suala la matumizi ya ndoa inadhihirisha ustaarabu mkubwa na ukomavu katika tendo hilo. Wanaopendana kwa dhati hawalali tu pamoja, bali wanaheshimiana pia na kushirikiana majonzi ya mwingine. Ishara ya upendo siyo kulala pamoja bali ni kuheshimiana. Wengi wanalala pamoja lakini bila mapendo kabisa.
(i) Kujua mwenzako anapenda nini na daima kufanya yale yanayomvuta akupende Wanaume na wanawake wanatofautiana katika mambo yanayowavutia. --Mwanamke ukumbuke daima kwamba Mwanaume anavutwa sana na mwanamke kwa kuguswa na mambo anayoyaona kwako hasa Mavazi, umbo lako, na usafi. Hivyo ukiwa makini katika haya ujue utamfurahisha sana mumeo.
Mwanaume ujue kuwa wanawake wanavutwa sana na wanaume kwa kuguswa na vitendo vya kumhudumia kwa upendo na maneno matamu ya kumfariji, kumliwaza na kumbembeleza. Kwa mwanamke, upendo ni vitendo vya ukarimu, kuhudumiwa na kuzungumza maneno ya upole na kuliwaza. Kwa mwanamke, upendo ni kutoa, ni kuhudumia, ni kusamehe. Upendo ni kusaidia, ni shukrani, upendo ni kutabasamu, ni kupongeza. Upendo ni vitendo vyote hivi. Upendo wa ndoa lazima uandamane na hisia za penzi, yaani hali ile isiyo kifani ya msisimuko wa moyoni na kujisikia mchangamfu na mwenye raha umwonapo mpenzi wako na kusema kila mara, « ananipenda nami nampenda »
KWA WOTE, dumisheni nia njema ya moyoni isiyobadilika, usikaripie wala kudhihaki, usilaumu tu bila kusifu, epuka kutoa harufu mbaya, zungumzeni kwa uhuru, usimnunie mwenzio wakati wowote, jaribu kutulia zaidi kwanza na kutafakari, matatizo yanapotokea, mlindie mwenzako siri, tendo la ndoa litayarishwe na lisifanywe haraka haraka, mfikirie kwanza mwenzako,
KIFUNGO CHA BINADAMU.

Tunaweza kumgawa Binadamu katika sehemu kuu tatu, ambazo ni: roho/nafsi (soul), akili (mind) na mwili (body). Sehemu zote hizi tatu katika mwili wa mwanadamu kwa kawaida hufanyakazi kwa ushirikiano/kwa pamoja. Unaweza kuona kwamba katika mambo mbalimbali akili zetu zinagundua na kung’amua vitu tofauti tofauti na kuvithibitisha kuwa ni sahihi, lakini inapofikia wakati wa maamuzi mambo yanageuka na wakati mwingine huwa kinyume kabisa. 

Tofauti kama hii inapojitokeza ni dhahiri kwamba nafsi na mwili havikupewa ushirikiano tangu mwanzo au huenda havikupewa nafasi ya kusikilizwa, kwa sababu nafsi/roho ndiyo inayopima ule ugunduzi/ung’amuzi na uthibitisho wa akili kama ni sahihi au la.
Hivyo basi, nafsi inapokuwa na mashaka juu ya ugunduzi/ung’amuzi wa akili ndipo inaposita katika suala zima la utekeleza wa yale matakwa ya akili, ndiyo maana unaona wakati mwingine unajikuta mzito katika kufanya jambo fulani au kutoa maamuzi fulani, unajawa na wasiwasi mkubwa juu ya jambo fulani. Hali hii inaweza kuendelea kwa muda mrefu endapo hautakuwa mwangalifu kwa sababu akili siku zote inajiona kuwa ipo juu zaidi ya nafsi/roho na mwili, hivyo kupelekea ulazimishaji wa mambo.

 Wakati mwingine inaweza kutokea kwamba mwili na roho vikashindwa kabisa kukubaliana na akili na hapo ndipo tunasema kwamba nipo “dilemma” (a situation in which a difficult choice has to be made between two or more alternative) yaani nipo njiapanda. Hali kama hii ikiendelea kwa muda mrefu mtu huyu hupata mahangaiko ya nafsi/roho. Mtu napofikia katika hatua kama hii huwa ni hatari sana kwani anaweza kufikia uamuzi mbaya sana ambao unaweza kuhatarisha maisha yake binafsi au jamii inayomzunguka kwa ujumla.

Labda utajiuliza kwa nini hali kama hii inaweza kutokea? Ni wazi kwamba katika mtazamo wa kidini mwanadamu ana maisha ya aina mbili yaani maisha ya kiroho na maisha ya kimwili. Mambo yaha kwa kawaida hayasigani hata kidogo na inapotokea yakasigana ndipo hali kama hii huweza kujitokeza. Na hii yote ni kazi ya yule mwovu shetani ambaye daima ndiye anayetufunga ama akili ama nafsi/roho au mwili.

Nina mifano mizuri sana inayoonesha namna ambavyo shetani anavyoweza kutufunga kiasi kwamba tukashindwa kujitambua. Siku moja nilikuwa sehemu fulani karibu na kilabu cha pombe za kienyeji, walikuwepo wazee wanne wamekaa katika benchi moja, wazee hawa kwa kweli ukiwaangalia utawaonea huruma jinsi walivyochakaa. Kwanza kati yao mmoja tu ndiye mwenye viatu, na hata yule mwenye viatu inaonesha ndiyo vya mwisho maana jinsi vilivyochakaa huwezi hata kuelezea. Na sidhani kama hata mwenyewe anakumbuka rangi yake ya asili.

Lakini jambo lililonishangaza ni kwamba, wazee wale walikuwa wanazungumza mambo ya busara na hekima, wanaelezea namna nzuri ya kuiongoza nchi hii, jinsi ya kuwa kiongozi bora ambaye utakubalika na wote. Walizungumzia tatizo la ajira kwa vijana na namna ya kukabiliana nalo. Kwa kweli wazee wale walinigusa sana kiasi kwamba nilitamani kuwachukua, na kuwapeleka kwenda kuishauri serikali katika mambo mbalimbali. Lakini ukijaribu kuzama katika tafakuri na kujiuliza ni kwa nini inakuwa hivyo? utang’amua kwamba watu hawa wako huru kabisa kiakili lakini kiroho na kimwili wamefungwa kabisa.

Vilevile hata katika maisha ya ndoa, utakuta mtu amefunga ndoa kabisa lakini bado hana utulivu, mara leo yuko na huyu, kesho yule, mtondogoo wale au utasikia mwenzangu hajalala nyumbani au amerudi usiku wa manane nk. mahangaiko yote haya ni ya nini? Nidhahiri kwamba watu wenye tabia kama hizi utakuta wamefungwa kabisa kimwili kiasi kwamba hawaoni raha yoyote Duniani zaidi ya hiyo. Hali kadhalika hata katika miisha ya uchumba, watu pamoja na kuwa na wachumba lakini utulivu bado ni sifuri.

Pia niliwahi kushiriki michezo mbalimbali ya vijiweni: kama vile bao, karata, pull table, nk. kwa kweli nilisikia mambo mazuri sana. Nilivutiwa sana jinsi walivyokuwa wakijadili namna ambavyo Mtumishi wa Mungu; Padre, Mchungaji, Shekhe nk. anavyopaswa kuwa. Nilistaajabu kuona hekima ya ajabu waliyokuwanayo watu wale, kisha nikajiuliza kwa nini hawa hawakuwa miongoni mwa viongozi wa dini au hata kuwa karibu na dini zao?! Nikang’amua kwamba watu hawa wamefungwa kabisa kiakili na kimwili ingawaje wanaoneka kana kwamba wapo huru kwa namna fulani.
Basi hivi ndivyo ambavyo binadamu anaweza kufungwa kabisa mpaka ukashangaa kwa nini yuko hivi na asiwe vile? au kwa nini yuko vile na asiwe hivi? Maana anachosema na anachotenda ni vitu viwili tofauti kabisa. Hali kama hii si ya kupewa nafasi katika maisha ya mwanadamu kwani inaweza kutupeleka motoni tukasahauliwa kabisa. 

Jaribu kuangalia mambo mbalimbali yanayotendeka katika ulimwengu wa leo ambayo yanasababisha Dunia kuwa sehemu isiyosalama kuishi. Mambo yenyewe ni kama vile: mauaji, ubakaji, ujambazi, uasherati, ufisadi, rushwa, uonevu, uchoyo, tama, uongo nk. yote haya yanasababishwa na kufungwa ama kiakili, kiroho, au kimwili.

Hivyo basi, jambo lakufanya ni kutompa shetani nafasi na badala yake tumpe Yesu nafasi katika maisha yetu na katika roho/nafsi zetu, kusudi aweze kutufungua pale ambapo tutakuwa tumefungwa na kuzuia tusije tukafungwa tena. Namna ya kumpa Yesu nafasi ni kwa kushiriki sakramenti mbalimbali za kanisa bila kulegalega na kutenda matendo ya huruma kila wakati, maana tunapo legalega ndipo tunapokaribisha hali ya kifungo.      

HURUMA YA MUNGU:

Hakuna kioo kinachoweza kuonesha sura pamoja na kisogo kwa wakati mmoja, hata ukitumia msaada wa vioo viwili kama wanavyotumia vinyozi. Kioo kama kioo hakiwezi kukuambia hata siku moja kama umependeza au umechukiza isipokuwa mawazo na akili yako ndivyo vinavyokuonesha hivyo.
Lakini tunaweza kupendeza zaidi tena kupita kiasi endapo tu tutawashirikisha wengine watuambie kama tunapendeza au la! Vilevile mwenzako ndiye awezaye kukurekebisha vizuri zaidi katika yale maeneo ambayo hawezi kuyafikia wala kuyaona kwa macho yako.
Ndugu zangu hali hii inajitokeza hata katika maisha yetu ya kiroho, watu hawapendi kuoneshwa madhaifu yao, hawapendi kukosolewa, hawapendi kuambiwa ukweli wala kusikia ukweli.
Kama ilivyorahisi kutazama uso wako kwa msaada wa kioo ndivyo ilivyovigumu kutazama kisogo chako, hata kwa msaada wa kioo. Mara nyingi sana sisi binadamu tunapenda kuangalia makosa ya wenzetu na kuyatolea hukumu. Mfano mzuri tumtazame mfalme Daudi.
Mfalme Daudi anasahau kwamba jambo alilolifanya linafanana kabisa na la yule tajiri, matokeo yake anaanza kuweka hasira na kutoa hukumu. Ndugu zangu, hii ndiyo hali halisi ya maisha ya binadamu wa leo.
Tumeona jinsi mfalme Daudi alivyomtendea Uria masikini wa watu kitendo cha kinyama mpaka Mungu anaamua kuingilia kati. Waswahili wanasema kuwa; “Makosa yote husameheka lakini si lile la kulala na mke wa mtu”.
Wapendwa katika Bwana, ni nani kwetu sisi asingemlaumu Daudi kwa kitendo alichokifanya kwa Uria!? Wengi wetu huwa tunalaumu sana na kutoa hukumu kwa makosa ya wengine lakini tunasahu kwamba hata sisi tunafanya hivyo hivyo tena hata zaidi ya Daudi.
Mfano: Viongozi wetu wa serikali:
Kilio kikubwa kilichotanda masikioni mwa watanzania waliowengi ni suala zima la UFISADI ambao ndiyo umepelekea hali ya maisha kuwa ngumu kila inapoitwa leo. Angalia vurugu nyingi zinazotokea hapa Tanzania kama vile, watu kugoma katika Nyanja mbalimbali hii yote kwa kiasi kikubwa inachangiwa na umasikini uliokidhiri katika jamii yetu. Huruma ya Mungu ni tofauti kabisa na Huruma ya binadamu. Binadamu anaweza kurundika lundo la vitu (silika ya kukusanya) ambavyo huwenda labda hata havitumii na mwingine ambaye hana hata kimoja akiteseka na hata kupoteza maisha bila msaada wowote kutoka kwa yule mwenye vitu.
Viongozi wetu wengi wamepoteza utu, hawamuogopi tena Mwenyezi Mungu, wanajilundikia mali za kila aina, wanaishi katika majengo ya kifahari yenye mageti zaidi ya mawili, wanatembelea magari ya kifahari na wanafanya starehe za kila aina.
Mali zote hizi wanazojilundikia pamoja na mabilioni ya fedha wanayojikusanyia, yote haya ni nguvu za wananchi waliowanyonge ambao wengi wao wanateseka sana kutokana na hali ngumu ya maisha. Wanafanyakazi usiku na mchana na bado wanalipa kodi kwa ajili ya maendeleo ya nchi, lakini cha kushangaza hata zile huduma muhimu hawazipati na matokeo yake wengi wanapoteza maisha yao.
Ndugu zangu wapendwa tazama matendo haya ya viongozi wetu wa nchi tuliowapa dhamana ya kutuongoza na kutulinda salama, wanafanya matendo kama yale aliyofanya mfalme Daudi ya kumdhulumu mnyonge wa Mungu. Hakiki nawaambia Mungu hatawaacha, atawalipa kadiri ya matendo yao, hataacha haki ya mnyonge ipotee bure.
Mfano: Taasisi zisizo za kiserikali; Sasa hivi watu wamebuni mradi kwa kuanzisha taasisi mbalimbali kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wenye matatizo mbalimbali, mfano: walemavu, watoto yatima, wajane nk. na wanaomba misaada kila pembe ya Dunia kwa ajili ya kuwasaidia watu hawa. Lakini hakuna kinachofanyika zaidi ya kujinufaisha wao wenyewe na kuwaacha walengwa wakizidi kutaabika.
Hata hawa nakuhakikishia Mungu hata waacha kamwe atawaadhibu kama alivyomuadhibu Mfalme Daudi. Mungu anajua adhabu wanayostahili.
Mfano: Katika Kanisa; wahenga wanasema kuwa “Ukitaka mtoto wako asilongwe, mpe Mchawi akulelee”. Mimi binafsi sinaimani sana na msemo huu, na wala nisingejaribu kuhatarisha maisha ya mtoto wangu.
Viongozi wetu wa kanisa, maaskofu, mapadre, wachungaji, watawa nk. hawa wote wamepewa dhamana ya kuchunga kondoo wa Mungu na kuwatangazia masikini habari njema. Je wanawajibika ipasavyo?
Hivi sasa hali ya kanisa inatisha, na inazidi kuwa mbaya kadiri siku zinavyoenda, kwani tunaona jinsi Mfalme Daudi anavyokasirika na kutoa laana kwa yule tajiri. Hivi ndivyo hata kanisa lifanyavyo sasa, linalaumu serikali na viongozi wake wakati hata lenyewe linafanya matendo yale yale. Samahani naomba nisieleke vibaya kwani hapa nazungumzia wale watumishi wa kanisa wasio waadilifu wanaofanya vitendo viovu na kulichafua kanisa.
Kweli inasikitisha sana unaposikia au unapoona mchungaji anatelekeza kundi alilokabidhiwa kuchunga na kwenda kufanya mambo yake binafsi. “Ashakumu si matusi”, naomba mniwieradhi wale wote nitakaowagusa au kuwakwaza kwa maneno yangu. Lengo langu si kutaka kuumbuana bali kusaidiana, kurekebishana na kukumbushana.
Si jambo la kushangaza siku hizi, kwani imekuwa jambao la kawaida kusikia lile gari au ile nyumba au ile bar au lile shamba au lile duka pale nk. ni mali ya Padre fulani,  Sister fulani au Brother fulani. Watu ambao wamekabidhiwa dhamana ya kuchunga kundi la Mungu na kuliongoza salama, sasa wamegeuka na kuanza kuchunga na kuongoza mali zao binafsi! Sasa tujiulize hawa kondoo waliokabidhiwa kwao watakwenda wapi?
Mapadre, wachungaji na hata watawa siku hizi wameamua kufanya biashara na kuanza kujilimbikizia mali kama watu wengine. Mbaya zaidi wengi wanadiriki hata kutumia fedha za Parokia/sadaka za waamini na kuziingiza katika biashara zao/miradi yao binafsi. Lakushangaza kabisa, hata wale watawa ambao wameweka agano na Mungu kwamba watashika ufukara, lakini sasa wamevunja agano hilo/nadhiri/viapo vyao na kuamua kutafuta mali/fedha kwa udi na uvumba.
Hata kama utajidai kuwa hutumii fedha za kanisa katika kuendesha miradi au biashara zako, unapaswa ujiulize kuwa, je hizo fedha ambazo unajidai si za sadaka je umezipata kwa njia ipi? Kumbuka kwamba, waamini au watu mbalimbali wanakupa kitu kutokana na wadhifa wako. Hivyo utumishi wako ndiyo unaokufanya upata hivyo vitu iwe ni fedha au nini. Hivyo basi kwa kuwa unapewa vitu kupitia wadhifa wako, kumbuka kwamba hata vitu hivyo ni mali ya kanisa maana umevipata kupitia kanisa (cheo chako).
Hebu jiulize; je watu wanaotoa sadaka ni watu wa hali gani? Je ni yatima, wajane, walemavu, wazee, vijana, watoto, matajiri au masikini? Kama ni watu wa hali zote unaonaje?
Ole wao wote wanaowadhulumu yatima, wajane, walemavu, wazee, masikini nk. Mungu anamwambia mfalme Daudi;
“Wewe ulifanya jambo hilo kwa siri, lakini mimi nitayafanya haya mbele ya Waisraeli wote hadharani.”
Kama mtakumbuka katika kilele cha maadhimisho ya mwaka wa Mapadre 2010. Sherehe zilizofanyika mjini Dodoma, Mwahadhama Polycarp Kardinali Pengo katika mahubiri yake alikemea kwa nguvu zake zote mambo kama haya. Aliwaambia Mapadre wote kwamba wametumwa kuwatangazia masikini habari njema. “…nawatangazia masikini habari njema lakini kwa kutojua vizuri nitafanya lipi ili nitangaze hiyo habari njema, wameingia katika kutafuta mali kwa kila njia lakini wote tunajua kwamba waliokwenda kwa malengo hayo mwishowe hawakuwasaidia watu masikini nao wenyewe wamemalizika kama masikini, kuliko masikini wale ambao walitegemea wangewasaidia. Kwa hiyo Mapadre, hiyo ni tajriba (experience) ambayo baadhi yetu tunaijua kabisa. Tufanye nini? hatuna lingine ambalo tunaweza kufanya isipokuwa kufuata mfano wake Bwana wetu Yesu Kristo. Ndugu Mapadre hamjasikia na wala hamtasoma mahali popote kwamba, Bwana wetu Yesu Kristo aliingia migodini kwenda kutafuta mali ili awaletee habari njema hawa masikini. Maisha yake mwenyewe yalikuwa ya umasikini wa kukithiri, hana hata pa kulaza kichwa chake. Alitegemea watu wengi…katika kutekeleza jukumu lake, tunamuona anamalizikia msalabani, kifo cha kudhalilika kabisa na bado anang’ang’ania kwamba nimeletwa hapa ili niwahubirie masikini habari njema. Homilia yake ikowapi?!” Pamoja na hayo Mwadhama aliwatia moyo Mapadre wake kwa kuwaambia kwamba; “Tuwatangazie maskini habari njema kwa kuzingatia na kung’ang’ania kabisa malengo ya upadre wetu hata kama watu watasadiki kwamba sisi si wakusikilizwa basi tuendelee kupiga kelele kama ile sauti iliayo nyikani, wasipowasikia watu Bweha watatusikia na mawe yatatusikia”. Kwa mafundisho haya tunaweza kuona jinsi Huruma ya Mungu itakavyokuwa kwao watakao mrudia na kuziacha njia zote za upotofu wa Dunia hii.
Vilevile tunafarijika sana tunapotafakari Upendo wa Mungu, kwani tunaona kuwa Upendo wa Mungu hauna mipaka, na hauwezi kufananishwa na upendo wa aina yoyote ile. Pia tunapata nguvu na matumaini makubwa pale tunapomtazama Bwana wetu Yesu Kristo Msalabani, kwani tunaona jinsi huruma ya Mungu ilivyokuu kwetu sisi kiasi kwamba tunashindwa kueleza kwa maneno. Mfalme Daudi aliliona hili na ndiyo maana aliamua kukimbilia kwake bila kupima ukubwa wa kosa alilotenda.
Hata sisi pamoja na maovu yote tuliyotenda bado Mungu hajachoka kutandaza mikono yake tayari kutupokea na kutukumbatia tena kwa upendo mkuu kama yule baba alivyofanya kwa mwana mpotevu au jinsi Mungu alivyomsamehe Mfalme Daudi. Haya yote yanawezekana ikiwa tu tutafuata nyayo za Mfalme Daudi, yaani kujichunguza na kujirudi huku tukiepuka nafasi zote za dhambi, kisha tuukimbilie mti wa uzima na kuukumbatia kwa mikono yote miwili bila kujibakiza.
Krito…?  

6 comments:

  1. Nimepata mafunzo maridhawa! Endelea kutuelimisha nama ulnavyofanya.

    ReplyDelete
  2. ahsante sana kwa mafundisho msingi kabisa katika maisha yetu

    ReplyDelete
  3. Asante Mufti Chomboz
    Nashukuru kwa mafunzo yako

    ReplyDelete
  4. Nakupa mkono wa tahania kwa mafunzo yako

    ReplyDelete
  5. Mume wangu amerudi!!! Baada ya miaka 1 ya ndoa iliyovunjika, mume wangu aliniacha na watoto wawili na maisha yangu yalivunjika. Nilitaka kuyamaliza, nusura nijiue maana alituacha bila chochote. Nimekuwa nimevunjika kihisia wakati huu wote na maisha yanaonekana kutokuwa na maana. Siku moja mwaminifu, nilipokuwa nikivinjari mtandao, nilikutana na baadhi ya shuhuda kuhusu Dk DAWN. Baadhi ya watu walishuhudia kwamba alimrudisha mpenzi wao wa zamani, wengine walishuhudia kwamba anarejesha tumbo na kuponya magonjwa kwa mimea. Nilipendezwa zaidi na upatanisho na mume wangu, ambao Dk. DAWN aliwezesha kumrudisha mume wangu ndani ya siku 3. Sasa mume wangu amerudi na tumekuwa tukiishi kwa furaha tangu wakati huo. Shukrani zote kwa Dk DAWN. Hapa, ninaacha mawasiliano yake kwa kila mtu. Maana kuna changamoto za aina yoyote,
    Barua pepe ( dawnacuna314@gmail.com )
    Whatsapp: +2349046229159

    ReplyDelete