Saturday, 2 November 2013

FASIHI SIMULIZIFASIHI SIMULIZI NA MASUALA MTAMBUKO YA KIJAMII BARANI AFRIKA HUSUSANI TANZANIA
Katika kujadili mada hii tutaanza na utangulizi ambao utahusisha maana ya fasihi simulizi kupitia wataalamu mbalimbali, chimbuko la fasihi simulizi kwa kutumia nadharia ya ubadilikaji taratibu na kisha maana ya masuala mtambuko katika jamii. Baada ya hapo kitafuata kiini cha mada yetu, ambapo tutaeleza dhima za fasihi simulizi katika jamii ya leo na namna zinavyohusiana na masuala mtambuko ya kijamii na mwisho kabisa kutakuwa na hitimisho na marejeo.
Fasihisi Simulizi imejadiliwa na wataalam mbalimbali miongoni mwa wataalam hao ni:  M.M. Mulokozi (1996) anasema, Fasihi Simulizi ni fasihi inayotungwa au kubuniwa kichwani na kuwasilishwa kwa hadhira kwa njia ya mdomo na vitendo bila kutumia maandishi.

TUKI (2004) Fasihi Simulizi ni kazi ya fasihi inayohifadhiwa na kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine kwa njia ya mdomo kama vile; hadithi, ngoma na vitendawili. 
Hivyo basi Fasihi Simulizi ni fasihi inayotokana na maneno ambayo huzungumzwa, hutolewa au kuimbwa ambapo mtungaji na mwasilishaji hutumia sanaa.
Baada ya kuangalia maana ya fasihi simulizi yafuatayo ni maaelezo kuhusu chimbuko la fasihi simulizi kupitia nadharia ya ubadilikaji taratibu ambayo itathibitisha kauli isemayo kuwa fasihi simulizi ni masalia ya kazi au sanaa za vizazi vya kale.
Kwa mujibu wa Okpewho, (1992) anasema kuwa mwanzilishi wa nadharia hii ni Charles Darwin ambaye anasema kuwa “viumbe hai vyote vimekuwa vikipitia mabadiliko mbalimbali ya muda mrefu hadi kufikia hali hii tuiyonayo sasa”.  Dhana yake hii imeleta ushawishi mkubwa kwa wanataaluma mbalimbali wa fasihi simulizi ambao wanaamini kwamba, fasihi simulizi ni masalia ya zamani au mabaki ya sanaa jadi zilizotangulia kama vile visasili, visakale, ngano, hekaya, methali, nyimbo, vitendawili nk.
Wanaendelea kusema kuwa sanaa hizi zilirithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine na ziliendelea kupoteza uhalisia wake kadri muda ulivyozidi kwenda. Nadharia hii ilitawaliwa na mbinu ya ulinganishi ambapo walijikita zaidi katika kulinganisha fasihi ya jamii moja na nyingine na katika ulinganishaji wao waliangalia zaidi kipengele cha maudhui kuliko kipengele cha fani.
Masuala mtambuko ni mambo yanayojitokeza katika Nyanja mbalimbali za kijamii, kwa mfano magonjwa, rushwa, ufisadi nk. Mfano wa Nyanja hizo ni kama vile siasa, uchumi, utamaduni na jamii kwa ujumla.
Licha ya wanaubadilikaji taratibu kuonesha uhalisia wa fasihi simulizi kuwa ni masalia ya kazi za kale au mabaki ya zamani, hoja hii haimaanishi kwamba fasihi simulizi haina thamani au uamilifu wowote katika jamii ya leo lahasha! Hivyo tunaungana na wanasosholojia ambao wanasisitiza kuwa uamilifu wa fasihi simulizi upo hai ila unabadilika tu kulingana na maendeleo ya jamii husika na dhima zake zinatawala masuala mtambuko kama ifuatavyo:
Kuburudisha; tanzu mbalimbali za fasihi simulizi hutumika kama nyenzo ya burudani katika Nyanja mbalimbali za kijamii. Mfano wa tanzu hizo ni kama vile hadithi, ushairi (nyimbo mbalimbali), semi (methali, vitendawili). Tanzu hizi hutoa burudani katika sehemu mbalimbali, mfano nyimbo, zipo nyimbo ambazo hutumika kutoa burudani katika sehemu mbalimbali kama vile harusini-nyimbo za harusi, nyimbo za nyiso hutoa burudani jandoni na unyagoni. Vilevile katika siasa zipo nyimbo ambazo hutumika kutolea burudani na uhamasishaji wakati wa kampeni za kisiasa. Hivyo basi kutokana na utanzu huu wa nyimbo kutumika kama chombo cha burudani katika Nyanja mbalimbali huonesha dhahiri kuwa ni kwa namna gani fasihi simulizi inavyojitokeza katika masuala mtambuko.
Kuelimisha; kupitia fasihi simulizi jamii hujipatia elimu ambayo huwasaidia kuijua vizuri historia yao, utamaduni, siasa ya nchi yao pamoja na itikadi. Mfano katika historia zipo kazi za fasihi simulizi ambazo huonesha historia, kazi kama utenzi wa Fumo Lyongo, utendi wa Shaka Zulu ambao hutupatia historia na utamaduni wa watu wa Afrika kusini. Pia ndani ya tendi hizo kuna masuala ya uongozi pamoja na siasa. Vilevile zipo methali ambazo huelimisha watu kufanya kazi kwa bidii ili kujiongezea nafasi yao kiuchumi, kwa mfano; “mgaagaa na upwa hali wali mkavu”. Kadhalika katika upande wa afya zipo methali zinazotoa elimu mfano “kinga ni bora kuliko tiba”. Hivyo basi utoaji huo wa elimu katika Nyanja tofauti tofauti huonesha ni kwa namna gani fasihi hii ilivyokuwa inajihusisha na masuala mtambuko ya kijami.
Kuhifadhi historia na utamaduni wa jamii; katika suala hili pia fasihi simulizi haikuwa nyuma kwani zipo kazi mbalimbali ambazo hutumika kama nyenzo kuu na muhimu za kuhifadhia amali za jamii kwa mfano visasili na visakale hutunza historia na utamaduni wa jamii husika, mfano; kisasili cha kibo na mawenzi hutunza historia ya Tanzania kuhusu mlima Kilimanjaro. Pia zipo methali ambazo hutunza utamaduni wa waafrika hususani Tanzania mfano; “Asiyesikia la mkuu huvunjika guu”, methali hii hutunza utamaduni wa kiafrika kuwa wadogo lazima wawasikilize na kuwaheshimu wakubwa. Kadhalika katika siasa kupitia kipera cha lakabu ya baba wa taifa huonesha historia ya kiongozi wa Taifa la Tanzania. Na hivyo ndivyo namna fasihi simulizi inavyojihusisha na masuala mtambuko.
Kuhamasisha umoja na mshikamano; suala hili pia hufanywa na aina hii ya fasihi simulizi katika jamii na hujidhihirisha katika Nyanja mbalimbali kama vile siasa, zipo methali ambazo uhamasisha suala hili:- “Umoja ni nguvu utengano ni udhaifu”, “Kidole kimoja hakivunji chawa”. Kwa upande wa nyimbo zipo pia ambazo huhamasisha suala hili kama vile nyimbo za chapuzo mfano; wawe-kilimo, kimai-uvuvi. Vileveli zipo nyimbo ambazo huhamasisha umoja na mshikamano wakati wa michezo.
Kukuza lugha; fasihi simulizi hujikita pia katika suala hili la ukuzaji lugha kupitia vipera mbalimbali ambavyo hufanyika katika nyanja mbalimbali kwa mfano nyanja ya elimu, vipo vipindi mbalimbali redioni na hata kwenye luninga ambavyo hutumika kufundishia lugha hasa kwa watoto kwa kupitia vipera vya fasihi simulizi kama vile vitendawili na methali, zipo pia chemshabongo na hadithi mbalimbali. Vilevile ipo michezo ya watoto ambayo hukuza lugha kama vile kauli tauria, mfano; “Katibu kata wa kata ya mkata alikataa katakata kukata miti katika kata ya mkata”. katika siasa uibukaji wa misimu mfano, chakachua, ngangari nk. pamoja na nyimbo hasa wakati wa kampeni husaidia kukuza lugha. Pia shughuli mbalimbali za kijamii mfano harusi, misiba kupitia nyimbo za watani pia hutoa mchango mkubwa katika kukuza lugha.
Kuonya na kukosoa jamii zipo tanzu na vipera mbalimbali vya fasihi simulizi ambavyo hujihusisha zaidi na kuiweka jamii katika nafasi iliyobora zaidi. Mfano; kimaadili kuna methali zinazoonesha maadili mema katika jamii mfano; “Samaki mkunje angali mbichi”, “Mkaidi hafaidi mpaka siku ya iddi”. Vilevile kiuchumi zipo methali ambazo huonya na kukosoa wale wote wenye tabia za kivivu katika kujitafutia maisha mfano, “Mtegemea cha ndugu hufa masikini”, “Fanyakazi kama mtumwa uishi kama mfalme”.
Vilevile kuongeza kipato; kupitia fasihi simulizi watu hujiajiri na kujipatia kipato. Kwa mfano; watu hujishughulisha na utanzi wa nyimbo mbalimbali kama vile nyimbo za kisiasa, kiuchumi pamoja na nyimbo za kiutamaduni ambapo kwa namna moja au nyingine huwasaidia katika suala zima la kujipatia kipato na kusukuma mbele gurudumu la maisha kwa ujumla.
Hivyo basi, kutokana na fasihi simulizi kujihusisha na masuala mtambuko katika jamii ya leo ni dhahiri kuwa maendeleo ya sanaa jadi yanapiga hatua na kamwe hayawezi kupotea kabisa, ila tu, upo uwezekano wa kubadilika kulingana na maendeleo ya jamii husika.


MAREJEO:
Mulokozi, M.M. (1996), Utangulizi wa Fasihi Simulizi ya Kiswahili, TUKI, Dar es Salaam.
TUKI, (2004), Kamusi ya Kiswahili Sanifu, (Toleo la Pili), East Africa: Oxford University Press na Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili, (TUKI).
Wamitila K.W. (2010), Kichocheo cha Fasihi Simulizi na Andishi, Nairobi: Focus Publication Ltd.

1 comment: