Sunday, 14 June 2015

NGANOSIFA YA NGANO NI UFUPI PAMOJA NA MUUNDO WA MOJA KWA MOJA. JADILI
Katika kujibu swali hili kwanza itaelezwa maana ya ngano kwa mujibu wa wataalamu mbalimbali, kisha kiini cha swali na mwisho litatolewa hitimisho ambapo tutatoa mapendekezo kuhusu maana ya ngano
Kwa kuanza na maana ya ngano, Hamisi na Madumulla (1989:5) wanaeleza kuwa
Ngano (vigano, hurafa) ni hadithi za kimapokeo zitumiazo wahusika kama wanyama, miti na watu kuelezea au kuonya kuhusu maisha. Utanzu huu unajumuisha fani kadhaa kama vile;
  • a)      Istiara, wakifasili kama hadithi ambayo maana yake ya wazi inawakilisha maana nyingine, iliyofichika (yaani hadithi nzima ni kama sitiari)
  • b)      Mbazi ni hadithi fupi yenye mafunzo itolewayo kama kielelezo wakati wa maongezi au wa kumkanya mtu.
  • c)      Kisa ni hadithi fupi ya kufurahisha kuhusu tukio la kweli.
Fasili hii inaonekana kuwa na udhaifu kwa sababu tunajua kwamba ngano si maelezo ambayo huelezwa bali ni masimulizi ambayo husimulia kuhusu kisa fulani na kupitia simulio hilo ndilo hutupatia maonyo na mafunzo na vilevile huweza kuburudisha.
Kwa mujibu wa Kubo na Wenzake (2011) Ngano ni masimulizi yanayotumia viumbe na vitu vingine visivyo na uhai kama wahusika. Viumbe hivyo ni pamoja na wanyama, mfano Fisi, Tembo, Sungura, Ndege na Wadudu. Wanaendelea kusema kuwa Ngano zinatumia muundo maalumu unaozitofautisha na masimulizi mengine. Vipengele vikuu vya Ngano ni pamoja na:
a) Visasili ni hadithi zinazoeleza kwa nini viumbe tofauti huwa na tabia, maumbile au uhusiano fulani.  Mfano: “sababu ya Mbuni kuwa na shingo ndefu.”
b) Hekaya ni ngano fupi zinazohadithia matukio yanayoonyesha hila, ujanja na hustaajabisha mara kwa mara Mfano: “Abunuwasi na Sufuria”
Abunuwasi alikwenda kwa jirani yake kuazima sufuria za kupikia katika karamu aliyokuwa nayo kwake. Jirani alimpa Abunuwasi sufuria huku akinung’unika, Abunuwasi hakufurahishwa na jinsi jirani yake alivyonung’unika.
Baada ya kuzitumia sufuria, Abunuwasi aliamua kumfunza jirani yake ujirani mwema. Akarejesha sufuria aliyokuwa ameazima, pamoja na nyingine ndogo. Jirani kuuliza kwa nini Abunuwasi amerejesha sufuria mbili badala ya moja aliyomwazima alisema,
“Rafiki yangu, sufuria yako ilikuwa na bahati nzuri, badala ya kuitumia ilipata mtoto ndio maana narejesha sufuria mbili badala ya moja”. Mwenye sufuria alishukuru sana.
Baada ya muda, Abunuwasi alimrudia jirani yake na kumwomba vyombo vya kutumia; jirani naye kwa matarajio ya kuongeza vifaa vya nyumbani, akamwazima Abunuwasi takribani kila kitu alichotaka.
Ilichukua muda mrefu bila kurejeshewa chochote kile, naye akaenda hadi kwa Abunuwasi. Akamkuta Abunuwasi ameshika tama, alimwelezea jirani kuwa:
“Vyombo vyake vilikuwa na bahati mbaya wakati huu kwani vilikufa vyote” Alipodadisi zaidi akamwambia chochote kizaacho bwana hufa, sufuria ilizaa mara ya kwanza, wakati huu vyombo vyako vilipatwa na mkasa vikafa vyote, pole ndugu. Hapo jirani alienda zake kwa kilio kingi.
c) Hurafa ni masimulizi ambayo hutumia wanyama kama wahusika katika kutoa ujumbe wake. Hutumia mbinu ya kuvipa uhai vitu na sifa za kibinadamu vitu ambavyo kwa kawaida havina uhai. Wanyama ambao hutumika sana katika hurufa/ kharafa ni kaka Sungura, Fisi, Mzee kobe, Chura, Ndege na Nyoka.
d) Istiara ni hadithi ya kimafumbo ambayo maana yake haijitokezi moja kwa moja. Maana yake ya wazi inawakilisha maana nyingine isiyokuwa ya wazi, mfano; 
Ngano ya “Msafiri na Ngamia”
Msafiri mmoja aliamua kupumzika kutokana na upepo mkali na vumbi la jangwani. Aliamua kukaa ndani ya hema yake hadi hali hiyo ya hewa ibadilike ndipo aendelee na safari yake.
Ngamia wake pale nje alikumbwa na baridi kali hivyo akaamua kumuomba hifadhi ndani ya hema la bwana wake. “Bwana nakuomba uniruhusu nitie kichwa ndani ya hema
nijiepushe na athari za upepo na mavumbi yaliyoko hapa nje”. Yule msafiri alikataa na kumweleza kuwa haingewezekana kwani hema lilikuwa dogo. Lakini ngamia alimrairai hadi bwana wake alipokubali.
Ngamia alipoona kuwa kichwa chake kiko ndani aliomba aingize shingo yake, akidai kuwa shingo haitachukua nafasi kubwa, naye msafiri alikakubali.
Baadaye akakubaliwa kuingiza hata nundu yake na hatimaye akaingiza wote mzima. Msafiri kutanabahi, alikuwa amerushwa nje, huku ngamia akidai kuwa wasingeweza kuenea pamoja kwani hema lilikuwa dogo. Basi msafiri akaumia nje huku baridi inamzizima ingawa hema lilikuwa lake.
Hali ya hewa ilipobadilika, msafiri alimwambia ngamia kuwa wangeendelea na safari. Baada ya siku kadhaa hali ya hewa ilibadilika, mvua kubwa ikanyesha naye msafiri akatafuta hifadhi ndani ya hema lake. Licha ya kuwa ngamia alimbembeleza angalau aijiepushe na baridi, msafiri alikuwa ameapa kutorudia kosa lake la wali.
Istiara hii inaonya dhidi ya wenyeji kuwaruhusu wageni umiliki mali zao; kama jamii za Kiafrika zilivyofanyiwa na wakoloni wakatwaa ardhi yao.
  • e) Ngano za kijanja ni masimulizi haya huhusu wanyama wadogo wanaotumia ujanja wa hali ya juu ili kujinasua na hali ngumu au mitego waliyotegewa.
  • f) Mbazi hii ni hadithi isiyokuwa ndefu inayotolewa katika maongezi ili kutoa mafunzo yenye uadilifu.
  • g) Ngano za mazimwi ni masimulizi yanayohusu majitu ya ajabu ambayo hudhuru na kumwangamiza binadamu
  • i) Ngano ya mtanziko haya ni masimuluzi ambayo mhusika mkuu anajikuta katika hali ngumu na anashindwa kutoa uamuzi wowote kwa kuwa kila aina ya uamuzi ungemletea athari mbaya.
Katika fasili ya Kubo na Wenzake (2011) inaonekana kueleza Ngano kwa kuegemea kwenye wahusika wanyama na wadudu na viumbe wengine wasiokuwa na uhai hawamuelezei binadamu
kama mhusika mojawapo wa ngano. Tunaona kwamba kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia mhusika binadamu naye aliingizwa katika Ngano.
Wamitila (2003)  anaeleza kuwa Ngano ni hadithi za kimapokeo ambazo huwatumia wahusika wa aina mbalimbali (wanyama , miti ,au  watu) kusimulia  tukio  au kisa fulani chenye mafunzo.
Anaendelea kusema kuwa kuna aina mbalimbali za ngano kama vile:
Ngano za mazimwi, Ngano za usuli, Ngano ya kishujaa, Ngano za hekaya, Ngano za hurafa au wanyama, Ngano za mtanziko, Ngano za kimafumbo (kuna ngano za Istiara, mbazi/vigano, mchapo/ kidahizo), Ngano za kichimba kazi/ kudhubahi na Soga.
Mulokozi (1996) anasema kuwa Ngano ni hadithi za kimapokeo zitumiazo wahusika kama wanyama, mazimwi, miti na watu kuelezea au kuonya kuhusu maisha.
Ikichunguzwa vema fasili hii ya Mulokozi, utaona ina udhaifu kwa sababu ngano kama mojawapo ya kipera cha fasihi simulizi ina dhima ya kuburudisha, kutunza amali za jamii, kuendeleza fani husika na sio kuonya tu. Hii ina maana kwamba mtu akisikiliza ngano au akisoma ngano atapata mafunzo vilevile ataburudika kutokana na ngano hiyo.
Senkoro (2011) anaeleza kuwa Ngano ni utanzu wa kifasihi simulizi ambao ulipitishwa toka kizazi kimoja hadi kingine kwa njia ya mdomo.
Kutokana na fasili ya Senkoro (kishatajwa) kwa sasa fasili hiyo haina mashiko kwa sababu Ngano huweza kuwasilishwa kwa kutazamwa kupitia luninga, kusomwa kwenye vitabu, kusikiliza kupitia vinasa sauti hii ni kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia ambayo ni tofauti na zamani ambapo ilitegemea kupitishwa kwa kutumia mdomo.
Hivyo tunaweza kusema kuwa ngano ni masimulizi ya hadithi za kimapokeo zinazotumia viumbe vyenye uhai na visivyo na uhai kama wahusika mfano; Wanyama kama vile Tembo, Sungura, Kobe na binadamu. Kutokana na aina Ngano zilizoelezwa na wataalamu mbalimbali  tunaweza kuziweka katika makundi makuu matano ambazo ni: Istiara, Mbazi, Hekaya, Mtanziko na Hurafa/kharafa.
Kutokana na swali, ni kweli kukubali kwamba, moja ya sifa zinazotumika kuelezea maana ya ngano ni ufupi pamoja na muundo wa moja kwa moja. Ili kudhibitisha usemi huu kazi hii itatumia sifa mbalimbali za ngano ambazo hutofautisha na tanzu nyingine za fasihi simulizi kama ifuatavyo;
Kwa kuanza na suala la wahusika, tukiangalia katika ngano wahusika wake hawaelezwi kwa undani zaidi bali huchukuliwa kwa kiwango cha jumla jumla ambapo wahusika hao mara nyingi huwa ni wahusika bapa ambao hawabadiliki kuanzia mwanzo wa hadithi hadi mwisho. Mtaalamu Senkoro (2011) anawagawa katika makundi makuu mawili ambayo ni wahusika wema na wahusika wabaya, vilevile anadai kuwa wahusika hawa ni wachache. Hivyo kutokana na maelezo hayo ndiyo yanayotumika kuelezea ufupi wa ngano.
Mfano wa Ngano:
“SHINGO YA MBUNI NA MAMBA” (Wamitila 2004)
Hapo zamani za kale mbuni na mamba walikuwa na urafiki mkubwa sana. Kila wakati mbuni alipokwenda mtoni kunywa maji alisalimiana na rafiki yake mamba kwa mapenzi makubwa. Mbuni alimthamini sana rafiki yake huyo. Ingawa mamba hula wanyama na ndege (akifanikiwa kuwashika) yeye hakuweza kumdhuru rafiki yake mbuni hata siku moja.
Siku moja mamba alisubiri wanyama waje kunywa maji kama kawaida yake kila siku. Yalikuwa mazoea yake kila wajapo kunywa maji, mamba anajificha majini na kusogea hadi walipokuwa wanakunywa maji hayo. Hapo alimrukia mnyama mmoja na kumng’ata kwa meno yake na kumvuta majini kwenda kumlia huko. Baada ya shibe alitoka majini na kijilaza mchangani kuota jua karibu na mto.
Basi siku moja mamba alikuwa na njaa, siku hiyo alitegemea wanyama kama kawaida yake. Lakini kwa bahati mbaya hakuna mnyama hata mmoja aliyekuja kunywa maji. Njaa ya ajabu ilimshika mamba asijue la kufanya. Alipokuwa katika hali hiyo alimwona rafiki  yake mbuni akaja. Sina njia nyingine isipokuwa kumshika mbuni na kumla kuizima njaa iliyonishika. Mbuni alimsogea na kumsalimu rafiki yake kama kawaida. Mbuni alitambua kuwa hakuwa na furaha kama kawaida yake.
‘Rafiki yangu mamba una nini?’ Aliuliza mbuni.
‘Kwa nini?’ Aliuliza mamba kwa sauti ya chini na ya unyonge.
‘Naona huna furaha kabisa’ Alisema mbuni.
‘Nina jino linalonisumbua sana’ Alisema mamba.
‘Jino?’ Aliuliza mbuni kwa msangao mkubwa.
‘Ndiyo, nilikuwa nikisubiri tu uniangalie na kunieleza hali ya jino hilo,’ Alisema mamba
‘Oh! Pole sana. Basi fungua kinywa niangalie’ Alisema mbuni
‘Ndiyo rafiki.  Jino la mwisho kabisa’ Alisema mamba.
Mbuni alikiingiza kichwa chake ndani kuliangalia jino la rafiki yake mamba. Mara tu alipofanya hivyo, mamba alikifumba kile kinywa chake na kuanza kujivuta kurudi majini. Mbuni naye alijitahidi kufurukuta. Alijitahidi kwa nguvu zake zote kujivuta nyuma. Kadiri Mbuni alivyojivuta nyuma ndivyo mamba naye alivyojivuta kuelekea majini kinyumenyume. Mvutano huo uliendelea mpaka kwa bahati mbuni akafanikiwa kufurukuta na kukitoa kichwa chake kwenye kinywa cha mamba. Alitimua mbio na kurudi zake porini. Urafiki wake na mamba uliisha siku hiyo.
Katika Ngano hii tunaelezwa jinsi mbuni na mamba walivyokuwa marafiki na mwisho tunaona wanakuwa maadui kwa sababu mamba hakuwa na urafiki wa kweli kwa mbuni. Hivyo hadithi hii ni fupi kwa sababu ina wahusika wawili ambao ni mbuni na mamba na hawajaelezwa kwa undani zaidi na hiyo ndiyo inayofanya hadithi hii kuwa fupi.
Mandhari pia huweza kufanya hadithi au Ngano kuwa fupi kwa sababu katika Ngano mandhari hayapewi nafasi kubwa ila tu pale ambapo yamehitajika yaongezee undani wa maudhui
(hasa kiishara) ama kwa hakika wakati mwingine hatuelezwi kabisa kuhusu mandhari kwa mujibu wa Senkoro (2011). Mfano wa Ngano.
“MWINDAJI NA BIBI KIZEE” (mfano wa hadithi ya Kiswahili)
Hapo zamani za kale palikuwa na mwindaji ambaye alikuwa na mke na watoto wawili. Siku moja mwindaji akaenda msituni kuwinda, alipofika huko hakufanikiwa kupata nyama aliamua kurudi nyumbani. Siku ya pili aliamka asubuhi na mapema akaenda tena msituni lakini alirudi nyumbani mikono mitupu. Siku ya tatu akaenda tena msituni alipofika alikaa chini ya mti mkubwa akisubiri wanyama.
Mara ghafla akatokea bibi kizee akamuuliza kwa nini yuko pale, Yule mwindaji alimhadithia bibi yule yaliyomsibu. Bibi Yule akampa mwindaji mayai matatu akamwambia aende nyumbani akifika apasue yai moja moja na aombe anachokitaka.
Mwindaji aliyachukua mayai akaenda nyumbani akafanya kama jinsi alivyoelekezwa, Alipasua yai la kwanza akaomba chakula wakala na familia yake wakashiba. Akapasua la pili akaomba nyumba ikatokea, akapasua la tatu akaomba awe na watumishi wakaja. Rafiki yake kuona hivyo akatamani na yeye awe kama mwenzake. Hivyo alimuuliza alivyofanya, yule mtu akamueleza yote aliyofanya.
Rafiki yake naye alifanya hivyo kama alivyoambiwa na yule mtu, naye ilipofika siku ya tatu akapewa mayai na Yule bibi kizee, akarudi nyumbani alipofika akakaa ili afikirie cha kufanya huku ameshikiria yale mayai mkononi. Mara yai moja likaanguka akasema macho yangu, mara mwili mzima akajaa macho, akasema tena macho yote yaondoke mara yakaondoka macho yote akabaki bila macho, akaomba tena naomba macho yangu yarudi mara yakarudi macho yake. Na hadithi yangu ikaishia hapo. Mfano mwingine wa Ngano ni
 Ngano ya “DEGE”  
Hapo zamani za kale waliondokea mtu, mkewe na mtoto wao wa kiume. Watu hao walikuwa na maisha mazuri tu ambayo hayana hitaji lisilokidhiwa. Siku moja, majira ya asubuhi sana, yule mtoto mwanamume alikuwa nje akicheza. Mara hiyo akamwona kipepeo mzuri mmmmmno. Mwenye rangi mzomzo, zilizooana kwa urembo na ulimbo wa ajabu.
Yule mtoto akawa anajaribu kumkamata yule kipepeo kwa kuchupa na kumrukia kama sungura na zabibu. Alichupaaaaaa, akaruka huyooo. Lakini kila akichupa na kuruka, utadhani waliagana na kipepeo yule, kwani kipepeo pia alichupa na kuruka. Mtoto alizidi kuchupa na kuruka, akiwa anamfuatia yule kipepeo. Yakawa ni mashindano ya kuchupa na kuruka. Haooooo! Msitu na nyika, msitu na nyika; hata kushtukia wako mbaliiii! Mtoto hajui mbele wala nyuma, hajui pa kupata njia wala pa kupotelea. Mradi tu alijikuta yuko peke yake, kachoka taabani wa Shaabani, kiu imemkamata kijana, ulimi nje nje kama wa mbwa. Na kipepeo naye nd'o hivo, haonekani tena.
Basi bwana! Kijana wetu huyo alikaa chini ya mti ambao ulikuwa umeambatana na mwamba uliokuwa katikati ya njia kubwa. Akawa anawaza ya nyumbani, lakini afanyeje masikini wa watu. Na jua nalo nd'o hivo linakwenda kama lilivyopangiwa. Njaa imembana, na kiu kimemkamata; afanye nini?
Ghafla, kijana wetu akaona matone yadondokayo kutoka kwenye mwamba. Matone yakazidi kudondoka, makubwa hayoo. Kijana akakurupuka huyoooo! Mbio kama vile kamwona tena yule kipepeo. Akaokota kifuu cha nazi, akayakinga yale matone. Akakinga weee! Hata wakati maji yale yanakaribia kujaa, akaona ayanywe kuituliza ile kiu yake kali. Akaelekeza kifuu chenye maji mdomoni mwake. Lakini, ghafla, likaja dege kubwa hilo! Dege lisilo na mfano. Mbawa zake zilikuwa zikipiga, na upepo karibu umwangushe kijana wetu. Hilooo, likakipiga kile kifuu na kuyamwaga yale maji yooote! Halafu likajiendea zake likimwacha kijana anahaha kwa kiu na woga. Lakini kijana wetu hakukata tamaa. Alikinga mara ya pili; tena akawa ameshikilia kifuu imara zaidi ya mara ya kwanza. Alipojaribu kunywa, lile dege hilooo! Likampokonya kile kifuu tena.
Mara ya tatu yalipotokea yale, kijana akaamua kwenda juu ya mwamba kuona kulikoni huko yanakotokea yale maji.Akapanda, akapanda, akapandaaaa! Halafu hukooo juu kabisa ya ule mwamba, kijana akalikuta joka! Joka joka hasaaa! Limelala utadhania limekufa, ijapokuwa macho yake makubwa kama nazi yalikuwa yakigeukageuka kama ya kinyonga. Kijana hakulikaribia dude lile; bali pale akagundua yalikokuwa yanatoka yale maji. Domo la joka lile lilikuwa wazi, na sumu yalo ikitiririka kama maji mferejini hadi kule chini ya mwamba. Kijana mwili ulimsisimka, moyo ukamchachatika. Alijua.
Ghafla, lile dege likaja tena. Mara hii si kwa kasi kama mwanzo. Masikini kijana wetu. Kule nyumbani wazazi wake wote wawili, wa kuukeni na wa kuumeni walikuwa wakikata roho kwa huzuni ya kumpoteza mtoto wao.
Lile dege likamjia yule mwanamume na kumchukua hangahanga, juu kwa juu. Likawa linampepea mwanamume yule asiungue jua. Lilipaaaaaaa. Halafu ghafla likaanza kushuka. Kijana mwanamume alipoangalia chini akajua kuwa karudishwa nyumbani kwao. Akafurahi, na hadithi yangu ikaishia hapo hapo.
Katika hadithi au Ngano hizi mbili tunaona kwamba mandhari hayapewi nafasi kubwa sana yaani hayaelezwi kwa undani zaidi mandhari yaliyotumiki yameongezea maudhui ili yaweze kueleweka vizuri kwa msomaji hivyo kufanya hadithi hizo kuwa fupi.
Suala la tukio au visa, Ngano mara nyingi hujengeka juu ya tukio moja au matukio mawili na tukio hilo humhusu mhusika mkuu mmoja ambaye hubeba wazo la Ngano husika. Hii husababisha ngano kuwa fupi kwa sababu hakuna mchanganyiko wa visa na matukio kama ilivyo katika riwaya. Mfano wa Ngano:
“PETE”
Paliondokea mtoto wa  mfalme na  mkewe  ambao  walikuwa wakiishi kwa raha.  Siku moja mtoto wa Kifalme aliondoka kwenda msituni kuwinda.  Baada ya muda alitokea ndege na kumnyang'anya pete yake na kukimbia nayo. Yule mtoto alianza kumfukuza yule ndege na kumrai ampe pete yake.
Mkewe alikaa mpaka usiku anamsubiri mumewe hajarudi. Kwa hivyo siku ya pili aliamua kwenda kumtafuta mumewe.  Kwa kuhofia jamaa wa pale wasijue kuwa mumewe hajarudi, aliamua kwenda kuvalia nguo za mumewe na kutoka kwenda kumtafuta. Baada ya kuvalia vizuri alibadilika sana na hakuwa na tofauti na mumewe. Baada ya hapo alimchukua mtumishi wake wa kike na kumvalisha nguo zake za kimalkia.
Alifunga safari na kwenda kumtafuta mumewe. Akaingia msitu na nyika, msitu na nyika, hadi akafika nchi nyingine.  Katika nchi hiyo alikuwepo mfalme ambae alikuwa na mtoto wa kike.  Kwa hivyo Mfalme alimpokea mtoto huyo wa kifalme aliyevalia nguo za mumewe, na katika kipindi chote alichokaa kwa mfalme hakujulikana kuwa ni mwanamke. Kwa hivyo alishughulishwa na kazi zote za kiume.  Siku moja mfalme alimshauri kuwa amuoze mwanawe.  Yule mtoto hakuweza kuipinga amri ya mfamle kwa hivyo alimuitikia na kukubali.  
Baada ya muda kupita, katika bandari ya mfalme kuliingia meli kutoka nchi za nje na mgeni aliyekuja alikuwa ni mumewe.  Baada ya meli kufika kuna bwana mmoja aliteremka na kwenda kuonana na mfalme wa nchi ile, na alimpelekea mfalme zawadi.  Mfalme baadaye alimkabidhi mkewe ili ampe yule mkwe wao vitu vya harusi. Katika vitu hivyo ilikuwamo ile pete ya mumewe. Pale pale yule mwanamke akafurahi sana kujua kuwa mumewe yu hai na ndiye aliyekuja na ile meli.  Ilipofika jioni alimwambia Mfalme kuwa atakwenda pwani kuonana na mgeni. Akaruhusiwa kwenda. Alipofika melini, akamjulisha yule bwana kuwa yeye ndiye mkewe. Akamueleza mkasa uliomkabili kwa mfalme wa kuozwa mtoto wa mfalme na hali yeye ni mwanamke.
Kwa hivyo alimshauri mumewe kuwa akubali yeye kuoa.  Kwa hivyo pale mipango ya harusi ilipangwa na kuamuliwa kuwa yeye atahudhuria siku ya harusi hiyo.
Siku ya harusi ilipowadia, walialikwa wageni wa kila aina.  Sasa wakati wa kuoa ni tayari, na baraza la mfalme limeshakutanika pamoja. Kadhi wapo tayari kwa kushuhudia harusi. Ndipo yule mwanamke aliposimama na kumtaka radhi mfamle kwa kumwambia, "Saydina Mfalme, napenda kukujulisha mbele ya raia zako kuwa mimi nilikubali kumuoa mwanao kutokana na usalama wangu na pia kuweza kumaliza shughuli ambazo nimezikusudia katika kupeleleza wapi nitampata mume wangu. Lakini Bwana mfamle mimi ni mwanamke na huyu bwana ambaye alikuletea zawadi ndie mume wangu. Na katika zawadi ndimo nimeikuta pete yake iliyonijulisha kuwa yu hai.  Leo ni mwisho wa msako wangu. Sasa kwa vile shughuli imeshapangwa, kwa hivyo hatuwezi kuivunja." 
Wakati huo, watu wote wamepigwa na mshangao na vinywa wazi na kuruhusu nzi wapenye na kupita.  Yule bibi aliendelea, "Kwa hivyo kwa radhi yangu nakubali mwanao aolewe na mume wangu." 
Watu walizidi kushangaa kwa yule mwanamke alivyokuwa jasiri kwa kuwa tayari kumtoa mumewe.  Mfalme alikubali kuwa mwanawe aolewe na yule bwana na alimshukuru na kumsifu
kwa kukubali kumtoa mumewe. Kwa hivyo mfalme alimuoza na kutangaza rasmi kuwa yule bwana atakuwa mfalme wa nchi ile na wataishi pale pamoja na wakeze.
Katika hadithi hii tunaona kuwa kuna tukio moja tu ambalo linahusu kutafutwa kwa pete iliyopotea. Hivyo kuwepo kwa tukio moja kumefanya ngano hiyo kuwa fupi.
Suala la muundo wa ngano ni wa moja kwa moja kama ambavyo wataalamu wengi wanaeleza mmoja wao ni Senkoro(2011) anasema kuwa Ngano huwa na muundo wa moja kwa moja kwa sababu mara nyingi huanza na kitangulizi kama:
“Paukwa”……..’Pakawa’- ‘kaondokea chenjagaa, kajenga nyumba kaka, mwanangu Mwana siti, kijino kama chikichi cha kujengea kikuta, na vilango vya kupita- Hapo kale alikuwako……”
Au
    “Atokeani”
    “Naam Twaibu!”
    “Atokeani!”
    “Naam Twaibu!”
   “Kaondokea Chenjagaa…”
Katikati
Habari yote huelezwa kwa kifupi kwa kusimulia mambo muhimu tu. Mfano; kukua, kuoa au kuolewa.
Mwisho
Kuishi raha mstarehe au kufa au hadithi yangu inaishia hapo, ndiyo miisho ya kawaida. Katika kufafanua zaidi ni kwamba simuliazi za ngano nyingi hazirejelei matukio mengine bali huwa ni tukio moja tu ambalo huelezwa kuanzia mwazo hadi mwisho.
Mfano: Ngano  
 “KAZI KWA MFALME”
Alikuwepo mtu na mkewe na watoto wao wawili.  Kutokana na hali ya maisha waliyonayo mtoto mkubwa aliamua kuondoka kwenda kutafuta kazi. Aliambiwa na watu kwamba kwa Mfalme kuna kazi, lakini kuna masharti yake, pindi ukishindwa utafungwa na ukimshinda mfalme atavua kilemba chake.  Masharti yenyewe ni: Mfalme atatoa vitandawili vyake uvijibu na wewe utowe vyako avijibu.
Siku ilipowadia mtoto alifika kwa mfalme na akapewa masharti na akayakubali.  Mtoto akaanza kutoa vitandawili vyake vikajibiwa vyote, zamu ya mfalme mtoto akashindwa na akapelekwa kufungwa.
Siku zilipita mtoto wa pili naye akaamua kumtafuta kaka yake. Alipita njia ile ile na kupewa masharti yale yale.  Alishindwa na akafungwa.
Mama yao alijaaliwa kupata mtoto wa mwisho na kila siku mtoto yule akifanya kosa mama yake husema, "Wawili wamepotea na kwa hiyo si kitu."
Yule mtoto yalimuingia ndani ya kichwa maneno yale, akamuuliza baba yake. Baba yake akamwambia, "Nenda kamuulize mama yako!"  Mama alimuhadithia yote yale. Mtoto akasema "Kesho kutwa nitakwenda kuwatafuta."  Mama alimkubalia, lakini baada ya kukaa na mumewe wakashauriana wakaona bora mtoto afe pale pale kuliko kufa kama walivyokufa wenziwe. Mtoto aliendelea kuwasihi mpaka wakamkubalia.
Siku ilipowadia mtoto alifunga mizigo yake tayari ili asubuhi sana aanze safari. Wakati amelala mtoto alioteshwa kuwa mama yake anataka kumuuwa, ameweka kisu ili akenda kumuaga amchome nacho.  Usiku ule ule aliamka na kuchonga kisu cha mbao na kukibadili na kile ambacho mama yake angeweza kumuuwa nacho. Kile kisu hasa akakichukua yeye.
Asubuhi alikwenda kumuaga. Alipogeuka nyuma mama alichukua kisu akamrushia, mtoto aligeuka nyuma na kumuuliza mama yake, "Nini hicho"?  Mama alisema "Ah nilikuwa nikijaribu tu sababu baba yako eti anataka kwenda kuwinda". Mtoto kuona vile akavunja safari akamwambia mama yake kuwa safari itakuwa kesho yake.
Ilipofika usiku alioteshwa tena mama yake kaweka mshale, alikwenda akauondowa na akauweka wa mbao.  Alipokwenda kumuaga alfajiri alimrushia nao, alipogeuka alimueleza maneno yale yale, na mtoto alivunja tena safari. Ikawa siku iliyofuatia usingizini alioteshwa tena, lakini hakujua kuna nini. Alipoamka alimuaga mama na baba yake. Alipewa chai na mkate na maandazi. Akanywa na kula, na mengine akafungiwa, mlikuwa mna maandazi yenye sumu.
Alianza safari yake ya kutwa nzima. Aliposikia njaa alitoa andazi lile lenye sumu, alitokea paka ikawa analia sana akamkatia andazi akampa, wakati paka anakula andazi yule mtoto anamtizama. Mara paka akawa anapepesuka; na mara akafa pale pale. Akatokea mbwa nae
akamla paka.  Mbwa baada ya muda akafa. Wakaja nguruwe watatu, wakamla mbwa nao wakafa. Wakaja wasasi sita nao wakakatiana nguruwe. Watu wawili wakachoma wakala wakafa.
Mambo yote yale mtoto anayatizama akachukua mikuki yao yote sita na like andazi kipande akenda zake. Alikwenda hadi alipofika kwa mfalme.  Mfalme alimueleza yale yale aliyowaeleza kaka zake na alikubali.  Mfalme alitoa vitandawili vyake vitatu na mtoto akavijibu. 
Zamu ikafika kwa mtoto.  Alikumbuka yaliyomtokea, na baadaye akasema, “Kitandawili!"
Akajibiwa, "Tega!"
"Nusu imeuwa moja, moja imeuwa tatu, tatu imeuwa sita”. Mfalme akawaza, hakujuwa la kumjibu. Hivyo alishindwa, na akavua kilemba chake akampa yule mtoto. Mtoto akashika ufalme na akawafungua ndugu zake pamoja na wote waliofungwa.  Mfalme mpya alikaa na kaka zake kwa raha zote.
Katika ngano hiyo muundo uliotumika ni muundo wa moja kwa moja ambapo tunaona jinsi kijana alivyopanga safari yake ijapokuwa kulikuwa na vikwazo vya kila aina lakini alifanikiwa kusafiri na kufika kwa mfalme na aliposhinda tunaona kuwa alikabidhiwa kuwa mfalme wa nchi hiyo.
Licha ya kuwa wataalamu wengi wanatumia kigezo cha ufupi na muundo wa moja kwa moja katika kuelezea maana ya ngano. Tunaona  kwamba wanaeleza hivyo ama kwa kutumia idadi ya kurasa, muda mfupi wa kusimulia Ngano au kwa kutumia vigezo tulivyoainisha.  
Hivyo kigezo cha ufupi wa ngano na muundo wa moja kwa moja katika kuelezea maana ya ngano kwa hakika kigezo hicho kina udhaifu kwa sababu ukichunguza kwa makini utagundua kuwa ngano si fupi bali ni ndefu, kwa sababu husimulia mambo mengi ijapokuwa huwa yamefumbwa sana au huelezwa kwa kutumia mafumbo ambayo huwa katika sitiari na lugha ya picha au ya kitaswira, hivyo ukifumbua taswira au sitiari hizo basi Ngano hiyo huwa ni ndefu.
Kwa kifupi tunaweza kusema kuwa urefu wa ngano umejificha katika usitiari na taswira zinazotumika katika kufupisha ngano. Kwa mfano ngano ikirejelewa maana inayopatikana katika ngano ya “Msafiri na Ngamia” utaona kuna ufupi mkubwa sana wa mawazo kutokana na
masimulizi yalivyowekwa kisitiari na kipicha zaidi, lakini maana ya ngano hii ni ndefu kuliko inavyosumiliwa.  
Istiara hii inaonya dhidi ya wenyeji kuwaruhusu wageni umiliki mali zao; kama jamii za kiafrika zilivyofanyiwa na wakoloni wakatwaa ardhi yake.
Katika ngano hiyo msimuliaji amefupisha ngano hiyo kwa kutumia sitiari ambapo tunaona kwamba Ngamia katika ngano hiyo ni wazungu waliokuwa wakoloni ambao walipokuja kutawala Afrika walimnyang’anya kila kitu Mwafrika kwa kumhaidi kuwa atapata vitu vingi lakini baada ya kuvipata walimnyanyasa, na Msafiri katika ngano hii ni Mwafrika ambaye anakubali kurubuniwa. Hivyo ngano hii ikisimuliwa itakuwa ndefu sana na sio kama inavyosimuliwa hapo juu.
Suala la muundo wa moja kwa moja, zikitazamwa baadhi ya ngano hazina muundo wa moja kwa moja, ili kuelewa ngano kama hiyo inabidi urejelee kipengele fulani katika ngano hiyo. Vilevile ili kuweza kugundua kuwa ngano zina muundo changamano inapaswa tuangalie muundo wa ndani wa ngano husika kwa kuchambua mawazo yaliyomo ndani, taswira zilizotumika au lugha ya picha iliyotumika ndipo tutagundua kuwa ngano zina muundo changamano. Mfano:
Ngano ya “MWANAMKE MGANGA WA MACHO
Hapo kale, palikuwa na mwanamke mmoja na mumewe, pamoja na rafiki yao wa kiume. Mwanamke huyo akakaa vizuri na mumewe na wakipendana sana na vile vile kumpenda Yule rafiki wa mumewe kwa kuona kuwa akimkera atakuwa kama alimkera mumewe. Sasa Yule bwana kazi yake ilikuwa ni biashara. Akitoka, siku nyengine hukaa mwezi hajarudi na kumuacha mkewe na yule rafiki yake kwa kuona kuwa yeye ndiye atayemaliza matatizo ya bibi yake. Na vile vile kama akiondoka humuachia mkewe mahitaji yote ibakie mengine madogo madogo tuu.
Basi siku hiyo yule bwana akondoka na hakurudi kwa siku nyingi sana. Basi Yule rafiki yake akaanza kubadilika roho, akawa amtaka yule mwanamke. Yule mwanamke akashangaa sana kusikia maneno aambiwayo na yule rafiki. Na hakusita kukataa katakata na kumwambia kuwa yeye hangeweza kufanya hivyo kwa sababu haielekei na anamuogopa mwenyezi Mungu. Yule mtu akawa hasikii, kila siku ampa maneno haya na yale, lakini mwanamke hakusita kukataa kwakuona si jambo zuri.
Hata siku hiyo akaona afanye mbinu ili ampate. Akenda asubuhi mbio na kumwambiwa ‘Ililetwa habari mumeo kaanguka msitu fulani. Sijui kama yuko hai kwa sababu yasemekana kuwa msitu huo una wanyama wabaya.
Bila kujua au kuona kuwa anamdanganya, bibi wa watu akavaa kanga wakapanda farasi wao kuelekea kokote kule alikoongozwa na Yule rafiki wa mumewe, wakaenda, wakaenda, wakaenda akaona hawafiki tu. Ikawa wapita misitu kwa misitu. Hata hukoooo, Yule bibi akamuuliza yule mwanamme. Naona usiku unaingia tena farasi kashachoka sana na hatujafika. Ni umbali gani tokea hapa?
Mwanamke  akamjibu “ sasa hivi tutafika. Tutafika tu Tutafanyaje na mumeo ndio hatumjui hali aliyo nayo?”
Waenda, wakaenda usiku ukaingia, wenda tuu. Hata farasi akawa hawezi tena kwenda kwa sababu ya giza wakashuka wakalala pale chini. Basi Yule mwanamme akaanza kumpasha Yule bibi, akamwabia. Hivyo siku zote hizi kukutaka ukawa hutaki kwa nini? Basi hakuna mume hakuna nini. Ni miye ndiye niliye na haja nawe. Sasa uhodari wako ushakwisha.
Basi yule bibi akawa hana la kufanya usiku ule akabaki kulia tu, lakini iwe nini?  Hapakuwa na mji wowote karibu nao angalau aweze kupita ntu akamsikia. Mambo yakawa ni kutapatapa tu. Yule  bwana akatimiza haja yake. Akamuacha yule bibi yu hoi hana fahamu. Yule mwanamme akaanza kurudi peke yake bila farasi. Farasi akamucha akaenda atakako na bibi chini.
Yule bibi alipata fahamu zake, asubuhi kweupe na kujiona yu pweke msitu ule mkubwa. Akajikokota kokota kwa sababu alikuwa kaumia kifua. Hata kufika mbele kidogo akawakuta watu wawili wanawinda. Kumbe ni tajiri mmoja mkubwa sana pamoja na mtumishi wake. Yule bibi akawapigia kelele akisema, “Enyi watu , nipatieni msaada! Nisaidieni, sijui niendako, wala Nitokako!”.
Yule tajiri aliposikia vile akaifuatilia sauti mpaka akamuona Yule bibi. Hapo akamuuliza maswali na mwanamke akajibu yote. Ndipo alipoamua kumuchukua kwake ili awe mkewe kwa vile atokako hakujui.
Basi yule bibi waliishi kwa furaha na yule tajiri lakini Yule mtumishi alianza kumtaka kama Yule rafiki yake mume wake. Yule bibi hakusita kukataa katakata, Baada ya kukataa yule mtumishi alimfanya yule bibi kama alivyofanywa na rafiki yake mume wake. Bibi yule aliamua kuondoka akaenda, akaenda hata akaona mji akaingia katika ule mji akabadilisha nguo na akavaa nguo za kiume.
Bibi yule akawa mganga wa macho, yule tajiri aliposikia kuwa katika mji ule kuna mganga wa macho aliamua kumpeleka mtumishi wake kwa yule mganga. Bibi yule alimwambia mtumishi  aeleze kisa chote kilichompata hadi akawa kipofu akaambiwa asiposema atakuwa kipofu milele yote. Yule mtumishi kusikia hivyo aliamua kusema kisa chote na yule bibi akamtibu.
Yule mume wake bibi alirejea kutoka safari akamkuta rafiki yake ni kipofu alipomuuliza mke wake alikokwenda alisema hajui kwa sababu haoni. Yule bwana aliumia sana kwa sababu walikuwa wakipendana na mke wake. Bwana yule aliamua kumtunza rafiki yake bila kujua kuwa ndiye aliyesababisha mke wake aondoke.
Basi yule bwana aliposikia kuna mganga wa macho aliamua kumpeleka rafiki yake naye alipofika aliambiwa aeleze kisa chote. Alipokuwa akieleza yule bwana alikuwa akisikitika sana. Baada ya kueleza yule bibi akamuuliza huyo mtu uliyemfanyia hivyo ukimuona utamfahamu, akajibu ndiyo, Yule bibi akavua zile nguo akamwambia mume wake ndo mimi mke wako.
Yule bwana alikasirika akasema atampa rafiki yake adhabu baada ya siku tatu, lakini yule rafiki yake alijiua siku ya tatu kabla ya hukumu. Yule tajiri naye alimuua yule mtumishi wake. Yule bwana na bibi yule wakaishi raha mstarehe.
Katika hadithi hii tunaona kwamba kuna urejeshi ambao ulikuwa ukifanywa na msimulizi ili kuelewa kisa kizima inabidi urejelee nyuma. Mfano kuna urejeshi ulifanywa na bibi ambapo alikuwa akimueleza tajiri kuhusu mambo yaliyompata.
Kutokana na maelezo hayo tunasema kuwa sifa ya ufupi na muundo wa moja kwa moja haitoshi katika kuelezea maana ya ngano kwa sababu kuna ngano nyingine zina muundo changamano na ngano si fupi kama watalaamu wengi wanavyodai bali ni ndefu. Hivyo unahitajika utafiti zaidi ili kuweza kueleza maana ya ngano kwa usahihi na si kuegemea upande mmoja.

 MAREJEO
Kubo M na wenzake (2011), Mwanaza Wa Fasihi simulizi.The National Education Services.Nairobi.
Khamis A.M na  J.S Madulla (1989), Mulika no; 21.Tuki. Dar ses salaam.
Mulokozi M.M (1996), Fasihi Ya Kiswahili. Chuo Kikuu  Huria Cha Tanzania. Dar es salaam.
Senkoro F.E.M.K (2011). Fasihi, Mfululizo wa lugha na Fasihi. KAUTTU. Dar es salaam.
Senkoro, F.E.M.K. (1996) "The Significance of the Journey Motif in Folktales from Zanzibar". Tasinifu ya Uzamivu, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Wamitila K.W. (2004), Kichocheo Cha Fasihi Simulizi na Fasihi Andishi.English press. Nairobi.


               


1 comment:

  1. kazi nzuri sana. ila ingependeza kutueleza muundo wa ngano

    ReplyDelete