Sunday, 8 December 2013

FONOLOJIA YA KISWAHILI

FONOLOJIA YA KISWAHILI
UTANGULIZI
USULI WA TAALUMA YA FONOLOJIA
Neno fonolojia linatokana na maneno mawili ya Kigiriki phone-sauti za kusemwa na logos- taaluma/mtalaa. Masimulizi yanadai kuwa taaluma hii ilianza zamani sana kati ya mwaka
460 kabla ya Masihia huko India ya kale, ambapo mtu aliyeitwa Panini, na ambaye huaminika kuwa ni baba wa isimu aliandika kuhusu fonolojia ya Kisansikriti katika matini aliyoiita Shiva Sutras. Ni katika andiko hili ndipo alipobainisha kuwepo kwa dhana ambazo leo hii hujulikana kama fonimu, mofimu na mzizi.

Baada ya andiko hilo, habari za taaluma ya fonolojia ni kama zilipotea kabisa katika uwanja wa isimu hadi ilipofika karne ya 19 ambapo wanaisimu wengine waliibuka na kuzungumzia upya masuala ya fonolojia. Miongoni mwa wanaisimu wa mwanzo
wanaotajwa kujihusisha na fonolojia ni Mpolandi "Jan Baudouin de Courtenay" , (pamoja na mwanafunzi wake wa zamani "Mikołaj Kruszewski" alipobuni neno fonimu mnamo mwaka 1876, na kazi yake, ijapokuwa hairejelewi sana, inachukuliwa kuwa ni mwanzo wa fonolojia mamboleo. Mwanaisimu huyu si tu alishughulikia nadharia ya fonimu, bali pia vighairi vya kifonetiki (ambavyo leo huitwa alofoni na mofofonolojia). Maandishi ya Panini (Sarufi ya Kisanskriti) pamoja na Jan Baudouin de Courtenay yalikuja kuwa na athari kubwa kwa anayeaminika kuwa baba wa nadharia ya Umuundo Mamboleo, Ferdinand de Saussure, ambaye pia alikuwa ni profesa wa Sansikriti.

Wanaisimu wote hawa walikuwa wanajaribu kulinganisha sauti za lugha za Asia Mashariki na za Ulaya, lengo lao likiwa ni kujua mizizi ya lugha zilizoitwa India-Ulaya. Kutokana na mkabala huo, katika kipindi hicho isimu ilikuwa Isimu-linganishi tu. Kutokana na tafiti zao hizo waliweza kupata maneno yenye sauti na maana zilizolingana, kufanana au kukaribiana. Utafiti huo uliweza kugundua jamii mbili za lugha ambazo ni jamii ya lugha za Kirumi na jamii ya lugha za Kijerumani. Baadhi ya wanaisimu mahususi kabisa wanaokumbukwa kuchangia katika maendeleo ya fonolojia ni pamoja na:
(i) Jan Baudouin de Courtenay (1845-1929)
Kama ilivyoelezwa hapo awali, huyu ni mwanaisimu aliyebuni dhana za foni na fonimu. Katika nadharia yake, alidai kuwa sauti za mwanadamu ni za aina mbili—foni na fonimu.  Alisema kuwa foni ni sauti za kutamkwa tu lakini fonimu ni sauti za lugha. Hata hivyo, de Courtenay hakutumia istilahi za foni na fonimu (kama zinavyotajwa sasa) bali alitumia istilahi za anthrophonics—foni na psychophonics—fonimu. Yeye alidai kuwa foni zipo karibu sana na taaluma ya kumuelewa binadamu pamoja na alasauti zake ambazo kwa hakika hutofautiana sana na za wanyama wengine. Na kuhusu fonimu, alidai kuwa zinahusu kumwelewa binadamu pamoja na akili zake na namna anavyofikiri katika akili yake. Alidai kuwa, mara nyingi, binadamu hupokea kinachotamkwa na kufasiliwa.
(ii) Ferdinand de Saussure (1887-1913)
Ni mwanaisimu wa Kiswisi anayejulikana kama baba wa isimu kutokana na mchango wake alioutoa katika taaluma hii. Yeye anakumbukwa zaidi kutokana na uwezo wake wa kutofautisha dhana alizoziita langue—mfumo wa lugha mahsusi na parole—matamshi ya mzungumzaji wa lugha husika. Langage hufafanuliwa kuwa ni uwezo alionao mzungumzaji wa lugha mahususi wa kuzungumza na kuelewa matamshi ya mzungumzaji mwingine wa lugha hiyohiyo. Ni sehemu ya lugha inayowakilisha maarifa kati ya sauti na alama. Ni mfumo wa alama kwa maana ya kiufundi tu. Dai lake la msingi ni kuwa alama inategemea vitu viwili—kitaja na kitajwa—hivyo ili mawasiliano yafanyike, mfumo wa ishara lazima ufahamike na ukubaliwe na wanajamii wote.
Kwa upande wa parole, anadai kuwa ni matendo uneni. Ni namna lugha inavyotamkwa katika hali halisi na mtu mmoja mmoja. Dhana ya parole inalingana na dhana ya performance (utendi) ya Noam Chomsky. Katika lugha, parole ni matamshi tofauti ya sauti moja—alofoni. Wanaisimu wanaonekana kukubaliana na madai ya Saussure kwakuwa inaelekea kuthibitika kuwa hakuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya kitaja na kitajwa [alama (lugha) na kinachowakilishwa (masilugha)], bali makubaliano baina ya wazungumzaji wa lugha moja husika ndiyo hutawala.
(iii) Nikolai Trubetzkoy (1890-1939)
Ni miongoni mwa waanzilishi wa taaluma ya fonolojia akichota mizizi ya taaluma ya isimu kutoka katika Skuli ya Prague. Mwanaisimu huyu aliandika misingi ya fonolojia kwa kutumia maarifa yaliyoibuliwa na Ferdinand de Saussure. Ni mtaalamu wa kwanza kufasili dhana ya fonimu. Aliandika vitabu vingi kwa lugha ya Kijerumani, miongoni mwake ni Grundzüge der Phonologie (Principles of Phonology, 1939), ambapo ni katika kitabu hicho ndimo alimotoa fasili ya fonimu pamoja na kubainisha tofauti baina ya fonetiki na fonolojia.
(iv) Noam Chomsky (1928-)
Huyu ni mwanaisimu wa Kimarekani anayevuma sana kwa mchango wake katika taaluma ya isimu kwa ujumla. Dhana za competence (umilisi) na perfomance (utendi) zimemfanya awe maarufu ulimwenguni. Dhana hizi zinaelezea tofauti baina ya maarifa na udhihirishaji wa maarifa hayo ya mtumiaji wa lugha. Katika fonolojia, Chomsky anakumbukwa kwa ufafanuzi wake wa dhana ya fonimu kwa mtazamo wa kisaikolojia. Anapochunguza dhana hii, hudai kuwa fonimu ni tukio la kisaikolojia, hivyo fonimu zimo kichwani mwa mzungumzaji wa lugha.
(v) Daniel Jones (1881-1967)
Ni mwanafonetiki kinara na maarufu kabisa katika nusu ya kwanza ya karne ya ishirini. Ni Mwingereza msomi ambaye alikuwa na shahada ya kwanza ya hisabati na shahada ya mahiri ya sheria, shahada ambazo hata hivyo, hakuwahi kuzitumia. Baadae, alisomea lugha na kuhitimu shahada ya uzamivu. Daniel Jones alifunzwa fonetiki na maprofesa mbalimbali, japokuwa aliathiriwa zaidi na Paul Passy na Henry Sweet. Hamu yake kuu ilikua kwenye nadharia ya fonetiki. Anafahamika zaidi kwa ufafanuzi wa dhana ya fonimu kwa mtazamo wa kifonetiki (ufafanuzi wake tutauchunguza katika sehemu ya mitazamo ya dhana ya fonimu).      
FONETIKI NA FONOLOJIA
Fasili ya taaluma ya fonolojia haiwezi kukamilika, na pengine kueleweka, iwapo hakuna linalosemwa kuhusiana na taaluma ya fonetiki. Hali hii inatokana na ukweli kuwa kuna uhusiano wa kinasaba kati ya fonolojia na fonetiki. Massamba na wenzake (2004:5) wananeneleza ukweli huu kwamba:
…fonetiki na fonolojia ni matawi mawili tofauti ya isimu lakini yenye kuhusiana sana. Uhusiano wa matawi haya unatokana na ukweli kwamba yote mawili yanajihusisha na uchunguzi na uchambuzi unaohusu sauti za lugha za binadamu.
Kutokana na ukweli huu, jitihada za kufasili dhana ya fonolojia inaelekea kuwa nyepesi, dhana hizi mbili zinapofasiliwa kwa mlinganyo. Tuanze na fonetiki:
FONETIKI NI NINI?
Fonetiki ni tawi la isimu linalochunguza sauti za kutamkwa na binadamu ambazo huweza kutumika katika lugha asilia. Massamba na wenzake (kama hapo juu) wanafasili fonetiki kuwa ni tawi la isimu linalohusika na uchunguzi na uchambuzi wa taratibu za utoaji, utamkaji, usafirishaji, usikiaji, na ufasili wa sauti za lugha za binadamu kwa ujumla. Wanasisitiza kwamba, kinachochunguzwa katika fonetiki ni [maumbo] mbalimbali ya sauti zinazoweza kutolewa na alasuti za binadamu (yaani sauti za binadamu zinazotamkwa tu). Kipashio cha msingi cha uchambuzi wa kifonetiki ni foni.
Foni ni sauti yoyote inayotamkwa na binadamu na inayoweza kutumika katika lugha fulani. Hivyo basi, foni ni nyingi sana na hazina maana yoyote. Wanafonetiki hudai kuwa foni zimo katika bohari la sauti (dhana dhahania) ambalo kila lugha huchota sauti chache tu ambazo hutumika katika lugha mahususi. Sauti chache zinazoteuliwa na lugha mahususi kutoka katika bohari la sauti huitwa fonimu.
Matawi ya Fonetiki: Kuna mitazamo miwili tofauti kuhusiana na matawi ya fonetiki. Mtazamo wa kwanza ni unaodai kuwepo matawi matatu; na mtazamo wa pili ni unaodai kuwepo matawi manne. Mtazamo wa kuwepo matawi matatu unataja fonetiki matamshi, fonetiki akustika, na fonetiki masikizi. Mtazamo wa kuwepo matawi manne (kama Massamba na wenzake (kama hapo juu), pamoja na matawi tuliyokwisha yataja, wanongezea tawi fonetiki tibamatamshi.
Fonetiki matamshi huchunguza jinsi sauti za lugha zinavyotamkwa kwa kutumia alasauti. Hususani, huchunguza namna na mahali pa kutamkia sauti husika. Fonetiki akustika huchunguza jinsi mawimbi ya sauti yanavyosafiri kutoka katika kinywa cha mtamkaji hadi kufika katika sikio la msikilizaji. Fonetiki masikizi hujihusisha na mchakato wa ufasili wa sauti za lugha, hususani uhusiano uliopo baina ya neva za sikio na za ubongo. Na fonetiki tibamatamshi ni tawi jipya lililozuka mwanzoni mwa karne hii, ambalo huchunguza matatizo ya utamkaji ambayo binadamu huweza kuzaliwa nayo au kuyapata baada ya kuzaliwa. Ni tawi linalojaribu kutumia mbinu za kitabibu kuchunguza matatizo na kutafuta namna ya kuyatatua.
FONOLOJIA NI NINI?
Fonolojia ni taaluma ya isimu inayochunguza mifumo ya sauti za kutamkwa zinazotumika katika lugha asilia mahususi za binadamu. Inapolinganishwa na fonetiki, inasisitizwa kuwa fonolojia ni tawi la isimu linalochunguza mifumo ya sauti za lugha mahususi tu, kama vile sauti za Kiswahili, Kiingereza, Kigogo, n.k. Hata hivyo, wapo wanaisimu wanaoelekea kukubaliana kuwa kuna fonetiki ya lugha mahususi pia, na kuna fonolojia ya jumla, na fonetiki ya lugha mahususi. Mathalani, Massamba (1996) licha ya kufasili fonolojia kuwa ni taaluma ya isimu inayochunguza mfumo wa sauti za lugha mahususi, anaenda mbele zaidi na kudai kuwa fonolojia inaweza kuchunguza sauti kwa ujumla wake bila kuzihusisha na lugha mahususi.
Akmajian na wenzake (2001), nao wanadokeza msimamo kama wa Massamba wanapodai kwamba fonolojia inaweza kuchunguzwa kwa mitazamo miwili tofauti. Kwanza, fonolojia kama tawi dogo la isimu linalochunguza mfumo na ruwaza za sauti za lugha mahususi ya binadamu; na pili, fonolojia kama sehemu ya nadharia ya jumla ya lugha ya binadamu inayohusika na tabia za jumla za mfumo wa sauti za lugha asilia za binadamu. Katika mhadhara huu, hata hivyo, tutakuwa wafuasi wa mtazamo unaoona kuwa fonolojia ni tawi la isimu linaloshughulikia mfumo wa sauti za lugha mahususi, hivyo tuna, kwa mfano, fonolojia ya Kiswahili, fonolojia ya Kiingereza, fonolojia ya Kiha, fonolojia ya Kihehe, na fonolojia ya Kibena. Kipashio cha msingi cha fonolojia ni fonimu.
FONIMU
Ni kipashio kidogo kabisa cha kifonolojia kinachoweza kubadili maana ya neno. Hivyo basi, fonimu ina maana, kwakuwa inaweza kubadili maana ya neno inapobadilishwa nafasi katika neno husika. Foni chache zilizoteuliwa kutoka katika bohari la sauti ili zitumike kwenye mfumo wa sauti za lugha mahususi ndiyo fonimu. Hivyo, fonimu ni chache ikilinganishwa na foni. Idadi ya fonimu za lugha hutofautiana kati ya lugha moja na nyingine. Mathalani, Kiarabu kina fonimu ishirini na nane (28), Kiswahili kina fonimu thelathini (30), Kifaransa kina fonimu thelathini na tatu (33), na Kiingereza kina fonimu arobaini na nne (44). Sauti ambayo huweza kubadilishwa nafasi yake katika neno lakini maana ikabaki ileile huitwa alofoni.
Alofoni ni kipashio cha kifonolojia kinachotaja hali ambapo fonimu moja hutamkwa na kuandikwa tofautitofauti bila kubadili maana ya neno. Mfano:
Fedha na feza

Sasa na thatha

Heri na kheri
Kwa kifupi, alofoni ni matamshi tofautitofauti ya fonimu (sauti) moja.
MITAZAMO YA DHANA YA FONIMU
Juhudi za kufasili dhana ya fonimu zilizofanywa na wanaisimu mbalimbali zimezua mitazamo mbalimbali ya namna ya kuchambua dhana hii. Hadi sasa, mitazamo mitatu ifuatayo ndiyo hujulikana zaidi.
Fonimu ni Tukio la Kisaikolojia
Huu ni mtazamo uliokuzwa na kutetewa na wanasarufi geuzi-zalishi, mwanzilishi wake akiwa ni Noam Chomksy. Kwa mujibu wa mtazamo huu, fonimu ni dhana iliyo katika akili ya mzungumzaji wa lugha. Mtazamo huu unadai kuwa kila mzungumzaji wa lugha ana maarifa bubu ya idadi na jinsi ya kutamka fonimu za lugha yake. Chomsky anayaita maarifa haya kuwa ni umilisi (competence). Anadai kuwa maarifa haya ya fonimu hufanana kwa kiasi kikubwa miongoni mwa wazungumzaji wa lugha moja husika. Kinachotofautiana ni jinsi ya kudhihirisha (kutamka)  fonimu hizo, yaani utendi (perfomance). Chomsky anabainisha kuwa kuna uwezekano mkubwa wa kuhitilafiana baina ya umilisi na utendi kutokana na matatizo mbalimbali ambayo mzungumzaji hukabiliana nayo. Matatizo hayo ni kama vile uchovu, ulemavu wa viungo vya matamshi (alasauti za lugha), athari za mazingira, ulevi, na maradhi. Hivyo, kutokana na hali hii, fonimu hubaki kuwa tukio la kiakili, yaani kisaikolojia tu.
Fonimu ni Tukio la Kifonetiki
Wafuasi wa mtazamo huu wanaongozwa na Daniel Jones. Daniel Jones anaiona fonimu kuwa ni [umbo] halisi.

..........................Inaendelea.................

31 comments:

 1. Kazi hii ni nzuri na inaelimisha. Pongezi

  ReplyDelete
 2. nimeridhishwa na chapisho hili ambalo limeniwezesha kuandika ripoti yangu kuhusu mchango wa chomsky na ferdinand katika ukuzaji wa isimu. heko kwako kaka.

  ReplyDelete
 3. pongezi sana mlumbi wa kiswahili ila kaka usisahau kuweka rejea

  ReplyDelete
 4. hongera sana kwa kuelimisha na kusaidia kutengeneza wanazuoni waliova

  ReplyDelete
 5. naomba kuelezwa umuhimu wa kujifunza fonolojia katika kiswahili

  ReplyDelete
 6. kazi nzuri sana, lakini, waweza elezakwa undani umuhimu wa mofolojia pekee

  ReplyDelete
 7. MIMI MSOMI WA KISWAHILI CHOU KIKUU CHA embu na ningeomba endelle na kuelezea kwa undani tofouti kati ya fonetiki na fonolojia

  ReplyDelete
 8. Mmi ni msomi wa kiwahili katika chuo kikuu cha Embu nchini Kenya na ningeomba ulinganishe na ulinganue fonetiki na fonolojia

  ReplyDelete
 9. Kazi njema..nakuvulia kofia

  ReplyDelete
 10. Napenda ulivyoelezea wazo la fonolojia na asili yake. Ni mufti mno. Hongera ndugu.

  ReplyDelete
 11. kazi nzuri kaka,linaridisha kila moja anayefanya utafiti

  ReplyDelete
 12. Mimi ni msomi wa kiswahili katika Chuo kikuu cha Garissa,kazi hii ni nzuri sana na kwa upande wangu,nafikiri nimefaidika sana

  ReplyDelete
 13. Shukrani sana kwa elimu hii,,,

  ReplyDelete
 14. Naomba marejeo ya hiyo kazi kwani ni kazi nzuri sana

  ReplyDelete
 15. Kazi nzuri sana naomba marejeo kk

  ReplyDelete
 16. SAfi sana tunaomba wanaisimu wengine pia waunge mkono kazi hizi kwa pamoja tukuze na kueneza kazi zetu kimitandao zaidi.

  ReplyDelete
 17. Kweli kazi ni nzuri pongezi You ndo bubujiko la maarifa

  ReplyDelete
 18. shukrani sufufu kwa kaziyo bora yenye kuelimisha

  ReplyDelete