NI
WAPI TUMEKOSEA?
Mhadhara nafungua, halaiki karibuni,
Hoja yangu naitoa, kwa makini
nyambueni,
Msipandwe
na hisia, mkavuruga amani,
Yangu hoja inahoji, NI WAPI
TUMEKOSEA?
Tumetenda
ndivyo sivyo, kwa kuwaza sivyo ndivyo,
Kwangu mimi ndivyo hivyo, yote nimeona
hivyo,
Nanyi wazeni vilivyo, mnene kama
ilivyo,
Yangu
hoja inahoji, NI WAPI TUMEKOSEA?
Na kasi mpya i wapi, na nguvu mpya ni
ipi!
Mkukuta
uko wapi, mkurabiti ni vipi!
Yangu
hoja inahoji, NI WAPI TUMEKOSEA?
Misitu
yatulilia, wanyama wanapotea,
Madini yana pepea, hakuna wa kuzuia,
Tumepuuza wosia, hamnazo kujitia,
Yangu
hoja inahoji, NI WAPI TUMEKOSEA?
Aridhi
wametoboa, fuko wamewachukua,
Mashimo yamebakia, uridhi wa vizalia,
Laana ya ng’ang’ania, kizazi hata
vizazi,
Yangu
hoja inahoji, NI WAPI TUMEKOSEA?
Dira
imetokomea, asilani si mzaha,
Baraka yawa balaa, na raha yawa karaha,
Kaka ana chekelea, kabwela ni mbaya
siha,
Yangu
hoja inahoji, NI WAPI TUMEKOSEA?
Tulidhani
mkulima, shamba tukamkabidhi,
Tukidhani analima, kumbe kaleta
wahodhi,
Kweli kaka maamuma, naomba mniwe radhi,
Yangu
hoja inahoji, NI WAPI TUMEKOSEA?
Ashakum
si matusi, kwa kuminya kidudusi,
Mhadhiri sijatusi, kukosoa si kutusi,
Nanyi pia msitusi, watusio maarasi,
Yangu hoja inahoji, NI WAPI TUMEKOSEA?
Eric F. Ndumbaro OFM Cap
0755978786
Mtunzi hongera sana kwa shairi lako zuri, kwani linafikirisha, linapendeza kwelikweli hasa pale uliposhangaa
ReplyDeletejuu ya ari mpya, kasi mpya na nguvu mpya. nami nathubutu kusema kuwa kiswahili ndio fimbo mwovu kumchapia.
KISWAHILI NDIO FIMBO
Kiswahili ndio fimbo, muovu kumchapia,
hasa atokaye ng'ambo, kichaa ametutia,
atulishaye makombo, mwishowe tunajifia,
kuchagua tulikosa, kuchagua ng'ombe zee.
kuchagua tulikosa, kaka dada, mama babu,
tulipewa visambusa, sasa maisha aibu,
tumefuga ng'ombe tasa, matibabu ni dhahabu,
kuchagua tulikosa, kuchagua ng'ombe zee.