Friday 8 November 2013

SHAIRI


NI WAPI TUMEKOSEA?

Mhadhara nafungua, halaiki karibuni,
Hoja yangu naitoa, kwa makini nyambueni,
Msipandwe na hisia, mkavuruga amani,
Yangu hoja inahoji, NI WAPI TUMEKOSEA?
Tumetenda ndivyo sivyo, kwa kuwaza sivyo ndivyo,
Kwangu mimi ndivyo hivyo, yote nimeona hivyo,
Nanyi wazeni vilivyo, mnene kama ilivyo,
Yangu hoja inahoji, NI WAPI TUMEKOSEA?

Maisha bora ya wapi, ari mpya nayo ipi!
Na kasi mpya i wapi, na nguvu mpya ni ipi!
Mkukuta uko wapi, mkurabiti ni vipi!
Yangu hoja inahoji, NI WAPI TUMEKOSEA?
Misitu yatulilia, wanyama wanapotea,
Madini yana pepea, hakuna wa kuzuia,
Tumepuuza wosia, hamnazo kujitia,
Yangu hoja inahoji, NI WAPI TUMEKOSEA?
Aridhi wametoboa, fuko wamewachukua,
Mashimo yamebakia, uridhi wa vizalia,
Laana ya ng’ang’ania, kizazi hata vizazi,
Yangu hoja inahoji, NI WAPI TUMEKOSEA?
Dira imetokomea, asilani si mzaha,
Baraka yawa balaa, na raha yawa karaha,
Kaka ana chekelea, kabwela ni mbaya siha,
Yangu hoja inahoji, NI WAPI TUMEKOSEA?
Tulidhani mkulima, shamba tukamkabidhi,
Tukidhani analima, kumbe kaleta wahodhi,
Kweli kaka maamuma, naomba mniwe radhi,
Yangu hoja inahoji, NI WAPI TUMEKOSEA?
Ashakum si matusi, kwa kuminya kidudusi,
Mhadhiri sijatusi, kukosoa si kutusi,
Nanyi pia msitusi, watusio maarasi,
Yangu hoja inahoji, NI WAPI TUMEKOSEA?

Eric F. Ndumbaro OFM Cap
0755978786

1 comment:

  1. Mtunzi hongera sana kwa shairi lako zuri, kwani linafikirisha, linapendeza kwelikweli hasa pale uliposhangaa
    juu ya ari mpya, kasi mpya na nguvu mpya. nami nathubutu kusema kuwa kiswahili ndio fimbo mwovu kumchapia.

    KISWAHILI NDIO FIMBO
    Kiswahili ndio fimbo, muovu kumchapia,
    hasa atokaye ng'ambo, kichaa ametutia,
    atulishaye makombo, mwishowe tunajifia,
    kuchagua tulikosa, kuchagua ng'ombe zee.

    kuchagua tulikosa, kaka dada, mama babu,
    tulipewa visambusa, sasa maisha aibu,
    tumefuga ng'ombe tasa, matibabu ni dhahabu,
    kuchagua tulikosa, kuchagua ng'ombe zee.

    ReplyDelete