KITUSHI CHA BABU NA MJUKUU
Mjukuu: Babu hebu nisaidie Mjukuu wako! maana naona maluweluwe. Hivi Babu! kile, vile, hivi na hivyo vilianza vile, hivyo au vilevile na wale je au ndo’ walewale. Maana wengi wanasema eti sawa na sawasawa ni sawasawa!! Napata mkanganyiko. Alafu na wale je? Walianza vile au vilevile kama wale? Mbona nashindwa kuelewa naona uvulivuli tu!! kati ya kile, kilekile, vile, vilevile na hivi, hivihivi na alafu tena eti hivyo na hivyo hivyo! ni sawa lakini si sawasawa!! Hapo Babu ndipo ninaposhaa’ maana kama vile ni vilevile na hivyo ni hivyohivyo na sawa ni sawasawa, sasa kwa nini vile vina kuwa hivyo, au vinakuwa sawasawa? Na kama hivyo ni vile au ni sawa na si sawasawa mbona sisi tuko hivi na si vile? Na kama kweli ni hivi kwa nini wewe unang’ang’ania vile na si hivyo wala hivyohivyo na wala hivi. Au Babu labda kwa sababu ya kale kamsemo kako ka “Jembe kwanza?” na kale wimbo kako kenye ubeti mmoja wenye vipande mshororo vitatu vyenye vina vya ukwapi, utao na mwanda!! huku kakiwa na uradidi wa neno moya!! teh!eeeee teheeee! teh!eeee teh! teh! teh! teh!...ha ha haha ha haaa…!!
Ati “ari mpya, nguvu mpya, na kasi mpya”
Babu: Ee waaa!! Sasa umeanza kukua mjukuu wangu, maana unaanza kuelewa mambo mazito yaliyosababisha vile na hivi vikawa hivyohivyo na wale na hawa wakawa walewale yaani kama lila na fila. Lakini mjukuu wangu nadhani umeghafilika kidogo, labda nikukumbushe kidogo.
Mimi sikusema kwa sababu bali nilisema hivi, na wala si vile wala hivyo nadhani sasa umeelewa tofauti kati ya kwa sababu na hivi. Halafu mjukuu wangu kumbuka kwamba nilikuambia hivi kama siyo vile, hivyo; utakapoona kile, hivi na hivyo badala ya vile, utang’amua vile na si kwamba hivi bali ni hivi na vile ambapo hivi ilianza kama vile na ilikuwa vile na ilibaki vile vile na si kwa sababu vilikuwa vilevile, bali kwa vile watu hawakupenda vile wakasema hivyo ndiyo maana wakawa hivi na ikawa hivi kwa kuwa walichukulia hivi ni kale na si vile!!
Teh!eeeee teheeee! teh!eeee teh! teh! teh! teh!...ha ha haha ha haaa…ahahahahaha! Na hisi nimekupoteza Mjikuu wangu! Tena kwenye mataa!! Pole sana. Lakini usijali maana yatakapowaka vile utajua cha kufanya, lakini pia uwe makini hivi kwa sababu yanaweza kukuvuruga kabisa, ambako ndiko kubaya zaidi kuliko vile. Lakini pia kumbuka hata “Roma haikujengwa kwa siku moja!” Vilevile elewa kwamba, hii ndiyo tofauti iliyopo kati ya tajriba ya wazee na watoto. Ila mjukuu wangu, nashindwa kuelewa kinachokuchanganya hasa ni kipi? Je ni kile, hiki au hivi, vile ama hivyo. Maana nimejaribu hata kuweka wino mzito na kuacha hewa katikati kusudi usichanganyikiwe lakini wapi! Ajabu kweli. Ama kweli “Elimu ya kukariri usigeuke nyuma” ukigeuka tu majanga!! Imekula kwako.
Mjukuu naomba uelewe mimi sijasema vile bali nimesema hivi… nadhani bado unatatizo la kuchanganya kati ya jembe na elimu. Ndiyo maana nimesema hivi, “elimu ya kukariri usigeuke nyuma”.
Mjukuu: Lakini babu, kwa nini usiniachie hilo shamba au kama vipi gawaurithi tu tujue moja! maana naona sasa unaanza kuongea vitu vya ajabu ajabu; mara hivi mara vile mara hivyo mara kile mara kale, halafu ukizingatia watoto wako wote ni mazuzu, si ukubali kwamba umeshindwa Babu!
Babu: (anafyumu!) Chup! Kweli nyani haoni kundule! Ni bora Zuzu kuliko mwehu au chizi, maana mwehu na chizi hawakawii kukufunga. Pia waswahili wanasema hivi; “Mcheza kwao hutunzwa!” na “Zimwi likujualo halikuli likakwisha”
Mjukuu: Kweli babu ni aibu kutangaza umeshindwa na kinyume chake ni busara kusema kwamba…!Aha! Samahani babu nimesahau nikasema hivi…! Halafu babu umesahau ile methali isemayo hivi, hahahahahaha! sasa nimekumbuka maana nilizoea kusema isemayo kwamba, kumbe ni isemayo hivi, “msema kweli ni mpenzi wa Mungu”. Lakini babu kama ni hivyo mbona vile na hivi haviendani?
Babu: Aka! mimi sikusema kwamba, Biblia na Siasa haviendani! bali wao ndiyo wanasema hivyo na vile wakasahau kwamba Mjomba Msalaba ndiye aliyeleta vyote hivi, sasa itakuwaje visigane? Nashangaa!
Mjukuu: babu mbona sikuelewi tena, yaani hivyo inakuwaje tena hivi!
Babu: “anyway”, utaelewa polepole maana nilishakuambia hivi “Roma haikujengwa siku moja”, halafu mambo haya huwa ni mwiko kuyazungumza maana utakapoanza tu hutaishia hapo tu, bali utang’amua kwamba hata mikono yako yenyewe haifanani (Mjukuu anaitazama mikono yake), halafu tena utagundua pia hata miguu yako pia haifanani na mbaya zaidi ni pale utakapoona kuwa hata macho nayo hayafanani, halafu… Yaani ni “…kama mtu aliyekula nyama ya mtu”
Mjukuu: babu mbona unachanganya ndimi tena! (babu anajibu...) “yes” utajuaje kama nilienda shule? Haya babu hayo tuyaache maana usije ukanitonesha majeraha yangu niliyoyapata katika zile shule zako. (Anaonesha hali ya wasiwasi). Babu kama mambo yenyewe ni mazito hivi!, afadhali tuyaache tuendelee na ile hoja yetu ya msingi. (Anatabasamu huku akimtazama babu yake, ambaye anaonekana kukerwa na mazungumzo ya mjukuu wake).
Ehe babu! Usinichoke mjukuu wako. Umesema utang’ang’ania mpaka mwisho wako ili kutunza heshima na jina lako huko kwa wajomba?
Babu: Haswaa! Hiyo ndiyo azima yangu mjukuu wangu.
Mjukuu: Lakini babu usifikirie sana hizo kauli zao, maana waswahili wanasema hivi kama siyo vile, “kelele za chura hazimzuii tembo kunywa maji”.
Na pia hata vipimo vya daktari vinaonesha kwamba umebakiza kidonge kimoja tu ili usinzie kama siyo kufa kabisa. Halafu hata hicho kidonge chenyewe ulishanyang’anywa na daktari lakini kwa sababu ya ubabe wa watoto wako akiwemo mama yangu walikuibia na kukufichia ndiyo maana mpaka sasa bado unadunda tu. Unadhani watu hawakugundua ujanja wako? Hebu niambie, kweli Isémbe niwakudanganyika kwa panzi? Wakati tayari alishakuweka katika himaya yake! Haliniingii akilini kabisa.
Babu: (amekasirika anaongea kwa jazba). Mjukuu wangu, sasa naona unakoelekea siko!, maana unathubutu hata kunipapasa makalio!, mimi nadhani umejichoka, waulize kaka zako yaliyowakuta. Usicheze na fagio la chuma.
Mjukuu: punguza jazba babu! Yaishe basi, maana sikutegemea kama kweli ungeweza kumpiga mkwara hata mjukuu wako! Lakini ni sawa tu, mbona hata baba yangu ulimnanilii… alipoonekana kukupinga, sembuse mjukuu!
Basi babu tuachane na hayo. Kuna jambo nataka nikuulize! (Anaonesha ishara ya kukubali kwa kutisa kichwa). Hivi zile kauli zako na misemo yako imeishia wapi, mbona hatusikii tena au umesahau kwa sababu ya uzee au kwa sababu ya elimu ya kukariri na kugeuka nyuma? Aha! Samahani babu kumbe ulisema ile ni elimu yetu! Okay. (Babu anatabasamu kama ilivyoada yake)
Babu: Nimeshakuambia hivi na zile haziendani kabisa, mbona unakichwa kigumu hivi mjukuu wangu!. Halafu hiyo okay umeitoa wapi?, maana shule zangu zinafundisha “Oke!” na siyo “Okay!”, anyway nadhani sikosa lako huenda ikawa ni lile soko huria. Kwa kweli kwa mwendo huu, hata hili shamba naogopa kukukabidhi. Sidhani kama utaliweza.
Mjukuu: Hapana babu. Usikasirike, sitasema hadharani maana najua kauli zako zitaamsha mengi. Basi babu tutaendelea nitakapotoka shambani.
Babu: Ewaaaaaa! Mjukuu wangu, hapo umenikuna.“Jembe kwanza” mengine yatafuata.
Mjukuu: hahahaha! Babu, hapo umechapia, si unaona sasa uliambiwa subiri gari lisimame wewe ukajifanya mzee wa town, ona sasa meno yote ya sebuleni huna, sasa sijui utakitamkaje maana ni aibu tupu jinsi unavyotamka!
Halafu babu, mara hii umeshasahau ulivyosema! Kweli babu uzee umeingia, “anyway” (anamwiga babu yake. Babu anatabasamu kusikia neno hilo). Ulisema kwamba… Aha! Samahani hukusema kwamba, ila ulisema hivi, “usione vyaelea vimeundwa!” Sasa babu kama ni hivyo mbona matrekta yote umeuza na pembejeo zote umeweka darini hutaki hata kuziteremsha. Halafu umesaha kuwa ushuru nao ni tatizo na ile milo ya ruzuku ndiyo kabisa shangazi anakula mwenyewe! Kweli babu kwa mtindo huu tutastawi na kupata nguvu kweli, kama milo yenyewe ambayo ndiyo tunategemea ikuzie na kustawisha miili, inaliwa na lishangazi halafu wewe ndiyo kwanza unasogeza miwani kana kwamba huoni vile. Babu, naona kwa mwendo huu vilivyoelea si kwamba vimeundwa bali ni vyepesi.
Aha! Samahani babu nimepitiwa kumbe umesema Jembe kwanza!
Lakini babu, kama ni Jembe kwanza, mbona zile, zile kule, zile pale, hizi, hizi hapa, hizo, hizo hapo, yale, yale pale, haya, haya hapa na yale kule, mbona yanaozea palepele chini, au ndo mtindo mpya wa kusindika? Nakama ni mpya mbona hatuendi kusindua? Tena babu hata wewe mwenyewe umeshuhudia juzi tu ulivyoenda Tanga, Morogoro, Mbeya, Iringa na ile mikoa mingine uliyoenda mwaka juzi kama siyo jana.
(babu anatikisa kichwa kana kwamba amesahau). (Mjukuu anacheka kwa sauti). Hahahahahaha! Babu hukawii kusema umesahau kama sisi tuliosoma kwa kukariri. Lakini babu usijali naelewa ni uzee ingawa uzee wako ni waajabu kidogo maana badala ya kutusimulia mambo ya nyumbani wewe umeng’ang’ana na kushadidia mambo ya akina mjomba, mara leo utasikia mjomba wa Amerika, mara kesho mjomba wa Asia kesho kutwa mjomba wa Ulaya na mtondogoo mjomba wa Afrika ya kati na kwingineko. Yaani wewe ni ulaya ulaya tu! Ndiyo maana hata bibi aliniambia hivi, hata ndoto zako zote siku hizi ni ulaya ulaya tu. Amakweli babu umeruka viwanja vingi, hongera kwa hilo.
Aha! Samahani babu unajua tena mjukuu wako…! Kumbe ni “Jembe kwanza”
Lakini babu, kama ni jembe kwanza mbona kule kwa wagosi wa kaya viwanda vimekufa yamebaki maziko! Sasa nyanya zetu tutazipeleka wapi? Na huko Asia ulikokwenda hujatuambia kama wanahitaji nyanya zetu. Halafu babu mi’ nashangaa ulivyomruhusu mjomba alete maepo, matunda damu na bilinganya, halafu umesahau kwamba hata kaka pia anayo! Au kwa sababu ya hiyo lugha wanayotumia, maana utasikia: grapes, lychee, apple, stasuma, peach, fig, strawberry nk.
Aha! Babu nivumilie mjukuu wako maana nasahau, kumbe ni Jembe kwanza!
Lakini babu kama ni jembe kwanza mbona vile vibinua mchanga na vile vigari vya kubebea milo ulizogawa na kuchimba aridhi vinavunjika vunjika, au ulikuwa umetuongezea ajira kwa kuongeza chuma chakavu? Kweli babu watoto huna maana wameshindwa hata kukushauri. Angalia sasa bei ya mwanga inavyozidi kuwa kubwa, umesahau kwamba hata kilimo kinahitaji umwagiliaji? Sasa unafikiri tutamwagia na nini! Mbona husomeki babu! Hata yale mashamba ya bibi umegawa kwa mjomba na mjomba naye kajenga kiwanda cha samaki. teh!eeeee teheeee! teh!eeee teh! teh! teh! teh!...ha ha haha ha haaa… nadhani ulikosea ni “Samaki kwanza” na si “jembe kwanza”
Aha! nisamehe Babu maana hata maandiko yanasema, “samehe saba mara sabini” nilisahau, Kumbe ni Jembe kwanza!
Lakini babu kama ni Jembe kwanza, mbona zile shule zako zinazoezuliwa na upepo hujasema kwamba zifundishe kilimo? Sasa babu hivi kweli kilimo bila elimu kitakwenda kweli? Au unafurahi kuona nyanya kwenye visado. Babu mi nafikiri mkulima mzuri ni yule aliyetayarishwa kuanzia huko nyuma maana hata gari lenyewe halidandiwi kwa mbele bali kwa nyuma. Na kama ni hivyo mbona sasa kilimo hakitiliwi mkazo tangu elimu ya sekondari? Na hata kama ni jembe kwanza mbona waliosoma kilimo hawapewi mkopo asilimia mia! Na kinyume chake sayansi kwanza asilimia mia. Ona babu unavyojikanganya.
Oho! Samahani nimesahau, kumbe na kilimo ni sayansi! Basi asilimia mia.
Babu ukienda tena kwa wajomba, hasa wale wenyewe kabisa waliotuita washenzi, hebu waulize waliwezaje? maana wao waliita “Green Revolution” sasa sijui ulitafsiri kutoka huko au? Maana wengine wanasema ni mapinduzi ya kijani, lakini mi sikuelewa maana hata siku ile nilipoambiwa nieleze maana yake nilidhani ni jina la wimbo wa bongo flava ndiyo maana nilishusha mistari na matokeo yake baba mdogo akakataa kutuonesha matokeo yetu.
Aha! Samahani babu sikujua kumbe ulisema Jembe kwanza!
Halafu babu, hivi hujagundua kwamba, semina na mikutano yote kuhusiana na jembe kwanza inafanyika mijini kama siyo vijijini!, teh!eeeee teheeee! teh!eeee teh! teh! teh! teh!...ha ha haha ha haaa… acha we!, ni jichekee mjukuu wa babu maana haya ni madudu,
(Babu kimya huku akivuta makohozi yake na kuyakusanya mdomoni)
Sijawahi kuona mtu akila badala ya mwingine. Aha! Nimesahau, inawezekana maana hata nilipokuwa mtoto mama aliniambia hivi yeye akishiba mimi nitachukulia kwenye nyonyo. Kama ni kwa njia hiyo, hapo nadhani umenishinda, basi itabidi kuongeza zaidi makongamano na midahalo ya kilimo mijini iliwakulima nao washibe kama mimi nilivyoshiba nilipokuwa mdogo. (Ghafla, pwaaa! Usoni).
Mjukuu: Babu vipi tena mbona hivi siungeniambia kama kopo limejaa nikamwage! (anaongea kwa masikitiko huko akijipangusa uso wake).
Aha! Samahani babu mwenzio nimepitiwa kumbe ni Jembe kwanza.
Babu hongera sana, hapa lazima nikupongeze, maana tangu nilipokuwa shuleni sijawahi kusikia mgomo wa mabwana shamba wala mabibi shamba na wala wakulima. Kweli hapa naamini kuwa Jembe kwanza mengine baadaye. Hapababu inabidi unieleze siri ya mafanikio haya makubwa. Lakini babu angalia isijeikawa kwamba wamejimegea mashamba ya nanilii… halafu wanafanya ubwana na bibishamba katika mashamba hayo! Sijui. Labda hata hilo ni jembe kwanza. Lakini kama si hivi basi na iwe vile hata huko kwingineko. Babu unakumbuka uliniambiaga kwamba Oh! Samahani babu siyo kwamba ni hivi “kimya kikuu…!” Sasa angalia wasije wakawa wameshatimiza ile kauli isemayo hivi, “Chukua Chako Mapema”.
Babu: teh!eeeee teheeee! teh!eeee teh! teh! teh! teh!...ha ha haha ha haaa… Umesemaje vile!
Mjukuu: Hapana babu hapa naomba nieleweke, mi nazungumzia mabibi na mabwana shamba, wala sina maana hiyo unayofikiri ila kawa wewe utaamua kufupisha shauri lako ila mi sikusema hivyo na wala sijakuambia ufanye hivyo. (Anamtazama babu yake) babu najua unamengi ya kuniambia na kujitetea lakini vumilia tu maana ulisema mwenyewe, jembe kwanza mengine yatafuata.
Sasa babu kama ni hilo jembe kwanza mbona gharama za usafiri na usafirishaji zinazidi kupanda? Unafikiri kaka atasafirijaje nyanya zake kutoka matombo mpaka mjini.
Aha! Samahani babu kumbe si usafiri ni Jembe kwanza.
Halafu babu kama ni Jembe kwanza mbona hawa wajomba unaowaleta huwaambii wafungue mashamba badala yake wanakupangia cha kufanya halafu na wewe unakubali tu. Halafu cha kushangaza zaidi unawakubalia hata kuchimba kajayeye ambazo tuliambiwa na babu mkubwa tusichimbe kwanza. Ona sasa wanachofanya, wanatuachia mashimo ya kufugia fuko na pimbi na wewe unanyamaza tu!
Aha! Kumbe si mifugo ni Jembe kwanza, samahani babu. Sikujua kwamba hata hayo mashimo ni sehemu ya kilimo, maana tunaweza kuyatumia kama maghala ya nafaka. Hee! Maendeleo hayo. (Babu anaonekana kukasirika. Mjukuu anasogea mbali)
Lakini babu hata mifugo si ipo kwenye kilimo, mbona unakasirika sasa! Na kama ipo kwenye kilimo mbona akinabinamu wananyang’anywa aridhi na kupewa wajomba! Sasa unafikiri hizo ng’ombe zitachungwa wapi! teh!eeeee teheeee! teh!eeee teh! teh! teh! teh!...ha ha haha ha haaa… (Anacheka na kujiambia mwenyewe). Kweli mjukuu hapa unababu kama siyo bubu maana jinsi alivyojikausha utadhani nanilii…!
Aha! Samahani babu sikujua kwamba hata hilo ni Jembe kwanza.
Babu: haya mjukuu wangu, nadhani umesema vya kutosha, au bado unataka kuendelea?
Mjukuu: Niendelee wapi babu wakati tayari umeshawaandaa shemejizo wanipige na vile vifuu moshi, unadhani sikujui ujanja wako wa kuwanyamazisha watu. Babu mimi nakuambia hakuna mtu aliyetegemea kama Sadamu au Gaddafi angekamatwa kama fuko tena katika yale mashimo aliyochimba mwenyewe. Sasa babu usipoangalia, hilo bomu unalotengeneza litakulipukia siku moja tukakuokote kwenye yale mashimo ya kajayeye walokuchimbia wajomba.
(Ghafla sauti inasikika kutoka ndani). Mjukuu… naam bibi. (anaitika mjukuu)
Bibi: haya mwambie babu yako mwingine ndani, hamuoni kuwa ni machweo sasa!
Mjukuu: babu sasa ni machweo tuingie ndani, tutaendelea kesho jioni.
(Wote wawili babu na mjukuu wanaelekea ndani ingawaje babu anaonekana kukunja uso mithili ya mbogo).
(Mahali ni palepale. Baraza linageuka kuwa kilabu cha pombe. Chizi anaonekana kwa mbali akielekea kilabuni huku akiimba wimbo wa “happy birthday”. Ghafla ananyamaza na kuanza kuangua kilio, wote wanashangaa kumuona Chizi analia, ghafla tena anaanza kucheka).
Kitaendelea….
No comments:
Post a Comment