Thursday 28 November 2013

SINTAKSIA


Katika kategoria zilizokuwa ndani ya Kiswahili ni neno la kategoria gani huchagua kategoria ipi?
Makala haya yatajadili  maana ya kategoria, yataainisha kategoria mbalimbali za maneno kwa mujibu wa wataalamu, yatajadili kategoria gani huchagua kategoria ipi katika tungo za Kiswahili, yatabainisha sababu zinazopelekea kategoria kuchaguana na kujaribu kuunda kanuni mbalimbali na hatimaye kuhitimisha.
Kategoria za maneno ni aina za maneno kadri ya uainisho wake kutegemeana na sifa za maneno husika kuwekwa katika kundi moja. Mfano Kategoria ya Nomino, Kategoria ya vitenzi, kategoria ya vivumishi.
Kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili Sanifu (2004) maneno yameainishwa katika makundi nane. Makundi hayo ni Nomino, Kitenzi, Kivumishi, Kiwakilishi, Kielezi, Kihusishi, Kihisishi na Kiunganishi. Ambapo kategoria hizi zimepangwa kulingana na sifa za maneno yanayoingia ndani yake.  

Kihore na wenzake (2003) wanaainisha kategoria saba za maneno nazo ni nomino, vitenzi, vivumishi, viwakilishi, viunganishi, vielezi na viingizi.
Kwa pamoja wataalam hawa wanakubaliana kuwepo kwa kategoria za maneno ingawa wanatofutiana katika idadi ya aina za kategoria.Tofauti hizi zinatokana na baadhi ya maneno yanaonekana kutoingia katika kategoria zilizoainishwa. Kwa mfano kategoria ya maneno kama
kwa, la, cha, vya na wa kwa mujibu wa Kihore na Wenzake (2003) yanaonekana kuwa viunganishi lakini tukiangalia dhima yake katika lugha ni kuhusisha aina za maneno mengine ambayo ni ya kategoria tofauti au kategoria finyu tofauti.
Vile vile tatizo linajitokeza pale ambapo maneno haya yanapofanya kazi tofauti tofauti katika lugha katika kigezo cha semantiki. Maneno ya lugha mfano neno na linafanya kazi kama kiunganishi na pia kama kihusishi. Hebu tuangalie mifano ifuatayo;
Mifano:  i) baba na mama
              ii) Amepigwa na Johari
Katika tungo ya kwanza neno “na” limefanya kazi kama kiunganishi na katika tungo ya pili limefanya kazi ya kuhusisha kitenzi amepigwa na nomino Johari. Kwa kuliona tatizo hilo Kamusi ya Kiswahili Sanifu ikaamua kuongeza aina ya nane ya maneno yaani Kihusishi.
Tatizo lingine linajitokeza katika baadhi ya maneno hususani kihisishi mara nyingine hutokea katika umbo la Kirai hususani kirai nomino,
Mfano Mungu wangu!
          Mtume!
         Yesu!
Maneno hayo huweza kubainishwa kama vihisishi ingawa ni nomino. Mwingiliano huu ndiyo unaoleta matatizo katika taaluma ya sintaksia, na ipo haja ya kufanya uanishaji wa aina za maneno tena au tukubaliane kuwa baadhi ya maneno ya tabia ya kughairi kanuni za lugha.
Sanjari na hilo neno aina ya kitenzi kimekuwa na tabia ya kubadili maana za tungo kadri kinavyonyambulishwa. Kitenzi kinabeba dhima ya mufidi, ufanyizi, unyume, uambatani, mwao kwa uchache kwa mujibu wa Khamis (2008). Kutokana na kitenzi nomino huzalishwa kwa sababu hiyo twaweza kusema bado tunahitaji mchakato utakaotuwezesha kutafuta ufumbuzi wa mwingiliano wa aina hizi.
Ingawa kuna mwingiliano huo lakini ni jambo la msingi kuangalia uhusiano wa maneno katika taaluma ya sintaksia . Katika kubaini uhusiano huo tunaangalia neno la kategoria gani huchagua kategoria nyingine, hatua ya kwanza tunaweka vikundi mbalimbali vya maneno ambavyo huashiria kuwepo kwa uhusiano wa karibu wa baadhi ya maneno.
Wataalam mbalimbali wamebainisha vikundi vya maneno hayo. Habwe na Karanja (2007:154) wanaainisha maneno katika makundi matatu ambavyo ni kundi Nomino (KN), kundi tenzi (KT) na kundi husishi (KH).
Chomsky na Halle (1968:08) wao wanachanganua tungo sentensi kwa kuainisha fungu Nomino (KN) na fungu Tenzi (KT). Hii ina maana kwamba wanatambua kuwepo kwa kundi na hivyo kuona kuwa maneno yanachaguana.
Katika mjadala huu maneno yanawekwa katika makundi yafuatayo;
Kikundi Nomino (KN), Kikundi kitenzi (KT), Kikundi husishi (KH), Kikundi vumishi (KV) na Kikundi elezi (KE). Katika ugawaji wa makundi haya neno linalotawala maneno mengine hukipatia jina kikundi hicho, mfano katika kundi nomino lifuatalo;
Baba mdogo katika kikundi nomino hiki neno Baba linatawala neno mdogo, nomino baba inatawala kivumishi mdogo.
Kwa kuchunguza vikundi hivyo vya maneno, tunaweza kugundua kuwa kategoria zina tabia ya  kuchaguana. Jambo la kujiuliza ni kwa nini kategoria huchaguana? Kategoria huchaguana kwa sababu zifuatazo:
Sababu ya mofo-sintaksia, Katika sababu hii tunazingatia mahusiano ya maumbo ya maneno yanavyopelekea kuchaguana. Msisitizo unawekwa katika upatanisho wa kisarufi unavyoruhusu kategoria anuai kuchaguana. Wazo hili pia limeelezewa na Khamisi kupitia kazi ya Steere (1870) anaeleza kuwa alijishughulisha na kupata maana tu iletwayo na umbo au sauti, hivyo ikafaa kuitwa Maelezo ya Sauti – maana. Pia Khamisi anaeleza “Mchango wa Steere tunaweza kusema kuwa wa kimofolojia na elezi bila kuwa na ufafanuzi” Mfano:
                                   Mtoto mzuri
N        V
Kitoto kizuri
N        V
Vitoto vizuri
                                   N         V
Kwa hivyo katika data hiyo hapo juu, maumbo ya maneno yamesababisha kuchaguana kwa maneno hayo.
Pia katika data ifuatayo utagundua kuwa maumbo ya maneno pia yanaweza sababisha kutochaguana kwa maneno;
                                   Mtoto kizuri
                                   Kitoto mzuri
                                   Vitoto kizuri
Ukichunguza data hiyo unagundua kuwa maneno hayo hayawezi kuchaguana, kwani maumbo ya maneno hayo hayaruhusu viambishi awali katika maneno yanayofuata.
Khamis (2008:4), anaeleza juu ya unyambulishaji usio na mipaka na unyambulishaji wenye mipaka. Hii inaonesha kuwa ni sababu nyingine ya kategoria ya maneno kuchaguana. Pia Guthrie (1962:203) kama anavyonukuliwa na Khamis (2008:5) unyambulishaji wenye mipaka huathiri tabia ya kitenzi kisintaksia kwa kuongeza yambwa, kupunguza yambwa au kutofanya chochote kile kwenye kitenzi, anaendelea kuzungumzia aina za minyambuliko kama fanyizi, mufidi, ambatani, nafsi, tendwa, uwezo, tuamo na nyume ambayo hupelekea kitenzi kuteua kategoria za maneno.
Mfano wa mnyambuliko mufidi,
Neno shika kabla ya kunyumbulishwa linaweza kuchukua nomino mbili mfano baba ameshika kikombe.
Lakini kitenzi shika kinaponyumbulishwa kwa kuongeza –i- tunapata shikia hivyo tunaweza kusema baba amemshikia mwalimu kikombe. Hivyo kitenzi hicho kimechukua nomino tatu.
Lakini hatuwezi kusema baba ameshika mwalimu kikombe. Kwa sababu kitenzi shika hakidhibiti nomino tatu.
Pia katika mnyambuliko fanyizi husababisha kitenzi kibebe Nomino.
Mfano;
Imb –ish-a watu, kiambishi –ish- kinafanya kitenzi imba kuchagua nomino watu. Ikifanya dhima ya kutendesha.
Lakini hatuwezi kusema imbisha ng’ombe, tungo hii haina mantiki, kwani ng’ombe hawezi kuimba.
Mnyambuliko wa utendwa pia unasababisha kitenzi kuteua kategoria ya maneno; Mfano, chez-w-a, fund-w-a vitenzi hivyo vinalazimisha kuteua kategoria ya nomino au kielezi. Mfano  Mtoto amechezwa unyago
Hapa kitenzi chezwa kinaruhusu nomino unyago, kwa sababu unyago unachezwa, lakini hatuwezi kusema mtoto amechezwa nguo, ingawa nguo ni nomino kama ilivyo unyago, lakini nomino hiyo haiwezi kuchezwa kwasababu kimaana tungo hii inakataa.
Dhana ya kitenzi si elekezi hujitokeza katika kitenzi ambacho hakiruhusu kuchukua nomino nyingine. Hapa kitenzi kinawekewa hali ya utendeka inayojidhihirisha katika umbo la –k na –ik.
Mfano:          kikombe kimevunjika
                        Maji yamechemka
Pia sababu ya Kisemantiki, ambapo maneno huchaguana kwa kufuata mantiki ya maana inayokusudiwa.  
Mfano:        anakunywa ugali
                      T                   N
Pamoja na ukweli kuwa kitenzi kunywa ni elekezi (kinaweza kubeba nomino, sababu za kisemantiki zinakataa, huwezi kunywa ugali. Kwa kuzingatia kanuni ifuatayo ya kitenzi kunywa:
                        Kunywa (T – ele) - ------   + [___kiminika]
                                                               +maji, soda, shalubati, bia
Sanjari na hilo kitenzi cha lugha ya Kiswahili kina tabia ya kubeba dhana mbalimbali na kusababisha maana kutofautiana. Kwa mfano kitenzi chenye mnyambuliko mufidi kina dhima  za kisemantiki zifuatazo kutokana na kuteua nomino zenye kubeba nduni tofauti tofauti kama ifuatavyo:
Mfano: pik – i –a     + N
                    T   +   N
                    +sababu
                    +mahali
                    +faida
                      
Mfano: a) pikia wali (faida)
             b) pikia nje   (mahali)
             c) pikia nini? (sababu)  
Hivyo maneno huweza kuchaguana kutokana na sababu za mofosintaksia, kisemantiki na sababu zinazotokana na tabia mbalimbali za vitenzi. Matumizi ya maneno katika tungo yoyote ile hutegemea sana mahusiano kati ya neno na neno ili tungo hiyo ilete maana, hivyo sio tu kusema Nomino inaweza kukaa na Kitenzi, inabidi kujiuliza maswali zaidi, je kila nomino itakaa karibu na kitenzi fulani? ni muhimu kuzingatia sababu zote zinazosababisha maneno kuchaguana ili kujenga maana katika lugha.
MAREJEO
Chomsky, N. na Morris Halle (1968), The Sound Patterns of English, NewYork: Harper and Row Publishers.
Kihore na wenzake (2009), SARUFI MAUMBO YA KISWAHILI SANIFU (SAMAKISA): Sekondari na Vyuo, Dar es Salaam: Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili(TUKI)
Khamisi, A.M (2008), Maendeleo ya Uhusika, Dar es Salaam: Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili







7 comments:

  1. kuna matumizi ya nadharia ya sarufi ya uamilifi wa leksika katika sentensi naomba kuelekezwa.

    ReplyDelete
  2. eleza matumizi ya nadharia ya sarufi ya uamilifu wa leksika katika sentensi za kiswahili

    ReplyDelete
  3. Fanya uchunguzi na usome kuhusu..sifa za kisemantiki za msamiati na kanuni za uteuzi zuifu(lexical semantic features and selectiona restricton rules)

    ReplyDelete
  4. Ni nini faida ya kuwa na kategoria katika lugha

    ReplyDelete
  5. Naomba unisaidie maelezo kuhusu kategoria za kisintaksia.

    ReplyDelete
  6. Kwanini kuna uainishaji tofauti tofauti wa maneno

    ReplyDelete
  7. Istilahi kiuzi msambao ina maana gani na ni vipi inavyotumika katika sintaksia

    ReplyDelete