SARUFI MAJUMUI NA UAMILIAJI LUGHA YA
PILI.
Makala
haya yataangalia maana ya sarufi majumui, masuala ya msingi yanayohusu maarifa
ya lugha, sifa za sarufi majumui, sarufi majumui na uamiliaji lugha ya pili na
mwisho tathmini.
Kwa
mujibu wa Chomsky (1976:29) kama alivyonukuliwa na Ellis (1996:430) sarufi
majumui ni mfumo wa kanuni na sheria ambazo ni msingi wa lugha za binadamu
(tafsiri yangu). Muasisi wa nadharia hii ni Noam Chomsky.
Msingi
wa nadharia hii ni kwamba binadamu anapozaliwa anakuwa na maarifa asilia ambayo
humsaidia katika ujifunzaji lugha; mambo ya ndani na nje ambao husaidia katika
uamiliaji wa lugha. Maarifa haya hupatikana pale tu binadamu anapozaliwa kwani
huwa na kifaa cha uamiliaji lugha ambacho kinakuwa na kanuni majumui na kanuni
badilifu ambazo hukutana na tajiriba (uwezo wa jamii katika lugha) na
kusababisha uamiliajli lugha kutokea.
Waamiliaji
wa lugha ya kwanza huwa na maarifa asilia ambayo huwawezesha kuiamili lugha yao
kwa kutumia maarifa hayo. Hivyo
maarifa hayo yanaamshwa na tajiriba ambayo
mjifunzaji anaikuta katika jamii iliyomzunguka na hatimaye kukutana na maarifa
asilia katika kifaa cha uamiliaji lugha hatimaye kuzalisha sarufi mahsusi ya
lugha husika.
Waamiliaji
wa lugha ya pili wanakuwa na lugha ya kwanza ambapo sifa za sarufi majumui bado
humwezesha kuamili lugha ya pili, kwani kanuni badilifu na kanuni majumui
zilizojengwa kwa misingi ya lugha ya kwanza hutumika katika kuamilia lugha ya
pili. Hivyo kwa mujibu wa nadharia ya sarufi majumui inamsaidia mjifunzaji
katika kuamili lugha ya pili.
Wataalam mbalimbali
wameweza kujadili juu ya uwezo wa sarufi majumui wa kuwa kifaa weazeshi cha
kujifunza lugha ya pili, kuna wataalam wanaokubali na wanaokataa mchango huo.
Kama
Flyn (1984-1987) anavyoelezea kama alivyonukuliwa na Ellis (1996:453) kifaa cha
uamiliaji lugha ya kwanza kitahusika na mchakato wa ujifunzaji lugha ya pili. Akaendelea
kusema kanuni badilifu za lugha ya kwanza na lugha ya pili zikiwa sawa ujifunzaji
utakuwa rahisi kwa sababu mjifunzaji wa lugha ya pili ana uwezo wa kuhusisha
miundo wakati kanuni hizo zikitofautiana kati ya lugha ya kwanza na lugha ya
pili ni vigumu kujifunza.
Flyin
yeye anaunga mkono juu ya sarufi majumui kuwa kifaa wezeshi katika ujifunzaji
wa lugha ya pili. Kwani anaamini bado maarifa ambayo mjifunzaji wa lugha ya
kwanza anayoyatumia katika ujifunzaji wa lugha hiyo, ndiyo yale yale
anayoyatumia mjifunzaji wa lugha ya pili.
Hata
hivyo Clahsen na Muysken (1986-1991) kama walivyonukuliwa na Ellis (1996:454)
wanasema uamiliaji wa lugha ya pili ni tofauti na uamiliaji lugha ya kwanza
muamiliaji lugha ya kwanza huwa na kifaa wezeshi cha uamiliaji lugha wakati wa
lugha ya pili hutumia mbinu za lugha ya kwanza katika kujifunza lugha ya pili
wanaendelea kusema muamiliaji lugha ya pili huhitaji nadharia ya isimu wakati
wajifunzaji lugha ya pili huhitaji naharia tambuzi.
Hata
hivyo sarufi majumui imeangaliwa katika mitazamo tofautitofauti, hivyo kuonesha
ubora lakini pia mapungufu yake katika ufundishaji wa lugha:
Kwa kuwa
na sarufi majumui tunaona kuwa sifa za lugha huingiliana, hivyo mwingiliano wa
lugha ya kwanza na ya pili unaweza kumwezesha muamiliaji lugha ya pili pale
miundo ya lugha ya kwanza na lugha ya pili itafanana na hata ikitofautiana
mjifunzaji anakuwa na uwezo wa kujiundia miundo yake itakayomsaidia katika
ujifunzaji wake kwa kutumia sifa majumui za lugha.
Flynn
(1984;1987) kama alivyonukuliwa na Ellis(1996;453) anaeleza kuwa “kifaa cha uamiliaji lugha ya kwanza kinaweza
kutumika katika uamiliaji wa lugha ya pili. Kama kanuni badilifu za lugha ya
kwanza na ya pili zinauhusiano hurahisisha ujifunzaji”. Hivyo yeye
anakubali kabisa kuwa sarufi majumui ni kifaa wezeshi katika ujifunzaji wa
lugha ya pili, anaamini sifa za mjifunzaji wa lugha ya kwanza ndizo ambazo anakuwa
nazo mjifunzaji wa lugha ya pili.
Aidha
Ellis (1994:461) anaeleza ubora wa sarufi majumui kuwa imetoa msingi wa
uibukaji wa nadharia zingine za ujifunzaji lugha baada ya kuegemea kwenye
maarifa asilia anayozaliwa nayo binadamu. Pia imeweza kueleza sifa majumui za
lugha mbalimbali za ulimwengu kwa ufupi, hivyo kusababisha sifa za lugha
kueleweka kwa urahisi kwa wajifunzaji wa lugha ya pili.
Kwa
mujibu wa Ellis (1994:458) udhaifu huu unajidhihirisha katika maeneo kadhaa,
kiini cha sarufi majumui yenyewe, pia mbinu zilizotumika kukusanyia data. Hivyo
inaonekana kuwa kuna tatizo katika mbinu za ufundishaji na namna ya ufundishaji
wa lugha ya pili.
Nadharia
ya sarufi majumui haikuonyesha namna gani mjifunzaji anapata ujuzi wa kutumia
maarifa asilia aliyozaliwa nayo lakini pia mbinu iliyotumia katika ukusanyaji
wa data ni ile mbinu ya kukusanya data isiyo ya vipindi maalum. Hivyo kupelekea
data zake kutoweza aminika.
Vilevile
clahsen na Muysken (1986), Meisel(1991) kama walivyonukuliwa na Ellis
(1996;454) muamiliaji wa lugha ya pili atakuwa tofauti na muamiliaji wa lugha
ya kwanza kwa sababu kifaa cha uamiliji lugha kipo tu kwa mtu anayejifunza
lugha ya kwanza na yule anayejifunza lugha ya pili huweza kusaidiwa na
maarifa/mbinu mbalimbali ya ufundishaji na mazingira. Hivyo hawa wanaona kuwa
safuri majumui si kifaa wezeshi katika ujifunzaji wa lugha ya pili.
Kuibuka
kwa nadharia zingine kunaonesha udhaifu wa nadharia ya sarufi majumui, mfano
Fabisz, N.
Anaelezea nadharia ya uzawa iliyoasisiwa na Andersen ambayo inasisitiza juu ya urithishaji wa lugha, pia nadharia ya
utamadunishi iliyoasisiwa na John Schumann (1978)inayosisitiza jinsi utamaduni
wa jamii ulivyo na mchango mkubwa katika ujifunzaji lugha kwani lugha huendana
na utamaduni mfano ni vigumu kujifunza lugha ya kiingereza kwa mswahili
kwasababu tunatofautiana katika utamaduni hata kama utajua kiingereza
hautafanana na mwingereza mzawa kwa kuwa yeye atatumia miundo ya lugha hiyo
akihusisha na utamaduni wake.
Hivyo
katika kujifunza lugha sarufi majumui sio kifaa wezeshi pekee cha uamiliaji
lugha pekee ambacho hutumika bali kuna vitu kama mazingira, motisha na urudiaji
wa mara kwa mara humpelekea muamiliaji lugha ya pili kujifunza lugha ingawa
kuna utofauti wa uamiliaji kuna wengine huchukua muda mrefu na wengine muda
mfupi, si lazima waamiliaji wa lugha ya pili wawe na sarufi majumui
inayofanana, hivyo tofauti zao wakati mwingine haziepukiki.
Kama
ubora na udhaifu wa sarufi majumui unavyojidhihirisha, hii inaonesha kuwa
sarufi majumui peke yake haitoshi kumfanya mjifunzaji wa lugha aweze kuamili
lugha ya pili vizuri, hivyo walimu wanashauriwa kutumia nadharia changamani
katika ufundishaji wao wa lugha ya pili ili kumwezesha mjifunzaji wa lugha ya
pili kuamili lugha hiyo vizuri.
Kimsingi
sarufi majumui inajidhihirisha kuwa ni kifaa wezeshi katika ujifunzaji wa lugha
ya pili licha ya kuwa na udhaifu wake, haipelekei kuiondoa katika hali ya
uwezeshi katika ujifunzaji wa lugha ya pili, kwani sifa majumui zinazopatikana
katika lugha mbali kwa kiasi kikubwa zinawasaidia wajifunzaji kujifunza lugha
ya pili, mfano wajifunzaji wanapogundua miundo ya lugha na uundaji wa misamiati
unaolingana itawawia rahisi katika ujifunzaji wao. Lakini hata ikitofautiana
sarufi majumui imefafanua namna ambavyo mjifunzaji huyu ataweza kujiundia
sarufi yake ambayo itakuwa imejengeka kwa misingi ya lugha ya kwanza.
Kuna
umuhimu wa kuwa na mazingira bora ya ujifunzaji ambapo mawasiliano yanapewa
msisitizo mkubwa katika nadharia mbalimbali, hivyo walimu hawana budi kujenga
mazingira hayo kwa wanafunzi wao ili waweze kujifunza lugha ya pili kwa
usahihi. Ikiwa ni pamoja na kubadilisha mazingira ya darasa kuwa mazingira
rafiki kwa mwanafunzi ambapo mawasiliano ndiyo kiini cha ujifunzaji.
Nadharia
ya sarufi majumui imeonekana ina mchango mkubwa katika tendo la ujifunzaji,
lakini haitoshi kusema ndiyo nadharia pekee ambayo inapaswa kutumiwa na walimu
katika ufundishaji wao kwani pia imeonekana kuwa na udhaifu, hivyo nadharia
zingine kama za utamadunishi, uzawa na urithishaji ni muhimu kuzipa umuhimu pia
ili tendo zima la kujifunza liweze fanyika, lakini pia cha msingi ni kujua
wajifunzaji hawawezi kuwa na uwelewa wa aina moja hata kama haya yote
yatatimia, hivyo kinachoangaliwa ni kufikia ile hali ya kawaida katika matumizi
ya lugha, ambapo kila mjifunzaji anatarajiwa afikie.
MAREJEO
Ellis, R. (1994), Second
Language Acquisition, USA: Oxford University Press
ISTILAHI
Externa
approach - mkabala wa nje
Intuition - ujuzi
Internar
approach - mkabala wa ndani
Parameter
- kanuni badilifu
Principles - kanuni majumui
Prompted - Papo hapo
Universal
grammar - sarufi majumui
No comments:
Post a Comment