Wednesday, 13 November 2013

SHAABAN ROBERT


DHANA YA MAPENZI KATIKA KAZI ZA SHAABAN ROBERT
Mapenzi ni hali ya kuingiwa moyoni na kuthamini mtu au kitu zaidi ya mwingine au kingine.
Pia mapenzi ni hali ya kujali jambo, kitu au mtu zaidi ya mwingine. S. Robert amejaribu kufafanua dhana ya mapenzi kama dhana pana sana, anaeleza kuwa:
  • Mapenzi ni hali ya kumpenda Mungu
  • Mapenzi ni yale ya kupendana sisi kwa sisi
  • Mapenzi ni yale yasiyo bagua umri, kabila au kazi, taifa, rangi nk.
  • Mapenzi ni yale yasiyojali tofauti baina ya watu
  • Mapenzi ni ile hali ya kupendana bila kikomo 
  • Mapenzi ni yale ya kuridhika na hali zetu. Mfano; katika kitabu chake cha Mapenzi Bora nk,

Dhana ya mapenzi imejitokeza katika kazi zake nyingi, kama vile; kazi za riwaya. Mfano, Adili na Nduguze S. Robert anamhusia mtoto wake Adili namna ya kumpenda mkewe na familiya yake. Pia katika kitabu cha Kusadika anaonesha jinsi viongozi wasivyo na mapenzi ya dhati.
S. Robert pia anaelezea sifa za mapenzi katika kazi zake nyingi. Amejaribu kueleza mapenzi kwa kuhusisha na vitu mbalimbali. Amefananisha mapenzi na kileo. Anasema, mapenzi ndio mwokozi wa mambo yote hapa Duniani. Mtu mwenye mapenzi ya kweli ni sawa na mtu aliyelewa hutenda kila kitu bila kujielewa.
Pia anasema, mapenzi ni uhai. Palipo na mapenzi ya kweli watu hustawi, huishi miaka mingi na panapokosekana  mapenzi ya kweli hawaishi miaka mingi.
Kifo ni mapato ya kukosekana kwa mapenzi ya dhati, “mapenzi kwangu uhai hukinai kama ninywae divai baridi katika kuzi.”
Asema kuwa, mapenzi ya kweli ni matamu kama asali. Kama asali ilivyotamu ndivyo mapenzi mapenzi ya kweli yaletavyo ladha isiyoisha. Mfano, katika Mapenzi Bora ubeti wa 46-61 na 68-80
Vilevile analingalisha mapenzi na nuru ya jua au mwezi. Anaamini kuwa palipo na mapenzi ya dhati ni sawa na nuru ya jua mchana na nuru ya mwezi usiku. Hivyo kwake yeye mapenzi ya dhati huondoa giza la usiku na huleta nuru/mwanga. Mapenzi ni nuru Duniani imuongozayo binadamu kama jua na mwezi. Ubeti wa 84.
Pia anaona kuwa, mapenzi ni sawa na mshipa wa damu kwa mwanadamu, au mti na mizizi. Anasema binadamu bila mishipa ya damu hawezi kuishi kama ilivyo mti na mizizi.
Vivyo hivyo jamii ikikosa mapenzi ya dhati haiwezi kuishi. Ni sawa na maji kwa binadamu kwani hukata kiu wakati wa jua kali. Hivyo mapenzi huzima kiu katika jamii kutokana na adha mbalimbali. ubeti wa 87-105.
“Dunia jangwa la kiu
Na sisi tusisahau,
Mapenzi faraja kwa kuzima kui hizo.”
S. Robert anaamini kuwa popote penye mgogoro nyuma yake yamekosekana mapenzi ya dhati. Anafananisha tena mapenzi ya dhati na Johari yaani kitu chenye thamani kupita kitu kingine. Hivyo anaona kwamba katika maisha ya kawaida mtu akikosa mapenzi ya kweli hawezi kufanya chochote.
Mapenzi ya dhati ni kitu chenye thamani kupita vitu vyote na wakati wote kina kinathamani, kwake. Mapenzi ni sawa na pambo la moyo. Katika hali ya kawaida akili hupambwa kwa maarifa lakini moyo hupambwa kwa mapenzi ya dhati, kwani mapenzi hutoka moyoni na maarifa hutoka akilini. Mpenzi hufurahisha moyo na yanathamani kuliko cheo na hayauzwi sokoni.
Pia Shaaban Robert ameeleza hasara na faida za kukosekana kwa mapenzi ya dhati katika jamii.
Faida ya kuwepo kwa mapenzi ya dhati katika jamii:
  • Mapenzi ya dhati huleta amani na utulivu.
  • Mapenzi ya dhati huondoa ubaguzi.
  • Mapenzi ya dhati huleta mshikamano katika jamii.
  • Mapenzi ya dhati huondoa ghasia za wivu, choyo, chuki nk.
  • Mapenzi ya dhati huleta haki na wajibu.
Hasara za kukosekana kwa mapenzi ya dhati katika jamii.
  • Kukosekana kwa mapenzi ya dhati huleta ubaguzi wa rangi
  • Kukosekana kwa mapenzi ya dhati husababisha chuki na fitina
  • Kukosekana kwa mapenzi ya dhati husababisha fujo na dhiki mbalimbali katika jamii
  • Kukosekana kwa mapenzi ya dhati husababisha dhuluma na rushwa
  • Kukosekana kwa mapenzi ya dhati husababisha kupotea kwa haki katika jamii
FALSAFA YA SHAABAN ROBERT JUU YA MAPENZI YA DHATI
Kwake mapenzi ya dhati ndio suluhisho la kila kitu Duniani. Je falsafa hii inaweza kusawiriwa hivi leo katika nyanja za kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni?
Pamoja na mtazamo chanya wa Shaaban Robert juu ya mapenzi. kwa kweli kwa mtazamo wangu naona kwamba, dhana ya mapenzi naweza kusema kuwa hii ni dhana ya kinadharia zaidi kwani huwezi kujua au kusema yapi hasa ni mapenzi ya kweli na ya dhati na yapi si ya kweli na ya dhati
S. Robert anaeleza mapenzi ya aina zote. Mfano, mapenzi ya;
  • Mke na Mume pamoja na watoto. Mfano, katika kitabu cha Maisha Yangu na Baada ya Miaka Hamsini.  
  • Mapenzi ya kifamilia – mfano; Maisha Yangu na Baada ya Miaka Hamsini, Riwaya ya Kufikirika
  • Mapenzi ya kindugu – Ameonesha mfano mzuri kwa kuishi na ndugu yake ambaye ni Yusuph Urenge. Mfano; katika Barua za Shaaban Robert.
  • Mapenzi ya mtu na muumba wake. Hapa shaaban Robert anaonesha Imani yake kwa Mungu. Pia katika vitabu vyake aliombea sana umoja wa dini.
  • Mapenzi ya mtu na Taifa lake (uzalendo) – S. Robert alipenda sana Taifa lake.
  • Mapenzi kwa mazingira – anaona kwamba kama kweli watu wana mapenzi ya dhati kwa mazingi kusingekuwa na mmomonyoko wa aridhi wala ukame, wala mafuriko nk.
Falsafa ya jumla ya Shaaban Robert ni kwamba, “Daima wema hushinda ubaya.”

No comments:

Post a Comment