Thursday, 10 March 2016

Ugumu wa Kufasili NenoNI VIGUMU KUFASILI MAANA YA NENO KIKAMILIFU”
Kazi hii itaonesha namna kulivyo na ugumu wa kufasili neno. Pia itaeleza kiini cha ugumu huo wa kufasili neno kikamilifu kwa kuzingatia fasili za wataalamu mbalimbali wa isimu.
TUKI (2004) wanadai kuwa neno kama kipashio cha usemaji ambacho hujengwa na mwanadamu au mkururo wa sauti zilizopangika kisilabi na ambazo hutambuliwa na wasemaji wa lugha inahusika kuwa kitu kimoja chenye maana mahususi. Naye Mdee (2010:5) anafasili neno kwamba ni mfululizo wa herufi ulioafungamana pamoja na kuzungukwa na nafasi tupu. Pia Kihore na wenzake (2001) wanafasili neno kwa kutulia maanani maelezo ya Lyons (1984:194-208) kuwa neno linaweza kufafanuliwa katika misingi ya kiumbo-sauti (yaani, kwa kuchunguza sauti zinazounda umbo zima), kiotografia (yaani kwa kuchunguza herufi zinazotumika katika kuliundika umbo lake) na kisarufi (yaani, kwa kuchunguza kilekinachowakilishwa na umbo husika katika lugha)
Spencer(1991:41) anafafanua  kuwa dhana ya neno ni dhana tata sana japokuwa   ni dhana muhimu sana katika nadharia za mofolojia.Wataalamu mbalimbali wamejaribu kufasili neno lakini kila  nadharia waliyoitumia kufasili neno  haikukidhi kueleza  neno ni nini hasa ukitofautisha na dhana nyingine kama leksikoni. Njia mojawapo ya kufasili neno ni kwa kuangalia sifa zake kiisimu yaani kifonolojia, kimofolojia na kisemantiki. Ikiwa kigezo hiki kitatumika  kwa lugha moja moja huweza kuwa na mafanikio lakini tatizo kubwa ni kupata vigezo majumui vitakavyokidhi lugha zote.
Katamba (1993:17) anadai kuwa wazo kuwa lugha huundwa na maneno huchukuliwa kwa mazoea ya watu wengi kwani hata mtu asiyejua kusoma na kuandika anatambua kuwa kuna maneno katika lugha yake. Kumekuwa na mawazo tofautitofauti juu ya neno hasa ni nini. Dhana ya neno hutumiwa katika fahiwa mbalimbali ambazo ni vigumu kuzitofautisha.
Mdee (2006:5) anadai kuwa umbo linalojulikana katika lugha ya kawaida kama neno lina utata kwani ni umbo lenye sura nyingi. Utata huu unatokana na mitazamo tofauti ya wanaisimu kuhusu kipashio hiki kitahajia, kimatamshi,na kimaana.
Kutokana na maelezo ya wataalamu hawa tunaweza kubaini mambo kadhaa yanayopelekea ugumu wa kufasili neno.
Mosi ni utofauti za lugha kuwa dhana ya neno hurejelewa tofautitofati katika lugha tofautitofauti kwa mfano lugha tenganishi, lugha ambishi bainishi, na lugha ambishi mchanganyo hubainisha maneno tofauti hivyo umbo moja laweza kuwa neno katika lugha moja lakini lisiwe neno katika lugha nyingine.
Ugumu mwingine unatokana na vigezo vinavyotumika kufasili neno. Hakuna kigezo kimoja kinachojitosheleza kufasili kwa ukamilifu dhana hii ya neno na kwamba kila kigezo huonekana kuwa na mapungufu.
Kwa upande mwingine ugumu wa kufasili neno unatokana na sababu kuwa dhana ya neno hutumiwa katika fahiwa mbalimbali ambazo ni vigumu kutofautisha,
kutokana na mifumo tofauti ya lugha tofautitofauti hivyo nivigumu kupata fasili moja ya neno inayoweza kujitosheleza katika lugha zote.
Ingawa wanaisimu hao wamejaribu kufasili dhana ya neno, lakini bado kumekua na mijadala kuhusu neno hasa ni nini kwa sababu kila fasili inayotolewa haijitoshelezi. Kiini cha ugumu wa kufasili neno kikamilifu ni kutokana na kuwepo kwa vigezo tofauti tofauti vinavyotumika kufasili neno. vigezo hivyo ni kigezo cha kifonolojia, kiotogirafia, kileksika na Kisemantiki na Kisintaksia. Hakuna kigezo mahususi ambacho kinaweza kutumika kwa lugha zote na tukapata fasili ya neno.
Kigezo cha kiotografia neno hufasiliwa kama ni mfululizo wa maandishi ambao unamwachano wa nafasi mwanzoni na mwishoni mwa neno lakini katikati ya maandishi hayo hakuna nafasi yoyote.
Naye Mdee (2010:5) anaunga mkono fasili ya neno kuwa ni mfululizo wa herufi zilizofungamana pamoja na kuzungukwa na nafasi tupu. “Mtoto anasoma kitabu vizuri” kutokana na nafasi zilizopo mwishoni mwa neno katika mfano huu kuna maneno manne, yaani “Mtoto, anasoma, kitabu, viziri”
Hata hivyo utaratibu wa kuweka mwisho na mwanzo mwa neno hauwekwi kiholela bali kuna kanuni za kiotogarafia ndizo hueleza sehemu ya kuweka nafasi na wapi nafasi isiwekwe na hii hutofautiana kutokana na lugha moja na nyingine.
Udhaifu wa kigezo hiki ni kwamba kigezo hiki huweza kutumika kwenye lugha yoyote yenye mfumo wa maandishi lakini si mifumo yote ya kimaandishi hufasili neno kwa kigezo cha kiotografia. Kwani lugha nyingine hazina nafasi au vitenganishi, mfano lugha ya Kilatini, Kieskimo mfano katika Kieskimo “tuntussuqatarniksaitengqiggtuq” hivyo basi fasili hiyo haina nafasi katika lugha ya Kieskimo na lugha nyingine zenye mfumo kama huo. Lakini pia suala la nafasi tupu hujidhihirisha katika lugha ya maandishi na si katika lugha ya mazungumzo. Hivyo swali la kujiuliza ni kwamba neno lipo katika maandishi tu.
Vilevile kuna maneno ambayo yana umbo moja lakini maana ni tofauti mfano
·        Kaa -tendo la kuketi kitako
·        Kaa- aina ya samaki
·        Kaa-Kipande cha ukuni chenye moto au kilichochomwa
Swali la kujiuliza ni, neno kaa limejitokeza mara tatu ni maneno tofauti au ni neno moja?
Upungufu mwingine wa fasili hii ni kwamba kuna utata katika maneno ambatani hasa katika kuandika maneno hayo kwani hakuna kanuni maalumu inayotumika.Wakati mwingine maneno ambatani huweza kuandikwa kwa kuyaunganisha maneno au kwa kuyatenga na kistri au kwa kuacha nafasi mfano
Bata mzinga, bata-mzinga, batamzinga uandishi ndio uko tofauti ila maana ni moja. je maneno ambatani yaliyoandikwa kwa kutenganisha kistari au kwa kuacha nafasi yatahesabiwa kama maneno mawili au moja.
Fasili hii ina mapungufu mengi kwasababu bado haielezi maana halisi ya neno. Kwa kuzingatia viambajengo vinavyounda dhana nzima ya neno kama vile silabi.hata hivyo fasili hii inaonyesha uwepo tu wa neno katika sentensi lakini haifasili.
Kigezo cha kileksika, fasili ya neno kwa kigezo hiki huchukulia neno kama dhana dhahania ya kileksika ambapo neno hurejelewa kama leksimu. Neno la kileksika ni msamiati wote uliopo katika kamusi.kwa hiyo neno la kileksika ni la kidhahania ambalo linaweza kuwa katika maandishi au katika mazyngumzo. Dhana hii huweza kufafanuliwa zaidi kwa mifano Kiswahili; cheza, chezesha, alicheza, chezeka.
Kwa mujibu wa fasili ya kileksika neno la msingi ni ''cheza'' ambalo ndilo limezalisha mengine yote.
Ugumu wa kigezo hiki ni kuwa katika lugha kuna maneno ambayo yakisimama peke yake hayana maana pia hayakuingizwa katika kamusi kama vidahizo ingawa maneno hayo yanapoandamana na mengine yanafanyakazi kama ya kisarufi katika lugha.kwa mfano “ya” “wa”, “cha” yakiwa katika sentensi yana maana.
·        Mtoto wa Juma anasoma Chuo kikuu.
·        Machungwa ya John yameoza.
Pia Katamba (1993:18) anadai  kuwa neno huweza kurejelewa kwa fahiwa mbalimbali yaani neno kama leksimu, neno kama umbo dhahiri, na neno kama neno la kisarufi.
Neno kileksika hurejelewa kama leksimu yaani ni kipashio dhahania chenye kuwakilisha maumbo anuai yanayotokana nacho. Kwa mfano:
  • Mwalimu→ mwalimu walimu
  • Refu → refu, ndefu, mrefu, kirefu
  • Safi→ safi, msafi , wasafi, usafi
  • Pika---> pika, mpishi, upishi
Kigezo cha kisintaksia hudai kuwa neno ni kipashio huru kidogo ambacho huweza kusimama peke yake (Spencer, 1991:42). Katika fasili hii ni kwamba iliwa neno litaweza kusimama peke yake kwa uhuru basi ni neno. Tatizo ni kuwa udogo na uhuru unaosemwa ni upi?  Katika Kiswahili neno ‘japokuwa ni neno huru? Uhuru wake ni upi? Katika kutoa maana yake au kuandikwa bila viambishi? Neno kama hili haliwezi kusimama peke yake likaleta taarifa fulani ingawa ni neno huru.
Ugumu mwingine upo katika kuelezea maneno ambatani yanayotokana na kuunganisha vipashio huru viwili si maneno? Pia katika viangami ni vipashio vidogo lakini si huru kwasababu haviwezi kusimama peke yake na kuleta maana  hivyo basi kutokana na fasili hii, tunapata neno la kisarufi ambapo neno hubadilika maana na umbo kulingana na nafasi lililosimama katika tungo hiyo.
Naye Mdee (2006:5) kama alivyomnukuu Cruse (1986:35) anaeleza sifa kuu mbili za neno. kwanza neno ni kipengele kidogo kabisa katika sentensi ambacho kinaweza kuhamishwa kutoka nafasi moja hadi nyingine bila kuathiri sarufi ya lugha katika sentensi hiyo. yaani maana ya sentensi hudhihirika maneno yanapobadili nafasi,
·        Jana mama alikuja  shule
·        2. Mama alikuja shule jana
Fasili hiyo haitoshelezi kueleza neno hasa ni nini kwani katika sentensi mbili, sentensi ya kwanza maneno yamehama na yameathiri sarufi na kuifanya sentensi hiyo kutokidhi haja za usahihi wa kisarufi.
Sifa nyingine inayobainishwa na Cruse ni kuwa neno ndicho kipashio kisichoruhusu kupachikwa kipashio chochote kati ya vijenzi vyake. Fasili hii ina upungufu kwani kuna uwezekano mkubwa wa kupachika vipashio baina ya vijenzi kwa mfano:
Aina anafundisha darasani.
Katika tungo hii ni wazi kuwa unaweza kupachika vipashio vingine kama bi, Anima, vizuri katikati ya tungo hizo na bado sentensi ikawa na maana kwa mfano:
  • Bi, Amina anafundisha vizuri darasani.
Spenser (1991:42) anadai kuwa kuna sifa chache za kisemantiki zinazoweza kutofautisha neno na vipashio vingine kama mofimu na virai. Japokuwa kigezo cha kisemantiki kinaweza kusaidia kutofautisha maana lakini hakijitoshelezi kufasili neno kikamilifu, kwa mujibu wa kigezo cha kisemantiki neno ni kipashio kidogo cha lugha chenye maana. Fasili hii inamaanisha kuwa neno lazima liwe na maana. Ugumu wa fasili hii unajitokeza katika maneno  yenye maana zaidi ya moja na maneno mawili au zaidi lakini yana maana moja kwa mfano  maneno ambatani kama:
i)                    Askarkanzu
ii)                   Mwananchi
iii)                 Mwanahewa
Pia nahau mfano:
i)                    Amefaa miwani– mlevi
ii)                   Ana mkono mrefu– mwizi
iii)                 Roho ya korosho – roho mbaya
Swali la kujiuliza ni kwamba kipashio kidogo hasa ni kipi na udogo huo ni upi? Na je nahau moja ni neno moja au maneno mawili, matatu tofauti kulingana na tungo kwa kuwa inabeba dhana moja ya neno?  na tungo ambatani ni neno moja au maneno mawili tofauti? Hivyo kigezo cha kisemantiki pekee hakijitoshelezi kueleza kiukamilifu neno ni nini. Katika tungo kama zile za kinahau huwa ni vigumu kupata maana ya tungo kwa kuangalia neno moja moja. Kwa mfano: Anamkono mrefu-mwizi Je, tungo hii ni neno au ni nini? Je, waweza kupata maana kwa kuangalia neno moja moja? Kutojibika kwa maswali hayo yote huonyesha kiini cha ugumu wa kufasili hii ya maana ya neno.
Kigezo cha kifonolojia hulifasili neno kwa kuangalia sauti zinazounda maneno. Fasili ya Massamba, (2004:66) inadai kuwa “neno ni kipashio cha usemaji ambacho hujengwa na mwandamano au mkururo wa sautizilizopangika kisilabi na ambazo hutambuliwa na wasemaji wa lugha inayohusika kuwa kitu kimoja chenye maana mahususi”. utata fasili hii ni kwanza inaangalia neno linalotamkwa au kusemwa tu bila kujali maneno yaliyoandikwa. Pili neno kuwa na maana mahususi ni dhana inayochanganya kama tulivyoona kuwa kuwa maneno yasiyo na maana yake mahususi ni mpaka yahusianishwe na maneno menengi. Kwa mfano: na, wa, cha na kwa. TUKI, (1990:58). naye Spencer, (1991) anaelezea sifa ya fasili ya kifonolojia kuwa katika baadhi ya lugha mipaka ya neno huweza kuonyeshwa kwa mkazo, tangamano la irabu na masharti zuizi ya kifonolojia.
Fasili hizi zina ugumu wake kuwa katika baadhi ya lugha neno huweza kuwa na mfuatano sawa wa silabi lakini likawa na maana tofauti kisarufi. Kwa mfano: neno la Kiswahili paa; neno hili huweza kuwa, enda angani, kitendo cha kuondoa samaki magamba, kuchukua baadhi ya makaa ya moto na kuweka mekoni. Swali lakujiuliza ni kuwa kipashio hiki kina mfuatano wa namna moja tu wa sauti lakini maana tofauti; je, ni maneno matatu au moja?. Katika mtazamo huu pia tunapata maneno ya kifonolojia ambayo hutokana na mfuatano wa silabi zinazotamkwa kama kiunzi kimoja cha utamkaji. Swali lakujiuliza katika ambatano kuna maneno mawili au Je, maneno haya mawili ni tofauti au moja? Hivyo basi kifonolojia yataonekana ni maneno mawili tofauti kwa kila neno lina maana inayojitosheleza lakini maneno ambatani kimaana ni neno moja kwa kuwa lina dhana moja na kimofolojia ni neno moja kwa kuwa uambatani ni njia mojawapo ya kuunda maneno na utata huzidi kuongezeka. Fasili hii huchukulia neno moja moja tu kitu ambacho huleta utata kwa sababu kuna mfuatano wa maneno mawili au zaidi yanayoelezea kitu kimoja.
Kwa kuhitimisha tunaona kuwa ni vigumu kufaili neno kwa kujikita katika kigezo kimoja hivyo ni vyema endapo tutafasili neno kwa kuhusianisha vigezo vyote yaani vigezo vya kisemantiki, kisintaksia, kifonolojia, kiotografia na kileksimu. Pia nivyema kuzingatia lugha mahususi tunapoeleza neno kwa sababu hakuna kigezo majumuu kwa lugha zote duniani kwani kila lugha ina mfumo wake.

MAREJEO
Katamba, F. (1993) Morphology. Macmillan Press LTD, London.
Kihore na wenzake (2001) SAMAKISA. TUKI, Dar es Salaam
Massamba, D. P. (2004). Kamusi ya Isimu na Falsafa ya Lugha. Dar es Salaam: TUKI
Mdee, J. S. (2010) Nadharia na Historia ya Leksikografia. TUKI, Dar es Salaam.
Spencer, A (1991) Morphological Theory: An Introduction to Word Structure in Generative Grammar: Basil Blackwell. UK.
TUKI (2004) Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Oxford University Press, Dar es salaam.

No comments:

Post a Comment