Wednesday 3 July 2013

KISWAHILI NA UCHOTARA

“KISWAHILI NI LUGHA CHOTARA”

(Mhadhara)
Mtazamo huu umezua mjadala mrefu wa kitaaluma kutokana na kwamba, miongoni mwa wataalam wanaounga mkono ni waswahili wenyewe ambao baadhi yao ni mabingwa wa lugha ya Kiswahili. Watu hawa wanajinasibisha na  ama Uarabu au Ushirazi, kwa sura na lugha yao na wengi wao ni wale walioitwa mashombe, ambao miongoni mwao ni; Alamin Mazrui na Ibrahimu Noor Shaarif. Hawa wameandika kitabu chao kiitwacho “The Swahili Idiom and Identity of an African People.”
Waamini wenye mtazamo huu wanaweza kugawanya katika makundi kadhaa:
i.             Wale wanaoamini kuwa lugha ya Kiswahili ilianza kama lugha chotara iliyokuwa inatumiwa na wanaume wa kiarabu na wanawake wa Pwani (ambao hawa kuwa wabantu) Hivyo, kwao asili ya lugha ya Kiswahili ilianza baada ya mwingiliano baina ya wageni na watu wa Pwani ya Afrika Mashariki.

Miongoni mwa watu wanaoegemea katika mtazamo huu ni Freeman Grenville (1959) ambaye aliandika makala iitwayo “Medieval Evidence for Swahili.” Lakini maelezo ya makala yake kwa kiasi kikubwa aliyachota katika kitabu kiitwacho; “Perplus of the Eritrean Sea.” Freeman alitoa maelezo kuhusu watu wa Rhapta, eneo ambalo linasemekana lipo karibu na mto Pangani. Anasema;
“Watu wa Muza huwatoza ushuru na kupeleka huko melindogo. Melindogo nyingi zilikuwa na manahodha wa kiarabu na mawakala wao, hawa wana wafahamu vizuri wakazi wa maeneo haya ya Muza na wanaishi na kuoana nao, na wanaijua lugha yao yote…”

Katika nukuu hii tunaweza kujifunza kwamba;
-     Kiswahili ni lugha Chotara ambayo ilianza mara baada ya ujio wa waarabu katika maeneo ya Pwani.
- Watu wa Pwani wa mwazo waliolewa na waarabu, na hawa kuwa wabantu.
Hapa tunaweza kujiuliza kwamba;
-    Kama hawa waarabu waliifahamu lugha ya watu wa Pwani, kwa nini tena ikazaliwa lugha chotara!
-    Lakini hiyo lugha ya watu wa Pwani waarabu waliyoifahamu ni ipi?
-         Kama watu hawa hawakuwa wabantu, walikuwa watu gani sasa?
-   Athari kubwa ya kibantu katika lugha ya Kiswahili ilitoka wapi sasa?
Mtaalamu mwingine ni Gray (1962). Huyu aliandika kitabu kilichoitwa; “History of Zanzibar from Middle ages 1856” Katika kitabu chake naye alichota mawazo mengi kutoka kwenye “Perplus of the Sea” Mtazamo wake haupishani sana na Freeman. Naye pia anaona kwamba Mswahili na lugha yake ni matokeo ya maingiliano kati ya waarabu na watu wa Pwani. Anasema:
“Yaelekea wafanyabiashara na mabaharia wa kiarabu walikuwa na mazoea ya kuweka makazi ya muda au ya kudumu katika sehemu mbalimbali za Pwani na visiwa vinavyokaribiana navyo….”
 Katika hoja hii tunaweza kupata mambo mawili:
-   Lugha ya Kiswahili ni mchanganyiko wa lugha mbili ya baba ambaye alikuwa mwarabu na mama ambaye ni makabila ya Pwani.
-   Mswahili ni lazima awe mtu aliyezaliwa na baba mwarabu na mama aliyetokea maeneo ya Pwani na makabila ya Pwani.
Mtaalamu mwingine ni Homo Sasson (1980) Katika makala yake iitwayo “The Coastal Town of Jumba la Mtwara.” Katika makala hii anaeleza kwamba;
“Pepo za kaskazi huvuma baina ya mwezi 9 na 3, ambazo ndizo waarabu walizozitumia kuja huku Afrika. Pepo za kusi ambazo ndizo walizozitumia kurudi kwao. Wafanyabiasha waliochelewa pepo za kusi iliwalazimu wakae Pwani kwa miezi 6. Katika kipindi hicho iliwalazimu kuwaoa wanawake wa Kibantu na hapo ndipo Kiswahili kikaanza…”
Kuhusu suala la kuoa wanawake wa Kibantu Homo Sasson anasema kwamba; “aridhi ya Pwani inarutuba nyingi na maisha yake yanavutia haikuwa taabu kwa waarabu kukaa Pwani kwa miaka michache hasa kama wangepata wasichana wa kibantu ambao ndio waliokuwa wenyeji wao. Bila shaka lugha ya Kiswahili ilianza kutokana na mwingiliano wa aina hii.”
Jina lenyewe linatokana na neno la Kiarabu “Sahil” (umoja) na wingi wake ni “Sawahil” likiwa na maana ya Pwani.
Anahitimisha kwa kusema kuwa 80% ya maneno ya Kiswahili yanatokana za lugha ya Kibantu ambayo ndio lugha ya mama na watoto. 20% inatokana na lugha ya Kiarabu ambayo ndio lugha ya baba ya biashara. Ikiwa inajaza mapengo pale ambapo maneno ya Kibantu hayatoshelezi au hayakuwepo kabisa.
Hoja za Msingi:
-         Kwa sababu walikosa usafiri ikabidi waoe wanawake wa Kibantu.
Maswali ya kujiuliza kutona na hoja hii:
1.   Je wakati wa ujio wa Waarabu lugha ya mawasiliano ilikuwa lugha gani? Chotara au Kiarabu?
2.    Lugha ya baba na mama ni ipi?
3.    Je hiyo lugha Chotara ilikuwa inatumika wapi?
4. Na kama lugha ya Kibantu ina 80% na Kiarabu 20% kwa hiyo lugha ya Kiswahili haina msamiati wowote wa lugha nyingine?
5.    Waarabu waliwaoa wale Wabantu halafu lugha Chorata ikatokeaje? Je ndugu zao wengine yaani kaka, dada, wazazi, shangazi walitumia lugha gani?
6.    Kama Kiarabu ni 80% hivi hiyo dhana ya uchotara inatoka wapi?

 KISWAHILI NI PIJINI
(Itaendelea wakati mwingine...)

No comments:

Post a Comment