Monday 1 July 2013

UAMILIAJI LUGHA NA UJIFUNZAJI LUGHA



Tofauti kati ya uamiliaji lugha na ujifunzaji lugha.
Mwanadamu anapozaliwa anakuwa na bohari la sauti mbalimbali zisizo na maana yoyote, na mara anapoanza kuishi katika jamii ndipo huanza kuibua sauti hizo katika mazingira ya kinasibu (pasipo yeye mwenyewe kutarajia) na kuanza kuzitafutia maana sauti hizo. Uibuaji wa sauti hizo huendana sambamba na mambo yanayomzunguka pamoja na yale anayoyatumia.
Hii tunaona hata kwa watoto wachanga jinsi wanavyoanza kuongea, kwanza huanza kwa kutoa sauti zisizo na maana yoyote kisha kadiridi wanavyokuwa ndivyo sauti hizo zinaanza kubadilika mpaka zikaeleweka na watu wanaomzunguka. Yote haya ufanyika kutokana na msaada wa mazingira, muda pamoja na jamii inayomzunguka.
Hivyo basi tunaona kwamba dhana ya uamiliaji lugha huanza mara tu mtoto anapozaliwa kisha hufuatiwa na dhana ya ujifunzaji lugha. Pamoja na hayo yote wapo wataalam mbalimbali waliojaribu kuelezea dhana hizi mbili kwa mapana zaidi huku wakitoa tofauti mbalimbali kati ya uamiliaji lugha na ujifunzaji lugha.  

Kwa kuanza na maana ya lugha, wanaisimu wengi wamewahi kutoa fasili mbalimbali kuhusiana na dhana ya lugha, miongoni mwa wanaisimu hao ni pamoja na;
Trudgil (1974) ambaye amenukuliwa na Mgullu (1999). Anasema kuwa “Lugha ni mfumo wa sauti za nasibu zinazotumiwa kwa mawasiliano miongoni mwa watu wa jamii fulani yenye utamaduni wake.
Mtaalam mwingine ni Sapir (1921) ambaye anasema kuwa Lugha ni mfumo ambao mwanadamu hujifunza ili autumie kuwasilishia mawazo, maono na mahitaji. Mfumo huu hutumia ishara ambazo hutolewa kwa hiari.
TUKI (1990) inasema: Lugha ni mfumo wa sauti zinazotumiwa na watu wa jamii fulani wenye utamaduni unaofanana ili kuwasiliana.
Kwa mujibu wa Msanjila na wenzake (2011) wakimnukuu Massamba (2004:19) wanasema kuwa “Lugha , kwa upande wake, hufasiliwa kuwa ni mfumo wa sauti nasibu ambazo zimebuniwa na jamii kwa madhumuni ya mawasiliano kati yao”. Jambo la msingi la kuzingatia katika fasili hii ni kuelewa kwamba dhima kuu ya lugha ni kuwezesha mawasiliano miongoni mwa jamii yaweze kufanyika.
Hivyo basi katika fasili zote hizi tunaweza kusema kuwa wataalam hawa kimsingi wanakubaliana kuwa lugha ni mfumo wa sauti za nasibu ambazo zimekubalika zitumike miongoni mwa wanajamii kwa lengo la kuwasiliana.
Pia dhana ya uamiliaji lugha imefasiliwa na Garman pamoja na Fletcher (1986) kama walivyonukuliwa na Hickman; wanasema kuwa, Uamiliaji lugha hautokei katika ombwe (patupu) kadiri watoto wanavyoamili lugha wanaamili mfumo wa ishara ambazo zinaonesha uhusiano muhimu katika nyanja ya ubongo na nyanja ya jamii katika maisha.
Naye Stephen Krashen na Tracy D.T (1983) wamejaribu kuelezea dhana hii ya uamiliaji. kwa kusema kuwa uamiliaji ni mchakato unaotokea katika nafsi iliyofichika akilini mwa mtu ambayo ndiyo imuongozayo kuongea au kuandika kwa urahisi. Hivyo wao wanaona kuwa uamiliaji hujitokeza kwa mtu katika hali ya ung’amuzi bwete pasipo muhusika mwenyewe kujitambua.
Na katika ujifunzaji lugha, Krashen na Tracy (1983) wanadai kuwa ujifunzaji ni mchakato wa kiufahamu wa kiakili au utambuzi wa nafsi unaojionesha katika kujifunza sharia na kanuni na miuundo ya lugha. Hivyo basi katika dhana hii wao wanaona kuwa ujifunzaji ni tukio la kiutambuzi, yaani mtu ana kuwa anafahamu au anatambua kuwa anajifunza lugha hivyo atapaswa kuzingatia kanuni na muundo wa lugha.
Mtalaam mwingine ambaye anaonesha kukubaliana na akina Krashen na mwenzake ni Gleason (1989) ambaye naye anaona kuwa uamiliaji lugha ni sawa na tukio linalotokea katika ung’amuzi bwete wakati ujifunzaji hutokea katika ung’amuzi tambuzi. Katika kuthibitisha hilo anasema kuwa;
Ujifunzaji lugha unazingatia kujua vipengele muhimu vya lugha ambavyo si lazima kuvifuata au kuvijua katika uamiliaji lugha bali vinakuja vyenyewe pasipo utambuzi au pasipo kujua. Vipengele hivyo ni kama vile; fonolojia, mofolojia, sintaksia, semantiki na pragmatiki.
Baada ya kutazama fasili na mitazamo mbalimbali iliyotolewa na wataalam hao juu ya lugha, uamiliaji lugha na ujifunzaji lugha, zifuatazo ni tofauti zilizopo kati ya Uamiliaji lugha na ujifunzaji lugha.
Uamiliaji lugha hutokea katika ung’amuzi bwete yaani pasipo mtoto wenyewe kujitambua kiakili, anajikuta tu ana uwezo wa kuzungumza vizuri bila kujua kwa nini anazungumza hivyo, wakati ujifunzaji lugha ni tukio la kiutambuzi. Yaani mtu anajua fika kwamba anajifunza lugha.
Vile vile katika uamiliaji lugha si lazima kufuata sharia na kanuni za lugha au vipengele vya lugha lakini katika ujifunzaji lugha lazima mtu aelewe vipengele vyote muhimu vya lugha.
Pia katika ujifunzaji lugha lazima kuwepo na mwalimu ambaye ni mtaalam wa lugha pamoja na mazingira fulani muhimu ambayo yatamfanya yule mjifunzaji lugha kuweza kujifunza lugha kwa urahisi zaidi. Mfano wa mazingira hayo ni kama vile shule au taasisi maalum kwa ajili ya ujifunzaji lugha. Lakini katika uamiliaji lugha haitajiki mtaalam wa lugha wala mazingira maalum kama hayo.
Vile vile katika uamiliaji lugha utamaduni wa jamii husika hauzingatiwi sana lakini katika ujifunzaji lugha lazima mjifunzaji lugha aelewe na azingatie utamaduni wa jamii husika ili kuepuka makosa ambayo yanaweza kusababisha uhusiano mbaya na wanajamii husika.
Vile vile uamiliaji lugha ndiyo unaotangulia kisha hufuatiwa na ujifunzaji lugha. Yaani mtoto huanza kuzungumza pasipo kujua taratibu za lugha kama vile, muundo wa lugha, kanuni za lugha na utamaduni wa lugha husika. Baada ya kujua kuzungumza ndipo hufundishwa sharia mbalimbali za lugha husika.
Pia kwa mujibu wa Jean (1992:123) anasema kuwa katika uamiliaji lugha watoto wachanga wanakuwa makini katika lugha tangu wanapozaliwa. Wanaanza kutoa maneno yanayotambulika katika kipindi cha miezi 12-15 na kuanza kuyaunganisha maneno hayo kuanzia miezi 18. Anaendelea kusema kuwa watoto wote wasio na matatizo ya kimaumbile na baadhi ya wenye matatizo, wataanza kuongea ikiwa watasikia lugha ikizungumzwa katika mazingira walimo. Hii ni tofauti na ujifunzaji lugha kwani mtu hata waze kujifunza lugha kwa njia ya kusikia tu.
Tofauti nyingine ni kwamba uamiliaji lugha una kikomo lakini ujifunzaji lugha hauna kikomo kwani unaendelea katika umri wowote haijalishi kijana au mzee.
Hivyo basi ninaweza kuhitimisha kwa kusema kuwa mtu yeyote anao uwezo wa kujifunza lugha na kuifahamu ikiwa tu atakuwa na akili timami pamoja na ala sauti zote zinazohusiana na ujifunzaji lugha ambazo hazijaathiriwa au kuathirika sambamba na kupewa mazingira ya kijamii ya kujifunza lugha ingawaje hatafikia uwepo wa uamiliaji.

MAREJEO:
Aitchison, J. (1992). Teach Yourself: Linguistics. (4th ed). Hodder & Stoughton Ltd Britain.
Berko, G.J. (1989). The Development of Language. A. Bell & Howell Information Company.
Fletcher, P. and Garman, M. (1986). Language Acquisition. Cambridge University Pess.
Krashen, Stephen D. and Tracy D. Terrell (1983). The Natural Approach. Language Acquisition in the Classroom: Pergamon Press. Oxford.
Mgullu, R.S. (1999). Mtalaa wa Isimu: Fonetiki, Fonolojia na Mofolojia ya KiswahiliDar es Salaam. Longhorn Publishers (T) Ltd.
Msanjila, Y.P. na wenzake. (2011). Isimujamii: Sekondari na Vyuo. TUKI. Dar es salaam
TUKI (1990). Kamusi Sanifu ya Isimu na Lugha: TUKI. Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment