Thursday, 23 May 2013

MWINGILIANO MATINI KATIKA TENDI



MATUMIZI YA MTINDO WA MWINGILIANOMATINI KWENYE TENDI
Macha, Noel E.

Ikisiri.
Makala  haya yana lengo la kutaka kujua kama tendi za Kiswahili huwa na mwingiliano matini  na  kubainisha  vipengele  vilivyoingiliana katika utanzu huu na dhima zake. Waandishi wa tendi mbalimbali za Kiswahili, wamekuwa wakitumia mtindo wa kuchanganya vipengele mbalimbali vya kisanaa katika kazi moja. Mbinu hii inatazamwa na makala haya kuwa ni mwingiliano matini katika tendi za Kiswahili. Mathalani, mwandishi  anayeandika  au simulia tendi za Kiswahili, hujikuta akichanganya matini za nyimbo, semi, hadithi  ndani  ya  hadithi,  maigizo,  matumizi ya ishara, ngoma  na  kadhalika.  Kuchanganya  huko  kwa vipengele  tofauti  katika  kazi  moja  ni  kitu  ambacho  kimezoeleka  sana  miongoni  mwa wanafasihi. Kipengele hiki kinahitaji kuandikiwa ili kuweza kuweka bayana kuwa katika tendi kunaweza kuwa na sifa mbalimbali za tanzu nyingine na kuziorodhesha ili zijulikane wazi. Hivyo makala haya yatakuwa na lengo la kuthibitisha uwepo wa mwingiliano huo.
1.0   Utangulizi
Mwingilianomatini  katika kazi za fasihi  ni  dhana  ambayo  imekuwa  ikijitokeza  sana kwa  sababu  mbalimbali  za  kifasihi. Wakati  mwingine  mwingiliano huu hubainishwa kabisa  na wataalamu wa  fasihi  simulizi kama  mtindo wa kawaida katika kumbo za fasihi. Kwa mfano, Mulokozi (1989)  anasema  kwamba mojawapo  ya  sifa  kuu  ya  fasihi  simulizi  ni  vipera  vyake  kuingiliana  katika utendaji.  Pamoja  na  mtindo  huo  kuwa  wa  kawaida  katika  fasihi,  bado  sababu zake hazijabainishwa wazi katika uhakiki wa kazi za fasihi. Kwa  mantiki  hiyo, kuna  haja  ya  kuchunguza  sababu  zake  ili  kupanua  uelewa  katika  taaluma  ya fasihi. Makala haya yana lengo la kuzionesha sababu hizo za kuingiza vipengele mbalimbali vya kisanaa katika fasihi kwa kuchunguza tendi.
Pengine, tuanze kwa kujiuliza swali, mtindo ni nini? kisha tutafasili dhana ya mwingiliano matini, tendi, kisha tutaangalia vipengele ambavyo vimeingiliana katika tendi za Kiswahili na dhima zake na mwisho ni hitimisho.
Tukianza na fasili ya mtindo; Senkoro (2011) anasema mtindo katika kazi ya fasihi ni ile namna ambayo msanii hutunga kazi hiyo na kuipa sura ambayo kifani na kimaudhui huainisha kanuni au kaida zilizofuatwa kama ni(za kimapokeo) au ni za kipekee. Wamitila K.W (2008) anasema mtindo ni sifa ya upekee ambayo huitambulisha kazi ya mtunzi au msanii fulani.
Kwa ujumla fasili hizi hazipishani sana, ukizichunguza utagundua kuwa mtindo hujihusisha na namna ambayo msanii huitunga kazi yake ambayo huwa na upekee wa namna fulani; upekee huu ndio unaoweza kuwatofautisha waandishi. Hivyo basi kwa kutumia mtazamo wa kimtindo tunaweza kufasili mwingilianomatini kama alivyofasili Senkoro (2011) kuwa ni mbinu ambayo huonyesha kutumiwa kwa utanzu mmoja wa fasihi katika kutolea au kuwasilisha utanzu mwingine. Kwa mfano; si jambo geni kukuta wimbo au kipande cha wimbo ndani ya ngano au hadithi. Hivyo basi tunaweza kusema kuwa mwingilianomatini ni ule uwepo wa sifa mbalimbali za matini moja au zaidi katika kazi fulani ya fasihi kama vile matumizi ya nyimbo, matumizi ya barua, ngoma, masimulizi ya hadithi ndani ya hadithi, misemo, nahau, majibizano, vicheko, picha na michoro na kadhalika. Baada ya hapo tuangalie tendi ni nini? Jibu la swali hili ni muhimu ili kupata uelewa wa awali katika hoja za makala haya. Zipo maana kadhaa zinazotolewa na wanafasihi mbalimbali  kuhusu dhana ya tendi.
Mulokozi (1996) anafafanua tendi kuwa, ni utungo wenye kusimulia matukio ya kishujaa yenye uzito wa kijamii au kitaifa. Matukio haya yaweza kuwa ya kihistoria lakini tendi nyingi huchanganya historia na visakale au visasili. TUKI (2004) wanasema tendi ni utanzu unafaa kusherekewa kishujaa. Hii inaonyesha kuwa tendi zinahusu matukio ya kishujaa yaweza kuwa ya kweli au ya kubuni, na yenye funzo fulani kwa jamii.
Kutokana na fasili ya tendi tunayopata kupitia maoni ya wataalamu hawa tunabaini kuwa utendi ni mojawapo ya tanzu za kazi za kifasihi. Utanzu huu unaweza kuwa katika umbom la kiusimulizi au la kiuandihi. Kwa mantiki hiyo, tendi kama zilivyo tanzu nyinginezo za kifasihi huwa na mitindo anuai. Mojawapo ya mittindo yake ni suala la mwingiliano matini.
Data  ya  makala  haya  imepatikana  kutoka  katika  sampuli  ya kitabu  cha Utenzi wa Nyakiiru Kibi kilichoandikwa na Mulokozi (1997). Uteuzi wa kitabu hicho kama sampuli umefanyika kwa nasibu. Unasibu huo umetokana na imani kuwa mbinu hii ya mwingilianomatini hujitokeza katika tendi zote. Hivyo  hakukuwa  na haja  ya  kuweka  vigezo  vingi  vya  uteuzi.  Lakini,  kwa  ujumla  makala  imeteua kitabu  hicho  kwa  kuzingatia  kigezo cha matukio yake  kuwa  na  ujumbe kwa jamii, lugha rahisi, muundo sahili. Utenzi huu unasimulia historia ya kuanzishwa kwa utawala wa ukoo wa Babito katika nchi ya Kiziba, wilaya ya Bukoba, karne ya 15. Babito walikua ni wahamiaji wa Kiluo kutoka Uganda.Walifika Kiziba kutokea Bunyoro nchini Uganda, ambako walikuwa tayari ni watawala. Historia ya Babito katika maeneo haya inaonyesha namna watu wa jamii na lugha mbalimbali hapo kale walivyokua na ushirikiano mzuri katika kujenga utaifa na ustawi wao. Siasa za ukabila na ubaguzi hazikua na nguvu. Mhusika mkuu katika andiko hili ni Nyakiiru. Huyu anasimuliwa kama mhusika shujaa. Nyakiiru alikua ni kiongozi wa kundi la Babito lilofika Kiziba kama mwaka 1945; ambapo alishirikiana na Kanyamaishwa, ambaye alikuwa ni mototo wa mfalme wa Kiziba aliyeitwa Ntumwa, kumwua mfalme huyo na hivyo kujichukulia madaraka ya utawala.
Hadithi ya utenzi huu imetokana na masimulizi ya wazee ambayo yamehifadhiwa katika vichwa vya watu na kupokezwa kwa mdomo tangu karne ya 15. Hata hivyo yako mambo kadha ya msingi ambayo yanajitokeza takribani katika masimulizi yote. Mambo hayo ndiyo mwandishi amejaribu kuyatumia kama kiini cha utenzi huu na amejaribu kuyapanga kisanaa ili kupata hadithi nzuri na yenye mshikamano na mtiririko mzuri unaofaa, na wenye mafunzo fulani kwa vizazi vya leo. Hivyo utenzi huu hausimulii historia kavu, bali unasimulia hadithi ya kusisimua inayotokana na historia iliyochanganyika na visakale ambayo ni masimulizi yanayohusu mashujaa wa kale ambayo yamechanganya ubunifu ndani yake na yaweza kuwa ya kweli au ya kubuni. Utenzi huu umekusudiwa usomwe na vijana. Hivyo lugha yake imerahisishwa kidogo ili ieleweke vizuri kwa walengwa.
2.0  Mwega wa Kinadharia
Makala haya yataongozwa na mwega wa kinadharia wa mwingilianomatini. Ili hadhira ya fasihi ielewe kazi yoyote ya fasihi lazima ihusishe vipengele vingine nje  ya  muktadha  wa  usomaji  au  usimulizi  ule  (Mshengyezi,  2003).  Dhana ya kuingiza vipengele hivi ndiyo huitwa mwingilianomatini.  Wataalamu
wanaounga mkono mawazo ya nadharia hii wanamtaja mwasisi wa nadharia hii kuwa ni Mikhail M. Bakhtin ambaye alikuwa mwanaisimu na mhakiki wa kazi za fasihi aliyeishi kati ya mwaka 1895-1975 (Njogu na Wafula, 2007). Njogu na Wafula  wanazidi  kusema  kuwa  Bakhtin  aliamini  kwamba  kazi  ya fasihi ina sauti mbalimbali  zinazoingiliana  na kupiga  mwangwi  katika  kazi  nyingine zilizotangulia,  zilizopo au  zitakazokuja  baadaye. Ufafanuzi  huo pia  uliwahi kutolewa  na  Wamitila  (2006)  aliposema  kuwa  Bakhtin  anaamini  kuwa  utanzu wa riwaya una uwezo wa kuingiza vipengele vya tanzu nyingine lakini ukabakia na  sifa  zake  kama  utanzu.  Hali  hiyo  ndiyo  pia  hujitokeza  katika  tendi mbalimbali  za  Kiswahili  ambazo  zina  mwingiliano  na  vipengele  vingi  sana katika  kazi  moja.  Kwa  ufafanuzi  wa  Wamitila,  utanzu  wa  fasihi  kuwa  na vipengele  vingine  ndani  yake  hakuondoi  hadhi  ya  utanzu  huo.  Kwa  ujumla, tunaposema  kuingiliana  kwa  matini  katika  kazi  za  fasihi  tunamaanisha  kazi moja ya kifasihi kuwa na sifa za tanzu nyingine ndani yake. Kabla hatujaenda kuona vipengele hivyo vilivyojitokeza katika tendi hebu tuangalie kwanza sifa za kifani za tendi za Kiswahili.
3.0    Sifa za Tendi za Kiswahili
Molukozi (1996) kama alivyomnukuu Finnegan (1970:108) anasema kuwa utanzu huu hautokei sana katika Afrika, pamekua na mjadala mrefu kuhusu fani hii. Wataalamu kama Okpewho (1979) Johnson (1986) Mulokozi (1987) na wengine wamethibitisha kuwa utendi ni fani iliyoenea sana katika Afrika, na wamejeribu kuonyesha baadhi ya sifa zake. Finnegan alibainisha sifa nne za tendi simulizi:
(i)                  Nudhumu: Utendi aghalabu ni utungo wa kishairi.
(ii)                Urefu: Anasema ni utungo mrefu.
(iii)               Upatanifu:  Anasema ni utungo ambao una visa vilivyounganika kimantiki.
Aidha Mulokozi anaendelea kusema kuwa zaidi ya sifa za utendi alizoelezea Finnegan, ambazo wengi wanaona hazitoshelezi, uchunguzi wao umedhihirisha kuwa utendi una sifa zifuatazo:
(i)              Hutolewa kishairi
(ii)            Huhusu matukio muhimu ya kihistoria au kijamii;
(iii)          Huelezea habari za ushujaa na mashujaa; hii inamaanisha kuwa husimulia juu ya maisha na matendo ya kishujaa ya mbabe wa utendi, kwa mfano kuzaliwa kwake, maswaibu yake, safari zake, uongozi wake kwa watu wake, na kifo chake.
(iv)   Matini (maneno) yake kwa kawaida hutungwa papo kwa papo (utendi hautungwi kabla ya kuhifadhiwa kichwani kwanza ili badaye utolewe kwa ghibu).
(v)           Hivyo, hutawaliwa na muktadha wa utungaji na uwasilishaji wake kwa jamii.
Baadhi ya tendi muhimu za Kiafrika ni Sundiata (au Sunjata) (Mali, Gambia, nk) Mwindo (Zaire), Silamaka (Mali) na Mvet (Gabon). Katika Afrika Mashariki, tunao ushahidi kuwa tendi ziko au zilikwepo katika jamii zifuatazo: Wachaga (Mlire); Wahehe (Mukwavinyika); Wanyambo na Wahaya (Kachwenjanja, Mugasha, nk); Wakwere na Wazinza. Anasema hata hivyo, uchunguzi bado hujakamilika, na huenda zipo jaamii nyingine zenye utanzu huu. Hatuwezi kupinga hoja za mtaalamu huyu wa fasihi kwani hoja zake zinaonekana kuwa na ushawishi kuwa tendi zilikwepo na pia zina sifa kama hizo alizobainisha hususani kuhusu mashujaa na matukio ya kishujaa;  yaweza kuwa ya kweli au ya kubuni au ya kihistoria. Hii ni kwa sababu tendi ni sanaa inayoambatana na hali fulani ya kijamii, hasa ile hali yenye vuguvugu la mapambano, na yenye asasi (kama vile ufalme)  zinazoweza kuidhamini sanaa ya utendi. Hii ni sanaa ambayo hufa, kwa vile mazingira yanayoilea na kuirutubisha hayapo tena, hivyo ni muhimu kuzirekodi na kuzihifadhi zile tendi chache tulizo nazo kabla hazijatoweka au kusahaulika kabisa na kupotea katika jamii. Baada ya kuona sifa hizo za tendi za Kiswahili sasa tuangalie vipengele vilivyojitokeza katika utanzu huu.
4.0   Tanzu Zinazojitokeza katika Tendi za Kiswahili
Tanzu  zinazojitokeza  katika  tendi  ni  nyingi, lakini  hapa  tutatumia  vipengele vichache tu vinavyojitokeza katika tendi za Kiswahili. Katika Utenzi wa Nyakiiru Kibi kuna vipengele au sifa mbalimbali za tanzu  nyingine ambazo mwandishi ameziingiza katika  utanzu huu, tanzu hizo ni kama hizi  zifuatazo:
4.1   Picha au Michoro mbalimbali
Makala yanatumia dhana ya picha na mchoro yakimaanisha uwakilishi wa sura ya  mtu/watu  au  kitu/vitu au mahali  kwenye  karatasi  au  kitu  chochote  kinachoweza kuandikwa  juu  yake. Sura  hiyo  inaweza  kuwa  imechorwa, imechongwa au tengenezwa. Katika utanzu huu picha zinaonekana katika jalada, pia katika ukurasa wa 1,2, 3, 7,8, 9,10,11, 12, 15 19, 20, 23, 24,25, 26, 28, 30, 33,39,44,50,54, 55, 60, 61, 64, 65,66, 69,75,83,87, 88,90 na 91. Mwandishi amejaribu kutumia michoro na picha katika utanzu huu ambako inasaidia kutoa ufafanuzi wa kina juu ya matukio yaliyojitokeza katika utenzi huu na vile vitu vilivyotumika katika utenzi huu na maeneo mbalimbali yaliyohusika au husishwa katika kukamilisha matukio au utendekaji wa matukio mbalimbali na picha za watu mbalimbali.
Kwa mfano katika jalada la kitabu mwandishi ameonesha mchoro wa ngoma ikimaanisha ngoma ni chombo muhimu cha kijadi katika jamii na picha za vibuyu hii ikidhihirisha kuwa kuna mambo ya kijadi yaliyokua yakitendeka katika jamii zetu na hii inaonesha uzalendo kwa kuenzi utamaduni wetu; pia katika kurasa za mwanzoni kabisa kunaonekana picha za watoto wamekaa wanasoma vitabu ikionesha kuwa ni ishara ya kuhamasisha watoto wajijengee utamaduni wa kujisomea vitabu, bado katika kurasa hizo kuna michoro ya ramani ambazo zinaonyesha maeneo yaliyozungumziwa katika utenzi huu; hii inasaidia wasomaji kuelewa kwa urahisi kile kilichozungumziwa katika kazi hii na kuweza kuvuta hisia zaidi na kujijengea taswira za ulimwengu mpya.
Aidha tukiangalia katika ukurasa wa 10,25,44,50 na 88 tunaweza tukaona jinsi mwandishi ameonesha picha za baadhi ya matukio yaliyokua yanatendeka mfano upigaji wa ngoma, Nyakiiru akipambana na chui, mapambano katika ukurasa wa 88 ambako Nyakiiru alitoka na jeshi lake akaenda kushambulia maadui Bugandika na watu wakauana sana; kwa kuangalia picha hizo zinavuta hisia za huzuni na wakati mwingine zinatujengea ujasiri kutokana na matukio ya kishujaa yaliyotokea. Katika tendi simulizi, dhana ya picha hujitokeza kwa sifa kadhaa za mwonekano wa wahusika wa tendi  zinazofafanuliwa  na  msimulizi  mbele  ya hadhira. Kwa  mfano, wadudu  watapewa  sifa ya jitu  kubwa  lenye  uwezo  wa kufanya maajabu makubwa kijiji  kizima, kwa mfano katika ukurasa wa 75  katika ubeti wa 724 na725 mwandishi amechora picha zinazoonesha jinsi senene walivyoweza kutishia kijiji kizima cha Baziba.

              724     Senene kwenye mashamba                 725     Senene miti kishika
                        Matawi yanavunjika                                      Senene kwenye miamba
                        Kwenye mapaa ya nyumba                            Matunda yanaanguka
                     Na mashina kupembea!                                     Senenewakatambaa!
Hivyo kipengele hiki cha michoro na picha mbalimbali ni moja ya sifa za utanzu mwingine ambazo tunaweza kusema zimeingizwa katika tendi, na michoro hii imesaidia kufanya matukio yaweze kueleweka kwa urahisi pale ambako hayakueleweka vizuri aidha yamepelekea kuleta uhalisia wa matukio na visa hivyo kwa  hadhira na jamii nzima. Hivyo michoro hukazia uelewa na kufikisha ujumbe kwa urahisi na kuimarisha maudhui, uhalisia wa jambo na huleta mvuto kwa wasomaji na kuchochea udadisi kwa hadhira.
4.2  Hadithi ndani ya Hadithi
Hadithi ndani ya hadithi  ni  dhana  inayomaanisha  simulizi  moja  kuingiliwa  na nyingine. Kwa  mfano, mwandishi kama msimulizi mkuu wa hadithi  anampa nafasi  mhusika  katika  hadithi kusimulia hadithi  nyingine. Katika  dhana  hii  kunakuwa  na  hadhira  tofauti  kutokana  na idadi  ya  usimulizi.  Mathalani, tunaposoma  hadithi  halafu  ndani  ya  hadithi  hiyo  tukakuta  mhusika  mwingine ndani ya hadithi hiyo akiwasimulia  wengine, hapo tunakuwa  na hadhira ya aina mbili. Sisi kama wasomaji  tunakuwa  hadhira,  na  wale  wanaosimuliwa  na mhusika  katika  hadithi  nao  pia  ni  hadhira  nyingine.  Kwa mfano, ndani ya hadithi ya kitabu cha Nyakiiru Kibi kuna wasimulizi wawili. Mmoja ni mwandishi mwenyewe akisimulia historia ya kuanzishwa kwa utawala wa ukoo wa Babito katika nchi ya Kiziba ambapo naye anasema hadithi hii imetokana na masimulizi ya wazee yaliyohifadhiwa kwenye vichwa vya watu. Msimulizi  mwingine ni Nyakiiru  wa hadithini  na Kanyamaishwa  wakimsimulia Mtukufu wa Omukama wa Jamala kuhusu maisha yao na walikotokea na jinsi walivyokua wanaishi na kazi waliyokua wanaifanya toka utotoni, ujuzi  walionao  na nasaba yao kwa ujumla. Hapa tunaona jinsi kipengele hiki kilivyojitokeza katika tendi hii na Nyakiiru na Kanyamaishwa wamekua kama wasimulizi na Mtukufu Omukama kawa kama hadhira katika ukurasa wa 67 ubeti wa 634 hadi 641.
Pia usimulizi mwingine unaonekana ukurasa katika wa 80 ubeti wa 775 hadi 780 ambako kuna masimulizi juu ya safari ya Nyakiiru na Kanyamaishwa walipokua wanaelekea Ikulu kwa Sulutani. Hata katika ukurasa wa 6 mwandishi amejaribu kuingiza masimulizi katika ubeti wa 55 ambako inaelezwa habari za kuwepo kwa Sulutani enzi za zamani ambaye alikua mkali kupindukia. Hivyo masimulizi haya yanasaidia kuingiza vionjo mbalimbali katika  tendi na kuendeleza uwepo wa matukio mbalimbali katika tendi hii huwafanya hadhira wasichoke kufuatilia matukio yanayoelezwa katika tendi na  kuongezea ufahamu wa mambo mbalimbali na kuyahusianisha na mazingira yao ya kila siku. Hiki nacho ni kipengele ambacho pia kinajitokeza  katika kazi za kifasihi kama vile tendi kwa sababu katika kila tukio huenda kukawa na tukio jingine ndani yake au kinachohusiana na tukio hilo,hivyo mwingiliano wa matukio hayo ndiyo unaopelekea uwepo wa mtindo wa mwingiliano matini katika  tendi za Kiswahili.
4.3  Maigizo
Maigizo  ni  matendo  ya  kumithilisha  kitu  au  tabia  fulani  kwa  nia  ya  kufikisha ujumbe  kwa  jamii. Matendo yanayoweza kuigizwa ni kama vile uchawi, ulevi, ugomvi, matambiko, uganga, michezo ya ngoma, kusalia miungu, mapambano, uwindaji, unyanyasaji, kuzaliwa kwa mtoto na  kadhalika.  Mambo  hayo hufanywa  na wahusika wa kimaigizo  mbele  ya  hadhira  ili  kufikisha ujumbe. Matendo  yanayofanywa  na  wahusika  wa  kimaigizo  siyo  halisi  kwa  kuwa wahusika wa kifasihi sio watendaji wake halisi, bali wahusika huvaa tu uhusika kama  nguo kwa  muda  ili kuwakilisha watendaji  halisi  katika  jamii.
Aidha, maigizo  ni kipengele  mojawapo  cha  sanaa  za  maonesho  chenye  sifa  zifuatazo:  dhana inayotendeka,  uwanja  unaotendewa, watendaji, hadhira (watazamaji), kusudio la kisanaa, muktadha wa kisanaa na ubunifu (Mulokozi, 1996). Katika tendi mara nyingi fanani hulazimika kuingiza matini  ya  maigizo  katika  usanii  wake.  Endapo  matukio  yanayotokea  katika  kisa  chake  yanaweza  kuigizika  basi  anayehadithia  hulazimika  kuigiza.  Kwa  mfano,  msimuliaji  wa hadithi  akisimulia  hadithi  yake  yenye  mhusika au wahusika  wanaoimba basi  msimuliaji  huyo  hujikuta  akiimba   mbele  ya  hadhira.  Huu ni uigizaji.  Kuna matendo   mbalimbali ambayo yameigizwa katika utenzi huu, yalikua yanatokea katika jamii kama vile uwindaji, mambo ya uganga au matumizi ya waganga jadi, wazee wa jadi na imani za kishirikina. Mfano uk. 18:156 mwandishi anaonyesha jinsi jamii ya Kiziba ilivyokuwa inaamini kutokana na maajabu yanayotokea katika jamii mfano Mtoto wa Malikia alivyotangulia kuota meno ya juu, waliamini kuwa ile ni ishara ya kutokea kwa balaa badae;
Pia kuna maigizo ya matambiko ambako familia ya Mfalme iliamua kutambikia baada ya kuona mwanao ameanza kuota meno ya juu wakahisi huu ni mkosi au kisirani katika familia yao kwa mfano katika ukurasa wa 47 ubeti wa 439 mwandishi anasema;  
            439      Sala wakazitongoa
                        Tambiko wakazitoa
                        Zipate kuwafikia
                        Miungu  wenye afua.
Aidha uigizaji   uliendelea katika mambo mengine yaliyokua yanatokea katika jamii kama vile unywaji wa pombe (ulevi) ambapo inaoeshwa kuwa jamii ilikua inakunywa pombe ili kupunguza mawazo au kusahau maswaibu yanayowakumba  na wakati mwingine kuongeza ujasiri wa kutenda jambo fulani kwa mfano katika  ukurasa wa  409 na 412 anaonyesha akina Nyakiiru  na Kanyamaishwa  walivyokua wanakunywa pombe mpaka  wanalewa kisha wanachukua silaha zao wanaenda mawindoni.                       
            409      Wote wamekwishalewa                                  
                        Na hawakujitambuwa
                         Mutalala  kazidiwa
                        Wengine  kuwapitia.
Maigizo mengine yalikua ya sherehe ambako tunaona familia ya mfalme ilikua inasherekea kuzaliwa kwa mtoto wa Malkia. Haya tunayaona katika ukurasa wa 9 ubeti wa 75 na 76 wanajamii wakihamasishwa kusherekea kwa kupita ngomezi (la mgambo).
              75     Likipigwa la mgambo                 76 “Malkia   mtukufu
                       Likilia lina jambo                           Kazaa mwana nadhifu
                    “Ikuluni kuna mambo                      Mwingine hafui dafu
                      Kajifungua malkia                        Kunawiri kazidia.”
Kipengele hiki cha maigizo huwa kinajitokeza sana katika kazi za kifasihi ikiwemo tendi kwa lengo la  kuweka msisitizo wa yale matukio yanayotendeka  katika jamii na kuleta uhalisia aidha wakati mwingine kuifanya jamii iamini kuwa matukio hayo yapo na bado yanatokea katika jamii na kujifunza kupitia matukio hayo. Hivyo kuwepo kwa kipengele hicho kinawakilisha mwingilianomatini katika tendi.
4.4  Semi
Semi  ni  tungo  au  kauli  fupifupi  za  kisanaa  zenye  kubeba  maana  au  mafunzo muhimu  ya  kijamii.  Semi  zinajumuisha  tanzu  kama  vile  methali,  vitendawili, mafumbo,  misimu,  lakabu  na  kauli-tauria  (Mulokozi,  1996). Fasili  hii ya Mulokozi haitofautiani sana na ile ya M’Ngaruti  (2008) anayesema kuwa  semi ni  tungo  au  kauli  fupi  za  kisanaa  zinazobeba  maana  au  mafunzo ya kijamii. Katika tendi watunzi wengi huingiza semi mbalimbali kwa lengo la kufikisha ujumbe kwa jamii fulani au wakati mwingine hutumika katika kuonya au kukataza jambo na kutoa tahadhari. Katika utenzi huu pia tunaona mwandishi ameingiza semi mbalimbali kama tunavyoziona katika kurasa zifuatazo 35, 37, 38, 48, 58 na 68. Semi hizo ni kama zifuatazo;
·         Misuli ya dume katika uk. 35:307.
·         Usiku wa kiza katika uk.35:310.
·         Wakata nguu na nyanda katika uk.36:320.
·         Giza ni mama wa nuru katika uk.37:331.
·         Uongozi si udhuru katika uk.37:333.
·         Penye mamba pana mto katika uk.38:345.
·         Penye moshi pana moto katika uk.38:345.
·         Maisha yangu ni yako katika uk.58:554.
·         Adui zako ni zetu katika uk.68:648.
Hizo ni baadhi ya semi ambazo zimejitokeza katika utenzi huu, hii ni dhahiri kuwa semi hizi hutumiwa katika kazi za kifasihi kwa lengo la kutoa ujumbe fulani, kuhamasisha suala fulani, kulinganisha vitu fulani na kutahadharisha jambo fulani. Mbali na hayo baadhi ya semi hukusudia kuleta mtiririko wa matukio utakaounganisha sehemu katika visa vyao.
4.5   Matumizi yaSemi
Katika utenzi huu pia matumizi ya nahau nayo yamejitokeza, ambako ni moja ya sifa za tanzu nyingine zilizoingizwa katika tendi. Nahau ni moja ya semi ambazo zina mafumbo ndani yake na zina lengo la kutoa ujumbe filani kwa njia ya kutumia maneno mengine tofauti na kitu kinachozungumziwa. Hivyo jamii hutumia nahau kwa lengo la kukosoa au kuelezea kitu au sifa na tabia za mtu kwa namna ya tofauti. Mara nyingi si rahisi kuweza kutambua maana ya hizo nahau kama we si miongoni mwa wanajamii wanaotumia nahau hizo. Hivyo wakati mwingine huwa ni vigumu kupata maana zake kwa haraka. Katika tendi nahau nazo zinatumika katika kukamilisha maudhui na kuongeza sifa za wahusika waliotumika. Miongoni mwa nahau hizo tunaziona katika kurasa na beti mbalimbali kwa mfano “Kaingia kwa mabavu” katika ukurasa wa 6 ubeti wa 60, “Mashavu yamemtuna” katika ukurasa wa 34 ubeti wa 297, “Damu inatuchemka” katika ukurasa wa 34 ubeti  wa 303, “kukata maini, kubwaga moyo, kumtia mtu simanzi”, “ana mguu mmoja” katika ukurasa wa 4 ubeti wa 33, “jicho lake ni jua” katika ukurasa wa 24 ubeti wa 17, “sauti yake ni radi” katika ukurasa wa 2 ubeti wa 27. Nahau hizi zimebeba mengi ndani yake ambayo yanalenga kufikisha ujumbe kwa jamii na pia zinasaidia kuweza kutambua muonekano wa kitu fulani na kufikirisha jamii.
4.6  Matumizi ya vilio na vicheko
Halikadhalika katika katika tendi huwa kuna maswaibu mbalimbali ambayo huibua hisia kwa wahusika ambazo zaweza kuwa za furaha au huzuni na kupelekea vilio au vicheko. Vicheko huwa vinaweza kuashiria mambo mengi katika jamii kama yafuatayo: furaha, kebehi au kejeli, mzaha au dharau. Kwa upande wa vilio navyo vyaweza kuashiria furaha, huzuni au majonzi, matatizo au mikosi, maumivu, uchungu na hasira. Katika utenzi huu vilio na vicheko vimetumika kwa mfano katika ukurasa wa 18, 20, 23, 25 na 34. Katika ubeti wa 34 ukurasa wa 820 mwandishi anaonesha vijakazi walivyokua wanalia Mukama alipouwawa.
                        820   Nao vijakazihao
                               Wakatoka mbiombio
                               Wakalia “Yoo! Yoo!
                               Mukama  wamemuua!”
Hivyo vilio na vicheko navyo vinadhihirisha kuwepo kwa mtindo wa mwingilianomatini katika tendi ambako vinakua na dhima nyingi kwa jamii kama vile kuonyesha hali aliyo nayo mtu kutokana na jambo fulani lililompata mfano furaha au huzuni na kadhalika.
4.7  Matumizi ya Taharuki
Taharuki ni ile hali ya kutamani kujua kuwa tukio fulani au jambo fulani linaishiaje au nini hatima yake. Ni hali ya kutaka kujua nini kitakachofuatia au kitakachotokea baada ya tukio fulani kuisha.Watunzi wengi wa kazi za kifasihi huunda kazi zao kwa kuingiza matukio yanayopelekea taharuki kwa hadhira. Hii huongezea ari kwa hadhira ya kutaka kujua ni nini kitakachofwatia mwishoni na kufwatilia kwa umakini mkubwa kisa au hadithi nzima. Haya yamejidhihirisha katika utenzi huu pale Malkia ana patwa na taharuki ni nini kitakachofwatia baada ya kuona mwanae kaanza kuota meno ya juu. Kwa mfano katika ukurasa wa 17 ubeti wa 153, 154 na 155. Hivyo tendi nyingi za Kiswahili huusisha matumizi ya taharuki; hii huleta hamu ya kuendelea kufwatilia hatima ya kisa fulani.
4.7   Matumizi ya Majigambo au Vivugo
Hizi ni ghani za kujisifia. Kwa kawaida hutungwa na kughanwa na mhusika mwenyewe. Kivugo hutungwa kwa ufundi mkubwa, kwa kutumia mbinu kama sitiari, vidokezi, ishara, takiriri na wakati mwingine hata vina (Mulokozi 1996:81). Mara nyingi hufanywa na wanaume yakifungamana na tukio maalumu katika maisha yake, kwa mfano kuingia vitani, kupambana na maadui kama vile wanyama wakali, kushinda jambo na kadhalika. Kipengele hiki halikadhalika hakijaachwa nyuma kwani katika tendi lazima pawepo na matukio mengi ya kishujaa waliyoyafanya watu na hivyo hujigamba mbele za watu kudhihirisha ushujaa wao, kwa mfano katika ukurasa wa 6 ubeti wa 57 hadi wa 61, 68, 75, 76, 109, 386 hadi 390, na 639 hadi 641. Katika beti hizi zote mtunzi ameonesha majigambo mbalimbali yaliyokua yanafanywa na wahusika, mfano ubeti wa 396 na 397 Nyakiiru na Kanyamaishwa wanajigamba mbele ya Sultani.
                        396     “Ni vyema kuyasikia                    397    “Nimezoea vita
                                    Maneno ya ushujaa                                Hupiga bila kusita
                                    Mimi pia nakwambia                               Kazi yangu ni kuteta
                                    Si mzembe kwa kuua.                              Mateto nina yajua.
4.8  Ngomezi
Baadhi ya makabila huweza kupeleka habari kwa njia ya ngoma. Midundo fulani ya ngoma huwakilisha kauli fulani katika lugha ya kabila hilo. Mara nyingi kauli hizo huwa ni za kishairi au kimafumbo (Mulokozi 1996:87). Anaendelea kusema kuwa hii ni fasihi simulizi inayowasilishwa kwa kutumia mlio wa ngoma badala ya mdomo; tunaziweka katika kundi la fasihi simulizi kwa vile ishara za ngoma zinazotumika huiga misemo, tamathali na viimbo vya usemaji wa lugha inayohusika. Halikadhalika ngoma imetumika katika utenzi huu ambako mtunzi anaonyesha katika ukurasa wa 19 amechora picha ya mtu akipiga ngoma kwa lengo la kutoa taarifa mbalimbali za kijamii kwa mfano kuzaliwa kwa mtoto wa Malkia, Kichwankizi ilitumika kutoa taarifa kwa wanakijiji wa Saza kuwa Nyakiiru atadhuru kijijini hapo, pia ilitumika kuashiria jambo au tukio fulani, kwa mfano katika ukurasa wa 56 ubeti wa 528 ngoma ilipigwa kuashira kuwa Nyakiiru ametawala. Hii bado ni ushahidi kuwa tendi za Kiswahili zina kaida ya kuwa na sifa za tanzu nyingine ndani yake.
4.9   Mianzo na miishio ya kifomula
Huu ni mtindo maalumu ambao hutumika sana katika usimuliaji wa kisa fulani ambapo fanani na hadhira wengi hutumia katika kuanza na kumalizia kusimulia kisa. Mtindo huu hutumiwa kwa lengo la kutaka kuvuta usikivu kwa hadhira, umakini na kuwajulisha kuwa huo ndiyo mwanzo wa usimulizi wa kisa fulani; au ndiyo mwisho wa hadithi au kisa kinachoelezewa. Mianzo hiyo yaweza kuanza hivi; hapo zamani za kale, paukwa.., Siku moja… pia huwa na miisho maalumu, kwa mfano, Wakaishi kwa raha mustarehe au hadithi yangu imeishia hapo… Katika utenzi huu mianzo na miisho hiyo ya kifomula imejitokeza katika ukurasa wa 6 ubeti wa 55 anaanza hivi; “Huko zama za zamani mwa… Na katika ukurasa wa 76 ubeti wa 729 anamalizia hivi; “Pia tangu siku hio….Matumizi ya kanuni hizi hutusaidia kubaini mwanzo na mwisho wa kisa fulani. Hivi navyo ni miongoni mwa vipengele vinanyojitokeza katika tendi za Kiswahili kama mwingilianomatini.
5.0  Hitimisho
Makala  haya  yanahitimisha  kwa  kusisitiza  kuwa tendi za Kiswahili  ni fani ambayo inahitaji  ubunifu  mkubwa wa fanani kulingana na muktadha  husika. Hali hii ndiyo inayofanya fani hii hasa  inapoigusa  hadhira ya tendi kuingiza dhana ya mwingilianomatini. Kama ilivyokwishaelezwa hapo awali kuwa uchanganyaji huu wa matini ni kitu cha kawaida na tendi za Kiswahili zina mwingiliano huo, lakini sababu za uchanganyaji huo zilikuwa bado hazijabainishwa wazi katika tendi za Kiswahili. Makala yameweza kufafanua dhana ya mwingilianomatini katika tendi za Kiswahili na umuhimu wake kifasihi. Ili kukamilisha malengo mbalimbali kisanaa, mwandishi hana budi kuhusisha matini mbalimbali katika kazi yake.
Marejeo
M’Ngaruti.  (2008)  Fasihi Simulizi na Utamaduni. Jomo Kenyatta
                   Foundation: Nairobi. 
Mulokozi, M.M.  (1989) Tanzu za Fasihi Simulizi. Katika, Mulika.  Na.  21.
                  Dar es Saalaam: Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili, kur. 1-24.
Mulokozi, M. M. (1996) Utangulizi wa Fasihi ya Kiswahili. OSW 105: Fasihi
                  ya Kiswahili. Dar es Salaam: Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.
Mulokozi, M. M. (1997) Utenzi wa Nyakiiru Kibi. ECOL Publicitions: Morogoro.
Mushengyezi, A. (2003) Twentieth Century  Literary  Theory.  LIT.  224:
                  Literature. Kampala: Makerere University.
Njogu, K. na R. M. Wafula. (2007)  Nadharia za  Uhakiki  wa  Fasihi.Jomo Kenyatta Foundation:                 
                   Nairobi.
Senkoro, F.E.M.K. (2011) Fasihi: Mfululizo wa Lugha na Fasihi KAUTTU: Dar es Salaam.
TUKI, 2004) Kamusi ya Kiswahili Sanifu. TUKI: Dar es Salaam.
Wamitila, K.W. (2006) Uhakiki  wa  Fasihi:  Misingi  na  Vipengele  Vyake.
                  Phoenix Publishers Ltd: Nairobi.
Wamitila, K.W. (2008) Kanzi ya Fasihi: Misingi ya Uchanganuzi wa Fasihi. Vide-Muwa
                    Publishers Ltd: Nairobi. 

6 comments:

  1. This comment has been removed by the author.

    ReplyDelete
  2. kazi nzuri mkuu,nimeisoma,nimielewa vizuri na imenisaidia kwa kiasi kikubwa ,ubarikiwe sana

    ReplyDelete
  3. kazi nzuri sana kwani inaumuhimu sana katik a kusoma

    ReplyDelete