Friday, 14 June 2013

DINI KATIKA TENDIDINI KATIKA TENDI ZA KIAFRIKA

Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam

MISEYEKI, lekumok

UTANGULIZI 
Makala hii inahusu namna ambavyo suala la imani za dini lilivyoweza kijitokeza kwa namna moja au nyingine katika tendi za Kiafrika. Katika makala hii kuna mapitio mbalimbali ya baadhi ya kazi za Tendi za Kiafrika. Mapitio hayo ndio yanachukuliwa kama sampuli ya data, iliyochambuliwa ili kuweza kubainisha namna ambavyo imani za dini zilivyojitokeza katika tendi hizo. Vilevile kuna makala mbilimbali zimepitiwa ili kuweza kubaini mwanya au pengo la kitaaluma katika uwanja huu wa tendi za Kiafrika.
PENGO LA KITAALUMA.
Kusudi la makala hii ni kuziba pengo lililoachwa na waandishi wengine waliowahi kujishughulisha na uandishi juu ya tendi za Kiafrika kwa ujumla wake. Waandishi waliotangulia wameandika mengi sana kuhusiana na tendi za Kiafrika lakini katu hawakuwahi kujikita kwa kina katika kipengele hiki cha imani za dini zinazojibainisha katika tendi za Kiafrika. Mwandishi aliyewahi kuandika mada inayoelekea kufanana na hii kidogo ni Mariam K. Deme. Aliyeandika kuhusu Nguvuasili/sihiri katika tendi simulizi za Kiafrika inavyo akisi imani ya dini katika jamii za Kiafrika (the supernatural in African Epics Traditions as a Reflection of the Religious Beliefs of African societies. Hivyo baada ya kuliona hilo ikanipasa kuandika makala hii inayohusiana na imani za dini zinazojibainisha katika tendi za Kiafrika, kwani si kweli kuwa zimeakisiwa na nguvuasili/sihiri pekee kama alivyoandika Mariam K. Deme.

Katika makala hii nimekusudia kuweka bayana dini zilizojibainisha katika kazi nyingi za tendi za Kiafrika. Ikiwa ni miongoni mwa vipengele ambavyo havijazungumziwa kwa kina katika makala nyingine zilizotangulia katika ulingo wa tendi za Kiafrika. Hii itawasaidia sana wasomaji na watafiti mbalimbali wanaojihusisha na tendi za Kiafrika.
UMUHIMU WA MAKALA HII
Makala hii inatazamiwa kuongeza maarifa katika uwanja wa Tendi za Kiafrika. Hii ni kutokana na ukweli kuwa makala hii imezidi kupanua mawanda ya Tendi baada ya kuandika kile kilichoachwa na wanazuoni wengine katika uwanja huu.
NADHARIA YA UCHAMBUZI.
Katika makala hii, nadharia iliyotumika kuchambulia kazi za kifasihi (Tendi) ni nadharia ya uasilia. Nguzo ya nadharia ya uasilia ni kuangalia maisha kama yalivyokuwa, yaani maisha asilia. Kwa hivyo lengo la uhakiki huu ni kutoa picha ya maisha kama yalivyokuwa (kwa ukweli wake wote) ili kueleza misingi ya maisha yalivyo sasa. Wakati mwingine inasemekana kwamba, uasilia hutoa picha halisi zaidi ya uhalisia. Nadharia ya uasilia huchagua maudhui maalum ya kuzingatia. Nadharia hii iliendelezwa na kundi la waandishi waliokuwa na tasnifu maalum ya kifalsafa.
MAANA YA TENDI
Tendi ni taaluma/fani ambayo imekuwa ikishughulikiwa na wataalamu mbalimbali kwa namna tofautitofauti. Baadhi ya walaamu waliotoa maana ya tendi ni pamoja na hawa wafuatao.
Mulokozi(1996) anasema kuwa Tendi ni “ushairi wa kishujaa wenye umbo la masimulizi. Kwa kawaida tendi huwa na mgogoro mkali na mtindo sahihi, japo wahusika wa matukio huweza kuwa wengi sana. mgogoro mkali na muundo sahili hutokea katika kisa”
SIFA ZA TENDI.
Kwanza, Tendi huwa na dhima mbalimbali. Tendi kama zilivyo fani zingine za fasihi huwa na sifa mbalimbali katika jamii. Dhima hizo ni kama vile kuelimisha, kuburudisha, kutunza amali za jamii pamoja na kukuza na kutunza lugha.  
Pili, Urefu. Mulokozi anabainisha kuwa suala la urefu ni suala linalobadilikabadilika. Hii inamaana kuwa Tendi huweza kuwa ndefu au fupi.
Tatu, sifa nyingine ya Tendi ni ile ya kuweza kuongeza jambo fulani au kupunguza. Baada ya kuona maana ya Tendi , hebu sasa tuangalie maana ya dini.
Kwa mujibu wa TUKI (2004) wanasema, dini “ni imani inayohusiana na mambo ya kiroho kwamba kuna muumba ambaye aliumba ulimwengu huu na kwamba ndiye mtawala wa kila kilichomo” wanaongeza kuwa “ni mfumo fulani wa imani hii na njia ya kuabudu, kusali na kuheshimu/kutii huyo muumba.”
Fasili ya TUKI inawiana kwa namna fulani na ile iliyotolewa na Oxford (2007) kuwa dini “ni imani kwa Mungu au miungu na shunghuli zihusianayo na mambo haya Baadhi ya dini zinazopatikana barani Afrika ni dini ya Kikristo, Uislamu na dini za kijadi. Katika sehemu ifauatayo tumefafanua kwa ufupi msingi wa kila kundi la dini.
Ukristo. Hii ni dini inayohusiana na mafundisho ya Yesu Kristo, dini hii iliingia barani Afrika kupitia kwa wamisonari waliokuwa wakala wa wakoloni ambao baadaye waliitawala Afrika miongo kadhaa. Hivyo, asili ya dini ni huko ulaya na mashariki ya kati ambako ndiko alikozaliwa Yesu Kristo miaka 2012 iliyopita. Hivi sasa dini hii ina wafuasi wengi kutoka sehemu mbalimbali za bara la Afrika na ulimwenguni kote.
Uislamu. Ni dini ambayo inafundisha kuwa kuna Mungu mmoja pekee na Muhammad ni Mtume wake, hii ni kwa mujibu wa Oxford (2007). Vilevile dini hii kama ilivyo Ukristo asili yake si bara la Afrika, bali ilianzia barani Asia. Dini hii ilifika huku barani Afrika kupitia kwa Waarabu ambao walikuja kwa dhumuni la kufanya biashara na pia kueneza dini ya Kiislam kwa Waafrika.
Dini za asili. Japokuwa imani hizi si rasmi sana katika jamii za Kiafrika lakini zipo na zina wafuasi wengi. Imani hizi zinahusiana na kuabudu Mizimu, majini, na hata sanamu (miungu). Imani hizi huhusisha Uchawi na matumizi ya Nguvuasili/sihiri. Vilevile ibada za dini hizi huhusisha sadaka za kumwaga damu (kutoa kafara)
Baada ya kuziangalia baadhi ya dini zinazopatikana barani Afrika, hebu sasa tuangaliea namna dini hizo zilivyojitokeza katika kazi mbalimbali za Tendi za Kiafrika.
DINI ZA ASILI
Kwa kuanza na upande wa dini za asili. Watunzi wa tendi za Kiafrika wamejaribu kuakisi maisha halisi ya Waafrika na imani zao. Vilevile zinaitwa za asili kwani hazina uhusiano wowote na wageni wa bara la Afrika kama zilivyo dini zingine bali waasisi wake ni Waafrika wenyewe.
Uakisi wa dini za asili tunaupata katika masimulizi ya Ozidi Saga (J.P. Clark) Katika masimulizi haya tunaona kuwa shujaa Ozidi anatumia mbinu za kijadi katika vita. Tunasimuliwa namna shujaa Ozidi alivyozaliwa na namna alivyokua hali ambayo ilikuwa tofauti na watu wengine. Ozidi aliweza kufanya mambo makubwa na ya kishujaa kwa kutumia nguvu za kichawi pamoja na miti shamba. Aliweza kujikinga na mabaya kwa kutumia elimu ya kichawi aliyopatiwa na Bibi yake. Kiujumla tunaona kuwa katika hadithi ya Ozidi Saga kuna usawiri wa miuungu, mizimu pamoja na nguvuasili/sihiri zingine. Tunaona kuwa shujaa wa Tendi za Kiafrika hawezi kutenda matendo ya kishujaa pasipo kutumia uwezo kutoka kwa miungu, mizimu pamoja na nguvuasili/sihiri zingine. Vilevile tunaona kuwa mashujaa au watu wengine huweza kuwasiliana na mizimu au miungu kwa njia ya kufanya matambiko na kutoa sadaka kwa njia ya kafara.
Kadhalika katika utendi wa Mwindo (Daniel na Mateene 1969) suala hili linajitokeza kwa kiasi kikubwa. Katika utendi huu tunamwona shujaa Mwindo akifanya mambo makubwa na ya kustaabisha kama vile kuongea akiwa tumboni, kuzaliwa na kuanza kuimba, kucheza na kukimbia, nk. Mambo haya aliyafanya si kwa kutumia nguvu na uwezo wake binafsi bali kwa kutumia uchawi na nguvu za kiganga. Vilevile mtunzi amebainisha namna ambavyo watu huabudu miungu wa kiasili/kijadi. Kwa mfano ameonyesha jinsi shujaa Mwindo alivyokuwa akimwomba mungu wa radi aitwaye Nkuba ili aweze kupambana na watu wote wa Tubondo. Suala hili la kuabudu miungu linatudhihirishia kuwa watu hawa walikuwa wakiamini katika dini zao za asili kama vile mizimu, miti mikubwa, mawe nk. Kiukweli Mashujaa wa tendi za Kiafrika hawezi kukamilika bila msaada toka kwa mizimu na matumizi ya sihiri/nguvuasili.
Baada ya kuona namna imani ya dini za asili ilivyo bainishwa vyema katika Tendi za Kiafrika hebu sasa tutazame na upande mwingine wa dini ya Uislamu, namna ambavyo imeweza kujitokeza katika tendi za Kiafrika.
UTENZI WA VITA VYA WADACHI KUTAMALAKI MLIMA.
Utenzi huu uliotungwa na Hemed bin Abdallahn ni utendi ambao umesheheni mambo kadha wa kadha yanayosawiri muktadha wa historia ya jamhuri ya Tanzania (Tanganyika) kwa kutumia elementi mbalimbali za kidini hususani dini ya kiislam. Katika utendi huu suala la kumuabudu Mungu mmoja linatiliwa mkazo. Jambo hili tunalikuta katika ubeti wa 12 mwandishi anaposema:
Sifa za Rabbi Majidi
Na mtume Muhammadi
Ufanyapo jitahidi
Kufuruni hutaingia”.
Kutokana na maelezo hapo juu ni dhahiri kuwa utenzi huu unahusiana na dini ya kiislamu inayosisitiza kumwabudu Mungu aliyeimba dunia hii na vyote vilivyomo. kadhalika katika ubeti wa5. Anasema   ;
Ndiye muumba wa bahari
Na shamsi na kamari
Na nyota zikakithiri
Ili anga la dunia.”
Vilevile katika utenzi huu tunaona jinsi waumini wa dini hii ya kiislamu wanavyomuomba Mungu ili awaepushie mbali mabalaa na majanga yanayoweza kuwakumba. Mwandishi amebainisha kwamba Mungu aliye mbinguni huwakinga waja wake dhidi ya adui. Katika ubeti wa 19. Mtunzi anasema
Tunusuru waja wako
Vita vya adui zako
Wakataa dini yako
Tusiabudu taaa.”
Baada ya maelezo haya tunaona kuwa dini ya kiislamu imejitokeza katika tendi za Kiafrika. Aidha tunaona kuwa watu wamekuwa wakitumia dini hii ili iwe kinga yao dhidi ya maadui na kutatua matatizo yanayowakumba. Hali hii pia imejihidhirisha katika utendi wa Inkishafi kama tutakavyoona hivi punde.      
Utendi wa Inkishafi ulitungwa na Sayyid Abdalah Bin Alin-Bin Nasir. Hapo awali utenzi huu uliandikwa kwa lugha ya Kiarabu na baadaye ulifasiriwa kwa lugha ya Kiswahili. Utenzi huu kwa kiasi kikubwa umezungumzia dini na maisha ya jamii kwa ujumla, Dini iliyozungumziwa katika utenzi huu ni dini ya kiislamu. Kwa mfano, mtunzi anaanza kwa kusema,
“Bismillah naikadimu,
Hali ya kutunga hino nudhumu,
Na ar- Rahmani kiirasimu
Bas ar-Rahimu nyuma ikae”.
Vilevile mwandishi/mtunzi anamalizia mashairi yake kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumpa nguvu na uwezo wa kutunga na kuhitimisha kazi hii ya utungaji. Mtunzi anamalizia kwa kusema hivi.
“sasa takhitimu tatia tama,
Atakofuata na kuyandana,
Rabbi hukuomba tujaaliye,
Rabbi mrahimu mwenye kutunga,
Na mezokhitimu mja malenga,
Sala na salamu ni zao kinga,
Rabbi tukubali ziwashukiye”.
Kupitia maelezo haya tunaona kuwa, maudhui ya utenzi huu wa Inkishafi kwa kiasi kikubwa ni ya dini ya kiislamu. Ambapo tunaona namna Mungu anavyopewa heshima kubwa kuwa yeye ndiye anatoa uwezo kutenda mambo yoyote katika jamii. Hivyo hata mashujaa hawawezi kudhihirisha ushujaa wao pasipo Mungu. Mwandishi/Mtunzi wa utenzi huu anakiri kuwa Mungu ndiye aliyemjalia uwezo wa kufanya kazi hii kwa ufanisi mkubwa hivyo hana budi kumshukuru. Maudhui ya kidini hususani dini ya Kiislamu yanapatikana pia katika utendi wa Hamziyya ulitungwa na sufii Al-Busiri. Kama ilivyokuwa kwa tenzi nyingi za Kiswahili za kale ambazo hapo awali ziliandikwa kwa kutumia lugha ya Kiarabu, na baadaye kutafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili, utendi huu pia mwanzoni kabisa uliandikwa kwa lugha ya Kiarabu kabla ya kutafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili.
Katika utenzi huu mwandishi ameelezea historia ya maisha ya mtume Muhammad. Kutokana na jambo hili tunabaini kuwa katika utendi huu dini ya kiislamu imeweza kusawiriwa vyema kwa sababu kwa mujimbu wa historia, mtume Muhammad ndiye mtume wa mwisho katika uislam. Hivyo basi tunaona kuwa utenzi huu wa Hamziyya ambao ni miongoni mwa Tendi za Kiafrika japokuwa ndani yake hakuna shujaa wa Kiafrika, lakini kwa sababu mandhari yake ni ya Afrika. Basi inatuhakikishia kuwa Afrika kuna dini ya kiislamu kama ilivyoonekana katika Utendi huu, kwani ni kweli kuwa Tendi ikiwa mwiongoni mwa matawi la fasihi lazima isadifu mambo yaliyoko kwenye jamii mahususi.
UTENZI WA MWANAKUPONA.
Huu ni utendi ulioandikwa na Alen, J,W.T. Katika utenzi huu mtunzi amelenga kuwaasa watu, hasahasa wanawake wa Afrika ili wawe na maadili. Vilevile mwandishi hakuwa mbali na suala la dini, kwani ameeleza kuwa Binadamu si lolote pasipo Mungu. Mungu ndiye muumba wa Dunia hii na vyote vilivyomo. Mfano mwandishi anasema.
“Kisake kutakarabu,
Bisumillahi kutubu,
Umtaye na habibu,
Na sahabaze pamoya.
Ukisa kulitangaza,
Ina la Mola Muweza,
Basi, tuombe majaza,
Mungu tatuwafikiya.
Mwana Adamu si kitu,
Na ulimwengu si wetu,
Walau hakuna mtu,
Ambao atasaliya.”
Katika beti hizi tatu kutoka kwenye utenzi wa Mwanakupona, tunapata mafundisho ya dini ya uislamu. Mafundisho haya yanatutahadharisha sisi Wanadamu kuwa huu ulimwengu tuishimo ndani yake si wetu, na hatutaishi milele bali tunapita. Vilevile inatufahamisha kuwa inatupasa kumwabudu Mungu ili atusaidie kuepukana na matatizo katika jamii. Hapa tunaona kuwa Tendi hazizungumzii ushujaa pekee, bali wakati mwingine huzungumzia masuala ya kiimani kama hivi.
UTENZI WA VITA VYA UHURU WA MSUMBIJI
Utenzi huu umetungwa na Mayoka 1978. Mtunzi ameeleza historia ya nchi ya Msumbiji kabla ya ukoloni, kipindi cha ukoloni na baada ya ukoloni. Wameonyesha jitihada zilizoonyeshwa na Wamsumbiji katika kujinasua dhidi ya makucha ya ukoloni. Vilevile suala la dini limejitokeza katika Utenzi huu, dini ya uislamu ndio iliyojitokeza kwa kiasi kikubwa. Mfano katika ubeti wa 28-30 Mtunzi anasema.
“Ni Allah pweke Mwenyezi,
Ndiwe Mwanamapinduzi,
Awali na zama hizi,
Zaidiyo na maize,
Hako atayazidia”.
Ndiwe pweke Mfinyanzi,
Ulofinyanga wapenzi,
FRELIMO wetu wenzi,
Walo dhahiri wakinzi,
Wa Ubeberu balia.
Wameifuata kweli,
Kauli yako Jalali
Wanamapinduzi kweli
Hawanao mushikeli
Uzidi kuwajalia”
Kutokana na nukuu za beti hizo hapo juu, tunaona kuwa suala la dini ya Uislamu katika tendi za Kiafrika/Kiswahili lina nafasi adhimu. Hii ni kutokana na ukweli kuwa mwandishi amebainisha kuwa Wamsumbiji walimwomba Mungu ili awasaidie katika Mapambano dhidi ya wakoloni.
HITIMISHO.
Baada ya kupitia kazi mbalimbali za kifasihi zinazohusiana na Tendi za Kiafrika imebainika kuwa Tendi nyingi zina imani za dini ya Uislamu zaidi ikilinganishwa na dini nyingine. Hii inatufanya kufikiria labda huwenda kuna uhusiano uliopo baina ya Uiislam na tendi za Kiafrika. Kama watu wakifanya utafiti zaidi katika kipengele hiki wanaweza kuweka wazi jambo hili. Kwa upande mwingine imani za jadi nazo zimezungumziwa kwa kiasi katika tendi, isipokuwa dini ya Kikristo ndio haijazungumziwa sana. Tunapendekeza uchambuzi wa kina ufanyike ili kubaini hali halisi kuhusu nafasi na dhima ya dini katika tendi za Kiafrika/Kiswahil.
MAREJEO.
Alen, J. W.T(1972) Utenzi wa Mwanakupona HEB
Biebuyck, Daniel and Kahombo C. Mateene 1969. The Mwindo Epic. California.
                                  University of California Press
Clark-Bekeleremo. J.P 1991 The Ozidi Saga; Washington.DC: Howard University
                                     Press.
Hemedi, Bin Abdallah, 1891. Utenzi wa Vita vya Wadachi: Education Services
                                     Centre ltd. Dar es salaam.
Jumanne M.M Mayoka 1978. Utenzi wa vita vya Uhuru wa Msumbiji. East Afrika
                                      Publication Arusha.
Kineene wa Mutiso 1997. Utenzi wa Hamziyyah, TUKI. Chuo kikuu cha Dar es
                                        salaam.
Mariam K, Deme. The Supernatural in African Epic Traditions as a reflection of
                                            the Religious belief of African societies.
Oxford. 2007. Oxford Students Dictionary. Oxford University press. UK. Sayyid Nassir. Utenzi wa Al- Inkishafi.
Taasisi ya Uchunguzi Wa Kiswahili (TUKI). (2004). Kamusi ya Kiswahili Sanifu.
                                            Oxford University Press. East Africa

No comments:

Post a Comment