Saturday 29 June 2013

UHAKIKI



Uchambuzi wa tamthiliya ya Sundiata kwa kuzingatia vipengele vya: harmatia, anagnorisisi, hubrisi, nemesisi, na peripeteia. 
Sundiata ni tamthiliya iliyoandikwa na Emmanuel Mbogo na kuchapishwa na TUKI (2011). Ni drama-tanzia inayotokana na dafina ya mapisi ya Afrika Magharibi, lakini ndani ya kioo hiki mwandishi amesanidi na kusawiri mahangaiko na kiwewe cha kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni kinachoendelea kukumba na kukumbatia bara lote la Afrika leo. Katika tamthiliya hii iliyoandikwa kwa ustadi mkubwa tunamwona Sundiata mara tu baada ya kufa baba yake, Maghan Kon Fatta ambaye alikuwa mfalme wa Nianiba Sundiata anadhulumia urithi wake na malkia na kumpatia Dankarani ambaye ni mtoto wake wa kumzaa. Baadaye baada ya mapambano makali Sundiata anafaulu kuchukua ufalme nakuwa mwanasiasa na jemedari shupavu akiongoza majeshi ili kupiga vita udhalimu na uongozi mbovu kama wa akina Sumanguru na hatimaye Sundiata anafaulu kumshinda mfalme Sumanguru, lakini Sundiata hapewi nafasi ya kufurahia ushindi wake na mara baada ya kuupata anapoteza maisha yake kupitia mikono ya mwanamke.
Baada ya kuangalia kwa ufupi historia ya kitabu, ufuatao ni uchambuzi wa tamthiliya ya Sundiata kwa kuzingatia dhana zifuatazo: Harmatia, Peripatea, Anagnorisis, Hubris na Nemesis.

Hamartia: kwa mujibu wa Moles, J L. (1984), ni neno la kigiriki lenye maana ya “kosa” la kuhukumu lifanywalo na mhusika kutokana na ufahamu mdogo wa kiakili au wa kimaadili ambalo humletea anguko, huzuni au kifo.
Hivyo tunaweza kusema kwamba hamartia ni dhana ya kosa limwingizalo mhusika katika ufu. Mhusika hukosea  kutokana na kosa la kimaadili na la kiutendaji au la kiufundi. Kwa mfano, Unapotaka kumuua nyoka sharti upige kichwa, ukikosea tu ukampiga mkia matokeo ni kwamba atakushambulia na kukugonga wewe mwenyewe.
Hivyo basi dhana hii ya harmatia inajidhihirisha katika tamthiliya hii ya Sundiata kwa wahusika mbalimbali kama vile katika (uk.8) tunamuona Sassuma akiwaeleza Waziri na Dankarani, anasema: “...uchawi na makafara ya Komkumba umekwishatengeneza ndwele ya uwete itaendelea, michirizi ya udenda wa domo lake katu hautakatika na tarehe ikifika tego la mwanasesere litamaliza fitina.
Hapa tunaona kuwa kosa alilolifanya Sassuma ni lile la kumfanya Sundiata kuwa kiwete na zezeta badala ya kumuua, kwani anasahau kuwa mtego huu utateguliwa na kumletea madhara yeye mwenyewe. Mfano, (uk.8) Kolokani anasema: tulifunuliwa siri ya kutuonyesha opoo la kutegua siri ya uwete wa kaka’ngu Sundiata”.  
Vilevile Harmatia imejitokeza inajitokeza kwa Keleye mke wa Koroma mjomba wa Sumanguru. Hii inajidhihirisha pale ambapo Keleye anakubali wito na kwenda kumwimbia nyimbo mfalme Sumanguru, lakini mfalme anaanza kuonesha dalili za kumtaka kimapenzi kutokana na sauti yake nzuri. Keleye hakukubali, hivyo mfalme alimruhusu aondoke na kumtaka aje tena usiku. Baada ya kufika nyumbani Keleye hakumwambia mumewe kuhusu yaliyomsibu. Na kitendo hiki cha kutomwambia mumewe ni kosa jingine ambalo Keleye analifanya bila kukusudia.    
Pia dhana hii inajitokeza tena kwa mfalme Sumanguru mfalme wa Soso pale ambapo Sumanguru anamchukua binti wa Sassuma malkia wa Nianiba anayeitwa Nana ambaye ametolewa kama zawadi ya kutaka suluhu baina ya falme hizi mbili. Mfalme Sumanguru anamfanya mmoja kati ya wake zake bila kujua malengo ya Nana ni nini.
Pia mfalme Sumanguru anafanya kosa jingine bila kujua kwa kumkamata Balla mjumbe aliyekuja na Nana na kumfunga katika jumba lilelile anamoishi yeye na wake zake. Kwa kufanya hivyo anawapa nafasi Nana na Balla kuweza kuwasiliana na kushauriana namna ya kumwangusha.
Hata katika (uk.70) tunaona harmatia inajitokeza kwa Sundiata pale ambapo baada ya kuuvamia ufalme wa Sumanguru anawaambia askari wake wote kwamba, wasiwatendee ukatili watoto na wanawake, na hata askari wote wanaosalimu amri (uk.70). Sundiata hakujua kwamba miongoni mwa wanawake hao yupo Sassuma ambaye ndiye adui yake mkubwa.
Dhana nyingine iliyojitokeza ni “peripatea” Kwa mujibu McKean, E. (2005) Peripetea ni matendo yanayomtoa mhusika kwenye kosa la awali na kumwingiza kwenye shimo au hatari kubwa zaidi ya ile ya awali. Baada ya tego la kwanza kuteguliwa Sassuma anaogopa madhara yatakayompata hivyo anamua kujihami kwa kuweka tego la pili kwa lengo la kumuua kabisa Sundiata, na hapo ndipo Sassuma anajikuta akiingia  kwenye “peripatea” ambapo hawezi kujitoa kabisa. Mfano (uk.13,15)
Konkomba: “(anatoa mkononi mwanasesere (‘mtu’) urefu kama mita moja hivi). Na tego la mwanasesere ndilo hili hapa.
Magwila: “Na hii hapa ndio hirizi ya moyo wake…uchome moyo huo ndani ya damu ya damu…”
Konkomba: “He! hatujasahau kuhusu mwanasesere. (kwa Dankarani). Kichwa chake ukikihifadhi chumbani mwako. Kiwiliwili kakitupe, usiku huu, pale njia panda. Katika giza nene sina shaka Sundiata arudipo atamkwaa. Magwila: “Na huu utakuwa mwanzo wa mauti yake”.
Hapa tunaweza kurejea kwa viongozi wengi wa kisiasa katika nchi za kiafrika, tunaona kuwa, baada ya kufanya makosa wanaanza kutafuta namna ya kujitakasa, lakini mara nyingi matokeo yake ndiyo kwanza wanajiingiza kwenye makosa makubwa zaidi ya yale ya kwanza.
Vilevile (uk.43) Baada kosa la kwanza, Keleye anajikuta akijiingiza katika hatari kubwa zaidi kuliko ile ya mwanzo ambayo tunaweza kuiita “peripatea”. Kitendo cha Keleye kurudi kwa mfalme Sumanguru, tena usiku ni kosa kubwa sana analolifanya Keleye, kwani kule chumbani mfalme alikuwa amejiandaa kufanya naye mapenzi, na kweli mfalme anafanikiwa kutimiza azma yake.
Pia Baada ya kosa la kwanza mfalme Sumanguru anajikuta akiingia katika “peripatea” kosa ambalo ni kubwa zaidi ya lile la kwanza kiasi kwamba hawezi tena kujitoa. Katika tanzia hapa huwa ni kilele cha mchezo. Hii inajitokeza pale ambapo Nana baada ya kushauriwa na Balla anaingia chumbani na kuanza kumlaghai kwa penzi motomoto mpaka analainika na wanakumbatiana na kuanguka kitandani “…taa polepole zinafifia.” (uk.45)
Vilevile katika (uk.73) tunamuona Sundiata anafanya kosa kubwa zaidi na kuingia katika hatari kubwa zaidi ambayo hawezi kujitoa tena, hii ni “peripatea”. Baada ya Sundiata kumuua Sumanguru wanawake wanamshangilia na kumzunguka huku mmoja wao ameshikilia taji kwa mkono mmoja anataka kumvisha wakati mkono mwingine kashikilia kisu kwa nyuma. Sundiata anasita kusogea na kuvishwa taji lakini akina mama wawili wanamhimiza asogee, anakubali na kuvishwa taji.
Dhana nyingine inayojitokeza baada ya peripatea ni “hubris” hii ni dhambi aitendayo mhusika na kumsababishia anguko au kifo. Mfano, viongozi wengi hasa Afrika dhambi kubwa waifanyayo ni ile ya kutokuachia madaraka pale muda wao unapokwisha kwa mujibu wa katiba, au mambo yanapokwenda kombo. Hivyo mara nyingi kinachofuata ni kupinduliwa kwa nguvu au kuuawa kama vile aliyekuwa Raisi wa nchi ya Libya. Kwa mfano katika tamthiliya Sassuma na Dankarani dhambi wanayoifanya ni ile ya kumnyang’anya Sundiata ufalme ambao tayari ulikwishatabiriwa na miungu ya wandigo kuwa Sundiata ndiye atakuwa mfalme.
Pia dhambi nyingine yaani hubris ni ile ya Keleye kufanya mapenzi na mfalme Sumanguru. Kitendo hiki ndicho kinachotudhihirishia dhambi yenyewe aliyoifanya Keleye.
Vilevile Nana anathibitisha kwa maneno yake mwenyewe jinsi mfalme Sumanguru alivyoingia kwenye hubris (uk.68) anamwambia Sundiata: Sumanguru katika wimbi langu la ulaghai akanifunulia siri. Alisema: “Nana mke wangu katika vita hivi, mimi siuliwi kirahisi. Mtu akitaka kumuuwa Sumanguru, kwanza atafute jogoo mweupe! Amchinje na damu yake anyunyize mara tatu kuizunguka ngome yangu. Kisha ang’owe karanga gumba achambue na kuyasambaza majani yake kuzunguka ngome ya Soso. Akifanya hayo yote ataivunja ngome na kuniuwa mimi Sumanguru”. Kitendo cha kutoboa siri ndiyo “Hubrisi” dhambi yeyewe ambayo humsababishia anguko la ufalme wake.
Pia dhambi yaani hubris ni pale Sundiata alipokubali  kuvishwa taji na mwanamke ambaye ndiye Sassuma, kwani kitendo hiki ndicho kilichopelekea kifo chake.
Dhana nyingine ni anagnorsis. Anagnorsis ni utambuzi wa ndani wa kosa alilofanya mhusika. Hii inajidhihirisha katika (uk.10) Sassuma anashangazwa na kustuka baada ya kuona tego lake limegunduliwa, anasema: “(hasira) Ishi! Phu! Tutaona! Tutaona! Tutaona! Hicho ni kiinimacho tu”.  Pia baada ya Sundiata kumwonesha Sassuma tego alilotegewa (mwasesere), alipata utambuzi kutokana na kosa alilofanya. (Uk.19) Sassuma: (usiyahi) Aaa! (kizunguzungu, anaanguka. Baadhi ya mawaziri wanamdaka na kumtoa nje).
Vilevile Keleye anapata utambuzi wa ndani katika akili yake ambao humjulisha kuwa kakosea na tayari kasha jitumbukiza katika anguko kuu, hii ni “anagnorisis” (uk.43,48). Keleye anatambua kuwa kitendo alichokifanya si sahihi, hivyo anaanza kujutia kosa lake. Analia huku anazungumza maneno ya kumtakia kifo mumewe, anasema: “Oh! Koroma mpenzi kufa ewe Koroma wangu, usikimbie, usimuepe adui, usiupige chenga mshale wake wa sumu ukuchome kifuani mwako, ukupekeche ubongo wako ukubakize huko uliko vitani” (uk.44). Pia hata katika (uk.48) anasema: “…Kwa nini hukuanguka ukabaki nyikani mwili wako ukawa chakula cha tai?” Keleye kila anapomkumbuka mumewe dhamira inamuuma kutokana na kitendo alichofanya na mfalme ambacho ndiyo “hubris” yaani ndiyo dhambi yenyewe.  
Pia  baada ya mfalme kuingia katika “hubris”/dhambi yenyewe sasa anapata utambuzi wa ndani katika akili yake ambao ndiyo “anagnorisis”, yaani humjulisha kuwa kakosea na tayari kishajitumbukiza katika anguko kuu zaidi. (uk.70) Sumanguru anatambua na kujutia kosa alilofanya. Anasema: “kama si hirizi yangu iliyoibiwa na Nana ningeweza kuung’oa muhugo katikati ya shamba la Sumanguru, kuigeuza jinsia yake na kumpachika kitumbua pahala pake!”
Dhana ya nyingine ni “nemesis”. Kwa mujibu wa Concise Oxford English Dictionary. (1999) nemesis ni adhabu ambayo haina budi kutokea kwa mhusika aliyestahili kutokana na matendo maovu aliyofanya (hubrisi). Dhana hii inajitokeza pale ambapo ufalme wa Dankarani unaangushwa na wote wawili malkia/Sassuma na Dankarani wanaamua kukimbia.
Vilevile Keleye anaingia katika “nemesis” yaani anguko lenyewe, pale anapoamua kunywa nyongo ya mamba kwa lengo la kujiuwa. Kitendo hicho ndicho kilichopelekea kifo chake. Tunaona mara baada ya kunywa sumu ambayo ni nyongo ya mamba, Keleye anapata adhabu ya kifo ambayo ilistahili kumpata kutokana na dhambi aliyoifanya. (uk.50) Keleye: “Ikabaki: Mjo-mba-aa Aa! Uchungu…nakufa. Nishike…(anakufa)”
Pia tunaona mfalme Sumanguru anapata adhabu ambayo ndiyo “nemesis” kutokana na matendo yake, (uk 73). “Mfalme Sundiata anamchoma sime ya tumboni Mfalme Sumanguru anaanguka kitandani na kufa.
Vilevile tunaona baada ya Sundiata kukubali ushauri wa wale wanawake anasogea na kuvishwa taji bila kujua anayemvisha ni nani na hapo ndipo Sassuma anamchoma kisu tumboni na kupelekea kifo chake. Mfano katika (uk.74) “…Sassuma akamsogelea na kuinama na kumvisha taji kwa mkono wa kushoto na kumchoma kisu mara tatu kwa mkono wa kulia, wanawake wote wakakimbia kwa mshtuko na mshangao. Sundiata anayumba kwa uchungu…(anaanguka, anakufa)”
Hivyo basi, kutokana na tamthiliya ya Sundiata tunaweza kusema kwamba, mwandishi Emmanuel Mbogo kwa kiasi kikubwa amefaulu kutuonesha jinsi dhana hizi zinavyojidhihirisha katika tamthiliya yake ambayo ni kama kielelezo tu cha kutuonesha uongozi wa kisiasa ulivyo katika nchi nyingi za kiafrika.
MAREJEO                              
Concise Oxford English Dictionary. (1999), (10th ). UK. Oxford University Press.
Mbogo, E. (2011). “Sundiata”. TUKI. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
McKean, E. (2005). The New Oxford American Dictionary. United Kingdom. Oxford University Press.
Moles, J L. (1984). "Aristotle and Dido's 'Hamartia”. Greece & Rome, Sec. Series, (31.1: 4854) JSTOR. St. Louis University Library, St. Louis.

No comments:

Post a Comment