Saturday, 29 June 2013

SHAIRIDAKTARI

Ilikuwa siku moja, mimi na wangu ugonjwa,
Kwenda kwa bwana mmoja, pale mnazi mmoja,
Nilifika na kungoja, tiba ya moja kwa moja,
Tiba hii tiba gani, mbona mimi sifahamu.

Masaa yalipotea, daktari jatokea,
Wasiwasi kunijia, moyo ukinisogea,
Mara kiza kikajaa, sebule kikazagaa,
Tiba hii tiba gani, mbona mimi sifahamu.

Ghafula nilishangaa, kumuona mwenye kaya,
Mrefu aliyejaa, mweupe kama papaya,
Sigara kashikilia, ubani na udi piya
Tiba hii tiba gani, mbona mimi sifahamu.

Shida yako naijua, punde aliniambia,
Kabla hajatulia, simu aliipokea,
Ni pale unapokaa, ubaya wametupia,
Tiba hii tiba gani, mbona mimi sifahamu.

Umeiacha asili, ya walo kutangulia,
Dunia kuikabili, maradhi meshikilia,
Hivyo hiyo ni akili, kweli ukifikiria,
 Tiba hii tiba gani, mbona mimi sifahamu.

Daktari katamka, bila hata ya kusita,
Kuwa yeye anataka, mizimu kuitafuta,
Nami bila kuridhika, mkono kanikamata,
Tiba hii tiba gani, mbona mimi sifahamu.

Ndani alinifungia, huku kishusha pazia,
Kauli nisozijua, daktari lizitoa,
Mara shusha sidiria, zimwile kulichanjia,
Tiba hii tiba gani, mbona mimi sifahamu.

Baada ya kunichanja, fahamu nilipoteza,
Waja wakanikongoja, na wengine nong’oneza,
Kuwa daktari Kija, Mola angempoteza,
Tiba hii tiba gani, mbona mimi sifahamu.

1 comment: