Saturday, 24 August 2013

JAALA YA SHUJAA.

JAALA YA SHUJAA WA TENDI ZA KIAFRIKA NA ULAYA.
Kalinjuma Dezidery-UDSM

Utangulizi
Katika makala hii tutajadili kuhusu jaala ya shujaa wa tendi za Kiafrika na Ulaya. Katika mjadala wetu tutazingatia jaala ya shujaa wa tendi na ukweli kuhusu mambo yanayofungamana na jaala yake. Katika kuthibitisha mjadala huu tutatumia hoja au mitazamo iliyotolewa kuhusu shujaa wa tendi za Kiafrika na Ulaya kuhusu jaala yao. Mitazamo hiyo miwili ilikuwa mtazamo wa shule ya Ulaya kuhusu tendi za Ulaya na mtazamo wa shule ya afrika kuhusu tendi za Kiafrika. Lakini katika mjadala wetu hatutaweza kujadili jaala ya shujaa bila kuangalia walau kwa ufupi maisha aliyopitia shujaa hadi anafikia anguko lake.
Katika makala hii, kazi mbalimbali zimeteuliwa na kupitiwa ili kuonesha ukweli wa kile kinachozungumziwa. Kazi hizo ni pamoja na utendi wa Nyakiiru Kibi (1997 ) kilichonadikwa na Mulokozi, utendi wa Mikidadi na Mayasa (1972) uliondikwa na Heneman, utendi wa Rasi ’IGhuli uliondikwa na Mgeni Bin Faqihi pamoja na utendi wa Mkwava wa Uhehe (1969) uliondikwa na Mulokozi. Kwa hiyo kupitia mapitio hayo walau tutaonesha kile kinacho kusudiwa si kwa undani sana kulingana na muda tuliokuwa nao.

Kama tulivyodokeza hapo mwanzoni, makala hii inakosoa mitazamo miwili ihusuyo shujaa na mambo yanayoambatana na jaala yake. Makala hii inalenga kuweka wazi mahusiano ya shujaa na jaala yake huku ikisaili mawazo ya wataalamu mbalimbali kama vile …………
Kwa kuanza na fikra za Okpehwo (1976). Yeye anasema kuwa shujaa wa tendi za Kiafrika huwa mhusika anayejitegemea. Kwa upande mwingine Kunene (1991) anasema shujaa anapaswa kuonekana akiwa peke yake asiye na msaada kufikia jaaala yake. Aidha utafiti wetu pia umezingatia fikra za  Bowra (1964) aliyewahi kuhoji na kusisitiza kuwa tendi za kiafrika hazina shujaa halisi kwa sababu jaala ya mashujaa wake imefungamana sana na matumizi ya nguvu zisizo za kibinadamuMakala hii inalenga kuangalia kama shujaa huwa mtumwa wa matendo yake au kama ni kama ni mtu asiyehusika na lolote hadi katika anguko lake. Mwazao haya yametumika kama kiongozi cha kujiuliza jaala ya shujaa ni ipi na imefungamana na nini?.
Katika kuchangia mawazo kuhusu shujaa wa tendi za Kiafrika shule ya kwanza iliongozwa na  Campbell (1949), Okpewho (1976), (1979), na wengine walionesha ukweli wa tendi za Kiafrika lakini  walishindwa kuangalia kwa undani na kuona mila ya jamii na imani yao inavyofungamana na shujaa. Mariam Konate (2007) katika makala ya Journal of Black Studies. Na shule ya pili ni ile ya akina Bowra (1964) Finnegan (1970), (1977) Zumthor (1983) mawazo yao wanakataa wazo lolote kuhusu uwepo wa tendi simulizi Afrika. Kwa mawazo ya kawaida walimaanisha kuwa hakuna shujaa.
Kumekuwepo na maoni tofautitofauti kuhusu jaala ya shujaa wa tendi za Kiafrika na Ulaya. Utofauti huo upo katika kuangalia namna mashujaa hao hufikia anguko lao. Anguko hili huwa katika pande mbili yaani upande wa anguko kama kifo au kama mafanikio anayopata mhusika baada ya kupitia mahangaiko na mapambano mbalimbali.
Katika makala hii nimeteua kazi nne za tendi. Mbili kutoka Ulaya ambazo ni utendi wa Mikidadi na Mayasa (1992) na utendi wa Rasi ’IGhuli Mgeni Bin Faqihi pamoja na mbili kutoka Afrika ambazo ni Mukwava wa Uhehe na utendi wa Nyakiiru Kibi. Katika tendi hizi hoja ya msingi ni kujadili jaala ya shujaa wa tendi za Kiafrika na jaala ya shujaa wa tendi Ulaya.
Okpewho na Innes wanadai kuwa mashujaa wa tendi za Kiafrika wanafanana na mashujaa wa tendi za Ulaya. Walitumia tendi za Odyssey na Illiad kulinganisha ufanano huo. Lakini pamoja na kufanana huko Okpewho anasema kuna tofauti kati ya mashujaa hao. Anasema mashujaa wa tendi za Kiafrika si watumwa wa miungu, wenyewe kwa nafsi zao hujitafutia jaala yao. Anasema mashujaa wa tendi za Kiafrika hujikuta wakifanikiwa ama kwa sababu ya mikono yao wenyewe au mikono ya watu wengine tena wa karibu yao, wakati mashujaa wa tendi za Ulaya anguko lao hufungamanishwa na nguvu za sihiri na katika mafanikio yao.
Katika makala hii tunahopji na kudadisi dai hilo kuwa kwa namna gani mashujaa hawa hufikia jaala yao. Je nikweli tendi zote za Ulaya shujaa hufikia anguko kwa msaada wa nguvu za sihiri au wengine hufikiaje anguko  lao?. Je kuna ufanano kati ya anguko la shujaa wa Kiafrika na Ulaya? Je? Shujaa wa tendi za Kiafrika si mtumwa wa miungu? Baada ya kuangalia maelezo hayo ya awali hatuna budi kupitia tendi teule ili kubainisha kisemwacho, tukianza na tendi za Ulaya, katika utendi ya Mikidadi na Mayasa mwandishi ametamalaki maisha yao yote hadi mwisho wanaoana baada ya kushinda vipingamizi walivyokuwa wamewekewa. Utendi huu uliondikwa na Heineman unaelezea pingamizi alizowekewa Mayasa hadi anaolewa. Katika utendi huu tutaangalia kwa ufupi maisha ya mashujaa hawa wawili ili kubaini mwisho wao ulikuwaje.
Katika utendi huu Jabiri hataki mtoto wake Mayasa aolewe na maskini kwa hiyo anaamua kuweka mahari kubwa itakayomshinda Mikidadi aliyekuwa maskini. Mahari aliyoweka inakubaliwa na Mikidadi na anaamua kwenda kuitafuta kwa upanga. Mikidadi katika kutafuta mahari anapambana na Jini na kumsomea dua. Mikidadi anateka mali nyingi baada ya kupambana na Luhani na kuwaokoa vijana wawili anakutana na majeshi ya Mtume Muhamad S.A.W. Mikidadi anajitambulisha kwao na wao wanajitambulisha kwake na anaeleza kisa chake kilichomfanya atafute mali. Masahaba hawa wanampa mali nyingi ili atimize malengo yake.
Mikidadi anatumiwa majeshi la Kasiri anapambana nayo na kuyashinda. Mikidadi anamteka amiri wao na kwenda aye kwa Kasiri. Wakati huo Kasiri ana hamu kubwa kumjua shujaa huyo. Anapofika anazungukwa tena na majeshi anayashinda yote. Mikidadi anarudi na kukuta harusi ya mchumba wake Mayasa na anaozwa kwa Maliki Bin Riyahi. Mikidadi anakabili jeshi lililoongozana na Mayasa, jeshi linataka suluhu na Mayasa anapewa nafasi achague anampenda yupi anamchagua Mikidadi. Jeshi linakataa uchaguzi huo na mapigano yanaibuka lakini Mikidadi alishinda jeshi.
Jabiri anamkaribisha Mikidadi, kumbe alitaka kulipiziwa kisasi na auawe na Maliki Bin Riyahi, Mikidadi analeweshwa na kutiwa nguvuni na majeshi ya Maliki. Lakini Mikidadi anamwambia mama yake Tamima asome dua na anapomaliza anapanda mnyama kwenda Madina kwa Mtume Muhamadi S.A.W. aliyekwisha ambiwa habari za Mikidadi. Tamima anapewa Ali na Haida kumsaidia Mikidadi. Jabiri na Maliki wanauawa na Mikidadi anachagua kupigana kwa ajili ya jihadi akapokelewa kwa furaha na Mtume.
Katika utendi huu tunaona jaala shujaa inaishia katika maisha ya raha kwa Mtume na katika kupambana kwake inadhihirika kuwepo kwa matumizi ya nguvu za sihiri mfano Mikidadi kuwa na uwezo wa kushinda kila jeshi bila kusaidiwa na mtu yeyote. Lakini pamoja na hayo tumegundua kuwa mashujaa wa tendi siyo tu hutegemea nguvu za sihiri bali hutegemea hata nguvu za kile kinachaaminiwa na wengi yaani Mungu ambapo wengine pia wanafungamanisha Mungu katika dini na sihiri. Mfano Mikidadi anapopambana na Jini aliamua kwa  kumsomea dua na Jini akashindwa, pia tunaona mama yake Mikidadi akisoma dua ili mwanae asiuawe na alifanikiwa.
Kwa hiyo kwa kuzingatia hoja ya Bowra kuwa tendi za Ulaya hutegemea sana sihiri, mbona kuna hata nguvu ambazo mimi naweza kuziita nguvu za kimungu ambazo kila mtu huweza kutumia na akafanikiwa kama shujaa Mikidadi alivyofanya? Tunaweza kusema kuwa bora angehitimisha kwa kusema kuwa mara nyingi hutumia nguvu za sihiri lakini lisiwe jibu la moja kwa moja kama alivyohitimisha.
Katika utendi wa Rasi ’IGhuli tunaoneshwa maisha aliyopitia shujaa huyu hadi anafikia anguko lake, Mukhariki Bin Shahabu kwa sababu ya jeuri yake na ushupavu anafungwa na baba yake, kwa msaada wa rafiki yake Muyai akaweza kutoroka na kumuua baba yake na kujinyakulia utawala. Akatawala kwa udhalimu mkubwa mpaka anapokuja kushambuliwa na majeshi yaliongozwa na Mtume Muhamadi. Mtume alitokewa na Malaika Juburii na kumwambie akamshambulie Mukhariki Bin Shahabu ibilisi alimdanganya na kujificha katika sanamu ya ’IGhul.
Katika vita hivyo vikali tunaoneshwa Mukhariki Bin Shahabu anakabidhi ujemedali kwa mtu mwingine na kukimbilia gerezani ambako anakutana na Ali wanapambana na Ali anafanikiwa kumkata kichwa na unakuwa mwisho wa Mukhariki Bin Shahabu. Katika mtiririko wa visa hadi anauawa hakuna sehemu ambayo tunaoneshwa akisaidiwa na nguvu za sihiri. Katika mapambano yake anapambana na vikosi vya Mtume na hakuna sehemu ambayo alishinda kikosi cha Mtume.
Kutokana na kiunzi cha nadharia ya Okpewho kuwa shujaa wa tendi za Kimagharibi hufungamana na nguvu za sihiri mbona hatuioni hapa? Inaonekana Mukhariki Bin Shahabu aliongozwa na nguvu zake mwenyewe huku akishirikiana na jeshi lake hadi anapofikia hatua ya kifo. Tungetegemea kuwa kwa kuwa shujaa huyu ni wa Kimagharibi aoneshe ushujaa wake katika mapambano wa maadui zake kwa kutumia msaada wa sihiri. Tukirejelea inasemekana Mukhariki Bin Shahabu alidanganywa na Ibilisi na kwenda kujificha katika sanamu iliyoabudiwa na Rasi ’IGhuli na wenzake kama Mungu wao. Huenda hapa mwandishi alilenga kutuonesha ufungamano wa Mukhariki Bin Shahabu na imani yake juu ya sanamu hilo.  Basi hizo siyo nguvu za sihiri kama zinavyotegemewa. Huenda shujaa huyu alikimbilia humo kujificha tu. Pia tunaoneshwa baada ya kuibwa sanamu lile haikuleta madhara yoyote kwa shujaa huyu.
Kwa hiyo maoni ya Okpewho kuwa mashujaa wa tendi za Kimagharibi hufungamana na nguvu za sihiri katika mafanikio au kuanguka kwa shujaa huenda ikawa si kwa tendi zote na shujaa wote. Sifa hii inaangukia katika baadhi ya shujaa na si  kwa kujumuisha.
Baada ya kuona dondoo za tendi hizo tuangalie pia tendi za Kiafrika. Katika jamii ya Kiafrika jaala ya shujaa imechukuliwa kama ya shujaa kujiandalia mwenyewe kwa mikono yake au kwa mtu wa karibu. Dai hili kwa kiasi linaweza kuwa na ukweli au likawa halina ukweli ndani yake. Katika tamthiliya  ya Mukwava wa Uhehe iliyoandikwa na Molokozi (1969) tutatoa muhutasari wa maisha ya Mukwava hadi kufikia anguko lake na baada ya hapo tutaangalia kama mawazo ya shule hizi mbili kuhusu jaala ya shujaa yanafungamana na tendi hii ili kuthibitisha uwepo wa mawazo hayo katika tendi za Kiafrika.
Katika utendi huu wa kihistoria tunaoneshwa jinsi shujaa Mukwava anavyopigana na wakoloni ili kuwakomboa watu wake. Tunaoneshwa ushujaa wa Mukwava katika matendo aliyokuwa akifanya. Tunaoneshwa akifukuza Wangoni hadi mpakani kwao akiwa na umri wa miaka kumi na nane. Tunaoneshwa matendo makubwa lakini anguko lake lilikuwa baada ya kusalitiwa na mtu wake wa karibu na anatoa siri yote kuhusu Lipuli na Wajerumani waliporudi tena waliangamiza majeshi yake na baada ya hapo Mukwava aliamua kujiua kwa kujipiga risasi.
Tunaona jaala ya Mkwava ni ya kutoka mikonono mwake na yaani aliamua ajiue ili kutodharirishwa na wazungu. Hapa hoja ya Okpewho kuwa jaala ya shujaa wa Kiafrika hutoka mikoni mwake inakubarlika lakini ni vigumu kukubaliana na mawazo ya Bowra (1964)  kuwa tendi za Kiafrika washenzi na wasiostarabika zimejikita katika matumizi ya uchawi. Tukimnukuu kutoka makala ya “Heroism and the Supernatural in Africa” anasema “the primitive and savage culture of Afrika are characterized by magic” kwanza ni udhalilishaji kusema Afrika ni washenzi na wasiostarabika kwani hakuna kitu ambacho kilikuwa Ulaya na hakipo Afrika japo hakikuwa na maendeleo ya juu.
Pili tunaweza kusema kuwa kulinganisha tendi za Kiafrika na matumizi ya uchawi ni kukosa hoja, kwani anaposema kuwa tendi za Ulaya ndizo huongozwa na nguvu zisizo za kawaida “supernatural power” ajue kuwa nguvu hizo hata Afrika zipo na zipo tendi zenye kuwa na sifa kama hizo. Mfano utendi wa Fumo Liyongo, Utendi wa Lwanda magere, shujaa Mwindo na nyigine. Pia katika hali ya kawaida masuala ya uchawi na sihiri ni mambo ambayo ni magumu kutenganishwa. Hapa ni bora kuangalia ufungamano wa jamii fulani na utamaduni wake.
Katika utendi huu wa Mukwava hakuna sehemu ambapo nguvu za kichawi zimetumika tofauti na matumizi ya nguvu za kawaida katika mapambano. Hapa tunaweza kutofautisha nguvu zinazotumiwa na Fumo Liyongo au Mikidadi na nguvu anazotumia Mukwava. Kwa hiyo ni vigumu kuhitimisha moja kwa moja kuwa tendi za Kiafrika hufungamana na uchawi. Hapa kunahitajika utafiti wa kina ili kubaini uchawi ni upi na sihiri ni ipi na je imani ya jamii fulani ni ipi kuhusu jambo fulani kiutamaduni.
Katika utendi wa Nyakiiru Kibi, tukiangalia maisha ya shujaa Nyakiiru Kibi na Kanyamaishwa hadi jaala ya Kanyamaishwa mwandishi anaonesha uzao wake na kutupwa kwake msituni hadi anaporudi kijijini bila kujua kama ndiyo kwao akiongozana na Nyakiiru Kibi na wakapigana na mtawala aliyekuwepo na Kanyamaishwa anamuua, kumbe ni baba yake na anamuua pasipo kujua.  Baada ya matanga Kanyamaishwa anaugua na anatembea kwa waganga ili kupata tiba lakini inashindikana na anafariki dunia na hili linakuwa anguko lake. Mwandishi anasema:
                                                        “Akafa Kanyamaishwa
                                                         Kakoma kutaabishwa
                                                         Shimoni katelemshwa
                                                          Watu wakamlilia”
Katika utendi huu mwandishi amejaribu kuonesha historia nzima ya Kanyamaishwa lakini hakuna sehemu inayoonesha akitumia nguvu za kichawi au nguvu za sihiri. Kanyamaishwa aliishi maisha ya kawaida na alipambana na kushinda vita bila kutumia nguvu za kichawi kama asemavyo Bowra. Hivyo kuna umuhimu wa kuzichunguza kwa undani hoja za wataalamu hawa kuhusu Afrika.
Kwa upande wa pili tukizingatia mawazo ya shule hizi mbili za Magharibi kuhusu tendi, tukiangalia ufawafu wa mawazo haya ya wataalamu kwa kuanza na mawazo ya wale  manaosema kuwa maisha ya shujaa lazima yawe ya kujitegemea; mawazo haya yanaungwa mkono  ya Okpewho (1976) anayesema  kuwa katika Afrika shujaa huwa mhusika mkuu akiwa na maana ya kuwa asitegemee kusaidiwa na ngunvu nyingine “the central of control”.
Mawazo haya hatuwezi kuyapa nafasi sana kwani kulingana na mawazo ya Saydou (1983) anasema utendi ni lazima uwe unafungamana na jamii na tamaduni zake. Hivyo anguko la shujaa huweza kusababishwa na kukiuka mila au utamaduni wa jamii yake au kwenda kinyume na matakwa ya miungu wake. Kwa hiyo kuanguka huko hatuwezi kusema kuwa kumemhusu shujaa peke yake bali kumeambatana na jamii nzima. Mfano katika tamthiliya ya Lwanda Magere anguko lake linafunamana na usaliti aliofanya juu ya mila ya jamii yake na wakuu wake. Kwa hiyo hoja kuwa tendi za Kiafrika hazifungamani na nguvu yoyote tunaona inakosa mashiko.
Tukirejelea tendi nyingi za Kiafrika ni dhahiri kuwa shujaa lazima aambatane na jamii yake hivyo upekee anaozungumzia ni upi? Jee ni upekee wa kushiriki peke yake katika kupambana hadi mwisho wake, au upekee wa kuweza kupinga mila na tamaduni zinazo mzunguka, au ni upekee upi hasa?
Kulingana na maelezo ya Okpehwo tunaweza kusema kuwa mawazo yake hayakinzani sana na na ya ya Kunene (1991). Kunene katika “Heroism and the Supernatural in Africa” anasema shujaa wa Kiafrika wanapaswa kuonekana akiwa peke yake asiye na msaada kufikia jaaala yake. Msaada huo huenda ni kama tuliotaja katika aya iliyopita yaani hatakiwi kujihusisha na nguvu za sihiri. Lakini mbona tendi nyingi za Kiafrika zina mambo ya sihiri?
Pia tukirejelea mawazo ya Bowra (1964) kuwa tendi za Waafrika washenzi na wasiostarabika zimejikita katika matumizi ya uchawi “the primitive and savage cultules of Africa are characterized by magic”. Katika kupitia mawazo ya mtaalamu huyu kiujumla ni kwamba ni vigumu kutenganisha kati ya nguvu za sihiri na nguvu za kichawi kwani yote ni mambo ya kidhahania yasiyoweza uelezewa kinaganaga bali mtu huelezea kulingana na mazingira au utamaduni anavyoelewa. Kwa maelezo hayo tunaweza kusema kuwa alimaanisha kuwa hata jaala ya mhusika hufungamana na matumizi ya nguvu za kichawi.
Ikiwa tutasema kuwa tendi za Kiafrika zinafungana na uchawi kwa kujumuisha itakuwa siyo sahihi kwani si kila tendi ya Kiafrika na Ulaya shujaa wake huwa na nguvu za kichawi au sihiri. Japokuwa katika Afrika inasemekana matumizi ya uchawi ni sehemu mojawapo ya utamaduni wa Waafrika. Kwa hiyo Bowra (keshatajwa) anaposema tendi za Kiafrika zimeegemea katika nguvu za kichawi huenda hakuchunguza utamaduni wa jamii za Kiafrika. Mfano kuna baadhi ya tendi za Kiafrika zinazofunngamana ha matukio ya kihistoria mashujaa wake hawafungamani na matumizi ya kichawi. Mfano utendi hizo ni kama vile utendi wa wa vita vya majimaji, utendi wa vita vya uhuru wa Kenya na Mkwava wa Uhehe.
Hata hivyo ni vyema kukiri kuwa katika Afrika zipo tendi ambazo zimefungamana na nguvu zisizo za kawaida yaani “supernatural” kama zilivyo tendi za Ulaya anazo zipa sifa hiyo. Mfano shujaa Mwindo kabla hajazaliwa alimwambia mama yake namna anatakavyozaliwa.
Pia katika tendi za Ulaya siyo kuwa zote shujaa huwa na nguvu za sihiri, kuna tendi nyingine huwa za kawaida na shujaa hupigana kama mtu anayejitegemea mpaka anapoanguka au kufanikiwa. Mfano utendi wa Rasi ’IGhuli shuja anaonekana kupambana na majeshi ya mtume hadi anaposhindwa na kukatwa kichwa na adui. Kama shujaa angekuwa anatumia nguvu za sihiri tusingetarajia kuona shujaa akikimbia na kujificha, tunategemea apambane hadi mwisho na kama ana nguvu za sihiri lazima zimsaidie mpaka ashinde.
 Kwa hiyo inaonekana kuwa wataalamu hawa waliandika hoja hizi kwa ajili ya kujiweka juu au kujipa hadhi ya juu na kuidumaza Afrika kama Bowra anavyoita Waafrika washenzi na wasiostaarabika. Hii yawezekana waliandika mawazo haya na kufikia hitimisho bila kufanya utafiti wa ndani ndiyo maana hoja zao zinaonekana kupata changamoto kubwa zinapohusishwa na hali ya tendi ilivyo duniani.
 Katika kuangalia mambo yanayofungamana na anguko la shujaa tumegundua kuwa kuna makosa au dhambi anayofanya shujaa na dhambi hiyo humfanya aanguke. Hoja hii tumeidhihirisha katika tendi zote za Kiafrika na Ulaya. Mara nyingi inaonekana shujaa hufanya kosa hili ama kwa kujua au kutojua na mwisho wake ni anguko. Mfano katika utendi wa Nyakiiru Kibi Kanyamaishwa anaanguka kwa sababu ya kufanya dhambi ya kumuua baba yake bila kujua. Katika utendi wa Rasi ’IGhuli shujaa Mukhariki Bin Shahabu kosa alilotenda ni jeuri yake na ushupavu wake alimuua baba yake na kutawala. Katika kutawala aliongozwa na moyo wa kidhalimu hadi napouawa na majeshi ya Mtume.
Hivyo katika tendi zote mashujaa watendao makosa kwa mikono yao huwapelekea anguko lao. Pia kwa hoja hii kuwa kila shujaa hufikia jaala yake kwa kufanya dhambi fulani inafungamana na mawazo ya Bowra ayayesema kifo au mafanikio ya shujaa wa Ulaya hufungamana na nguvu za sihiri, kutokana na utendi wa Ras ’IGhuli uliotumika kama kiwakilishi cha tendi za Ulaya unapingana na sifa za shujaa kuongozwa na nguvu zisizo za kawaida katika kufaulu au kufa kwa shujaa. Tunaona shujaa wa utendi huu akifa kwa kukatwa kichwa na askari mwenzake. Ja sihiri ilijificha wapi?
Vilevile jaala ya shujaa hufungamana na mapambano kwa ajili ya jamii yake ili kuikomboa na ungozi mbaya uliopo au kutaka kupindua utawaala uliopo kwa nguvu. Tendi vyingi huoesha kifo cha shujaa ama kwa kuuawa, kujiua au kupotea kabisa. Mfano utendi wa Nyakiiru Kibi shujaa Kanyamaishwa anafikia kifo baada ya kupindua utawala wa baba yake, Mkwava wa Uhehe anguko lake ni katika kupambana kuwakomboa wananchi wake kutokana na uvamizi wa wadachi, pia katika utendi wa Mikidadi na Mayasa, Mikidadi anapambana ili kumuoa mayasa nayingine nyingi.
Hivyo ni dhahiri kuwa mashuajaa wengi wa tendi hufikia jaala yao wakati wakipambana  kwa ajili ya maisilahi ya jamii yao na hata masilahi  yao binsfsi kama Mikidadi. Kuanguka au kufaulu kwao ni ishara ya masuala mbalimbali katika jamii.
Kwa kuhitimisha tunaweza kusema kuwa jaala ya shujaa inaonekana kufanana kati ya Afrika na Ulaya kwani matukio wanayofanya ni yale yale ya kishujaa yenye kuambatana na matukio yasiyo ya kawaida na yakushangaza. Lakini jambo la msingi linalopaswa kuzingatiwa na kufanyiwa uchunguzi zaidi kwa kutafiti katika tendi nyingi za Kiafrika na Ulaya ni kutafuta usawazisho wa hoja kuwa mashujaa wa tendi za Kiafrika na Ulaya wanafanana. Hakuna tena hoja kuwa shujaa wa Kiafrika na Ulaya wanatofautiana kwa kuwa shujaa wa Kiafrika anatumia uchawi na wa Ulaya anatumia sihiri bali yapaswa kusema kuwa mashujaa hawa hawatofautiani labda namna ya utendaji wao ndiyo unatofautiana.

Marejeo.
Faqih, B.M. (1855) Utenzi wa Rasi ’IGhuli. Dar es Salaam. TPH.
Heinman (1972) Utendi wa Mikidadi na Mayasa. Nairobi: E.A. Ltd.
Kanote, D.M (2009) Heroism and the Supernatural in the Afrcan Epic: Toward a Critical Analysis. From Journal of Black Studies. Western Michingan University: SAGE.
Kunene, D.P (1991) Journey in the African Epic: From Rearch in Africa Literatures. Indiana University Press.
Mulokozi, M.M (1997) Utenzi wa Nyakiiru Kibi. Morogoro: ECOL Publication.
Mulokozi, M.M (1969) Mukwava wa Uhehe. Dar es Salaam: DUP.


1 comment:

  1. Nawashukuru kwa msaada wenu katika kufanikisha lugha inasonga mbele

    ReplyDelete