Saturday 24 August 2013

UCHAMBUZI WA MAKALA


UISLAMU NA MAENDELEO YA KISWAHILI 
"Mwenda Makuthuria".
 

Uwasilishaji 

Muhtasari.

Katika makala haya, mwandishi anakusuadia kueleza mchango wa uislamu katika maendeleo ya Kiswahili. Hii ni baada ya kusoma kazi mbalimbali za wataalamu tofauti na kuona kuwa maandiko mengi yanaelezea maendeleo ya Kiswahili yalivyochangiwa na dini ya kikristo, vita, biashara, utawala wa kikoloni na kusahau mchango uliotolewa na uislamu.


Mwandishi anauona mchango uliotolewa na dini ya kikristo kama vile wamishionari walioandika na kufanya kazi mbalimbali katika kukuza Kiswahili kwa mfano John Krapf aliyekuwa mwanachama wa Shirika la Wamishiori (Church Missionary Society)  alisaidia sana katika uandaaji wa kitabu kilichoitwa Outline of the Elements of the Kisuaheli Language with Special Reference to Kinika Dialect. Askofu Edward Steer A Handbook of the Swahili Language as Spoken in Zanzibar. Pamoja na kufasiri nyimbo mbalimbali pia waliandika kamusi za Kiswahili mfano Fredrik Johnson alipata nguvu kubwa ya kuandaa kamusi iliyoitwa Standard English-Swahili Dictionary na A standarnd Swahili-English Dictionary, hizi zote zilichapishwa mwaka 1939 na bado zinatumika mpaka leo. Huu ulikuwa mchango mkubwa sana katika kukuza Kiswahili Afrika Mashariki. Hapa Kiswahili kinajadiliwa kama lugha na sio kama fasihi.

Kundi lingine lililochangia kukua na kuendelea kwa lugha ya Kiswahili ni kundi la  wanaleksikografia. Hawa waliandaa sarufi ya lugha ya Kiswahili katika maandishi hatimaye kukiwezesha Kiswahili kufundishwa kama lugha ya pili katika Afrika Mashariki ilihali ni lugha ya wenyeji. Lakini pamoja na mchango huo waandishi hawa wameshindwa kueleza ukweli kwani wanaeleza ukweli wa mchango wa kikristo na kusahau kovu lililoandikwa na Waswahili katika historia ya Waswahili kuhusu usafirishaji wa mamilioni ya watumwa kwenda nje, hivyo wamesahau mchango wa uislamu wakati, uislamu uliingia Afrika Mashariki mapema kuliko dini ya kikristo yaani hata kabla ya ujio wa wageni kutoka Ulaya. Pia ni wazi kwamba kwa mara ya kwanza wanazuoni wa kiislamu ndio walioweka Kiswahili katika matini kwa kutumia hati za Kiarabu (Kemima 2001). Hili ndilo pengo la kitaaluma aliloligundua na analishughulikia kama ifutavyo.

Mwandishi ameuanza mjadala wake kwa kufafanua maana ya uislamu. Anasema uislamu ni neno lenye asili ya Kiarabu likiwa na maana ya amani, usafi na kujitolea, hivyo dini ya kiislamu inaweza kutazamwa kama hali ya mtu au binadamu kujitoa mwenyewe na kuyakubali mafundisho na misingi ya Allah. (mwenyezi Mungu). Mwislamu ni mtu yeyote anayekubali mafundisho na misingi ya Allah. Allah alitoa misingi hii ya imani ya dini ya kiislamu kupitia kwa mtume wake mtukufu Muhammadi. Misingi ya imani hii ilitolewa kwa lugha ya Kiarabu ambayo mpaka sasa bado inatumika kama lugha ya kutolea mafundisho ya imani ya dini ya kiislamu ijapokuwa lugha nyingine zinatumika kutolea ufafanuzi wa maneno hayo .

Baadaye mwandishi wa makala anatufahamisha kuhusu historia ya kuingia kwa dini ya Kiislamu hapa Afrika Mashariki. Anahusisha suala hili na maingiliano ya kijamii kati jamii za pwani ya Afrika Mashariki na  wageni kutoka Mashariki ya Kati na  Mashariki ya Mbali yaliyokuwapo karne nyingi zilizopita.. Kadhalika, kuingia kwa dini ya Uislamu Afrika Mashariki na maeneo mengine kumehusishwa na kipindi cha Hijira mwaka 622 AD.  Hijira kilikuwa ni kipindi cha mtawanyiko, ueneaji au uhamaji wa watu kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine. Kipindi hiki kilikuwa na ugomvi baina ya waislamu na wasiokuwa waislamu na kusababisha adhabu na usumbufu mkubwa. Waarabu wengi waliokuwa waislamu  walihama kutoka Mecca na kusambaa duniani kote. Watu walisumbuka maeneo ya kwenda kutokana na imani ya dini yao, ndipo walipokimbilia Afrika hususani Misri, Ethiopia na wengine walikuja Afrika Mashariki. Waarabu waislamu wa mwanzo kuja Afrika Mashariki walikuwa ni pamoja na mfalme al Husain ibn Ali na watoto wake wa kiume sita, walifikia maeneo ya Manda, Pate, Tanga, Mafia na Kilwa katika Afrika Mashariki na maeneo ya Komoro.

Waarabu walipofika Pwani ya Afrika Mashariki walianza kuingiliana na wenyeji wa upwa huo (Waswahili). Maingiliano ya kiutamaduni baina ya makundi haya mawili yalipelekea kuathiriana kiimani na vitu vingine vya kiutamaduni mfano, masuala ya ndoa, mavazi, vyakula, urithi na uchukuaji wa leksimu katika lugha. Waswahili wengi walijiunga na dini hiyo ya kiislamu, na kwa njia hii Waswahili wasingeweza kuepuka kujifunza lugha ya Kiarabu ili waweze kuielewa Kurani.  Pamoja na hayo utamaduni wa Kiarabu ulikuwa na vitu vingi zaidi kuliko utamaduni wa Waswahili na hii ilipelekea Waswahili wengi kuukubali utamaduni wa Kiarabu kwa haraka. Matokeo yake utamaduni wa Waswahili uliiga mambo mengi kutoka katika utamaduni wa Kiarabu, kama vile; katika leksimu maneno ya Kiarabu ni kama Allah, mola, subana, maulana, karama, kurani, tawadha, ramadhani, swala, msikiti, kaaba, kibra, bismilahi. Kiutamaduni Waswahili walivutiwa na namna ya uvaaji kwa mfano wanawake kuvaa hijabu na ushungi na kwa upande wa wanaume huvaa magauni marefu yaitwayo kanzu. Pia sheria zao za ndoa ziliongozwa na kanuni za dini ya kiislamu ziitwazo sharia.

Ujio wa wageni ulivyozidi kuongezeka katika maeneo mbalimbali ya Afrika Mashariki wageni hao walipokelewa na wenyeji Waswahili waliokuwa wamesilimu. Wageni hao walipata makazi mapya kutoka kwa wenyeji waislamu, Waarabu waliingiliana na Waswahili na hivyo kusababisha kuoana baina yao. Walijifunza utamaduni wa Waswahili na lugha ya Kiswahili wakati huohuo waliweza kubadilisha imani za Waswahili na kuwaingiza katika uislamu. Makazi yao yalikuwa katika maeneo ya Lamu, Mombasa, Zanzibar na maeneo mengine ya pwani ya Afrika Mashariki. Katika makazi hayo walijishughulisha na biashara ambapo baadae zilikua na kufika Afrika ya Kati, katika maendeleo yote hayo Waarabu hawakuitenga dini yao katika maeneo yao ya kazi mfano huko Zanzibar Kiswahili chini ya Sultani Seyyid Said wa Omani alipoanzisha makazi 1982 na kuhamia kabisa 1840 alikuta Kiswahili kimekwisha enea na kuwa lingua franka. Utawala wa sultani huyo na watawala wengine chini yake walijifunza lugha hiyo na kuifanya kuwa lugha ya kiutawala iliyopelekea Kiswahili kuwa na hadhi ya juu.

Katika kuenea kwa dini hii Waarabu na Waswahili waliosilimika walijihusisha na biashara na katika biashara zao walitumia lugha ya Kiswahili, hatimaye kuiwezesha lugha hii kusambaa katika maeneo ya ndani au ya bara. Katika kila kituo cha biashara waliweza kujenga misikiti ili wanapopata mapumziko yao waweze kuswali. Vituo vya kibiashara vya  bara kutoka pwani kama vile Tanga, Bagamoyo, Tabora, Shinyanga, Kigoma hadi Kongo ambako mfanyabiashara mwaarabu maarufu aliyekuwa mwislamu kwa asili aliyeitwa Hemed Mohammed Er Murjeb akijulikana kwa jina la TIPU TIP alitumia Kiswahili katika shughuli nzima ya biashara. Watu waliijua lugha ya Kiswahili kama lugha ya waungwana yaani watu waliostaarabika. Katika vituo hivyo walijenga shule za kiislamu karibu na  misikiti yao, madarasa yalijengwa kwa ajili ya kuwafundishia wenyeji namna ya kusoma, kuandika na misingi ya dini ya kiislamu. Lugha ya kufundishia ilikuwa ni Kiswahili. Kwa upandse mwingine katika misikiti lugha ya Kisawhili na Kiarabu vilitumika kama lugha ya mawasiliano. Kwa njia hii lugha ya Kiswahili ilionekana kukubalika sana na wenyeji na kupelekea kusambaa bara na maeneo ya mbali, hivyo wakati dini ya kiisalmu ikiendelea kusambaa na lugha ya Kiswahili ilizidi kusambaa kutokana na lugha hiyo kueneza dini ya kiislamu.

Nchi nyinginezo kama Rwanda lugha ya Kiswahili ilisambaa baada ya Wanyarwanda kuwaruhusu Wajerumani nchini mwao kama watawala karne ya 19. Waislamu Waswahili waliwasaidia Wajerumani kama wapagazi na wakalimani. Kwa kutumia fursa hii, Waswahili na bila shaka waislamu walieneza dini yao kwa kutumia lugha ya Kiswahili. Lugha ya Kiswahili pia ilitumika katika elimu kwa mfano katika kufundishia shule za kijadi. Chifu wa Rwanda Yuhi Masinga alikubali kujifunza Kiswahili pamoja na watawala wa Rwanda wa wakati huo ili kukuza mahusiano baina yao na Wajerumani.

Kipindi hiki kinahusishwa sana na kuasisiwa kwa luha ya Kiswahili ncjini Rwanda (Shabani1983). Kwa upande mwingine, Geraldi (1981) anasema kuwa Kiswahili kiliingia nchini Uganda kabla ya mwaka 1862 kupitia biashara ya masafa marefu. Kama ilivyokuwa kwa upande wa Rwanda, dini ya kiislamu ilichangia kuenea kwa lugha hii katika eneo hili. Anaeleza kwamba Waswahili waliokuwa waislamu katika makampuni ya wafanyabiashara wa Kiarabu walianzisha ligha hii nchini Uganda. Ilipokelewa na kuanza kutumika kwa mara ya kwanza katika mahakama za kifalme.

Wazo hili liliungwa mkono na Khatibu (1983:31) anasema Kabaka Mwanga alikuwa mzungumzaji mzuri wa lugha ya Kiswahili akifanya mawasiliao na utawala wa Kiingereza uliokuwa na makao yake Zanzibar hivyo Kiswahili kilienea sambamba na uislamu katika ngome ya Buganda na hivi leo nchi ya Uganda ina kipao mbele katika kusambaza Kiswahili mfano katika Chuo Kikuu cha Uislamu Uganda ni moja ya mifano ya asasi kubwa zainazoshughulika na kufundisha, kufanya utafiti na kutoa mafunzo mbalimbali kwa lugha ya Kiswahili ingawa sera ya lugha nchini Uganda haikukipa fursa Kiswahili kuenea zaidi.

Mwisho nchini Burundi bwana Marcel (1983:55) anathibitisha kuwa Waarabu ndio waliloeneza Kiswahili nchini humo ijapokuwa hakueleza mbinu walizotumia katika kueneza Kiswahili hicho.

DATA ALIZOZITUMIA.

Alisoma vitabu na makala mbalimbali. Vitabu na makala hayo vmeorodheshwa mwishoni mwa makala haya. Kwa ufupi, makala yake imetokana na data za utafiti wa maktabani.

HITIMISHO

Mwandishi anahitimisha kwamba pamoja na mchango wa biashara, dini ya kikristo, utalii na mambo mengineyo kuchangia katika maendeleo ya Kiswahili lakini uislamu hauwezi kusahaulika, kutokana na jinsi kilivyochangia maendeleo ya Kiswahili Afrika ya Mashariki na kati kwa ujumla.

MAMBO YA MSINGI

Mambo ya msingi anayoelezea mwandishi ni pamoja na chimbuko la uislamu hapa Afrika Mashariki: anasema kuwa uislamu uliletwa na Waarabu, ulikuja kabla ya dini ya kikristo, ulichangia kwa kiasi kikubwa kukuza na kueneza Kiswahili kabla ya mataifa ya Ulaya. Uislamu ulikuwa sambamba na shughuli za kibiashara, Waswahili waliokuwa wamesilimika ndio waliohusika kwa kiasi kikubwa katika kukuza na kueneza Kiswahili pwani ya Afrika ya Mashariki na Bara hata kufika Afrika ya kati. Anakubali kwamba Kiswahili kinatumika kama lugha ya pili katika kufundishia dini ya kiislamu Afrika ya Mashariki na Kati, wakati huohuo Kiswahili kilikuwa kama lingua franka. 

MCHANGO WAKE KATIKA TENDI

Mwandishi anakiri kuwa historia ya Waswahili ilikuwa katika masimulizi, hivyo ujio wa Waarabu  uliweza kuhifadhi fasihi hiyo sumilizi katika matini kwa kutumia hati za kiarabu kwa mara ya kwanza na wanazuoni wa Kiarabu. Hii ndiyo ilikuwa fasihi ya Waswahili iliyohifadhika katika maandishi ikieleza dhamira za maadili ya jamii yao kwa mfano kufanya kazi, umuhimu wa dini kwa watu, umuhimu wa familia ambapo ni miongoni mwa dhamira nyingi ambazo zinajadiliwa katika tendi nyingi za Kiswahili mfano wa tendi hizo zinazojadili dhamira hizi ni Utendi wa Hamziyya, Tambuka, Herakali, Inkishafi na Utenzi wa Mwana Kupona. Baadhi ya tendi hizi zinatupa mwelekeo kuwa zilikuwepo hata kabla ya biashara ya utumwa, mfano utenzi wa Herakali ambao hujulikana kama utendi wa Tambuka wa mwaka 1728.

MAMBO YALIYOELEZWA KINYUME NA UKWELI WA MAMBO

Dhima ya Wanaleksikografia katika kukuza lugha ya Kiswahili

Mwandishi anadai kuwa wazungu walioeneza Kiswahili kipindi cha Uingereza walikuwa wanaleksikografia. Hii si kweli kwani wao walikuwa wafanya biashara, wapelelezi na wamishionari tu. Lengo la kuandika kamusi lilikuwa ni kwa ajili ya kuwasaidia wazungu wenzao kujifunza lugha kutoka huko kwao ili wakija pwani ya Afrika Mashariki waweze kuwasiliana vyema na wenyeji, ili wapate malighafi kutoka Afrika Mashariki.

Utamaduni wa Kiarabu una vitu vingi vya kiutamaduni kuliko wa Kiswahili

Mwandishi anadai kuwa kuja kwa Waarabu pamoja na dini ya kiislamu kulichangia sana maendeleo ya lugha ya Kiswahili kwa sababu utamaduni wa Kiarabu ulikuwa na vitu vingi vya kiutamaduni.

Hoja hii haina mashiko kwa sababu historia inaonyesha kuwa mahusiano ya kibiashara ndiyo yaliyopelekea kuwepo kwa maingiliano ya kijamii na hatimaye kusababisha hali ya kuazimana na kubadilishana mila na desturi miongoni mwa jamii zilizohusika. Kwa mfano kutoka Asia, Waswahili walipata vitu kama vile nguo na shanga, kwa upande mwingine jamii za Afrika Mashariki zilitoa bidhaa kama vile ngozi za wanyama, magamba ya kobe, pembe za ndovu na nyinginezo. Bidhaa hizo zilipelekwa nchi za nje kama vile India. 

HOJA NZITO: Dhima ya Dini ya Kiislamu

Dini ya kiislamu imechangia kukuza na kueneza Kiswahili Afrika Mashariki na Kati. Kadhalika imechangia katika kuathiri fasihi ya Kiswahili.

Mambo yaliyochangia au kuchochea athari za Kiarabu katika isimu na fasihi ya Kiswahili toka Arabuni ni pamoja na elimu ya madarasa kama vile kusoma na kuandika lugha ya Kiarabu, kusoma kaswida, sira ya mtume. Pia taaluma ya tafsiri ambapo hadithi za mtume zilitafsiriwa kutoka lugha ya Kiarabu kwenda katika lugha ya Kiswahili, pia tafsiri za Kuran. Mbali na elimu ya madrasa, kulikuwepo pia elimu katika ngazi mbalimbali hadi mpaka katika ngazi ya chuo kikuu.

Maingiliano hayo yalichangia jamii hizi kuazimana mila na tamaduni mbalimbali ikiwemo fasihi na isimu.

Kwa mfano, kuingia kwa hati za maandishi ya lugha ya Kiarabu kulichangia mambo kadhaa kama vile kuiweka na kuihifadhi historia ya Waswahili katika maandishi kwa kutumia hati ya Kiarabu.

Ni wazi kuwa Afrika kulikuwa na tendi ambazo zilikuwa katika masimulizi ambapo baada ya ujio wa Waarabu zikawekwa katika maandishi, Mfano Hamziyya,nk
MAPENDEKEZO

Katika mjadala wake hajatuonyesha kuwa uislamu unajitenga na biashara. Hivyo ni vema angezungumzia uislamu bila kuambatanisha na biashara, kama walivyotueleza wakristo kuhusu dini yao. Kwa maana hiyo angeweza kutueleza kuwa Kiswahili kimeenezwa na biashara na si dini. Vinginevyo athibitishe kuwa dini ya Kiislamu imefungamana na kada nyinginezo za maisha kama vile biashara, ndoa, na kila kitu katika maisha.
Kwa maana hiyo, tulitaraji pia mwandishi aeleze utata wa mada zihususo dini na fasihi. Mtazamo wa dini ya kiislamu na dini ya kikristo kuhusu sanaa, na maisha kwa jumla ni mmoja? Labda hiki ndicho kilichowafanya wahakiki wa mwanzo kutojadili dhima ya dini ya kiislamu katika kukuza lugha ya Kiswahili na fasihi ya Kiswahili.

HOJA TETE

Utafiti ufanyike ili kujua uwezekano wa tendi hizi kama ziliwahusu Waswahili na utamaduni wao au ziliwahusu Waarabu kwani maudhui ya tendi nyingi kati ya hizi alizorojeleamwandishi yanaelekea kujadili maadili na maonyo ya jamii ambazo zinahusiana sana na uislamu.

MAREJEO

Bosha, I. (1993). Taathira za Kiarabu Katika Kiswahili Pamoja na Kamusi Thulathiya. Dar es Salaam: Dar es Salaam University Press
Bosha, I.1994. Athari za Kiarabu katika Kiswahili Sanifu. Tasnifu ya Uzamili (Isiyochapishwa), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
Chimerah, R.1998. Kiswahili: Past, Present and Future Horizons. Nairobi: Nairobi University Press
Chiraghdin, S. na Mnyampala, M. 1977. Historia ya Kiswahili. Nairobi: O.U.P.

Gerard, Albert 1981. African Language Literatures: An Introduction to the Literary History of Sub- Saharan Africa. Harlow: Longman Burntmill (pp. 93 – 153)
Kimemia, J. N. 2001. Kiswahili: The Dilemma of Developing The National Language. Egerton University Press
Khatib, M. S. 1983. Historia na Maendeleo ya Kiswahili Zanzibar. Katika: TUKI. Lugha ya Kiswahili. Makala za Semina ya Kimataifa ya Waandishi wa Kiswahili 1. Dar es Salaam: Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (uk. 19 – 50)

Marcel, B.1983. Lugha ya Kiswahili Nchini Burundi. Katika: TUKI. Lugha ya Kiswahili. Makala za Semina ya Kimataifa ya Waandishi wa Kiswahili I. Dar es Salaam: Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (uk. 55 – 61)

Massamba, D. P. B. 1986. “On the Inflence of Local Languages on Kiswahili: The case of Mara Region in Tanzania.” In: Kiswahili: Juzuu 53/1 na 53/2 (pp. 67 – 83)
Mazrui, A.A. and A. Mazrui, 1995. Swahili State and Society: The Political Economy of an African Language. Nairobi: East African Education Publishers
Mbaabu, I. 1978. Kiswahili Lugha ya Taifa. Nairobi: K.L.B

Mbaabu, I. 1985. New Horizons in Kiswahili. Nairobi: K.L.B

Mbaabu, I. 1991. Historia ya Usanifishaji wa Kiswahili. Nairobi: Longman Kenya Ltd. The Journal of Pan African Studies, vol.2, no.8, March 2009
Mukuthuria, M. 2001. Matatizo Yanayokabili Kiswahili Karne ya Ishirini na Moja. Katika: Islamic University Journal, Vol. 2 No.2, Mbale – Uganda (uk. 135 – 142).
Mwongera, N.S. 1994. An Economic History of the Imenti of Mt. Kenya, 1800 – 1945. [Unpublished M. Phil. Thesis] Moi University.
Nurse, D. and Spear, T. (1985) The Swahili: Reconstructing the History and Language of an African Society, 800 – 1500. University of Pennsylvania Press.
Ogutu, M. A. and Kenyanchui, S. (1987) An Introduction to African History up to 1885. Nairobi: College of Adult and Distance Education, University of Nairobi.
Prins, A.H.J. (1967) Swahili Speaking Peoples of Zanzibar and the East African Coast. London: International African Institute.
Sengo, T. S. Y. (1998) Kiswahili na Uisilamu Afrika Mashariki. Unpublished Semina Paper, Islamic University in Uganda.

Shabani, Mujyambere, H. 1983. Lugha ya Kiswahili Nchini Rwanda. Katika: TUKI. Lugha ya Kiswahili: Makala za Semina ya Kimataifa ya Waandishi wa Kiswahili 1. Dar es Salaam: Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (uk. 51 – 54).Hali/hadhi ya Kiswahili nchini Uganda ikoje? Kwa nini?
  • Serikali ya Wakoloni wa Kingereza ina mchango gani huko Uganda katika kukiza na kukididmiza Kiswahili?
  • Makala imesema lolote kuhusu athari za Uislamu katika fasihi ya Kiswahili? Kwa nini?
  • Mjadala huu unatukumbusha tudadisi kuhusu uhusiano kati ya Uislamu na jadi ya tendi Barani Afrika. Katika mjadala huo lazima tukumbuke mambo kama vile kuja kwa hati za maandishi ya Kiarabu, kuja kwa fasihi ya Kiarabu kama vile masimulizi ya Alfulelaulela na hekaya za Abunuasi, kutafsiriwa kwa hadithi za mtume na Kurani (visa vingi vya kidini), ……

1 comment:

  1. KUNA USHAHIDI WOWOTE WA NDOA KATI YA WASWAHILI NA WAARABU?....NAOMBA MSAADA KAMA UPO

    ReplyDelete