UCHAMBUZI WA TAMTHILIYA YA MUKWAVA WA UHEHE.
Uwasilishaji
UTANGULIZI
Mukwava wa Uhehe ni tamthiliya iliyoandikwa na Mulokozi (1988) na kuchapishwa kwa mara ya kwanza mwaka 1979 na Dar es Salaam University Press.
Tamthiliya hii inamuhusu zaidi Mukwava wa kihistoria ambaye alikuwa ni miongoni mwa viongozi mashuhuri wanaokumbukwa katika historia ya Afrika kwa kuwaongoza watu wao katika vita vya utetezi dhidi ya majilio ya kimabavu ya wakoloni. Uvamizi huo wa kikoloni katika Afrika ulijitokeza kwa nguvu hasa katika nusu ya pili ya karne ya kumi na tisa, na mwanzoni mwa karne ya ishirini. Uvamizi huo ulijitokeza wakati huo kwa sababu ya mabadiliko ya kiuchumi yaliyotokea huko Ulaya. Viwanda vilikuwa vimepanuka na hivyo walihitaji wafanyakazi wengi zaidi, mali ghafi nyingi zaidi kuliko awali, eneo kubwa kwa ajili ya upatikanaji rahisi wa mali ghafi hiyo pamoja na soko kubwa zaidi kwa ajili ya bidhaa zao.
Tamthiliya hii ina vitendo viwili. Kitendo cha kwanza kimegawanyika katika maonyesho sita (6) na kitendo cha pili kimegawanyika katika maonyesho manne (4).
KITENDO CHA KWANZA
Onyesho la 1
Ni onyesho linaloonyesha sherehe iliyofanyika Ivaha, baada ya mashujaa kurudi kutoka vitani ambapo sherehe hiyo iliambatana na ngoma na vigelegele kwa ajili ya kuwapokea mashujaa akiwamo shujaa mkuu Mwanafyale Mtage.
“Mwakiyombwe: Leo tunampokea Mwanafyale Mtage kutoka vitani. Ni huyo anawasili mnaweza kusikia ngoma na vigelegele…..Mwanafyale Mtage mwana wa Mutwa wetu, Muzangila wa Image, shujaa wa Uhehe na jemadari aliyeleta ushindi. Shujaa huyu aliambatatana na mashujaa wadogo akiwamo; Mpangile, Ngosingosi, Mwamugumba, Sekulanga, Musatima, Mubogomasori ambao waliwapiga wamasai. Lengo la sherehe hii ilikuwa ni kuwakabidhi mashujaa hawa kwa Mutwa Mukwava.”
Onyesho la 2
Ni onyesho linalotendeka nyumbani kwa Semusilamugunda mke mkubwa wa Mukwava. Nyumbani kwa Semusilamugunda anapita mke mdogo wa Mukwava ambaye ni Muganga. Semusilamugunda anamshauri Mukwava aunde udugu na Wadachi kwa kuoa msichana wa kidachi ili wasitishe mapigano. Semusilamugunda alimshauri Mukwava amwoe Mdachi lakini Mukwava alikataa ushauri wake.
Onyesho la 3
Ni onyesho linaloonyesha muktadha wa Dar es Salaam, sebuleni kwa Nyundo ambamo wamo Wadachi akiwemo Nyundo, Kasisi, Kaufmann na Gavana wakigawana majukumu ya kufanya. Kasisi alipewa jukumu la kusambaza dini ya kikristo, Kaufmann alipewa jukumu la kufanya biashara na Nyundo alipewa jukumu la kwenda uheheni kumkamata Mukwava.
Onyesho la 4
Ni onyesho linaloelezea mabishano kati ya askari wawili ambao ni Mwangimba na Mwamusamba, pia mabishano kati ya koo mbili, ukoo wa Muyovela na ukoo wa Mamuyinga.
Onyesho la 5
Onyesho hili linaonyesha Mubogamasoli anamtuma mtumwa wake kwenda kwa Wadachi kuwaambia kama watamsaidia kuupata ufalme wa Uhehe basi atawasaidia kuuteka uhehe. Kabla mtumwa hajafikisha ujumbe kwa Wadachi anatoa siri kwa Mupangile ambaye ni miongoni mwa askari wa Uhehe. Pia onyesho hili linaonyesha askari waliokuwa wamejificha vichakani wanauteka msafara wa Wadachi uliokuwa unaongozwa na Nyundo. Nyundo anauwawa pia bunduki 300 za Wadachi zinatekwa na askari kadhaa ambao walikuwa wanawasidia Wadachi walitekwa. Kwa upande wa Uhehe shujaa Ngosingosi aliuwawa na Wadachi na Mubogamasoli aliuwawa kwa amri ya Mukwava kwa kitendo cha kutaka kuisaliti nchi yake na kushirikiana na Wadachi baada ya kukosa ufalme wa Uhehe. Kitendo cha kuuliwa Mubogamasoli ndicho kinamfanya Musatima kwenda kushirikiana na Wadachi.
Onyesho la 6
Ni onyesho linaloonyesha Merkl anapeleka taarifa kwa Gavana kuwa kikosi cha Wadachi kimetekwa, baadhi ya askari wa kidachi wameuwawa akiwemo Nyundo na wengine wametekwa na wahehe. Kitendo hicho cha kuuwawa kwa Wadachi kinamfanya Gavana amtume Karani amchunguze Von Zelewski na Sajin Merkl kama ni Wadachi halisi kwa asili au ni watu wa mataifa tu walioajiriwa katika jeshi lao, kwa sababu hawawezi wakashindwa na washenzi katika vita.
KITENDO CHA PILI
Onyesho la 1
Onyesho hili linaonyesha matayarisho ya vita kwa upande wa Uhehe yakiambatana na uchezaji wa ngoma na kusalia miungu (matambiko). Matayarisho ya vita hufanyikia Ivaha (Ikulu ya Uhehe).
Onyesho la 2
Ni onyesho linaloonyesha mapambano ya vita kati ya Wadachi na Wahehe, katika mapigano hayo baadhi ya mashujaa walikamatwa na kuuwawa. Mtoto wa mwanamke aliyetumwa na Mukwava kama mpelelezi aliuwawa, pia Mwakiyombwe aliuwawa. Mke wa Mukwava, dada yake na mtoto wake Sapi wanapelekwa kifungoni Dar es Salaam.
Onyesho la 3
Onyesho hili linamhusu Musatima ambaye yupo kwenye Misheni ya Tosamaganga akiwa na Kasisi, katika maongezi yao Kasisi anamwambia Musatima kuwa Mupangile amekamatwa na kunyongwa na Wadachi. Baada ya kusikia kifo cha Mupangile, kifo hicho kilimsikitisha Musatima ambaye alikuwa kaka wa kuchanjana damu na Mupangile.
“Musatima: Ndugu yangu amenyongwa na wewe umenidhihirishia kunyongwa kwake. Na sasa unakuja kuniambia bila haya kwamba nichukue nafasi yake! Ahsante sana, hisani yako siitaki. Sasa nimejitambua mimi ni nani na wewe ni nani. Nimejua nipo wapi. Kwa heri; hutaniona tena. Nilidanganywa. Bali sasa nimeivuka njia panda, na kutoka hapa nitaifuata njia ya kweli, njia ya haki, njia ya Mupangile ndugu yangu……..Ah, Mupangile ndugu yangu, Mupangile ndugu yangu.”
Onyesho la 4
Ni onyesho linaloonyesha Musatima anarudi kwa Mukwava kuomba msamaha na kukiri makosa yake.
“Musatima: Ni majuto Mutwa wangu. Ni uchungu ulio moyoni mwangu. Nimeyagundua makosa yangu. Nilikuwa nimepotea sasa nimejitafuta na kujua nipo wapi”.
Muda ambao Musatima alikwenda kuomba msamaha alikuwa ameshatoa taarifa zote kuhusu Uhehe na alipojificha Mukwava. Kutokana na taarifa alizozitoa Musatima ndipo Wadachi walipoanza safari ya kwenda kumtafuta Mukwava alipo naye Mukwava alikuwa na taarifa kuwa anatafutwa, ndipo Mukwava anaonekana kujiua mwenyewe baada ya kusikia anatafutwa.
“Mukwava: …Naweza kusikia sauti za shangwe za mashujaa hao zikiniita. Nchi yangu inaniita. NINAKWENDA! (anajipiga risasi na kufa hapohapo)”.
Hivyo Mukwava hakutaka kuuwawa na Wadachi akaamua kujiua mwenyewe. Na baada ya Mwangimba ambaye alikuwa mlinzi wa Mukwava alipoona Mukwava amejiua ndipo na yeye akajipiga risasi.
Baada ya kuangalia maonyesho yaliyojotokeza katika tamthiliya ya Mukwava wa Uhehe ifuatayo ni miktadha iliyojitokeza katika katika tamthiliya hii.
Tamthiliya ya Mukwava wa Uhehe ina muktadha wa kihistoria, kifasihi na kijamii.
MUKTADHA WA KIHISTORIA
Ni muktadha unaoonyesha matukio mbalimbali ya kihistoria ambayo ni ya kweli. Muktadha wa kihistoria katika tamthiliya hii kwanza kabisa unamhusu Mukwava wa Uhehe ambaye alikuwa kiongozi miongoni mwa viongozi mashuhuri wanaokumbukwa katika historia ya Afrika kwa kuwaongoza watu wao katika vita vya utetezi dhidi ya majilio ya mabavu ya ukoloni.
Muktadha mwingine wa kihistoria ni ujilio wa Wadachi katika pwani ya Afrika Mashariki na shughuli zo walizokuwa wakizifanya kama biashara, kueneza dini na kutafuta maeneo ya kutawala (uk 38 na 39).
Muktadha mwingine ni wa mapigano ya Wahehe na makabila mengine ya Kiafrika, mfano, Wangoni, Wamasai, Wasangu na Wanyamwezi, haya yamejitikeza katika onyesho la kwanza.
Muktadha huu unatuonyesha kwamba jamii za zamani zilikuwa zinatawaliwa na mfalme aliyeitwa Mutwa na utawala huo ulikuwa ni wa kurithishana kiukoo. Mfano Mukwava alikuwa Mutwa wa Wahehe. Mifano ya maeneo yaliyokuwepo zamani ni Kwilenga, ambayo kwa sasa ni Kalenga, Ruvaha ambayo kwa sasa ni Ruaha na mji mwengine ni Misheni ya Tosamaganga.
MUKTADHA WA KIJAMII
Muktadha katika tamthiliya hii umegawanyika katika sehemu mbili ambazo ni muktadha wa jamii ya Wahehe na muktadha wa jamii ya Wadachi.
Muktadha wa jamii ya Wahehe, unahusu zaidi imani na utamaduni wao. Imani yao imejikita zaidi katika kuamini kuwa miungu ndio msingi mkuu wa shughuli zao. Mfano, wanaamini katika mahoka na wahenga. Hivyo kabala hata ya kwenda vitani walitambikia mizimu yao.
Mukwava: (kwa mganga) Dawa za kuzinduka na kuagua tayari.
Muganga: Kila kitu tayari Mutwa wangu.
Mukwava: Umeona?
Muganga: Nchi nimeizindika. Lakini nchi haijawa dhahiri. Tusubiri tuone.
Mukwava: Sii kitu. Lete dawa ya kuwazindika mashujaa.
Muganga: (akiinua tunguli moja) Hii ni dawa ya kuwazindika mashujaa, dawa ya ujasiri na nguvu. (Mukwava anapokea tunguli la dawa, analiinua juu na kusali kwa mahoka).
Mukwava: Enyi wahenga mlioko Lihoka, enyi mababu mliopumzikia Ng’uluhe. Enyi wahenga mliolala Lung’emba. Enyi mahoka wa taifa letu mlioko Muhwana. Tusikilizeni wana wenu enyi miungu watukufu, tujalieni nguvu, tujalieni baraka, na usalama. Tujalieni ushindi tuihami nchi yenu mababu zetu…. (Uk 73, 74).
Muktadha wa jamii ya Wadachi, katika muktadha wa jamii ya Wadachi umeegemea katika imani. Wadachi walikuwa na imani tofauti na Wahehe, wao waliamini katika Kristo ambaye walisema ndiye Mungu wa kweli. Ujio wa Wadachi ulianza kufifiza na kubeza imani ya Wahehe hivyo walifungua misheni mbalimbali kwa ajili ya kueneza dini ya kikristo kwa Wahehe na makabila mengine ya Kiafrika.
MUKTADHA WA KIUTAMADUNI
Muktadha huu unahusu utamaduni wa Wahehe, mfano sherehe za kimila ambazo zilikuwa za kuwapokea mashujaa waliokuwa vitani. Sherehe hizo huambatana na ngoma na unywanji pombe za kikabila (uk 24).
“Mwakiyombe: Asante bwana Mubogamasoli. Nafurahi kuwatangazia Wahehe wote kwa niaba ya Mutwa Mukwava kuwa sherehe za kuadhimisha ushindi zimekwisha kuanza rasmi, Mutwa wetu ametoa ng’ombe kumi na mitungi mia ya pombe ya vichwa kwa heshima ya siku hii. Kila mtu anywe, ale na kufurahi, hata penye uwingu panaweza kuwa na ung’avu”.
MUKTADHA WA KIFASIHI
Muktadha wa kifasihi uliokuwepo katika jamii ya Wahehe ilikuwa fasihi simulizi kwani jamii hiyo haikuwa na fani au taaluma ya kusoma na kuandika, hivyo fasihi na historia ya Wahehe ilirithishwa kizazi na kizazi kwa kutumia masimulizi ya hadithi na uchezaji wa ngoma katika shughuli mbalimbali za kijamii.
FANI NA MAUDHUI
Muundo wa tamthiliya ya Mukwava wa Uhehe imejengwa na vitendo viwili. Kitendo cha kwanza kina maonyesho sita na kitendo cha pili kina maonyesho manne. Tamthiliya hii ni ya masimulizi iliyo katika majibizano ya wahusika. Pia kuna maelezo ya jukwaa ambayo huonyesha matendo na maleba ya wahusika.
Kisa/hadithi ya tamthiliya.
Tamthiliya hii inasimulia mapigano ya kihistoria kati ya jamii ya Wadachi na jamii ya Wahehe.
Vitushi na mpangilio wake katika tamthiliya.
· Kitushi cha kwanza kinahusu Wahehe kwenda kupigana vita msituni na kupotelea hukohuko (uk 9).
· Kitushi cha pili ni mapambano dhidi ya Wahehe na Wamasai yakiambatana na sherehe za kuwapongeza mashujaa baada ya kuwashinda Wamasai (uk 24).
· Kitushi cha tatu ni ushawawishi uliofanywa na Semusila kwa Mukwava juu ya kuunda udugu na Wadachi kwa kumwoa binti wa kidachi ili wasitishe mapigano na Wadachi (uk 34, 35).
· Kitushi cha nne kinahusu Wadachi ambao waligawana majukumu ya kufanya, ambapo Nyundo alipewa jukumu la kwenda kumkamata Mukwava wa Uhehe (uk 44).
· Kitushi cha tano kinaonyesha maandalizi ya vita kwa Wahehe ambayo yanaambatana na sherehe (matambiko) onyesho la nne.
· Kitushi cha sita kinaonyesha vita kati ya Wahehe na Wadachi ambapo wahehe wanaonekanma kushindwa baada ya kusalitiana wenyewe.
Topo
Katika tamhiliya hii kuzaliwa kwa shujaa imejitokeza katika onyesho la kwanza katika kitendo cha pili ambapo mwandishi anasema, siku aliyozaliwa Mukwava jua lilisimama wima, mawingu yaliyeyuka katika anga lote na ulimwengu mzima ulitambua. (uk 72)
Motifu mbalimbali za Tamthiliya hii na jinsi zinavyokamilisha muundo
Katika Tamthiliya hii motifu mbalimbali zimejitokeza ikiwemo motifu ya msako, ya safari na motifu ya kifo.
Motifu ya safari
· Safari ya watu wa mataifa mengi waliosafiri kwenda mbali maporini kwenda kupigana na kupotelea hukohuko (uk 19).
· Safari ya Wahehe kwenda kuwapiga Wamasai (uk23).
· Safari ya Wadachi kutoka Dar es saalam kwenda Uheheni kwenda kumkamata Mukwava.
· Safari ya Mukwava kutoka Ivaha kuelekea Kwilenga ili kuwakimbia Wadachi
Motifu ya Msako
· Motifu hii inahusu Wadachi kusaka ngome ya Ivaha mahali ilipo.
· Wadachi wanamsaka Mukwava porini alikokimbilia.
Motifu ya kifo
· Katika tamthiliya hii kuna vifo vya mashujaa mbalimbali. Kifo cha kwanza ni cha Ngosingosi ambaye aliuwawa na Wadachi. Kifo cha pili cha Mwakiyombwe ambaye aliuwawa na Wadachi kwa kukataa kutoa taarifa za Mukwava. Kifo kingine ni cha Mubogamasoli aliuwawa kwa amri ya Mukwava kwa sababu ya kutaka kuisaliti Uhehe.
· Pia kifo cha mtoto wa mwanamke aliyeuwawa na Wadachi baada ya kuona mtoto ndiye aliyekuwa akimpa mwanamke huyu kiburi cha kuwajibu majibu ya kashfa Wadachi.
· Motifu nyingine ya kifo ni kifo cha Nyundo ambaye aliuwawa na kikosi cha askari wa Uhehe. Pia kifo cha Mukwava aliyejiuwa kwa kutotaka kuwa mtumwa na pia kutotaka kuuliwa na Wadachi.
· Kifo kingine ni cha Mwangimba ambaye alijiua baada ya kumwona Mukwava kajiua.
Motifu hizi zinakamilisha muundo kwa kuangalia mpangilio wa visa na matukio yalivyoundwa yaani chanzo cha msafara wa Wadachi ni kumsaka Mukwava ambao ulisababisha tukio la kujiua kwa Mukwava.
Shujaa wa tamthiliya
Shujaa katika tamthiliya hii ni Mukwava ambae ni shujaa wa kihistoria na kiutamaduni ambae anafuata utamaduni wa Wahehe ambao kunywa pombe ya kienyeji, kucheza ngoma na kutambika. Usawiri wa shujaa huyu ni matendo mbalimbali ya kishujaa ambayo aliyokuwa anayafanya katika jamii ya Uhehe ambayo aliyafanya kabla ya vita vya Wadachi, matendo hayo ni kama kupigana na makabila mabalimbali kama vile Wangoni, Wamasai, Wanyamwezi pamoja na Wasangu ambapo ilipepelekea yeye kuonekana ni shujaa na kutunukiwa ufalme wa juu (Mutwa) uk 23.
“Mukwava: Vizuri! Wahehe, ingawa tuliwashinda Wamasai na tuliwashinda Wangoni na Wanyamwezi na Wasangu lakini hao sisi sio maadui zetu hasa.
Pia shujaa huyu anaonekana kushindwa mwishoni kutokana na kuona vita vya Wadachi vinamshinda na kuamua kujiua mwenyewe (uk 103).
“Mukwava: ……naweza kusikia sauti za shangwe za mashujaa hao zikiniita. Nchi yangu inaniita. NINAKWENDA! (Anajipiga risasi na kufa hapohapo)”.
Tabaka la shujaa: tabaka analotoka shujaa ni tabaka la juu kati ya matabaka ya juu mawili yaliyokuwa katika jamii ya Wahehe.
Dhamira anazowakilisha shujaa huyu ni kama zifuatazo;
Umoja na ushikamano, shujaa huyu aliunganisha jaamii mbalimbali na kuunda jamii moja ya wahehe, pia alishirikiana na viongozi/ mashujaa wadogowadogo walioko chini yake kama vile Mwangimba, Mtage, Ngosingosi, Mwakiyombe.
Licha ya dhamira hiyo kuna dhamira nyengine ni pamoja na ujasiri, uzalendo na kujitoa muhanga.
Katika tamthiliya hii jaala ya shujaa ni anguko la kujiua mwenyewe kwa kujipiga risasi baada ya kuona kuwa baadhi ya wanajamii wa Kihehe wamemsaliti na kuona kuwa vita vya wadachi vimemzidi nguvu na kuona kuwa kuliko kuishi mtumwa bora ajiue.
Wahusika wanaomuunga shujaa.
Wahusika wanaomuunga shujaa ni pamoja na Mtage, Semusila, Ngosingosi, Mwangimba, Muganga na Mupangile.
Hatima ya wahusika hawa, baadhi yao walikufa kwenye mikono ya wadachi mfano, Ngosingosi, Mupangile (uk 96, 97) na baadhi walifungwa gerezani na wadachi huko Dar es Salaam ambao ni Mtage, Mke wa Kwava, mtoto wa Kwava ambaye ni Sapi (uk 88).
“Sakarani: vizuri sana mtoto mzuri sana wewe (kwa Merkl) hawa mateka wengine wapeleke gerezani. Huyu mke wa Kwava na huyu dada yake na huyu motto wake Sapi watasafirishwa wakafungwe huko Dar es Salaam. Si vizuri kuwaweka hapa watu wawaone kila siku. Wengine hawa waliobaki tutajua la kuwafanya. Haya, Sajini!”
Wahusika wanaompinga shujaa
Wanaompinga shujaa ni Mubagamasoli na Musatima. Hawa walimpinga kwa sababu Mubagamasoli, Mukwava alimchukulia mpenzi wake na pia alimpinga kwa sababu alimuuwa baba yake, onyesho la tano. Musatima alimpinga kwa sababu Mukwava alikuwa anaupa hadhi ya juu ukoo wa Mamuyinga ambapo ndipo alitoka Mukwava na pia kumuua kaka yake Mubagamasoli. Hatima yake wahusika hawa walipelekea anguko la shujaa Mutwa Mukwava.
Lugha na mbinu nyingine za kisanaa.
Lugha iliyotumika ni lugha rahisi isiyokuwa na msamiati mgumu, pia lugha hii ni ya masimulizi ambayo inasimulia zaidi kuhusu historia ya Mutwa Mukwava katika jamii ya Wahehe pamoja na vita ya Wadachi ambayo ipo katika muundo wa daiolojia.
Mbinu nyingine za kisanaaa zilizojitokeza katika tamthiliya hii ni pamoja na;
Tashibiha, mfano
“Waoga kama viroboto” (uk 38)“Makanwa yake kama ya kima” (uk 38)“Mrefu kama jadi yetu, mpana kama dunia” (uk 20)“Ushujaa wangu ulimnasa kama ulimbo” (uk47).
Tanakali sauti, mfano;
“Ptuu! (Anatema)” (uk 26)
Tashihisi, mfano
“Hata mti unaweza kuwa na masikio” (uk 27).
Methali, mfano
“Akutangukiaye chaneni ukuzidi tonge” (uk 28).“Kuchavyo sivyo kuchwavyo” (uk 27)“Penye uyoga hapakosi mavi” (uk 28)“Kwa mwoga huenda kicheko na kwa shujaa huenda kilio” (uk 48)“Ukuni mfupi hauwaki mekoni” (uk 24)“Damu nzito kuliko maji” (uk 24)
Misemo; mfano
“Usimwone simba kalala ukadhani paka” (uk 53)
Takriri, mfano
“Sikilizeni, sikilizeni, enyi wahehe mlioko katika lipuli hapa..” (uk 49)
Fomula
Tamthiliya hii ya Mukwava wa Uhehe haina fomula yaani haina mianzo na miisho ya kifomula.
Dhima na nafasi ya utendi huu
Katika jamii utendi huu una dhima ya kuelezea historia nzima ya jamii ya Wahehe pamoja na kiongozi wao Mutwa Mukwava jinsi alivyopigana na wakoloni yaani Wadachi, pamoja na baadhi ya makabila yakiwemo Wamasai, Wangoni, Wanyamwezi pamoja na Wasangu. Na jamii ikisha soma huelewa kuhusu historia au maisha ya Mutwa Mukwava wa uhehe, pamoja na maisha ya uongozi wake kwa ujumla. Kwa hiyo tamthiliya hii ya Mutwa Mukwawa ni ya kihistoria na si ya kisasili.
Utamaduni
Utamaduni katika tamthiliya hii umejikita zaidi katika jamii ya Wahehe. Utamaduni huo uliambatana na masuala ya kijadi ambayo ni matambiko yaani miungu waliyokuwa wakiiamini ambayo ni mahoka na wahenga pamoja na ngoma walizokuwa wakizipiga ambazo ziliambatana na uchinjwaji wa ng’ombe na unywaji wa pombe (uk 73,74). Kwa hiyo utamaduni huu ni wa jamii ya Wahehe. Kupitia shujaa,,,,,, tunafahamu kuwa huyu alikuwa shujaa wa kijadi.
Utaifa
Utendi huu sio wa taifa bali ni wa jamii ya Wahehe kwa sababu unaelezea Mutwa wao pamoja na mila na desturi yao.
Dini
Imani iliyojitokeza katika tamthiliya ya Mukwava wa Uhehe ni kuabudu miungu ambao ni Mahoka na Wahenga, hawa ndio jamii ya Wahehe waliokuwa wakiomba shida zao mbalimbali mfano kushinda katika vita, njaa pamoja na ukame.
Tamthiliya hii ni tendi kutokana na wataalamu wawili wanavyoelezea ili tendi iwe tendi kuna sifa zinazostahiki. Wataalamu hao ni Johnson (1978, 1979) na Mulokozi (2002).
Johnson (1978, 1979) anasema kuwa shujaa wa Kiafrika lazima awe na nguvu ya sihiri na nguvu ya rijali.
Mulokozi (2002) anakubaliana na Johnson kwamba mashujaa wa Kiafrika labda waathiriwe na mtazamo wa Ulaya bali sio watumwa wa miungu. Bali, shujaa wa Afrika lazima wawe na nguvu ya sihiri (nguvu za kiuchawi), nguvu za shakii (nguvu za mtu za urijali na ubunifu wake na za kijadi) na nguvu za watu anaokumbana nao ambao humfanya aanguke au asianguke.
Hivyo kutokana na wataalamu wa hapo juu tunahitimisha kuwa tamhiliya ya Mukwava wa Uhehe ni tamthiliya ya kishujaa kwani ushujaa wa shujaa Mukwava unatokana nguvu zake mwenyewe, nguvu za sihiri na nguvu za watu waliomfanya aanguke. Kadhalika huu ni utendi ambao upo katika umbo la tamthiliya au drama.
No comments:
Post a Comment