Sunday, 25 August 2013

UCHAMBUZI


UCHAMBUZI WA TAMTHILIYA YA FUMO LIONGO ILIYOANDIKWA NA EMMANUEL MBOGO
(Uwasilishaji)

UTANGULIZI

Haya ni masimulizi ya kitendi yaliyowekwa katika umbo la tamthiliya, ambapo mwandishi wa tamthiliya hii Emmanuel Mbogo  amechota visa na matukio kutoka katika utendi wa Fumo Liyongo na kuweka ubunifu wake.  Katika tamthiliya hii mwandishi anamtumia mhusika Fumo Liongo kama shujaa wa kitendi, katika kumuelezea Fumo Liongo mwandishi anagawa visa vyake katika vitendo vitano na kila kitendo kina maonesho mbalimbali.

Katika kitendo cha kwanza (onesho ni mji wa Pate) mwandishi anaanza kwa kuwaonesha wananchi wa Pate wakienda kumlaki Liongo baada ya kurudi kutoka vitani ambako aliweza kumshinda adui yake Sango Vere. Liongo anapokelewa kwa shangwe na watu wa Pate na kuhutubia umati akiwapa hali halisi ilivyokuwa katika uwanja wa kivita. Katika onesho la pili tunamuona mfalme na waziri kiongozi wakipanga mikakati ya kumuua Liongo.
Matukio ya kitendo cha pili yanaanzia  katika mji wa Fumo Liongo ambapo tunamuona Fumo Liongo akiwa na mama yake (Mbwasho) pamoja na Sada ambaye ni kijakazi wa Liongo, katika sehemu hii tunaona Liongo akipewa maonyo na mama yake juu ya mienendo yake juu ya Mfalme Daudi (onesho ni mji wa liongo). Onesho linalofuata tunaona Liongo anakaribishwa katika chakula cha mchana na mfalme ili waweze kumnasa kwa kumtilia sumu (nyongo ya mamba) katika chakula, na laiti ikishindikana kufa kwa sumu basi waweze kumnasa na kumtia gerezani. Katika onesho hili mfalme anafanikiwa kumnasa Liongo na kumtia gerezani.
Kitendo cha tatu, tunaona Liongo anatoroka gerezani kwa msaada wa mama yake na Sada, hii inatokana na tupa iliyowekwa katika mkate ambayo ilimsaidia katika kukata kamba alizokuwa amefungwa.
Katika kitendo cha nne tunaona Fumo Liongo akirudi nyumbani akiwa amejeruhiwa baada ya kutoroka gerezani, anamuaga mama yake pamoja na Sada na kuchukua silaha zake na kutokomea katika msitu wa kuzimuni kumkimbia mfalme Daudi. Huku ikulu kwa mfalme, tunamuona mfalme Daudi na waziri kiongozi wakipanga mipango mingine ya kumkamata Liongo na kumuua, ndipo lilipopatikana wazo la kumtumia mtoto wa kambo wa Liongo aitwaye Zahidi.
Katika kitendo cha tano tunaona Zahidi akiwasili ikulu kwa mfalme kuja kupokea agizo la kwenda kutafuta siri ya kifo cha Liongo huku akiwa ameahidiwa mambo mbalimbali na mfalme endapo atafanikisha, Zahidi baada ya kujazwa uongo kichwani mwake na Mfalme pamoja na Waziri Kiongozi anafunga safari mpaka msituni kwa Liongo na pasipo matarajio Zahidi anafanikiwa kupata siri ya kifo cha Liongo baada ya Liongo mwenyewe kumpatia siri hiyo. Habari zote alizoelezwa zahidi anamfikishia Mfalme na ndipo Mfalme anampatia sindano ya shaba na Zahidi anamchoma Liongo kitovuni akiwa usingizini. Mwisho tunaona Liongo akikata roho kisimani mbele ya mama yake na umma wa watu wa Pate.
Hivyo basi, kutokana na utangulizi huo tunaona kuwa visa na matukio katika tamthiliya ya Fumo Liongo ni vya kiusiganifu ukilinganisha na vile vilivyomo katika Utendi wa Fumo Liyongo. Mfano tukio la kusalitiwa kwa shujaa Liongo katika tamthiliya hii lilifanywa na mtoto wa kumkuta wa Liyongo aliyejulikana kwa jina la Zahidi, tukio hili ni tofauti kabisa na lile lililojitokeza katika utenzi wa Fumo Liongo. Hata katika uelezwaji wa kifo cha Fumo Liongo kimeelezwa tofauti katika tamthiliya hii.
Kutokana na kuanguka kwa shujaa katika tamthiliya hii, tunaona tamthiliya hii inaangukia katika kumbo la tamthiliya za Kiaristotle yaani tanzia. Hii inatokana na anguko la shujaa wa tamthiliya hii. Anguko la mhusika mkuu ndio sifa ya msingi katika tanzia.
Hali kadhalika Kutokana na nadharia ya Kiaristotle inatueleza kuwa tendi lazima iwe na sifa ya kinudhumu, urefu wa kutosha, uunganifu na isawiri maisha ya shujaa. Kutokana na sifa hizi za tendi kama zinavyobainishwa na Finnegan, tamthiliya hii ya Fumo Liongo licha ya kubeba baadhi ya sifa za kitendi lakini umbo la tamthiliya lililonalo linaiweka tamthiliya hii kuwa si tendi kwa kuwa inashindwa kukidhi vigezo hivyo.
Ingawa kwa mujibu wa nadharia hii tamthiliya hii inaondolewa katika makundi ya tendi lakini kimsingi tamthiliya hii yaonekana kuwa ni tendi kwani mabadiliko katikia jamii ndio yanayotupa umbo hili la tendi. Ikumbukwe kuwa tendi zilianza kama masimulizi ya kijadi, baadae ikawekwa katika umbo la kishairi na leo hii tunaona tendi katika umbo la tamthiliya. Ni katika msingi hii ambapo yawezekana baadae kutakuta tendi hizi katika umbo la riwaya.
Baada ya kuangalia utangulizi wa tamthiliya hii ufuatao ni uchambuzi:
Muktadha, Katika tamthiliya hii muktadha uliojitokeza ni kama ifuatayo:
Muktadha wa kihistoria, masimulizi yamejikita katika kuelezea matukio mbalimbali ya kihistoria katika jamii ya watu wa Pate. Mwandishi katika masimulizi yake anataja miji ya kihistoria kama vile Pate pamoja na uwepo wa dola ya kifalme ambazo zilibeba utamaduni wa utawala wa Waafrika. Masimulizi yanaeleza juu ya mfalme aliyejulikana kwa jina la Daudi Mringwari ambaye alikuwa na uchu wa madaraka na hakutaka nafasi yake ichukuliwe na mtu mwingine. Ni katika misingi hii ya uongozi ambapo Mfalme Daudi alipoanza kumchukia Fumo Liongo kwa kuwa alikuwa na sifa ambazo alimzidi.
Muktadha wa kijamii, katika tamthiliya hii mwandishi anataja jamii mbalimbali za Kiafrika. Mwandishi anaonesha shughuli na mambo mbalimbali yanayofanywa na jamii ya watu wa Pate, hali kadhalika mwandishi anaonesha masuala yahusuyo sherehe ambazo zilijumuisha ngoma na nyimbo ambazo zilikuwa zinafanywa na wanajamii wa Pate.
Kazi hii pia kijamii inasawiri mivutano ya kijamii iliyokuwepo barani Afrika ambapo watu waligombana wenyewe kwa wenywe.. vita vya kikabila, kiutawala... migogoro ya kijamii....vuguvugu lililosababishwa na kuongezeka kwa watu, kuanza kukua kwa miji, na vijiji.... mgogoro kati ya maisha ya mijini na maashambani.
Muktadha wa kifasihi, masimulizi katika tamthiliya hii ni matokeo ya tendi simulizi ambapo yamesheheni ubunifu na visa vyake vimetiwa chumvi ili kuleta utofauti katika  masimulizi. Katika kazi hii mwandishi ametumia mbinu mbalimbali za kisanaa kama vile matumizi ya nyimbo ili kusindikiza utendaji wa tamthiliya hii.
Muundo kwa mujibu wa BAKIZA (2010) wanasema kuwa ni umbo la kitu kulingana na kitu kilivyotengenezwa. Katika tamthiliya hii ya Fumo Liongo ni tamthiliya ambayo ina muundo wa kihadithi yaani ni masimulizi ambayo ni ya moja kwa moja, ambapo matukio yanafuatana toka mwanzo hadi mwisho. Katika kufanikisha muundo huu mwandishi amegawa matukio yake katika vitendo vitano vyenye maonesho ndani yake na kila onesho amelipa jina lake. Hivyo mwandishi ameanza kwa kuonesha jinsi Fumo Liongo anavyopokelewa kutokana na ushindi alioupata kutoka vitani, harakati za mfalme za kutaka kumuua Liongo na mwisho kifo cha Liongo.
Ili kuukamilishi muundo huo mtunzi ametumia vitushi mbalimbali. Wamitila (2003) anasema ni sehemu ya hadithi au kisa fulani. Kisa hicho kinaweza kuwa na mambo mbalimbali, katika tamthiliya hii vitushi mbalimbali vilivyojitokeza ni pamoja na mvutano baina ya Liongo na mfalme Daudi.
Usaliti, hili ni tukio au sehemu ya kisa ambayo imetumika katika kujenga kisa kizima. Mwandishi amemtumia mhusika Zahidi ambaye ni mtoto wa Liongo baada ya kuahidiwa na mfalme Daudi alimsaliti baba yake na kumuua.
Mvutano huu ndio unaoibua au kujenga kisa kizima katika tamthiliya hii, kutokana na chuki aliyonao mfalme Daudi kwa kuhofia nafasi yake, ndio iliyosababisha mfalme kutumia mbinu mbalimbali ili kumuua Liongo. Ni mvutano huu uliosababisha kifo cha shujaa Liongo. Usaliti huu ni sehemu ya kisa.
Wamitila (2003) anasema kuwa motifu ni dhana inayotumiwa kurejelea wazo kuu na sehemu ya dhamira katika fasihi, huweza pia kuelezea elementi fulani ya kimuundo au kimaudhui inayotawala kazi fulani.
Katika tamthiliya hii ya Fumo Liongo kuna motifu mbalimbali zilizojitokeza, motifu hizo ni kama zifuatazo:
Motifu ya safari, hii ni motifu inayojitokeza katika tamthiliya hii, katika tamthiliya hii tunaona Zahidi mtoto wa Fumo Liongo anatembea siku mbili kutoka Galla kwenda Pate ili kupeleka taarifa kwa Liongo kuwa mama yake amezaa mtoto wa kiume. Pia lengo lingine la safari yake ni kupeleka zawadi kwa mfalme kutokana na kukubali Liongo kuzaa na raia wake.
Pia kuna motifu ya kifo ambayo imejitokeza kwa shujaa Liongo na mwanae, Liongo anauwawa kwa kuchomwa na sindano ya shaba kitovuni mwake baada mwanawe wa kambo kuahidiwa mali, mke na kupewa uongozi na mfalme Daudi. Hii inasababishwa na Liongo kutoa siri ya kifo chake kwa mwanawe huyo. Pia motifu nyingine ya kifo inajitokeza pale ambapo waziri Msheki anapouwawa na mfalme Daudi kwa sababu ya kumteteta Liongo. Motifu hizi zote ndizo zilizosaidia katika usukaji wa visa na matukio katika kukamilia tamthiliya hii.
Katika tamthiliya hii mhusika mkuu ni Liongo ambaye anatokea katika tabaka la chini, kutokana na ushujaa wake Liongo anakuwa mtu maarufu na anayependwa na watu katika jamii yake. Hivyo katika tamthiliya hii kupitia mhusika Liongo anaibua dhamira mbalimbali kama ilivyofafanuliwa hapa chini.
Dhamira ya ushujaa
Mhusika Liongo katika tamthiliya hii amechorwa kama mtu shujaa anayepigania haki. Ushujaa wa Liongo unaonekana kutokana na jitihada zake alizozifanya katika kuhakikisha anawakomboa wanajamii yake juu ya utawala wa mfalme Daudi. Mambo ya kishujaa ambayo Liongo anayafanya ni pamoja na kutoroka gerezani, kupambana na adui yake Sango Vere katika vita (uk 1) na hatimaye kumshinda. Pia Liongo alipambana na askari watatu ambao walitumwa na mfalme ili wamuue lakini Liongo alifanikiwa kuwaua askari wawili na kumjeruhi mmoja.
Uzalendo na mpigania haki za wanyonge, mwandishi Mbogo anamuonesha Liongo kama mzalendo katika kupigania nchi yake, baada ya taarifa za kuvamiwa kwa dola ya mfalme Daudi na adui Sango Vere, Liongo aliongoza majeshi yake kwenda kumng’oa na kumsambaratisha adui huyo ambaye alionekana kuwa ni mtu hatari katika mapambano.
Dhamira nyingine anazoziwakilisha ni kama vile heshima na maadili, upendo katika familia.
Jaala (TUKI 2004) wanaeleza kuwa jaala ni mambo mtu afanyayo kwa uwezo wake Mungu, majaliwa.
Kutokana na tamthiliya hii, mwandishi Emmanuel Mbogo ameonesha mambo mbalimnali ambayo shujaa Liongo ameyafanya, amefanya kutokana na majaliwa aliyopewa na Mungu/miungu. Miongoni mwa mambo hayo ni kama vile:-
Liongo  alikuwa ni mtu shujaa ambaye alipendwa sana na jamii yake kutokana na mambo aliyowafanyia, hivyo kutokana sifa yake ya ushujaa sifa zake zilivuka mipaka ya nchi yake na kufika hata sehemu jirani. Mambo yote ya kishujaa ambayo alikuwa anayafanya yalitokana na uwezo aliopewa na Mungu ambao watu wengine hawakuwa nao.
Liongo alikuwa ni mwimbaji mzuri katika sherehe mbalimbali ambazo ziliambatana na ngoma, mwandishi anaonesha kuwa hata pale ambapo Liongo alikosekana katika ngoma basi watu walijua kuwa liongo kakosekana. Kila Mbajuni alikuwa anahitaji kusikia Liongo akiimba. mfano (uk 13)
MADI: kila Mbajuni Liongo! Liongo! Imba liongo! Imba Liongo! sijui hawajui kuwa wewe ni binadamu unaweza kuchoka?
Kutokana na harakati hizi za Fumo Liongo wapo wahusika ambao wanamuunga mkono Liongo. Wahusika hao ni kama wafuatao:
Msheki, huyu alikuwa ni waziri katika serikali ya mfalme Daudi, ni mtu mwenye msimamo katika maamuzi ndani ya uongozi wa mfalme Daudi. Msheki alipinga kabisa suala za kuuliwa kwa Liongo kwani aliona kuwa hakuwa na kosa. Mfano (uk 5)
MSHEKI: kuwa Fumo Liongo ni mzalendo na shujaa wa dola hii.
Kutokana na msimamo aliokuwa nao waziri Msheki, Mfalme Daudi aliamuru Msheki auwawe kwa kupigwa nyundo kichwani na kutoswa baharini. Mfamo (uk 7)
MRINGWARI : Hiyo! Mtalimbo toka utosini! Kisha mtoseni baharini.
Hivyo kutokana na amri hiyo ya mfalme, Msheki alipigwa nyundo kichwani na kutoswa baharini.
Machaka, huyu ni mfanyakazi katika ikulu ya mfamle Daudi, ni mtu aliyekuwa anamuunga mkono Liongo, katika harakati zake za kuhakikisha Liongo anakiepuka kifo alifanikiwa kubadilisha kinywaji kilichokuwa kina sumu aina ya nyongo ya mamba ambayo aliwekewa Fumo Liongo. Mashaka alijitahidi kutembea kwa haraka ili kumuwahi Liongo ili amwambie kuwa Zahidi anakuja kukuua lakini alichelewa. Hadi mwisho wa tamthiliya Machaka anafanikiwa kuwaambia umma wa pate kuwa mfalme ndiye aliyemuua Liongo.
Mbwasho na Sada ni wahusika ambao walikuwa wanamuunga mkono Liongo kwani ndio waliofanikisha kutoroka kwa Liongo kutoka Gerezani. Katika kumuunga mkono huku Sada anaishia kuwekwa gerezani na kupata mateso makubwa huku wakimtuhumu kuwa anajua wapi Liongo amekimbilia.( uk 29). Mjadala wetu unadhihirisha kuwa mara nyingi mashujaa wa Kiafrika wanakuwa na msaada wa kundi la watu anaowaongoza.
Kwa upande mwingine wapo wahusika wanaompinga Liongo, wahusika hao wanawakilishwa na Mfalme daudi na Waziri Kiongozi.
Mfalme Daudi, katika uongozi wake mfalme Daudi aliona ana deni kubwa endapo atamuacha Liongo akiwa hai, hivyo alimchukia Liongo kutokana na umaarufu wake ambao ulikuwa unazidi kuongezeka siku hadi siku. Ni katika misingi hii ambapo mfalme aliamua kumuua Fumo Liongo.
Waziri kiongozi, ni mshauri mkuu wa mfalme Daudi, ni mtu ambaye alisuka mipango yote ya kumuua Liongo. Ni mtu aliyeaminika sana na mfalme katika ushauri kwani hata pale ambapo mfalme hukosa njia thabiti ya kumuua Liongo waziri kiongozi alitoa njia mbadala.
Fomula katika tamthiliya hii ni kwamba mwandishi ameanza kwa kuonesha jinsi watu wa Pate wanavyompokea shujaa Liongo kutoka vitani, na mwandishi anamalizia masimulizi yake kwa kuonesha huzuni na vilio vilivyotanda baada ya kifo cha Liongo. Hivyo mwandishi ametumia mianzo na miisho ya kifomula.
Tamthiliya ya  Fumo Liyongo ina dhima na nafasi katika jamii, dhima hizo tunaweza kuzigawa katika makundi matatu ambazo ni historia, utamaduni na dini.
Historia, katika historia tamthiliya hii ya Liongo inaweza kuwa chanzo cha data za kihistoria, wanajamii wanaweza kujua masuala mbalimbali yaliyokuwa yanatokea katika jamii za kipindi hicho. Pia itasaidia kwa watu kujua kuwa Liongo ni moja ya mashujaa wa kiafrika ambaye aliwahi kuishi, kwani masimulizi yanaeleza kuwa Liongo ni moja ya watu ambao waliwahi kuishi.
Hali kadhalika, katika historia itasaidia watu kuona mfumo wa utawala wa kipindi cha zamani na hali ilivyokuwa katika uongozi.
Kwa upande wa utamaduni, tamthiliya ya Fumo Liongo imesheheni masuala  mbalimbali ya kitamaduni kama vile nyimbo na ngoma, hivyo kupitia tamthiliya hii watu watajifunza juu ya utamaduni wa jamii za kipindi hicho. Pia tunaona kuwa suala la ngoma na nyimbo ni suala lililotumika katika kipindi hicho kama sehemu ya burudani. Hivyo tamthiliya hii imejikita katika kuonesha maisha na utamaduni wa jamii wa Wabajuni huko Pate. Kupitia  tamthiliya hii tunaweza kusema kuwa Liongo ambaye ndiye mhusika mkuu na shujaa wa utendi huu ni shujaa wa kiutamaduni kwa sababu anasawiri masuala nyeti yahusuyo utamaduni na jadi za wa Waswahili.

Hivyo kwa kiasi fulani tunaweza kusema kuwa tamthiliya ya Fumo Liongo ni kiwakilishi cha taifa la Waswahili kwani katika masimulizi ya tamthiliya hii yamesawiri mandhari, utamaduni na maisha ya Waswahili kwa ujumla.

Marejeo
BAKIZA(2010) Kamusi ya Kiswahili Fasaha.Kenya.Oxford University Press. East African Limited.
Mbogo, E (2009) Fumo Liongo.Dar es salaam University Press. Dar essalaam
TUKI (2004) Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Dar es salaam.TUKI.
Wamitila K.W (2003) Kamusi ya Fasihi:Istilahi na Nadharia.Nairobi.Focus Publication. 

No comments:

Post a Comment