Sunday, 22 September 2013

ASILI YA KISWAHILI



ASILI YA KISWAHILI: FREEMAN GENVILLE KATIKA “MEDIEVAL EVIDENCES FOR SWAHILI”
Kwanza tutaangalia nini maana ya neno asili, pia tutaeleza kwa ufupi mitazamo mbalimbali kuhusu asili ya lugha ya Kiswahili, halafu tutaangalia kwa undani kiini cha mada yetu kwa kuchanganua vyema mawazo ya Freeman Grenville katika makala yake inayoitwa ‘Medieval Evidences for Swahili’ pia tutaonesha ubora pamoja na udhaifu wake na mwisho tutatoa hitimisho.
Neno asili kwa mujibu wa Massamba na wenzake (1999:3) ni jinsi kitu au jambo lilivyotokea au lilivyoanza.  Fasili hii ni nzuri na inajitosheleza kwa maana kwamba jambo au kitu kinaweza kutokea kibahati kama ilivyo katika lugha au linaweza kuanzishwa.

Hivyo basi asili ya lugha ya kiswahili bado ni mjadala mrefu ambapo wataalamu mbalimbali wanahitilafiana juu ya asili au chimbuko la lugha ya kiswahili. Wapo wanaokinasibisha kiswahili na kiarabu kwa kutumia kigezo cha msamiati na dini ya kiislamu. Wengine wanashikilia kiswahili ni kibantu kwa kutumia hoja za kiisimu na kihistoria. Wapo wanaokinasibisha kiswahili na uchotara baadhi yao wanaoshikilia msimamo huu ni Freeman Grenville na Homo Sasson.
Katika makala yake Grenville inayoitwa “Medieval Evidences for Swahili” anagusia juu ya ujio wa waarabu na asili ya lugha Kiswahili kwa kutumia vyanzo mbalimbali kama vile historia ya mji wa Kilwa ambapo anataja majina ya utani ya wafalme wa kipindi hicho kama vile Nguo mingi, Mkoma watu na Hasha hazimfiki pia ametumia historia ya mfalme wa Pate ambayo ilivunjika katika mwaka 1890 kutokana na uvamizi wa Witu. Grenvile pia ametumia maelezo ya wasafiri mbalimbali waliofika katika upwa wa Afrika mashariki na wasafiri hao ni kama vile Al - Masoud na Al - Idris.
Akifafanua kuhusiana na ujio wa waarabu, Grenville anaeleza kuwa Al – Idris ni mwanazuoni wa Ulaya katika mahakama ya mfalme Roger ii huko Sicily     (1100 – 1166), huyu alikuwa mtu wa kwanza kugundua kuwa jina la kwanza la Zanzibar ni Unguja. Pia alitaja majina ya ndizi zilizopatikana huko kama vile kikonde, muriani, mkono wa tembo, sukari pia kuna aina nyingine ziliitwa omani. Huyu hakutumia neno ndizi ila alitumia neno la kiarabu.
Inasadikika kuwa ndizi zilifika pwani baada ya mwanzoni mwa karne ya 6. Anaendelea kufafanua kuwa mvumbuzi wa mji wa kilwa Al ibn al – Husain ibn al alipofika kilwa alikuta inakaliwa na mwisilamu aliyeitwa Muriri Wabari, jina hili si la kiarabu na wa inaonekana kama ni kihusishi pia alikuwa na msisikiti ambapo ndipo alipozikiwa, msikiti uliitwa kibala.
Kwa hiyo kutokana na maelezo haya ya Grenville ni dhahiri kuwa majina ya ndizi zilizotajwa na Al - Idris kama vile sukari, mkono wa tembo na kundi inaonesha kuwa lugha ya Kiswahili ilikuwapo hata kabla ya ujio wa waarabu pia waarabu walifika pwani ya Afrika mashariki mapema ingawa hajaeleza wazi ni lini waarabu hawa walifika pwani na hii ni kutokana na uwepo wa msikiti na dini ya kiisilamu huko kilwa.
Halikadhalika majina ya utani ya wafalme wa kilwa waliyopewa kutokana na tabia zoa kama vile Nguo nyingi, alipewa jina hili kutokana na kuzungushia himaya yake kwa nguo zenye rangi mbalimbali pia Mkoma watu alipewa jina hilo kutokana na ukatili wake. Hivyo hii inadhihirisha kuwa watawaliwa walikuwa ni wabantu ambao walikuwa na lugha yao na bila shaka lugha hiyo ilikuwa ni Kiswahili.
Kuhusu uchotara wa lugha ya Kiswahili katika uk 10 katika makala yake anaeleza kuwa “Kiswahili kimechukua mengi na kiashiria cha kwanza cha uathiriano huo katika pwani ya Afrika Mashariki kipo katika kitabu cha Periplus of Erythrean Sea kilichoandikwa na mwandishi nahodha asiyejulikana jina aliyetokea Alexandria katika karne ya 1. Grenville anaeleza kuhusu watu wa Rapta eneo hili halijulikani wapi lilipo, lakini inasadikika kuwa eneo hili lipo
katika mlango wa mto pangani. Anasema watu wa Muza hutoza ushuru na kupeleka huko meli ndogo nyingi wakiwa na manahodha na mawakala wa kiarabu. Hawa walifahamu vizuri wakazi wa maeneo hayo na kuoana nao. Wanajua vijiji vyao vyote na wanajua lugha yao. Anafafanua kuwa lugha iliyozaliwa ilitokana na muingiliano wa kuoana huko ilikuwa ni Kiswahili ingawa hatujui kuwa watu wa Rapta ni wa aina gani lakini haielekei kuwa ni wabantu.”
Kwa mujibu wa maelezo hayo Kiswahili ni lugha chotara iliyotokana na mwingiliano wa kuoana kati ya wanawake wa pwani ambao sio wabantu na wanaume wa kiarabu. Wanawake hawa ambao si wabantu walikuwa wakazi wa Rapta.
Pia inaoneka kuwa Kiswahili ni lugha iliyozuka kibahati katika kipindi hicho cha kuoana ili kukidhi haja ya mawasiliano baina ya watu hao wanaotumia lugha mbili tofauti.
Kimsingi maelezo ya Freeman Grenville katika makala yake ya “Medieval Evidences for Swahili” juu ya asili ya Kiswahili tunaweza kupata ubora ufuatao:-
Kwanza anahusisha Kiswahili na ujio wa waarabu. Freeman katika maelezo yake ananasibisha asili ya lugha ya Kiswahili na baada ya ujio wa waarabu ambao ndio ulipelekea mwingiliano huo.
Pia kwa mujibu wa Freeman Kiswahili ni lugha chotara ambayo ilianza baada ya ujio wa waarabu
Grenville anafafanua majina mbalimbali ya zamani kama vile chakula kwa mfano majina ya ndizi kama vile mkono wa tembo, sukari, muriani, omani ambayo wataalamu wanaonasibisha Kiswahili na kibantu hutumia ushahidi huu kunasibisha Kiswahili na kibantu. Pia anataja jina la Wakilimi ambalo      linaamana ya wafalme. Pia anataja majina ya utani ya waflme kama vile nguo nyingi na mkoma watu ambayo yalikuwa yanatumiwa maeneo ya pwani.
Pia Grenville katika makala yake ametaja majina mbalimbali ya Kiswahili ambayo ni kama vile kalala (sehemu ya mnazi inayobeba matunda), bwana, mkulu  – ngulu (Mungu), muriri wa bari, mtetezi, lughajuu, pia katika makala hii kuna ushari.            
“tulikwetu manda twali tulitenda”,
“yeo tukitendwa twakataa kwani?”,
“hutupa ukuta wathipetapeta”,
“kutwa ni kuteta hatuna amani.”
Pia katika makala hii ingawa upo ubora kuhusu asili ya Kiswahili lakini maelezo ya Grenville yanaonekana kuwa na udhaifu kwa kiasi kikubwa, baadhi ya madhaifu hayo ni kama vile yafuatayo:-
Katika makala yake anaeleza kuwa Al - Idris alikuwa ni mwanazuoni wa Ulaya, je mantiki ipo wapi je ni kweli alikuwa ni mwanazuoni wa Ulaya? si kweli alikuwa mwanazuoni wa Ulaya bali alikuwa mwanazuoni wa Kiislamu kutoka morocco. 
·        Grenville ameshindwa kufafanua kuwa watu wa Rhapta ni watu gani licha ya kueleza kuwa watu hawa sio wabantu.
·        Hajatueleza ni lugha ipi iliyokuwa ikitumiwa na watu wa Rapta kabla ya ujio wa waarabu.
·    Grenville hajatueleza kuwa hao waarabu waliingia pwani ya Afrika mashariki kipindi gani.
·        Hajatueleza uchotara wa lugha ya Kiswahili umetokana kati ya kiarabu na lugha gani.
·        Kama hao waarabu waliwafahamu wenyeji pamoja na lugha zao hakukuwa na sababu ya kuzuka kwa lugha chotara.
·        Freeman Grenville ameshindwa kueleza kuwa wale wanawake walioolewa na waarabu kama walikuwa sio wabantu je walikuwa watu gani walitumia lugha gani.
Kwa kuhitimisha ni kuwa, kutoka na kuhitalafiana kusuhu asili ya lugha ya Kiswahili tunakubaliana na wataalamu wanaokinasibisha Kiswahili na kibantu kwa kutumia hoja za kiisimu na kihistoria.
Marejeo
 Freeman Grenville medieval evidences  for Swahili 1959.
Massamba D.P.B na wenzake (1999) Sarufi  Miundo ya Kiswahili Sanifu (SAMIKISA), TUKI, Dar es salaam.

12 comments:

  1. heko kwako kwa kazi nzuri mno

    ReplyDelete
  2. Heko kwa kazi nzuri pamoja na utafiti wako.

    ReplyDelete
  3. Nimeridhika kwa kazi hiyo nzuri...
    Ningependa kufahamu ushahidi na upungufu kuwa kiswahili ni lugha ya pijini au kikirioli.

    ReplyDelete
  4. Kazi ni nzuri endelea kuwafunza waswahili na wapenzi wa kiswahili

    ReplyDelete
  5. Kazi nzuri tunahitaji kujifunza mengi kuhusu asili ya lugha yetu ili tupate maarifa mengi na tuzidi kukuza lugha hii ya kiswahili.

    ReplyDelete
  6. kazi inahitaji marejeleo ya kutosha.vilevile jitahidi kuhariri kazi yako. Pia toa maana zaidi ya moja katika kufasili maana, mfano asili. zaidi ya hayo hongera sana

    ReplyDelete
  7. This comment has been removed by the author.

    ReplyDelete
    Replies
    1. kwa nini kiswahili kikawa na maneno ya kiarabu wakati chenyewe kilikuwepo kabla ya ujio wa waarabu katika mwambao wa afrika mashariki???

      Delete
  8. This comment has been removed by the author.

    ReplyDelete
  9. Herufi za mwanzo zilizokuwa zinaiwakilisha lugha ya kiswahili ni zipi?, mimi naamini zilikuwepo ambazo sio hizi za kiingereza sababu waingereza sio waloanzisha kiswahili iweje zitumike herufi za lugha yao wakati wao sio walioanzisha kiswahili???

    ReplyDelete
  10. Je, Ugunduzi wa Ali-Idris, Safari ya Marco Polo & Historia ya kilwa, ni vitabu gani has a huonesha hizo taarifa?

    ReplyDelete