TOFAUTI KATI YA
UAMILIAJI LUGHA NA UJIFUNZAJI LUGHA.
Mwanadamu
anapozaliwa anakuwa na bohari la sauti mbalimbali zisizo na maana yoyote, na
mara anapoanza kuishi katika jamii ndipo huanza kuibua sauti hizo katika
mazingira ya kinasibu (pasipo yeye mwenyewe kutarajia) na kuanza kuzitafutia
maana sauti hizo. Uibuaji wa sauti hizo huendana sambamba na mambo
yanayomzunguka pamoja na yale anayoyatumia.
Hii
tunaona hata kwa watoto wachanga jinsi wanavyoanza kuongea, kwanza huanza kwa
kutoa sauti zisizo na maana yoyote kisha kadiridi wanavyokuwa ndivyo sauti hizo
zinaanza kubadilika mpaka zikaeleweka na watu wanaomzunguka. Yote haya ufanyika
kutokana na msaada wa mazingira, muda pamoja na jamii inayomzunguka.
Hivyo
basi tunaona kwamba dhana ya uamiliaji lugha huanza mara tu mtoto anapozaliwa
kisha hufuatiwa na dhana ya ujifunzaji lugha. Pamoja na hayo yote wapo wataalam
mbalimbali waliojaribu kuelezea dhana hizi mbili kwa mapana zaidi huku wakitoa
tofauti mbalimbali kati ya uamiliaji lugha na ujifunzaji lugha.
Kwa kuanza na maana ya lugha, wanaisimu wengi
wamewahi kutoa fasili mbalimbali kuhusiana na dhana ya lugha, miongoni mwa
wanaisimu hao ni pamoja na;
Trudgil
(1974) ambaye amenukuliwa na Mgullu (1999). Anasema kuwa “Lugha ni mfumo wa
sauti za nasibu zinazotumiwa kwa mawasiliano miongoni mwa watu wa jamii fulani
yenye utamaduni wake.
Mtaalam
mwingine ni Sapir (1921) ambaye anasema kuwa Lugha ni mfumo ambao mwanadamu
hujifunza ili autumie kuwasilishia mawazo, maono na mahitaji. Mfumo huu hutumia
ishara ambazo hutolewa kwa hiari.
TUKI
(1990) inasema: Lugha ni mfumo wa sauti zinazotumiwa na watu wa jamii fulani
wenye utamaduni unaofanana ili kuwasiliana.
Kwa
mujibu wa Msanjila na wenzake (2011) wakimnukuu Massamba (2004:19) wanasema
kuwa “Lugha , kwa upande wake, hufasiliwa kuwa ni mfumo wa sauti nasibu ambazo
zimebuniwa na jamii kwa madhumuni ya mawasiliano kati yao”. Jambo la msingi la
kuzingatia katika fasili hii ni kuelewa kwamba dhima kuu ya lugha ni kuwezesha
mawasiliano miongoni mwa jamii yaweze kufanyika.
Hivyo
basi katika fasili zote hizi tunaweza kusema kuwa wataalam hawa kimsingi
wanakubaliana kuwa lugha ni mfumo wa sauti za nasibu ambazo zimekubalika
zitumike miongoni mwa wanajamii kwa lengo la kuwasiliana.
Pia
dhana ya uamiliaji lugha imefasiliwa na Garman pamoja na Fletcher (1986) kama
walivyonukuliwa na Hickman; wanasema kuwa, Uamiliaji lugha hautokei katika
ombwe (patupu) kadiri watoto wanavyoamili lugha wanaamili mfumo wa ishara
ambazo zinaonesha uhusiano muhimu katika nyanja ya ubongo na nyanja ya jamii
katika maisha.
Naye
Stephen Krashen na Tracy D.T (1983) wamejaribu kuelezea dhana hii ya uamiliaji.
kwa kusema kuwa uamiliaji ni mchakato unaotokea katika nafsi iliyofichika
akilini mwa mtu ambayo ndiyo imuongozayo kuongea au kuandika kwa urahisi. Hivyo
wao wanaona kuwa uamiliaji hujitokeza kwa mtu katika hali ya ung’amuzi bwete
pasipo muhusika mwenyewe kujitambua.
Na
katika ujifunzaji lugha, Krashen na Tracy (1983) wanadai kuwa ujifunzaji ni
mchakato wa kiufahamu wa kiakili au utambuzi wa nafsi unaojionesha katika
kujifunza sharia na kanuni na miuundo ya lugha. Hivyo basi katika dhana hii wao
wanaona kuwa ujifunzaji ni tukio la kiutambuzi, yaani mtu ana kuwa anafahamu au
anatambua kuwa anajifunza lugha hivyo atapaswa kuzingatia kanuni na muundo wa
lugha.
Mtalaam
mwingine ambaye anaonesha kukubaliana na akina Krashen na mwenzake ni Gleason
(1989) ambaye naye anaona kuwa uamiliaji lugha ni sawa na tukio linalotokea
katika ung’amuzi bwete wakati ujifunzaji hutokea katika ung’amuzi tambuzi.
Katika kuthibitisha hilo anasema kuwa;
Ujifunzaji
lugha unazingatia kujua vipengele muhimu vya lugha ambavyo si lazima kuvifuata
au kuvijua katika uamiliaji lugha bali vinakuja vyenyewe pasipo utambuzi au
pasipo kujua. Vipengele hivyo ni kama vile; fonolojia, mofolojia, sintaksia,
semantiki na pragmatiki.
Baada
ya kutazama fasili na mitazamo mbalimbali iliyotolewa na wataalam hao juu ya
lugha, uamiliaji lugha na ujifunzaji lugha, zifuatazo ni tofauti zilizopo kati
ya Uamiliaji lugha na ujifunzaji lugha.
Uamiliaji
lugha hutokea katika ung’amuzi bwete yaani pasipo mtoto wenyewe kujitambua
kiakili, anajikuta tu ana uwezo wa kuzungumza vizuri bila kujua kwa nini
anazungumza hivyo, wakati ujifunzaji lugha ni tukio la kiutambuzi. Yaani mtu
anajua fika kwamba anajifunza lugha.
Vile
vile katika uamiliaji lugha si lazima kufuata sharia na kanuni za lugha au
vipengele vya lugha lakini katika ujifunzaji lugha lazima mtu aelewe vipengele
vyote muhimu vya lugha.
Pia
katika ujifunzaji lugha lazima kuwepo na mwalimu ambaye ni mtaalam wa lugha
pamoja na mazingira fulani muhimu ambayo yatamfanya yule mjifunzaji lugha
kuweza kujifunza lugha kwa urahisi zaidi. Mfano wa mazingira hayo ni kama vile
shule au taasisi maalum kwa ajili ya ujifunzaji lugha. Lakini katika uamiliaji
lugha haitajiki mtaalam wa lugha wala mazingira maalum kama hayo.
Vile
vile katika uamiliaji lugha utamaduni wa jamii husika hauzingatiwi sana lakini
katika ujifunzaji lugha lazima mjifunzaji lugha aelewe na azingatie utamaduni
wa jamii husika ili kuepuka makosa ambayo yanaweza kusababisha uhusiano mbaya
na wanajamii husika.
Vile
vile uamiliaji lugha ndiyo unaotangulia kisha hufuatiwa na ujifunzaji lugha.
Yaani mtoto huanza kuzungumza pasipo kujua taratibu za lugha kama vile, muundo
wa lugha, kanuni za lugha na utamaduni wa lugha husika. Baada ya kujua
kuzungumza ndipo hufundishwa sharia mbalimbali za lugha husika.
Pia
kwa mujibu wa Jean (1992:123) anasema kuwa katika uamiliaji lugha watoto
wachanga wanakuwa makini katika lugha tangu wanapozaliwa. Wanaanza kutoa maneno
yanayotambulika katika kipindi cha miezi 12-15 na kuanza kuyaunganisha maneno
hayo kuanzia miezi 18. Anaendelea kusema kuwa watoto wote wasio na matatizo ya
kimaumbile na baadhi ya wenye matatizo, wataanza kuongea ikiwa watasikia lugha
ikizungumzwa katika mazingira walimo. Hii ni tofauti na ujifunzaji lugha kwani
mtu hata waze kujifunza lugha kwa njia ya kusikia tu.
Tofauti
nyingine ni kwamba uamiliaji lugha una kikomo lakini ujifunzaji lugha hauna
kikomo kwani unaendelea katika umri wowote haijalishi kijana au mzee.
Hivyo
basi ninaweza kuhitimisha kwa kusema kuwa mtu yeyote anao uwezo wa kujifunza
lugha na kuifahamu ikiwa tu atakuwa na akili timami pamoja na ala sauti zote
zinazohusiana na ujifunzaji lugha ambazo hazijaathiriwa au kuathirika sambamba
na kupewa mazingira ya kijamii ya kujifunza lugha ingawaje hatafikia uwepo wa
uamiliaji.
MAREJEO:
Aitchison,
J. (1992). Teach Yourself: Linguistics. (4th
ed). Hodder & Stoughton Ltd Britain.
Berko,
G.J. (1989). The Development of Language. A. Bell & Howell Information Company.
Fletcher,
P. and Garman, M. (1986). Language
Acquisition. Cambridge University Pess.
Krashen,
Stephen D. and Tracy D. Terrell (1983). The
Natural Approach. Language Acquisition in the Classroom:
Pergamon Press. Oxford.
Mgullu,
R.S. (1999). Mtalaa wa Isimu: Fonetiki,
Fonolojia na Mofolojia ya Kiswahili. Dar es Salaam. Longhorn Publishers
(T) Ltd.
Msanjila,
Y.P. na wenzake. (2011). Isimujamii:
Sekondari na Vyuo. TUKI. Dar es salaam
TUKI
(1990). Kamusi Sanifu ya Isimu na Lugha:
TUKI. Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment