Thursday 24 October 2013

MAWANDA YA KISWAHILI



MAWANDA YA KISWAHILI KATIKA DUNIA YA UTANDAWAZI.
Utandawazi ulianza polepole kuingia katika lugha ya Kiswahili tangu enzi za utawala wa Kikoloni. Hali hii ilisababisha mabadiliko kadha wa kadha hususani katika lugha ya Kiswahili. Mabadiliko hayo yanaweza kujidhihirisha katika nyanja mbalimblai kama vile; Utamaduni (Dini, na Elimu), Biashara na Utawala. Vyote hivi kwa pamoja vilisaidia kukuza na kueneza lugha ya Kiswahili ndani na nje ya Afrika.
Utawala wa Kikoloni katika kipindi hicho uliambatana na kuanzishwa rasmi kwa vyombo vya habari kama vile magazeti na redio. Maendeleo yalizidi kuongezeka zaidi na zaidi hasa katika kipindi cha Ukoloni mamboleo, ambapo tunaona vyombo vipya vya upashanaji habari kama vile; luninga, tovuti. barua pepe, simu nk.  Hali hii imesaidia kuimarisha utandawazi wa Kiswahili kuwa na mawanda mapana zaidi kimatumizi.

Lugha ya Kiswahili ni miongoni mwa lugha zinye mawanda mapana zaidi katika Dunia ya Utandawazi. Kwani leo hii tunashuhudia Kiswahili kikifundishwa katika nchi mbalimbali duniani, kwa kuzitaja chache: Uingereza, Ujerumani, Italia, Marekani, China, Korea, Afrika Kusini, Libya, Ghana, Rwanda, Burundi nk.
Pia lugha ya Kiswahili inasikika katika vyombo mbalimbali vya habari duniani kama vile Iran Swahili redio nk. Nchi mbalimbali duniani zimeanzisha idhaa ya Kiswahili katika kurusha habari mbalimbali zinazojiri ulimwenguni pote. 
Kutokana na athari chanya za Utandawazi, kumekuwa na ushindani wa pekee katika masuala mbalimbali husasuni katika Lugha ya Kiswahili. Hivi sasa katika Ulimwengu wa Utandawazi, lugha ya Kiswahili inaonekana kuwa na mashiko makubwa ikilinganishwa na lugha nyingine za Kibantu.
Pia ni moja kati ya lugha inayokubalika na watu wengi katika Afrika na hata nje ya Afrika. Hii inajibainisha kutokana na idadi ya kubwa ya watumiaji. Watu wengi hutumia lugha ya Kiswahili katika mawasiliano, katika biashara, katika dini, katika shughuli za kijamii, katika shughuli za kidiplomasia, katika elimu nk. Hivyo basi, hali hii inakifanya Kiswahili kuingia katika Utandawazi kwa minajili ya kuunganisha jamii mbalimbali Ulimwenguni.
Vilevile kutokana na utandawazi ajira zinaongezeka kwa kasi sana, Mathalani wageni mbalimbali kutoka nchi za Kiafrika na zisizo za Kiafrika ambao hawazungumzi lugha hii adhimu ya Kiswahili huja Afrika Mashariki kwa lengo la uwekezaji. Wageni hawa hulazimika kujifunza Kiswahili kwa hali na mali ili kudumisha mahusiano na wenyeji wake na hatimaye kufikia malengo yao.
Hivyo basi, kutokana na mmiminiko huu wa wageni katika nchi za Afrika Mashariki ni dhahiri shahiri kunapelekea hitaji kubwa la waalimu wa lugha kwa ajili ya kufundisha Kiswahili pamoja na wataalam wa tafsiri na ukalimani. Hata hivyo bado Watanzania na Wakenya wengi huchukuliwa na nchi mbalimbali kwa lengo la kufundisha lugha ya Kiswahili katika nchi zao.
Hali kadhalika Utandawazi umesaidia kuongeza msamiati na istilahi katika lugha. Kiswahili ni miongoni mwa lugha zilizonufaika na matokeo ya Utandawazi. Leo hii lugha ya Kiswahili imefumbata istilahi kemkem zilizotokana na Utandawazi, hususani katika maendeleo ya sayansi na teknolojia, siasa, utamaduni na uchumi. Kwa mfano; tunashuhudia maendeleo ya sayansi na teknolojia jinsi yalivyosababisha mfumuko wa istilahi nyingi za kimtandao katika lugha ya Kiswahili.
Pia Utandawazi umesaidia kuongeza idadi ya watumiaji wa lugha ya Kiswahili. Ambapo inakadiriwa kuwa, katika nchi za maziwa makuu idadi ya watumiaji wa lugha ya Kiswahili ni zaidi ya milioni 70. Hali hii inakifanya Kiswahili kuwa na hadhi ya juu ukilinganisha na lugha nyingine za kibantu.
 Pamoja na hayo, Waswahili wana msemo usemao, “Hakuna kizuri kisicho na kasoro.” Hali kadhalika Utandawazi nao una kasoro zake. Hivyo basi Baada ya kuangalia matokeo chanya ya Utandawazi sasa tuangalia matokeo hasi au madhara ya Utandawazi katika lugha ya Kiswahili.
Matokeo ya utandawazi yamesababisha baadhi ya watu kudharau lugha ya kiswahili. Lugha hii hivi sasa inaonekana kama lugha ya watu wa tabaka la chini wasio na kitu/makabwela. Mtazamo huu umewafanya wazazi wengi kuwapeleka watoto wao katika shule zinazofundisha kwa lugha ya Kiingereza maarufu kama English medium/International School.
Vilevile Watu huiona lugha ya Kiswahili kuwa ni lugha ya watu wenye mtazamo finyu na wasio jua kitu chochote katika Ulimwengu huu. Hali hii inawafanya wasomi na wasio wasomi kuchanganya msimbo wakati wa uzungumziji wao ilihali tu waonekane kuwa wanajua mambo.
Pia, Kiswahili kinaonekana kuwa si lugha ya sayansi na teknolojia, na kwamba haiwezi kutumika katika shughuli mbalimbali za kisayansi kama vile, katika taaluma ya ufundi nk.  Hii pia hujidhihirisha katika maelekezo ya bidhaa mbalimbali zinazotengenezwa nchini kwa ajili ya soko la ndani. Tunaona lugha za kigeni kama vile Kiingereza hutumika kuelezea namna ya kutumia bidhaa husika.
Baada ya kuangalia athari chanya na hasi katika lugha ya Kiswahili, ni vyema tujipe wasaa japo kwa ufupi tuangalie namna Kiswahili kinavyokabiliwa na changamoto mbalimbali.
Pamoja na umaarufu mkubwa na hadhi yake, Kiswahili bado kinakumbana na matatizo makubwa ya mtazamo/dhana na matumizi katika jamii mbalimbali ndani na nje ya Afrika. Jamii za wasomi na zisizo za wasomi, wazee kwa vijana, watajiri kwa msikini nk.
Katika hoja ya dhana, bado kuna baadhi ya watu wanaonasibisha Kiswahili na dini ya Uiislam. Hali hii imetokana na historia ya Waarabu katika bara la Afrika hususani katika Afrika Mashariki. Ujio wa Waarabu uliambatana na uenezaji wa dini ya Kiislam kwa kutumia lugha ya Kiarabu. Lugha ambayo imeonekana kuwa na mfanano mkubwa wa kimsamiati na lugha ya Kiswahili.
Hivyo kutokana na dini ya Kiislam kutumia Kiarabu na wingi wa msamiati wa Kiarabu katika lugha ya Kiswahili imekuwa ni tatizo kubwa miongoni mwa watumiaji wa lugha hii. Mfano nchi kama vile Burundi na Uganda ni miongoni mwa nchi zinazokinasibisha Kiswahili na dini ya Kiislam.
Vilevile kumekuwa na upinzani mkubwa kutoka katika nguvu za kidola. Nchi nyingi zenye uwezo wa kimamlaka kama vile Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Ureno nk. zinafanya kila jitihada kuhakikisha lugha zao zinaendelea kufunika lugha nyingine zenye nguvu kama vile Kiswahili. Wanafanya hivi kwa kuhofia kwamba Kiswahili kinaweza kuua lugha zao.
Kubezwa kwa lugha ya Kiswahili na kushadidiwa kwa lugha za kigeni, kuwa ndizo lugha pekee zenye uwezo na zinazofaa kutumika katika shughuli mbalimbali za kiuchumi. Hivyo Kiswahili kuonekana kuwa hakifai kutumiwa katika shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Kasumba, mpaka leo baadhi ya Watanzania wameendelea kushikilia mawazo ya kishenzi/Kikoloni kuwa Kiingereza ndio lugha bora kuliko Kiswahili. Kitu ambacho kimewafanya watu wengi kuwahusudu, kuwatukuza na kuwaogopa wale wanaoongea Kiingereza au lugha za kigeni. Kasumba hii imewafunga akili na kushindwa kung’amua kwamba Kiingereza ni sawa na lugha nyingine tu.
Kusuasua kwa sera ya lugha. Sera ambayo ingekipa hadhi Kiswahili kuwa lugha ya kufundishia katika ngazi zote za elimu. Na kukifanya kiingereza kuwa somo tu kama masomo mengine. Hivyo ucheleweshwaji huu unarudisha nyuma maendeleo ya Kiswahili na jamii kwa ujumla.
Kukosekana kwa moyo wa uzalendo kwa viongozi wa nchi. Serikali inashindwa kufadhili kwa kutoa mikopo asilimia mia kwa wanafunzi wanaosoma Kiswahili Vyuo Vikuu. Hali hii inawafanya wanafunzi kutoona uthamani na umuhimu wa kujifunza lugha ya Kiswahili, lugha ambayo inatangaza utamaduni wao. Matokeo yake vijana wengi na hata watu wazima wanathamini sana utamaduni wa kimagharibi kuliko utamaduni wao.
Pia kumekuwa na mtazamo potofu kuwa Kiswahili ni lugha ya watu duni kitaaluma. Hii ni dhana potofu kabisa inayoasisiwa na baadhi ya wasomi kabisa. Wengi wanaona kuwa Kiswahili ni lugha ya watu walioishia elimu ya msingi/darasa la saba. Hivyo hufanya watu wengi kuwa na mshawasha wa kujifunza Kiingereza kwa kasi kubwa na kudharau Kiswahili.


MAREJEO:
BAKITA, (2004), Makala ya siku ya Kiswahili Kiswahili na Utandawazi, Dar es salaamu
TUKI, (2004), Kamusi ya Kiswahili Sanifu, Toleo la pili, Oxford university press, Nairobi

2 comments: