Thursday 24 October 2013

KUSIGANA NA KULANDANA KWA MSAMIATI


KUFANANA NA KUTOFAUTIANA KWA LEKSIKOGRAFIA, LEKSIKOLOJIA NA LEKSIKONI.
Katika kujadili mada hii tutaanza kufasili maana ya leksikografia, leksikolojia na leksikoni kisha tutajadili zaidi kuhusu tofauti zilizopo baina ya leksikografia, leksikolojia na leksikoni na mwishowe tutaweka hitimisho la mada yetu pamoja na marejeo.
Wataalamu mbalimbali wametoa fasili ya Leksikografia kama vile  Mdee (1985) anaeleza leksikografia ni usawiri wa kamusi, Huu ni utaalamu au utaratibu wa kukusanya msamiati pamoja na tafsiri yake na kuupanga katika kitabu cha maneno ambacho huitwa Kamusi.
Fasili hii ya Mdee ina udhaifu kwani Kamusi siyo lazima iwe imeandikwa katika kitabu pekee, bali kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia siku hizi kamusi zimeweza kuandikwa katika elektroniki mfano kompyuta na simu za mkononi.

Hali kadhalika Oxford dictionary (2001) Leksikografia ni kitendo cha kuunda kamusi.
Hivyo basi kutokana na fasili hizo tunaweza kufasili leksikografia kuwa  ni sehemu ya isimu inayojihusisha na uundaji wa kamusi. Leksikografia inafafanua maneno na kuweka wazi matumizi na miundo ya maneno.
Taaluma hii ya leksikografia tunaweza kuigawa katika sehemu kuu mbili:-
(1)   Leksikografia ya vitendo
(2)   Leksikografia ya kinadharia
Leksikografia ya vitendo. Ni sanaa ya kukusanya, kuandika na kuhariri kamusi. Wakati Leksikografia ya kinadharia. Ni mwongozo wa kitaaluma wa kueleza na kufafanua uhusiano wa semantiki, sintagmatiki na pragmatiki katika leksikoni ya lugha, kuendeleza nadharia zinazounda kamusi na kuhusianisha data katika kamusi.
Kwa ujumla leksikografia inajihusisha na kubuni, kukusanya, kutumia na kutathimini kamusi kwa ujumla. Hali kadhalika leksikografia inajihusicha na fonolojia, mofolojia, semantiki au maana pamoja na miundo ya maneno kwa ujumla.
Pia  kwa mujibu wa Oxford (2001) leksikolojia inahusu mfumo, maana na tabia za maneno.
Hivyo tunaweza kufasili leksikolojia kuwa ni sehemu ya isimu inayojishughulisha na maneno, asili na maana, mofolojia ya maneno, mahusiano ya maana ya maneno, makundi ya maneno na leksikoni kwa ujumla. Wakati mwingine leksikografia huchukuliwa kama tawi au sehemu ya leksikolojia. Lakini vitu hizi havipaswi kuchanganywa kwa sababu wanaleksikolojia wanaoandika kamusi ndiyo wanaleksikografia. Ikumbukwe kuwa leksikolojia halisi ipo katika nadharia tu kwa sababu leksikografia sifa yake kubwa ipo katika vitendo ingawa ina nadharia yake.
Hali kadhalika tunaweza kufasili leksikoni kama ilivyofasiliwa na oxford (2001) kuwa ni msamiati wa mtu, lugha au tawi la maarifa. Huu ni ule msamiati wote uliopo kichwani mwa mzungumzaji wa lugha. Leksikoni ndio nguzo au chanzo cha data za wanaleksikolojia na wanaleksikografia katika mchakato mzima wa uandaaji wa kamusi.
Baada ya kuangalia fasili ya dhana hizo tatu sasa tujikite katika Mfanano uliopo baina ya leksikografia, leksikolojia na leksikoni kama ifuatavyo:-
Leksikografia, leksikolojia na leksikoni zinajihusisha na msamiati wa lugha. Leksikografia hukusanya msamiati na maana zake na kutunga kamusi ambalo hutoa ufafanuzi juu ya msamiati ya lugha. Hali kadhalika leksikolojia hujihusisha na msamiati katika kuelezea maana na matumizi ya maneno husika kwa jamii husika. Pia leksikoni ni jumla ya msamiati uliopo katika kichwa cha binadamu ambapo wanaleksikografia na wanaleksikolojia wanaweza kuutumia msamiati huo katika kuunda kamusi ya lugha.
Leksikolojia na leksikografia hutegemea watumiaji wa lugha katika kukusanya data zake kwani zote hujihusisha na leksikoni. Hivyobasi leksikografia na leksikolojia hutegemea leksikoni iliyopo kichwani mwa mtumiaji wa lugha.
Leksikografia na leksikolojia zimetokana na maneno ya kigiriki ambayo ni “lexico” likiwa na maana ya maneno. Leksikolojia limetokana na neno “lexico” (maneno) na logos (sayansi) ikimaanisha sayansi ya maneno wakati leksikografia imetokana na neno “lexico”  (maneno) na “graph” (kuandika) ikiwa na maana ya kuandika maneno.
Zote zinahusika na uwanja wa kiisimu ujulikanao kama semantiki. Leksikografia licha ya kujihusisha na nyanja nyingine kama vile fonolojia na mofolojia pia inajihusisha kwa kiasi kikubwa na semantiki kwani hata hapo mwanzoni kamusi ziliandikwa kwa kuzingatia semantiki. Huangalia maana ya msamiati katika kutunga kamusi hali kadhalika leksikolojia pia hujikita katika maana na matumizi ya msamiati. Leksikoni iliyopo kichwani mwa mzungumzaji hebeba maana ya maneno katika lugha.
Zote zinahusu etimolojia ya maneno Katika kupata data za kimofolojia na kisemantiki za leksimu, kamusi pia hutusaidia katika kutapa taarifa za kimuundo zinazohusu asili ya maneno na taarifa za kihistoria kuhusu mabadiliko ya maneno na matumizi ya maneno.
Baada ya kuangalia ufanano huo sasa tugeukie katika Utofauti uliopo baina ya leksikografia, leksikolojia na leksikoni. Utofauti huo unaweza kufafanuliwa kama ifuatavyo:
Leksikografia inafikiriwa kuwa ni kongwe kuliko leksikolojia kwani utungaji wa kamusi inasadikika kuwa ulifanywa na wayunani tangu karne ya kwanza hata hivyo maandishi hayakuwa kamusi kama tujuavyo leo bali yalikuwa maana ya maneno na maana zake. Orodha ya namna hiyo ilikusanywa na wakina Pamphilus, Athicists (karne ya pili) na Hesyelius (karne ya tano) wote wa Alexandria. Wakati leksikolojia ilianza miaka ya 1820 ingawa inasemekana kuwa kulikuwa na wanaleksikolojia kabla ya neno leksikolojia kupatikana. Vilevile leksikoni iliyopo kichwani mwa mzungumzaji hupata au huamili katika kipindi cha makuzi. Hivyo mtu hupata msamiati kadri anavyokua katika jamii. Bila shaka leksikoni ndiyo nguzo kuu ya leksikografia na leksikolojia.
Tofauti nyingine ipo katika Malengo. Malengo ya leksikografia kiujumla ni kubuni, kukusanya, kutumia na kutathimini kamusi au kuunda kamusi. Wakati leksikolojia malengo yake ni kuchunguza etimolojia, maana na matumizi ya maneno. Malengo ya leksikoni ni kuhifadhi msamiati kichwani mwa mzungumzaji itakayomsaidia katika mawasiliano.
Pia tofauti nyingine ni Mabadiliko. Kila siku msamiati mpya huongezeka katika leksikoni iliyopo kichwani mwa mzungumzaji. Leksikoni hubadilikabadilika. Maneno mapya huongezeka, baadhi ya maneno mapya huongezeka. Baadhi ya maneno hudendeshwa na mengine huboreshwa. Lakini katika leksikografia, mwanaleksikografia anapounda kamusi yake hubaki kama ilivyo hadi hapo atakapounda kamusi nyingine iliyobora kupita ile ya kwanza. Hivyobasi ni vigumu kamusi kuweza kupokea mabadiliko ya msamiati na maana zake mara kwa mara kuendana na mabadiliko ya jamii. Kwa upande wa leksikolojia kwa kiasi fulani huweza kupokea mabadiliko kwani leksikolojia ipo katika nadharia.
Tofauti nyingine ni kuwa Leksikolojia hujihusisha na sifa za jumla, sifa ambazo zinaweza kuonekana katika mpangilio maalumu wakati leksikografia inajihusisha na sifa ya maneno kiupwekeupweke. Zgusta (1973:14).
Hali kadhalika Katika taaluma ya leksikolojia maana ya maneno ni elekezi ambayo yanaongozwa na nadharia ya kisemantiki na muundo wa maneno wakati katika leksikografia maana zake nyingi ni fafanuzi ambapo maana ya maneno hutegemea na wazungumzaji wa lugha siyo mwanaleksikografia (Mtengenezaji wa kamusi).
Tofauti nyingine ni Idadi kamili ya maneno. Kiujumla hauwezi kutambua idadi kamili ya msamiati katika leksikoni iliyopo kichwani mwa mzungumzaji kwani kila siku mzungumzaji huingiza msamiati mpya kichwani mwake. Hivyo ni vigumu kutambua idadi halisi ya msamiati alionao. Lakini katika leksikografia idadi ya msamiati uliopo katika kamusi huweza kujulikana na kubainishwa wazi wazi. Hii inatokana na ukweli kwamba kamusi huwa na idadi ya misamiati kulingana na aina ya kamusi ambayo mwanaleksikografia amedhamiria kuiandaa.
Tofauti nyingine ni uwasilishwaji wa misamiati kama vile Kichwani au katika maandishi. Inatambuliwa kuwa leksikoni ipo kichwani mwa mzungumzaji wa lugha, ambayo humwezesha katika kukabiliana na majukumu yake ya mawasiliano na wakati mwingine leksikoni hii iliyopo kichwani mwa mzungumzaji huwa ndio chanzo cha data zitumiwazo na wanaleksikografia katika kutunga au kuandaa kamusi. Ila tunapozungumzia leksikografia hapa tunapata nafasi ya kuiona misamiati na maana zake katika maandishi. Hivyo maandishi haya ambayo huitwa kamusi huwa ni ufafanuzi tosha juu ya maneno au misamiati inayotumiwa na watumiaji wa lugha.
Hivyo basi kwa kuhitimisha tunaweza kusema kuwa licha ya tofauti zilizopo juu ya dhana hizi tatu, lakini leksikografia, leksikolojian na leksikoni zinahusiano wa karibu hasa katika mchakato mzima wa kukusanya na kuandaa kamusi. Hivyo hatuwezi kuzitenganisha dhana hizo bila kuona mapungufu.

MAREJEO.
Mdee, J.S (1985) “Ukusanyaji wa data ya Leksikografia na Matatizo yake: Mifano kutoka Kiswahili katika Mulika na. 17. Dar es salaam. TUKI
Mdee, J.S (1997) Nadharia na Historia ya Leksikografia. Dar es salaam. TUKI Oxford (2001) Concise Oxford Dictionary. UK. Oxford University Press.

1 comment: