Friday, 4 October 2013

TAATHIRA KATIKA FASIHIMSINGI WA KUWEPO MOTIFU ZA AINA MOJA KATIKA TANZU ANUAI ZA FASIHI ZA MATAIFA/MAKABILA TOFAUTITOFAUTI ULIMWENGUNI.
Katika mada hii tutaanza kufafanua juu ya nadharia ya taathira, mwingiliano matini na usambamba kisha tutafafanua juu ya dhana ya motifu kabla ya kuingia moja kwa moja katika kiini cha mada yetu.
Nadharia ya taathira. Hii ni nadharia iliyoasisiwa na shule ya Ufaransa wakati wa kuchunguza fasihi linganishi katika sehemu mbalimbali ulimwenguni. Guyard, M.F na Tieghem wanafafanua nadharia hii kuwa, uchukuaji wa mawazo kutoka katika kazi moja ya fasihi kwenda nyingine inahusishwa pia na uchukuaji au upelekaji wa wazo kutoka katika aina moja ya jamii kwenda nyingine.
Carre. J.M anaamini taathira ni sawa na upokeaji yaani kazi moja inakuwa na vipengele fulani fulani kutoka fasihi nyingine.
Zhirmunwk anaeleza kuwa ni mchakato wa upokezi usio wa bahati mbaya hivyo mtunzi anautumia kwa makusudio na vipengele hivyo ni vya kiutamaduni na kiitikadi.

Nadharia uingilianomatini. ni dhana inayohusishwa na mnadharia wa kifaransa Julia Kristeva ambaye aliizua kutokana na nadharia ya usemezano ya Mikhail Bakhtin, wafuasi wa nadharia hii ya mwingiliano matini wanaoshikilia kuwa kazi za kifasihi kuingiliana na kuhusiana katika kile kinachoweza kuitwa “mwanda wa kimwingiliano matini”
Nadharia ya usambamba. Katika nadharia hii tunachunguza mfanano wa mabadiliko ya kijamii na namna yalivyochagiza kuwapo kwa mikondo mbalimbali ya kifasihi. Waasisi wa nadharia hii wanafafanua kuwa jamii mbili au tatu zilizopitia katika hatua zenye kufanana katika maendeleo zinafanana pia katika fasihi yake.
Tamthiliya ya KILIO CHETU ni tamthiliya inayojaribu kuvunja ukimya uliotawala miongoni mwa jamii katika kutatua matatizo makubwa ambayo chimbuko lake ni mahusiano ya kijinsia, katika tamthiliya hii vijana wanatoa sauti za masononeko kuhusu juu ya wazazi, walezi na watawala wanaolifumbia macho suala hili nyeti. Hivyo inajaribu kuwapa vijana elimu ya mahusiano ya kijinsia badala ya kupewa hofu na vitisho.
Pia tamthiliya ya orodha iliyoandikwa na Steve Reynolds hii ni tamthiliya inayojadili juu ya ukosefu wa elimu ya ukimwi ambapo mwandishi anamtumia muhusika Furaha ambaye alijiingiza katika mahusiano pasipo kufahamu madhara ambayo angeweza kuyapata, hatimaye kutokana na makosa ambayo aliyafanya ambayo yalimpelekea kupata virusi vya ukimwi ambapo ilimpelekea kifo chake.
Zifuatazo ni motifu mbalimbali zilizojitokeza katika kazi hizi mbili za tamthiliya.
Motifu ya dhamira; Waandishi wa tamthiliya ya kilio chetu na orodha wamejitahidi kuibua dhamira mbalimbali ambapo kwa kiasi kikubwa dhamira za vitabu hivi viwili zimeelekea kufanana, baadhi ya dhamira kubwa zilizojitokeza katika tamthiliya hizi ni kama vile:-
Athari za ukimwi. Mwandishi wa kitabu cha kilio chetu amemtumia muhusika joti katika kuibua dhamira hii ya madhara ya ukimwi ambapo Joti aliambukizwa virusi vya ukimwi iliyopelekea kifo chake (UK 32 sehemu ya sita). Pia katika tamthiliya ya orodha mwandishi ameibua dhamira kama hii kwa kumtumia muhusika Furaha ambaye pia alifariki kwa ugonjwa wa ukimwi.
Mapenzi katika umri mdogo; Waandishi wa tamthiliya hizi hawakutupilia mbali suala la baadhi watu  kuwa na uhusiano wa kimapenzi na watoto wadogo, katika kitabu cha orodha mwandishi amemtumia muhusika Bwana Ecko ambaye alikuwa ni mtu mzima lakini alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na Furaha ambaye alikuwa mtoto mdogo. Pia katika tamthiliya ya orodha mwandishi amemtumia muhusika Joti kuwa na uhusiano wa kimapenzi na chausiku ambaye alikuwa ni msichana mkubwa kwake.
Ukosefu wa elimu ya jinsia. Waandishi wa tamthiliya hizi wamejaribu kuonesha kwa mapana jinsi vijana wanavyojiingiza katika matatizo kutokana na ukosefu wa elimu ya jinsia. Kwa mfano katika tamthiliya ya kilio chetu tunamuona muhusika Joti akiwa kama kielelezo cha watu waliokosa elimu ya jinsia ambapo madhara yake ilimpelekea kupata maambukizi ya ukimwi, vilevile katika tamthiliya ya orodha mwandishi amemtumia pia muhusika Furaha kuonesha jinsi gani alivyokosa elimu ya jinsia ambapo ilimpelekea pia kupata maambukizi ya virusi vya ukimwi vilivyompelea kifo chake.
Motifu ya ujumbe; kupitia tamthiliya zote hizi mbili waandishi wanaonekana kushabihiana katika kipengele cha ujumbe, baadhi ya ujumbe ambao unafanana ni kama vile:-
Madhara ya kujihusisha na mapenzi katika umri mdogo. Katika tamthiliya zote mbili tunaona kuwa suala la mapenzi katika umri mdogo ni hatari kwani huweza kupekea maambukizi ya ukimwi ambayo hupelekea kifo kama ilivyojitokeza kwa muhusika furaha katika tamthiliya ya orodha na Jori katika tamthiliya ya kilio chetu.
Umuhimu wa elimu ya jinsia. Katika tamthiliya hizi waandishi wanabainisha kuwa elimu ya jinsia kwa vijana ni muhimu kwani kama vijana wengi wangepatiwa elimu hii basi wangeweza kuepukana na matatizo yasiyo ya lazima kama vile maambukizi ya virusi vya ukimwi. Kwa mfano katika tamthiliya ya kilio chetu mwandishi amemtumia muhusika Suzi ambaye hakupatiwa elimu ya jinsia, pia muhusika Furaha hakuwa na ufahamu juu ya elimu ya jinsia ambapo iliwapelekea kuoata maambukizi ya virusi vya ukimwi.
Motifu ya wahusika; Sifa za baadhi ya wahusika wa tamthiliya ya orodha zinashabihiana moja kwa moja na baadhi ya sifa za wahusika katika tamthiliya ya kilio chetu. Mfano sifa za muhusika Suzi katika tamthiliya ya kilio chetu zinashabihiana moja kwa moja na sifa za muhusika Furaja katika tamthiliya ya orodha. Baadhi ya sifa hizo ni kama zifuatazo:- wahusika wote wawili wamekosa elimu ya jinsia pia walijiingiza katika mtandao wa wapenzi wengi.
Motifu ya mtindo; Katika tamthiliya zote mbili waandishi wanaelekeana kushabihiana katika mtindo walioutumia kuwasilisha kazi zao. Waandishi wote wawili wametumia mtindo wa majibizano au dayalojia.
Motifu ya falsafa. Pia falsafa za waandishi wote wawili yaani medical aid foundation wa kilio chetu na Steve Reynolds wa tamthililiya ya orodha zinaonekana kufanana. Wote wanaamini kuwa elimu ya jinsia itolewe ili kusaidia kuwaokoa vijana kupata maambukizi ya virusi vya ukimwi.
Motifu ya mandhari. Katika tamthiliya zote mbili waandishi wote wametumia mandhari halisi. Mandhari hizo ni kama vile mitaani, shuleni, nyumbani nakadhalika.
Hivyo basi kutokana na utokeaji wa motifu hizo nadharia ya usambamba, taathira na mwingiliano matini unatupa msingi wa utokeaji wa motifu hizo kama ifuatavyo:-
Kutokana na nadharia ya kitaathira utokeaji wa motifu zinazofanana katika kazi mbili za watunzi wawili tofauti ni kwasababu ya makutano ya sehemu fulani ya watunzi hao, mtagusano (inatokana na kusoma kazi ya mtunzi mwingine). Hii ni sababu ya kutokea kwa motifu zilizoorodheshwa hapo juu. Kuathiri huko kunaweza kuwa hasi au chanya, moja kwa moja au siyo moja kwa moja.
Baada ya kujadili nadharia ya taathira inavyojadili msingi wa kuwepo kwa motifu zinazofanana katika kazi mbili tofauti za kifasihi, sasa tunarejelea nadharia ya mwingiliano matini. Nadharia hii inaeleza kuwa mwingiliano matini ni uhusiano kati ya matini moja na nyingine ambapo matini hiyo huathiri namna ya usomaji wa matini nyingine. Hapa mtunzi asilia hatazamwi kama muasisi bali hutazamwa kama mdokoaji wa vipengele mbalimbali vya kifasihi na kuviweka katika kazi moja ya fasihi. Mfano wa kipengele mandhari, wahusika, dhamira na ujumbe. Mfano katika tamthiliya ya orodha inaelekea kufanana na vipengele vilivyo katika tamthiliya ya kilio chetu. Uwezo wa kuchanganua kazi hizi hutegemeana na jukumu la muhakiki kutumia nadharia ya mwingiliano matini.
Kwa kutazama motifu ya wahusika katika kazi hizi mbili zimeonekena kuingiliana kwani muhusika Furaha katika tamthiliya ya orodha amechorwa wasifu wake unaofanana na muhusika suzy katika tamthiliya ya kilio chetu kwani wote walijihusisha na mapenzi katika umri mdogo, wote walikosa elimu ya jinsia, wote wamepata malezi ya mama kuliko baba.
Halikadhalika katika nadharia ya usambamba, ineleza kuwa msingi wa kuwepo kwa motifu zinazofanana katika kazi mbili tofauti za kifasihi ni kutokana na mabadiliko ya kijamii iliyopelekea kuwepo kwa mikondo mbalimbali ya kifasihi.
Nadharia hii imefafanuliwa hivyo na shule ya kimarekani. Msisitizo ni kuwa kazi mbili zilizopitia katika mfumo mmoja hupelekea kufanana kimtindo na kimuundo kwa waandishi wawili tofauti. Mfano tamthiliya ya orodha iliyoandikwa mwaka 2006 na tamthiliya ya kilio chetu iliyoandikwa mwaka 1995 zote zimeandikwa katika kipindi kimoja cha maendeleo ya kiutandawazi katika jamii.
Hivyo basi kwa mujibu wa nadharia hii ya usambamba inavyotueleza tunaona kuwa sababu kuu ya kufanana kwa kazi mbili za fasihi ni kutokana na mfumo wa maisha uliokuwepo katika kipindi hiki cha utunzi wa kazi hizi mbili.
Hivyo basi licha kuwepo kwa nadharia ya kitaathira, mwingiliano matini na usambamba katika kuelezea misingi ya kuwepo kwa motifu katika kazi mbili za mataifa tofauti, sisi tunaona kwamba nadharia ya mwingiliano matini ni bora zaidi katika kurejelea msingi wa kuwepo kwa motifu zinazofanana kazi hizo. Hii ni kwa sababu matini huwa na tabia ya kubeba matini nyingine mfano katika kipengele vya wahusika, mandhari na dhamira.
 MAREJEO
Medical Aid Foundation. (1995). KILIO CHETU. Tanzania Publishing House Ltd. Dar es salaam.
Senkoro. F.E.M.K. (2011). Fasihi. KAUTTU Ltd. Dar es salaam.
TUKI. (2004). Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Oxford University Press. Dar es salaam.
Wamitila. K. W. (2003). Kamusi ya Fasihi. Istilahi na nadharia. Focus Publishers Ltd. Nairobi. Kenya.No comments:

Post a Comment