UCHUNGUZI SAMBAMBA DHIDI YA
MAMBO YA KUFIKIRIKA
Uchunguzi katika uandishi wa kubuni ni
jambo la lazima ili mtunzi asiandike vitu ambavyo havishawishi kukubalika. Kwa
maneno mengine, kufanya uchunguzi ni kufanya utafiti. Je, utafiti ni nini? Hebu
tuangalie baadhi ya wataalamu wanasemaje kuhusiana na istilahi hii ya utafiti.
Kothari (2009:1) anasema kuwa,
kwa msemo wa kawaida 'utafiti' ni kutafuta maarifa ili kuelewa jambo
fulani. Utafiti ni utafutaji wa taarifa kisayansi na kwa kufuata utaratibu
fulani kuhusiana na mada fulani. Kwa uhakika, utafiti ni
sanaa ya kuchunguza
mambo kisayansi.
KKS (2000:445) inaelezea kuwa,
'utafiti' ni uchunguzi wa kisayansi au kitaaluma ambao umelenga
kugundua, kufasiri, au utumiaji wa maarifa mapya, nadharia, au kanuni fulani.
Advance Learner's Dictionary of Current
English inasema kuwa, 'utafiti' ni kufanya uchunguza kwa umakini au ni
kutafuta taarifa mpya katika tawi lolote la maarifa. (1952:1069)
Redman na Mory wanasema kuwa, 'utafiti'
ni utaratibu unaofanywa ili kupata maarifa mapya. (The Romance of Research,
1923:10)
Clifford Woody anasema 'utafiti'
unajumuisha mambo tano ambayo ni: kuelezea tatizo, kuunda nadharia tete,
kukusanya, kuratibu, na kutathmini data, kufanya udedushi na kufikia hitimisho,
na kupima kama hitimisho linasadifu nadharia tete.
Kitula King'ei na Catherine Kisovi
(2005:13) wanasema 'utafiti' ni: shughuli ya kitaaluma ambayo inamaanisha
kupekua, kuchunguza, kuratibu, kufichua au kupeleleza. Pia inaweza kumaanisha
kuchanganua jambo, dhana au hali fulani kwa shabaha ya kuielewa hasa kwa undani
jinsi ilivyo.
Kwa hiyo, baada ya kuona nini maana ya
'utafiti', mwandishi wa kubuni hana budi kuzingatia maana ya dhana hiyo ili
imwongoze katika 'safari yake ya uandishi'. Kwa maneno mengine, hapa
ndipo mantiki ya kutembea na shajara pamoja na kalamu inapopata mashiko. Kwa
kuwa, katika kutembea kwako na hekaheka za maisha, utakutana na vituko au
mikasa ambayo utapenda kuitumia katika ubunifu wako. Je, usipoweka kumbukumbu
utawezaje kuwasilisha kitu chenya 'uhalisi sambamba' wa maisha tuishiyo?
No comments:
Post a Comment