SINTAKISIA
HAIWEZI KUTENGANISHWA NA VITENGO VINGINE VYA LUGHA.
Katika kujadili mada hii, kwanza tutatoa fasili ya sintaksia
kwa mujibu wa wataalam mbalimbali, fasili ya lugha, tutafafanua uhusiano uliopo
kati ya sintaksia na vitengo vingine vya lugha na mwisho tutatoa hitimisho juu
ya mjadala wetu.
Kwa mujibu wa Massamba na wenzake (1999) Sintaksia ni utanzu
wa sarufi unaojihusishana uchunguzi wa mpangilio wa maneno katika sentensi na uhusiano wa vipashio vyake. Wanaendelea
kusema, utanzu huu huchunguza sheria au kanuni zinazofuatwa katika kuyapanga maneno
ili yalete maana inayokubalika na kueleweka katika lugha husika.
Pia Habwe na Karanja (2004) wanasema Sintaksia ni utanzu wa
isimu unaoshughulikia muundo wa sentensi na elementi nyingine zinazounda
sentensi kama vile kategoria za maneno, vikundi na vishazi.
Kutokana na fasili hizi inaonekana kuwa Massamaba na wenzake
wamefafanua zaidi kwa kuonesha kuwa licha ya kuzingatia kanuni na sheria za
kupanga maneno lakini pia ni lazima maneno hayo yawe na uhusiano. Kwa upande
mwingine Habwe na Karanja wameshindwa kuelezea suala hili, wao wanaona sintaksia
inashughulika na muundo wa sentensi na vipashio vyake.
Kwa mantiki hii tunakubaliana na fasili ilyotolewa na
Massamaba na wenzake kuwa Sintaksia ni utanzu wa sarufi unaojihusisha na
uchunguzi wa mpangilio wa maneno katika sentensi na uhusiano wa vipashio vyake, kwa kuzingatia
sheria na kanuni za lugha husika ili kuleta mawasiliano.
Katika fasili ya lugha, wataalam wengi wanakubaliana kuwa
lugha ni mfumo wa sauti nasibu ambazo hutumiwa na jamii kwa madhumuni ya
mawasiliano kati yao. Baadhi ya wataalam wanao kubaliana na fasili hii ni
Massamba na wenzake (Wameshatajwa).
“Kitengo” kwa mujibu wa TUKI (2004) ni mahali pateule
palipotengwa kwa shughuli maalum. Tunaporejea katika muktadha wa lugha tunaweza
kusema kuwa vitengo vya lugha ni vipengele muhimu vinavyounda maarifa ya lugha
kwa ujumla. Kwa fasili hii, vipengele vinavyounda maarifa ya lugha ni
fonolojia, mofolojia, sintaksia na semantiki.
Kwa hiyo kutokana na kwamba sintaksi pia ni kitengo mojawapo
kinachounda maarifa ya lugha, tunakubali kwamba, sintaksia haiwezi
kutenganishwa na vitengo vingine vya lugha kutokana na uhusiano mkubwa uliopo
baina ya vitengo hivi. Vitengo hivi hutegemena na kuathiriana. Hivyo basi
tunaweza kuonesha jinsi sintaksia isivyoweza kutenganishwa na vitengo vingine
vya lugha yaani fonolojia, mofolojia na semantiki kama ifuatavyo:
Uhusiano baina ya fonolojia na sintaksia. Massamba na
wenzake (Wameshatajwa) wanafasili fonolojia kuwa ni uchambuzi wa mfumo wa sauti
katika lugha mahususi. Wanaendelea kusema ni jinsi ambavyo vitamkwa au sauti za
lugha zinavyoungana ili kujenga maneno yanayokubalika katika lugha.
Kwa hiyo tunaweza kusema kuwa kuungana kwa vitamkwa ili
kujenga maneno yanayokubalika katika lugha
fulani hutegemea mpangilio sahihi wa vitamkwa. Na kwa kuwa neno ni
kiwango cha msingi cha uchambuzi katika sintaksia basi fonolojia ina uhusiano
wa moja kwa moja na sintaksia.
Mifano ifuatayo huthibitisha hoja hii:
Mfano 1.“Anapika”. Hili ni neno lakini pia ni sentensi,
hivyo huweza kuchanganuliwa kifonolojia kama ifuatavyo: a|n|a|p|i|k|a|, mpangilio wa sauti umeunda
neno “anapika”.
Mfano 2.a. baba. Limeundwa na (KIKI).
b. abab. Limeundwa na (IKIK).
Katika mfano 2a tunaona neno “baba” lina maana na limefuata
kanuni na mpangilio unaokubalika wakati mfano 2b neno “abab” halina maana
katika lugha ya Kiswahili kwa sababu halina mpangilio mzuri wa fonimu.
Kwa mifano hii tunaona kwamba hatuwezi kuwa na miundo
mikubwa katika sentensi bila kuwa na mpangilio sahihi wa sauti katika lugha.
Kwa hiyo sintaksia haiwezi kukamilika bila fonolojia.
Uhusiano baina ya mofolojia na sintaksia. Mofolojia ni
kitengo kingine cha lugha ambacho kwa mujibu wa Rubanza (1996) ni taaluma
inayoshughulikia vipashio vya lugha katika kuunda maneno. Kutokana na fasili
hii, kipashio cha msingi katika uchambuzi wa kimofolojia ni neno ambalo ndilo
hutumika kuunda darajia ya sintaksia.
Vilevile maumbo ya kimofolojia huathiri vipengele vingine
vya kisintaksia, kwa mfano, sentensi zifuatazo hufafanua zaidi:
1. Mtoto anacheza.
2. Watoto wanacheza.
Katika mifano hii tunaona kwamba mofimu m- na wa- katika
upande wa kiima zimeathiri utokeaji wa mofimu a- na wa- katika upande wa
kiarifu.
Pia kanuni za mfuatano na mpangilio wa mofimu au viambishi
zikifuatwa huunda maneno katika miundoya kisintaksia. Mfano:
1. Alicheza =
a-li-chez-a
2. Anaimba = a-na-imb-a
Kwa ujumla kipengele cha umoja na wingi katika maumbo ya
kimofolojia ndicho kinachoathiri umbo linalofuata jina na kuathiri muundo wa
sentensi nzima. Mfano:
1. Mwalimu alikuwa
anafundisha.
2. Walimu walikuwa
wanafundisha.
Tunaona katika mifano hii maumbo ya umoja na wingi ya maneno
Mwalimu na Walimu yameathiri mpangilio mzima wa sentensi.
Uhusiano baina ya semantiki na sintaksia. Habwe na Karanja
wakimnukuu Richard na Wenzake (1985) wanasema Semantiki ni stadi ya maana. Semantiki
ni utanzu unaochunguza maana katika lugha ya mwandamu. Wanaendelea kusema
semantiki hutafiti maana za fonimu, mofimu, maneno na tungo.
Kwa hiyo kutokana na fasili hii maana hushughulikiwa katika vitengo au
viwango vyote vya lugha ambavyo ni fonolojia, mofolojia na sintaksia.
Mfano: a) Paka mweusi amepotea.
b) Mweusi paka amepotea.
c)Amepotea mweusi paka.
Katika mifano hii tunaona kwamba sentensi a) ina maana
kutokana na kwamba imefuata mpangilio sahihi wa maneno katika tungo na sentesi
zilizobaki hazina maana kutokana na sababu kwamba hazijafuata mpangilio ulio
sahihi.
Kwa mantiki hii, kwa kuwa semantiki hushughulikia viwango
vyote vya lugha, basi hushughulikia pia kiwango cha sintaksia ambapo huangalia
maana za tungo. Tungo yoyote ni lazima ilete maana inayokubalika na
wazungumzaji au watumiaji wa lugha husika, kama itakuwa kinyume basi haitakuwa
tungo bali ni orodha ya maneno tu.
Mfano:
Mtoto anacheza mpira uwanjani.
Mtoto uwanjani mpira anacheza.
Tukiangalia mifano hii tutagundua kwamba katika sentensi ya
kwanza mpangilio wake wa vipashio unaleta maana lakini sentensi ya pili haina
maana kutokana na kuwa na mpangilio mbaya wa maneno.
Kwa hiyo tunaweza kuhitimisha kwa kusema kuwa sintaksia
haiwezi kutenganishwa na vitengo vingine vya lugha kwa kuwa kuna uhusiano wa
moja kwa moja baina ya vipengele hivi vya lugha na kwa hiyo hutegemeana kati ya
kipengele kimoja na kingine. Kwa mfano, huwezi kupata mofolojia (neno) bila
kupitia ngazi ya fonolojia na pia huwezi kuwa na ngazi ya sintaksia
(sentensi/tungo) bila kupitia ngazi ya fonolojia na mofolojia lakini vitengo
vyote hivi hutawaliwa na kitengo cha semantika ili kuleta mawasiliano miongoni
mwa wazungumzaji.
MAREJEO
Habwe,
J na P. Karanja (2007). Misingi ya Sarufi
ya Kiswahili. Nairobi: Phoenix Publishers Ltd.
Massamba,
D.P.B na wenzake (1999). Sarufi Miundo ya
Kiswahili Sanifu: Sekondari na Vyuo. Dar essalaam: TUKI.
Rubanza,
Y.I (1996). Mofolojia ya Kiswahili.
Dar es salaam: Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.
TUKI
(2004).Kamusi ya Kiswahili Sanifu.
Dar es salaam: TUKI.
sadakta. kazi nzuri jamani.
ReplyDeletechuo kikuu cha Maseno
Kenya.
Nakuunga mkono
DeleteKazi nzuri mwl be blessed
ReplyDeleteKuntu kabisa kazi murua,
ReplyDelete#mpenzi wàlugha jimnie
Kuntu kabisa kazi murua,
ReplyDelete#mpenzi wàlugha jimnie
Kazi safi mwalimu
ReplyDeleteKazi nzuri
ReplyDeleteKazibmashaAllah pambee
ReplyDeleteHongera,makala haya namefafanuliwa vyema
ReplyDeleteMakala nzuri sana
ReplyDeletekazi nzuri mel
ReplyDelete