Monday, 3 February 2014

VIONJO VYA FASIHI SIMULIZIKUNA FAIDA GANI YA KUIENDELEZA F. SIMULIZI IKIWA JAMII NYINGI SASA HIVI ZINAJUA KUSOMA NA KUANDIKA?
Wengi mtakubaliana nami kwamba, Maendeleo ya Sayansi na Teknolojia ulimwenguni, kamwe hayaondoi uwepo wa fasihi simulizi, bali yanaleta athari katika fasihi simulizi ama chanya ama hasi.
Pia tutambue kwamba, jamii yoyote ulimwenguni inapoendelea katika nyanja yoyote ile athari hazikwepeki. Na hii ni kanuni inayofahamika ulimwenguni kote.
Hivyo basi, hata kama jamii nyingi duniani zinajua kusoma na kuandika, bado umuhimu wa kuiendeleza fasihi simulizi katika ulimwengu wa leo upo palepale. Tena katika kipindi hiki cha maendeleo ya Sayansi na Teknolojia mimi naona umuhimu huu ni mkubwa sana kuliko hata miaka ya nyuma.
Awali ya yote katika kujadili swali hili ningependa tujadili kwa kifupi
maana ya fasihi simulizi kwa mujibu wa wataalam mbalimbali. Baada ya hapo tutaangazie kiini cha swali letu, ambapo tutafafanua mambo yanayotufanya tuienzi na kuiendeleza fasihi simulizi katika jamii yetu ya leo. Pia tutaangali faida zinazotokana na kuiendeleza fasihi simulizi katika jamii zinazojua kusoma na kuandika.
Fasihi Simulizi ni nini?
Wataalamu mbalimbali wametoa maoni yao kuhusu maana ya FS. Miongoni mwao ni Finnegan (1970), Matteru 1979), Balisidya (1983), Okpewho (1992) na wengine wengi. Ili kuweza kubaini maana ya FS ni vema kudurusu fasili zilizotolewa na wataalamu hawa. Lengo hasa ni kutaka kufahamu ubora na udhaifu wa fasili zao, hatimaye tuweze kuunda fasili muafaka zaidi kuhusu maana ya FS.
  • F.S yaweza kuelezwa kwamba, hutegemea msanii ambaye huiumba kwa maneno katika tukio maalum (Finnegan, 1970)
  • Ni fasihi inayotegemea mdomo katika kutolewa na kuenezwa kwake… (M.L.Matteru, 1979)
  • Ni aina ya fasihi ambayo hutumia mdomo katika kuumbwa, kuwasilishwa na kusambazwa kwa waasikilizaji na watumiaji wake (Balisidya, 1983)
  • F.S humaanisha fasihi itolewayo kwa neno la mdomo… (Okpewho, 1992)
  • F.S ni kazi ya sanaa inayotumia lugha kazi hii ya sanaa huhifadhiwa kwa kichwa na kusambazwa kwa njia ya masimulizi ya mdomo… (M.Msokile, 1992)
  • Ni fasihi inayotungwa au kubuniwa kichwani na kuwasilishwa kwa hadhira kwa njia mdomo na vitendo bila kutumia maandishi (Mulokozi, 1996)
  • Neno F.S linamaanisha hadithi za jadi, nyimbo, mashairi, vitendawili na methali ambavyo hutolewa kwa neno la mdomo (Bukenya na Wenzake, 1997)
  • Sanaa hii iitwayo Fasihi, inaweza kuhifadhiwa kwa njia kuu mbili: kwa njia ya mdomo na kimaandishi. Aina ya kwanza, ambayo tunajihusisha nayo katika sehemu ya kwanza inajulikana kama F.S (Wamitila, 2003)
Ø  Fasili hizi hazigusii lolote kuhusu matumizi ya nyenzo za sayansi na teknolojia katika kubuni, kutongoa na kuhifadhi sanaa husika. Nyenzo kama vile, Radio, Video, DVD, VCD, Televisheni, Kompyuta na Wavuti….. kwa sasa zinatumika katika kutolea na kurekodia tanzu za F.S kama vile hadithi……
Ø  Katika F.S fanani na hadhira huwapo ana kwa ana: dhana ya kuwapo ana kwa ana pia inahitaji mjadala (uwezekano wa kuwa na aina mbalimbali za hadhira)
Kwa nini tuendelee kuienzi na kuiendeleza fasishi simulizi wakati jamii nyingi zinajua kusoma na kuandika?
Hali hii husababishwa na vionjo vyake vya kiutendaji ambavyo kamwe havipatikani na wala haviwasilishwi kwa njia ya maandishi (F.A). Vionjo hivyo ni kama ifuatavyo:
Kutabasamu: Katika maandishi hadhira haiwezi kuona wala kusikia tabasamu la fanani wala kicheko chake. Lakini katika fasihi simulizi vyote hivi huonekana na kusikika. Hivyo huifanya hadhira iende sambamba na fanani. Mfano majigambo.
Hisia za huruma na furaha: Katika maandishi mambo haya hayawezi kukuingia kwa haraka na kukufanya uhuzunike au ufurahi na hadhira wenzako pamoja na fanani. Lakini katika fasihi simulizi mambo haya huweza kukuingia kwa urahisi na kukubadilisha haraka sana kimwili na hata kimtazamo. Mfano maigizo ya jukwaani.
Kucheka, kupiga makofi na kuuliza maswali: Katika fasihi simulizi husaidia sana hadhira kujiona ipo karibu na fanani, na katika hali hiyo ndiposa ujumbe wa fanani unaweza kuwaingia vizuri zaidi. Lakini katika maandishi mambo haya hayawezekani kabisa. Pia hata ikitokea hadhira haijamwelewa fanani itabaki katika hali hiyo mpaka mwisho wa maandishi.
Katika Fasihi simulizi ya Kiafrika vitendo huwasilisha dhamira kwa urahisi zaidi  kuliko maneno matupu. (Maneno hayajisemei yenyewe!)

No comments:

Post a Comment