Saturday, 1 February 2014

KISWAHILI

KILIO CHA MAMA YANGU
Mwenzenu nimefikiri, nimeshindwa kung’amua,
Kila nikitafakari, najiona naelea,
Hili lazima nikiri, niufukuze utwea,
Na leo ndiyo kikiri, jipu ninalitumbua,
Kilio cha mama yangu, ni kicheko kwa mgeni.
Staajabu ya Musa, uone ya Firauni,
Nabii wamemsusa, nyumbani hana thamani,
Anazidi kuhohosa, kajibanza pembezoni,
Mgeni ndiyo kabisa, kapandishwa kileleni,
Kilio cha mama yangu, ni kicheko kwa mgeni.
Uhuru wangu ni upi, hapa kwetu Tanzania?
Na kosa langu ni lipi, mbona mwaninyanyapaa!
Nimeshindwa fanyakipi, mpaka mwanikataa!
Hata mkinena vipi, hii ni yenu junaa,
Kilio cha mama yangu, ni kicheko kwa mgeni.

Babu nyanya naye pia, wote nimelatamia,
Elimu nikaitoa, nao wakajipatia,
Wazazi wenu ‘melea, sifa wakanimwagia,
Tena wakajivunia, pote walipotembea,
Kilio cha mama yangu, ni kicheko kwa mgeni.
Iweje vikaragosi, waseme sinayo hadhi,
Wakati mimi mwasisi, wahenga niliwahodhi,
Ikhlasi mwajitusi, kwa kunena yasokidhi,
Taifa mwalinajisi, Kingereza kunafidhi,
Kilio cha mama yangu, ni kicheko kwa mgeni.
Mashuleni mwanitenga, tena hadi chekechea,
Sekondari mwanipinga, mwasema sijakomaa,
Mwazidi kuvangavanga, ukweli kupotezea,
Vyuoni sijajipanga, kauli mnaitoa,
Kilio cha mama yangu, ni kicheko kwa mgeni.
Mwakataa nitawale, bondeni na mlimani,
Mwasema sina udole, nasaba yangu ni duni,
Mnanifanya sefule, kunibeza jukwaani,
Mgeni yu mteule, katawala mashuleni,
Kilio cha mama yangu, ni kicheko kwa mgeni.
Kingereza sikatai, naomba nieleweke,
Ninasema kwa bidii, warui na wakereke,
Wengi wenu hamjui, japo mwaleta makeke,
Nawasihi kwa utii, ung’eng’e usitumike,
Kilio cha mama yangu, ni kicheko kwa mgeni.
Kingereza kifundishwe, kama somo peke yake,
Na wala kisiapishwe, kuwatawala wenzake,
Kiswahili nihusishwe, na tena ifahamike,
Kwa wote nitambulishwe, jamii ikafunguke,
Kilio cha mama yangu, ni kicheko kwa mgeni.
Kiswahili nitumike, elimu kuitolea,
Wakusoma wanishike, wakafaulu mamia,
Wajuzi waongezeke, tuokoe Tanzania,
Popote tufahamike, kwa ubora wa bidhaa,
Kilio cha mama yangu, ni kicheko kwa mgeni.
Ukweli mnaujua, japo mwajishebedua,
Siasa zimewajaa, uongo mwanizushia,
Taifa mwalihadaa, eti sijatapakaa,
Ni nani kawaambia, mbona mnajitungia!
Kilio cha mama yangu, ni kicheko kwa mgeni.
Tayari ‘mevavagaa, na kuvuka vizingiti,
Wenyewe mwajionea, matendo ya ithibati,
Wageni wanirukia, na kunishika kititi,
Wenyeji mwasuasua, mwatupiana kijiti,
Kilio cha mama yangu, ni kicheko kwa mgeni.
Asia wataradhia, mdomoni niwakae,
Tena wanikimbilia, hawataki nipotee,
Huku wananiambia, kiasi gani watoe,
Na ninyi mwanikemea, mdomoni nikimbie,
Kilio cha mama yangu, ni kicheko kwa mgeni.
Ulaya wananiita, wanapenda wanijue,
Kila siku wanivuta, wanataka nihamie,
Na ninyi mnanigwata, mwataka nitokomee,
Taifa mnaliketa, hamtaki lisogee,
Kilio cha mama yangu, ni kicheko kwa mgeni.
Duniani nasifika, kwa kuleta utaifa,
Hatamu nimeishika, yanisifu mataifa,
Mpaka yanialika, kwa kuwa ninayosifa,
Sasa ninafahamika, japo mwaniona lofa,
Kilio cha mama yangu, ni kicheko kwa mgeni.

………………………………………………………

1 comment:

  1. Pole sana kaka kilio cha mama kweli kimekuumiza, lakini si wewe tu mliaji tupo wengi tunalia. machozi tele shavuni maisha kwetu magumu. chanzo ni kikosi cha watetezi hawatambui kuwa nasi tu watu. chozi sikufuti ila tuzidi pambambana tutafika.

    ReplyDelete